Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Waamini Katika Kutwaa Umbo Jipya?
    Mnara wa Mlinzi—1997 | Mei 15
    • Je, Waamini Katika Kutwaa Umbo Jipya?

      “WAMKUMBUKA msichana jirani uliyemwonea shauku ya kipumbavu ulipokuwa ukikua hapa India?” Mukundbhai akamwandikia mwanaye, aliye mwanafunzi wa chuo kikuu huko Marekani. “Ataolewa baada ya majuma machache. Nilidhani wapaswa kujua.”

      Kwa nini huyo baba alimjulisha mwanaye habari hiyo? Kwa vyovyote, Mukundbhai alikomesha waziwazi mapenzi hayo ya utineja miaka mingi iliyopita. Isitoshe, huyo mwana alikuwa amekuwa Marekani akifuatia elimu ya juu kwa miaka sita. Hakuwa amewasiliana na huyo msichana wakati huo, na Mukundbhai alijua hilo.

      Mbona, basi, ahangaike? Alihangaika kwa sababu Mukundbhai aliamini katika kutwaa umbo jipya, au kuzaliwa upya.a Ikiwa kwa kutukia yale mapenzi ya utotoni kati yao wawili yalikuwa kwa sababu ya kuwa washirika katika maisha yao ya awali, ungekuwa ukatili kuwatenganisha sasa wakiwa na umri wa kutosha kufunga ndoa. Mukundbhai alitaka tu kumjulisha mwanaye juu ya hiyo hali kabla ya huyo msichana kuwa mke wa mtu mwingine katika maisha haya.

      Fikiria kisa kingine. Msichana mwenye umri wa miaka minne alikuwa amelazwa akiwa na maumivu makali mara kadha wa kadha katika hospitali fulani huko Mumbai, India. Tatizo lake lilikuwa mshipa wenye kasoro moyoni mwake. Wazazi wake matajiri walisononeshwa kumwona mtoto wao akiteseka. Lakini walisababu hivi: “Lazima tukubali jambo la hakika kwamba tuna mtoto asiye na afya nzuri. Lazima awe alifanya jambo fulani katika maisha yake ya awali ili astahili jambo hili.”

      Itikadi katika kutwaa umbo jipya ina fungu muhimu maishani mwa mamilioni ya watu walio katika Dini ya Hindu, Dini ya Buddha, Dini ya Jaini, Dini ya Sikh, na dini nyingine zilizoanzia India. Mambo yaliyoonwa maishani—kuanzia na kushikwa na mapenzi hadi kuteseka sana —yanaonwa kuwa matokeo ya matendo yaliyofanywa katika maisha ya awali au maisha za awali.

      Watu wengi katika nchi za Magharibi wanavutiwa pia na fundisho la kutwaa umbo jipya. Mwigizaji wa kike wa Marekani, Shirley Mac­Laine adai kuamini katika kutwaa umbo jipya. Mwandikaji Laurel Phelan wa Vancouver, British Co­lum­bia, Kanada, adai kuwa na makumbukumbu ya maisha 50 mbalimbali zilizopita. Katika mahoji ya Gallup ya 1994 yaliyofanywa kwa ajili ya CNN/USA Today, zaidi ya watu wazima 270 kati ya 1,016 walidai kuwa wanaamini katika kutwaa umbo jipya. Imani katika kutwaa umbo jipya ni sehemu pia ya harakati ya Muhula Mpya. Lakini ni uthibitisho gani unaotegemeza itikadi hiyo?

      “Makumbukumbu ya maisha yaliyopita!” wasema wanaoamini katika kutwaa umbo jipya. Basi, Ratana mwenye umri wa miaka mitatu aliye Bangkok alipoanza kuwa na “makumbukumbu ya maisha yake yaliyopita akiwa mwanamke wa kidini aliyekufa katika miaka yake ya 60,” watazamaji walio wengi walikubali kisa chake kuwa ithibati halali ya kutwaa umbo jipya.

      Hata hivyo, kuna shaka. Na kwaweza kuwa na mafafanuzi mengine ya makumbukumbu yahesabiwayo maisha ya awali.b Katika kitabu chake Hinduism: Its Meaning for the Liberation of the Spirit, Nikhilananda, mwanafalsafa Mhindu asema kwamba ‘mambo yaonwayo baada ya kifo hayawezi kuthibitishwa kwa kufikiri.’ Hata hivyo anasisitiza kwamba “uwezekano wa fundisho la kuzaliwa upya ni mkubwa kuliko kutowezekana kwalo.”

      Lakini je, Biblia hutegemeza fundisho hilo? Nalo Neno la Mungu lililopuliziwa hutoa tumaini gani kwa ajili ya wafu?

      [Maelezo ya Chini]

      a “Kutwaa umbo jipya,” chasema kichapo The New Encyclopædia Britannica, kwamaanisha “kuzaliwa upya kwa nafsi katika kuwako kumoja au zaidi kunakofuatana, kuwezako kuwa kwa binadamu, mnyama, au, katika visa fulani, mmea.” Maneno “kuzaliwa upya” yanatumiwa pia kufafanua tukio hilo lakini maneno “kutwaa umbo jipya” hukubaliwa na watu wengi. Kamusi kadhaa za lugha ya Kihindi hutumia maneno hayo kwa kubadilishana.

      b Ona ukurasa wa 5-7 katika toleo la Amkeni! la Juni 8, 1994.

      [Picha katika ukurasa wa 4]

      Je, anaadhibiwa kwa sababu ya dhambi zake katika maisha ya awali?

  • Je, Wapaswa Kuamini Katika Kutwaa Umbo Jipya?
    Mnara wa Mlinzi—1997 | Mei 15
    • Je, Wapaswa Kuamini Katika Kutwaa Umbo Jipya?

      YULE mwana-falsafa Mgiriki Plato alihusianisha kushikwa na mapenzi na lile wazo la kutwaa umbo jipya. Aliamini kwamba baada ya kifo cha mwili, nafsi, kwa kuwa ni isiyoweza kufa, huhamia “makao ya maumbo yenye kutakata.” Kwa kuwa haina mwili, hiyo hubaki huko kwa wakati fulani, ikitafakari juu ya hayo maumbo. Baadaye inapotwaa umbo jipya wakati wa kuzaliwa upya, nafsi hukumbuka lakini si kwa udhahiri na hutamani makao ya maumbo. Kulingana na Plato, watu hushikwa na mapenzi kwa sababu wao huona katika mpenzi wao umbo bora la uzuri wanalokumbuka isivyo dhahiri na wanaotafuta.

      Kutambua Chanzo na Msingi

      Fundisho la kutwaa umbo jipya hutaka kwamba nafsi iwe isiyoweza kufa. Basi, asili ya kutwaa umbo jipya lazima ivumbuliwe kwa kurudi nyuma hatua kwa hatua hadi kwa watu au mataifa yaliyokuwa na itikadi hiyo. Kwa msingi huo, watu fulani wanafikiri kwamba ilianzia Misri la kale. Wengine wanaamini kwamba ilianzishwa katika Babiloni la kale. Ili kuletea sifa dini ya Kibabiloni, ukuhani wayo ulitokeza fundisho la uhamaji wa nafsi (kutoka mwili mmoja hadi mwingine mtu afapo). Hivyo wangeweza kudai kwamba mashujaa wao wa kidini walikuwa maumbo mapya ya wazazi wa kale wenye kutokeza, ingawa walikuwa wamekufa muda mrefu uliopita.

      Hata hivyo, itikadi ya kutwaa umbo jipya ilipevuka kabisa huko India. Wenye hekima Wahindu walikuwa wakishindana na matatizo ya ulimwengu wote mzima ya uovu na ya kuteseka miongoni mwa wanadamu. ‘Hayo yaweza kupatanishwaje na dhana ya Muumba mwadilifu?’ waliuliza. Walijaribu kusuluhisha hitilafiano kati ya uadilifu wa Mungu na maafa yasiyotazamiwa na ukosefu wa usawa ulimwenguni. Hatimaye, walibuni “sheria ya karma,” sheria ya sababu na matokeo—‘chochote apandacho mtu, hicho ndicho atakachovuna.’ Walitayarisha ‘taarifa ya hali ya fedha’ yenye mambo yote ambamo faida na hasara katika mojawapo ya maisha zinathawabishwa au kuadhibiwa katika maisha yafuatayo.

      “Karma” humaanisha tu “tabia.” Mhindu husemwa kuwa ana karma nzuri ikiwa yeye hupatana na kawaida za kijamii na kidini na husemwa kuwa ana karma mbaya ikiwa hafanyi hivyo. Tabia, au karma yake, huamua wakati wake ujao katika kila kuzaliwa upya kunakofuata. “Watu wote huzaliwa wakiwa na programu ya utendaji wa kiutu, hasa wakiwa wametayarishwa na matendo yao katika maisha za awali, ingawa vitabia vyao vya kimwili huamuliwa na urithi,” asema mwana-falsafa Nikhilananda. “[Hivyo] mtu ni mbuni wa ajali yake mwenyewe, mjenzi wa tokeo lake mwenyewe la hatima.” Hata hivyo, mradi wa mwisho ni kuwekwa huru kutoka katika duru hiyo ya uhamaji na kuunganishwa na Brahman—uhalisi wa mwisho. Yaaminiwa kwamba hilo hufikiwa kwa kujitahidi kufikia tabia yenye kukubaliwa kijamii na ujuzi wa pekee wa Hindu.

      Hivyo fundisho la kutwaa umbo jipya hutumia fundisho la hali ya kutokufa kwa nafsi kuwa msingi walo nalo huliendeleza kwa kutumia sheria ya karma. Acheni tuone Neno la Mungu lililopuliziwa, Biblia, lina yapi ya kusema kuhusu mawazo hayo.

      Je, Nafsi Ni Isiyoweza Kufa?

      Ili kujibu swali hilo, acheni tugeukie mamlaka ya juu zaidi katika habari hiyo—Neno la Muumba lililopuliziwa. Katika kitabu cha kwanza kabisa cha Biblia, Mwanzo, twajifunza maana sahihi ya “nafsi.” Kwa habari ya kuumbwa kwa mtu wa kwanza, Adamu, Biblia yasema hivi: “BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” (Mwanzo 2:7) Kwa wazi, nafsi si kile mwanadamu anacho bali ni kile alicho. Neno la Kiebrania litumiwalo hapa kwa nafsi ni neʹphesh. Hilo hupatikana mara 700 hivi katika Biblia, nayo hairejezei kamwe sehemu iliyo kando au isiyo ya kimwili ya binadamu bali sikuzote hurejezea kitu kiwezacho kuguswa na cha kimwili.—Ayubu 6:7; Zaburi 35:13; 107:9; 119:28.

      Ni nini kinachoipata nafsi wakati wa kifo? Fikiria kilichompata Adamu wakati wa kifo chake. Alipotenda dhambi, Mungu alimwambia hivi: ‘Utairudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.’ (Mwanzo 3:19) Fikiria jambo linalomaanishwa na maneno hayo. Kabla ya Mungu kumwumba kutoka mavumbini, Adamu hakuwako. Baada ya kifo chake, Adamu alirudia hali ileile ya kutokuwako.

      Kwa kusema kisahili, Biblia hufundisha kwamba kifo ni kinyume cha uhai. Kwenye Mhubiri 9:5, 10, twasoma hivi: “Walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.”

      Hilo lamaanisha kwamba wafu hawawezi kufanya au kuhisi chochote. Hawana mawazo yoyote tena, wala hawakumbuki chochote. Mtunga-zaburi ataarifu hivi: “Msiwatumainie wakuu, wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake. Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, siku hiyo mawazo yake yapotea.”—Zaburi 146:3, 4.

      Biblia huonyesha waziwazi kwamba wakati wa kifo nafsi haihami na kuingia mwili mwingine, bali hufa. “Roho [“nafsi,” NW] ile itendayo dhambi itakufa,” Biblia yataarifu kwa mkazo. (Ezekieli 18:4, 20; Matendo 3:23; Ufunuo 16:3) Hivyo, fundisho la hali ya kutokufa kwa nafsi—msingi wenyewe wa nadharia ya kutwaa umbo jipya—halipati tegemeo lolote katika Maandiko. Bila tegemeo hilo, nadharia hiyo huanguka. Basi, sababu ya kuteseka tuonako ulimwenguni ni nini?

      Kwa Nini Watu Wanateseka?

      Sababu ya msingi ya kuteseka kwa kibinadamu ni kutokamilika ambako sisi sote tunarithi kutoka kwa Adamu mwenye dhambi. “Kupitia mtu mmoja dhambi iliingia katika ulimwengu na kifo kupitia dhambi, na hivyo kifo kikasambaa kwa watu wote kwa sababu wote walikuwa wamefanya dhambi,” yasema Biblia. (Waroma 5:12) Tukiwa tumezaliwa kutoka kwa Adamu, sisi sote huwa wagonjwa, huzeeka, na hufa.—Zaburi 41:1, 3; Wafilipi 2:25-27.

      Zaidi, sheria ya maadili ya Mungu isiyobadilika hutaarifu hivi: “Msiongozwe vibaya: Mungu si wa kudhihakiwa. Kwa maana lolote lile mtu analopanda, hilo atavuna pia; kwa sababu yeye anayepanda katika mwili wake atavuna ufisadi kutokana na mwili wake.” (Wagalatia 6:7, 8) Hivyo, mtindo-maisha wa ngono za ovyo-ovyo waweza kuongoza kwenye msononeko wa kihisia-moyo, mimba zisizotakwa, na magonjwa ya kupitishwa kingono. “Asilimia 30 yenye kushangaza ya kansa zenye kuua [Marekani] yaweza kwa msingi kulaumiwa uvutaji wa sigareti, na idadi sawa na hiyo yaweza kulaumiwa mtindo-maisha, hasa mazoea ya ulaji na ukosefu wa mazoezi,” lasema gazeti Scientific American. Misiba fulani inayosababisha kuteseka ni tokeo la mwanadamu kutumia vibaya mali za dunia.—Linganisha Ufunuo 11:18.

      Ndiyo, mwanadamu ndiye wa kulaumiwa kwa nyingi za taabu zake. Hata hivyo, kwa kuwa nafsi si isiyoweza kufa, ile sheria ya ‘kuvuna upandacho’ haiwezi kutumika kuhusianisha kuteseka kwa kibinadamu na karma—matendo ya maisha yadhaniwayo kuwa ya awali. “Yeye ambaye amekufa ameondolewa hatia ya dhambi yake,” yataarifu Biblia. (Waroma 6:7, 23) Hivyo matunda ya dhambi hayapitishwi hadi kwenye maisha ya baada ya kifo.

      Shetani Ibilisi pia husababisha kuteseka kwingi. Kwa hakika, ulimwengu huu unatawalwa na Shetani. (1 Yohana 5:19) Na kama vile Yesu Kristo alivyotabiri, wanafunzi Wake wangekuwa ‘vitu vya kuchukiwa na watu wote kwa sababu ya jina lake.’ (Mathayo 10:22) Tokeo ni kwamba, mara nyingi waadilifu hukabili matatizo mengi zaidi kuliko wanayokabili waovu.

      Katika ulimwengu huu matukio fulani hutokea ambayo visababishi vyayo havijulikani. Mkimbiaji mwenye mbio zaidi aweza kujikwaa na kushindwa katika shindano la mbio. Jeshi lenye uweza laweza kushindwa na majeshi madogo. Mtu mwenye hekima aweza kushindwa kupata kazi nzuri na kwa hiyo apatwe na njaa. Watu wenye uelewevu bora kabisa wa kusimamia biashara waweza, kwa sababu ya hali, kushindwa kutumia ujuzi wao na hivyo kujikuta katika umaskini. Watu wenye ujuzi waweza kupatwa na hasira ya kisasi ya wale wenye mamlaka na kukosa upendeleo. Kwa nini iko hivyo? “Kwa sababu wakati na tukio lisilotazamiwa huwapata wote,” ajibu Mfalme Solomoni mwenye hekima.—Mhubiri 9:11, NW.

      Wanadamu wameteseka kwa muda mrefu kabla ya wenye hekima Wahindu kujaribu kufafanua ni kwa nini kuteseka kuko. Lakini je, kuna tumaini la wakati ujao ulio bora zaidi? Na Biblia hutoa ahadi gani juu ya wafu?

      Wakati Ujao Wenye Amani

      Muumba ameahidi kwamba karibuni atakomesha jamii ya ulimwengu iliyopo ambayo iko chini ya uongozi wa Shetani. (Mithali 2:21, 22; Danieli 2:44) Jamii mpya adilifu ya kibinadamu—“dunia mpya”—itakuwa uhalisi wakati huo. (2 Petro 3:13) Wakati huo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Hata maumivu makali ya kifo yataondolewa mbali, kwa kuwa Mungu “atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu halitakuwapo tena kamwe. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.”—Ufunuo 21:4.

      Kwa habari ya wale wakaao katika ulimwengu mpya wa Mungu ulioahidiwa, mtunga-zaburi alitabiri hivi: “Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele.” (Zaburi 37:29) Isitoshe, wasikivu “watajifurahisha kwa wingi wa amani.”—Zaburi 37:11.

      Mukundbhai, aliyetajwa katika makala iliyotangulia, amelala usingizi katika kifo bila kujua ahadi za ajabu za Mungu. Lakini mamilioni ya watu ambao wamekufa bila kumjua Mungu wana tazamio la kuamshwa katika ulimwengu huo mpya wenye amani, kwa kuwa Biblia yaahidi hivi: “Kutakuwa na ufufuo wa waadilifu na wasio waadilifu pia.”—Matendo 24:15; Luka 23:43.

      Neno “ufufuo” latafsiriwa hapa kutoka neno la Kigiriki a·naʹsta·sis, linalomaanisha kihalisi “kusimama tena.” Hivyo ufufuo huhusisha kutendesha upya kwa kiolezo cha maisha ya mtu.

      Muumba wa mbingu na dunia ana hekima isiyo na kikomo. (Ayubu 12:13) Kukumbuka violezo vya maisha za wafu si tatizo kwake. (Linganisha Isaya 40:26.) Yehova Mungu pia ana upendo mwingi. (1 Yohana 4:8) Kwa sababu hiyo, yeye aweza kutumia kumbukumbu lake kamilifu, si kwa minajili ya kuadhibu wafu kwa sababu ya ubaya ambao wamefanya, bali ili kuwarudisha kwenye uhai katika dunia iliyo paradiso wakiwa na utu waliokuwa nao kabla hawajafa.

      Kwa mamilioni ya watu kama Mukundbhai, ufufuo utamaanisha kuwa na wapendwa wao tena. Lakini wazia uwezalo kumaanisha kwa wale wanaoishi sasa. Kwa kielelezo, chukua mwana wa Mukundbhai, ambaye amekuja kujua kweli ya ajabu juu ya Mungu na makusudi yake. Yafariji kama nini kwake kujua kwamba baba yake hakukwama katika duru isiyoelekea kwisha ya kuzaliwa upya mara nyingi, kila duru ikiwa imezingirwa na uovu na kuteseka! Yeye amelala usingizi tu katika kifo, akingojea ufufuo. Yasisimua kama nini kwake kutafakari uwezekano wa kushiriki na babaye siku moja yale ambayo yeye mwenyewe amejifunza kutoka katika Biblia!

      Ni mapenzi ya Mungu “kwamba watu wa namna zote waokolewe na kuja kwenye ujuzi sahihi wa kweli.” (1 Timotheo 2:3, 4) Sasa ndio wakati wa kujifunza jinsi wewe, pamoja na mamilioni ya watu wengine ambao tayari wanafanya mapenzi ya Mungu, waweza kuishi milele katika dunia iliyo paradiso.—Yohana 17:3.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki