Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Ni Nini Kingekuwa Bora Zaidi kwa Mtoto?
    Amkeni!—1997 | Desemba 8
    • Ni Nini Kingekuwa Bora Zaidi kwa Mtoto?

      KUTALIKI au kutotaliki? Hili ni swali kuu katika akili za watu wengi waliooana wasio na furaha. Miaka mingi iliyopita talaka ilichukiwa, na mara nyingi ilishutumiwa, kwa sababu za kiadili na kidini. Na kwa kawaida wazazi wowote waliooana wasio na furaha walikaa pamoja kwa ajili ya watoto wao. Hata hivyo, katika nyakati za karibuni viwango vya ulimwengu huu vimebadilika sana. Leo, talaka yakubalika kwa wengi.

      Lakini ijapokuwa talaka yakubalika, idadi yenye kuongezeka ya wazazi, mahakimu, wanasayansi wa kijamii, na wengine, wanaeleza hangaikio lao kuhusu matokeo mabaya ya talaka kwa watoto. Sasa maoni zaidi ya hadhari yanasikika. Uthibitisho wenye kuongezeka waonyesha kuwa talaka yaweza kuwa na matokeo yenye kuangamiza kabisa kwa mtoto. Wazazi wanasihiwa kufikiria matokeo ya talaka kwao wenyewe na kwa watoto wao. Mwanasoshiolojia Sara McLanahan, wa Chuo Kikuu cha Princeton, ataarifu kwamba “kati ya thuluthi mbili na robo tatu za familia zinazotaliki labda zapaswa kulipatia wakati zaidi na kulifikiria zaidi ikiwa wanafanya jambo lililo sawa.”

      Uchunguzi wa hivi karibuni waonyesha kuwa watoto wa talaka wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata mimba wakiwa matineja, kukataa shule, kushuka moyo, kutaliki katika ndoa zao wenyewe, na kuwa wapokeaji wa msaada. Katika nchi za Magharibi, mtoto 1 kati ya 6 huathiriwa na talaka. Mwanahistoria Mary Ann Mason, katika kitabu chake kuhusu malezi ya mtoto katika Marekani, aonelea hivi: “Mtoto aliyezaliwa katika 1990 alikuwa na karibu nafasi ya asilimia 50 ya kuwa katika mamlaka ya mahakama katika kesi inayohusu mahali mtoto huyo atakapoishi na ataishi na nani.”

      Kwa kusikitisha, wakati wote uhasama hauishii na talaka, kwani wazazi waweza kuendelea kupigana katika mahakama kuhusu malezi ya watoto na haki za kutumia wakati nao, wakiwaongezea watoto wao mkazo. Makabiliano haya ya kihisia-moyo yenye upinzani katika mazingira ya chumba cha mahakama hujaribu uaminifu-mshikamanifu wa watoto kwa wazazi wao na mara nyingi huwafanya wajihisi kuwa wasio na nguvu na wenye hofu.

      Mshauri wa familia alisema: “Talaka haiwaokoi watoto. Wakati mwingine huwaokoa watu wazima.” Uhalisi ni kwamba kwa kutalikana, wazazi waweza kutatua matatizo yao wenyewe, lakini kwa wakati uleule, wanaweza kusababisha hasara kwa watoto wao, ambao waweza kutumia muda uliobaki wa maisha yao wakijaribu kulipia hasara hiyo.

      Machaguo ya Malezi ya Mtoto

      Katika uhasama na mkazo wa kihisia-moyo katika talaka, ni vigumu sana kuzungumzia ni nani atakayepewa malezi ya watoto ya baadaye katika hali yenye utulivu na ya kimantiki. Ili kupunguza makabiliano ya wazazi na kuepuka upinzani katika mahakama, mamlaka fulani ya mahakama hutoa njia ya badala ya kusuluhisha mabishano, kama vile upatanisho nje ya mahakama.

      Ukishughulikiwa vizuri, upatanisho huwaruhusu wazazi kufikia upatano badala ya kuachia hakimu uamuzi juu ya watoto. Ikiwa upatanisho hauwezekani, wazazi waweza kufikia upatano wa malezi na haki za kutumia wakati na watoto kupitia kwa mawakili wao. Wazazi wafikiapo upatano na kuuandika katika maandishi, hakimu aweza kuweka sahihi agizo lililo na matakwa yao.

      Wakati wazazi hawawezi kukubaliana kuhusu mpango wa malezi, mfumo wa sheria katika nchi nyingi utatoa namna ya kujaribu kuhakikisha kuwa faida za watoto zinalindwa. Hangaikio kuu la hakimu litakuwa watoto, si wazazi. Hakimu atafikiria mambo mengi yanayohusiana, kama vile matakwa ya wazazi, uhusiano wa mtoto na wazazi wote wawili, upendeleo wa mtoto, na uwezo wa kila mzazi wa kuandaa utunzaji wa kila siku. Kisha hakimu ataamua mtoto ataishi wapi na ataishi na nani vilevile jinsi wazazi watakavyofikia maamuzi ya maana kuhusu wakati ujao wa mtoto.

      Katika makubaliano ya mzazi mmoja kuwa mlezi, huenda mzazi huyo akawa na mamlaka ya kufanya maamuzi. Katika makubaliano ya malezi ya pamoja, wazazi wote wawili lazima wakubaliane katika maamuzi muhimu, kama vile utunzaji wa afya ya mtoto na elimu.

      Maswali Yawezayo Kukabiliwa

      Wanapokabili hali ya kwenda mahakamani kwa ajili ya malezi ya mtoto, wazazi walio Mashahidi wa Yehova ni lazima wafikirie pia kilicho bora zaidi kwa habari ya hali ya kiroho ya watoto. Kwa kielelezo, namna gani ikiwa mzazi asiye Shahidi anapinga kuwazoeza watoto kwa kupatana na Biblia? Au namna gani ikiwa mzazi asiye Shahidi ametengwa na ushirika wa kutaniko la Kikristo?

      Hali kama hizi zaweza kufanya iwe vigumu zaidi kwa wazazi Wakristo kufanya maamuzi. Wanataka kutenda katika njia yenye hekima na yenye kiasi, na pia wanataka kudumisha dhamiri safi mbele ya Yehova wanapoyafikiria kwa sala yaliyo bora zaidi kwa watoto.

      Katika makala zifuatazo, tutaangalia maswali kama haya: Inapompa mzazi malezi ya watoto, sheria husema nini kuhusu dini? Naweza kukabilianaje kwa mafanikio na magumu ya kesi ya malezi kwa mafanikio? Naweza kukabilianaje na kupoteza malezi ya watoto wangu? Nayaonaje makubaliano ya malezi pamoja na mzazi aliyetengwa na ushirika?

  • Malezi ya Mtoto—Dini na Sheria
    Amkeni!—1997 | Desemba 8
    • Malezi ya Mtoto—Dini na Sheria

      KATIKA kesi za talaka na malezi ya mtoto, dini yaweza kuwa jambo la maana—na lililo tata. Kwa kielelezo, maswali kama haya yafuatayo yaweza kutokea.

      Je, hakimu apaswa kufikiria ushuhuda akidai kuwa mzazi mmoja ni asiyestahili kuwa mlezi wa mtoto kwa sababu mzazi huyo ni mshiriki wa dini fulani, hasa dini isiyo mashuhuri? Je, hakimu apaswa kufikiria ushuhuda kuhusu itikadi na mazoea ya kidini ya wazazi ili aweze kuamua ni dini ipi ingekuwa bora zaidi kwa mtoto, kulingana na maoni yake? Je, basi apaswa kuamuru kwamba mtoto alelewe katika dini hiyo na akataze kabisa mtoto kufunuliwa kwa dini nyinginezo?

      Leo, watu wengi zaidi na zaidi wanaoa au kuolewa katika dini na malezi ya kabila tofauti na yao. Kwa hiyo wenzi hawa wanapotalikana, watoto huenda tayari wakawa na uhusiano katika dini mbili tofauti. Wakati mwingine, mzazi anayehusika katika mashauri ya talaka huenda karibuni akawa amekubali kirasmi dini fulani ambayo ni tofauti na ile aliyokuwa nayo hapo awali. Ushirika wa dini mpya huenda ukawa jambo la kuimarisha katika maisha ya mzazi huyo na la maana sana kwake lakini usiojulikana kwa watoto. Hivyo swali jingine latokea, Je, mahakama yaweza kumzuia mzazi kuwapeleka watoto katika ibada za kidini za dini hiyo kwa sababu tu ni tofauti na dini ambayo wazazi hao waliizoea hapo awali?

      Haya ni maswali magumu. Yahitaji hakimu kufikiria si mahitaji ya mtoto tu bali pia mapendezi na haki za wazazi.

      Haki za Msingi za Wazazi na Watoto

      Ni kweli kuwa mahakimu waweza kushawishiwa na maoni yao ya kibinafsi ya kidini. Lakini katika nchi nyingi si rahisi kwa haki za kidini za wazazi au za mtoto kupuuzwa. Nchi hizi huenda zikawa na katiba ambazo huwakataza mahakimu kutozuia haki za msingi za wazazi za kuelekeza malezi ya mtoto, kutia ndani elimu na mafunzo ya kidini ya mtoto.

      Kwa upande ule mwingine, mtoto vilevile ana haki ya kupokea mazoezi kama haya kutoka kwa wazazi wake. Kabla ya hakimu kuingilia kisheria mazoezi ya kidini ya mtoto, mahakama lazima isikie uthibitisho wenye kusadikisha kwamba “mazoea hususa ya kidini yanatokeza tisho la papohapo na kubwa kwa hali njema ya kimwili ya mtoto.” (Italiki ni zetu.) Tofauti za kidini tu au hata uhasama kati ya wazazi kuhusu dini haitoshi kuipa serikali haki ya kuingilia.

      Katika Nebraska, Marekani, msimamo wenye ufikirio uliochukuliwa na mama aliye mmoja wa Mashahidi wa Yehova katika bishano la malezi watolea kielezi jinsi ambavyo maandalizi ya kisheria huwalinda wazazi wote wawili na watoto. Baba asiye Shahidi hakutaka binti yao ahudhurie ibada za kidini za Mashahidi wa Yehova katika Jumba la Ufalme. Mahakama ya chini zaidi ilikubaliana na baba huyo.

      Kisha mama huyo akakata rufani kwenye Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Nebraska. Mama huyo alibisha kuwa hakukuwa na uthibitisho wowote wa papohapo au mkubwa wa tisho kwa hali njema ya mtoto katika utendaji wowote wa Mashahidi wa Yehova. Mama huyo alitoa ushuhuda “kwamba kuhudhuria na kushiriki katika utendaji wa kidini wa wazazi wote wawili kungemwandalia . . . mtoto msingi wa kuamua ni dini ipi ambayo angependelea afikapo umri wa kutosha kuelewa.”

      Mahakama ya juu zaidi ilibadili uamuzi wa mahakama ya chini zaidi na ikatoa hukumu kuwa “mahakama ya chini zaidi ilitumia vibaya busara yake katika kuwekea mipaka haki ya mama mlezi ya kuongoza malezi ya kidini ya mtoto wake mchanga.” Hakukuwa na uthibitisho wowote kuwa huyo mtoto alikuwa akidhuriwa na kuhudhuria ibada za kidini katika Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova.

      Haki za Wazazi Wasio Walezi

      Wakati mwingine, wazazi waliotalikana hujaribu kutumia mabishano kuhusu mazoezi ya kidini kama njia ya kupata udhibiti wa watoto. Kwa kielelezo, katika Khalsa v. Khalsa, kesi katika jimbo la New Mexico, Marekani, wazazi wote wawili walikuwa wamezoea Dini ya Sikh wakati wa ndoa yao. Lakini muda mfupi baada ya kutalikana, mama huyo akageuka kuwa Mkatoliki na akaanza kuwavunja moyo watoto wasizoee Dini ya Sikh.

      Baba alikasirika, akalipeleka jambo hilo mahakamani katika jaribio la kupata mamlaka zaidi ya kuelekeza mazoezi ya kidini ya watoto wake kuelekea Dini yake ya Sikh. Mahakama iliitikiaje ombi la baba huyo? Ilikataa ombi lake. Mahakama iliamuru kuwa “wakati watoto walipokuwa [naye], hawangeweza kushiriki kwa hiari ama kwa kulazimishwa katika utendaji wowote wa Sikh, kutia ndani utendaji wowote wa kanisa, kambi ya Sikh au siku ya utunzaji katika kitovu cha Sikh.”

      Baba huyo alikata rufani uamuzi huo kwenye Mahakama ya Rufani ya New Mexico. Mahakama hii ya juu zaidi ilikubaliana na baba huyo na ikabadili uamuzi wa mahakama hiyo ya chini. Mahakama ya rufani ilitaarifu hivi: “Mahakama zapaswa kushikamana sana na sera ya kutopendelea kati ya dini, na yapaswa kuingilia katika eneo hili nyetivu na lenye kulindwa kikatiba ambapo tu kuna uthibitisho wa wazi na wenye kuthibitika wa dhara kwa watoto. Vizuizi katika eneo hili vyatokeza hatari ya kwamba mipaka iliyowekwa na mahakama itaingilia kwa njia inayopinga katiba uhuru wa kuabudu wa mzazi au itaonwa kuwa na athari hiyo.”

      Uamuzi kama huo wafuata mstari mrefu wa kanuni ambazo zimeimarishwa vema katika nchi nyingi. Mzazi mwenye kukubali sababu atafikiria kanuni hizi. Kwa kuongezea, mzazi Mkristo atafikiria kwa uangalifu uhitaji wa mtoto wa kuwasiliana na wazazi wote wawili, na pia jukumu la mtoto la kuonyesha heshima kwa mama na baba.—Waefeso 6:1-3.

      Upatanisho Nje ya Mahakama

      Ijapokuwa upatanisho nje ya mahakama huenda usiwe rasmi sana kama kusikia mbele ya hakimu, mzazi hapaswi kuuchukulia kwa njia isiyo rasmi. Makubaliano yoyote ya pamoja au mkataba wowote uliofikiwa katika utaratibu huu wa malezi waweza kufungwa kwa maagizo ya mahakama ya baadaye. Kwa hiyo, lingekuwa jambo la hekima kwa mzazi kutafuta habari kutoka kwa mwanasheria wa mambo ya familia mwenye uzoefu ili kuhakikisha kwamba mambo yote yanayohusiana na malezi yanashughulikiwa ifaavyo na kwa usawa.

      Kila mzazi lazima achukue wakati wa kujitayarisha kwa ajili ya utaratibu wa upatanisho. Tabia ya mzazi kuelekea wengine na mwenendo wake wakati wa utaratibu wa upatanisho waweza kuathiri sana matokeo. Mara nyingi sana, wazazi wanaotalikana huwa na hisia nyingi sana kuelekea hatua hiyo ya talaka hivi kwamba wanakosa kuona masuala ya maana: Ni nini lililo bora zaidi kwa mtoto? Mtoto anahitaji nini ili akue kiakili, kihisia-moyo, na kimwili?

      Kumbuka kwamba katika maoni ya kisheria, jambo la msingi katika upatanisho si tofauti ya kidini au ya jambo jingine lolote la kibinafsi, bali ni jinsi wazazi wawezavyo kupata njia ya kukubaliana na kutafuta mapatano kwa ajili ya manufaa ya watoto. Huenda mzazi akakabiliwa na ubaguzi wa kidini, au ubaguzi mwingine wowote, maswali yasiyotazamiwa, au miongozo ya hila iliyokusudiwa kufadhaisha na kukasirisha. Kasoro za kila mzazi huenda zikatokezwa wazi au hata kutiliwa chumvi. Hata hivyo, wanaohusika wanapobaki wakiwa wenye kukubali sababu, azimio laweza kufikiwa.

      Wakati mwingine, utaratibu wa upatanisho waweza kuonekana ukichukua muda mrefu na wenye kuvunja moyo. Kibadala ni hatua ya mahakama yenye kuchukua wakati mrefu, pamoja na kutiwa aibu kwa waziwazi, mzigo wenye kulemea wa kifedha, na athari zenye hasara kwa mtoto. Hili kwa hakika si lenye kutamanika. Kama vile na matatizo mazito yote maishani, mzazi Mkristo atataka kufikia utaratibu wa upatanisho kwa sala, akikumbuka mwaliko uliopuliziwa “umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini, naye atafanya.”—Zaburi 37:5.

      Lakini namna gani ikiwa suluhisho haliwezi kufikiwa na hakimu anampa malezi ya mtoto yule mzazi mwingine? Au namna gani ikiwa mmoja wa wazazi wanaotalikana ametengwa na ushirika wa kutaniko la Kikristo? Pia, mmoja apaswa kuonaje malezi ya pamoja na ya mzazi mmoja tu? Maswali haya na kanuni za Biblia zinazohusiana zitazungumziwa katika makala ifuatayo.

      [Sanduku katika ukurasa wa 6]

      Sifa Tatu za Maana

      Hakimu mmoja wa mahakama ya familia aliyehojiwa na Amkeni! alisema kuwa kati ya sifa zilizo muhimu atafutazo katika mzazi ni hizi tatu zifuatazo:

      Kukubali Sababu—kuwa tayari kumruhusu mzazi yule mwingine wakati wa kuwa na mtoto (ikiwa tu hakuna tisho la kimwili au la kiadili kwa mtoto)

      Kuwa Mwenye Hisia Nyepesi—ufahamu wa mahitaji ya kihisia-moyo ya mtoto

      Kujidhibiti—maisha ya kinyumbani yenye usawaziko ambayo yangechangia hali yenye utulivu ambapo mtoto angenawiri

      Miongozo ya Kihukumu

      Kwa kuweka miongozo, mahakimu fulani wamejaribu kuepuka mizozano isiyo ya lazima kuhusu viwango vya kidini vya mzazi. Kwa kielelezo:

      1. Uhusiano wenye maana kati ya mtoto na wazazi wote wawili wapasa kukaziwa. Hakimu John Sopinka wa Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada alionelea kwamba kila mzazi apaswa kukubaliwa “kushiriki katika utendaji ambao utachangia kumtambulisha mzazi kuwa alivyo hasa [kutia ndani mazoea ya dini yake]. Mzazi asiye mlezi hatarajiwi kujifanya asivyo au kuchukulia mtindo-maisha wenye udanganyifu wakati anapokuwa na watoto.”

      2. Kumzuia mzazi asiye mlezi asimfunze mtoto itikadi zake za kidini ni kuhalifu uhuru wa kidini wa huyo mzazi, isipokuwa pale ambapo kuna uthibitisho wa wazi wa madhara ya papohapo au makubwa kwa mtoto.

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Mahakimu wana jukumu zito katika kesi za malezi

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      Mpatanishi anaweza kuwasaidia wazazi kusuluhisha tofauti bila kuwa na utaratibu wa mahakama wenye kuchukua muda mrefu

  • Malezi ya Mtoto—Maoni Yaliyosawazika
    Amkeni!—1997 | Desemba 8
    • Malezi ya Mtoto—Maoni Yaliyosawazika

      MARA nyingi magumu hasa hutokea baada ya talaka, kung’ang’ania shauku na udhibiti wa mtoto. Ule msemo “Kwahitaji wawili ili kupigana vita” si kweli sikuzote. Huenda ikahitaji mzazi mmoja tu aliye na jeuri atakaye mambo yafanywe atakavyo. Mwanasheria wa familia katika Toronto, Kanada, alionelea: “Katika sheria za familia, kila kitu huongozwa na hisia-moyo na hisia za watu zahusika.”

      Badala ya kufikiria lililo bora zaidi kwa mtoto, wazazi wengine huendeleza mabishano kwa muda mrefu kwa kuanzisha majadiliano kuhusu masuala yasiyofaa. Kwa kielelezo, wengine wamejaribu kuthibitisha kuwa malezi yapaswa kubadilishwa kwa kuwa mzazi yule mwingine ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova na atamnyima mtoto ‘njia ya kawaida ya maisha.’

      Yule asiye Shahidi aweza kutoa suala kuhusu kusherehekea sikukuu za kuzaliwa, Krismasi, au hata Halowini. Wengine huenda wakalalamika kuwa ushirika wa mtoto na marekebisho ya kijamii yangezuiwa ikiwa mtoto angeamua kutoisalimu bendera. Au huenda wengine wakapendekeza kuwa mtoto angedhuriwa kisaikolojia kwa kuandamana na mzazi katika kuzungumza na wengine kuhusu Biblia. Wazazi fulani wasio Mashahidi hata wamedai kuwa maisha ya mtoto yangehatarishwa kwa sababu mzazi aliye Shahidi hangetoa idhini kwa mtoto ili atiwe damu mishipani.

      Mkristo hukabilije ugumu wa mabishano kama hayo yenye kujaa hisia? Jibu lenye kujaa hisia—“kuzima moto kwa moto”—halitakuwa na matokeo. Ikiwa jambo hilo lapelekwa mbele ya hakimu, kila mzazi atakuwa na fursa ya kusikiwa. Ni jambo la maana zaidi kukumbuka shauri la Biblia lisemalo: “Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.” (Zaburi 55:22) Kwa kutafakari juu ya kanuni hizi za Biblia na kuzitumia, wazazi wanaweza, kwa msaada wa Yehova, kukabiliana na tukio lolote la mwisho linalohusu malezi ya mtoto.—Mithali 15:28.

      Kukubali Sababu

      Suala kuu ni hali njema ya mtoto. Ikiwa mzazi ni mwenye kudai sana, aweza kupoteza malezi ya mtoto na hata apate kwamba mapendeleo yake ya kutumia wakati na mtoto yamewekewa vikwazo. Mzazi mwenye hekima hujiendesha kwa njia yenye amani, akikumbuka shauri la Biblia lisemalo: “Msirudishe ovu kwa ovu kwa yeyote. . . . Iachieni nafasi hasira ya kisasi . . . Usijiache mwenyewe ushindwe na lililo ovu, bali fuliza kushinda lililo ovu kwa lililo jema.” (Waroma 12:17-21) Iwe ni mahakamani, katika ofisi ya wakili, au pamoja na mkadiriaji wa malezi ya mtoto, wazazi wapaswa ‘kuacha hali yao ya kukubali sababu ijulikane kwa watu wote.’—Wafilipi 4:5.

      Nyakati fulani mwenzi aliyetenganishwa atajaribu kuwadanganya wengine kwa kutokeza matatizo yenye kuongoza vibaya na ya kukisiwa tu. Ni jambo la hekima kupigana dhidi ya mwelekeo wa kibinadamu wa kuitikia kupita kiasi mashambulizi haya ya maneno. Afya, dini, na elimu ni mambo yanayopendwa sana na wenzi waliotenganishwa kwa kutunga hila katika kusikizwa kwa kesi ya kubishania malezi.—Mithali 14:22.

      Kukubali sababu kwatia ndani uwezo wa kufikiria kwa uangalifu mambo ya hakika na kuzungumza ili kufikia makubaliano ya kiasi. Hakuna mzazi apaswaye kusahau kuwa hata baada ya talaka, mtoto bado ana wazazi wawili. Wazazi wametalikana lakini hawajamtaliki mtoto. Kwa hiyo, isipokuwa katika hali zenye kupita kiasi, kila mzazi apaswa kuwa na uhuru wa kutenda kama mzazi wakati anapokuwa na mtoto. Kila mmoja apaswa kuwa na uhuru wa kueleza hisia zake na kanuni zake na kushiriki pamoja na mtoto katika utendaji unaokubalika kisheria, wa kidini au mwingineo.

      Ebu tuchunguze matokeo ya maamuzi yawezayo kufanywa na mahakama: (1) malezi ya pamoja, (2) malezi ya mzazi mmoja, na (3) kuwekewa mipaka kwa mapendeleo ya kuwa na mtoto. Tofauti ni nini kati ya malezi ya pamoja na malezi ya mzazi mmoja? Waweza kukabilianaje unapopoteza malezi? Namna gani ikiwa mzazi mmoja ametengwa na ushirika?

      Malezi ya Pamoja

      Mahakimu wengine huhisi kwamba ni muhimu kusitawisha uwasiliano kati ya mtoto na wazazi wote wawili. Kusababu kwao kwategemezwa na chunguzi za utafiti zinazoonyesha kwamba watoto wanaweza kupatwa na mkazo na madhara ya kihisia-moyo kidogo zaidi baada ya talaka ikiwa wazazi wataweza kushiriki malezi. Badala ya kuhisi kuwa ametupwa na mzazi mmoja, mtoto huyo atakuwa na hisi ya kupendwa na wazazi wote wawili na kushirikishwa katika nyumba zote mbili. “Malezi ya pamoja ni njia ya kuwahusisha wazazi wote wawili,” asema mwanasheria mmoja wa familia.

      Hata hivyo, Dakt. Judith Wallerstein, mkurugenzi mkuu wa Kitovu cha Mabadiliko Katika Familia, katika Corte Madera, California, aonya kwamba kufanya malezi ya pamoja yafaulu, yahitaji wazazi wenye ushirikiano na mtoto ambaye ni mwenye kubadilikana na mwenye kupatana na watu. Sifa hizi ni za maana kwa sababu katika malezi ya pamoja wazazi wote wawili hudumisha haki ya kisheria ya kushiriki katika kufanya uamuzi kuhusu masuala makuu yanayohusu afya, elimu, malezi ya kidini, na maisha ya kijamii ya mtoto wao. Lakini hili hufanikiwa tu ikiwa wazazi wote wawili wanabaki wakiwa wenye kukubali sababu katika kufikiria lililo jema zaidi kwa mtoto wao badala ya linalowapendeza kibinafsi.

      Malezi ya Mzazi Mmoja

      Huenda mahakama ikampa malezi mzazi ambaye, katika maoni yake, aweza kuandaa vizuri zaidi mahitaji ya mtoto. Huenda hakimu akaamua kwamba mzazi mlezi awe ndiye pekee afanyaye maamuzi kwa habari ya masuala ya maana yanayohusu hali njema ya mtoto. Mara nyingi, mahakama hufikia uamuzi huo baada ya kusikiliza matokeo ya uchunguzi wa wakadiriaji—hawa kwa kawaida huwa ni wanasaikolojia, madaktari wa magonjwa ya akili, au wafanyakazi wa umma.

      Watetezi wa malezi ya mzazi mmoja huhisi kuwa mpango huo humwezesha mtoto kuwa imara zaidi. Wazazi wanaposhindwa kuwasiliana au wanapoelekea kutowasiliana pamoja kwa matokeo, mahakimu wengi wa kesi hupendelea mpango huu wa malezi. Bila shaka, mzazi asiye mlezi haachwi nje kabisa ya maisha ya mtoto. Haki za kutumia wakati pamoja na mtoto kwa kawaida hupewa mzazi asiye mlezi, na wazazi wote wawili wanaweza kuendelea kumwandalia mtoto mwongozo, upendo, na shauku inayohitajiwa.

      Mapendeleo ya Kutumia Wakati Pamoja na Mtoto

      Ni jambo lisilo la hekima kwa wazazi kuona malezi ya mtoto kama kuna “mshindi” na “aliyeshindwa.” Wazazi hufanikiwa na wanakuwa “washindi” wanapowaona watoto wao wakikua kuwa watu wazima waliokomaa, hodari, na wenye kuheshimika. Kufaulu katika kulea mtoto hakutegemei ni nani amepewa malezi ya mtoto na sheria. Kwa kutii masharti ya sheria za mahakama katika mambo ya malezi ya mtoto, hata wakati yaonekanapo kuwa yasiyo haki, Mkristo ataonyesha “ujitiisho kwa mamlaka zilizo kubwa.” (Waroma 13:1) Ni la maana pia kukumbuka kuwa huu si wakati wa kupigania shauku au uaminifu-mshikamanifu wa watoto wako kwa kumdharau yule mzazi mwingine katika jaribio la kuharibu uhusiano wake nao.

      Kuna vielelezo vya Biblia vya wazazi wenye kumhofu Mungu ambao, kwa sababu tofauti-tofauti walitenganishwa na watoto wao. Kwa kielelezo, Amramu na Yokebedi, wazazi wa Musa, wakitenda kwa hali njema zaidi ya mtoto wao, walimweka katika kisafina chenye kuelea “akakiweka katika majani kando ya mto.” Wakati huyu mtoto mchanga sana alipopatikana na binti Farao, walidumisha tumaini lao katika Yehova. Wazazi hawa wenye hekima na wenye imani walithawabishwa kwa kupewa mapendeleo ya “kutumia wakati pamoja naye” ambao waliutumia kwa matokeo kumzoeza mvulana huyo katika njia ya Yehova. Musa akakua kuwa mtumishi mwenye kutokeza wa Mungu wa kweli.—Kutoka 2:1-10; 6:20.

      Ingawa hivyo, namna gani ikiwa mzazi mmoja ametengwa na ushirika? Je, mzazi aliye Mkristo apaswa kumruhusu kutumia wakati na mtoto? Hatua ya kutenga na ushirika wa kutaniko hubadili tu uhusiano wa kiroho kati ya mtu huyo na kutaniko la Kikristo. Kwa kweli, hutenganisha vifungo vya kiroho. Lakini uhusiano wa mzazi na mtoto hubaki bila kuguswa. Mzazi aliyepewa malezi anapaswa kuheshimu haki za mzazi aliyetengwa na ushirika za kutumia wakati pamoja na mtoto. Hata hivyo, ikiwa mzazi aliye mlezi atokeza tisho la papohapo au kubwa kwa hali njema ya mtoto ya kimwili au ya kihisia-moyo, basi mahakama (si mzazi mlezi) yaweza kupanga kuwe na mtu wa tatu mtoto anapotumia wakati na mzazi huyo mwingine.

      Hauwi Peke Yako Kamwe

      Mashauri ya talaka na mabishano ya malezi ya mtoto ya baadaye huwa yenye kuchosha kihisia-moyo. Ndoa ambayo ilianza kukiwa na matumaini sasa imevunjwa-vunjwa pamoja na miradi walioitamani, mipango, na matarajio ya wenzi hao. Kwa kielelezo, kukosa uaminifu au kutendwa vibaya sana kwaweza kumfanya mke mwaminifu-mshikamanifu kutafuta ulinzi wa kisheria kwake na kwa mtoto wake. Lakini, hisia za hatia na za kutostahili zaweza kuendelea anapofikiria kwa makini kosa lilikuwa nini au jinsi ambavyo mambo yangaliweza kushughulikiwa kwa matokeo zaidi. Wenzi wengi wa ndoa huhofia jinsi watoto wao watakavyotenda kuelekea kuvunjika kwa familia. Kushindana mahakamani kwa ajili ya malezi kwaweza kuwa hali ya kubadilika-badilika kihisia-moyo ambayo haitahini tu uaminifu-maadili wa mtu akiwa mzazi, bali pia hujaribu imani ya mtu na itibari yake katika Yehova.—Linganisha Zaburi 34:15, 18, 19, 22.

      Mwenzi asiye na hatia achaguapo kuchukua hatua kwa sababu ya kutendwa vibaya kwa mtoto au kutendwa vibaya kupita kiasi kwa mwenzi au kulinda afya yake dhidi ya hatari ya maradhi yenye kuambukizwa kingono kutoka kwa mwenzi asiye mwaminifu, hakuna sababu kwa mwenzi huyo asiye na hatia kuhisi hatia au kuhisi kwamba ameachwa na Yehova. (Zaburi 37:28) Mwenzi asiye mwaminifu au mwenye kutenda vibaya ndiye ameuchafua mkataba mtakatifu wa ndoa na ‘ametenda kwa hiana’ kwa mwenzi wake.—Malaki 2:14.

      Endelea kuwa na “dhamiri njema” mbele ya wanadamu na mbele ya Yehova kwa kutumia kanuni za Biblia, ukimtendea mwenzi wako mliyetenganishwa naye kwa kufuatia haki, na kuonyesha kunyumbulika katika mapatano yenu ya malezi. “Ni bora kuteseka kwa sababu mnatenda mema, ikiwa mapenzi ya Mungu yataka hivyo, kuliko kwa sababu mnatenda ovu.”—1 Petro 3:16, 17.

      Kwa habari ya watoto, wanahitaji uhakikishio kwamba mvunjiko wa familia haukuwa kosa lao. Wakati mwingine mambo hayaendi vile yalivyopangiwa. Lakini kutumia kanuni za Biblia kwaweza kupunguza athari ya talaka kwa kutia moyo kuwe na mazungumzo ya wazi na yenye uelewevu kati ya wazazi na watoto. Kwa kielelezo, hili laweza kufanywa kwa kuwaruhusu watoto wawe na sehemu katika kupangia maisha ya familia ya baada ya talaka. Kwa kuwa na subira na mwenye fadhili na kwa kupendezwa na hisia za watoto na kusikiliza maelezo yao, utafanya mengi katika kuwasaidia kujipatanisha na ratiba na mipango mipya ya kuishi.

      Wengine Waweza Kusaidia

      Si wazazi tu wanaoweza kumsaidia mtoto anayepitia mvunjiko wa familia. Washiriki wa familia, walimu, na marafiki waweza kufanya mengi kuunga mkono na kuwatia moyo watoto wa talaka. Hasa wazakuu waweza kufanya mengi kuchangia usawaziko wa watoto na hali njema ya kihisia-moyo.

      Wazakuu Wakristo waweza kuwaandalia watoto mafunzo ya kiroho na utendaji wenye kujenga, lakini wapaswa kuwa wenye staha kuelekea maamuzi ya wazazi kuhusu mazoezi ya kidini, kwa kuwa ni wazazi, si wazakuu, walio na mamlaka ya kiadili na kisheria ya kufanya maamuzi haya.—Waefeso 6:2-4.

      Wakiwa na tegemezo kama hilo, watoto wa talaka waweza kuvumilia mvunjiko wa ndoa ya wazazi wao. Na waweza kuendelea kutazamia mbele baraka za ulimwengu mpya wa Mungu, ambapo familia zote zitakuwa huru kutoka katika “utumwa wa uharibifu na kuwa na uhuru wenye utukufu wa watoto wa Mungu.”—Waroma 8:21; 2 Petro 3:13.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki