Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kitabu Cha Biblia Namba 31—Obadia
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
    • 1. Ni nini kinachoonyesha ujumbe ndio wa maana, wala si mjumbe?

      KATIKA mistari 21 tu, Obadia, kitabu kilicho kifupi zaidi ya vyote vya Maandiko ya Kiebrania, chatangaza juu ya hukumu ya Mungu iliyoleta mwisho wa taifa, huku kikitabiri shangwe ya ushindi ya hatimaye ya Ufalme wa Mungu. Maneno ya utangulizi yaeleza hivi tu: “Maono yake Obadia.” Mahali na wakati alipozaliwa, ni wa kabila gani, maelezo marefu juu ya maisha yake—hakuna lolote la hayo linalosemwa. Kwa uwazi, utambulisho wa nabii huyo silo jambo lililo la maana; ujumbe huo ndio wa maana, na uko hivyo kwa kufaa, kwa sababu kama vile Obadia mwenyewe alivyotangaza, huo ni ‘habari kutoka kwa Yehova.’

      2. Unabii wa Obadia wakaza fikira juu ya nchi gani, na ni nini kilichofanya wakaaji wayo wahisi wakiwa salama?

      2 Habari hiyo yavuta uangalifu wayo mkuu juu ya Edomu. Likianzia kusini kutoka Bahari ya Chumvi kandokando ya Araba, bara la Edomu, ambalo pia lajulikana kuwa Mlima Seiri, ni nchi yenye mawe-mawe iliyo na milima mirefu na vibonde vya kina kirefu. Kwenye vituo fulani, mfululizo huo wa milima kuelekea mashariki mwa Araba wafikia mwinuko wa meta 1,700. Wilaya ya Temani ilijulikana sana kwa ajili ya hekima na moyo mkuu wa watu wayo. Umbo la bara lenyewe, pamoja na kinga zayo za asili, lilifanya wakaaji walo wahisi wakiwa salama na wenye fahari.a

      3. Je! Waedomi walikuwa wametenda kama ndugu kwa Israeli?

      3 Waedomi walikuwa wazao wa Esau, ndugu ya Yakobo. Jina la Yakobo lilibadilishwa kuwa Israeli, na kwa hiyo Waedomi walikuwa na uhusiano wa karibu na Waisraeli; hivi kwamba wakawaona kuwa ‘ndugu.’ (Kum. 23:7) Hata hivyo mwenendo wa Edomu haukuwa wa kidugu hata kidogo. Muda mfupi kabla ya Waisraeli kuingia Bara Lililoahidiwa, Musa alimpelekea habari mfalme wa Edomu akiomba ruhusa ya kupitia bara lake kwa amani, lakini kwa kuonyesha uadui, Waedomi walikataa bila huruma, na wakaunga mkono katao lao kwa kujionyesha nguvu zao. (Hes. 20:14-21) Ingawa walitiishwa na Daudi, baadaye wao pamoja na Amoni na Moabu walitungia Yuda hila katika siku za Yehoshafati, wakamwasi Mfalme Yehoramu mwana wa Yehoshafati, wakatia mikononi mwao mateka Waisraeli kutoka Gaza na Tiro, na kuvamia Yuda katika siku za Mfalme Ahazi ili wachukue mateka wengi hata zaidi.—2 Nya. 20:1, 2, 22, 23; 2 Fal. 8:20-22; Amo. 1:6, 9; 2 Nya. 28:17.

      4. (a) Ni kitendo gani cha kudharaulika ambacho chaonekana wazi ndicho kilichotokeza msingi wa tangazo la hukumu la Obadia juu ya Edomu? (b) Ni uthibitisho gani unaodokeza kwamba 607 K.W.K. waelekea zaidi kuwa ndiyo tarehe ya uandikaji?

      4 Uadui huo ulifikia kilele katika 607 K.W.K. wakati Yerusalemu lilipofanywa ukiwa na vikosi vya Kibabuloni. Waedomi hawakulitazama jambo hilo kwa kulikubalia tu bali pia walihimiza washindaji hao wakamilishe kabisa ukiwa huo. “Bomoeni! Bomoeni hata misingini!” ndivyo walivyopaaza sauti. (Zab. 137:7) Kura zilipotupwa kuhusu nyara zilizotekwa, wao walikuwa miongoni mwa wale ambao wangeshiriki uporaji huo; na wakati watoro kati ya Wayahudi walipojaribu kutoroka kutoka bara hilo, wao walifunga barabara na kuwatia mikononi mwa adui. Kwa wazi jeuri hiyo ya wakati wa uharibifu wa Yerusalemu ndiyo msingi wa tangazo la hukumu lililoandikwa na Obadia, na bila shaka liliandikwa wakati kitendo chenye kudharaulika cha Edomu kilipokuwa kingali kibichi akilini. (Oba. 11, 14) Kwa kuwa Edomu yenyewe yaonekana ilitekwa na kunyang’anywa mali zayo na Nebukadreza katika muda wa miaka mitano baada ya uharibifu wa Yerusalemu, kitabu hicho lazima kiwe kiliandikwa kabla ya wakati huo; 607 K.W.K. wadokezwa kuwa ndio waelekea zaidi kuwa tarehe yenyewe.

      5. (a) Ni nini kinachotoa uthibitisho wa kwamba maandishi ya Obadia ni asilia na kweli? (b) Obadia alitimizaje matakwa ya nabii wa kweli, na kwa nini jina lake lafaa?

      5 Unabii wa Obadia juu ya Edomu ulitimizwa—wote! Katika kufikia upeo wao, unabii huo waeleza hivi: “Nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa BWANA [Yehova, NW] amesema hayo.” (Mst. 18) Edomu iliishi kwa upanga na ilikufa kwa upanga, na hakuna kidalili chochote cha kubakia kwa wazao wayo. Hivyo maandishi hayo yathibitishwa kuwa ni asilia na kweli. Obadia alikuwa na sifa zote za nabii wa kweli: Yeye alinena kwa jina la Yehova, unabii wake uliheshimu Yehova, na ulitimia kama vile ilivyothibitishwa na historia iliyofuata. Jina lake kwa kufaa lamaanisha “Mtumishi wa Yehova.”

      YALIYOMO KATIKA OBADIA

      6. Yehova anenaje juu ya Edomu, na ni kutoka wapi yeye ataishusha chini?

      6 Hukumu juu ya Edomu (Mist. 1-16). Kwa amri ya Yehova, Obadia ajulisha njozi yake. Mataifa yaagizwa yaje kujiunga katika vita juu ya Edomu. “Inukeni ninyi; na tuinuke tupigane naye,” Mungu aamuru. Ndipo, akielekeza maneno yake kwa Edomu yenyewe, akadiria-kadiria msimamo iliyo nao. Edomu ni ndogo tu miongoni mwa mataifa na ni yenye kudharaulika, hata hivyo yajivuna kwa kimbelembele. Yahisi ikiwa salama kwa kukaa miongoni mwa majabali yaliyoinuka sana, ikiwa na uhakika kwamba hakuna awezaye kuishusha chini. Hata hivyo, Yehova atangaza kwamba hata kama makao yayo yangekuwa ya juu sana kama ya tai, hata kama ingefanya kiota chayo kiwe miongoni mwa nyota zenyewe, kutoka huko yeye angeishusha chini. Wakati wayo wa adhabu umefika.—Mst. 1.

      7. Ni kwa kadiri gani Edomu itatekwa nyara?

      7 Ni jambo gani litatendeka kwake? Kama wezi wangeteka nyara Edomu, wao wangechukua kile tu walichotaka. Hata wakusanya zabibu wangeacha mabakizio ya kuokotwa na maskini. Lakini kilichoko mbele kwa ajili ya wana wa Esau ni kibaya kuliko hicho. Hazina zao zitanyang’anywa kabisa. Wale wale walio wafungamani wa Edomu ndio watamgeuka. Wale ambao wamekuwa marafiki wake wa karibu watamnasa katika wavu akiwa kama mtu asiye na utambuzi. Wanaume wake wenye kujulikana kwa ajili ya hekima, na mashujaa wake wenye kujulikana kwa ajili ya uhodari wa kivita hawatakuwa msaada katika wakati wa afa lake.

      8. Kwa nini adhabu ya Edomu ni kali sana?

      8 Lakini kwa nini apate hiyo adhabu kali? Ni kwa sababu ya jeuri ambayo wana wa Edomu walitenda wana wa Yakobo, ndugu zao! Wao walishangilia anguko la Yerusalemu na hata kujiunga pamoja na wavamizi wao kugawana nyara zilizotekwa. Kwa kutoa hukumu kali, kama kwamba Obadia ashuhudia matendo hayo maovu sana, Edomu yaambiwa hivi: Hupaswi kushangilia taabu kubwa ya ndugu yako. Hupaswi kuzuia mkimbio wa watoro wake na kuwatia mikononi mwa adui. Siku ya Yehova ya mhesabiano iko karibu, nawe utaitwa kutoa hesabu. Utatendwa jinsi ulivyotenda.

      9. Ni kurejeshwa gani ambako kwatabiriwa?

      9 Kurejeshwa kwa nyumba ya Yakobo (Mist. 17-21). Tofauti na hivyo, wakati umekaribia nyumba ya Yakobo irejeshwe. Watu watarudi Mlima Sayuni. Wao watameza nyumba ya Esau kama vile moto hufanyia mabua makavu. Watateka bara kuelekea kusini, Negebu, jimbo lenye milima-milima la Esau na Shefela; kuelekea kaskazini watamiliki bara la Efraimu na Samaria, na jimbo la mbali kufikia Sarepta; kuelekea mashariki watachukua eneo la Gileadi. Lazima Edomu yenye kiburi ikome kuwako, lazima Yakobo arejeshwe, na “huo ufalme utakuwa ni mali ya BWANA [Yehova, NW].”—Mst. 21.

      KWA NINI NI CHENYE MAFAA

      10. Ni unabii gani mbalimbali mwingine uliotabiri kuangamizwa kwa Edomu, na kwa nini itakuwa na mafaa kufikiria hayo pamoja na Obadia?

      10 Akishuhudia uhakika wa utimizo wa ujumbe huo wa hukumu juu ya Edomu, Yehova alikuwa na matangazo kama hayo yaliyotolewa na manabii wake wengineo. Yenye kutokeza miongoni mwayo ni yale yaliyoandikwa katika Yoeli 3:19; Amosi 1:11, 12; Isaya 34:5-7; Yeremia 49:7-22; Ezekieli 25:12-14; 35:2-15. Matangazo ya mapema bila shaka yalirejezea vitendo vya uadui katika nyakati zilizopita, ambapo yale ya tarehe ya baadaye kwa wazi ni mashutumu juu ya Edomu kwa ajili ya mwenendo wayo usiosameheka, warejezewa na Obadia, wakati ambapo Wababuloni waliteka Yerusalemu. Itaimarisha imani katika nguvu za Yehova za unabii tukichunguza jinsi misiba iliyotabiriwa ilivyopata Edomu. Zaidi ya hayo, itajenga uhakika katika Yehova kuwa Mungu ambaye sikuzote hutekeleza kusudi lake lililoelezwa.—Isa. 46:9-11.

      11, 12. (a) Wale waliokuwa na “amani” pamoja na Edomu walikujaje kumshinda nguvu? (b) Ni kupitia hatua gani Edomu ikaja ‘kukatiliwa mbali hata milele’?

      11 Obadia alikuwa ametabiri kwamba ‘watu wa mapatano na’ Edomu, wale “waliofanya amani” nayo, wangekuwa wale ambao wangemshinda nguvu. (Oba. 7) Amani ya Babuloni pamoja na Edomu haikuendelea. Wakati wa karne ya sita K.W.K., vikosi vya Kibabuloni chini ya Mfalme Nabonido vilishinda Edomu.b Hata hivyo, karne moja baada ya uvamizi wa Nabonido wa bara hilo, Edomu yenye uhakika ingali ilitumaini kujitokeza tena, na kuhusu hilo, Malaki 1:4 yaripoti hivi: “Ijapokuwa Edomu asema, Tumepondwa-pondwa, lakini tutarudi na kupajenga mahali palipoachwa hali ya ukiwa; BWANA [Yehova, NW] wa majeshi asema hivi, Wao watajenga, bali mimi nitaangusha.” Ijapokuwa jitihada za Edomu za kujitokeza tena, kufikia karne ya nne K.W.K. Wanabatea walikuwa wameimarika kabisa katika bara hilo. Wakiwa wamesukumwa kutoka bara lao, Waedomi walikalia sehemu ya kusini ya Yudea, iliyokuja kuitwa Idumea. Hawakufaulu kamwe kushinda tena bara la Seiri.

      12 Kulingana na Yosefo, katika karne ya pili K.W.K. Waedomi waliosalia walitiishwa na mfalme Myahudi John Hirkano 1, wakalazimishwa kukubali tohara, na polepole wakafyonzwa ndani ya utawala wa Kiyahudi chini ya liwali wa Kiyahudi. Kufuatia uharibifu wa Kiroma wa Yerusalemu katika 70 W.K., jina lao lilitokomea kutoka kwa historia.c Ilikuwa sawa na alivyokuwa ametabiri Obadia: “Utakatiliwa mbali hata milele. . . . Wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau.”—Oba. 10, 18.

      13. Ni nini kilichopata Wayahudi, kinyume cha Waedomi?

      13 Kinyume cha ukiwa wa Edomu, Wayahudi walirejeshwa kwenye bara la kwao katika 537 K.W.K. chini ya uliwali wa Zerubabeli, ambako walijenga upya hekalu katika Yerusalemu na kuimarika kabisa katika bara hilo.

      14. (a) Ni onyo gani linalopatikana kwa yale yaliyopata Edomu? (b) Wote wapaswa kukiri nini, kama Obadia, na kwa nini?

      14 Jinsi ilivyo wazi kwamba kiburi na kimbelembele huongoza kwenye msiba! Acheni wote wanaojikweza kwa kiburi na kusimanga kwa ukatili dhiki inayopata watumishi wa Mungu waonywe na yaliyopata wa Edomu. Acheni wakiri, kama Obadia, kwamba lazima “ufalme utakuwa ni mali ya BWANA [Yehova, NW].” Wale wanaopigana na Yehova na watu wake watakatiliwa mbali kwa wakati usiojulikana, lakini Ufalme wenye fahari na umaliki wa milele wa Yehova utasimama umeondolewa malawama milele!—Mst. 21.

  • Kitabu Cha Biblia Namba 32—Yona
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
    • Kitabu Cha Biblia Namba 32—Yona

      Mwandikaji: Yona

      Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 844 K.W.K.

      1. Ni maswali gani yanayojibiwa katika kitabu cha Yona, na chaonyesha nini juu ya rehema ya Yehova?

      YONA—misionari kwenye nchi ya kigeni wa karne ya tisa K.W.K.! Yeye alikuwa na maoni gani juu ya mgawo wake kutoka kwa Yehova? Huo ulimfungulia maono gani mapya? Je! aliwapata watu katika mgawo wake wakiwa waitikiaji? Kuhubiri kwake kulifaulu kwa kadiri gani? Maandishi ya kutazamisha ya kitabu cha Yona yajibu maswali hayo. Yakiwa yameandikwa wakati ambapo taifa teule la Yehova lilikuwa limevunja agano pamoja Naye na kutumbukia katika ibada-sanamu ya kipagani, maandishi hayo ya kiunabii yaonyesha kwamba rehema ya Mungu si kwa taifa moja tu lolote lile, wala hata si kwa Israeli pekee. Zaidi ya hayo, yakweza rehema kuu na fadhili za upendo za Yehova, tofauti na ukosefu wa rehema, saburi, na imani ambao mara nyingi sana huonekana katika mwanadamu asiyekamilika.

      2. Ni nini kinachojulikana kuhusu Yona, naye alitoa unabii mwaka gani hivi?

      2 Jina Yona (Kiebrania, Yoh·nahʹ) lamaanisha “Njiwa.” Yeye alikuwa mwana wa nabii Amitai wa Gath-heferi katika Galilaya katika eneo la Zabuloni. Kwenye 2 Wafalme 14:23-25 twasoma kwamba Yeroboamu mfalme wa Israeli alieneza mpaka wa taifa kulingana na neno ambalo Yehova alinena kupitia Yona. Hiyo ingeuweka wakati wa kutoa unabii kwa Yona uwe 844 K.W.K. hivi, mwaka ule wa kupanda kitini kwa Yeroboamu 2 wa Israeli na miaka mingi kabla ya Ashuru, yenye mji mkuu kule Ninawi, kuanza kutawala Israeli.

      3. Ni nini kinachothibitisha simulizi la Yona kuwa asilia?

      3 Hakuna shaka kwamba simulizi lote zima la Yona ni asilia. “Mkamilishaji wa imani yetu, Yesu,” alirejezea Yona kuwa mtu wa kikweli na akatoa fasiri iliyopuliziwa juu ya mawili kati ya yale matukio ya kiunabii yaliyo katika Yona, hivyo akionyesha kwamba kitabu hiki kina unabii wa kweli. (Ebr. 12:2, NW; Mt. 12:39-41; 16:4; Luka 11:29-32) Sikuzote kitabu cha Yona kimewekwa na Wayahudi miongoni mwa vitabu vyao vilivyokubaliwa nao hukiona kuwa cha kihistoria. Unyoofu wa Yona mwenyewe katika kueleza makosa na udhaifu wake mbalimbali, bila jaribio lolote la kuficha, huonyesha pia maandishi hayo kuwa ya kweli.

      4. Yawezekana ni samaki wa aina gani alimmeza Yona? Hata hivyo, ni nini iliyo habari ya kutosha kuturidhisha?

      4 Namna gani juu ya “samaki mkubwa” aliyemeza Yona? Kumekuwako kukisia-kisia kwingi juu ya huyo alikuwa samaki wa aina gani. Nyangumi-shahawa aweza kabisa kumeza binadamu mzima. Ndivyo na yule papa-mweupe mkubwa sana. Hata hivyo, Biblia yaeleza hivi kwa wepesi: “BWANA [Yehova, NW] akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona.” (Yona 1:17) Aina ya samaki huyo haikutajwa. Haiwezi kupambanuliwa kwa uhakika kama alikuwa nyangumi-shahawa, papa-mweupe mkubwa sana, au kiumbe mwingine wa baharini asiyetambulishwa.a Maandishi ya Biblia kwamba alikuwa “samaki mkubwa” ni habari ya kutosha kuturidhisha.

      YALIYOMO KATIKA YONA

      5. Yona aitikiaje mgawo wake, na tokeo ni nini?

      5 Yona apewa mgawo kwenda Ninawi, lakini akimbilia mbali (1:1-16). “Basi neno la BWANA [Yehova, NW] lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.” (1:1, 2) Je! Yona apendezwa sana na mgawo huo? Hata kidogo! Yeye akimbilia mbali kuelekea upande ule mwingine, akipanda meli ya kwenda Tarshishi, yawezekana ni Hispania. Meli ya Yona yakutana na dhoruba kubwa. Kwa kuhofu mabaharia waitisha msaada, “kila mtu akamwomba mungu wake,” huku Yona akiwa amelala katika ngama ya meli. (1:5) Baada ya kuamsha Yona, wao watupa kura kwa jaribio la kugundua ni nani wa kulaumika kwa mashaka yao. Kura yaangukia Yona. Sasa ndipo yeye anapowajulisha kwamba yeye ni Mwebrania, mwabudu wa Yehova, na kwamba akimbilia mbali kutoka kwenye furushi lake alilopewa na Mungu. Awaalika wamvurumishe ndani ya bahari. Baada ya kufanya jitihada zaidi za kusalimisha meli dhorubani, mwishowe wamtupa Yona kutoka melini. Bahari yaacha fujo.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki