Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • km 2/08 kur. 7-8
  • Ripoti ya Ujenzi wa Ofisi ya Tawi ya Tanzania

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ripoti ya Ujenzi wa Ofisi ya Tawi ya Tanzania
  • Huduma Yetu ya Ufalme—2008
Huduma Yetu ya Ufalme—2008
km 2/08 kur. 7-8

Ripoti ya Ujenzi wa Ofisi ya Tawi ya Tanzania

Tunafurahi kuwajulisha kuhusu ujenzi wa ofisi mpya ya tawi hapa nchini Tanzania.

Ijapokuwa kazi kubwa ilifanywa na shirika fulani lililopewa kandarasi ya ujenzi, sasa tuna kikundi cha ndugu na dada 20 kutoka nchi 8 tofauti wanaofanya kazi ili kufanikisha mradi huo. Jukumu kuu la ndugu hao ni kuhakikisha kwamba kazi bora inafanywa na michango inatumiwa vizuri.

Zaburi 127:1 inasema: “Yehova mwenyewe asipoijenga nyumba, ni bure kwamba wajenzi wake wameifanyia kazi ngumu.” Ni wazi kwamba Yehova amebariki kazi ya ujenzi ya watu wake, inayofanikisha kazi yetu ya kuhubiri na kufundisha ulimwenguni pote, kazi ambayo Yesu aliwaamuru wafuasi wake wafanye. Hii si mara ya kwanza kwa watu wa Yehova kutumia shirika la ujenzi. Kwa mfano, Hiramu Mfalme wa Tiro alipewa kandarasi ya kumletea Sulemani mierezi na miberoshi kwa ajili ya ujenzi wa hekalu.

Je, Yehova alibariki mpango huo? 1 Wafalme 8:10, 11 inazungumzia jinsi ambavyo, wakati wa kuwekwa wakfu kwa hekalu, utukufu wa Yehova ukiwakilishwa na wingu ulijaa katika jengo hilo lililokamilishwa. Vivyo hivyo, leo tunaona uthibitisho wa kwamba Yehova anabariki mradi wetu wa ujenzi hapa Tanzania.

Kama makutaniko yote yalivyojulishwa katika barua iliyotumwa mapema, shirika hilo la ujenzi lilianza kazi Mei 2, 2006. Kazi kubwa imefanywa tangu wakati huo.

Majengo hayo mapya yanatia ndani majengo matatu ya makazi yenye orofa mbili ambayo yana vyumba kwa ajili ya watu 56, Jumba la Ufalme litakalotumiwa na familia ya Betheli na makutaniko ya eneo hilo, na jengo lingine lenye orofa mbili litakalokuwa na ofisi mbalimbali, dobi, chumba cha kulia, na jiko. Isitoshe, tutakuwa na bohari itakayotumiwa kama depo ya vichapo, na karakana za idara mbalimbali za kudumisha majengo hayo. Pia kutakuwa na jengo lililo na sehemu ya kuchuja na kuhifadhi maji inayoweza kuchukua lita 50,000, nasi tutakuwa na mfumo wetu wenyewe wa kusafisha maji-taka. Kufikia wakati barua hii ilipoandikwa, ujenzi wa kuta zote na paa ulikuwa umekamilishwa na kazi ya kukamilisha sehemu za ndani za majengo inasonga mbele vizuri.

Vifaa vingi vilivyotumiwa katika mradi wetu vilinunuliwa hapa nchini. Hata hivyo, vifaa tata kama vile vya umeme na mabomba viliagizwa kutoka ng’ambo. Ndugu zetu katika ofisi nyingine za tawi walisaidia kutafuta, kununua, na kusafirisha vifaa hivyo vilivyowekwa katika Betheli yetu mpya. Bila shaka tunathamini utegemezo huo kutoka kwa undugu wetu wa kimataifa.

Tunatazamia kuhamia majengo hayo mpya mnamo Machi 2008. Tunamwomba Yehova aendelee kubariki mradi wetu na roho ambayo ninyi akina ndugu na dada mnaendelea kuonyesha katika kutegemeza kazi ya Ufalme.

Ndugu zenu,

Ofisi ya Tawi ya Tanzania

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki