Albania
ALBANIA ni nchi ndogo lakini yenye historia ndefu. Imekaliwa na watu wa mataifa na makabila mbalimbali, imeng’ang’aniwa na serikali kuu za ulimwengu, na kutengwa kwa miaka mingi na mataifa mengine. Ingawa Mashahidi wa Yehova nchini humo wamekumbwa na matatizo na dhiki nyingi, Yehova Mungu amewategemeza na kuwabariki kwa ufanisi wa kiroho. Masimulizi yafuatayo ni historia fupi inayoonyesha jinsi “mkono wa Yehova” umewategemeza watumishi wake wanyenyekevu nchini humo.—Mdo. 11:21.
Kwa karne nyingi, kumekuwa na mizozo ya kidini nchini Albania kwa kuwa nchi hiyo imetawaliwa na serikali mbalimbali za kigeni. Kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1500, eneo hilo lilikuwa limegawanyika kidini, kukiwa na Waislamu, Waothodoksi, na Wakatoliki.
Mwishoni mwa miaka ya 1800 wenyeji walianza kujivunia utaifa na vyama vingi vya kizalendo vikaanzishwa. Watu wengi wa Albania ni maskini na wengi wao wanalaumu miaka mingi ya utawala wa kigeni. Kufikia mwaka wa 1900, Waalbania walitaka kuwa huru na kujitawala, masuala yaliyosababisha vita kati yao na Serbia, Ugiriki, na Uturuki. Hatimaye, mwaka wa 1912, Albania ikajitangaza kuwa nchi huru.
Baadaye, karibu dini zote kubwa-kubwa zikawa zimefutiliwa mbali na sera za serikali. Baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, serikali ya Kikomunisti ilipiga marufuku dini zote na kutangaza Albania kuwa nchi ya kwanza ulimwenguni isiyoamini kuwapo kwa Mungu.
‘KUIKUBALI KWELI KWA SHANGWE’
Kabla ya mwaka wa 56 W.K., mtume Paulo aliripoti kwamba yeye na wenzake walikuwa wamehubiri habari njema kwa ukamili “mpaka Ilirikamu,” jimbo la Roma ambalo wakati huo lilitia ndani eneo ambalo leo ni Albania. (Rom. 15:19) Yaelekea kwamba wakati huo kulikuwa na Wakristo wa kweli katika eneo hilo, kwa kuwa kulingana na historia, Ukristo nchini Albania ulianza katika karne ya kwanza.
Katika siku zetu, ibada ya kweli ilianza katika eneo hili mwaka wa 1921. Mwaka huo ndugu John Bosdogiannis, aliyekuwa Krete, alituma barua Betheli ya Brooklyn na kuomba kutembelea “darasa” la kujifunza Biblia huko Ioannina, ambako leo ni sehemu ya Ugiriki. Karibu wakati huohuo, Waalbania wengi, kutia ndani Thanas (Nasho) Idrizi na Costa Mitchell, walihamia New England, Marekani. Walipojifunza kweli, walibatizwa bila kukawia. Ndugu Idrizi alirudi Gjirokastër, Albania, mwaka wa 1922, akiwa Mwalbania wa kwanza kurudi nyumbani na kweli za Biblia. Yehova alibariki roho yake ya kujidhabihu, nao watu wakaanza kuikubali kweli. Baadaye, Waalbania wengine waamini waliokuwa wakiishi Marekani wakarudi nyumbani pia. Naye Costa Mitchell akaendelea kuwahubiria Waalbania waliokuwa wakiishi Boston, Massachusetts, Marekani.
Sokrat na Thanas Duli (Athan Doulis) walizaliwa nchini Albania, hata hivyo walihamia Uturuki wakiwa wangali wadogo. Sokrat alirudi Albania mwaka wa 1922. Mwaka uliofuata, Thanas pia, mwenye umri wa miaka 14, akarudi kumtafuta ndugu yake. “Nilipofika nyumbani,” akaandika, “sikumpata ndugu yangu. Alikuwa akifanya kazi zaidi ya kilomita 200 kutoka nyumbani. Hata hivyo, nilipata magazeti ya Mnara wa Mlinzi, Biblia, na mabuku saba ya Studies in the Scriptures, pamoja na vijitabu vingine vya Biblia. Inaonekana kwamba hata katika eneo hilo la mbali lenye milima-milima, kulikuwa na Wanafunzi wa Biblia wenye bidii waliokuwa wameishi Marekani ambao walirudi wakiwa na kiasi fulani cha ujuzi wa Biblia nao waliupenda ujumbe wake.” Ndugu hao wawili walipokutana hatimaye, Sokrat—aliyekuwa tayari amebatizwa—hakusita kumfundisha ndugu yake, Thanas, ukweli.
Mwaka wa 1924, kazi nchini Albania ilianza kusimamiwa na ofisi ya Rumania. Ijapokuwa kazi ya kuhubiri haikuwa imetia mizizi, gazeti la Mnara wa Mlinzi la Desemba 1, 1925, liliripoti: “Vijitabu The Harp of God, The Desirable Government na The World Distress vilikuwa vimetafsiriwa na kuchapishwa katika lugha ya wenyeji . . . Vimesambazwa kwa wingi nao Waalbania wanaikubali kweli kwa shangwe.”
Wakati huo, Albania ilikuwa imesambaratika kutokana na migogoro ya kisiasa. Namna gani Mashahidi wa Yehova? “Mwaka wa 1925, kulikuwa na makutaniko matatu nchini Albania, na Wanafunzi wa Biblia waliokuwa mbali,” akaandika Thanas. Pia, anataja kwamba walikuwa na upendo mwingi tofauti kabisa na watu wengine waliokuwa na mizozo, kiburi, na roho ya mashindano. Huku Waalbania wengi wakiondoka nchini, wengine waliokuwa wamejifunza kweli walikuwa wakirudi, wakiwa na hamu kubwa ya kuwafundisha watu wao wa ukoo kuhusu Ufalme.
Wakati huohuo huko Boston, hotuba za watu wote zilikuwa zikitolewa katika lugha ya Kialbania Jumapili asubuhi, kukiwa na wahudhuriaji 60 hivi. Waliohudhuria walikuwa wanafunzi wenye bidii waliopenda sana kusoma mabuku ya Studies in the Scriptures. Pia kitabu The Harp of God (Kinubi cha Mungu) kilisomwa sana, licha ya makosa fulani katika tafsiri. (Kwa mfano, mwanzoni kichwa cha kitabu hicho kilitafsiriwa, The Guitar of God [Gita ya Mungu].) Hata hivyo, kitabu hicho kiliwasaidia Waalbania wengi kujifunza kweli za Biblia na kuimarisha imani yao.
“MSIWASUMBUE!”
Gazeti la Mnara wa Mlinzi la 1926, liliripoti kwamba watu 13 walihudhuria Ukumbusho wa kifo cha Kristo nchini Albania. Kulingana na Kitabu cha Mwaka cha 1927, kulikuwa na ndugu 15 hivi nchini Albania, waliokuwa wakitangaza ujumbe wa Ufalme na nchini Marekani kulikuwa na ndugu 30 hivi Waalbania, waliotamani sana kuwasaidia watu wa kwao kupata ujuzi wa kweli. Ndugu hao 15 wa Albania walifurahi kuwa na hudhurio la watu 27 kwenye Ukumbusho mwaka 1927, zaidi ya mara mbili ya wale waliohudhuria mwaka uliotangulia.
Hata kufikia mwishoni mwa miaka ya 1920 bado kulikuwa na msukosuko wa kisiasa nchini Albania. Serikali iliyokuwa ikiongozwa na kasisi Mwothodoksi, Fan Noli, ilitawala kwa muda kisha ikapinduliwa na Rais Ahmed Bey Zogu. Rais huyo alitangaza Albania kuwa ufalme, ambamo yeye mwenyewe, Mfalme Zog wa Kwanza, ndiye mwenye mamlaka ya mwisho.
Mwaka wa 1928, Lazar Nasson, Petro Stavro, na ndugu wengine wawili, walisafiri kutoka Marekani hadi Albania ili kuonyesha sinema ya “Photo-Drama of Creation.” Wakati huohuo, makasisi wawili kutoka Marekani, mmoja Mkatoliki na mwingine Mwothodoksi, walikuwa wamekuja Albania kumtembelea Mfalme Zog wa Kwanza.
“Jihadharini!” kasisi Mkatoliki akamtahadharisha Zog. “Watu kutoka Marekani wamekuja kuwavuruga.”
Hata hivyo, kasisi Mwothodoksi hakukubaliana naye. Aliwajua ndugu hao kwa sababu awali walikuwa wafuasi wa kanisa lake huko Boston. “Ikiwa kila mtu hapa Albania angekuwa kama watu hao,” akamwambia Zog, “huhitaji kufunga milango ya makao yako!”
“Basi waacheni,” akajibu Zog, “msiwasumbue!”
Mwaka huohuo kitabu Songs of Praise to Jehovah, cha Kialbania kilichapishwa huko Boston, nao akina ndugu wa Albania wakajifunza muziki na maneno ya nyimbo hizo. Nyimbo mbili zilizopendwa na wengi ni “Fear Not, O Little Flock” na “To the Work!” Nyimbo hizo ziliwaimarisha akina ndugu katika miaka iliyofuata yenye msukosuko.
Kwa kawaida Waalbania hupenda kusema mambo waziwazi, hawafichi lolote. Ijapokuwa huenda wengine wakaona kwamba Waalbania wanazungumza kwa ukali, miongoni mwao ni mazungumzo tu ya kawaida na yenye kusisimua. Waalbania wakishika jambo fulani, huwezi kuwanyamazisha au kuwazuia kuchukua hatua. Bila shaka utu huo umechochea jinsi wanavyopokea habari njema.
BAADA YA DHIKI, FARAJA
Kwa sababu ya kuongezeka kwa matatizo ya kisiasa na kiuchumi, Waalbania wengi walikuwa wakiihama nchi hiyo, na baadhi yao walijifunza kweli wakiwa New England na New York. Popote palipokuwa na Waalbania wengi, kweli ilitia mizizi. Wakiwa na hamu ya kupata vitabu zaidi, akina ndugu walifurahi kupokea vijitabu Kingdom na The Crisis katika Kialbania.
Wakati huohuo, serikali ya Albania ilikuwa imewanyang’anya akina ndugu baadhi ya vitabu walivyokuwa navyo. Hata hivyo, katika mwaka wa 1934, Bulletin (inayoitwa Huduma Yetu ya Ufalme leo) iliripoti hivi kutoka Albania: “Tunafurahi kuwajulisha kwamba Waziri wa Haki ametoa amri kwa mikoa yote kwamba kuanzia sasa na kuendelea, tunaweza kusambaza vitabu vyetu kwa uhuru . . . Akina ndugu wamerudishiwa vitabu na vijitabu vyote walivyokuwa wamenyang’anywa . . . Sasa ndugu saba wamekodi gari nao wanazuru miji ya mbali wakiwa na vitabu huku wale ndugu wengine wakihubiri maeneo ya karibu.” Hivyo, mwaka wa 1935 na 1936, akina ndugu waligawa vitabu na vijitabu zaidi ya 6,500!
“USAMBAZAJI WA HABARI UNAOAMINIKA KUWA WA KIHISTORIA”
“Kutakuwa na majaribio ya usambazaji wa habari unaoaminika kuwa wa kihistoria,” likatangaza gazeti la Uingereza la Leeds Mercury mapema mwaka wa 1936. “Hotuba ya mwinjilisti, Judge Rutherford, atakayotoa huko Los Angeles, itasambazwa.” J. F. Rutherford, aliyekuwa akisimamia kazi ya Mashahidi wa Yehova wakati huo, angetoa hotuba ambayo ingesambazwa kotekote nchini Marekani na Uingereza kupitia redio na simu, na kusikiwa katika nchi kadhaa za Ulaya. “Kuna Nchi moja ya Ulaya ambayo haitasikia hotuba hiyo,” makala hiyo ya Mercury ikamalizia. “Nchi hiyo ni Albania, ambayo haina huduma za simu.”
Hata hivyo, majuma machache baada ya hotuba hiyo, Nicholas Christo wa kutaniko la Kialbania huko Boston aliandikia makao makuu: “Tungependa kuwajulisha kwamba kulingana na habari tulizopata hivi majuzi kutoka Albania, hotuba ya Judge Rutherford kuhusu ‘Kuyatenganisha Mataifa’ ilisikika nchini Albania, nchi nyingine zaidi katika orodha ndefu ya nchi zilizosikiliza hotuba hiyo. Ilisikika katika sehemu mbili . . . , yaelekea kupitia mawimbi ya redio ya masafa mafupi. . . . Akina ndugu walikuwa na msisimuko usio na kifani kwa kuisikia sauti ya Judge Rutherford.”
Wahubiri wa Albania walikuwa wakiendesha mikutano yao jinsi gani kabla ya gazeti la Mnara wa Mlinzi kuanza kuchapishwa katika Kialbania? Wengi wa Waalbania waliojifunza kweli walikuwa wamesomea katika shule za Kigiriki kusini mwa Albania. Hivyo, haikuwa vigumu kwao kujifunza Mnara wa Mlinzi katika Kigiriki. Wengine walitumia gazeti la Kiitaliano au Kifaransa. Akina ndugu walikuwa wakitafsiri vichapo vyao mikutano ikiendelea.
Huko Boston funzo la Mnara wa Mlinzi katika lugha ya Kialbania lililokuwa likifanywa Jumatatu jioni liliongozwa kwa kutumia gazeti la Kigiriki. Licha ya hayo, akina ndugu waliwafundisha watoto wao vizuri, na baadaye, wana na binti zao, wapwa, wajukuu na vitukuu wakawa watumishi wa wakati wote. Ndugu Waalbania walijulikana sana kwa bidii yao katika kazi ya kuhubiri hivi kwamba watu wakawa wanawaita ungjillorë, yaani, “waeneza- injili.”
WENYE MAMLAKA WAHUBIRIWA
Mwaka wa 1938, mwaka mmoja kabla ya Mfalme Zog kupinduliwa, dada zake wawili walienda Boston. Mwezi Desemba gazeti Consolation (ambalo leo huitwa Amkeni!) liliripoti: “Mabinti wa kifalme kutoka Albania walipokuja Boston, mimi na shahidi mwingine kutoka kutaniko la Kialbania la Mashahidi wa Yehova huko Boston, tuliwatembelea hotelini na kuwapa ujumbe wa Ufalme wa Mungu. Walitupokea vizuri.”
Mashahidi hao wawili ni Nicholas Christo na dada yake Lina. Mbali na mabinti wa kifalme walikutana na watu wengine watano wenye vyeo, kutia ndani balozi wa Albania nchini Marekani, Faik Konitza [Konica]. Kabla ya kukutana nao, kikundi hicho kilisomewa kadi ya ushuhuda ya Kialbania inayoeleza jinsi kweli imehubiriwa miongoni mwa Waalbania. Miongoni mwa mambo mengine kadi hiyo ilisema: “Tunafurahi kuwajulisha kwamba ujumbe huu umehubiriwa nchini Albania pia kwa miaka mingi na makumi ya maelfu ya vitabu vimegawanywa kwa wenye mamlaka na watu wa Albania ili kuwapa ujuzi na faraja.”
Balozi Konitza akawaambia mabinti hao wa kifalme: “Wangependa mwasaidie kuhakikisha kwamba kazi yao ya kuhubiri inaendelea bila usumbufu nchini Albania. Dini yao ni ‘mpya,’ na wanaamini kwamba ulimwengu [uliopo sasa] karibuni utakwisha halafu Kristo atatawala kisha hata wafu watafufuliwa.”
Bwana Konitza alipataje kujua mengi hivyo kuhusu ujumbe wa Ufalme? Gazeti Consolation lilieleza kwamba ni “kwa sababu shahidi fulani, kabla ya . . . kujifunza kweli miaka kadhaa awali, alimfahamu vema . . . naye alikuwa amemhubiria mara nyingi.”
VITA VYA PILI VYA ULIMWENGU VYATOKEZA MAJARIBU
Katika miaka ya 1930, Italia ilianza kutawala Albania, naye Mfalme Zog na familia yake wakaikimbia nchi hiyo mwaka wa 1939. Majeshi ya Kifashisti yaliyoivamia nchi hiyo kutoka Italia yalipiga marufuku vitabu vyetu na kuamuru kwamba wahubiri 50 waliokuwako wasiendelee kuhubiri. Mwaka wa 1940, vitabu 15,000 vilichukuliwa kwa nguvu. Agosti 6, huko Këlcyrë, majeshi hayo yaliwakamata ndugu tisa na kuwafungia katika seli ndogo. Baadaye wakapelekwa gerezani mjini Tiranë. Walikaa humo kwa miezi nane bila kufunguliwa mashtaka kisha wakahukumiwa vifungo vya kati ya miezi kumi na miaka miwili u nusu.
Kwa kawaida, wafungwa walikuwa wakipata chakula kutoka kwa watu wa familia. Hata hivyo, katika kisa hiki, waliopaswa kuandalia familia walikuwa gerezani. Chakula kingepatikana wapi?
“Tulipokea gramu 800 za mkate uliokauka, kilo tatu za mkaa, na kipande cha sabuni kila baada ya siku 15,” akumbuka Nasho Dori. “Mimi na Jani Komino tulikuwa na pesa za kutosha kununua kilo moja ya maharagwe. Tulitumia mkaa kuyapika, kisha tukayauza kijiko-kijiko kwa wafungwa wengine. Punde si punde tukawa tukipika maharagwe sufuria tano. Mwishowe, tukawa na pesa za kutosha kununua nyama.”
Mwaka wa 1940/1941, majeshi ya Ugiriki yalivamia upande wa kusini wa Albania na kuwalazimisha watu wajiunge nao. Katika kijiji kimoja ndugu fulani alipokataa, akisema kwamba haungi mkono upande wowote, askari-jeshi walishika nywele zake na kuanza kumburuta na kumpiga mpaka akazirai.
“Ungali mkaidi?” ofisa-msimamizi akamuuliza kwa hasira ndugu huyo alipopata fahamu.
“Bado siungi mkono upande wowote!” akajibu ndugu huyo.
Askari hao wakiwa wametamauka, wakamwacha aende zake.
Siku kadhaa baadaye, ofisa huyo alienda nyumbani kwa ndugu huyo aliyemtesa na kumpongeza kwa ujasiri wake. “Siku chache zilizopita, niliua Waitaliano 12 na nikapata medali,” akasema. “Lakini dhamiri yangu inanisumbua, nami naona aibu kuivaa. Ninaibeba mfukoni kwa sababu najua kwamba inawakilisha jeuri.”
WATAWALA WAPYA—MAJARIBU YALEYALE
Katikati ya mapigano na machafuko ya vita, pole kwa pole Chama cha Kikomunisti cha Albania kilikuwa kikipata umaarufu, licha ya jitihada za serikali ya Kifashisti. Mwaka wa 1943, askari-jeshi waliokuwa wakipigana na Wakomunisti walimkamata ndugu mmoja, wakamtupa ndani ya lori, wakampeleka vitani, na kumkabidhi bunduki. Akaikataa.
Kamanda akamfokea, “Wewe ni Mkomunisti! Kama ungekuwa Mkristo, ungepigana sawa tu na makasisi!”
Kamanda huyo akawaamuru askari-jeshi wamuue ndugu huyo. Walipokuwa tayari kufyatua risasi, ofisa mwingine akafika na kuuliza ni nini kinachoendelea. Alipoambiwa msimamo wa ndugu huyo, alitangua amri hiyo, naye ndugu huyo akaachiliwa.
Septemba 1943, Wafashisti waliondoka nayo majeshi ya Ujerumani yakashambulia na kuua watu 84 mjini Tiranë katika usiku mmoja. Mamia walipelekwa katika kambi za mateso. Wakiwa huko akina ndugu waliandika maandiko yenye kufariji na kuwapa tumaini. Mtu alipomaliza kusoma, alipaswa kurudisha ili mtu mwingine pia asome. Wakati huo, wakitumia vijitabu vichache walivyokuwa wameficha, waliendelea kuhubiri. Walitumia visehemu vya Biblia nao hawakuwa na Biblia nzima mpaka katikati ya miaka ya 1990.
Kufikia 1945, ndugu 15 walikuwa wametiwa kifungoni. Wawili kati yao walikuwa katika kambi ya mateso, ambapo mmoja wao aliteswa mpaka akafa. Huku akina ndugu wakiteswa nchini Albania kwa sababu ya kutounga mkono majeshi ya Ujerumani na nchi nyingine zilizokuwa zikiunga mkono, ndugu Waalbania waliokuwa wakiishi Marekani walifungwa kwa sababu ya kutopigana dhidi ya majeshi hayo.
Wakati wa vita nchini Albania, vitabu ambavyo akina ndugu walinyang’anywa vilikuwa vikiwekwa katika majengo ya forodha. Vita vilipopamba moto, jengo hilo liliporomoka, na vitabu vyetu vingi vikaanguka na kutapakaa barabarani. Baadaye, wapita-njia waliokota vitabu na vijitabu na kuanza kuvisoma! Na bila kukawia akina ndugu wakaokota vilivyosalia.
Mwaka wa 1944, majeshi ya Ujerumani yaliondoka Albania, na majeshi ya Kikomunisti yakaanzisha serikali ya mpito. Mara moja, akina ndugu wakatuma maombi ya kuchapisha upya vijitabu, lakini ombi lao halikukubaliwa. “Mnara wa Mlinzi linashambulia makasisi,” ndugu wakaambiwa, “nasi hapa Albania bado tunawaheshimu makasisi.”
VITA VYAKOMA LAKINI MATESO YAENDELEA
Serikali ya Kikomunisti ilitoza ushuru wa juu, ikataifisha mali ya watu, viwanda, biashara, maduka, na majumba ya sinema. Watu hawakuwa na ruhusa ya kununua, kuuza, au kukodi mashamba, na mazao yote yalikuwa ya serikali. Januari 11, 1946, nchi ya Albania ilijitangaza kuwa Jamhuri ya Watu wa Albania. Chama cha Kikomunisti kilishinda uchaguzi na kuanza kutawala, Enver Hoxha akiwa mkuu wa nchi.
Shule nyingi zaidi zilifunguliwa, nao watoto wakaanza kufundishwa kusoma na kuandika, ingawa serikali haikutaka mtu yeyote asome kitabu chochote kisichounga mkono Ukomunisti. Serikali ilitunyang’anya vitabu, karatasi chache zilizokuwa zimebaki, na taipureta kadhaa ambazo akina ndugu walikuwa nazo.
Kila mara akina ndugu walipojaribu kuomba kibali cha kuchapisha vitabu, walinyimwa na kutishwa. Hata hivyo, walisimama imara. “Yehova ametupa jukumu la kuwajulisha watu wa Albania makusudi yake,” wakawaambia wenye mamlaka, “nanyi mnatuzuia. Shauri yenu.”
Ni kana kwamba wenye mamlaka walisema: ‘Hapa Albania sisi ndio wenyewe! Serikali yetu si ya kitheokrasia, nasi hatuna haja nanyi wala Mungu wenu, Yehova, ambaye hata hatumtambui!’ Ndugu hao hawakukata tamaa bali waliendelea kuhubiri habari njema mahali popote na wakati wowote ambapo wangeweza.
Kuanzia mwaka wa 1946 ikawa lazima watu wapige kura, na yeyote aliyekataa alionwa kuwa adui wa serikali. Mikutano na kazi ya kuhubiri ilipigwa marufuku. Akina ndugu walifanya nini?
Katika mwaka wa 1947 ndugu 15 hivi waliokuwa Tiranë, walikuwa wamepanga kampeni ya kuhubiri. Walikamatwa, Biblia zao zikapasuliwa, nao wakateswa. Walipoachiliwa waliamriwa wasiende popote bila idhini ya polisi. Magazeti yalimdhihaki Yesu na Yehova.
Ndugu Waalbania waliokuwa wakiishi Boston walipata habari hizo, na mnamo Machi 22, 1947, wakamwandikia Enver Hoxha barua ya kurasa mbili kwa niaba ya Mashahidi wa Yehova nchini Albania. Walieleza kwamba Mashahidi wa Yehova si tisho kwa serikali na kwamba wapinzani wa kidini ndio wanaochochea mashtaka ya uwongo kwa sababu vitabu vyetu vinafichua matendo yao yasiyopatana na mafundisho ya Kikristo. Barua hiyo ilimalizia kwa kusema: “Wajumbe wa Albania kwa Umoja wa Mataifa wakiongozwa na Bwana Kapo walipozuru Boston, tuliwatembelea hotelini. Bwana Kapo alitupokea vizuri na bila upendeleo akausikiliza ujumbe wetu.” Kwa miaka mingi, Hysni Kapo alikuwa mmojawapo wa watu wenye mamlaka kuu zaidi nchini Albania. Licha ya ombi hilo, matatizo yalizidi.
Mwaka wa 1947, Albania ikajiunga na Muungano wa Sovieti na Yugoslavia na kuanza kuzozana na Ugiriki. Mwaka uliofuata, Albania ikakata mahusiano kati yake na Yugoslavia na kuboresha uhusiano wake na Muungano wa Sovieti. Yeyote ambaye hakuunga mkono maoni ya serikali alifukuzwa nchini. Kwa sababu ya msimamo ambao akina ndugu walichukua, walikumbwa na upinzani mkali na kuchukiwa.
Kwa mfano, mwaka wa 1948, ndugu na dada sita walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya Ukumbusho katika kijiji kidogo. Polisi wakaingia ghafula mahali walipokuwa wakikutania na kuwapiga kwa saa nyingi kabla ya kuwaruhusu waondoke. Majuma kadhaa baadaye, polisi walimkamata ndugu aliyetoa hotuba ya Ukumbusho na kumlazimisha asimame kwa saa 12. Usiku wa manane, mkuu wa polisi akafoka, “Kwa nini ulivunja sheria?”
“Kwetu sisi, sheria ya Bwana ni muhimu zaidi kuliko sheria ya nchi!” ndugu huyo akamjibu.
Akiwa na ghadhabu, polisi huyo akamzaba kofi, kisha alipoona ndugu huyo akigeuza kichwa chake akamuuliza, “Unafanya nini?”
“Nimekuambia sisi ni Wakristo,” ndugu huyo akasema. “Yesu alitufundisha kwamba mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie la pili.”
“Kwa sababu hiyo ni amri ya Bwana wenu,” akasema polisi huyo mwenye ghadhabu, “sitamtii, sitakupiga! Ondoka!”
“NITAENDELEA KUHUBIRI”
Sotir Ceqi alikuwa Mwothodoksi shupavu aliyekuwa akiishi Tiranë. Akiwa mtoto aliugua tibii ya mifupa naye alikuwa na maumivu makali ya miguu. Alipokuwa na umri wa miaka 17 hivi, alishuka moyo sana hivi kwamba alitaka kujiua kwa kujitupa mbele ya gari-moshi. Kabla tu ya kufanya hivyo, Leonidha Pope, mtu wa familia yao, akamtembelea. Bila kujua nia ya Sotir, Leonidha akamwambia kwamba Yesu aliwaponya wagonjwa na kwamba dunia itakuwa paradiso. Pia, akampa Sotir Biblia yenye Maandiko ya Kigiriki, ambayo Sotir alianza kuisoma mara moja.
“Mambo niliyokuwa nikisoma yalikuwa yenye kuburudisha kama maji baridi,” akasema Sotir. “Nilikuwa nimeipata kweli!”
Baada ya siku chache bila kuonana na Leonidha, Sotir akawaza: ‘Biblia inasema kwamba Yesu alihubiri. Mitume na wanafunzi walihubiri. Bila shaka ninapaswa kufanya vivyo hivyo.’
Basi, Sotir akaanza kuhubiri. Akiwa na Biblia mkononi na mkono ule mwingine ukiwa na mkongojo, alienda nyumba kwa nyumba akihubiri kwa ujasiri.
Idara ya Usalama wa Nchi, Sigurimi, ndiyo iliyokuwa na jukumu la kulinda usalama wa taifa katika miaka hiyo. Kwa kuwa sikuzote idara hiyo ilikuwa chonjo kuona tisho lolote dhidi ya Ukomunisti, Sotir aliyekuwa na bidii ya kuhubiri hangeweza kuwaponyoka. Walimkamata, wakamfungia kwa saa nyingi, wakampiga, na kumwamuru asihubiri.
Sotir alipoachiliwa, aliwasiliana na Leonidha, ambaye alimpeleka kwa Spiro Karajani, daktari aliyekuwa amejifunza kweli miaka kadhaa awali. Mbali na kumtibu, Spiro alimsaidia Sotir kuielewa kweli vizuri zaidi.
“Ukikamatwa tena,” Spiro akamshauri Sotir, “kabla ya kutia sahihi chochote, hesabu kila neno na kila mstari. Tia mstari mwishoni mwa maneno yao. Usiache nafasi yoyote. Soma kila kitu kwa uangalifu. Hakikisha kwamba kile unachotia sahihi ndicho ulichosema.”
Siku mbili tu baadaye, polisi wakamkamata Sotir akihubiri tena. Kwenye kituo cha polisi, maofisa walimwamuru atie sahihi taarifa ya polisi. Kabla tu ya kutia sahihi, akakumbuka shauri la Spiro. Licha ya kushinikizwa na polisi afanye haraka, Sotir alihakikisha kwamba amesoma kila neno.
“Samahani,” akasema, “Siwezi kutia sahihi. Sikusema maneno haya. Nikitia sahihi taarifa hii, nitakuwa nasema uwongo, nami siwezi kusema uwongo.”
Polisi hao waliposikia hivyo, wakatengeneza mjeledi wa kamba na kuanza kumpiga Sotir. Alipozidi kukataa, wakamlazimisha ashike nyaya za umeme na kuanza kumpiga kwa umeme.
“Maumivu yaliponizidia,” Sotir akumbuka, “nilisali kwa machozi. Kisha ghafula, mlango ukafunguka. Nikamwona afisa mkuu. Alitupa jicho kisha akageuka. ‘Acheni!’ akaamuru. ‘Mnavunja sheria!’” Walijua vizuri kwamba mateso ni kinyume cha sheria. Polisi wakaacha kumtesa, lakini hawakuacha kumshinikiza Sotir atie sahihi taarifa hiyo. Hata hivyo, alikataa katakata.
Mwishowe wakasema: “Sawa basi!” Kisha, shingo upande, wakaandika taarifa ya Sotir mwenyewe iliyokuwa na ushahidi mzuri. Wakamkabidhi. Licha ya kupigwa kwa saa nyingi na kupigwa kwa umeme, Sotir alisoma kila neno kwa makini. Sentensi ilipoishia katikati ya mstari, alitia mstari mwishoni mwa sentensi hiyo.
“Ulijifunzia wapi kufanya hivi?” maafisa hao wakauliza kwa mshangao.
“Yehova alinifundisha kutotia sahihi mambo ambayo sikusema,” akajibu Sotir.
“Haya, na ni nani anayekupa hiki?” afisa mmoja akamuuliza huku akimpa kipande cha mkate na jibini. Ilikuwa mwendo wa saa tatu usiku, naye Sotir alikuwa na njaa kali, kwa kuwa hakuwa ameonja chochote siku nzima. “Ni Yehova? Hapana. Ni sisi.”
“Yehova ana njia nyingi,” Sotir akajibu. “Yeye ndiye ameichochea mioyo yenu.”
“Tutakuacha uende zako,” wakasema maafisa hao waliokuwa wametamauka, “lakini ukihubiri tena, utakiona.”
“Kama ni hivyo, msiniachilie kwa sababu mkiniachilia, nitaendelea kuhubiri.”
“Na usithubutu kumwambia yeyote mambo yaliyokupata hapa!” afisa akamwamuru.
“Nikiulizwa,” akasema Sotir, “siwezi kudanganya.”
Polisi akamfukuza, “Ondoka!”
Sotir ni mmoja tu kati ya wengi walioteswa kwa njia hiyo. Baada ya masaibu hayo, Sotir akabatizwa.
Kwa miaka mingi, barua zilichujwa na ni ripoti chache sana zilizopatikana kutoka nchi ya Albania. Kadiri ilivyozidi kuwa hatari kusafiri na kuhudhuria mikutano, ikawa vigumu kwa akina ndugu nchini kudumisha mawasiliano. Kwa sababu hakukuwa na usimamizi wowote wa kitengenezo, haikuwa rahisi kujua yaliyokuwa yakitendeka. Hata hivyo, idadi ya watu waliokubali kweli ilizidi kuongezeka. Mwaka wa 1940 kulikuwa na ndugu na dada 50 nchini Albania na mwaka 1949 idadi hiyo ilikuwa imefikia 71.
ONGEZEKO LA KITHEOKRASI KATIKATI YA MSUKOSUKO WA KISIASA
Katika miaka ya 1950, mambo yalikuwa magumu hata zaidi. Chuki ya kisiasa kati ya Albania na Ugiriki iliongezeka. Uhusiano wa kidplomasia kati ya Albania na nchi za Uingereza na Marekani ulikuwa umevunjika. Isitoshe, uhusiano wa Albania na Muungano wa Sovieti ulikuwa mashakani. Albania ilianza kujitenga na kujitegemea. Mawasiliano yote yalikuwa yakipigwa darubini.
Hata hivyo, mara kwa mara, ndugu wawili walifaulu kutuma barua na postikadi kwa akina ndugu nchini Uswisi. Ndugu wa Uswisi walijibu katika Kifaransa au Kiitaliano, wakitumia lugha ya mafumbo. Kupitia postikadi hizo, ndugu wa Albania wakapata kujua kuhusu kusanyiko lililofanywa huko Nuremberg mwaka wa 1955. Habari kuhusu uhuru ambao ndugu wa Ujerumani walikuwa wamepata baada ya utawala wa Hitler, ziliwatia moyo ndugu wa Albania kubaki imara katika imani.
Kufikia 1957, Albania ilikuwa na wahubiri 75. Ijapokuwa idadi kamili haikupatikana, “kulikuwa na hudhurio kubwa” kwenye Ukumbusho, kikaripoti Kitabu cha Mwaka cha 1958, na kuongezea, “ndugu wa Albania bado wanahubiri.”
Kitabu cha Mwaka cha 1959 kiliripoti: “Mashahidi hao waaminifu wa Yehova wanaendelea kufanya yote wawezayo. Wamewahubiria watu kweli na hata wamejaribu kuchapisha vitu fulani. Wanashukuru kwa nyama ya wakati unaofaa ambayo imewafikia mara kwa mara, hata hivyo, watawala wa kikomunisti wamefunga njia zote za kuwasiliana na nchi nyinginezo.” Ripoti hiyo ilimalizia kwa kusema: “Ingawa watawala wa nchi wanawazuia akina ndugu wa Albania kuwasiliana na jamii ya Ulimwengu Mpya, hawawezi kamwe kuizuia roho takatifu ya Mungu isitende juu yao.”
MAPAMBANO YAENDELEA
Wakati huo kila mtu alipaswa kubeba kitambulisho cha kijeshi. Waliokataa walipoteza kazi au kufungwa. Nasho Dori na Jani Komino walifungwa kwa miezi kadhaa tena. Ingawa wachache waliogopa kwamba watapoteza kazi zao na hivyo wakalegeza msimamo wao, bado kulikuwa na ndugu washikamanifu walioadhimisha Ukumbusho mwaka wa 1959, na ndugu na dada wengi waliendelea kuhubiri bila woga.
Mwaka wa 1959 Wizara ya Haki ilivunjwa, nao wanasheria hawakuruhusiwa kuendelea kufanya kazi. Chama cha Kikomunisti kiliunda na kutekeleza sheria zote. Wale ambao hawakupiga kura walionwa kuwa adui. Hali ya woga na wasiwasi ilikuwa imetanda.
Mara kwa mara ndugu wa Albania walituma ujumbe wakieleza jinsi hali zilivyo ngumu, hata hivyo, wameazimia kuendelea kuwa washikamanifu. Wakati huohuo, makao makuu huko Brooklyn yaliendelea kujaribu kuwasiliana na ndugu huko Albania. John Marks, aliyezaliwa kusini mwa Albania, ambaye alikuwa akiishi Marekani, aliombwa ajaribu kupata kibali cha kuingia Albania.
Mwaka mmoja na nusu baadaye, John alifanikiwa kupata kibali, ingawa mke wake Helen hakupata. John alifika Durrës Februari 1961 na kusafiri hadi Tiranë. Alikutana na dada yake, Melpo, aliyekuwa ameanza kupendezwa na kweli. Melpo alimsaidia kukutana na akina ndugu siku iliyofuata.
John aliongea na ndugu hao kwa muda mrefu kisha akawapa vitabu na magazeti kadhaa aliyokuwa ameficha katika sanduku lake. Ndugu hao walisisimuka. Hawakuwa wametembelewa na ndugu kutoka nje ya Albania kwa zaidi ya miaka 24.
Kulingana na John, kulikuwa na ndugu 60 katika miji mitano na wengine wachache katika vijiji vidogo-vidogo. Mjini Tiranë, ndugu walijaribu kukutana kisiri mara moja kwa juma, siku ya Jumapili, ili kusoma pamoja vitabu walivyokuwa wameficha tangu 1938.
Kwa kuwa kwa muda mrefu mawasiliano kati yao na tengenezo yalikuwa yamekatizwa, ndugu hao wa Albania walihitaji kufahamishwa mambo ya kitengenezo na kweli za karibuni. Kwa mfano, akina ndugu na dada walikuwa wakiongoza mikutano na hata akina dada walikuwa wakitoa sala. Baadaye John aliandika: “Akina ndugu hawakujua jinsi dada hao wangeitikia, hivyo wakaniomba nizungumze nao faraghani, nami nikafanya hivyo. Nafurahi kwamba waliyakubali marekebisho hayo.”
Licha ya umaskini wao, watumishi hao waaminifu waliunga mkono kazi ya Ufalme kwa bidii. Kwa mfano, John anakumbuka ndugu wawili waliokuwa wazee kwa umri kutoka Gjirokastër ambao walikuwa wameweka akiba “kutokana na pesa kidogo walizokuwa nazo, nao walikuwa wamekusanya kiasi walichotaka kutoa kiwe mchango kwa Sosaiti.” Kila mmoja wao alikuwa amehifadhi zaidi ya sarafu za dhahabu zenye thamani ya dola 100.
Ndugu wa Tiranë walithamini kupokea kijitabu Preaching and Teaching in Peace and Unity, kilichotoa mwongozo kuhusu jinsi makutaniko yanapaswa kutenda, hata chini ya marufuku. Kisha, mnamo Machi, John akafanya Ukumbusho huko Tiranë nyumbani kwa Leonidha Pope, kukiwa na hudhurio la watu 37. Baada ya hotuba hiyo, John akapanda mashua na kurudi Ugiriki.
Baada ya ndugu katika makao makuu kusoma ripoti ya John kuhusu ziara yake nchini Albania, walimweka Leonidha Pope, Sotir Papa, na Luçi Xheka kusimamia Kutaniko la Tiranë na vilevile kazi nchini Albania. Spiro Vruho akawekwa kuwa mwangalizi wa mzunguko. Alipewa mgawo wa kutembelea makutaniko na kukutana na akina ndugu kila jioni, akitoa hotuba na kuzungumza pamoja nao habari zilizo kwenye vitabu na magazeti. Tengenezo lilifanya kila liwezalo ili kuwasaidia ndugu nchini Albania kuwa na nguvu kiroho na kwenda sambamba na tengenezo.
Kwa kuwa barua zilikuwa zikichujwa, tengenezo halingeweza kutuma maagizo hayo kupitia barua. Badala yake, John aliwasilisha habari hizo kidogo-kidogo kwa akina ndugu akitumia lugha ya mafumbo kwa kurejelea kurasa fulani-fulani katika vitabu. Muda si muda, ripoti zikaanza kuonyesha kwamba ndugu hao wameelewa vizuri maagizo waliyopewa. Ndugu watatu waliokuwa Tiranë walitenda wakiwa Halmashauri ya Nchi, naye Spiro alikuwa akiyatembelea makutaniko kwa ukawaida.
Ndugu nchini Albania walitafuta mbinu za kutuma ripoti za utumishi wa shambani katika makao makuu. Mbinu moja ilikuwa kutuma postikadi kwa akina ndugu hususa waliokuwa ng’ambo. Kisha, kwa kutumia kalamu yenye ncha nyembamba, ripoti hizo ziliandikwa kwa mafumbo chini ya stempu. Kwa mfano, waliandika ukurasa wa kijitabu Preaching and Teaching unaozungumzia “wahubiri.” Kando yake wakaandika idadi ya wahubiri waliotoa ripoti mwezi huo. Kwa miaka mingi, akina ndugu waliokuwa ng’ambo walitumia njia kama hizo kuwasiliana na ndugu nchini Albania.
MWANZO MZURI—KISHA MATATIZO
Ingawa Halmashauri ya Nchi ilijitahidi kuendeleza ibada safi, matatizo yalikuwa njiani. Mwaka wa 1963, Melpo Marks alimwandikia John, ndugu yake, kwamba ndugu wawili wa Halmashauri ya Nchi, Leonidha Pope na Luçi Xheka, hawakuwa “pamoja na familia zao” na kwamba mikutano haifanywi. Baadaye kukawa na fununu kwamba Spiro Vruho yuko hospitalini, naye Leonidha Pope na Luçi Xheka ni wagonjwa, andiko la Matendo 8:1, 3 lilirejelewa, ambapo Sauli wa Tarso aliwatia Wakristo gerezani. Ni nini kilichokuwa kikiendelea?
Leonidha Pope, Luçi Xheka, na Sotir Ceqi walikuwa wakifanya kazi katika kiwanda fulani ambapo washiriki wa Chama cha Kikomunisti walifanya mkutano na wafanyakazi wote, wakipigia debe dhana za Kikomunisti. Siku moja, kulipokuwa na mazungumzo kuhusu mageuzi, Leonidha na Luçi walisimama na kusema: “Hapana! Mwanadamu hakutokana na nyani!” Siku iliyofuata walichukuliwa na kutenganishwa na familia zao, na kupelekwa kufanya kazi uhamishoni katika miji ya mbali, adhabu ambayo huitwa internim (korokoroni) na Waalbania. Luçi alipelekwa katika milima ya Gramsh. Kwa kuwa waliamini kwamba Leonidha ndiye “mkubwa” wao, walimpeleka katika milima ya Burrel, yenye mawe-mawe na baridi kali. Miaka saba ilipita kabla ya kurudi nyumbani kwao, Tiranë.
Kufikia Agosti 1964, karibu mikutano yote iliacha kufanywa. Ripoti chache zilizopokewa zilionyesha kwamba ndugu hao walikuwa chini ya uchunguzi mkali wa Sigurimi. Stempu moja ilikuwa na ujumbe huu: “Mwombeni Bwana kwa niaba yetu. Nyumba zinapekuliwa. Hawaturuhusu kujifunza. Watatu wako korokoroni.” Mwanzoni, ilidhaniwa kwamba ndugu Pope na Xheka walikuwa wameachiliwa, kwa kuwa wao tu ndio waliojua mbinu hiyo ya kuandika chini ya stempu. Hata hivyo, baadaye ilikuja kujulikana kwamba Frosina, mke wa Luçi, ndiye aliyekuwa ametuma ujumbe huo.
Akina ndugu waliokuwa wakiongoza hawakuwako. Nao waliobaki hawakuweza kuwasiliana kwa sababu ya upelelezi wa Sigurimi. Hata hivyo, ndugu waliokuwa korokoroni waliwatolea ushahidi mzuri mtu yeyote waliyekutana naye. Watu wa Gramsh walikuwa wakisema: “Ungjillorë [wainjilisti] wako hapa. Hawajiungi na jeshi, lakini wanatujengea madaraja na kurekebisha majenereta.” Sifa nzuri ya ndugu hao ilijulikana kwa miaka mingi.
ALBANIA YAWA TAIFA LISILOAMINI KUWAPO KWA MUNGU
Albania ilivunja uhusiano wake na Muungano wa Sovieti na kujiunga na China. Dhana za Kikomunisti zilikuwa zimeanza kuenea sana hivi kwamba Waalbania kadhaa walianza kuvaa mavazi kama yale ya Mao Tse-tung, Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha China. Kufikia 1966, Enver Hoxha, alifutilia mbali nyadhifa katika jeshi, na kwa sababu ya hali hiyo ya wasiwasi, upinzani wowote uliozuka ulizimwa.
Magazeti ya serikali yalianza kuchapisha makala zilizokashifu dini, na kudai kwamba dini ni “hatari kwa jamii.” Halafu huko Durrës, kikundi cha wanafunzi kikatumia buldoza kuharibu kanisa. Muda si muda, katika mji mmoja baada ya mwingine, majengo ya kidini yakaanza kuharibiwa. Mwaka wa 1967, huku serikali ikiongoza katika vita dhidi ya dini, Albania ikawa nchi ya kwanza isiyoamini kuwapo kwa Mungu. Wakati ambapo nchi nyingine za Kikomunisti zilikuwa zikijaribu kudhibiti dini, Albania iliamua kuzikomesha kabisa.
Viongozi fulani wa dini ya Kiislamu, Waothodoksi, na Wakatoliki walitupwa gerezani kwa sababu za kisiasa. Hata hivyo, walio wengi kati yao waliendelea na maisha yao kwa sababu walilegeza msimamo na kuacha kabisa mambo ya dini. Majengo fulani ya kale ya kidini yaligeuzwa na kuwa majumba ya makumbusho. Haikuruhusiwa kuwa na misalaba, sanamu, misikiti, au minara ya kidini. Neno “Mungu” halikutajwa kamwe isipokuwa iwe ni kwa dharau. Mabadiliko hayo yalifanya hali ya kina ndugu iwe ngumu.
Katika miaka ya 1960, ndugu kadhaa walipoteza maisha yao. Wahubiri waliobaki ambao walikuwa wametawanyika waliendelea kuitetea kweli kwa kadiri ambavyo wangeweza. Lakini hata watu wenye kupendezwa walikuwa na woga mwingi wasiweze kusikiliza.
UPENDO WA KWELI HAUKUFIFIA KAMWE
Mwaka wa 1968, Gole Flloko aliwaandikia John na Helen Marks barua kuhusu afya yake iliyokuwa ikidhoofika. Ilikuwa marufuku kuhubiri na kufanya mikutano. Hata hivyo, Gole, mwenye umri wa miaka 80 na kitu, alieleza jinsi alivyokuwa akizungumza na marafiki na watu aliokutana nao sokoni, katika bustani, au kwenye mikahawa. Muda mfupi baadaye, Gole alikufa akiwa mwaminifu. Kama wengine wengi nchini Albania, hakuna chochote ambacho kingeweza kuuzima upendo wake kwa Yehova na kwa ile kweli.
Umri wake ukiwa umesonga sana, Spiro Vruho, hangeweza tena kufanya kazi ya kuzunguka. Mapema mwaka wa 1969, alipatikana akiwa amekufa ndani ya kisima. Sigurimi ilidai kwamba alijiua. Je, ndivyo ilivyokuwa?
Ingawa inadaiwa kwamba Spiro aliacha barua inayosema kwamba alikuwa ameshuka moyo sana, mwandiko haukuwa wake. Pia, kabla ya kufa, hakuna shaka kwamba Spiro alikuwa mwenye shangwe. Isitoshe, alikuwa na alama nyeusi-nyeusi shingoni, jambo linaloonyesha kwamba alishambuliwa. Hakuna kamba iliyopatikana kisimani, ambayo angeweza kuwa alitumia kujinyonga, nayo mapafu yake hayakuwa na maji.
Miaka kadhaa baadaye, ikapata kujulikana kwamba Spiro alikuwa ameambiwa asipopiga kura, yeye na familia yake watatupwa gerezani na kunyimwa chakula. Ndugu huko Tiranë walipata habari kwamba Spiro aliuawa siku moja kabla ya uchaguzi, na kutupwa kisimani. Mbali na kisa hicho kulikuwa na ripoti nyingine nyingi zilizodai kwamba Mashahidi wa Yehova wamejiua.
MIAKA YA KUTENGWA KWA LAZIMA
Mwaka 1971, Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote walifurahi washiriki zaidi walipoongezwa kwenye Baraza Linaloongoza huko Brooklyn, New York. Kulikuwa na matarajio makubwa ilipotangazwa kwamba makutaniko yataanza kuwa na wazee na watumishi wa huduma. Hata hivyo, ilichukua miaka mingi kabla ya ndugu zetu wa Albania kusikia kuhusu mabadiliko hayo ya kitengenezo. Walipata habari hizo wakati watalii kutoka Marekani walipokutana kifupi na dada Llopi Bllani huko Tiranë. Waliambiwa kwamba hakuna mikutano iliyokuwa ikifanywa, na kwamba kuna Mashahidi watatu tu watendaji katika mji huo, ingawa kwa kweli walikuwa wengi zaidi.
Kosta Dabe alikuwa nchini Ugiriki tangu 1966 akijaribu kutafuta kibali cha kurudi nyumbani kwao, Albania. Akiwa na umri wa miaka 76, alitaka kuwafundisha watoto wake kweli. Alipokosa kibali, Kosta aliacha pasipoti yake ya Marekani kwenye mpaka wa Albania na kuingia nchini, akijua kwamba huenda asiweze kamwe kutoka.
Mwaka wa 1975, Mwalbania fulani na mke wake kutoka Marekani waliingia nchini Albania wakiwa watalii. Waliandika kwamba upelelezi ni “mkali sana” na kwamba Mashahidi wa Yehova wanachunguzwa sana. Viongozi rasmi wa watalii, wengi wao kutoka Sigurimi, waliandamana na watalii kila mahali walipoenda. Baada ya watalii kuondoka, Sigurimi iligeuzia fikira zake watu wowote waliokuwa wamewasiliana na watalii hao. Wenye mamlaka hawakuwapenda wala kuwaamini watalii. Watu waliwaogopa wageni.
Novemba 1976 barua kutoka kwa Kosta Dabe iliripoti kwamba watu watano walihudhuria Ukumbusho huko Vlorë. Alijua kwamba kulikuwa na Mashahidi wawili, ambao kila mmoja wao alifanya Ukumbusho akiwa peke yake, mmoja mjini Përmet na mwingine Fier. Mjini Tiranë, Ukumbusho ulifanyiwa sehemu mbili, wawili walikutanika sehemu moja na wanne wakakutanika sehemu nyingine. Hivyo, kwa kutegemea habari alizojua, hudhurio la Ukumbusho mwaka wa 1976 lilikuwa angalau watu 13.
Miaka kadhaa baadaye, Kulla Gjidhari alikumbuka jinsi alivyoadhimisha Ukumbusho: “Asubuhi nilitengeneza mkate na kutayarisha divai. Jioni ya siku hiyo nilifunga mapazia na kuchukua Biblia niliyokuwa nimeificha nyuma ya choo. Nilisoma Mathayo sura ya 26 kuhusu jinsi Yesu alivyoanzisha Ukumbusho. Nilisali, nikauinua mkate, kisha nikaurudisha chini. Halafu nikasoma mistari zaidi ya Mathayo, nikasali tena, nikainua divai, kisha nikairudisha chini. Baada ya hayo, nikaimba wimbo. Kimwili, nilikuwa peke yangu, lakini nilikuwa na hakika kwamba ninaungana na ndugu zangu ulimwenguni pote!”
Kulla hakuwa na watu wengi wa ukoo. Miaka kadhaa awali Spiro Karajani alimchukua na kumlea, naye aliishi pamoja na Penellopi binti ya Spiro huko Tiranë. Spiro alikufa mwaka wa 1950 hivi.
ALBANIA YAZIDI KUJITENGA
Kipindi kipya cha kujitenga kilianza mwaka wa 1978 Albania ilipokata uhusiano na China. Katiba mpya ilikusudiwa kufanya Albania kuwa nchi inayojitegemea kwa kila jambo, ikiwa na sheria kali zinazoongoza kila sehemu ya maisha, kutia ndani maonyesho, dansi, vitabu, na sanaa. Muziki ulioaminika kuwa wa uchochezi ulipigwa marufuku. Waandishi walioidhinishwa tu ndio walioruhusiwa kuwa na taipureta. Yeyote aliyepatikana akifungulia vituo vya televisheni vya nchi nyingine alihojiwa na Sigurimi.
Katika hali hiyo yenye kukandamiza sana, ndugu kutoka Austria, Marekani, Sweden, Ujerumani, na Uswisi waliingia nchini wakiwa watalii na kujitahidi kuwasiliana na akina ndugu. Wachache waliopatikana walithamini sana jitihada hizo. Hata hivyo, akina ndugu kwa ujumla walikuwa wametengwa na wenzao hivi kwamba haikuwa rahisi kujua kwamba kuna mgeni.
Mwaka wa 1985, dikteta aliyekuwa ametawala kwa muda mrefu, Enver Hoxha, wa Albania akafa. Kisha kukawa na mabadiliko mengi ya kiserikali na kijamii. Mwaka uliofuata John Marks akafa, naye mke wake, Helen, aliyekuwa na umri wa miaka 60 na kitu, akaamua kwenda Albania. “Ukipata shida yoyote huko,” wenye mamlaka wakamwambia alipokuwa akitafuta kibali cha kuingia nchini humo, “shauri yako.”
Ziara ya Helen ya majuma mawili iliwafaa sana wahubiri wachache waliokuwa Albania. Hatimaye, Helen akakutana na Melpo, dada ya John, aliyekuwa amehubiriwa na ndugu yake miaka 25 iliyopita. Ingawa bado hakuwa amebatizwa, Melpo alitumiwa kwa miaka mingi na tengenezo kuwasiliana na akina ndugu nchini humo.
Helen alikutana pia na Leonidha Pope na Vasil Gjoka, aliyebatizwa mwaka wa 1960. Helen akapata kujua kuhusu Mashahidi saba waliokuwa bado hai katika sehemu mbalimbali nchini. Aliwajulisha akina ndugu wa Albania mambo mapya ya kitengenezo na jinsi kazi ilivyokuwa ikisonga mbele katika nchi nyingine za Kikomunisti. Kwa busara, Helen aliwahubiria watu wowote aliokutana nao. Hata hivyo, alitambua kwamba kulikuwa na matatizo mengi ya kiuchumi nchini Albania.
“Ili kupata maziwa kidogo tu,” asema, “mtu angelazimika kupanga foleni kuanzia saa 9 usiku. Maduka mengi hayakuwa na chochote.”
Mwaka wa 1987, ofisi ya tawi ya Austria na ya Ugiriki zilijitahidi kutuma ndugu zaidi nchini Albania. Mwaka wa 1988, Ndugu na Dada Peter Malobabic kutoka Austria, waliingia nchini humo wakiwa watalii. Walimpa Melpo blauzi aliyoipokea kwa furaha. Hata hivyo, alifurahi hata zaidi kupata kitabu “Mambo Mawili Yasiyobadilika Asiyoweza Mungu Kusema Uongo” kilichokuwa ndani ya blauzi hiyo.
Baadaye mwaka huo, ndugu mwingine na mke wake wakakutana na Melpo wakiwa na vitabu zaidi, hata hivyo walihitaji kujihadhari sana kwa sababu maofisa wa Sigurimi walikuwa wakiwachunguza kwa makini kama mwewe. Ndugu hao wageni walipata fursa chache sana za kuwasiliana na ndugu zao hasa wakati ambapo viongozi wa watalii hawakuwa pamoja nao. Walipata habari kwamba Leonidha ni mgonjwa na kwamba ndugu wengi wa Albania wamezeeka nao hawangeweza kutembea sana.
HALI ZAANZA KUBADILIKA
Hali ya kisiasa ilianza kubadilika mwaka wa 1989. Hukumu ya kifo kwa wanaojaribu kutoroka Albania ilifutiliwa mbali. Helen alizuru tena nchi hiyo katika majira ya kiangazi. Alitumia saa nyingi akiwasilisha habari na maagizo aliyokuwa amekabidhiwa. Vasil Gjoka pia aliwatembelea akina ndugu kwa vipindi vifupi kulingana na uwezo wake.
Maofisa wa Sigurimi walipata habari kwamba Helen yuko nchini nao wakaamua kumtembelea. Badala ya kumsumbua, walimwambia kwamba wanataka zawadi kutoka Marekani. Kwa muda mfupi tu walikuwa wamebadilika!
Ukuta wa Berlin ulibomolewa Novemba 9, 1989, na punde baadaye matokeo yake yakaanza kuonekana nchini Albania. Machi 1990 ghasia dhidi ya Ukomunisti zilizuka huko Kavajë. Maelfu ya watu walimiminika katika ofisi za ubalozi za nchi za kigeni mjini Tiranë wakitaka kuondoka nchini. Wanafunzi walidai mabadiliko nao wakagoma kula.
Februari 1991, umati mkubwa wa watu ukaiangusha sanamu ya Enver Hoxha, yenye urefu wa mita 10, iliyokuwa kwa miaka mingi katika Bustani ya Skanderbej huko Tiranë. Kulingana na watu hao, dikteta huyo hakuwapo tena. Mwezi wa Machi, Waalbania 30,000 hivi waliteka nyara meli kadhaa kutoka Durrës na Vlorë na kusafiri hadi Italia wakiwa wakimbizi. Mwezi huohuo, uchaguzi wa vyama vingi ulifanywa kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi. Ingawa Chama cha Kikomunisti kilishinda uchaguzi huo, ni wazi kwamba serikali ilikuwa imedhoofika.
Helen Marks alizuru Albania mara ya mwisho mnamo Agosti 1991, hata hivyo, wakati huo hali zilikuwa zimebadilika. Mwezi mmoja tu awali, serikali ilikuwa imeanzisha wizara ya dini, na kuhalalisha tena utendaji wa kidini baada ya miaka 24. Akina ndugu hawakupoteza wakati. Waliongeza mara moja bidii yao katika kazi ya kuhubiri na kupanga mikutano ya kutaniko.
Vasil Gjoka alizuru ofisi ya tawi ya Ugiriki ambako alikaa kwa muda fulani akijifunza jinsi ya kupanga kazi ya kuhubiri. Kwa kuwa hakujua Kigiriki vizuri, ndugu waliojua Kialbania kidogo walimfundisha Vasil kwa kadiri walivyoweza. Aliporudi Tiranë, Vasil alitumia kwa bidii yote aliyokuwa amejifunza na kujaribu kupanga vizuri zaidi mikutano miwili iliyokuwa ikifanywa kila juma. Mkutano mmoja ulikuwa funzo la gazeti la Mnara wa Mlinzi la Kialbania, lililokuwa limeanza kuchapishwa karibuni.
“Zamani, mikutano ilikuwa ikifunguliwa kwa wimbo na sala,” akumbuka ndugu mmoja, “tulikuwa tukiimba nyimbo tulizojifunza kutoka kwa ndugu wa kitambo. Kisha tukajifunza na baada ya funzo tulikuwa tukimalizia kwa wimbo mmoja—au mbili, au tatu, au zaidi! Hatimaye, tukafunga kwa sala.”
Mwezi wa Oktoba 1991 na Februari 1992, Thomas Zafiras na Silas Thomaidis walileta vitabu na magazeti Albania kutoka Ugiriki. Walikutana na ndugu huko Tiranë na pia wahubiri wa Berat ambao hawakuwa wamebatizwa. Walitayarisha orodha za watu wengi waliokuwa na hamu ya kujifunza na kupata msaada. Baada ya kuwa mayatima kiroho kwa muda mrefu, wengi walikuwa na njaa kali ya kiroho. Kwa mfano, huko Berat, watu wanaopendezwa walikuwa wakifanya mikutano, ijapokuwa hakukuwa na ndugu yeyote ambaye amebatizwa. Ni nini kingeweza kufanywa ili kuwashughulikia watu hao wenye njaa kiroho?
MGAWO AMBAO HAUKUTAZAMIWA
Michael na Linda DiGregorio walikuwa wamishonari katika Jamhuri ya Dominika. Babu na nyanya ya Michael ni baadhi ya Waalbania waliobatizwa Boston, miaka ya 1920, naye Michael alijua Kialbania kwa kiasi fulani. Kwa hiyo, Ndugu na Dada DiGregorio walipoamua kutembelea familia yao nchini Albania mwaka wa 1992, waliuliza Baraza Linaloongoza ikiwa wanaweza kukutana na akina ndugu watakapokuwa nchini humo kwa siku tatu. Walishangaa Baraza Linaloongoza lilipowaomba wabaki Albania kwa miezi mitatu, wasaidie kupanga kazi ya kuhubiri.
Katika ofisi ya tawi huko Roma, ndugu kutoka Ugiriki na Italia waliwapasha habari akina DiGregorio kuhusu hali nchini Albania na kuwaonyesha picha za baadhi ya akina ndugu wa Albania, kutia ndani Vasil Gjoka. Ndugu na Dada DiGregorio waliposafiri kwenda Tiranë mwezi wa Aprili 1992, kwa mara nyingine tena Waalbania waliokuwa ugenini waliruhusiwa kurudi nchini. Hata hivyo, bado kulikuwa na migogoro ya kisiasa, nao watu walikuwa na wasiwasi kuhusu wakati ujao.
Michael na Linda walipokuwa wakitembea kutoka katika uwanja wa ndege, familia ya Michael ilikuja mbio kuwalaki. Wakati huohuo, Michael akamtambua Vasil Gjoka, aliyekuwa ameelezwa kwamba akina DiGregorio wanawasili siku hiyo.
“Wewe nenda na familia,” Michael akamwambia Linda, “naja sasa hivi.”
Baada ya kumkumbatia Linda, watu wa familia wakabeba mizigo ya akina DiGregorio na kuharakisha kuelekea kwenye magari, huku Michael akienda haraka kukutana na Vasil.
“Nitarudi Tiranë Jumapili,” Michael akamwambia Vasil akiwa na haraka, “tutaonana.”
Koço, mtu wa familia ya Michael iliyokuwa Albania, ambaye hakujua kwamba Michael na Linda ni Mashahidi wa Yehova, akamwendea haraka na kumwambia: “Unafanya nini? Hatuzungumzi na watu tusiowajua!”
Walipokuwa wakisafiri katika njia zenye kupinda-pinda kuelekea Korçë, akina DiGregorio wakaona jinsi nchi hiyo ilivyokuwa tofauti kabisa na Karibea. “Kila kitu kilikuwa kimezeeka, chenye rangi ya kahawia au kijivu-jivu, na kimejaa vumbi,” akumbuka Michael. “Kulikuwa na seng’enge kila mahali. Watu walionekana hoi. Magari yalikuwa machache sana. Madirisha yalikuwa yamevunjika. Wakulima walikuwa wakilima kwa majembe. Mambo yalikuwa vilevile yalivyokuwa zamani za akina babu na nyanya! Tulihisi kana kwamba tumerudi enzi hizo!”
“MUNGU ALIKUWA NANYI KATIKA SAFARI YENU”
Koço alikuwa na kitu fulani alichokuwa ameficha kwa muda mrefu, naye alitaka kumwonyesha Michael. Nyanya ya Michael alipokufa, familia iliyokuwa Boston iliandikia familia iliyokuwa Albania barua ndefu. Kurasa kumi za kwanza zilizungumzia hasa mambo ya kifamilia, lakini kuelekea mwisho wa barua hiyo, familia hiyo ilieleza kuhusu ufufuo.
“Polisi waliichunguza barua hiyo,” Koço akamwambia Michael, “na kusoma kurasa chache za kwanza. Kisha wakachoka na kusema: ‘Chukueni! Ni mambo ya kifamilia tu!’ Niliposoma sehemu ya mwisho, nilifurahi sana kusikia kuhusu Mungu!”
Ndipo Michael akaeleza kwamba yeye na Linda ni Mashahidi wa Yehova, kisha akamhubiria Koço kwelikweli.
Kama ilivyokuwa nyakati za Biblia, Waalbania huhisi kwamba ni jukumu lao kuwatunza na kuwalinda wageni wao. Kwa hivyo, Koço akasisitiza kwamba ataambatana na Michael na Linda kwenda Tiranë.
“Tulipofika Tiranë, hatukuipata nyumba ya Vasil,” akumbuka Michael, “kwa sababu barabara hazikuwa na majina. Kwa hiyo, Koço akapendekeza tuulizie kwenye ofisi ya posta.”
“Aliporudi kutoka posta,” asema Linda, “Koço alikuwa ameduwaa, nasi tukaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Vasil.”
Baadaye, Koço akaeleza: “Nilipoingia posta na kumuulizia Vasil, waliniambia: ‘Mtu huyo ni mtakatifu! Una habari amepatwa na nini? Tiranë nzima, hakuna mtu mwadilifu kama huyo!’ Niliposikia hivyo, nikajua kwamba Mungu alikuwa nanyi katika safari yenu! Siwezi kuwazuia!”
KUPANGA MAMBO TIRANË
Vasil alifurahi sana kuwaona akina DiGregorio, nao walizungumza kwa saa nyingi. Jioni ndipo Vasil alipowaeleza kwamba Jani Komino, aliyekuwa amefungwa pamoja na Nasho Dori, alikufa asubuhi hiyo. Kwa nini Vasil hakwenda kwenye mazishi ya ndugu huyo mpendwa aliyekuwa rafiki yake mkubwa? “Kwa sababu,” akaeleza, “nilikuwa nasubiri mtu aliyetumwa na Baraza Linaloongoza.”
Michael na Linda walihitaji kukaa Tiranë, hata hivyo, serikali ya wakati huo haikuwaruhusu wageni kukaa mjini. Wangefanya nini?
“Tuliacha mambo mikononi mwa Yehova,” asema Michael, “na hatimaye tukapata nyumba ndogo ya kukaa.”
“Wenye nyumba ndio waliokuwa na ufunguo,” akumbuka Linda, “nao waliingia na kutoka wapendavyo. Isitoshe, tulikuwa tukipita katika nyumba ya mwingine ili kuingia kwetu. Lakini angalau, nyumba yetu haikuwa njiani, nasi hatukutaka kuwa hadharani sana.”
Akina DiGregorio waliwasikiliza kwa saa nyingi ndugu wazee wa Tiranë wakisimulia majaribu waliyokuwa wamevumilia. Hata hivyo, mojawapo ya matatizo ni kwamba baadhi ya ndugu hao hawakuaminiana.
“Kivyake, kila mmoja alikuwa mwaminifu,” akumbuka Michael, “hata hivyo walishuku uaminifu wa wenzao. Hata hivyo, ijapokuwa hawakuwa na uhusiano wa karibu kati yao, hawakujitenga nasi. Baada ya kuzungumzia hali hiyo kwa utulivu, walikubali kwamba jambo kuu ni kulitangaza jina la Yehova. Waliungana katika upendo na kuwa na matumaini kuhusu wakati ujao.”
Ilionekana wazi kwamba kutaniko lilikuwa limebaki nyuma sana. Kwa mfano, Kulla Gjidhari na Stavri Ceqi walipokiona kijitabu cha Kuyachunguza Maandiko Kila Siku, walifungua-fungua kurasa zake, wasijue ni nini.
“Oh, Manna!” Stavri akasema kwa sauti, akirejelea kile kitabu Daily Heavenly Manna for the Household of Faith, kilichokuwa kikitumika zamani, Stavri alipojifunza kweli.
“Samahani,” akauliza Kulla, “Ndugu Knorr anaendeleaje? Rafiki yake Fred Franz yu mzima?” Maswali hayo yalionyesha wazi jinsi walivyokuwa wamebaki nyuma.
ULIKUWA UKUMBUSHO WA PEKEE!
Chumba kidogo ambacho akina ndugu walikuwa wakitumia kwa ajili ya mikutano yao, nyumbani kwa Vasil Gjoka, kilikuwa kidogo sana kisiweze kutumiwa kwa ajili ya Ukumbusho. Badala yake, wahudhuriaji 105 walikusanyika katika chumba ambacho awali kilikuwa makao makuu ya gazeti la Chama cha Kikomunisti. Hiyo ndiyo mara ya kwanza mjini Tiranë kwa Ukumbusho kufanyiwa mahali pa umma. Ijapokuwa kulikuwa na wahubiri 30 tu nchini Albania mwaka wa 1992, walishangilia hudhurio la watu 325 kwenye Ukumbusho.
Kikundi cha watu wenye kupendezwa huko Tiranë kilikuwa kikiongezeka, huku hudhurio nyumbani kwa Vasil likifikia watu 40. Wapya fulani walitaka kuwa wahubiri, na wengine walitaka kubatizwa. Akina ndugu walitumia muda mwingi wakipitia maswali pamoja na waliotaka kubatizwa. Kwa sababu kitabu Tumefanywa Tengenezo Tutimize Huduma Yetu hakikuwa kimechapishwa katika Kialbania, kila swali lilihitaji kutafsiriwa kwa ajili ya wale waliotaka kubatizwa. Wengine walifundishwa vizuri ili kuhakikisha kwamba wanaielewa kweli. Ingawa hakuna yeyote kati yao aliyekuwa amejifunza Biblia kwa njia rasmi, ilishangaza kuona kina cha ujuzi wao wa Biblia.
KUTAMBULIWA KISHERIA HATIMAYE!
Majuma kadhaa yaliyofuata, akina ndugu walitumia muda mwingi wakizungumza na wanasheria na maafisa wengine, wakijaribu kusajili kisheria kazi ya kuhubiri Ufalme. Tayari kikundi cha akina ndugu na watu wanaopendezwa kilichokuwa Tiranë kilikuwa kimetoa maombi rasmi, lakini sasa kulikuwa na serikali nyingine mamlakani, kwa hiyo, jitihada zilihitajiwa.
“Kila mahali tulipokwenda, tulikwenda kwa miguu,” akumbuka ndugu mmoja. “Tulipokuwa tukitembea mjini, tulikuwa tukikutana na waziri wa haki za kibinadamu, waziri wa mambo ya ndani, waziri wa haki, mkuu wa polisi, washiriki wa mahakama ya kikatiba, na watu wengine wenye mamlaka. Watu hao walikuwa na fadhili na walifurahi kwamba mambo yalikuwa yameanza kuwa mazuri. Tayari wengi wao walijua kuhusu ungjillorë. Hakukuwa na shaka kamwe kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa wakiendesha shughuli zao nchini Albania.”
Kwa majuma kadhaa, maafisa walikuwa wamesema kwamba serikali itawasajili rasmi Mashahidi wa Yehova, lakini hakuna lolote lililofanywa. Hata hivyo, matumaini yalipatikana wakati Angelo Felio, ndugu kutoka Marekani mwenye asili ya Kialbania, alipotembelea familia yao mjini Tiranë. Alipokuwa Albania, Angelo aliandamana na ndugu hao kwenda kumwona mshauri wa waziri wa serikali aliyekuwa na mamlaka ya kutusajili rasmi. Mshauri huyo alifurahi alipojua kwamba familia ya Angelo inatoka katika eneo moja na familia yao.
“Kwenu ni wapi?” akamwuliza Angelo. Kwa kushangaza, wote walikuwa watu wa kijiji kimoja.
“Ukoo wenu?” akauliza.
Amini usiamini, walikuwa watu wa familia moja, lakini familia zao hazikuwa zimeonana kwa miaka mingi.
“Karatasi zenu ziko sawa, nami nilikuwa tayari kuwasaidia,” akasema. “Lakini sasa, sina budi kufanya hivyo, kwa kuwa wewe ni wetu!”
Siku chache baadaye, mshauri huyo akawakabidhi akina ndugu Oda Na. 100, iliyowatambua kisheria Mashahidi wa Yehova nchini Albania. Hatimaye, ibada ya Mungu wa kweli, Yehova, iliyokuwa imepigwa marufuku tangu 1939, ikatambuliwa kisheria na huru! “Hatuna maneno ya kufafanua tulivyohisi moyoni siku hiyo,” akina DiGregorio wakasema.
Majuma kadhaa baadaye, ofisi ya tawi ya Ugiriki, iliyokuwa ikisimamia kazi nchini Albania, ikamtuma Robert Kern azuru Tiranë. Robert aliwatangazia akina ndugu wenyeji kuhusu kusajiliwa kwao na kuundwa kwa Kutaniko la Tiranë. Pia, aliwajulisha kwamba mipaka ya eneo la kutaniko hilo ni “nchi nzima ya Albania.” Kazi ya kuhubiri nyumba kwa nyumba ilihitaji kufanywa kwa bidii. Mjini Tiranë, nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala ilikodiwa kwa ajili ya makao ya wamishonari na ofisi. Nyumba hiyo ilipakana na chumba kingine kikubwa ambacho kingeweza kutumiwa kuwa Jumba la Ufalme la kwanza.
KONDOO ALIYEKUWA AMEPOTEA APATIKANA
“Kuna Mashahidi wowote Vlorë?” akina ndugu wakauliza walipokuwa wakizungumzia maendeleo katika kazi ya kuhubiri nchini Albania. Baadhi yao walimjua ajuza mmoja ambaye yasemekana alikuwa amerukwa na akili. Halafu mwanamke fulani akaja ofisini na kusema kwamba yeye na familia yake ni ungjillorë na kwamba mtu fulani anayeitwa Areti ndiye aliyewafundisha kweli huko Vlorë. Kwa hiyo ndugu wa Tiranë wakafunga safari mpaka Vlorë kumtafuta Areti.
Areti Pina, mwanamke mfupi mkongwe, akawakaribisha nyumbani kwake. Hata hivyo, alionekana kuwa mnyamavu. Walipomjulisha kwamba wao ni ndugu zake wa kiroho, hakujishughulisha.
“Naomba niwaulize maswali kadhaa,” akasema Areti baada ya kimya cha muda. Kisha akaanza kuwanyeshea maswali: “Mnaamini Utatu? Mungu anaitwa nani? Mnaamini moto wa mateso? Inakuwaje tunapokufa? Dunia je? Ni wangapi watakaoenda mbinguni?”
Ndugu hao wakajibu maswali yake yote.
Kisha Areti akauliza: “Huwa mnahubiri?”
“Ndiyo,” ndugu mmoja akajibu, “tunahubiri.”
“Lakini,” akaongeza, “mnahubiri jinsi gani?”
Ndugu huyo akamjibu: “Nyumba kwa nyumba.”
Areti akaanza kutokwa na machozi, akasimama, na kuwakumbatia ndugu hao.
“Sasa najua kwamba ninyi ni ndugu zangu!” akasema. “Watu wa Yehova tu ndio wanaohubiri nyumba kwa nyumba!”
Vikundi vya Kiprotestanti huko Vlorë vilikuwa vimesikia kwamba Areti ni mtu wa dini navyo vikamwomba ajiunge nao. “Lakini sikutaka kuchangamana kamwe na Babiloni Mkubwa!” akawaeleza ndugu hao. “Kwa hiyo, nilitaka kuhakikisha kwamba kwa kweli ninyi ni ndugu zangu wa kiroho!”
Areti alibatizwa kitambo, mwaka wa 1928, akiwa na umri wa miaka 18. Alikuwa akipanda na kushuka milima, akihubiri na Biblia mkononi mwake. Ijapokuwa Areti alikuwa amepoteza mawasiliano na ndugu zake kwa miaka mingi, aliendelea kuhubiri kwa uaminifu akiwa peke yake.
“Yehova ni Mungu wa ajabu,” akasema Areti huku akibubujikwa na machozi. “Hakunisahau kamwe!”
Watu walidhani Areti amerukwa na akili kwa kuendelea kumwamini Mungu katika nchi iliyokuwa ikitawaliwa na watawala wakatili. Hata hivyo, Areti hakuwa amerukwa na akili. Akili yake ilikuwa timamu kabisa!
KUNA MENGI YA KUFANYWA!
Kwa kuwa sasa kazi yetu ilikuwa imesajiliwa kisheria, kulikuwa na mengi ya kufanywa ili kuwasaidia wengi nchini Albania wapendezwe na ujumbe wetu. Akina ndugu walihitaji kufundishwa mambo mapya na kuimarishwa kiroho. Vitabu vilihitajiwa katika lugha ya Kialbania kwa ajili ya akina ndugu na wengine shambani. Pia, wahubiri zaidi walihitajiwa haraka. Msaada ungetoka wapi?
Mwaka wa 1992, mapainia wa pekee waliwasili kutoka Italia na Ugiriki, na kuhudhuria mtaala wa kujifunza Kialbania. Wakati huohuo, kikundi kidogo kikaanza kutafsiri vitabu vyetu. Ijapokuwa nyakati nyingine hakukuwa na umeme kwa siku 21 mfululizo, akina ndugu hawakuvunjika moyo, badala yake waliendelea kufanya kwa bidii kazi waliyokuwa nayo.
Pia kulikuwa na kazi nyingi ya mkono. Kulipokuwa na baridi, makao ya wamishonari yalihitaji kupashwa moto. Lakini haikuwezekana kununua kuni Albania. Ndugu hao walifanya nini? Ndugu kutoka Ugiriki waliwasaidia kwa kutuma magogo ya miti na msumeno wa umeme. Hata hivyo, bado kulikuwa na tatizo, kwa kuwa mlango wa jiko ulikuwa mdogo, na hakukuwa na umeme wa kuendesha msumeno. Ndugu mmoja alikuwa na rafiki aliyekuwa na shoka. Rafiki huyo alikuwa akiishi upande wa pili wa Tiranë. Kwa kuwa hakukuwa na mabasi, ilichukuwa saa mbili kufikisha shoka hilo kwa makao ya wamishonari, nalo lilipaswa kurudishwa kabla ya giza kuingia. “Sote tulipokezana zamu ya kutema kuni,” akumbuka mmishonari mmoja, “nasi tukafukuza baridi!”
Huku kuni zikiendelea kutemwa na mitaala ya lugha ikiendelea, kikundi cha watafsiri wa Kialbania walitembelewa kwa mara ya kwanza na Nick na Amy Ahladis kutoka katika Huduma za Tafsiri, Patterson, New York. Ndugu na Dada Ahladis waliwatembelea tena baadaye mara kadhaa. Mtazamo wao wenye fadhili na usawaziko uliwasaidia watafsiri hao wapya, nao wakajifunza haraka na kufanya kazi nzuri. Ofisi ya tawi ya Italia ilikuwa ikichapa vitabu na kuvituma Albania.
Kazi yote hiyo haikuwa ya bure kwa kuzingatia jinsi wahubiri wengi walivyopata matokeo mazuri. Wahubiri wapya waliwaka roho pia. Kwa mfano, Lola, alikuwa mhubiri mpya, hata hivyo, alihubiri saa 150, 200, au hata zaidi kila mwezi! Aliposhauriwa awe na usawaziko na kupanga utumishi wake vizuri, Lola alijibu: “Maisha yangu hayakuwa na maana yoyote hadi sasa! Sina lingine la kufanya na wakati wangu!”
KAZI YASONGA MBELE
Mwezi wa Machi 1993, ulikuwa mwezi wa pekee nchini Albania. Mapainia wa pekee walianza migawo mipya huko Berat, Durrës, Gjirokastër, Shkodër, Tiranë, na Vlorë; gazeti la Mnara wa Mlinzi la Machi 1 lilikuwa toleo la kwanza kutafsiriwa na kikundi cha kutafsiri Kialbania; akina ndugu walifanya mkutano wao wa kwanza wa Shule ya Huduma ya Kitheokrasi, na kwa mara ya kwanza mikutano yote mitano ikafanywa; toleo la kwanza la Huduma Yetu ya Ufalme likatolewa; na kusanyiko la kwanza la pekee likafanywa Skanderbej Square katika Ballet-Opera Theater, huko Tiranë.
Wajumbe waliwasili kutoka Ugiriki na Italia ili kufurahia kusanyiko hilo la pekee la kihistoria. Nasho Dori alifungua kusanyiko hilo kwa sala, akimshukuru Yehova kwa baraka zote walizokuwa wakifurahia. Hudhurio lilikuwa 585, na 41 wakabatizwa! Kati yao mlikuwa watoto na wajukuu wa ndugu waliokuwa wamemtumikia Yehova kwa uaminifu nchini Albania.
Kulikuwa na msisimuko mkubwa mwaka wa 1993 kwa sababu ya kusanyiko la kwanza la wilaya lililofanywa nchini Albania. Lilihudhuriwa na watu zaidi ya 600, kukiwa na wajumbe kutoka Austria, Italia, Ufaransa, Ugiriki, na Uswisi. Ndugu wa Albania walikuwa na furaha kama nini kwamba baada ya kuwa mayatima kiroho kwa muda mrefu sana, sasa wangeweza kuchangamana kwa uhuru na ndugu wengi sana hivyo kutoka katika nchi nyingi!
Ili kuwe na utaratibu mzuri zaidi, Baraza Linaloongoza liliweka rasmi Halmashauri ya Nchi. Halmashauri hiyo ilikuwa na Ndugu Nasho Dori, Vito Mastrorosa, na Michael DiGregorio. Halmashauri hiyo ilifanya kazi chini ya usimamizi wa ofisi ya tawi ya Italia. Mojawapo ya majukumu yao ya kwanza lilikuwa kutafuta mahali kwa ajili ya ofisi na pia kikundi cha watafsiri kilichokuwa kikiongezeka.
Stefano Anatrelli kutoka Italia alikuwa katika kikundi kilichofuata cha mapainia wa pekee kilichoanza kujifunza Kialbania. Baada ya kujifunza lugha hiyo kwa majuma matano, aliombwa afike ofisini, kisha akaambiwa: “Tungependa uwatembelee mapainia wa pekee na vikundi ukiwa mwangalizi wa mzunguko.”
“Itawezekanaje, na hata sijajua kuzungumza Kialbania kwa ufasaha!” akasema Stefano kwa mshangao. Hata hivyo, aliuona mgawo huo kuwa pendeleo kubwa. Baada ya kusaidiwa kutayarisha hotuba kadhaa, Stefano akang’oa nanga kuelekea sehemu za mbali zaidi za Albania. Miaka 30 hivi ilikuwa imepita tangu Spiro Vruho alipotembelea akina ndugu akiwa mwangalizi wa mzunguko wakati wa marufuku. Mwaka wa 1995, Stefano aliwekwa rasmi kuwa mshiriki wa Halmashauri ya Nchi.
Mwaka wa 1994, kikundi cha tatu cha mapainia, kutoka Italia, kikaja Albania. Wahubiri wapya wa Albania walichochewa sana na bidii ya mapainia hao. Kufikia mwishoni mwa mwaka wa utumishi wa 1994, kulikuwa na wahubiri 354.
Hata hivyo, wahubiri wengi walikuwa na matatizo ya kihisia. Haikuwa rahisi kubadilika kutoka katika mfumo wenye kukandamiza sana na kuingia katika mazingira huru kabisa. Walipokuwa chini ya serikali ya kidikteta, walilazimika kuwa waangalifu kutoonyesha hisia zao waziwazi, hasa kuelekea watu wa nchi nyingine. Lakini, ndugu na dada hao waliotoka nchi nyingine waliwaelewa na pole kwa pole wakawasaidia kuonyesha hisia zao kwa uhuru zaidi.
Mwaka huohuo ndugu na dada wenye umri mkubwa na pia wahubiri wapya walifurahi kumwona Theodore Jaracz, ndugu wa kwanza wa Baraza Linaloongoza kuzuri Albania. Watu zaidi ya 600 walikusanyika kusikiliza hotuba aliyotoa Tiranë.
Wakati huohuo, uwanja ulikuwa umenunuliwa Tiranë kwa ajili ya ofisi. Kwa muda usiozidi miezi sita, kikundi cha ndugu wenye bidii kutoka nchi za kigeni walikarabati jumba la zamani lililokuwa katika uwanja huo, wakalifanya kuwa ofisi za kisasa, na kujenga makao yanayoweza kutoshea watu 24. Programu ya wakfu ilifanywa Mei 12, 1996, wakati ambapo Ndugu Milton Henschel wa Baraza Linaloongoza alipozuru Albania.
WALIHUBIRI PEKE YAO
Kijana fulani anayeitwa Arben huko Korçë, alisoma vitabu vya Biblia alivyokuwa ametumiwa na dada yake na kutambua kwamba vina ukweli. Aliandikia ofisi ya Albania, na kwa muda akaendelea kujifunza kweli kupitia barua. Ili kumsaidia kiroho, ndugu wawili walifunga safari ya pekee kwenda kumtembelea. Walipokuwa wakizungumza na Arben, ilionekana wazi kwamba anastahili kuwa mhubiri. Ndugu hao wawili wakaandamana naye hadi katikati ya Korçë ili aone wanavyowahubiria wapita-njia.
Arben asimulia: “Kisha wakanipa magazeti na kusema, ‘Haya, ni zamu yako sasa.’ Wakaniambia niendelee peke yangu, nami nikaendelea.”
Miezi kadhaa ilipita kabla ya mapainia wa pekee kuja kumsaidia. Hata hivyo, watu aliowahubiria walimsikiliza. Punde si punde baada ya mapainia wa pekee kufika, kikundi kikaanzishwa.
Kuelekea mwisho wa mwaka huo, mapainia waliokuwa Vlorë waliipigia simu ofisi, wakisema kwamba Areti Pina ni mgonjwa na anataka kuonana na ndugu wanaosimamia mambo. Ndugu alipofika, Areti alimwambia kila mtu aondoke chumbani ili aongee na ndugu huyo faraghani.
“Sina muda mrefu wa kuishi,” akasema, huku akipumua kwa shida. “Nimekuwa nikifikiria, nami nataka kukuuliza jambo fulani. Siwezi kuelewa mambo yote, hata hivyo, nahitaji kujua, Je, mambo yanayotajwa katika kitabu cha Ufunuo yametimia?”
“Ndiyo, Areti, mengi yametimia,” akamjibu ndugu huyo, kisha akamtajia mambo kadhaa ambayo bado hayajatimia. Areti alisikiliza kwa makini kila neno.
“Sasa naweza kufa kwa amani,” akamwambia. “Nilitaka kujua tuko karibu kadiri gani.”
Kwa miaka mingi Areti alikuwa mhubiri mwenye bidii—iwe alihubiri milimani akiwa peke yake au akiwa kitandani alipokuwa mgonjwa. Muda mfupi baada ya mazungumzo hayo, Areti akafa akiwa mwaminifu, akiwa na tumaini la kutawala pamoja na Yesu mbinguni.
ALIKUWA NA IMANI YENYE NGUVU HADI MWISHO
Nasho Dori, akiwa na umri wa miaka 80 na kitu, alikuwa mgonjwa na dhaifu. Lakini kikundi kimoja cha akina ndugu kilihitaji sana kutiwa moyo naye—vijana waliotakiwa kujiunga na jeshi. Makasisi wa Kiothodoksi huko Berat, ambao waliona kijicho kwa sababu ya ongezeko la Mashahidi wa Yehova, waliwashinikiza wenye mamlaka wawafunge vijana hao.
Ndugu sita vijana waliokataa kujiunga na jeshi wangeweza kufungwa miezi kadhaa. Akijua kwamba wanahitaji kutiwa moyo, Nasho aliketi kitandani na kurekodi ujumbe kwenye video kwa ajili yao.
“Msiogope,” Nasho akawahimiza ndugu hao vijana. “Haitakuwa mara ya kwanza. Yehova atakuwa nanyi. Mkitupwa gerezani, msiwe na wasiwasi. Hatimaye jina la Yehova litatukuzwa.”
Afya ya Nasho ilipozidi kuzorota, aliwaita akina ndugu na kuwaambia: “Nimemwomba Yehova msamaha. Juma lililopita nilikuwa na maumivu makali sana hivi kwamba nikaomba nife. Kisha nikawaza, ‘Yehova, wewe ndiwe Chanzo cha uhai. Uhai una thamani sana machoni pako. Nilikuwa nikiomba kitu ambacho ni kinyume cha mapenzi yako. Tafadhali nisamehe!’”
Nasho alipopata habari kwamba idadi ya wahubiri nchini Albania imefikia 942, akasema: “Hatimaye tumepata umati mkubwa nchini Albania!” Siku chache baadaye, akafa, akiwa na tumaini la kutawala pamoja na Yesu mbinguni.
TRAZIRA—WAKATI WA MCHAFUKO
Kufikia 1997, kulikuwa na udhalimu, na ufisadi mwingi. Waalbania wengi waliuza kila kitu walichokuwa nacho na kuweka pesa zao zote katika miradi ya kujitajirisha upesi. Miradi hiyo ilipoporomoka, watu hao wenye uchungu mwingi walianza kufanya maandamano.
Wakati huohuo, kusanyiko la pekee lilipokuwa likiendelea, dada aliyekuwa ameajiriwa na ofisa mwenye cheo kikubwa aliwajulisha akina ndugu kwamba waziri mkuu anataka kujiuzulu. Dada huyo alipata habari kwamba kutakuwa na jeuri isiyo na kifani. Programu ya kusanyiko ikakatizwa ili akina ndugu warudi nyumbani haraka. Saa mbili baada ya programu kwisha, nchi nzima ilikuwa katika hali ya hatari na amri ya kutotoka nje ikatolewa.
Hakuna aliyejua kinachoendelea. Kulikuwa na uvumi mwingi. Ni uvamizi wa nchi nyingine au ni siasa za nchi? Ile miradi ya kujitajirisha upesi ilikuwa imeporomoka, na watu wengi walikuwa wamepoteza mali zao zote. Fujo zikazuka Vlorë. Watu walivunja ghala za silaha na kupora silaha zote. Vituo vya habari viliporipoti mambo yaliyokuwa yakiendelea, watu katika mji mmoja baada ya mwingine wakaingilia jeuri. Nchi nzima ikachafuka, nao polisi wakashindwa kudhibiti hali. Albania ikasambaratika, huku maasi na uvunjaji wa sheria vikienea.
Wengi kati ya wale watumishi wa wakati wote 125 waliokuwa Albania wakakimbilia Tiranë kutafuta usalama. Waalbania wengi waliwalaumu wageni kwa sababu ya mambo yaliyokuwa yakiendelea, kwa hiyo, jambo la busara likawa mapainia wote kutoka nchi za kigeni waondoke. Kwa kuwa uwanja wa ndege ulikuwa umefungwa, baadhi ya mapainia waliokuwa wametoka Italia walipelekwa Durrës, bandari iliyokuwa mikononi mwa wenyeji waliokuwa wamejihami. Baada ya kusubiri kwa saa 12 katika hali ya wasiwasi, mapainia hao waliabiri meli ya kurudi nyumbani kwao.
Halmashauri ya Nchi ilikuwa ikiwasiliana kila siku na ndugu katika sehemu mbalimbali nchini. Kipindi cha asubuhi, kulikuwa na utulivu wenye kutia wasiwasi. Lakini kuanzia alasiri watu walikuwa wakifyatua bunduki zao na kuendelea usiku kucha mpaka karibu mapambazuko. Wengine hata walikuwa na makombora ya kuangusha ndege. Baadaye ghasia hizo zikaanza kuitwa trazira, au msukosuko.
“HATIMAYE JINA LA YEHOVA LITATUKUZWA”
Arben Merko, mmoja wa wale ndugu sita wa Berat waliofungwa kwa sababu ya kutokuwamo, asimulia: “Katika chumba changu gerezani, kulikuwa na shimo dogo ukutani. Mfungwa katika chumba jirani akaniuliza mimi ni nani.” Arben alimhubiria kwa majuma kadhaa. Siku moja hakumsikia tena.
Baada ya Arben kufunguliwa, kijana fulani alifika mlangoni pake. Arben hakumtambua, hata hivyo, sauti yake haikuwa geni—ni yule jirani yake gerezani.
“Nimekuja kukupa kifaa hiki,” kijana huyo akamwambia Arben, akimkabidhi amplifaya.
“Wakati wa trazira,” akamwambia Arben, “Niliiba amplifaya hii katika Jumba lenu la Ufalme. Lakini mambo uliyoniambia nilipokuwa gerezani, yalinichochea sana. Nataka kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu, kwa hiyo nimeirudisha kwako.”
Arben akakumbuka ujumbe wa mwisho wa Nasho Dori aliorekodi kwa ajili ya vijana washika-utimilifu: “Hatimaye jina la Yehova litatukuzwa.”
KUTUNZA KONDOO ZA YEHOVA
Wazee kutoka nchi nyingine walipoondoka nchini, makutaniko mengi na vikundi vikubwa vilibaki mikononi mwa watumishi wa huduma waliokuwa na umri wa miaka 19, 20 hivi. Siku moja, watatu kati yao, walijasiria kusafiri kutoka Vlorë hadi Tiranë. Wakijua kwamba kuna upungufu wa chakula, ndugu wa Halmashauri ya Nchi waliwauliza ikiwa kuna chochote wanachohitaji.
“Tumeishiwa fomu za kujaza ripoti za utumishi wa shambani,” vijana hao wakajibu. Kama vile waaminifu wa kale, walihangaikia uhitaji wa kiroho kuliko mahitaji ya kimwili. Kisha wakasema kwamba watu wanaitikia vizuri habari njema kwa sababu ya woga na kukosa tumaini.
Punde baada ya Ukumbusho, ofisi ilipokea simu. “Sisi ni kikundi cha dada zenu hapa Kukës,” akasema mmoja wao, “nasi tumekuwa tukifanya mikutano peke yetu tangu mapainia walipoondoka.”
Kwa sababu ya ghasia, ndugu wa Tiranë walikuwa wamepoteza mawasiliano na wahubiri wa Kukës. Hata hivyo, kikundi cha wahubiri saba ambao hawakuwa wamebatizwa kilifanya Ukumbusho sehemu mbili. Ijapokuwa walikuwa na shaka kwamba huenda hawakufanya Ukumbusho ifaavyo, waliripoti hudhurio la watu 19 katika sehemu zote mbili. Kwa kushangaza, licha ya amri ya kutotoka nje na hali ngumu, mwaka wa 1997, Ukumbusho nchini Albania ulihudhuriwa na watu 3,154. Na licha ya mchafuko, wahubiri waliendelea kuhubiri na kuwafariji wengine, huku wakijiendesha kwa tahadhari.
Halmashauri ya Nchi ilipopata habari kwamba akina ndugu wa Gjirokastër wanahitaji chakula na vitabu, walijadili iwapo ni salama kutuma lori huko. Hata hivyo, mazungumzo yao yalikatizwa na dada aliyewajulisha kwamba mtangazaji wa habari anayeweza kuwapa habari muhimu amekuja kuwaona.
Ijapokuwa mtangazaji huyo hakujua mambo waliyokuwa wakizungumzia, aliwashauri: “Vyovyote vile, msiende kusini kesho. Tumepokea habari kwamba kuna njama fulani mbaya inayopangwa Tepelenë.” Kwa kuwa lori la kwenda Gjirokastër lingepitia Tepelenë, ndugu hao wakaamua kufutilia mbali safari hiyo.
Siku iliyofuata, mwendo wa saa tano hivi, taarifa ya pekee ya habari ikaripoti kwamba mapambano makali sana yalikuwa yamezuka Tepelenë na kwamba daraja lililo mjini limelipuliwa. Ndugu hao walimshukuru Yehova kama nini kwamba walizuiwa kwenda huko!
Kwa majuma kadhaa, familia ya Betheli ilisikia milio ya risasi usiku kucha, na mara nyingi walifanya ibada yao ya asubuhi huku kukiwa na milio ya risasi na mabomu. Risasi zilikuwa zikifyatuliwa ovyo, na sikuzote kulikuwa na hatari ya kupatwa na moja ya risasi hizo. Kwa sababu ya kiusalama, familia ya Betheli haikutoka nje, nao watafsiri waliketi sakafuni mbali na madirisha huku wakiendelea na kazi yao.
Aprili 1997, wanajeshi 7,000 wa vikosi vya Umoja wa Mataifa walifika ili kurejesha utulivu nchini. Kufikia Agosti, wanajeshi hao walikuwa wameondoka Albania, na ikawezekana kwa akina ndugu kupanga kusanyiko la wilaya. Wahubiri walifurahi sana; kwa kuwa kwa miezi mingi walikuwa wakikutanika katika vikundi vidogo-vidogo tu.
Wanyang’anyi wenye silaha walizuilia baadhi ya mabasi yaliyokodiwa na akina ndugu ili kuwapeleka kusanyikoni. Hata hivyo, walipojua kwamba abiria hao ni Mashahidi wa Yehova, walisema: “Ninyi watu mko tofauti! Hatuwezi kuwadhuru.”
Trazira iliathiri jinsi gani kazi ya kuhubiri? Badala ya kuzuia ukuzi, hatari na wasiwasi ziliwafanya watu wengi watambue uhitaji wao wa kiroho. Kwa miezi 15 tu, wahubiri wapya 500 walianza kushiriki katika kazi ya kuhubiri, nayo idadi ya wahubiri ikapita 1,500.
KOSOVO YAANGAZIWA
Baada ya trazira, ni kana kwamba bunduki zilitoweka, nayo makutaniko yakaendelea kukua. Hata hivyo, matatizo yalianza kuzuka katika nchi jirani ya Kosovo. Vita vilivyokuwa vikiendelea huko viliathiri Albania, kwa kuwa vikundi vya wakimbizi vilikuwa vikija. Wahubiri Waalbania hawakupoteza wakati. Walianza kuwapa wakimbizi hao ujumbe wenye tumaini na vitabu vyenye kufariji. Pia walitunza kikundi cha Mashahidi wa Yehova na watoto wao, watu wapatao 22.
Mwezi wa Agosti, vita vilipoisha, ndugu wa Kosovo wakarudi kwao. Hata hivyo hawakurudi peke yao. Waliandamana na ndugu Waalbania na Waitaliano, kutia ndani mapainia wa pekee, waliotaka kutoa msaada wa kiroho uliohitajiwa. Kufikia mwisho wa mwaka wa utumishi wa 1999, kulikuwa na wahubiri 1,805 Albania na 40 Kosovo.
UTHABITI ZAIDI WA KIROHO
“Ni vizuri kwamba tunatafsiri vitabu vingi,” Nasho Dori akasema kabla ya kufa, “lakini tunachohitaji sana ni Tafsiri ya Ulimwengu Mpya—Biblia nzuri inayoweza kutusaidia kujenga imani yetu!” Miaka mitatu tu baada ya Nasho kufa, mwaka wa 1999, Baraza Linaloongoza lilitoa kibali Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo itafsiriwe katika Kialbania.
Kwenye kusanyiko la 2000, wahudhuriaji Waalbania walipata zawadi ya pekee. Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ilitangazwa katika Kialbania! Kikundi cha watafsiri wenye bidii kilijikakamua kuukamilisha mradi huo katika muda unaopungua mwaka mmoja. Painia wa kawaida aliyekuwa mbunge Mkomunisti awali aliandika: “Ni jambo lenye kupendeza kama nini! Baada ya kuichunguza tafsiri hii, ndipo tu nimetambua jinsi Biblia hii inavyopendeza, lugha yake sanifu, ushairi, na masimulizi yenye kupendeza. Niliposoma jinsi Yesu alivyofanya miujiza na jinsi alivyokemewa na kudhihakiwa, hisia nyingi sana ziliibuka moyoni, hisia ambazo sijawahi kuwa nazo. Niliviona waziwazi akilini vikao vyote vyenye kuchochea hisia!”
Wakati huo kulikuwa na wahubiri 2,200 nchini Albania nayo familia ya Betheli ilikuwa na watu 40. Nyumba za kukaa zilikuwa zimekodishwa, hata hivyo, vyumba zaidi vilihitajika. Hivyo, Baraza Linaloongoza liliidhinisha uwanja wa ekari saba ununuliwe viungani vya mji wa Tiranë katika eneo la Mëzez. Ili kusimamia vizuri zaidi eneo kubwa zaidi la Albania na Kosovo, Halmashauri ya Nchi ikawa Halmashauri ya Tawi mwaka wa 2000.
Septemba 2003, ujenzi wa ofisi mpya ya tawi ulipoanza, Albania ilikuwa na wahubiri 3,122. Wakati huohuo, kazi kubwa ya kutafsiri Maandiko ya Kiebrania ilikuwa imefanywa. Kazi ya kuhubiri ilikuwa ikisonga mbele, nao wahubiri walikuwa wakifanya maendeleo kiroho. Wengi kati ya wale vijana 20 waliokuwa katika darasa la kwanza la Shule ya Mazoezi ya Kihuduma iliyofanywa Agosti 2004 walikuwa matineja walipokuwa wakiongoza mambo makutanikoni wakati wa trazira miaka michache iliyotangulia. Walifurahi sana kwamba sasa wamepata mazoezi zaidi ya kitheokrasi!
‘IBILISI ANA HASIRA’
Mnamo Februari 2005, gazeti moja lilichapishwa likiwa na kichwa, “Yehova Huwafundisha Watu Kujiua Wenyewe!” Ripoti za televisheni na magazeti zilieneza uvumi kwamba msichana mmoja aliyejiua ni Shahidi wa Yehova. Ukweli ni kwamba, msichana huyo hakuwahi kujifunza wala kuhudhuria mikutano. Hata hivyo, wapinzani walitumia tukio hilo kutushambulia kufa na kupona.
Walimu waliwadhihaki watoto wa Mashahidi. Akina ndugu walifutwa kazi. Watu wakaanza kudai tupigwe marufuku. Ijapokuwa akina ndugu walijaribu kujadiliana na vyombo vya habari, habari zilizidi kuwa mbaya.
Ni wazi kwamba watumishi wa Yehova walihitaji mwongozo na utegemezo ili kukabiliana na mashambulizi hayo mapya. Kwa hiyo, ofisi ya tawi ikapanga hotuba ya pekee itolewe. Hotuba hiyo ilikazia umuhimu wa kuendelea kuhubiri kweli ili kuzuia kuenea kwa uongo huo. Ndugu walitiwa moyo wazungumze na watu badala ya kujikunyata kwa woga. Wangeweza kuwasaidia watu wanyoofu waone kwamba idadi ya Mashahidi wa Yehova imeongezeka sana katika miaka ya karibuni, jambo ambalo halingewezekana ikiwa Mashahidi wanajiua wenyewe. Mashambulizi hayo hayakuwa mapya. Ndugu walikumbushwa ripoti za uwongo zilizoenezwa kuhusu Spriro Vruho miaka ya 1960, anayedaiwa kuwa alijiua mwenyewe. Ripoti hizi za karibuni zaidi hazikutimiza chochote ng’o!
Miezi michache baadaye, mwezi wa Agosti, David Splane wa Baraza Linaloongoza alijumuika na wajumbe wengine 4,675 kutoka Albania na Kosovo kwenye kusanyiko lao la wilaya. Wasikilizaji hawakuweza kuzuia shangwe yao Ndugu Splane alipotangaza kutolewa kwa Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika Kialbania!
“Haikosi ndiyo sababu Shetani anajaribu kutuzuia!” akasema ndugu mmoja wa zamani. “Ana hasira kwa sababu watu wa Yehova wana mengi mazuri.”
Licha ya ripoti mbaya kwenye vyombo vya habari, watumishi wa Mungu nchini Albania walizidi kuongezeka. Wengi kati ya waume wasioamini na watu wa ukoo walioona wazi kwamba habari hizo hazina msingi walianza kujifunza Biblia na kuwa wahubiri. Licha ya kwamba Shetani alikuwa ameanzisha mashambulizi ya kufa na kupona, mapenzi ya Yehova yaliendelea kutimizwa. Familia ya Betheli ilihamia ofisi ya tawi mpya, na darasa la pili la Shule ya Mazoezi ya Kihuduma likaanza.
KUWEKWA WAKFU KWA OFISI YA TAWI
Mnamo Juni 2006, Theodore Jaracz na Gerrit Lösch wa Baraza Linaloongoza, walikuwa miongoni mwa wajumbe 350 kutoka katika nchi 32 waliohudhuria programu ya kuweka wakfu ofisi mpya ya tawi. Mwingine aliyehudhuria programu hiyo ni Sotir Ceqi, aliyekuwa ameteswa kwa kupigwa kwa umeme katika miaka ya 1940. Sasa, akiwa na umri unaokaribia miaka 80, angali akitumikia kwa shangwe.
“Siku hii ni kama ndoto,” akasema Frosina Xheka, ambaye angali akitumikia kwa uaminifu licha ya magumu ya miaka mingi. Polikseni Komino, mjane wa Jani, alihudhuria, naye alisimulia kuhusu binti na wajukuu zake, ambao ni mapainia wa kawaida. Vasil Gjoka pia alikuwako, akitembea kana kwamba ana kibyongo kwa sababu ya kuteseka kwa miaka mingi. Machozi yalimlengalenga alipokumbuka safari ya kwenda kumtembelea Leonidha Pope na kubatizwa kisiri mwaka wa 1960.
Ofisi ya tawi ya awali huko Tiranë ilifanywa kuwa Majumba ya Ufalme matatu na makao ya wamishonari 14. Madarasa sita ya Shule ya Mazoezi ya Kihuduma yametokeza mapainia wa pekee waaminifu na wenye kujinyima ambao wamekuwa msaada mkubwa shambani. Mapainia zaidi ya 950 wa kawaida na wa pekee wanaonyesha roho hiyo pia ya kueneza injili.
SAFARI NI NDEFU
Ndugu na dada zetu nchini Albania wanathamini sana Biblia na vitabu ambavyo vimetafsiriwa katika lugha yao. Kazi ya Yehova katika eneo hili inazidi kusonga mbele. Mbali na ndugu wanaume wenye bidii na uwezo wanaozoezwa kubeba majukumu ya kitheokrasi, “wanawake wanaotangaza habari njema ni jeshi kubwa.”—Zab. 68:11.
Mashahidi wa Yehova nchini Albania ni ushahidi tosha wa maneno haya yaliyoongozwa kwa roho: “Silaha yoyote itakayofanywa juu yako haitafanikiwa, na ulimi wowote utakaoinuka juu yako katika hukumu wewe utauhukumu. Hilo ndilo fungu la urithi la watumishi wa Yehova.” (Isa. 54:17) Kwa sababu ya nguvu na fadhili zisizostahiliwa za Yehova, walisonga mbele licha ya kuwa chini ya serikali ya kidikteta, minyanyaso, upweke, habari za uwongo kwenye vyombo vya habari, na matatizo ya kibinafsi.
Watu wa Yehova nchini Albania wanatazamia wakati ujao wakiwa na hakika kwamba Mungu atawaonyesha upendo mshikamanifu na kuwabariki. Yajapokuwa magumu, wanashangilia tumaini lililowekwa mbele yao na pia pendeleo la kuufanya moyo wa Baba yao wa mbinguni ushangilie. (Met. 27:11; Ebr. 12:1, 2) Jambo moja ambalo limejitokeza wazi katika historia ya kitheokrasi ya Albania ni hili: Yehova hasahau kamwe jinsi watumishi wake, vijana kwa wazee, wanavyojidhabihu iwe ni kwa njia kubwa au ndogo.—Ebr. 6:10; 13:16.
[Blabu katika ukurasa wa 130]
Mwanzoni kichwa cha kitabu hicho kilitafsiriwa The Guitar of God (Gita ya Mungu)
[Picha katika ukurasa wa 140]
“Kama ungekuwa Mkristo, ungepigana sawa tu na makasisi!”
[Blabu katika ukurasa wa 189]
“Tumeishiwa fomu za kujaza ripoti za utumishi wa shambani”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 132]
Maelezo Mafupi Kuhusu Albania
Nchi
Albania iko sehemu ya kusini mashariki ya bara Ulaya, kaskazini mwa Ugiriki na mashariki mwa Italia. Ina ukubwa wa kilomita mraba 28,750, nayo pwani yake yenye urefu wa kilomita 362 huanzia Bahari ya Adriatiki hadi Bahari ya Ionia. Fuo zenye mchanga mweupe na maji ya samawati pamoja na milima mirefu ni baadhi ya maumbile ya Albania, kuanzia Vlorë hadi Sarandë. Sehemu ya kaskazini na ya ndani zaidi ya nchi ina milima-milima, nao upande wa kusini-magharibi wa nchi una udongo wenye rutuba unaotumiwa kwa ajili ya kilimo.
Watu
Inakadiriwa kwamba kuna watu wapatao 3,600,000 nchini humo, wengi wao wakiwa Waalbania wenyeji, na asilimia ndogo ya Waroma, Wagiriki, na Waserbia.
Hali ya hewa
Sehemu tambarare za pwani upande wa kusini, joto huwa la wastani wa nyuzi 26 sentigredi. Hata hivyo, majira ya baridi kwenye milima ya Dibër iliyo kaskazini, kunakuwa na baridi kali kufikia nyuzi 25 sentigredi chini ya kiwango cha kuganda.
Chakula
Pai inayoitwa byrek, yenye gamba la chembechembe za vitobosha hutayarishwa kwa mchicha, jibini, nyanya, vitunguu na mboga nyinginezo au nyama. Chakula kinachoitwa tava e kosit, kinachotengenezwa kwa nyama ya kuku au kondoo iliyookwa katika rojo la mtindi na kiungo kinachoitwa dill. Waalbania wanapenda kutumia kijiko, kwa kuwa chakula chao huwa na supu na mchuzi. Mara nyingi, kwenye pindi za pekee, wakati ambao kondoo huliwa, mgeni mheshimiwa huandaliwa kichwa cha kondoo. Vitinda-mlo vinatia ndani vitobosha (kama kilicho kwenye picha upande wa kulia) na kadaif, vitumbua vyenye shira au asali na karanga. Chakula cha msingi ni mkate. Ukitaka kumwambia mtu umekula, unamwambia “Hëngra bukë,” yaani “nimekula mkate.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 134]
Makusanyiko ya Awali
Mbali na Mikutano ya Watu Wote ya Kialbania siku ya Jumapili, Waalbania huko New England, Marekani, kwa kawaida walishirikiana na makutaniko ya Kiingereza au Kigiriki. Miaka ya 1920 na 1930, Waalbania walifurahi kuhudhuria makusanyiko ya Kigiriki. Hata hivyo, walifurahi kuwa na beji za lugha yao wenyewe, zinazosema: “Kusanyiko la Siku Tatu la Wanafunzi wa Biblia Waalbania.”
[Picha]
Beji (kulia) iliyovaliwa na ndugu wa Albania (chini) kusanyikoni huko Boston mwishoni mwa miaka ya 1920
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 151, 152]
“Yehova Hakutuacha Kamwe!”
FROSINA XHEKA
ALIZALIWA 1926
ALIBATIZWA 1946
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alijifunza kweli alipokuwa kijana. Ijapokuwa wazazi wake walimpinga, na wenye mamlaka wakamtenga na wengine, sikuzote alihisi akiwa karibu na Yehova na tengenezo lake. Alikufa akiwa mwaminifu mwaka wa 2007.
◼ FROSINA alijifunza kweli kutoka kwa ndugu zake katika miaka ya 1940. Wazazi wake ambao hawakuwa Mashahidi walimfukuza nyumbani kwa sababu alikataa kuolewa na mwanamume waliyemchagulia. Familia ya ndugu mmoja, Gole Flloko, ilimchukua na kukaa naye kama binti yao.
“Pindi moja nilikamatwa kwa sababu ya kukataa kupiga kura,” asema Frosina. “Nilikuwa peke yangu katika chumba. Ghafula nikazingirwa na maofisa 30 hivi. Mmoja wao akasema kwa sauti kubwa, ‘Unajua tunaweza kukufanya nini?’ Nilihisi kwamba Yehova yu nami na kusema, ‘Hamwezi kufanya lolote ambalo Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova hatawaruhusu mfanye!’ Walidhani nina wazimu, wakaniambia, ‘Ondoka!’ Waona, sikukosea. Yehova alikuwa nami!”
Mwaka wa 1957, Frosina aliolewa na Luçi Xheka, na hatimaye wakawa na watoto watatu. Mapema miaka ya 1960, Luçi aliwekwa kuwa mshiriki wa Halmashauri ya Nchi, iliyokuwa imeundwa ili kusimamia kazi nchini Albania. Muda si muda akahukumiwa kifungo cha miaka mitano huko Gramsh, mbali na Frosina na watoto wake. Akiwa huko, Luçi aliendelea kuhubiri na kuzungumza kuhusu tengenezo la Yehova. Watu wa Gramsh wanamkumbuka hadi leo hii.
Luçi alipokuwa kifungoni, Chama cha Kikomunisti kiliweka jina la Frosina katika orodha ya washukiwa, na kwa sababu hiyo asingeweza kununua chakula. Frosina anasema: “Haikudhuru. Ndugu wachache waliokuwapo walinigawia chakula chao! Tulisonga mbele kwa kuwa Yehova hakutuacha kamwe!”
Luçi alipokufa, ikawa vigumu kukutana na akina ndugu. Hata hivyo, Frosina aliendelea kuhubiri. Anakumbuka: “John Marks alitutembelea miaka ya 1960. Hatimaye nilipokutana na mke wake, Helen, mwaka wa 1986, ni kana kwamba tulikuwa tumejuana kwa muda mrefu. Luçi nami tulikuwa tukiwatumia akina Marks ujumbe kisiri, nao wakawa wakiwatumia ndugu huko Brooklyn.”
Marufuku ilipoondolewa mwaka wa 1992, Frosina alikuwa mmoja wa Mashahidi tisa waliobatizwa ambao walikuwa wamebaki Albania. Alikuwa wa kawaida katika mikutano naye alikuwa shambani siku aliyokufa mwaka wa 2007. Muda mfupi kabla hajafa, Frosina alisema: “Nampenda Yehova kwa moyo wangu wote! Sijawahi kamwe kufikiria kuridhiana imani yangu. Nilijua kwamba nina familia kubwa ulimwenguni pote, lakini sasa siamini ninapoona jinsi familia yetu ya kitheokrasi ilivyo kubwa hapa Albania. Yehova amekuwa nasi sikuzote, nasi tungali katika mikono yake yenye upendo!”
[Picha]
Frosina Xheka mwaka wa 2007
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 159, 160]
Tangu Siku za Uhaba Hadi Siku za Wingi
VASIL GJOKA
ALIZALIWA 1930
ALIBATIZWA 1960
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alichukua msimamo thabiti katika kweli chini ya serikali ya kidikteta. Leo, ni mzee wa kutaniko mjini Tiranë.
◼ NAKUMBUKA nikiona gazeti la Mnara wa Mlinzi la Kigiriki nyumbani kwetu huko Barmash miaka ya 1930. Baba yangu aliyaelekezea kidole na kusema, “Watu hawa wana ukweli!” Sikujua alichomaanisha hadi miaka mingi baadaye. Nilipenda kuisoma Biblia, ijapokuwa ilikuwa hatari kuwa nayo. Katika mazishi ya mkwe wangu, nilikutana na ndugu kutoka Tiranë. Nilimwuliza kuhusu ishara ya “siku za mwisho” inayotajwa katika Mathayo sura ya 24. Alinifafanulia, na tangu hapo nikaanza kumwambia kila mtu niliyeweza, mambo niliyokuwa nikijifunza.
Mwaka wa 1959, nilihudhuria mkutano pamoja na akina ndugu uliofanyiwa nyumbani kwa Leonidha Pope. Nilikuwa nimesoma kitabu cha Ufunuo nami nikauliza mnyama mwitu na Babiloni Mkubwa wanaozungumziwa humo ni nani. Akina ndugu waliponifafanulia, nikajua kwamba huu ni ukweli! Nikabatizwa mwaka mmoja baadaye.
Nilikuwa na bidii katika kazi ya kuhubiri, na kwa sababu hiyo, nikafutwa kazi. Basi nikachukua mkokoteni na kuanza kubebea watu mizigo mjini Tiranë. Ijapokuwa nilikuwa nikionana na akina ndugu mara chache sana nami sikuwa na vitabu, niliendelea kuhubiri.
Mapema miaka ya 1960, kabla ya Leonidha Pope kufungwa, alipata vitabu kadhaa vya Kigiriki vilivyokuwa vimeingizwa kisiri nchini Albania. Alivitafsiri kwa sauti, huku nikiandika katika daftari mambo aliyokuwa akisema. Kisha, akaniagiza nifanyize nakala na kuwatumia akina ndugu waliokuwa Berat, Fier, na Vlorë.
Kumekuwa na mabadiliko makubwa katika miaka ya 1990! Nafurahi kuona wingi wa vitabu ambavyo Yehova ametupa. Tangu 1992 hadi leo, tumewagawia watu magazeti milioni 17 ya Kialbania! Vitabu vipya vinatafsiriwa katika Kialbania, nasi tuna Biblia nzima ya Tafsiri ya Ulimwengu Mpya katika lugha yetu! Ninapokumbuka wakati ambapo hatukuwa na vitabu, ninatokwa na machozi ya furaha. Kuwa na vitu vichache kwa muda mrefu kumetusaidia kuthamini chochote kile!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 163, 164]
Nilipata Kazi Bora Nyumbani
ARDIAN TUTRA
ALIZALIWA 1969
ALIBATIZWA 1992
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alijifunza kweli nchini Italia na baadaye akarudi Albania. Ni mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Albania.
◼ NILIKUWA na umri wa miaka 21 mwaka wa 1991 nilipoondoka Albania pamoja na maelfu ya wakimbizi wengine. Tuliteka nyara meli iliyokuwa ikienda Italia. Albania ilikuwa nchi maskini sana, nami nilifurahi kwamba nimeponyoka. Nilidhani kwamba ndoto yangu ilikuwa imetimia.
Baada ya siku mbili huko Brindisi, Italia, nilitoroka kambi ya wakimbizi nikaenda kutafuta kazi. Mwanamume fulani alinipa kijikaratasi kidogo kilichotolewa fotokopi chenye ujumbe wa Biblia katika Kialbania kisha akanialika kwa mkutano jioni hiyohiyo. Nikawaza moyoni: ‘Mbona nisiende? Huenda nikapata kazi!’
Sikutazamia kamwe kukaribishwa kwa shauku kadiri hiyo. Baada ya mkutano katika Jumba la Ufalme, kila mtu alinisalimu kwa shauku. Familia moja ikanialika kwa mlo. Hizo zilikuwa fadhili na heshima zilizoje kwangu mimi Mwalbania asiyefaa kitu tena mkimbizi haramu!
Katika mkutano uliofuata Vito Mastrorosa aliniambia kwamba ikiwa ningependa anaweza kujifunza nami Biblia. Nilikubali na mara moja nikatambua kwamba nimepata kweli. Agosti 1992, nikabatizwa nchini Italia.
Mwishowe nikapata vibali vyote vinavyohitajika vya kukaa nchini. Nilipata kazi nzuri nami nilikuwa nikiwatumia pesa watu wa familia yangu waliokuwa Albania. Hata hivyo, nilianza kuwaza: ‘Sasa, kwa kuwa Mashahidi wana uhuru nchini Albania, lazima kuna uhitaji mkubwa. Nirudi nikatumikie huko? Watu wa familia yangu wataonaje? Wanahitaji sana pesa ninazowatumia. Watu wengine watasemaje?’
Kisha nikapigiwa simu kutoka ofisi ya Tiranë, na kuombwa kwenda kufundisha Kialbania kikundi cha mapainia wa pekee kutoka Italia, ambacho kingehamia Albania mwezi wa Novemba mwaka huohuo. Uamuzi wao ulinifanya nifikirie kwa uzito. Walikuwa wakielekea eneo nililotoka. Ijapokuwa hawakujua lugha inayozungumzwa huko, walikuwa na hamu kubwa ya kwenda huko. Mimi ni mwenyeji wa Albania. Ninafanya nini Italia?
Niliamua kupanda meli na kuandamana na mapainia hao. Mara tu nilipofika, nikaanza kutumikia katika Betheli hiyo ndogo. Asubuhi nilikuwa nikifundisha Kialbania na alasiri nilikuwa nikitafsiri. Mwanzoni, watu wa familia yangu hawakufurahi. Lakini walipoelewa ni kwa nini nilirudi Albania, wakaanza kusikiliza habari njema. Punde si punde, wazazi wangu, dada zangu wawili, na ndugu yangu mmoja wakabatizwa.
Je, ninajuta kuacha kazi na pesa nchini Italia? Sijuti kamwe! Nilipata kazi bora Albania. Kwangu mimi, kazi bora na inayoleta shangwe ya kudumu ni kazi ya kumtumikia Yehova kwa vyote ulivyo navyo!
[Picha]
Ardian na mke wake, Noadia
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 173, 174]
Mwisho wa Kufanya Mikutano Kisiri
ADRIANA MAHMUTAJ
ALIZALIWA 1971
ALIBATIZWA 1993
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alialikwa kuhudhuria mkutano uliofanywa kisiri, halafu mambo yakabadilika ghafula. Sasa anatumikia akiwa painia wa pekee.
◼ BINAMU yangu alipokufa mwaka wa 1991, nilimsikia mwanamke aitwaye Barie, akitumia Biblia kumtia moyo shangazi yangu. Mara moja nikaanza kuuliza maswali, kisha nikaombwa nikutane na rafiki yake, Rajmonda kazini kwao. Familia ya kina Rajmonda ilikuwa ikifanya mikutano katika “darasa.” Rajmonda alinieleza kwamba sina budi kujifunza Biblia kwa muda, kwa sababu wapya hawaruhusiwi kuingia katika darasa hilo mara moja. Nilipendezwa sana na mambo niliyokuwa nikijifunza, na muda si muda, nikaruhusiwa kuhudhuria.
Darasa hilo lilikuwa na watu ambao hawakuwa wamebatizwa, waliokuwa wakikutanika pamoja na Sotir Papa na Sulo Hasani hapo awali. Miaka kadhaa mapema, maofisa wa Sigurimi walikuwa wamepenya kisiri na kuwasaliti akina ndugu kwa polisi. Kwa hiyo, wote walijiendesha kwa tahadhari nao walikuwa waangalifu sana kabla ya kumwalika mtu yeyote ahudhurie mikutano!
Katika mkutano wa kwanza niliohudhuria, nilipata kujua kwamba tunapaswa kuwa na orodha ya rafiki zetu na kuwaambia mambo tunayojifunza. Nilizungumza na Ilma Tani. Muda mfupi baadaye, aliruhusiwa kuja darasani. Kikundi chetu kidogo cha watu 15 kikaongezeka upesi.
Mnamo Aprili 1992, Michael na Linda DiGregorio walizuru Berat. Ilipendekezwa tualike watu wote waje kusikiliza hotuba ya Ndugu DiGregorio. Watu 54 wakahudhuria. Hakuna hata mmoja kati yetu aliyekuwa amebatizwa. Baada ya hotuba hiyo, tulikuwa na maswali mengi ya kuwauliza Ndugu na Dada DiGregorio. Hatimaye tukajua jinsi tunavyopaswa kutimiza huduma yetu.
Muda mfupi baadaye, Mashahidi wa Yehova wakatambuliwa rasmi kisheria. Ilma nami pamoja na ndugu wawili tukaenda Tiranë kujifunza jinsi ya kuhubiri nyumba kwa nyumba. Tuliombwa tutakaporudi Berat tuwafundishe wengine. Tulijitahidi sana. Mapainia wa pekee wanne kutoka Italia walipopewa mgawo wa kwenda Berat, mnamo Machi 1993, kutaniko lilipiga hatua, na kuanza kufanya mikutano miwili kila juma.
Mwezi huo wa Machi, Ilma pamoja nami tulibatizwa katika kusanyiko la pekee lililofanywa Tiranë. Watu 585 walihudhuria. Tukaanza upainia wa kawaida na baada ya muda tukawekwa kuwa mapainia wa pekee wa kwanza wenyeji. Sasa tulikuwa na uhuru wa kufanya mambo. Tukapewa mgawo wa kwenda Korçë.
Baadaye, Ilma akaolewa na Arben Lubonja, aliyekuwa akihubiri Korçë akiwa peke yake. Mwishowe, wakaanza kufanya kazi ya mzunguko, na sasa wanatumikia Betheli. Nafurahi kwamba nilimwalika Ilma!
Hivi majuzi, nilipokuwa nimeketi katika kusanyiko la wilaya lililohudhuriwa na watu zaidi ya 5,500, nilikumbuka jinsi tulivyokuwa tukifanya mikutano yetu kisiri. Yehova amefanya mabadiliko makubwa kama nini! Sasa mikutano na makusanyiko yanafanywa hadharani. Ingawa mamia ya kina ndugu wamehama kutoka Berat kwa sababu za kiuchumi, kikundi kidogo kilichokuwapo sasa kimepanuka na kuwa makutaniko matano makubwa!
[Picha]
Ilma (Tani) na Arben Lubonja
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 183]
“Sawa, Twende!”
ALTIN HOXHA NA ADRIAN SHKËMBI
WALIZALIWA 1973
WALIBATIZWA 1993
MAELEZO MAFUPI KUWAHUSU Waliacha chuo kikuu ili kuwa mapainia, nao sasa ni wazee wa kutaniko.
◼ MAPEMA mwaka wa 1993, walikuwa wanafunzi wa chuo kikuu huko Tiranë. Rafiki yao aliwasimulia kwa saa kadhaa kuhusu mambo aliyokuwa akijifunza kutoka kwa Mashahidi wa Yehova. Kila kitu kiliungwa mkono na Biblia. Baadaye walijifunza mengi zaidi, wakatumia mambo waliyokuwa wamejifunza, na kubatizwa mwaka huohuo. Kisha, wakaenda kuhubiri Kuçovë, ambako hakukuwa na wahubiri wowote.
Waliporudi Tiranë, Adrian akamwambia Altin: “Tunafanya nini shuleni? Twende Kuçovë tukahubiri!”
Altin akamjibu, “Sawa, twende!” Miezi saba baada ya kubatizwa, wakarudi Kuçovë.
Yehova alibariki sana jitihada zao. Leo, Kuçovë kuna wahubiri watendaji zaidi ya 90. Mashahidi wapatao 25 wamehama ili kwenda kutumikia wakiwa mapainia au Wanabetheli. Adrian na Altin walijifunza Biblia na wengi wao.
Akifikiria kuhusu chuo kikuu, Altin anatabasamu na kusema: “Mtume Paulo aliamua kutofuatia kazi ya kimwili, nami katika mwaka wa 1993, nilifanya uamuzi kama huo. Sijuti kamwe kusema, ‘Sawa, twende!’”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 191, 192]
Mkana-Mungu Afundisha Kuhusu Mungu
ANASTAS RUVINA
ALIZALIWA 1942
ALIBATIZWA 1997
MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Kabla ya kujifunza kweli kutoka kwa watoto wake, alikuwa akiwafundisha wanajeshi waliokuwa chini ya usimamizi wake kwamba hakuna Mungu. Leo, ni mzee wa kutaniko na painia wa pekee.
◼ MWAKA wa 1971, baada ya kufuzu mafunzo ya kijeshi, nikawa kamishna wa kisiasa wa brigedi. Niliitwa hivyo kwa kuwa serikali ilikuwa imepiga marufuku vyeo rasmi vya kijeshi mwaka wa 1966. Baadhi ya majukumu yangu yalitia ndani kuwatia wale waliokuwa chini ya usimamizi wangu kasumba ya kwamba hakuna Mungu. Niliwafundisha ile falsafa ya kwamba dini ni kasumba ya watu.
Nilikuwa na mke na watoto watatu. Mwaka wa 1992, mwana wangu Artan, alianza kuhudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova huko Tiranë. Kisha akawa akienda na dada yake, Anila. Kwangu mimi, walikuwa wakipoteza wakati na mambo ya upuuzi. Kwa hiyo, tulibishana sana nyumbani.
Siku moja, nilichukua gazeti la Mnara wa Mlinzi na kuanza kulisoma. Kwa kushangaza, ujumbe wake ulikuwa wenye kusadikisha. Hata hivyo, ijapokuwa Artan na Anila walikuwa wakinitia moyo nijifunze Biblia, sikukubali. Niliamini kwamba hakuna haja ya kujifunza Biblia ikiwa humwamini Mungu. Katika mwaka wa 1995, kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? kilitangazwa katika Kialbania. Artan na Anila wakanipa kimoja. Hicho ndicho kilichonisadikisha. Kwa kweli, kuna Mungu! Sikuwa tena na udhuru; sikuwa na budi kujifunza. Muda si muda, mke wangu Lirie, akajiunga nami, nasi hatukuwa na shaka kamwe kwamba tumeipata kweli.
Kusema kweli, nilichukua muda kufanya maendeleo. Nilikuwa na umri wa miaka 53. Haikuwa rahisi kubadili maoni yangu wa kisiasa na kijeshi. Lazima nikiri kwamba Muumba, Yehova, ndiye aliyenisaidia kusonga mbele.
Sikutaka kuwa mhubiri kwa sababu ningelazimika kuwahubiria watu walewale niliokuwa nimewafundisha kwamba hakuna Mungu. Wangenionaje? Siku moja tulipokuwa tukijifunza, Vito Mastrorosa alinisomea masimulizi ya Sauli wa Tarso. Hiyo ndiyo dawa niliyohitaji! Sauli aliwatesa Wakristo, akajifunza kweli, kisha akahubiri. Nilijua kwamba Yehova atanisaidia kufanya vivyo hivyo.
Nyakati nyingine mimi hucheka ninapotafakari jinsi Yehova anavyoendelea kunisaidia kuwa mpole zaidi, na mwenye kukubali sababu, na kuondolea mbali ukali wa kijeshi. Pole kwa pole ninabadilika.
Sibishani na watoto wangu tena kuhusu kweli. Badala yake, ninawaonea fahari. Artan ni painia wa pekee na mzee wa kutaniko. Binti zangu Anila na Eliona, wanatumikia Betheli, mjini Tiranë.
Mimi na Lirie ni mapainia wa pekee. Tunaliona kuwa pendeleo kuwafundisha watu kweli kumhusu Muumba wetu Mkuu na kuwaona wakifanya mabadiliko maishani. Ni furaha kama nini kuwapa watu tumaini hakika linalotegemea ahadi za Mungu wa kweli na aliye hai, Yehova!
[Picha]
Kuanzia kushoto kuelekea kulia: Artan, Anila, Lirie, Anastas, Eliona, na mume wake, Rinaldo Galli
[Ramani/Grafu katika ukurasa wa 176, 177]
MFUATANO WA MATUKIO—Albania
1920-1922 Waalbania wajifunza kweli Marekani.
1922 Thanas Idrizi arudi Gjirokastër baada ya kujifunza kweli.
1925 Madarasa matatu madogo ya funzo la Biblia nchini Albania.
1928 “Photo-Drama of Creation” yaonyeshwa katika miji mingi.
1930
1935-1936 Kampeni kubwa ya kuhubiri yafanywa.
1939 Mashahidi wa Yehova wapigwa marufuku.
1940
1940 Ndugu tisa wafungwa kwa sababu ya kutokuwamo.
1946 Serikali ya Kikomunisti yaanza kutawala.
1950
1960
1960 Halmashauri ya Nchi yaanza kusimamia kazi nchini Albania.
1962 Washiriki wa halmashauri hiyo wapelekwa katika kambi ya kazi ngumu.
1967 Albania yajitangaza rasmi kuwa nchi isiyoamini Mungu.
1980
1990
1992 Mashahidi wa Yehova watambuliwa kisheria.
1996 Milton Henschel ahudhuria kuwekwa wakfu kwa Betheli ya kwanza.
1997 Trazira yaanza.
2000
2005 Biblia nzima ya Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Kialbania yatangazwa.
2006 Ofisi ya tawi yawekwa wakfu huko Mëzez, Tiranë.
2010
[Grafu]
(See publication)
Jumla ya Wahubiri
Jumla ya Mapainia
4,000
3,000
2,000
1,000
1930 1940 1950 1960 1980 1990 2000 2010
[Ramani katika ukurasa wa 133]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MONTENEGRO
KOSOVO
MAKEDONIA
UGIRIKI
Ioannina
Ziwa Scutari
Ziwa Ohrid
Ziwa Prespa
BAHARI YA ADRIATIKI
ALBANIA
TIRANË
Shkodër
Kukës
Burrel
Mëzez
Durrës
Kavajë
Gramsh
Kuçovë
Fier
Berat
Korçë
Vlorë
Tepelenë
Këlcyrë
Barmash
Përmet
Gjirokastër
Sarandë
[Picha katika ukurasa wa 126]
[Picha katika ukurasa wa 128]
Baada ya kujifunza kweli huko New England, Marekani, Thanas Idrizi alipeleka habari njema Gjirokastër, Albania
[Picha katika ukurasa wa 129]
Sokrat Duli alimfunza ndugu yake kweli
[Picha katika ukurasa wa 137]
Nicholas Christo aliwahubiria habari njema watu wenye vyeo vya juu nchini Albania
[Picha katika ukurasa wa 142]
Barua ya kurasa mbili ambayo ndugu Waalbania walioishi Boston walimtumia Enver Hoxha
[Picha katika ukurasa wa 145]
Leonidha Pope
[Picha katika ukurasa wa 147]
“Yehova alinifundisha kutotia sahihi mambo ambayo sikusema.”—Sotir Ceqi
[Picha katika ukurasa wa 149]
Helen na John Marks kabla ya John kurudi Albania
[Picha katika ukurasa wa 154]
Spiro Vruho alitumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko
[Picha katika ukurasa wa 157]
Llopi Bllani
[Picha katika ukurasa wa 158]
Licha ya kuwa peke yake, Kulla Gjidhari aliadhimisha Ukumbusho
[Picha katika ukurasa wa 167]
Michael na Linda DiGregorio
[Picha katika ukurasa wa 172]
Oda Na. 100 iliyowatambua kisheria Mashahidi wa Yehova
[Picha katika ukurasa wa 175]
Mkutano wa kutaniko katika Jumba la Ufalme la kwanza, 1992, Tiranë
[Picha katika ukurasa wa 178]
Areti Pina alihubiri kwa uaminifu akiwa peke yake
[Picha katika ukurasa wa 184]
Jumba la zamani lililofanywa kuwa ofisi za kisasa
[Picha katika ukurasa wa 186]
“Mkitupwa gerezani, msiwe na wasiwasi.”—Nasho Dori
[Picha katika ukurasa wa 194]
David Splane akitangaza kutolewa kwa Biblia nzima ya “Tafsiri ya Ulimwengu Mpya” katika Kialbania
[Picha katika ukurasa wa 197]
Wamishonari wanaotumikia Albania sasa
[Picha katika ukurasa wa 199]
Ofisi ya Tawi ya Albania
Halmashauri ya Tawi: Artan Duka, Ardian Tutra, Michael DiGregorio, Davide Appignanesi, Stefano Anatrelli