Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb10 kur. 200-255
  • Belize

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Belize
  • 2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • HISTORIA YA MAPEMA
  • MBEGU ZA KWELI ZATIA MIZIZI
  • WATU WENGI WASAIDIWA KUPATA KWELI
  • BIDII YALETA MATOKEO MAZURI
  • ROHO YA YEHOVA ILIWAVUTA
  • WAMISHONARI WA KWANZA WAFIKA
  • KAZI YAENDELEA KUJAPOKUWA VIZUIZI
  • KAZI NYINGI SANA
  • WAMISHONARI WENGINE HAWARUHUSIWI KUINGIA NCHINI
  • KAZI YA KUHUBIRI YASONGA MBELE
  • JUMBA JIPYA LA UFALME LAHITAJIKA
  • WATU WANAOONGEA KIHISPANIA WAKUBALI KWELI
  • “WAKRISTO WA KWELI HUHUBIRI NYUMBA KWA NYUMBA”
  • MATOKEO MAZURI YA SAFARI ZA MASHAMBANI
  • WAKEKCHI WAKUBALI KWELI
  • MATOKEO MAZURI YA SAFARI ZA BAHARINI
  • MATOKEO MAZURI KATIKA MAENEO AMBAYO HAYAJAGAWIWA YEYOTE
  • “VITISHO VYAKE HAVINGEWEZA KUNIZUIA”
  • MPINZANI AKUBALI KWELI
  • BELIZE YAKUMBWA NA KIMBUNGA
  • “BI. PRATT, TAFADHALI TUOMBEE”
  • KUKUSANYIKA ILI KUFUNZWA NA YEHOVA
  • WATU WANAOONGEA KICHINA WAKUBALI KWELI
  • OFISI YA TAWI YA MEXICO YASIMAMIA KAZI NCHINI BELIZE
  • WATU WA MATAIFA YOTE WAUNGANA
2010 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb10 kur. 200-255

Belize

NCHI maridadi na yenye joto ya Belize iko kwenye Rasi ya Yucatán, na inapakana na Mexico, Guatemala, na Bahari ya Karibea. Nchi hii ndogo ambayo hapo awali iliitwa Honduras ya Uingereza, ina tamaduni, lugha, desturi, vyakula, na dini nyingi mbalimbali.

Belize ina wakaaji 300,000 hivi, kwa hiyo, hakuna msongamano wa watu nchini humo, kama ilivyo katika nchi nyingine za Amerika ya Kati. Katika misitu minene ya mvua kuna ndege na wanyama maridadi, kama vile chui wa Amerika, ambaye si rahisi kumwona. Nchini humo pia kuna mabomoko mengi ya kale ya Wamaya na milima mikubwa ambayo imepambwa kwa miti mirefu na maporomoko maridadi ya maji. Pia, kuna mapango mengi yenye kuvutia ambayo baadhi yake yameunganishwa kwa mito inayojipinda-pinda yenye maji safi sana. Matumbawe makubwa ya Belize yanayoanzia upande wa kusini wa pwani hadi upande wa kaskazini, yana marijani nyingi za aina mbalimbali. Visiwa vidogo vyenye minazi na mchanga mweupe vinatapakaa kotekote kwenye matumbawe hayo.

HISTORIA YA MAPEMA

Waarawaki na Wakaribu, waliohamia Belize kutoka Amerika Kusini, walikuwa kati ya wakaaji wa kwanza wa nchi hii. Yaelekea utamaduni wa Wamaya ulisitawi nchini Belize mamia ya miaka kabla ya Wazungu kufika kwenye mabara ya Amerika, ambayo waliyaita Ulimwengu Mpya. Kulikuwa na vituo vya sherehe na mahekalu ya fahari ya Wamaya nchini humo.

Hakuna habari nyingi kuhusu jitihada za mapema za Wazungu za kuitawala Belize. Kinachojulikana ni kwamba Wahispania walijaribu kuwatawala Wamaya, lakini wakashindwa. Maharamia kutoka Uingereza walikuja kuishi kwenye eneo la pwani mwaka wa 1638. Katikati ya miaka ya 1600, watu waliofanya biashara ya miti ya logwood (iliyotumiwa kutengeneza rangi ya bei ghali), walikuwa wamehamia Belize.

Waingereza waliwaleta watumwa nchini humo kufanya kazi ya kukata miti ya logwood na mikangazi. Watumwa hao walinunuliwa masokoni huko Jamaika na Marekani, au waliletwa moja kwa moja kutoka Afrika. Ijapokuwa wasimamizi wa watumwa wa biashara ya mbao hawakuwa wakatili kama wasimamizi wa watumwa katika sehemu nyingine za Amerika, bado hali ya maisha ya watumwa hao ilikuwa mbaya na mara nyingi walitendwa kikatili. Watumwa wengi waliasi, wakajiua, au wakatoroka na kuanzisha jamii zilizojitegemea nchini humo. Belize ilitangazwa kuwa koloni ya Uingereza mwaka wa 1862 na ikapata uhuru mwaka wa 1981.a

MBEGU ZA KWELI ZATIA MIZIZI

James Gordon alikuwa kati ya Mashahidi wa kwanza kufika Belize. Siku hizo Mashahidi wa Yehova waliitwa Wanafunzi wa Biblia wa Kimataifa. James alibatizwa nchini Jamaika mwaka wa 1918. Mtu huyo mwembamba mwenye sauti nyororo alihamia Belize kutoka Jamaika mwaka wa 1923. Alihamia kijiji cha mbali cha Wamaya kinachoitwa Bomba, alikooa na kupata watoto. Ijapokuwa alikuwa mbali sana na ndugu zake Wakristo, aliwahubiria marafiki na majirani habari njema.

Habari njema ya Ufalme ilifikia sehemu nyingine za koloni hii ya Uingereza jinsi gani? Mwaka wa 1931, Freida Johnson, mwanamke mdogo Mmarekani aliyekaribia umri wa miaka 60, alianza kuhubiri katika maeneo mbalimbali ya Amerika ya Kati. Alisafiri peke yake, nyakati nyingine kwa farasi, naye alihubiri katika miji, vijiji, na mashamba ya migomba yaliyotapakaa kwenye pwani ya Bahari ya Karibea.

Freida alifika kwenye jiji linaloitwa Belize City mwaka wa 1933, na akakodi chumba kidogo kwa Bi. Beeks. Kila asubuhi Bi. Beeks alimsikia Freida akisoma Biblia na kuimba wimbo kabla ya kuondoka. Freida alijulikana kwa kuhubiri kwa bidii bila kuchoka. Kwa mfano, hakupumzika saa za adhuhuri kama watu wengi wanavyofanya katika maeneo yenye joto. Alikaa nchini Belize kwa miezi sita, na alimhubiria mwokaji Thaddius Hodgeson aliyeanza kupendezwa. Ijapokuwa alihubiri hasa huko Belize City, Freida alitembelea pia sehemu fulani za mashambani. Kijijini Bomba alikutana na James Gordon. Utumishi wa Freida uliwawezesha watu waliokuwa na imani moja kufahamiana na kuanza kukutanika pamoja.

WATU WENGI WASAIDIWA KUPATA KWELI

Ijapokuwa ilikuwa vigumu kuwasiliana siku hizo, James na Thaddius waliendelea kuwasiliana huku kila mmoja akiendelea kuhubiri katika eneo lake. Mwaka wa 1934, Thaddius aliandikia makao makuu huko Brooklyn na kuomba santuri na sahani zenye hotuba za Biblia zilizorekodiwa.

Kila Jumamosi jioni, Thaddius alicheza sahani zenye hotuba hizo mbele ya jengo la Mahakama Kuu, katika bustani ndogo ambamo kikosi cha jeshi kilikuwa kikifanya mazoezi hapo awali. Bustani hiyo iliitwa “Uwanja wa Vita.” Jina hilo lilifaa sana, hasa wakati ndugu Thaddius alipocheza sahani zenye hotuba za Ndugu Rutherford kwenye upande mmoja wa bustani hiyo, huku Jeshi la Wokovu likipiga ala za muziki kufuatana na kishindo cha ngoma kubwa ya Beaumont Boman, kwenye upande mwingine. Hata hivyo, muda si mrefu, Beaumont alikubali ujumbe wa Ufalme, na akajiunga na Thaddius kwenye upande wake wa uwanja huo. Beaumont alisema, “Namshukuru Mungu wangu Yehova kwa kufanya niache kupiga ile ngoma!”

Ndugu walipenda pia kuhubiri karibu na soko kwenye kituo cha magari yanayokokotwa na nyumbu ambayo yalitumiwa kupeleka bidhaa kotekote mjini. Kituo hicho kiliitwa Kituo cha Nyumbu. Thaddius alikuwa mtu mrefu mwenye sura nzuri na ngozi ya kahawia. Alijulikana kuwa msemaji mwenye shauku, na mara nyingi alitoa hotuba kwenye kituo hicho. Ijapokuwa watu wa Belize wanapenda Biblia, wengi wameshikilia sana dini zinazojidai kuwa ni za Kikristo. Hata hivyo, watu wenye moyo mweupe kama vile James Hyatt na Arthur Randall, ambao walikuwa wametoka Jamaika, walikubali habari njema.

Kaskazini mwa Belize City, Thaddius alianza kufanya mikutano katika duka lake la mikate. Alisukuma kando meza ya kuwahudumia watu, na akaweka mbao juu ya viti ili pawe na mahali pa kutosha pa kuketi. Kusini mwa mji, mikutano ilifanywa nyumbani kwa Cora Brown. Nora Fayad anakumbuka kwamba alipokuwa msichana mdogo, Mashahidi wachache walioishi katika eneo lao walikuwa wakikutana katika ua wa jirani yao, Arthur Randall.

BIDII YALETA MATOKEO MAZURI

Mashahidi hao wa kwanza walijulikana kwa kuhubiri bila kuchoka. Kwa mfano, James (Jimsie) Jenkins aliyekuwa kipofu, alitembea kwa miguu kotekote Belize City, akitumia fimbo yake. Molly Tillet anasema kwamba sauti yake ilisikika mbali sana alipohubiri sokoni! James anakumbukwa pia kwa kusikiliza kwa makini mikutanoni. Kwa kawaida aliketi akiwa amejiegemeza kwa fimbo yake ili asikie kila neno. Alikumbuka maandiko mengi ya Biblia ambayo aliyakariri katika kazi ya kuhubiri.

James Gordon, alijulikana katika vijiji vilivyo karibu na Bomba kwa kumhubiria kila mtu aliyekutana naye. Alibeba vitabu vyake katika sanduku la mbao za mkangazi kwa mkono mmoja, na santuri katika ule mkono mwingine. Asubuhi na mapema kila Jumapili, alisafiri kwa mtumbwi wake mtoni mpaka eneo ambako angehubiri, kisha akatembea kwa miguu siku nzima akihubiri. Jioni watu walimwona akirudi, giza lilipoanza kuingia. Baada ya chakula cha jioni, James aliongoza funzo la Biblia pamoja na watoto wake sita mpaka alipokuwa amechoka sana hivi kwamba alishindwa kushika kitabu chake.

Wakati huo, mke wa Ndugu Gordon hakuwa Shahidi. Siku moja, Ndugu Gordon alipokuwa ameondoka, mke wake aliteketeza karibu vitabu vyake vyote vya Biblia. Aliporudi na kuona kile alichokuwa amefanya, James hakufoka kwa hasira. Alisema tu kwa sauti imara, “Usijaribu kufanya hivyo tena kamwe!” Watoto wake walivutiwa kuona jinsi alivyojizuia, kwa maana walijua tendo la mke wake lilimuumiza sana.

ROHO YA YEHOVA ILIWAVUTA

Jumapili moja asubuhi, James alimhubiria Derrine Lightburn aliyekuwa mfuasi mwenye bidii wa Kanisa la Anglikana. Derrine alichukua kitabu The Harp of God. Hakusikia yote ambayo mtu huyo mwenye sauti nyororo alisema, lakini alitaka kuelewa ujumbe wake. Baadaye, alipokaa na mama yake mkubwa Alphonsena Robateau, huko Belize City, mtu fulani alifika langoni na kuomba ruhusa ya kuingia uani.

Derrine alimwambia Alphonsena, “Anafanana na yule mtu aliyeniletea kile kitabu kizuri, ambacho nilikueleza kukihusu!”

Hata hivyo, yule mtu hakuwa James Gordon bali James Hyatt. Alitumia santuri yake kuwachezea wanawake hao wawili sahani yenye hotuba na akamwachia Alphonsena kitabu The Harp of God. Ingawa walikuwa wamejihusisha sana na siasa, Alphonsena na dada yake Octabelle Flowers, walikuwa wakitafuta kweli. Mambo ambayo Alphonsena alisikia siku hiyo yalifanya amwambie Octabelle hivi kwa shauku: “Wajua, mtu fulani alikuja hapa na akaongea kuhusu Ufalme wa Mungu. Nafikiri tumepata kile ambacho tumekuwa tukikitafuta!” Octabelle alihakikisha alikuwapo ndugu huyo aliporudi. Wanawake wote watatu—Alphonsena, Octabelle, na Derrine—walikubali kweli na wakabatizwa mwaka wa 1941.

Mama ya Alphonsena na Octabelle alikuwa amekufa muda mfupi uliopita, na Amybelle Allen, dada yao mdogo, alimwomba Mungu afe pia ili awe pamoja na mama yake mbinguni. Octabelle alimwalika Amybelle asikilize hotuba yenye kichwa, “Wafu Wako Wapi?” Amybelle alikubali mwaliko huo na tangu siku hiyo hakuacha kuhudhuria mikutano.

Olga Knight ambaye ni binti ya Derrine anasema: “Watu hao walivutwa na roho ya Yehova kwa kusoma tu vitabu na kuhudhuria mikutano. Walisisimka sana walipopata kweli hivi kwamba muda si muda walianza kuwaeleza wengine yale ambayo walikuwa wamejifunza.”

Kwa mfano, baba ya Olga anayeitwa Herman Lightburn, alikubali kweli baada ya kusoma kitabu Children alipokuwa amelazwa hospitalini. Yale aliyojifunza yalifanya awe na shauku sana hivi kwamba kila Ijumaa (Siku ya 5) alikodi lori ili apeleke kikundi cha wahubiri kwenye vijiji vya karibu ili watoe ushahidi huko. Alihubiri sana pia katika eneo la mashambani la Black Creek, alikokuwa na shamba.

Olga anasema: “Wazazi wangu walihubiri kando ya Mto Belize, na saa za jioni watu walikuja wakiwa wamebeba taa zao ili wasikilize. Kila asubuhi tulipokuwa likizoni katika shamba la baba, tulienda kuhubiri Crooked Tree. Mimi, wazazi wangu, mama yangu mkubwa, Amybelle, na binti yake Molly Tillet, tulisafiri kwa farasi wa baba yangu kuelekea huko. Tulipofika, farasi waliachwa malishoni nasi tulijifunza Biblia pamoja na watu waliopendezwa. Baadhi ya familia hizo zilikubali kweli.”

Wahubiri wapya wa kwanza walibatizwa mwaka wa 1941 katika Bahari ya Karibea, karibu na Belize City. George Longsworth alikuwa mmoja wao, naye alikuwa painia kuanzia mwaka huo mpaka alipokufa mwaka wa 1967 akiwa na miaka 87. Alisafiri mbali sana akiwa amepanda farasi ili kuhubiri katika miji na vijiji kwenye maeneo ya mashambani, ambako habari njema hazikuwa zimehubiriwa bado. Bidii ya George ya kuhubiri bila kuchoka na ya kuhudhuria mikutano yote iliwatia moyo hasa wapya. Yehova alitumia watumishi hao waaminifu na wenye bidii kwa njia kubwa ili kuwavuta watu wenye moyo mweupe wajiunge na tengenezo lake.

WAMISHONARI WA KWANZA WAFIKA

Elmer Ihrig na Charles Heyen waliohitimu darasa la kwanza la Gileadi, walifika Oktoba 5, 1945. Siku iliyotangulia, eneo lililo umbali wa kilomita 160 hivi kusini ya Belize City, lilikuwa limekumbwa na kimbunga. Barabara ya uwanja wa ndege ilikuwa imefurika maji, hivyo, wamishonari hao wawili walibebwa kwa malori makubwa ya jeshi umbali wa kilomita 16 mpaka jijini. Thaddius Hodgeson aliweka matofali ya sementi na masanduku ya mbao mbele ya nyumba yake ili wamishonari hao walipofika waweze kuingia bila kupita majini.

Ndugu huko Belize walingojea kwa hamu wamishonari hao wa kwanza. James Gordon, León Requeña, na Rafael Medina, walisafiri kutoka sehemu ya kaskazini ya nchi hadi Belize City ili waonane na wamishonari hao wapya. Safari hiyo haikuwa rahisi siku hizo! Ismael Medina, mjukuu wa Rafael anaeleza: “Hakukuwa na barabara kubwa kutoka sehemu za kaskazini mpaka Belize City. Kulikuwa na vijia tu vya magari yanayokokotwa na nyumbu. Sehemu walizopitia hazikuwa na nyumba. Kwa hiyo, usiku ulipoingia walilala popote pale walipokuwa wamefika, ingawa eneo hilo lina nyoka wengi. Baada ya kuonana na wamishonari na kupokea maagizo na vitabu, ndugu hao watatu walirudi kwa miguu. Safari hiyo ilichukua siku kadhaa!”

Wamishonari hao walijulishwa kwa wasikilizaji kwa njia isiyo ya kawaida kwenye Kituo cha Nyumbu. James Hyatt alianza hotuba kwa kuwashutumu vikali makasisi kwa sababu ya mafundisho yao ya uwongo, na baadhi ya watazamaji wakaanza kutoa matusi. Ghafula, katika umalizio wa hotuba yake, akawaelekezea wamishonari kidole na kusema, “Ninawakabidhi hao wawili kwenu!” Kwa maneno hayo machache, ndugu hao wapya walijulishwa kwa wasikilizaji!

Bila shaka, ndugu hao wa kwanza walimpenda sana Yehova na kweli za Biblia, na walichukia sana mafundisho ya uwongo ya dini. Ilikuwa wazi pia kwamba wale wamishonari wenye uzoefu wangeweza kuwasaidia ndugu hao wenye bidii wawe wahubiri stadi zaidi.

Wamishonari hao wawili walianza kuhubiri huko Belize City, lililokuwa na wakaaji 26,700 hivi wakati huo. Jiji hilo lilikuwa limejengwa futi moja tu juu ya usawa wa bahari na halikuwa na mitaro ya kutosha ya kuondoa maji. Isitoshe, kulikuwa na joto kali na unyevu mwingi. Hakukuwa na mabomba ya maji, lakini karibu kila nyumba ilikuwa na pipa la mbao lililotumiwa kukusanya maji ya mvua. Nyakati nyingine mvua ilikuja kwa fujo, kama ilivyokuwa mwaka wa 1931, wakati kimbunga kilipoharibu mji huo na watu zaidi ya 2,000 wakafa.

KAZI YAENDELEA KUJAPOKUWA VIZUIZI

Ingawa kazi ya Mashahidi wa Yehova haijawahi kupigwa marufuku nchini Belize, vitabu vyetu vilipigwa marufuku kwa kipindi fulani wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Lakini, muda mfupi kabla ya wamishonari kufika, vizuizi hivyo vilikuwa vimeondolewa.

Hata hivyo, toleo la Mnara wa Mlinzi la Julai 15, 1946, lililozungumzia utendaji wa wale wamishonari wawili nchini Belize, lilisema hivi: “Katika sehemu za mashambani, kasisi fulani wa Kanisa Katoliki bado anajaribu kuendeleza ile marufuku juu ya vitabu vinavyotumwa kwa njia ya posta. Makasisi wa Kanisa Katoliki hawawataki wamishonari hao wa Mashahidi wa Yehova nchini humu; na kasisi mmoja Mmarekani mwenye asili ya Ireland . . . amekasirika kwa sababu Serikali ya Ukoloni ya Uingereza imewaruhusu kukaa nchini humu. . . . [Wamishonari] hao wawili walimkumbusha kasisi huyo kwamba yeye mwenyewe ni Mmarekani. Walipomtajia kwamba takwimu za magereza ya Marekani zinaonyesha wazi kwamba Kanisa Katoliki haliwasaidii Wamarekani wawe na mwenendo mzuri, aliondoka haraka akiwa amefedheheshwa.”

Mwaka wa 1944 wahubiri saba walitoa ripoti, na hiyo ndiyo ripoti sahihi ya kwanza ya idadi ya wahubiri nchini Belize. Ili kutoa ushahidi vizuri zaidi, wahubiri walianza kutumia kadi za kutoa ushahidi walipohubiri nyumba kwa nyumba. Kabla ya mwaka mmoja kwisha baada ya wamishonari kufika, idadi ya wahubiri ilikuwa imeongezeka hadi 16.

Mwaka wa 1946, Nathan H. Knorr na Frederick W. Franz, kutoka makao makuu, walitembelea Belize na kufungua ofisi ya tawi humo. Ndugu Knorr alitoa hotuba kuhusu mpango wa usimamizi, na kueleza umuhimu wa kutoa ripoti ya utumishi wa shambani kwa kutumia fomu zilizoandaliwa. Ndugu Franz naye aliwahimiza ndugu wawaonyeshe wengine rehema kwa kuendelea kuhubiri ujumbe wa Ufalme. Baadaye katika juma hilo, watu 102 walisikiliza wakati Ndugu Knorr alipoeleza kwa nini watu wanaopendezwa wanapaswa kufurahia kushirikiana na watu wa Yehova. Watu wengi wenye kupendezwa walisikiliza hotuba hiyo. Aliwatia moyo wajifunze Biblia kwa ukawaida pamoja na Mashahidi.

Mwaka uo huo, Charles na Annie Ruth Parrish na Cordis na Mildred Sorrell walifika. Truman Brubaker na Charles na Florence Homolka walifika mwaka wa 1948. Walikaribishwa kwa mikono miwili, kwa maana kazi ilikuwa nyingi.

KAZI NYINGI SANA

Elmer Ihrig aliandika: “Wakati huo kulikuwa na kutaniko moja tu dogo, hakukuwa na makutaniko katika maeneo ya mashambani. Nilikuwa nikienda kwenye maeneo hayo na kukaa kwa majuma kadhaa, huku nikipanda mbegu kwa kuwaachia watu vitabu na magazeti, na kutoa hotuba.” Katika mwaka huo wa kwanza, Charles Heyen alikuwa akisafiri kwa lori mpaka Orange Walk, ambako alihubiri na kuwatia ndugu moyo wafanye mikutano kwa ukawaida.

Hakukuwa na njia nyingine ya kufikia miji ya sehemu za kusini ila kwa mashua. Kwa hiyo, Elmer na Charles walisafiri kwa mashua inayoitwa Heron H mpaka Stann Creek (sasa unaitwa Dangriga) na Punta Gorda, miji miwili ya pwani ya Wagarifuna. Walikuwa na lengo la kuanzisha kazi ya kuhubiri huko. Siku hizo, ilichukua saa 30 kusafiri kwa mashua kutoka Belize City mpaka Punta Gorda. Elmer alisafiri mpaka Punta Gorda, kisha akawatolea watu 20 hivi hotuba ya watu wote katika sebule ya hoteli ambamo alikaa.

Olga Knight anakumbuka kwamba Elmer aliandamana na familia yao mpaka kijiji cha mbali cha Crooked Tree, ambako baba yake aliongoza mikutano chini ya miti, kando ya mto. Ndugu wenyeji walithamini kazi ya wamishonari na unyenyekevu wao.

Mwaka wa 1948 wahubiri walikuwa 38 kwa wastani, na makutaniko manne yalikuwa yameanzishwa nje ya Belize City. Makutaniko hayo madogo ya mashambani yalikuwa na wahubiri wachache tu, kama vile familia ya Lightburn huko Black Creek, familia ya Gordon huko Bomba, familia ya Humes na ya Aldana huko Santana, na Ndugu Requeña na Medina huko Orange Walk. Wamishonari na mapainia wa pekee walihubiri hasa huko Belize City, kama walivyokuwa wametiwa moyo kufanya. Yehova alibariki jitihada zao nyingi, na idadi ya watu wenye mioyo myeupe waliotaka kuwa watumishi wa Yehova iliongezeka daima.

Ndugu Knorr, alitembelea Belize tena mnamo Desemba 1949, na ziara yake ilikuwa ya wakati unaofaa na yenye kutia moyo. Alishinda jioni moja kwa wamishonari akiongea nao kuhusu changamoto za utumishi wao. Wahubiri wengi wapya walitaka kumtumikia Yehova, lakini hawakuona umuhimu wa kujiweka wakfu na kubatizwa. Ndugu Knorr aliwakumbusha wamishonari kwamba wanahitaji subira, uvumilivu, na kuwapenda watu. Pia aliwakumbusha kwamba tayari walikuwa wamepata matokeo mazuri.

WAMISHONARI WENGINE HAWARUHUSIWI KUINGIA NCHINI

Mwaka wa 1957 ndugu walitambua kwamba serikali ilikuwa ikichunguza kwa makini utendaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Belize. Kwa mfano, ndugu walipokuwa wakionyesha sinema fulani ya Mashahidi wa Yehova huko Orange Walk, ofisa mmoja wa polisi aliwahoji ndugu kutoka ofisi ya tawi. Alitaka kujua walikuwa wamefika kijijini humo saa ngapi na wangeondoka saa ngapi. Alisema kwamba angeripoti mambo hayo kwa mkuu wa polisi na akawaeleza kwamba polisi aliyevalia mavazi ya raia alikuwa amehudhuria kusanyiko hivi majuzi na kutoa ripoti kama hiyo.

Kati ya mwaka wa 1951 na 1957 wamishonari wengine kumi walikuwa wameruhusiwa kuingia nchini humo. Mnamo Juni 1957, ndugu walishtuka walipopokea barua kutoka kwa polisi na idara ya uhamiaji iliyosema: “Serikali ya Honduras ya Uingereza [sasa inaitwa Belize] imeamua kwamba kuanzia sasa, hakuna Wahudumu wa Shirika lenu kutoka ng’ambo, watakaoruhusiwa kuingia Honduras ya Uingereza.” Ombi la kumwona gavana ili kujua sababu ya uamuzi huo lilikataliwa mbali.

Dini nyingine pia hazikuruhusiwa kuongeza idadi ya wamishonari, lakini ziliruhusiwa kumleta mmishonari mwingine iwapo mmoja angehitaji kuondoka nchini. Mashahidi wa Yehova hawakuruhusiwa kufanya hivyo, ingawa wawili kati ya wamishonari wao walikuwa wameacha utumishi wao. Mwaka wa 1960 ndugu waliwaandikia wenye mamlaka nchini Belize, na vilevile huko London, na kuwaeleza kwamba hawaombi idadi ya wamishonari iongezwe, bali wanaomba kibali cha kuwaleta wengine badala ya wale wanaohitaji kuondoka nchini.

Walijibiwa kifupi hivi: “Gavana amefanya uamuzi thabiti wa kutoruhusu shirika la Watch Tower Bible and Tract Society kuwaleta wamishonari wengine nchini Honduras ya Uingereza.”

Ndugu walipoomba kuongea naye, waliambiwa: “Gavana alifanya uamuzi thabiti mwaka wa 1957 wa kutoruhusu Shirika lenu kuwaleta wamishonari wengine nchini Honduras ya Uingereza; kwa hiyo, Mheshimiwa haoni haja yoyote ya kuongea nanyi tena kuhusu jambo hili.” Ilionekana kama ndugu wangelazimika kusalimu amri.

Mwishowe, baada ya kuendelea kupeleka maombi kwa karibu miaka mitano, ofisi ya tawi ilipokea barua mnamo Oktoba 1961 kutoka Idara ya Usimamizi ya Belize. Ilisema hivi: “Nimeagizwa kuwaarifu kwamba maombi yenu ya karibuni yamechunguzwa na Serikali ya Honduras ya Uingereza, ambayo imeamua kwamba kwa sasa, itawapa wamishonari wengine kutoka ng’ambo kibali cha kuingia nchini humu, iwapo wamishonari wowote kutoka ng’ambo walio nchini humu watahitaji kuondoka.” Hivyo, wamishonari Martin na Alice Thompson kutoka Jamaika waliruhusiwa kuingia Belize mwaka wa 1962.

KAZI YA KUHUBIRI YASONGA MBELE

Ni wazi kwamba wanadini walijaribu kuzuia kazi yetu. Je, walifaulu? Ripoti ya mwaka wa utumishi wa 1957 ilionyesha kilele kipya cha wahubiri 176 katika makutaniko saba. Belize ilikuwa na wakaaji 75,000 wakati huo, hili linamaanisha kwamba kulikuwa na mhubiri 1 kwa watu 400. Mwaka wa utumishi wa 1961 kulikuwa na wahubiri 236, ongezeko la asilimia 34, yaani, kulikuwa na mhubiri 1 kwa watu 383! Ahadi ya Yehova kwa watu wake ni ya kweli: “Silaha yoyote itakayofanywa juu yako haitafanikiwa, na ulimi wowote utakaoinuka juu yako katika hukumu wewe utauhukumu.” (Isa. 54:17) Kazi ya kuhubiri ilisonga mbele.

Wanaume na wanawake wengi waliojifunza Biblia waliishi pamoja bila kufunga ndoa, na baadhi yao walikuwa na zoea la kuacha mwenzi mmoja na kuchukua mwingine. Lakini walipoelewa matakwa ya Yehova, wengi walijitahidi sana kufunga ndoa na walikuwa tayari kulipa pesa nyingi ili kufanya hivyo. Baadhi yao walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 80!

JUMBA JIPYA LA UFALME LAHITAJIKA

Mnamo Desemba 1949, ndugu walikodi Jumba la Uhuru huko Belize City kwa ajili ya mfululizo wa hotuba nne za pekee ambazo zingetolewa mwezi wa Januari 1950. Siku iliyotangulia hotuba ya mwisho, ilitangazwa kwenye redio kwamba jumba hilo lingetumiwa kwa ajili ya ibada ya mazishi ya mwanamke maarufu. Ijapokuwa ndugu walipeleka malalamiko kwa wenye jumba hilo, hotuba ya pekee ilivurugwa na watu ambao waliingia na kuanza kufanya matayarisho kwa ajili ya ibada hiyo, huku wakipiga kelele sana. Hatimaye, ndugu waliwaomba polisi waingilie kati. Ni wazi kwamba ndugu walihitaji Jumba la Ufalme. Majumba yote huko Belize City yalitumika kama vilabu au kwa ajili ya kucheza dansi, na kodi zilikuwa za juu.

Donald Snider, aliyekuwa mwangalizi wa ofisi ya tawi, anaeleza: “Jumapili jioni, watu 174 walihudhuria Funzo la Mnara wa Mlinzi. Jumba tunalotumia halina nafasi kwa watu wengi hivyo, basi, watu kadhaa wanalazimika kusimama. Na kwa sababu watu wanasongamana sana, joto linakuwa jingi.” Ofisi ya tawi na makao ya wamishonari yalihamishwa mara kadhaa kutoka jengo moja la kukodiwa hadi lingine.

Ujenzi wa jengo lenye ghorofa moja ulianza mnamo Septemba 1958. Ofisi ndogo ya tawi na makao ya wamishonari yalikuwa chini, na juu kulikuwa na ukumbi. Ujenzi ulimalizika mnamo mwaka wa 1959, na mwishowe Kutaniko la Belize City likawa na Jumba la Ufalme!

WATU WANAOONGEA KIHISPANIA WAKUBALI KWELI

Watu wengi wanaoongea Kihispania wamekubali kweli na kujiunga na watu wa Yehova nchini Belize. Mnamo mwaka wa 1949, ndugu walikuwa wakihubiri katika maeneo ambako Kihispania kinatumiwa, lakini wakati huo hakuna mmishonari hata mmoja aliyeongea lugha hiyo. Hata hivyo, baadaye wamishonari waliojua Kihispania walitumwa huko. Mmoja wao alikuwa Leslie Pitcher, aliyefika mwaka wa 1955. Alitumwa huko Benque Viejo, mji wenye wakaaji wanaoongea Kihispania. Mji huo uko magharibi mwa Belize karibu na mpaka wa Guatemala. Alipofika, baadhi ya wenyeji walikuwa wakimngojea. Walijua jinsi gani kwamba anakuja?

Mwaka mmoja hivi kabla ya hapo, katika mji wa San Benito nchini Guatemala, Natalia Contreras alikuwa amejifunza kweli na kubatizwa. Alivuka mpaka na kuingia Belize ili kuwahubiria watu wake wa ukoo walioishi Benque Viejo. Mmoja wao ni Serviliano Contreras, aliyemsikiliza Natalia kwa makini alipoeleza maoni ya Biblia kuhusu ibada ya sanamu, na akakubali kweli. Alikuwa Shahidi mwaminifu hadi alipokufa mwaka wa 1998, akiwa na umri wa miaka 101. Wengi wa watoto wake na wajukuu wake ni Mashahidi. Ijapokuwa wahubiri walikuwa wachache tu huko Benque Viejo siku hizo, walivuka mpaka wa Guatemala na kuhubiri katika mji wa Melchor de Mencos, ambako walifanya mikutano. Hatimaye, kutaniko lilianzishwa huko Melchor de Mencos, na ndugu wa Kutaniko la Benque Viejo bado wanajulikana kwa bidii yao.

Kuanzia mwaka wa 1956, baadhi ya hotuba za makusanyiko ya wilaya na ya mzunguko zilitolewa katika Kihispania. Miaka mingi baadaye, mnamo Februari 1968, hotuba zote za kusanyiko la mzunguko zilitolewa katika Kihispania kwa mara ya kwanza. Watu 85 walihudhuria na 4 wakabatizwa katika kusanyiko hilo lililofanywa kwenye Jumba la Ufalme huko Orange Walk.

Marcelo Dominguez na Rafael Medina, ndugu wawili walioongea Kihispania, pamoja na Mashahidi wengine walioongea lugha hiyo kama vile Dionisio na Catalina Tek, walihudhuria kwa uaminifu mikutano na makusanyiko ya Kiingereza, ijapokuwa hawakuelewa lugha hiyo vizuri. Hatimaye, mnamo Oktoba 1964, kutaniko la Kihispania lilianzishwa huko Orange Walk, na wahubiri 20 waliokuwa wakishirikiana na kutaniko la Kiingereza wakajiunga nalo.

Katika miaka ya 1980 kulikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi jirani ya El Salvador na Guatemala, kwa hiyo, watu wengi walikimbilia Belize. Kati yao walikuwa Mashahidi walioongea Kihispania, wakiwemo wazee wa kutaniko, watumishi wa huduma, na mapainia. Mashahidi hao na wamishonari waliojua lugha mbili kutoka nchi ambako Kihispania kinatumiwa, walisaidia kuwahubiria watu wanaoongea Kihispania.

“WAKRISTO WA KWELI HUHUBIRI NYUMBA KWA NYUMBA”

Siku moja, wageni wawili walibisha mlango wa Margarita Salazar mjini Orange Walk na kumuuliza, “Je, unamjua Shahidi wa Yehova anayeitwa Margarita Salazar?” Wageni hao, Teófila Mai aliyekuwa na miaka 23 na mama yake, walikuwa wakaaji wa kijiji cha August Pine Ridge, umbali wa kilomita 34 kutoka Orange Walk. Kwa nini walikuwa wakimtafuta Margarita?

Teófila anaeleza: “Yapata mwaka mmoja mapema, mtoto wangu wa kiume mwenye umri wa miezi tisa alikuwa mgonjwa sana. Kwa hiyo, nikampeleka kijijini Botes kwa bikira mtakatifu anayeitwa Santa Clara, ili amponye. Nilisafiri kwa lori, na nilikaa katika kiti cha mbele. Dereva aliyeishi katika eneo letu alianza kunihubiria. Baada ya kuniuliza kwa nini ninampeleka mtoto wangu huko Botes, aliniambia kwamba Biblia inashutumu ibada ya sanamu. Nilivutiwa sana kusikia jambo hilo. Mtu huyo aliendelea kunifunza kweli nyingi za Biblia ambazo alikuwa amefundishwa na Mashahidi wa Yehova.”

Teófila anaongeza: “Katika safari moja yule dereva wa lori aliniambia kwamba Wakristo wa kweli huhubiri nyumba kwa nyumba. Alinieleza kwamba Mashahidi wa Yehova wanafanya hivyo na kwamba wao huwasomea watu maandiko kama vile Sefania 1:14 na 2:2, 3. Basi, huku nikiwa nimemshika mkono mtoto wangu wa kiume na kumbeba yule mchanga, nilienda nyumba kwa nyumba huko August Pine Ridge na kuwasomea jirani zangu maandiko hayo. Baadaye dereva huyo aliniambia kwamba iwapo ningetaka kujua kweli, ingenibidi kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. Alinieleza kuwahusu akina Salazar na kuniambia mahali ambapo ningeweza kuwapata huko Orange Walk. Sikuwa nimewahi kufika Orange Walk, kwa hiyo, niliandamana na mama yangu nilipoenda kuwatafuta.”

Margarita anakumbuka asubuhi ambapo Teófila na mama yake walimtembelea kwa mara ya kwanza. Anasema: “Waliuliza maswali mengi ya Biblia, na tulizungumza kwa muda mrefu. Walitaka kujua kama ni kweli kwamba Mashahidi wa Yehova wanawasaidia watu kuielewa Biblia, hata kama watahitaji kusafiri mbali sana ili kuwafundisha. Niliwahakikishia kwamba ndivyo ilivyo, na kuwaahidi tungewatembelea kijijini kwao baada ya kila majuma mawili ili kuwafundisha Biblia.”

Margarita na mume wake Ramón walipofika August Pine Ridge, Teófila alikuwa amewakusanya watu sita wa jamaa yao waliotaka kujifunza Biblia. Baadaye, mapainia waliokuwa Orange Walk walijiunga na ndugu na dada Salazar waliposafiri kwenda August Pine Ridge. Walisafiri kwa ukawaida umbali wa kilomita 34 kwenye barabara nyembamba ya vumbi yenye mashimo mengi ili kuhubiri kijijini, huku Teófila na watu wa jamaa yake wakijifunza Biblia. Mara nyingi Amybelle Allen alilala kijijini humo ili aongoze mafunzo ya Biblia. Teófila alibatizwa mwaka wa 1972, miezi mitano baada ya kuanza kujifunza Biblia. Kutaniko lilianzishwa huko August Pine Ridge mwaka wa 1980, na watu 37 wa jamaa ya Teófila wamekubali kweli.

MATOKEO MAZURI YA SAFARI ZA MASHAMBANI

Ingawa Belize City, na miji mingine mikubwa nchini Belize ilikuwa ikihubiriwa kikamili, maeneo ya mashambani hayakuwa yakihubiriwa kwa ukawaida. Wamishonari wa kwanza nchini Belize walisafiri kwa mashua hadi miji ya kusini, lakini baadaye barabara ikajengwa ambayo iliziunganisha wilaya za kusini za Stann Creek na Toledo na sehemu nyingine za nchi. Mapema mwaka wa 1971, ofisi ya tawi ilipanga safari za kila mwaka za kuhubiri mashambani ili kupeleka ujumbe wa Ufalme kwa Wamaya wa kabila la Wamopan na Wakekchi, kwenye maeneo ya mbali ya msitu wa mvua wa Belize.

Ndugu na dada walisafiri kwa magari ya kukodiwa na mitumbwi ili kutembelea vijiji na miji kuanzia Dangriga hadi Punta Gorda. Pia walisafiri hadi Barranco upande wa kusini, karibu na mpaka wa Guatemala. Nyakati nyingine ndugu kadhaa walisafiri katika gari moja, huku wakiandamana na wengine wawili au wanne waliosafiri kwa pikipiki. Kila usiku walipumzika katika kijiji tofauti. Mchana, wale ndugu waliosafiri kwa gari walihubiri kijijini, huku wale waliosafiri kwa pikipiki wakihubiri wawili-wawili katika mashamba ya mbali.

Katika eneo la Punta Gorda, ndugu walitembea kutoka kijiji kimoja hadi kijiji kingine, wakiwa wamebeba mizigo yao mgongoni. Mara nyingi iliwabidi kuzungumza na alcalde (chifu) kwenye cabildo (mahali ambapo wazee wa kijiji wanakutana) kabla ya kuwahubiria wanakijiji.

Mmishonari anayeitwa Reiner Thompson anasema: “Walipofika katika kijiji kimoja, ndugu waliwakuta wazee hao wamekutana kwenye cabildo, wakizungumzia mpango wa kuvuna mahindi. Baada ya mkutano huo, wazee hao waliwaomba akina ndugu waimbe wimbo mmoja wa Ufalme. Ndugu hao walikuwa wamechoka, wenye njaa, na hawakuwa na kitabu cha nyimbo.” Ndugu Thompson anaongeza, “Waliimba kwa moyo wao wote, na wazee hao wakafurahi sana.” Muda si muda, kutaniko lilianzishwa kijijini Mango Creek na baadaye San Antonio, kimoja kati ya vijiji vikubwa zaidi vya Wamaya.

Santiago Sosa anaeleza, “Nyakati nyingine tulitembea usiku kutoka kijiji kimoja hadi kingine ili kwenda sambamba na ratiba yetu. Ilitubidi kutembea kwa kufuatana katikati ya barabara ili kuepuka nyoka waliokuwa vichakani kando-kando ya barabara. Pia, ilitubidi kujifunza jinsi ya kutoa maji ya kunywa katika mmea fulani, wakati maji yetu yalipoisha.”

Nyakati nyingine, ndugu katika kikundi waliandamana wawili-wawili au wanne-wanne ili kuhubiri katika maeneo tofauti ya kijiji. Kisha, walikutana tena jioni. Ndugu wawili walikuwa wakiachwa nyuma ili kupika. Santiago anasema hivi huku akicheka: “Nyakati nyingine ilikuwa balaa tupu, kwa kuwa baadhi ya akina ndugu hawakujua kupika. Ninakumbuka nikitazama mlo fulani na kuuliza, ‘Hiki ni chakula gani?’ Kisha ndugu aliyekipika akasema, ‘Sijui, lakini ni chakula.’ Kwa kuwa mpishi hakujua amepika chakula gani, tuliamua kwanza tumpe mbwa koko fulani aliyekonda chakula hicho. Lakini hata mbwa huyo mwenye njaa akakataa katakata kukila!”

WAKEKCHI WAKUBALI KWELI

Rodolfo Cocom na mke wake Ofelia walihama kutoka Corozal, wakaenda kijiji cha mbali cha Wakekchi kinachoitwa Crique Sarco, upande wa kusini. Ofelia alikulia katika kijiji hicho ambacho kilitembelewa na Mashahidi mara moja tu kwa mwaka, wakati wa safari zao za mashambani. Alipokuwa na umri wa miaka 14, Ofelia alipata kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele chini ya mchungwa na akaanza kukisoma. Alitaka kujua mengi zaidi, lakini tamaa hiyo ilitimizwa baadaye akiwa tayari ameolewa na anaishi na mume wake huko Corozal. Ofelia na mume wake Rodolfo walijifunza Biblia pamoja na mapainia wa pekee wawili, Marcial na Manuela Kay.

Walipohamia Crique Sarco mwaka wa 1981, Rodolfo na mke wake walitaka kuendelea kujifunza na Mashahidi, kwa hiyo, Rodolfo akaenda Punta Gorda kuwatafuta. Alitembea kwa miguu na pia kusafiri kwa mashua mtoni na baharini, kwa muda wa saa sita. Huko Punta Gorda, alikutana na Donald Niebrugge, painia aliyepanga kujifunza pamoja naye na mke wake kupitia barua. Hata hivyo, walikabili tatizo fulani. Hakukuwa na kituo cha posta huko Crique Sarco.

Donald anaeleza, “Nikiwa kwenye kituo cha posta huko Punta Gorda, niliuliza jinsi ambavyo ningeweza kutuma barua Crique Sarco. Nilielezwa kwamba kuna kasisi anayeenda huko mara moja kwa juma.” Kwa hiyo, kwa kipindi cha miezi sita, kasisi huyo alipeleka na kurudisha barua zetu bila kujua kwamba alikuwa akiwasaidia Mashahidi wa Yehova kuongoza funzo la Biblia.

Donald anasema, “Kasisi huyo alipogundua alichokuwa akibeba, alikasirika sana na akakataa kabisa kubeba barua zetu.”

Katika kipindi hicho, Donald alisafiri mara kadhaa kwenda Crique Sarco ili kujifunza na Rodolfo na mke wake. Katika safari iliyofuata ya mashambani, Rodolfo alianza kuhubiri. Donald anaendelea kusema, “Tuliandamana naye kwa siku nne na kuhubiri katika vijiji kadhaa. Kushirikiana na akina ndugu katika safari hiyo kulimsaidia Rodolfo kufanya maendeleo.”

Rodolfo anaeleza, “Mimi na Ofelia tulikuwa tukienda kuhubiri kijijini kwetu ili kuwaeleza wengine mambo tuliyokuwa tumejifunza. Watu niliojifunza nao walipata upinzani mkali zaidi kuliko sisi. Baadhi yao walinyimwa dawa, chakula, na nguo zilizotolewa kama msaada kwa wanakijiji. Mama-mkwe wangu pia alitupinga sana. Mimi na Ofelia tulitambua kwamba hatungeweza kufanya maendeleo ya kiroho tukiwa Crique Sarco. Tulihitaji kuhudhuria mikutano, kwa hiyo, tukahamia Punta Gorda ili kuendelea kujifunza. Huko tulifanya maendeleo ya kiroho na kubatizwa mwaka wa 1985.” Leo, Rodolfo na Ofelia wanashirikiana na Kutaniko la Ladyville, ambapo Rodolfo ni mtumishi wa huduma.

MATOKEO MAZURI YA SAFARI ZA BAHARINI

Safari za baharini zilipangwa kila mwaka ili kuwahubiria watu kwenye visiwa na vijiji vya pwani. Vijiji kama vile Hopkins, Seine Bight, Placencia, na Punta Negra, na pia Monkey River Town, havikufikika kwa barabara. Pindi moja, wakati samaki aina ya kamba-mti hawakuwa wengi baharini, Polito Bevens alitumia mashua yake kwenda kuhubiri pamoja na mapainia wawili na wamishonari wawili. Iliwachukua majuma mawili kusafiri kutoka kaskazini hadi kusini, nao walihubiri katika maeneo yote waliyopitia.

Donald Niebrugge ambaye mara nyingi alijiunga na ndugu katika safari za mashambani na baharini, anakumbuka wakati walipoazima mashua ya Ambroncio Hernandez kwa ajili ya safari ya baharini. Baada ya safari hiyo, Ambroncio, aliyeitwa Bocho na marafiki wake, alianza kujifunza Biblia.

Donald anasema, “Mwaka uliofuata, mimi na mke wangu na ndugu mwingine na mke wake, tulipanga safari ya baharini ya majuma mawili. Tulitaka kusafiri hadi eneo la kusini kabisa la pwani, lakini wakati huo Bocho alikuwa ameuza mashua yake. Alipendekeza tuzungumze na mvuvi mwingine. Mvuvi huyo alikubali sisi mapainia wa pekee wanne, Bocho, pamoja na mvuvi mwenzake, tusafiri naye kwa mashua yake. Wakati wa safari hiyo, Bocho alianza kuhubiri. Tulipofika kwenye bandari ya Placencia, tulipata mashua nyingi zilizokuwa zimetia nanga, kwa hiyo tukahubiri mashua kwa mashua. Wale wavuvi ambao hawakuwa waamini, walitusaidia sana katika majuma hayo mawili. Siku moja tuliporudi baada ya kuhubiri kijijini siku nzima, wavuvi hao wawili walikuwa wamenunua kuku na kutupikia chakula kwenye jiko la mafuta-taa.” Wakati wa safari ya baharini ya mwaka uliofuata, Bocho alikuwa amebatizwa. Amekuwa mzee wa kutaniko huko Belize City kwa miaka 18 iliyopita.

MATOKEO MAZURI KATIKA MAENEO AMBAYO HAYAJAGAWIWA YEYOTE

Wilaya ya Toledo iliyo kusini mwa Belize ina msitu mkubwa wa mvua, vilima vingi na mabonde mengi. Pia ina vijiji kadhaa vya Wamaya wa kabila la Wamopan na Wakekchi. Nyumba zao zimeezekwa kwa nyasi na zina sakafu za udongo. Maisha ya wanavijiji ni magumu na wanafanya kazi nzito ya kulima kwa majembe ya kawaida. Wakati wa kiangazi, wanalazimika kubeba maji ili kumwagilia mashamba yao ya mahindi, maharagwe, na kakao. Wanawake wengi wanafuata utamaduni wa Wakekchi wa kushonelea mapambo kwenye nguo na kutengeneza vikapu vinavyouzwa kwenye maduka ya bidhaa za watalii kotekote nchini. Vijana wengi wanaondoka vijijini kwenda kusoma au kufanya kazi katika maeneo yenye watu wengi nchini.

Katika mwaka wa 1995, Frank na Alice Cardoza waliombwa kutumika kama mapainia wa pekee wa muda mwezi wa Aprili na Mei katika Wilaya ya Toledo, ili wasaidie kugawa trakti Habari za Ufalme Na. 34, “Kwa Nini Maisha Yamejaa Matatizo Sana?” Frank anasema: “Nilikuwa nimeshiriki katika moja kati ya safari za mashambani zinazofanywa kila mwaka katika eneo hili, na niliona kwamba Wamaya wangeweza kusaidiwa vizuri zaidi kama mtu angehamia wilayani Toledo. Ofisi ya tawi ilipendekeza nikodi mahali pa kukaa huko San Antonio, nianzishe kikundi cha funzo la Biblia, na kutoa hotuba ya pekee. Tulipaswa kugawa trakti Habari za Ufalme katika kijiji hicho na pia katika vijiji vingine vinane.”

Frank na Alice waliongoza funzo la Biblia la watu kadhaa kila juma katika chumba cha chini ya ardhi walichokodi katika nyumba fulani. Katika muda wa majuma kadhaa, familia tatu hadi nne zilianza kuhudhuria. Pia, watu hao wenye kupendezwa walikuwa wakiandamana na Frank na mkewe kwenda kwenye mkutano wa Shule ya Huduma ya Kitheokrasi na Mkutano wa Utumishi huko Punta Gorda. Walisafiri kwa gari kuukuu kwenye barabara ya vumbi na iliwachukua muda wa saa moja kufika Punta Gorda. Katika mwezi wa kwanza, Frank alitoa hotuba ya pekee huko San Antonio. Jesús Ich, aliyekuwa amehudhuria mkutano kwa mara ya kwanza, alisikiliza kwa makini sana. Alikuwa mfuasi wa Kanisa la Nazarene na alifurahi sana kujua kwamba fundisho kuhusu moto wa mateso si fundisho la Biblia bali ni la kipagani. Baada ya mkutano huo, alimwita Frank kando na kumuuliza maswali mengi kuhusu moto wa mateso. Hivyo, Jesús alianza kujifunza Biblia na akabatizwa mwaka mmoja baadaye.

Baada ya kutumika kwa muda wa miezi miwili wakiwa mapainia wa pekee wa muda, Frank na Alice walikabili uamuzi muhimu. Frank anasema, “Tulikuwa tumeanzisha mafunzo mengi sana hata tulishindwa kuyaongoza yote vizuri. Mioyo yetu na dhamiri zetu hazingeweza kuturuhusu kurudi katika nyumba yetu yenye starehe huko Ladyville. Kama tungeamua kukaa San Antonio, tungeweza kupata mahali pazuri pa kuishi kwa kukodi nyumba iliyokuwa juu ya chumba chetu cha chini ya ardhi. Ningeweza kutengeneza sinki ndogo ya kuoshea vyombo, kifaa cha kukusanya maji ya mvua kutoka kwenye paa, na baadaye, labda kuweka umeme na kutengeneza choo cha kuvuta maji. Tulisali kwa Yehova kuhusu jambo hilo, tukiwa na hakika kwamba angebariki jitihada za kuanzisha kutaniko katika eneo hilo. Kisha, tukawaandikia ndugu katika ofisi ya tawi na kuwajulisha kwamba tulikuwa tayari kukaa San Antonio tukiwa mapainia wa kawaida.”

Baada ya muda mfupi, Yehova alibariki uamuzi wa Frank na mke wake. Kabla ya miezi sita kupita, mkutano wa kwanza wa watu wote ulifanywa mwezi wa Novemba katika nyumba waliyokodi. Na mnamo Aprili mwaka uliofuata, wakaanza kufanya Shule ya Huduma na Mkutano wa Utumishi huko San Antonio. Kikundi hicho kidogo kilifurahi sana kwa kuwa haikuwa lazima kusafiri kwenda kuhudhuria mikutano Punta Gorda, umbali wa kilomita 65 kwenda na kurudi.

“VITISHO VYAKE HAVINGEWEZA KUNIZUIA”

Upesi, kikundi cha wanafunzi wa Biblia huko San Antonio walianza kufanya maendeleo, na ilivutia kuona jinsi walivyoipenda kweli. Frank anaeleza: “Vijijini, wanawake hasa wana haya sana, na kulingana na mila zao wanajitiisha kwa baba na waume zao. Ni kinyume cha utamaduni wao kuzungumza na watu wasiowajua. Kwa hiyo, ilikuwa vigumu sana kwao kuhubiri nyumba kwa nyumba.”

Priscilian Sho aliyekuwa na miaka 20 wakati huo na ambaye hakuwa amebatizwa, alitaka sana kuwahubiria jirani zake. Pindi moja, Priscilian na shemeji yake Amalia Sho walikuwa wakifanya ziara za kurudia, walipokabili tatizo fulani wasilotazamia.

Priscilian anasema: “Sikuwa nimemwambia baba yangu ninaenda kuhubiri, kwa sababu alikuwa amenikataza na nilimwogopa. Jumapili hiyo asubuhi, tulipokuwa tukihubiri, tulimwona baba yangu mbele ya kanisa lake la Baptisti. Mwanzoni, tulijificha kwenye nyasi kwa kuwa hatukutaka atuone. Lakini nikasema, ‘Wajua nini Amalia, Yehova anatuona. Hatupaswi kumwogopa baba yangu. Tunapaswa kumwogopa Yehova.’”

Baba yake alikasirika sana, lakini Priscilian alikabili tatizo kubwa hata zaidi. Baba yake hakutaka kwa vyovyote Priscilian awe Shahidi wa Yehova. Baada ya kusali kuhusu tatizo hilo hadi mkesha wa kusanyiko ambapo angebatizwa, Priscilian alizungumza na baba yake bila kumwogopa.

Alimwambia, “Kesho ninaenda Belize City.”

“Unaenda kufanya nini?” baba akamuuliza.

“Ninaenda kubatizwa,” Priscilian akamjibu. “Ninaenda kufanya yale ambayo Yehova anataka nifanye. Ninakupenda, lakini ninapaswa kumpenda Yehova pia.”

“Je, kwa kweli unaenda kubatizwa?” akamuuliza kwa hasira.

“Ndiyo,” Priscilian akamjibu. “Matendo 5:29 linasema lazima nimtii Mungu kuliko mwanadamu.”

Baba ya Priscilian aliondoka kwa hasira. Priscilian anasema: “Sikuhisi nikiwa salama hadi pale nilipopanda gari, tayari kwenda kusanyikoni. Sikujua angefanya nini wakati ambapo ningerudi nyumbani baada ya kusanyiko. Lakini nilijua kuwa wakati huo ningekuwa nimebatizwa, kwa hiyo, hata kama angeniua, ningekuwa nimefanya jambo linalofaa.”

Ingawa baba ya Priscilian hakumuumiza aliporudi nyumbani, baadaye alitisha kumuua. Priscilian anasema, “Lakini alitambua kwamba vitisho vyake havingeweza kunizuia, na tangu wakati huo, yeye si mkali sana kwangu.”

MPINZANI AKUBALI KWELI

Kikundi kipya cha wahubiri wenye bidii huko San Antonio kilikuwa kinafanya maendeleo ya kiroho wakati Frank na Alice Cardoza walipopata barua ghafula kutoka kwa baraza la kijiji ambayo iliwaamuru waondoke San Antonio. Hapo awali, baraza hilo lilikuwa limempa Frank kibali cha kukaa kijijini San Antonio baada ya kulipa ada fulani. Sasa, mwanakijiji mmoja mashuhuri alitaka Frank na Alice wafukuzwe kijijini. Kwenye mkutano mmoja wa baraza, wanafunzi watatu wa Biblia wa Frank walimtetea. Kisha, mtu aliyemkodishia Frank na mke wake nyumba akalionya baraza hilo kwamba wakiwafukuza, wao ndio watakaomlipa kodi ya nyumba ambayo Frank na Alice walikuwa wakimlipa. Kisha, Frank mwenyewe akawapa barua kutoka kwa Idara ya Ardhi iliyosema kwamba mtu anayekodi nyumba ya mtu binafsi hawezi kufukuzwa. Mwishowe, baraza hilo liliwaruhusu kukaa San Antonio.

Basilio Ah, ambaye zamani alikuwa alcalde (chifu) na mwanasiasa mashuhuri, ndiye aliyetaka Frank na Alice wafukuzwe. Basilio alitumia mamlaka yake kwa kila njia ili kuwapinga Mashahidi wa Yehova kijijini San Antonio. Walipotaka kiwanja ili kujenga Jumba la Ufalme, aliwaonya, “Hamtajenga Jumba la Ufalme katika kijiji hiki!” Hata hivyo, ndugu walipata kiwanja na wakajenga Jumba la Ufalme dogo lenye kuvutia. Jambo la kushangaza ni kwamba Basilio alikuwa kati ya wale waliokuwapo wakati jumba hilo lilipowekwa wakfu mnamo Desemba 1998. Ni nini kilichokuwa kimetokea?

Wana wawili wa Basilio waliokuwa wameoa, walikuwa na matatizo ya familia. Basilio alikuwa ameliomba kanisa lake mara mbili liwasaidie wanawe, lakini hakupata jibu lolote. Kisha, wanawe wakaanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova. María, mke wa Basilio alianza kutambua kwamba wanawe walikuwa wakifanya mabadiliko na kuwa watu wazuri, na maisha ya familia zao yalikuwa yakiboreka. Kwa hiyo, María akawaomba Mashahidi wajifunze Biblia pamoja naye.

“Nilitaka sana kumjua Yehova Mungu,” María anasema, “na nilimwambia mume wangu tunapaswa kwenda kwenye Jumba la Ufalme ili kujifunza mengi zaidi kumhusu Mungu.” Ingawa Basilio bado aliwachukia Mashahidi na Frank Cardoza, ambaye alimwita “yule mgeni,” alivutiwa sana na mabadiliko ambayo wanawe walifanya kwa kufuata kweli za Biblia katika maisha yao. Basilio aliamua kuwachunguza Mashahidi wa Yehova, na baada ya kuzungumza nao mara kadhaa, akakubali kujifunza Biblia. Alitaka kujifunza Biblia na nani? Si mwingine, ila “yule mgeni,” Frank Cardoza!

Basilio anaeleza: “Mambo niliyojifunza katika Biblia yalibadili maoni yangu. Nilikuwa Mkatoliki kwa miaka 60, na nilikuwa nikiwasha uvumba mbele ya sanamu kanisani. Niliona kuwa mambo niliyokuwa nikijifunza kumhusu Yehova yamo katika kitabu chake mwenyewe, Biblia. Ninaona aibu kuhusu jinsi nilivyomtendea Frank Cardoza, ambaye sasa ni ndugu yangu. Siogopi kusema kwamba nilikosea. Nilikuwa mwenye bidii kuhusiana na mambo niliyofikiri yanafaa kijiji changu na dini yangu. Lakini niliacha kufuata mapokeo ya kuponya kwa nguvu za pepo ambayo yanapendwa na Wamaya wengi vijijini kwetu. Niliacha pia kushiriki katika harakati za kisiasa za Wamaya.” Leo, Basilio na María Ah wanamtumikia Yehova kwa furaha wakiwa wahubiri waliobatizwa.

Watumishi wa Yehova wana upendo, shangwe, na bidii. Katika maeneo ya mbali ya Belize, wahubiri wengi wanatembea kwa muda wa saa tatu au zaidi, wakipanda vilima na kuteremka ili kuwatembelea wenye nyumba, na hawapendi kukosa mikutano. Kwa mfano, jioni moja Andrea Ich alikuwa amepewa mgawo wa kuwa mwenye nyumba katika Shule ya Huduma ya Kitheokrasi. Siku hiyo alikuwa ametembea pamoja na wanawe umbali wa kilomita tatu hadi tano msituni kuchuma maparachichi. Wakati huo nyigu walimuuma mara 23. Hata hivyo, alienda nyumbani, akaipikia familia yake, na pia akaenda mkutanoni na kutimiza mgawo wake. Uso wake ulikuwa umefura kwa sababu ya kuumwa na nyigu, lakini alikuwa mwenye furaha. Inatia moyo kuona kwamba ingawa huenda ndugu na dada zetu Wamaya wakasafiri siku nzima kwa lori au basi ili kuhudhuria makusanyiko, wanafurahi kujiunga na ndugu zao kumwabudu Mungu wa kweli, Yehova.

BELIZE YAKUMBWA NA KIMBUNGA

Katika miaka 115 iliyopita, nchi ya Belize imekumbwa na vimbunga na dhoruba 51. Tangu mwaka wa 1930, vimbunga 12 vimeikumba Belize moja kwa moja au vimepita karibu, na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa na vifo vingi. Kimbunga Hattie kilichokuwa kikali sana, kilikumba Belize asubuhi na mapema Oktoba 31, 1961. Upepo ulivuma kwa mwendo wa kilomita 300 kwa saa, nayo maji ya baharini yakafurika nchi kavu na kusababisha vifo vya mamia ya watu. Belize City, ambalo liko futi moja juu ya usawa wa bahari, lilijaa matope yenye kina cha futi moja. Ripoti moja ya ofisi ya tawi ilisema: “Ndugu wengi [huku Belize City] hawakupatwa na majeraha makubwa, lakini nyumba zao zimeharibika vibaya au zimeharibika kabisa. Wamepoteza nguo zao au zimeharibiwa na maji.

“Matingatinga yanaondoa takataka barabarani na mioto mikubwa inateketeza nyumba zilizoharibika. Hapa kwenye makao [ya wamishonari], maji yenye kina cha futi mbili yalifurika na kusababisha uharibifu mkubwa. Nje, maji yalikuwa yenye kina cha futi tisa, . . . lakini tunafurahi kwamba msingi wa makao ya wamishonari ulijengwa ukiwa juu. . . . Si rahisi kupata chakula . . . , na maiti bado zinakusanywa.”

Siku kumi baadaye, ofisi ya tawi iliripoti: “Hali [huko Dangriga] ni mbaya zaidi kuliko hapa [Belize City]. Watu wanalazimishwa kufanya kazi kwa muda wa saa nane kwa siku ili wapate hati za kununulia vitu. Jeshi linasimamia shughuli zote, na hakuna bidhaa zinazoweza kununuliwa kwa pesa.” Vijana wawili wa kiume walikufa, naye baba yao akavunjika miguu nyumba yao ilipoanguka. Vijana hao walikuwa wahubiri wenye bidii, na mmoja wao aliyekuwa na miaka 12 alijulikana kwa kuwahubiria walimu wake.

Kiini cha kimbunga hicho kilipita katikati ya Belize City na Dangriga, ambako nyumba na mali za ndugu wengi ziliharibiwa kidogo au kabisa. Baada ya kimbunga hicho kupita, gavana alitumia mamlaka yake na kutangaza amri ya kutotembea nje usiku. Pia, aliagiza jeshi la Uingereza lihakikishe amri hiyo imefuatwa na liwapige risasi waporaji. Wanaume, wanawake, au watoto waliovunja amri hiyo walikamatwa na kuzuiliwa usiku kucha.

Ijapokuwa hali zilikuwa zenye vurugu, ndugu walianza kuhubiri na kufanya mikutano haraka iwezekanavyo. Haikuwa rahisi kufanya hivyo kwa kuwa watu wengi walikaa katika mabanda yaliyozungukwa na maji na matope. Lakini watu walihitaji ujumbe wenye kufariji wa habari njema ya Ufalme, na Mashahidi wa Yehova walikuwa tayari kujitolea ili kuwapelekea ujumbe huo.

Maisha yalikuwa magumu sana, lakini upendo na ukarimu wa Mashahidi wa Yehova wa nchi nyingine, uliwatia moyo sana akina ndugu nchini Belize. Masanduku 25 ya nguo na vitu vingine vilitumwa kutoka ofisi nyingine za tawi na kugawiwa Mashahidi na pia jirani zao wasio Mashahidi. Ofisi ya tawi na Jumba la Ufalme ni kati ya majengo machache ambayo hayakuharibiwa na kimbunga hicho. Kwa hiyo, serikali ilipoomba Jumba la Ufalme litumike kama mahali ambapo watu wangeweza kukimbilia wakati wa kimbunga, ndugu walikubali mara moja.b

“BI. PRATT, TAFADHALI TUOMBEE”

Kwa siku tatu mfululizo mnamo Oktoba 2000, wakaaji wa mji wa San Pedro kwenye Kisiwa cha Ambergris walikumbwa na Kimbunga Keith. Kimbunga hicho kiliandamana na mvua nyingi, na upepo ulivuma kwa mwendo wa kilomita 205 kwa saa. Eneo la Ladyville lililo umbali wa kilomita 16 kutoka Belize City, lilifurika kwa maji ya mvua yenye kina cha sentimita 80. Ndugu 42 walikimbilia Jumba la Kusanyiko huko Ladyville. Karibu nyumba zote kwenye Kisiwa cha Caulker ziliharibiwa. Wahubiri 57 kwenye kisiwa cha Ambergris na Caulker walipoteza karibu mali zao zote, na baadhi yao wakapoteza kila kitu. Kwa majuma kadhaa, visiwa vyote viwili havikuwa na umeme, maji, wala huduma za simu. Waziri mkuu alitangaza wilaya ya Belize, Orange Walk, na Corozal, na pia kisiwa cha Ambergris na Caulker kuwa maeneo ya msiba. Amri ya kutotembea usiku ilitekelezwa katika eneo lote lililoathiriwa ili kuzuia uporaji.

Cecilia Pratt, aliyekuwa painia wa pekee huko kisiwani Caulker, alisikia maonyo kuhusu kimbunga hicho, hivyo akapanga kwenye mfuko vitu ambavyo angehitaji iwapo angelazimika kukimbia wakati ambapo kimbunga kingekumba eneo hilo. Siku hiyo, alikuwa amekusanya ripoti za utumishi wa shambani kutoka kwa dada 12, na alikuwa amepanga kuondoka alasiri kwa mashua ili kuzipeleka kwenye ofisi ya tawi barani. Cecilia alifunga ripoti hizo vizuri kwa plastiki na kuziweka kwenye ule mfuko wake. Kama ilivyotarajiwa, usiku Cecilia na baadhi ya dada hao walilazimika kukimbilia shule moja iliyojengwa kwa matofali ya sementi, nao dada wale wengine wakakimbilia kituo fulani cha umma.

Cecilia anasema, “Upepo uling’oa mabati ya darasa tulimokuwa. Ilibidi sote tuchukue vitu vyetu na kukimbilia darasa lingine. Tulihisi kana kwamba jengo zima lilikuwa likitikiswa na upepo, hata ingawa lilikuwa limejengwa kwa matofali. Tulipotazama nje, ilikuwa kana kwamba tumezungukwa na bahari—eneo lote lilikuwa limejaa maji. Sisi akina dada tulikaa pamoja, na kusali kwa bidii. Watu 40 wa dini tofauti-tofauti ambao walikuwa katika darasa hilo waliogopa sana. Baadhi yao walisema, ‘Hii ni kazi ya Mungu.’ Mhubiri mmoja Mkatoliki alinikaribia na kuniambia, ‘Bi. Pratt, tafadhali tuombee.’ Nami nikamjibu, ‘Siwezi kuwaombea. Mimi ni mwanamke, na sina kofia.’ Naye akasema, ‘Basi, unaweza kutumia kofia yangu.’ Sikuwa na hakika kama ningeweza kumwombea kila mtu, lakini nilitaka watu hao wajue kwamba si Yehova aliyeleta kimbunga hicho. Kwa hiyo, nilisali pamoja na wale dada kwa sauti kubwa ili kila mmoja asikie. Baada tu ya kumaliza sala, na kila mmoja kusema ‘Amina,’ upepo ulitulia! Wakati huo kiini cha kimbunga kilikuwa kikipita juu yetu. Yule mhubiri Mkatoliki alisema: ‘Hiyo ni sala nzuri. Mungu wako ndiye wa kweli.’ Baada ya hapo, hawakutaka sisi Mashahidi watano tuondoke hapo, na kwa siku tatu zilizofuata, walitupa chakula na kahawa.

“Hata hivyo, nilikuwa na wasiwasi kuwahusu wale wahubiri wengine. Asubuhi iliyofuata, niliondoka kwenda kuwatafuta upepo ulipotulia. Kulikuwa na miti iliyoanguka na uharibifu kila mahali. Baadhi ya nyumba zilikuwa zimebebwa na upepo umbali wa mita 10 hadi 15 kutoka mahali zilipokuwa awali. Nilienda kwanza kwenye kituo cha umma ambapo niliwapata dada wawili na watoto wao. Nyumba ya dada mmoja ilikuwa imeharibiwa kabisa lakini alikuwa hai.”

Baada ya kimbunga hicho, ilikuwa vigumu kwa ofisi ya tawi kukusanya ripoti za utumishi wa shambani za makutaniko yaliyokuwa yameathiriwa. Lakini ripoti kutoka Kisiwa cha Caulker ndizo zilizokuwa za kwanza kufika. Cecilia alikuwa ameziweka vizuri kwenye ule mfuko wake, na aliwapa akina ndugu waliokuja kuwajulia hali kutoka ofisini.

Katika majuma yaliyofuata, ndugu kwenye visiwa vilivyoathiriwa walipata msaada, nao wafanyakazi wa kujitolea wakawasaidia kusafisha na kukarabati nyumba zao na pia Jumba la Ufalme kwenye Kisiwa cha Ambergris.

Merle Richert, mmoja kati ya wafanyakazi hao wa kujitolea kisiwani Caulker, anasema: “Kwanza tuliandaa mahali pa kulala na kupanga jinsi ambavyo msaada ungegawanywa. Siku iliyofuata, tulianza kukarabati nyumba za wahubiri. Jumapili, sote tulienda kuhubiri asubuhi. Kisha tukatayarisha mahali pa kufanyia mikutano kwenye ua wa nyumba ya dada fulani. Tulitengeneza viti vya mbao kwa ajili ya wasikilizaji na pia jukwaa kwa kutumia kisiki cha zamani cha mnazi. Tulibadili saa za mikutano ili tusivunje ile amri ya kutotembea nje kuanzia saa 2:00 usiku. Watu 43 walisikiliza hotuba ya watu wote na Funzo la Mnara wa Mlinzi.”

KUKUSANYIKA ILI KUFUNZWA NA YEHOVA

Katika miaka ya 1960, hema lilitumiwa kwa ajili ya makusanyiko yaliyofanywa sehemu mbalimbali nchini. Lakini, kupiga hema kubwa ni kazi ngumu inayochukua siku nyingi. Santiago Sosa anaeleza: “Tulikuwa tukianza kazi mwanzoni mwa juma. Kazi hiyo ilihusisha kupiga hema, kubeba benchi kutoka kwenye Jumba la Ufalme, na kuomba viti. Wakati huo chakula kilikuwa kikiandaliwa kusanyikoni, kwa hiyo tuliomba vyombo vya kupikia na mara nyingi tulikesha usiku kucha ili kupika na kumaliza kazi. Nyakati nyingine tungepanga kila kitu vizuri, lakini upepo mkali ungevuma usiku na kuviangusha vyote. Siku iliyofuata, tungelazimika kupanga vitu hivyo tena. Lakini hakuna aliyelalamika.”

Jeanne Thompson anakumbuka kusanyiko lililofanywa mashambani kati ya Belize City na Orange Walk. Ndugu walihitaji kufyeka kichaka kilichokuwa karibu na Jumba la Ufalme kabla ya kupiga hema na kupanga benchi. Jeanne anasema, “Kulinyesha siku zote za kusanyiko la wilaya, na maji yakafurika kwenye hema. Kwa hiyo, tulipoketi tuliweka miguu yetu juu ya benchi iliyokuwa mbele yetu. Hatukujua kwamba eneo hilo lilikuwa na nyoka wengi wenye sumu. Hivyo, mvua hiyo ilitusaidia kwa sababu tulilazimika kukaa hemani na karibu na Jumba la Ufalme. Ingekuwa hatari kutembea vichakani.”

Katika miaka ya 1970 makusanyiko yalifanywa katika kisiwa kidogo kinachoitwa Bird’s Isle, umbali wa mita 120 kutoka Belize City. Mmiliki wa kisiwa hicho alikuwa amejenga ukumbi wenye umeme, maji, na vyoo, ambao alikusudia kuutumia kwa ajili ya burudani. Akina ndugu walijenga daraja la mbao lililounganisha kisiwa hicho na bara, na hivyo kuandaa mahali patulivu na penye amani kwa ajili ya makusanyiko.

Mnamo Machi 1983, kiwanja kilikodiwa kutoka kwa serikali ili kujenga Jumba la Kusanyiko huko Ladyville. Mwanzoni, akina ndugu walijenga kibanda cha muda kwa ajili ya makusanyiko na matukio mengine muhimu. Kisha, mwaka wa 1988, jengo fulani la chuma cha pua likanunuliwa nchini Guatemala na kuletwa kwenye kiwanja hicho cha Ladyville, ili litumiwe kama Jumba la Kusanyiko la kudumu.

WATU WANAOONGEA KICHINA WAKUBALI KWELI

Tangu miaka ya 1920, wahamiaji Wachina wamekuwa wakiishi Belize, na wengi wao wanafurahia kusoma vitabu vyetu katika lugha yao. Kwa mfano, Roberta Gonzalez anaeleza: “Nilitaka kumhubiria mwanamke mmoja wa Taiwan aliyekuwa na duka la mikate, lakini nilijua hakupenda mambo ya dini na sikuzote alikuwa na shughuli nyingi sana. Pia nilijua kwamba alikuwa na vijana wawili. Kwa hiyo, siku moja nilipokuwa katika duka lake, nilimpa kitabu Vijana Huuliza katika Kichina na kumwomba maoni yake kukihusu. Siku kadhaa baadaye, nilipopita kwa gari karibu na duka hilo, nilimwona mwanamke huyo akinipungia mkono kwa bidii. Niliposimamisha gari, alinieleza kwa shauku kwamba tangu nimwachie kitabu hicho, amekuwa akiningoja nirudi. Alisema kwamba vijana wengi katika familia za Wataiwan wanakuwa na matatizo mengi baada ya kuhamia Belize. Alionelea kwamba wote wanahitaji kusoma kitabu Vijana Huuliza. Alimwomba mwanawe ahesabu familia zote za Wataiwan mjini ambazo zilikuwa na vijana, kisha akaomba vitabu 16 kwa sababu alitaka kuipa kila familia kitabu kimoja kama zawadi.”

Mnamo Oktoba 2000, ofisi ya tawi iliandaa darasa la miezi mitatu ili mapainia na wahubiri waliokuwa tayari kuwahubiria Wachina wajifunze lugha ya Mandarin. Matokeo yakawa nini? Kikundi cha lugha ya Kichina chenye mapainia kadhaa kilianzishwa, na sasa kimekuwa kutaniko. Ingawa kuna upinzani mkali, Wachina fulani wamekubali habari njema na wanafurahia upendo wanaoonyeshwa kutanikoni.

Kwa mfano, Monje Chen alikubali funzo la Biblia mwaka wa 2006. Mwanzoni, familia yake ilimuunga mkono, lakini muda si muda wakaanza kumdhihaki na kumpinga Monje. Kwa ghafula, familia yake iliuza mali zao zote, hata duka ambalo Monje alisimamia, na kumpa muda wa saa moja aamue kuacha dini yake mpya na kuhama pamoja nao kwenda nchi nyingine. Alikataa kukana imani yake mpya, kwa hiyo, familia yake ikahama na kumwacha bila chochote. Monje alihamia kwa ndugu fulani na akaendelea kujifunza Biblia na kuhudhuria mikutano kwa ukawaida. Anasema: “Nilisitawisha uhusiano wa karibu pamoja na Yehova, naye alinitunza. Kujifunza Biblia na kutafakari kumenisaidia. Akina ndugu pia wamenisaidia kwa kunitia moyo.”

Monje alibatizwa Novemba 2008, na mtazamo wa familia yake umekuwa mzuri baada ya kuona jinsi ambavyo mwenendo na usemi wake umebadilika. Monje anaongeza: “Kumtii Yehova hakukunifanya maskini, bali kuliniletea furaha. Yehova hakuniacha, bali aliniruhusu niishi kati ya ndugu wenye umoja na upendo.”

OFISI YA TAWI YA MEXICO YASIMAMIA KAZI NCHINI BELIZE

Baada ya Baraza Linaloongoza na Halmashauri ya Tawi ya Belize na Mexico kuchunguza kwa makini mahitaji yanayohusiana na kazi ya Ufalme, baraza hilo liliamua kwamba ofisi ya tawi ya Mexico isimamie kazi nchini Belize. Ofisi hiyo ilianza kusimamia kazi nchini humo Januari 1, 2001, na mpango huo umewanufaisha na kuwafurahisha akina ndugu nchini Belize.

Tangu wakati huo, ofisi ya tawi ya Mexico imesaidia kusimamia ujenzi wa Majumba ya Ufalme kadhaa nchini Belize. Jumba la Ufalme lenye majumba mawili ya kukutania liliwekwa wakfu huko Belize City, Machi 16, 2002. Siku iliyofuata kulikuwa na programu ya kuweka wakfu makao mapya na maridadi ya wamishonari, na pia Jumba la Kusanyiko lililofanyiwa ukarabati huko Ladyville. Wengi ambao walikuwa wamemtumikia Yehova kwa uaminifu kwa zaidi ya miaka 50 au 60 walikuwa miongoni mwa wale waliofurahia hotuba ya kuyaweka wakfu majengo hayo. Hotuba hiyo ilitolewa na Gerrit Lösch wa Baraza Linaloongoza. Kumekuwa na maendeleo mazuri tangu Kikundi cha Ujenzi wa Majumba ya Ufalme kianzishwe, nacho kimesaidia kujenga Majumba ya Ufalme 20 kotekote nchini.

Mwaka wa 2007, mapainia 325 walikuja nchini Belize kutoka Mexico ili kuhubiri katika maeneo yasiyohubiriwa kwa ukawaida. Mapainia hao walichochea sana roho ya kuhubiri nchini Belize. Kwa sababu hiyo, idadi ya mapainia nchini humo imeongezeka sana.

Tofauti na viongozi wa dini ambao huomba kila mwaka ili Belize isikumbwe na vimbunga, Mashahidi wa Yehova walipewa mwongozo unaofaa kuhusu hatua za kuchukuliwa wakati wa dharura, kabla ya msimu wa kimbunga wa mwaka wa 2007. Walithamini mwongozo huo kama nini wakati Belize ilipokumbwa na Kimbunga Dean mwezi wa Agosti. Ndugu waliokuwa hatarini walihamishwa na kupelekwa katika nyumba za akina ndugu waliokuwa katika maeneo salama. Baada ya kimbunga hicho kupita, Mashahidi kutoka maeneo yote nchini walisaidia kukarabati nyumba na Majumba ya Ufalme. Kwa sababu hiyo, kituo kimoja cha redio kiliwasifu Mashahidi wa Yehova na kusema kwamba wao ni mfano wa kuigwa.

WATU WA MATAIFA YOTE WAUNGANA

Yehova amebariki kazi nchini Belize na sasa kuna wahubiri 1,800, na kila mhubiri anahitaji kuwahubiria watu 149. Kuna uwezekano mkubwa wa ongezeko nchini Belize, kwa kuwa mtu mmoja kati ya kila watu 39 anahudhuria Ukumbusho!

Kazi ya kufanya wanafunzi nchini Belize katika miaka 80 iliyopita imetokeza mchanganyiko wa watu mbalimbali wenye sifa nzuri za Kikristo, ambao wameunganishwa na “lugha safi,” yaani, kweli kumhusu Mungu na makusudi yake. Mashahidi wa Yehova nchini Belize wanatumia vizuri lugha safi ili kutoa ushahidi unaomtukuza Yehova, Mungu wetu mwenye upendo. Wanafanya hivyo “bega kwa bega” pamoja na ndugu na dada zao duniani kote.—Sef. 3:9.

[Maelezo ya Chini]

a Ijapokuwa Belize iliitwa Honduras ya Uingereza mpaka mwaka wa 1973, jina Belize litatumiwa katika masimulizi haya yote, isipokuwa iwe lazima kutumia lile jina la zamani kwa sababu ya muktadha.

b Kwa sababu ya kimbunga hicho, jiji la Belmopan lililo mbali na pwani, lilifanywa kuwa jiji kuu badala ya Belize City.

[Blabu katika ukurasa wa 224]

“Dereva wa lori aliniambia kwamba Wakristo wa kweli huhubiri nyumba kwa nyumba”

[Blabu katika ukurasa wa 234]

“Hatupaswi kumwogopa baba yangu. Tunapaswa kumwogopa Yehova”

[Sanduku katika ukurasa wa 208]

Maelezo Mafupi Kuhusu Belize

Nchi

Sehemu ya pwani ni tambarare, lakini nchi imeinuka upande wa kusini kuelekea Milima ya Maya. Misituni kuna chui wa Amerika, puma, tumbili weusi wenye mlio mkali, nguruwe wa mwituni, mijusi wakubwa wa kijani kibichi, mamba, na aina 60 hivi za nyoka. Kuna nyoka fulani mwenye sumu kali sana anayeitwa fer-de-lance, ambaye wenyeji wanapenda kumwita yellow-jaw tommygoff. Pia, kuna aina 600 hivi za ndege kama vile macaw mwekundu aliye katika hatari ya kutoweka, na yule ndege maridadi anayeitwa keel-billed toucan. Baharini kuna matumbawe na pia viumbe wengi kama vile sifongo, nguva, samaki kasuku, barakuda, na papa-nyangumi.

Watu

Wakaaji ni wa makabila na asili mbalimbali kama vile Wamaya (wa kabila la Wakekchi, Wamopan, na Wayucatec), Wakrioli (mchanganyiko wa Waafrika na Wazungu), Wamestizo (mchanganyiko wa Wahispania na Wamaya), Wagarifuna (mchanganyiko wa Waafrika na Wakaribu), Wahindi wa Mashariki, Walebanoni, Wachina, na Wazungu kama vile Wajerumani na Waholanzi, walio wafuasi wa kanisa la Menno.

Lugha

Kiingereza ndiyo lugha rasmi, lakini watu wanaongea pia lugha ya Krioli ya Belize, Kihispania, Kigarifuna, Kikekchi, Kimaya, Kijerumani, na Kichina cha Mandarin.

Kazi

Watu wengi hufanya kazi katika mashamba ya miwa au matunda, au katika makampuni yanayouza mazao hayo nje ya nchi. Wengi pia hufanya biashara ya uvuvi na utalii.

Chakula

Wakaaji ni wa tamaduni nyingi tofauti, hivyo, kuna vyakula mbalimbali vitamu. Chakula cha kawaida kinachopendwa ni mchanganyiko wa wali na maharagwe yaliyochemshwa pamoja katika maziwa ya nazi. Mara nyingi kinaandaliwa pamoja na samaki, kuku, au nyama ya ng’ombe iliyokaangwa au kuchemshwa, na ndizi mbivu zilizokaangwa. Wengi wanapenda pia vyakula vitamu vya baharini.

Hali ya hewa

Belize ni nchi ya Amerika ya Kati, kwenye pwani ya Bahari ya Karibea. Kwa hiyo, ina hali ya hewa yenye joto na unyevu mwingi, na mara nyingi hukumbwa na vimbunga.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 215]

Wagarifuna Wakubali Kweli

BEVERLY ANN FLORES

ALIZALIWA 1961

ALIBATIZWA 1993

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Yeye ni Mgarifuna aliyekubali kweli na sasa anawasaidia Wagarifuna wenzake kumjua Yehova.

◼ WAGARIFUNA ni wazao wa watumwa waliofunga ndoa na Wakaribu wenyeji, mapema katika miaka ya 1600. Lugha yao ya Kigarifuna ni aina ya Kiarawaki, ambacho kina maneno ya Kifaransa na Kiswahili.

Dini ya Wagarifuna ni mchanganyiko wa mapokeo na desturi za Waafrika, Wahindi wenyeji wa Amerika, na hasa mapokeo ya Kanisa Katoliki. Kwa mfano, sherehe ya dugu inahusisha desturi zenye madoido za kuwatuliza mababu waliokufa kwa kuwatolea vinywaji na chakula. Beverly anasema: “Mama yangu hakuamini sherehe ya dugu. Hakuamini kwamba Mungu angeweza kukubali chakula hicho chote kifunikwe ardhini. Alipenda kusema, ‘Chakula kinaandaliwa ili watu wale! Na kama wafu ni wapendwa wetu, mbona warudi kutuumiza?’”

Beverly anaeleza mambo yaliyotukia alipojifunza kweli. “Nilitamani kwenda Dangriga kuwahubiria watu wetu. Nilijua kwamba Wagarifuna wengi wangekuwa tayari kumsikiliza mtu wa kabila lao kuliko mtu mwingine. Wengi wanasikiliza ninapozungumza Kigarifuna, na watu kadhaa wameanza kushirikiana na kutaniko. Wametambua kwamba hawatauawa na pepo wakiacha mila zisizopatana na Maandiko.”

[Saduku/Picha katika ukurasa wa 218]

“Yehova Alituandalia Mahitaji Sikuzote”

LILLY MILLER

ALIZALIWA 1928

ALIBATIZWA 1960

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Aliwalea watoto sita peke yake, na amekuwa mtumishi wa wakati wote kwa miaka 47.

◼ LILLY anasimulia kwa sauti nyororo: “Mwaka wa 1959, Amybelle Allen alizungumza nami kuhusu Biblia. Kanisani tulikuwa tumeonywa kuwahusu ‘manabii wa uwongo’ waliokuwa wakienda nyumba kwa nyumba. Nilikubali kujifunza kwa kutumia Biblia peke yake, nikakubali kweli, na nikabatizwa mwaka uliofuata.

“Mwanzoni niliona ni vigumu kuhubiri. Mikono yangu ilitetemeka sana hivi kwamba karibu nishindwe kushika Biblia yangu. Lakini tamaa yangu ya kuwaeleza wengine yale ambayo nilikuwa nikijifunza ‘ikawa kama moto unaowaka ambao ulikuwa umefungiwa ndani ya mifupa yangu,’ kama Yeremia alivyosema, na ilinibidi kuhubiri, watu wasikilize wasisikilize.”—Yer. 20:9.

Lilly alifaulu jinsi gani kuwalea watoto sita akiwa peke yake huku akiendelea na utumishi wa wakati wote? Lilly anasema: “Nilitoa sala kwa Yehova, na yeye akaniwezesha kuendelea. Mara tatu kila juma niliamka saa tisa na nusu usiku ili kutengeneza biskuti. Binti zangu walinisaidia kuzioka katika jiko la kuni, na watu walipanga mstari ili kuzinunua zikiwa bado moto. Baada ya kuuza biskuti zote, watoto wangu walienda shuleni nami nikaenda kuhubiri. Yehova alituandalia mahitaji sikuzote.”

Lilly amekuwa painia huko Corozal tangu mwaka wa 1969. Mwana wake mkubwa na binti wawili wameanza utumishi wa wakati wote, na amewasaidia watu 69 kufikia ubatizo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 227, 228]

Safari za Mashambani—Kuhubiri Katika Msitu wa Mvua

“Mnamo Machi 1991, ndugu na dada 23 kutoka nchini kote walikusanyika Punta Gorda ili washiriki katika safari ya siku kumi ya kuhubiri katika maeneo ya mbali ya msitu wa mvua,” anaeleza Martha Simons. “Tulibeba nguo, blanketi, bembea za kulalia, na vitabu vya Kiingereza, Kihispania, na Kikekchi. Pia tulibeba chakula cha kutosha kilichotia ndani keki 200.

“Asubuhi iliyofuata tulianza safari katika bahari yenye mawimbi na tulisafiri kwa mtumbwi uliotengenezwa kwa mti mkubwa wa msufi. Tulipofika kijijini Crique Sarco, tulipakua mizigo yetu na kupiga kambi. Ndugu walifunga bembea za kulalia, huku dada wakipika chakula tunachopenda sana—mchuzi wa mkia wa nguruwe. Mchuzi huo ni mchanganyiko wa mhogo, viazi vikuu, ndizi mbichi, nazi, mayai yaliyochemshwa, na mkia wa nguruwe. Habari zilienea kwamba tulikuwa tumefika, na muda si muda Wakekchi wengi kutoka kijijini wakaja kutusalimu. Kwa njia hiyo, tuliweza kuwahubiria watu wote kijijini kwa muda wa saa mbili. Usiku huo, ndugu walilala kwenye bembea chini ya kituo cha polisi kilichojengwa juu ya nguzo, nao akina dada wakalala kwenye cabildo, nyumba iliyoezekwa kwa nyasi ambapo wazee wa kijiji wanakutana.

“Siku iliyofuata tulipakia mizigo yetu tena kwenye mtumbwi na kusafiri kuelekea upande wa juu wa mto. Sehemu fulani za mto huo zilijaa mizizi ya mkoko iliyofanya maeneo hayo yawe yenye giza na yenye kuogopesha. Baada ya muda wa nusu saa hivi, tulishuka kwenye mtumbwi na kutembea kwa miguu msituni kwa muda wa saa moja na nusu hadi kijiji cha Sundaywood. Watu wa kijiji hicho ni wadogo na wana ngozi yenye rangi ya maji ya kunde na nywele nyeusi zilizonyooka. Wengi wao hawakuwa na viatu, na wanawake walivaa shanga na sketi zinazovaliwa na wenyeji. Nyumba zao zilizoezekwa kwa nyasi zilikuwa na sakafu ya udongo, na hazikuwa na migawanyo ndani wala vifaa kama viti, meza, na kadhalika, ila tu bembea za kulalia. Kando ya nyumba hizo, palikuwa na sehemu ya kupikia iliyotumiwa na watu wote.

“Watu hao walikuwa wenye urafiki sana, na wengi walipendezwa na ujumbe wetu. Walivutiwa hasa tulipowaonyesha vitabu vya lugha yao ya Kikekchi na tulipowasomea maandiko katika Biblia zetu za Kikekchi.

“Siku iliyofuata, tuliamshwa na jogoo, ndege wa mwituni, na tumbili wenye mlio mkali. Baada ya kufurahia kiamsha-kinywa, tuliwarudia watu wote waliopendezwa tulipowahubiria siku iliyotangulia. Tulianzisha mafunzo kadhaa ya Biblia na tukawatia moyo wote waendelee kujifunza peke yao hadi turudi kujifunza nao mwaka ujao. Siku zilizofuata tuliingia ndani kabisa msituni ili kufikia vijiji vya mbali, na wote waliopendezwa tuliwatia moyo pia waendelee kujifunza peke yao hadi turudi.

“Baada ya kufurahia safari yetu ya siku kumi msituni, tulifikiria safari yetu ndefu, vijiji vingi tulivyotembelea, na wote tuliozungumza nao. Tulimwomba Yehova alinde mbegu za ukweli tulizopanda hadi turudi mwaka ujao. Miguu yetu iliuma, tulikuwa tumechoka; lakini mioyo yetu ilijaa shukrani kwa Yehova kwa sababu ya shangwe tuliyopata kwa kushiriki katika safari ya mashambani ya mwaka huu.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 235, 236]

Wamaya Wanaompenda Yehova

JORGE NA NICOLAS SHO (PAMOJA NA DADA YAO, PRISCILIAN)

WALIZALIWA 1969 na 1971

WALIBATIZWA 1997

MALEZI Kupatana na mila za Wamaya, watoto wanapaswa kuwatii wazazi wao kikamili, hata kama watoto hao ni watu wazima waliofunga ndoa.

◼ NICOLAS na Jorge walipomjua na kumpenda Yehova, baba yao alipinga vikali utendaji wao wa Kikristo.

Nicolas anasema, “Nilimweleza baba yangu kwamba nilikuwa nikijifunza mambo yenye faida, lakini kwa kuwa alikuwa mfuasi wa Kanisa la Baptisti hakufurahia mambo niliyomweleza. Niliacha kujifunza Biblia kwa mara kadhaa kwa sababu sikutaka kumuumiza. Lakini nilijua kwamba kwa kunywa pombe pamoja na baba yangu sikuwa nikiwawekea watoto wangu mfano mzuri. Mke na watoto wangu walihuzunika sana hivi kwamba hawakuwa wanatabasamu kamwe.

“Nilipoanza kujifunza Biblia na kuhudhuria mikutano ya Kikristo kwa ukawaida, kweli niliyojifunza ilinisaidia kuacha mwenendo mbaya. Nilifanya kazi kwa bidii na nilitumia mapato yangu kuisaidia familia yangu. Sasa, mimi na familia yangu tunamtumikia Yehova kwa bidii, na kuna furaha na shangwe nyumbani kwetu.”

Kisa cha Jorge kilikuwa sawa na cha Nicolas. Alikuwa na matatizo ya familia kwa sababu alikunywa pombe na kutumia lugha chafu, na hakuwa anapatikana nyumbani mwishoni mwa juma. Lakini alipojifunza Biblia, mwenendo wake ulibadilika sana.

Jorge anaeleza, “Nilipofanya maendeleo, baba alizidi kunipinga. Alituita manabii wa uwongo. Alitisha kutushambulia kwa upanga wake mara kadhaa. Ndugu Cardoza, ambaye alinifundisha Biblia, alikuwa amejitahidi kututayarisha mapema kuhusu upinzani. Alituuliza: ‘Tuseme baba yenu atawaambia mwondoke nyumbani, mtafanya nini?’ Nilimjibu, ‘Baba yangu ananipenda na hawezi kufanya hivyo.’ Lakini inasikitisha kwamba hivyo ndivyo alivyofanya.

“Hata hivyo,” Jorge anaendelea kusema, “nilipenda mambo niliyokuwa nikijifunza, na maisha yangu yalikuwa yanaboreka. Familia yangu ilifaidika kwa sababu nilikuwa nikisitawisha sifa za Kikristo. Tuliheshimiana na kufurahia kuwa pamoja. Leo, kazi ya kuhubiri inaniletea shangwe nyingi, na kwa msaada wa Yehova, mimi ni painia wa kawaida.”

[Picha]

Frank Cardoza alimhubiria Jorge

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 238, 239]

Shangwe ya Kutumika Katika Eneo Lenye Uhitaji Mkubwa

Ni hatua kubwa kuhamia nchi yenye uhitaji mkubwa wa watangazaji wa Ufalme. Lakini mtu anahitaji kujitahidi sana na kujidhabihu ili kuendelea kukaa katika nchi aliyohamia. Wengi wa ndugu na dada zetu wamekabili hali hizo kwa shangwe na ustahimilivu.

Kwa mfano, Arthur na Roberta Gonzalez na mwana wao mwenye umri wa miaka mitatu, Dalton, walihamia Belize kutoka Marekani mwaka wa 1989. Roberta anasema, “Jambo gumu zaidi lilikuwa kuacha kazi nzuri yenye mshahara mnono na kuja kuishi katika nchi ambamo watu wengi hawana kazi.”

“Naam,” Arthur naye anasema, “ni lazima umtegemee Yehova. Ninaposoma katika Biblia kumhusu Abrahamu, ninashangaa kwamba aliacha nyumba yake, watu wa jamaa, na hali alizozoea. Lakini Yehova alimtunza. Sisi tulikabili tatizo la kujifunza lugha ya Krioli ya Belize. Lakini tulimtegemea Yehova, naye alitutunza.”

Frank na Alice Cardoza walihamia Belize kutoka California mwaka wa 1991 ili wafanye utumishi wa painia. Frank anasema, “Niliposoma kitabu cha Matendo, nilitaka kuwa mmishonari. Lakini kwa kuwa tuna watoto wanne, nilijua hatungestahili kuhudhuria Shule ya Gileadi. Kwa hiyo, binti yetu mdogo alipomaliza shule, tulipata nafasi ya kuhamia nchi nyingine. Tuliposoma kwenye Mnara wa Mlinzi kuhusu Belize, tuliamua kuhamia huku.”

Alice anasema, “Nilikubali kuhamia Belize kwa miaka mitatu tu, lakini sasa tumeishi hapa kwa miaka 18, na ninafurahia kuwa hapa!”

Frank anaongeza, “Tunawapenda watu na tunapenda kufanya kazi, kwa hiyo ni rahisi kwetu kuwa na uhusiano wa karibu na wale wanaompenda Yehova. Kuanzisha mafunzo mengi sana ya Biblia na kuona watu wakikubali kweli, kumefanya tufurahie sana miaka ambayo tumekaa Belize. Hatuna nia ya kuacha pendeleo hili la pekee.”

Carl na Martha Simons walihamia Belize kutoka Texas mwaka wa 1988. Martha anaeleza: “Tulipohama, mtoto wetu wa kwanza alikuwa na miaka kumi na wa pili alikuwa na miaka minane. Nchini Belize tulihubiri mchana kutwa pamoja na kutaniko katika vijiji vya mashambani. Pia tulishirikiana na kutaniko kujenga Jumba la Kusanyiko, na wakati wa makusanyiko, nyumba yetu ilijaa ndugu na dada waliokuja kukaa nasi. Tunafurahi kwamba tuliweza kuwalea watoto wetu hapa, kwa kuwa walishirikiana na mapainia wa pekee na wamishonari. Naam, nyakati nyingine tulitaka kupanda ndege na kurudi nyumbani, hasa tulipokosa umeme, maji ya bomba, betri, au huduma za simu. Hata hivyo, kama tungeombwa kufanya uamuzi tena, bila shaka hatungebadili uamuzi wetu wa kuhamia Belize, licha ya panda shuka nyingi ambazo tumekabili nchini humu. Maisha yetu yameboreka kwa sababu ya kutumika katika eneo lenye uhitaji mkubwa.”

[Picha]

Kushoto hadi kulia: Dalton, Roberta, Arthur, na mama yake, Martha Gonzalez

Alice na Frank Cardoza

Carl na Martha Simons

[Sanduku katika ukurasa wa 250]

“Mungu Anatujali!”

ALEJANDRO NA REBECCA (BECKY) LACAYO

WALIZALIWA 1950 na 1949

WALIBATIZWA 1966 na 1959

MAELEZO MAFUPI KUWAHUSU Baada ya kumaliza masomo katika Shule ya Gileadi mwaka wa 1972, walitumika wakiwa wamishonari nchini El Salvador, Belize, Nikaragua, Mexico, na Honduras. Sasa wanaishi Marekani ambapo ndugu ni mwangalizi wa mzunguko, lakini hawajasahau kamwe wakati walipofanya kazi ya kutoa msaada nchini Belize.

◼ JUMATATU, Oktoba 2, 2000, Becky aliandika, “Tuko katikati ya Kimbunga Keith. Kumenyesha mfululizo kwa siku mbili na nusu hivi.”

Siku iliyofuata, baada ya mvua na upepo kutulia, Alejandro na painia wa pekee Donald Niebrugge walipeleka msaada kwenye Kisiwa cha Ambergris. Waliungana na wazee wawili kisiwani Ambergris na kuwatembelea wahubiri wote wa makutaniko mawili ya kisiwa hicho ili kuwajulia hali.

Becky anasema, “Siku ya Jumatano (Siku ya 3), ndugu kutoka sehemu mbalimbali nchini walileta kwenye ofisi ya tawi chakula, maji, na nguo kwa ajili ya ndugu wa visiwa vilivyoathiriwa. Muda si muda, sehemu ya mapokezi na maktaba ilijaa vitu walivyoleta.”

Wakati huohuo, Alejandro na ndugu wengine watatu walipeleka msaada kisiwani Caulker. Walisali pamoja na akina ndugu kisiwani humo na kuwatia moyo. Mashahidi na pia watu wasio Mashahidi waliguswa moyo sana na upendo na hangaiko la ndugu hao waliowatembelea. Mwanamke mmoja alilalamika, “Nimekuwa nikitoa michango kanisani kwa miaka mingi, na hakuna mtu hata mmoja wa kanisa langu ambaye amekuja kunijulia hali.”

Dada mmoja alisema hivi huku akilia kwa furaha: “Watazame watu wengine, na ututazame! Mungu anatujali!”

[Picha katika ukurasa wa 244, 245]

MFUATANO WA MATUKIO—Belize

1923 James Gordon ahubiri Bomba.

1930

1933 Freida Johnson ahubiri Belize City.

1934 Thaddius Hodgeson aongoza mikutano katika duka lake la mikate.

1940

1941 Wahubiri wa kwanza wabatizwa Belize City.

1945 Wamishonari wa kwanza wafika.

1946 Ofisi ya tawi yaanzishwa.

1950

1957 Wamishonari wazuiwa wasiingie nchini.

1959 Jumba la Ufalme, ofisi ya tawi, na makao ya wamishonari yajengwa.

1960

1961 Wamishonari waruhusiwa tena kuingia nchini.

1961 Kimbunga Hattie chakumba Belize.

1971 Kisiwa kinachoitwa Bird’s Isle chatumiwa kwa ajili ya makusanyiko kwa mara ya kwanza.

1980

1988 Jumba la Kusanyiko lajengwa huko Ladyville.

1990

2000

2000 Kimbunga Keith chakumba Belize.

2001 Ofisi ya tawi ya Mexico yasimamia kazi nchini Belize.

2002 Jumba la Ufalme lenye majumba mawili (kushoto), Jumba la Kusanyiko lililofanyiwa ukarabati, na makao ya wamishonari yawekwa wakfu.

2010

[Grafu]

(See publication)

Jumla ya Wahubiri

Jumla ya Mapainia

1,800

1,200

400

1930 1940 1950 1960 1980 1990 2000 2010

[Picha katika ukurasa wa 244]

Mashua iliyojaa akina ndugu wakienda kusanyikoni

[Ramani katika ukurasa wa 209]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MEXICO

GUATEMALA

Melchor de Mencos

BAHARI YA KARIBEA

BELIZE

Kisiwa cha Ambergris

San Pedro

Kisiwa cha Caulker

WILAYA YA COROZAL

Corozal

WILAYA YA ORANGE WALK

Orange Walk

August Pine Ridge

WILAYA YA BELIZE

Bomba

Santana

Crooked Tree

Black Creek

Ladyville

Belize City

WILAYA YA CAYO

BELMOPAN

Benque Viejo

WILAYA YA STANN CREEK

Bonde la Stann Creek

Dangriga

Hopkins

Seine Bight

WILAYA YA TOLEDO

Mango Creek

Placencia

Monkey River Town

Punta Negra

San Antonio

Punta Gorda

Sundaywood

Barranco

Crique Sarco

Mto Belize

MIL. YA MAYA

[Picha katika ukurasa wa 200]

[Picha katika ukurasa wa 206]

Alphonsena Robateau na Amybelle Allen pamoja na mapainia wa pekee watatu

[Picha katika ukurasa wa 207]

Herman na Derrine Lightburn pamoja na mwana wao, Stephen

[Picha katika ukurasa wa 210]

Mashahidi wakiwa na gari la kukokotwa lenye kipaza sauti, Belize City, miaka ya 1940; (1) Thaddius Hodgeson, (2) George Longsworth

[Picha katika ukurasa wa 213]

Elmer Ihrig alihubiri kwenye maeneo ya mbali

[Picha katika ukurasa wa 214]

Charles Heyen aliwatia ndugu moyo wafanye mikutano kwa ukawaida

[Picha katika ukurasa wa 221]

Ofisi ya tawi, makao ya wamishonari, na Jumba la Ufalme huko Belize City

[Picha katika ukurasa wa 223]

Kusanyiko la kwanza la mzunguko katika Kihispania lilifanywa kwenye Jumba la Ufalme la Orange Walk, 1968

[Picha katika ukurasa wa 229]

Mapainia wa pekee Marcial na Manuela Kay

[Picha katika ukurasa wa 230]

Kijiji cha Wamaya, wilayani Toledo

[Picha katika ukurasa wa 240]

María na Basilio Ah

[Picha katika ukurasa wa 246]

Cecilia Pratt

[Picha katika ukurasa wa 249]

Ndugu wakiwa wameketi katika hema kwenye kusanyiko la mzunguko, Punta Gorda, miaka ya 1960

[Picha katika ukurasa wa 251]

Becky na Alejandro Lacayo

[Picha katika ukurasa wa 252, 253]

Jengo la chuma cha pua lililo hapa chini sasa linatumiwa kama Jumba la Kusanyiko (kulia)

[Picha katika ukurasa wa 253]

Jumba la Kusanyiko lililofanyiwa ukarabati

[Picha katika ukurasa wa 254]

Ndugu na dada kwenye Jumba la Ufalme lenye majumba mawili, wakati lililopokuwa likijengwa huko Belize City

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki