Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • mwbr20 Juni kur. 1-3
  • Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha
  • Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha—2020
  • Vichwa vidogo
  • JUNI 1-7
  • JUNI 8-14
  • JUNI 15-21
  • JUNI 29–JULAI 5
Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha—2020
mwbr20 Juni kur. 1-3

Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha

JUNI 1-7

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MWANZO 44-45

Kutafuta Hazina za Kiroho

it-2 813

Kurarua Mavazi

Ilikuwa njia ya kawaida ya kuonyesha huzuni kati ya Wayahudi na watu wengine wa maeneo ya Asia, hasa waliposikia kuhusu kifo cha mtu wa karibu wa ukoo. Katika visa vingi, kurarua mavazi kulihusisha kurarua sehemu ya mbele kiasi cha kutosha kuonyesha kifua, na si kurarua vazi lote hivi kwamba lisiweze kuvaliwa tena.

Mara ya kwanza ambapo zoea hilo linaonekana katika Biblia ni wakati Rubeni, mwana wa kwanza wa Yakobo, aliporudi na kumkosa Yosefu ndani ya shimo la maji. Alirarua mavazi yake na kusema: “Mtoto amepotea! Sasa mimi—nitafanya nini?” Akiwa mwana wa kwanza, Rubeni ndiye aliyekuwa na wajibu wa kumtunza ndugu yake mdogo. Yakobo baba yake alipoambiwa kuhusu kifo cha mwana wake alirarua mavazi yake na kuvaa nguo za magunia ili kuomboleza. (Mwa 37:29, 30, 34) Na ndugu wa kambo wa Yosefu walipokuwa nchini Misri walionyesha huzuni yao kwa kurarua mavazi yao wakati ambapo Benjamini alishutumiwa kuwa mwizi.—Mwa 44:13.

JUNI 8-14

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MWANZO 46-47

“Waokolewa Kutokana na Njaa Kali”

w87 5/1 15 ¶2

Kuhifadhi Uhai Katika Wakati wa Njaa

2 Miaka ile saba ya utele ikaisha, na njaa ikaanza sawa na vile Yehova alivyokuwa ametabiri—njaa, si katika Misri tu, bali “juu ya uso wa dunia.” Wakati watu wenye kukumbwa na njaa katika Misri walipoanza kumlilia Farao awape mkate, Farao aliwaambia: “Nendeni kwa Yusufu. Lo lote awaambialo yeye, ndilo mtakalopasa kufanya.” Yusufu aliuzia Wamisri nafaka mpaka pesa zao zikamalizika kabisa. Ndipo alipokubali mifugo yao iwe malipo. Mwisho, watu wakamjia Yusufu, wakisema: “Tununue sisi na nchi yetu kwa ajili ya mkate, nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa kwa Farao.” Kwa hiyo Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Wamisri. —Mwanzo 41:53-57; 47:13-20, NW.

Kutafuta Hazina za Kiroho

it-1 220 ¶1

Mtazamo na Ishara

Kufumba macho ya aliyekufa kwa mkono. Yehova alipomwambia Yakobo, “Yosefu atayafumba macho yako kwa mkono wake” (Mwa 46:4), alikuwa akimaanisha kwamba Yosefu angeyafumba macho ya Yakobo baada ya kifo chake, ingawa kwa kawaida hilo lilikuwa jukumu la mwana mzaliwa wa kwanza. Kwa hiyo, inaonekana kwamba Yehova alikuwa akimwonyesha Yakobo kuwa haki ya kuwa mzaliwa wa kwanza inapaswa kumwendea Yosefu.—1Nya 5:2.

nwtsty habari za utafiti Mdo 7:14

Watu 75 kwa ujumla: Huenda Stefano hakuwa akinukuu mstari fulani hususa katika Maandiko ya Kiebrania alipotaja idadi ya watu wa familia ya Yakobo kuwa 75. Idadi hiyo haipatikani katika maandishi ya Wamasora ya Maandiko ya Kiebrania. Mwa 46:26 inasema: “Wazao wote wa Yakobo walioenda Misri pamoja naye walikuwa 66, bila kuhesabu wake wa wanawe.” Mstari wa 27 unaendelea kusema: “Watu wote wa nyumba ya Yakobo waliokuja Misri walikuwa 70.” Hapa watu wanahesabiwa kwa njia mbili tofauti, inaonekana kwamba idadi ya kwanza inataja wazao wa asili wa Yakobo na idadi ya pili inaonyesha jumla ya wote walioingia Misri. Idadi ya wazao wa Yakobo inatajwa pia katika Kut 1:5 na Kum 10:22 kuwa watu “70.” Inaonekana kwamba Stefano anatoa idadi nyingine inayotia ndani watu wengine wa ukoo wa Yakobo. Watu fulani wanasema kwamba idadi hiyo inatia ndani watoto na wajukuu wa Manase na Efraimu, wana wa Yosefu, ambao wanatajwa katika tafsiri ya Septuajinti ya Mwa 46:20. Wengine wanasema kwamba idadi hiyo ilitia ndani wake wa wana wa Yakobo ambao hawakutiwa ndani ya idadi iliyotajwa katika Mwa 46:26. Kwa hiyo, huenda idadi ya watu “75” ndiyo jumla ya watu wote. Hata hivyo, huenda idadi hiyo ilitegemea nakala za Maandiko ya Kiebrania zilizokuwa zikisambazwa katika karne ya kwanza W.K. Kwa miaka mingi, wasomi wamejua kwamba “75” ndiyo idadi iliyotajwa katika Mwa 46:27 na Kut 1:5 kwenye Septuajinti ya Kigiriki. Isitoshe, katika karne ya 20, vipande vya Vitabu vya Kukunjwa vya Bahari ya Chumvi vinavyoonyesha Kut 1:5 katika Kiebrania vilipatikana, navyo vinataja idadi ya watu kuwa “75.” Huenda idadi ambayo Stefano alitaja inategemea moja kati ya maandishi hayo ya kale. Hata iwe ufafanuzi gani ndio sahihi, idadi ambayo Stefano alitaja inatuonyesha njia nyingine tu ya kuhesabu jumla ya idadi ya wazao wa Yakobo.

JUNI 15-21

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MWANZO 48-50

“Wenye Umri Mkubwa Wanaweza Kutufundisha Mengi”

it-1 1246 ¶8

Yakobo

Muda mfupi kabla ya kifo chake, Yakobo aliwabariki wajukuu wake, wana wa Yosefu, na kwa mwongozo wa Mungu alimtanguliza Efraimu aliyekuwa mdogo mbele ya Manase ndugu yake mkubwa. Kisha Yakobo akamwambia hivi Yosefu, ambaye angepokea urithi maradufu uliokusudiwa kwa ajili ya mzaliwa wa kwanza: “Mimi ninakupa sehemu moja zaidi ya nchi kuliko ndugu zako, ambayo nilichukua kutoka mikononi mwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.” (Mwa 48:1-22; 1Nya 5:1) Kwa kuwa Yakobo alikuwa amenunua sehemu ya ardhi iliyo karibu na Shekemu kutoka kwa wana wa Hamori kwa amani (Mwa 33:19, 20), inaonekana kwamba ahadi hiyo ambayo Yakobo alimpa Yosefu ilikuwa wonyesho wa imani ya Yakobo, kwa kuwa alitoa unabii kuhusu ushindi wa wakati ujao ambao wazao wake watapata dhidi ya Kanaani kana kwamba tayari ulikuwa umetimizwa kwa upanga na upinde wake mwenyewe. (Ona AMORI.) Urithi maradufu ambao Yosefu alipata katika nchi hiyo ulitia ndani sehemu mbili ambazo makabila ya Efraimu na Manase yalipewa.

it-2 206 ¶1

Siku za Mwisho

Unabii Ambao Yakobo Alitoa Kabla ya Kufa. Yakobo alipowaambia watoto wake hivi, “Kusanyikeni pamoja niwaambie yatakayowapata katika kipindi cha mwisho cha zile siku,” alimaanisha wakati ujao ambapo maneno yake yangeanza kutimia. (Mwa 49:1) Zaidi ya karne mbili mapema, Yehova alikuwa amemwambia Abramu (Abrahamu) babu ya Yakobo kwamba uzao wake ungeteswa kwa miaka 400. (Mwa 15:13) Hivyo, katika kisa hiki, wakati ujao ambao Yakobo aliuita “kipindi cha mwisho cha zile siku” hakingeanza mpaka baada ya ile miaka 400 ya kuteswa kuwa imekwisha. (Kwa habari zaidi kuhusu Mwanzo 49, ona makala zinazomhusu kila mwana wa Yakobo.) Inaweza kutarajiwa kwamba unabii huo ungetumiwa pia kuwahusu “Israeli wa Mungu”.—Gal 6:16; Ro 9:6.

Kutafuta Hazina za Kiroho

it-1 289 ¶2

Benjamini

Uwezo wa kupigana wa wazao wa Benjamini ulionyeshwa katika unabii ambao Yakobo alitoa kabla ya kufa ambapo alisema hivi kumhusu mwana wake mpendwa: “Benjamini ataendelea kurarua kama mbwamwitu. Asubuhi atakula mawindo, na jioni atagawanya nyara.” (Mwa 49:27) Wapiganaji wa kabila la Benjamini walijulikana kwa uwezo wao wa kutumia kombeo, wakirusha mawe kwa mkono wa kulia au wa kushoto na kulenga shabaha kiasi cha “kulenga unywele bila kukosea.” (Amu 20:16; 1Nya 12:2) Mwamuzi Ehudi aliyetumia mkono wa kushoto na ambaye alimuua Mfalme Egloni aliyewakandamiza Waisraeli alikuwa wa kabila la Benjamini. (Amu 3:15-21) Pia inafaa kutaja kwamba katika wakati unaoweza kusemwa kuwa “asubuhi” katika taifa la Israeli, kabila la Benjamini, ambalo lilikuwa “kabila dogo zaidi kati ya makabila ya Israeli,” lilitokeza mfalme wa kwanza wa Israeli, yaani, Sauli mwana wa Kishi, ambaye alikuwa mpiganaji hodari dhidi ya Wafilisti. (1Sa 9:15-17, 21) Vivyo hivyo, wakati unaoweza kusemwa kuwa wa “jioni,” Malkia Esta na Waziri Mkuu Mordekai waliokuwa wa kabila la Benjamini walitumiwa kuwaokoa Waisraeli wasiangamizwe katika Milki ya Uajemi.—Est 2:5-7.

JUNI 29–JULAI 5

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | KUTOKA 4-5

Kutafuta Hazina za Kiroho

it-2 12 ¶5

Yehova

Hivyo, “kujua,” hakumaanishi tu kufahamu kitu au mtu. Nabali aliyekuwa mpumbavu alijua jina la Daudi lakini bado aliuliza, “Daudi ni nani?” yaani alikuwa akiuliza “Kwani ana cheo gani?” (1Sa 25:9-11; linganisha 2Sa 8:13.) Vivyo hivyo pia, Farao alimwambia Musa hivi: “Yehova ni nani, hivi kwamba nitii sauti yake na kuwaruhusu Waisraeli waende zao? Simjui Yehova kamwe, na isitoshe, sitawaruhusu Waisraeli waende zao.” (Kut 5:1, 2) Ni wazi kwamba Farao alimaanisha kwamba hakumwona Yehova kuwa Mungu wa kweli wala hakuwa na mamlaka juu ya mfalme wa Misri au utendaji wake, wala hakuwa na uwezo wa kutekeleza mapenzi yake kama Musa na Haruni walivyosema. Lakini sasa Farao na watu wote wa Misri, pamoja na Waisraeli, wangejua maana halisi ya jina hilo, na yule aliyewakilishwa na jina hilo. Kama Yehova alivyomwonyesha Musa, hilo lingetokea wakati ambapo Mungu angetimiza kusudi lake kuwaelekea Waisraeli, kuwakomboa, kuwapa Nchi ya Ahadi, na hivyo kutimiza agano alilofanya na mababu zao. Kwa njia hiyo, kama Mungu alivyosema, “hakika mtajua kwamba mimi ni Yehova Mungu wenu.”—Kut 6:4-8; ona MWEZA-YOTE.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki