Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • mwbr21 Januari kur. 1-6
  • Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha
  • Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha—2021
  • Vichwa vidogo
  • JANUARI 11-17
  • JANUARI 18-24
  • HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MAMBO YA WALAWI 22-23
  • “Sherehe Zilizo na Maana Kwetu”
  • it-1 826-827
  • JANUARI 25-31
  • FEBRUARI 1-7
  • FEBRUARI 8-14
  • FEBRUARI 15-21
  • FEBRUARI 22-28
Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha—2021
mwbr21 Januari kur. 1-6

Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha

JANUARI 11-17

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MAMBO YA WALAWI 20-21

“Yehova Amewatenga Watu Wake”

it-1 1199

Urithi

Mali yoyote anayopewa mtu anayestahili au aliye na haki ya kumiliki baada ya mwenye mali kufa; kitu chochote kutoka kwa mzazi au mmiliki wa awali ambacho mtu anapitishiwa. Kitenzi cha Kiebrania kinachotumiwa ni na·chalʹ (nomino, na·chalahʹ). Neno hilo linamaanisha kupokea au kutoa urithi, mara nyingi kwa kupitishiwa. (Hes 26:55; Eze 46:18) Kitenzi ya·rashʹ hutumiwa pia kumaanisha ‘kuwa mrithi,’ lakini mara nyingi zaidi hutumiwa kumaanisha, ‘kumiliki’ mbali na kupitishiwa. (Mwa 15:3; Law 20:24) Neno hilo pia linamaanisha kunyang’anya au ‘kufukuza’ linapotumiwa katika masuala ya vita. (Kum 2:12; 31:3) Maneno ya Kigiriki yanayotumiwa kuhusu urithi yanahusianishwa na neno kleʹros, ambalo awali lilimaanisha “kura” lakini baadaye likaja kumaanisha “fungu” na hatimaye likamaanisha “urithi.”—Mt 27:35; Mdo 1:17; 26:18.

it-1 317 ¶2

Ndege

Baada ya Gharika, Noa alipotoa dhabihu ya wanyama, alitoa pia dhabihu ya “viumbe wanaoruka walio safi.” (Mwa 8:18-20) Baadaye, Mungu aliwaruhusu wanadamu kula ndege maadamu tu hawangekula damu yake. (Mwa 9:1-4; linganisha Law 7:26; 17:13.) Hivyo, ni wazi kwamba ‘usafi’ wa aina fulani ya ndege kipindi hicho, ulikuwa ishara ya kwamba Mungu alikubali ndege watolewe kuwa dhabihu; masimulizi ya Biblia yanaonyesha kwamba ndege wangeweza kutumiwa kama chakula, na hakuna ndege aliyeonwa kuwa “asiye safi” mpaka Sheria ya Musa ilipoanza kutumiwa. (Law 11:13-19, 46, 47; 20:25; Kum 14:11-20) Biblia haitaji kihususa sababu zilizofanya ndege fulani waonwe kuwa ‘wasio safi’ kisherehe. Hivyo, ingawa si wote, ndege wengi kati ya walioonwa kuwa si safi walikuwa wawindaji au walikula mizoga. (Ona HUDIHUDI.) Amri hiyo iliondolewa baada ya agano jipya kuanzishwa. Mungu alimwonyesha Petro jambo hilo waziwazi kupitia maono.—Mdo 10:9-15.

Hazina za Kiroho

it-1 563

Kujikatakata Mwilini

Sheria ya Mungu ilikataza kihususa kwamba watu wasijikatekate mwilini kwa ajili ya mtu aliyekufa. (Law 19:28; 21:5; Kum 14:1) Amri hiyo iliwekwa kwa sababu Waisraeli walikuwa watu watakatifu kwa Yehova, mali ya pekee. (Kum 14:2) Kwa msingi huo, Waisraeli hawakupaswa kujihusisha na mazoea yoyote ya ibada ya sanamu. Pia, kuomboleza kwa njia hiyo iliyopita kiasi iliyotia ndani kujikatakata mwilini, hakukuwafaa watu waliojua vizuri hali ya wafu na tumaini la ufufuo. (Da 12:13; Ebr 11:19) Amri hiyo ya kutojikatakata mwilini iliwasaidia Waisraeli kuheshimu uumbaji wa Mungu, yaani, mwili wa mwanadamu.

JANUARI 18-24

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MAMBO YA WALAWI 22-23

“Sherehe Zilizo na Maana Kwetu”

it-1 826-827

Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu

Siku ya kwanza ya Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu ilikuwa kusanyiko takatifu, iliyokuwa pia sabato. Siku ya pili, Nisani 16, kuhani aliletewa tita la mavuno ya kwanza ya shayiri, ambalo lilikuwa zao la kwanza kutokea katika eneo la Palestina. Kabla ya sherehe hiyo, mkate wowote, nafaka zilizokaangwa, au nafaka zilizotoka kuvunwa zingeweza kuliwa. Kwa njia ya mfano, kuhani alitoa mavuno ya kwanza kwa Yehova kwa kutikisa tita hilo mbele na nyuma huku mwanakondoo dume wa mwaka mmoja akitolewa kama dhabihu ya kuteketezwa pamoja na unga laini uliochanganywa na mafuta na toleo la kinywaji. (Law 23:6-14) Hakukuwa na sheria yoyote iliyosema kwamba nafaka au unga uteketezwe kwenye madhabahu, ingawa mambo hayo yalifanywa baadaye na makuhani. Mbali na kutoa dhabihu ya mazao bora ya kwanza wakiwa taifa, kila familia na mtu binafsi aliyekuwa na uwezo wa kutoa dhabihu za shukrani, angeweza kufanya hivyo katika sherehe hiyo.—Kut 23:19; Kum 26:1, 2; ona MAZAO YA KWANZA.

Umuhimu. Kula mikate isiyo na chachu pindi hiyo kulipatana na maagizo ambayo Yehova alimpa Musa, kama inavyotajwa katika Kutoka 12:14-20, kutia ndani amri hii nzito katika mstari wa 19: “Kwa siku saba, unga uliokandwa ambao umetiwa chachu usipatikane ndani ya nyumba zenu.” Katika Kumbukumbu la Torati 16:3, mikate isiyo na chachu inaitwa “mikate ya mateso,” na kila mwaka mikate hiyo iliwakumbusha Wayahudi jinsi walivyotoka haraka katika nchi ya Misri (wakati ambapo hawakuwa na wakati wa kutia chachu unga wao uliokandwa [Kut 12:34]). Hilo liliwakumbusha Waisraeli jinsi walivyokombolewa kutokana na mateso na vifungo. Yehova aliwaambia wafanye hivyo ‘sikuzote za maisha yao ili wakumbuke siku waliyotoka katika nchi ya Misri.’ Kutambua uhuru wao wakiwa taifa na kwamba Yehova alikuwa Mkombozi wao, kuliweka msingi mzuri wa sherehe ya kwanza kati ya sherehe tatu kuu zilizofanywa kila mwaka katika taifa la Israeli.—Kum 16:16.

it-2 598 ¶2

Pentekoste

Matunda ya kwanza ya mavuno ya ngano yalipaswa kushughulikiwa kwa njia tofauti na matunda ya kwanza ya shayiri. Sehemu mbili za kumi za kipimo cha efa cha unga wa ngano (Lita 4.4; kilogramu 2.6) uliotiwa chachu, uliokwa na kuwa mikate miwili. Mikate hiyo ilipaswa “kutoka nyumbani,” yaani, ilipaswa kuwa sawa na mikate iliyotengenezwa kwa ajili ya kuliwa nyumbani wala si kwa ajili ya kutumiwa katika ibada takatifu. (Law 23:17) Dhabihu za kuteketezwa na dhabihu ya dhambi ilitolewa hivyo pia, pamoja na wanakondoo dume wawili kama dhabihu ya ushirika. Kuhani alitikisa mikate hiyo na wanakondoo mbele za Yehova kwa kuweka mikono yake chini ya mikate na vipande vya kondoo, kisha akavitikisa mbele na nyuma, akionyesha kwamba dhabihu hizo zilikuwa zinatolewa mbele za Yehova. Baada ya mikate na mwanakondoo kutolewa kama dhabihu, kuhani aliruhusiwa kula vikiwa dhabihu ya ushirika.—Law 23:18-20.

JANUARI 25-31

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MAMBO YA WALAWI 24-25

“Mwadhimisho wa Miaka 50 na Uhuru wa Wakati Ujao”

it-1 871

Uhuru

Mungu wa Uhuru. Yehova ni Mungu wa uhuru. Alilipatia taifa la Israeli uhuru kutoka katika utumwa nchini Misri. Aliwaambia kwamba hawangekuwa maskini ikiwa wangetii amri zake. (Kum 15:4, 5) Daudi alizungumzia “usalama” uliokuwa ndani ya minara yenye ngome ya jiji la Yerusalemu. (Zb 122:6, 7) Hata hivyo, Sheria ilisema kwamba ikiwa mwanamume atakuwa maskini, anaweza kujiuza akiwa mtumwa ili aweze kuiandalia familia yake na yeye mwenyewe mahitaji ya msingi. Hata hivyo, kulingana na Sheria, mtumwa Mwebrania aliwekwa huru katika mwaka wa saba wa utumishi wake. (Kut 21:2) Katika Mwadhimisho wa Miaka 50, wakaaji wote nchini waliwekwa huru. Kila mtumwa Mwebrania aliwekwa huru, na kila mwanamume alirudi kwenye ardhi yake ya urithi.—Law 25:10-19.

it-1 1200 ¶2

Urithi

Ardhi haikupaswa kuuzwa kwa muda wa kudumu kwa kuwa ilikuwa mali ya familia moja kutoka kizazi kimoja mpaka kizazi kinachofuata. Kuuzwa kwa ardhi kulikuwa sawa na kuikodisha kulingana na thamani ya mazao ambayo yangevunwa. Bei yake ilitegemea idadi ya miaka hadi Mwadhimisho wa Miaka 50 ambao ungefuata, wakati ambapo ardhi hiyo ingekuwa mali ya mmiliki wa kwanza ikiwa haikuwa imekombolewa. (Law 25:13, 15, 23, 24) Sheria hiyo ilitia ndani nyumba zilizokuwa katika majiji ambayo hayakuwa yamezingirwa na kuta, kwa kuwa nyumba hizo zilihesabiwa kuwa mashamba. Mmiliki alikuwa na haki ya kuikomboa nyumba iliyokuwa katika jiji lililozingirwa na ukuta. Haki hiyo ilidumu kwa mwaka mmoja tangu alipoiuza, baada ya hapo, ingekuwa mali ya yule aliyenunua. Katika kisa cha nyumba zilizokuwa katika majiji ya Walawi, haki ya kukomboa ilikuwa ya kudumu kwa kuwa Walawi hawakuwa na urithi wa ardhi.—Law 25:29-34.

it-2 122-123

Mwadhimisho wa Miaka 50

Walipotii sheria ya Mwadhimisho wa Miaka 50, taifa lao lililindwa dhidi ya hali mbaya tunayoona leo katika nchi nyingi ambazo zina makundi mawili tu ya watu, matajiri kupindukia na maskini hohehahe. Faida walizopata watu binafsi ziliimarisha taifa hilo, kwa maana hakuna aliyekandamizwa sana na hali mbaya ya kiuchumi, na kila mtu angeweza kutumia kipaji chake na uwezo wake kuchangia masilahi ya taifa. Ikiwa Waisraeli wangetii, Yehova angebariki mazao yao na kuwaelimisha, nao wangefurahia serikali bora kabisa na ufanisi ambao unaweza kuletwa tu na utawala wa Yehova.—Isa 33:22.

FEBRUARI 1-7

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | MAMBO YA WALAWI 26-27

“Jinsi ya Kupokea Baraka za Yehova”

it-1 223 ¶3

Kustaajabisha

Kutokana na njia aliyotumia Yehova kushughulika na Musa, Musa alidhihirisha nguvu zenye kustaajabisha (Kiebrania, moh·raʼʹ) machoni pa watu wa Mungu. (Kum 34:10, 12; Kut 19:9) Wale waliokuwa na imani walionyesha woga unaofaa wa mamlaka ya Musa. Walitambua kwamba alitumiwa na Mungu kutoa maagizo. Waisraeli walipaswa pia kustaajabia mahali patakatifu pa Yehova. (Law 19:30; 26:2) Hilo lilimaanisha kwamba walipaswa kuheshimu mahali patakatifu kwa kuabudu kulingana na mwongozo wa Yehova na kuishi kulingana na sheria zake zote.

Hazina za Kiroho

it-2 617

Magonjwa

Yaliyosababishwa na Kutotii Sheria ya Mungu. Waisraeli walionywa kwamba ikiwa wangekataa kushikamana na agano lao pamoja na Mungu, ‘angeleta magonjwa katikati yao.’ (Law 26:14-16, 23-25; Kum 28:15, 21, 22) Katika Maandiko, afya nzuri, iwe ya kimwili au katika maana ya kiroho, inahusianishwa na baraka kutoka kwa Mungu (Kum 7:12, 15; Zb 103:1-3; Met 3:1, 2, 7, 8; 4:21, 22; Ufu 21:1-4), kwa upande mwingine, ugonjwa huhusianishwa na dhambi na kutokamilika. (Kut 15:26; Kum 28:58-61; Isa 53:4, 5; Mt 9:2-6, 12; Yoh 5:14) Hivyo, ingawa ni kweli kwamba katika visa fulani Yehova Mungu alisababisha moja kwa moja magonjwa kwa watu, kama vile ukoma kwa Miriamu, Uzia, na Gehazi (Hes 12:10; 2Nya 26:16-21; 2Fa 5:25-27), inaonekana kwamba katika visa vingi magonjwa yaliyowapata watu au mataifa yalikuwa matokeo yasiyozuilika ya dhambi walizotenda. Walikuwa wakivuna walichopanda; miili yao ilipata madhara yaliyotokana na dhambi zao. (Gal 6:7, 8) Kuhusu watu waliofanya uasherati mchafu sana, mtume alisema kwamba Mungu ‘aliwaacha katika uchafu, ili miili yao ivunjiwe heshima kati yao wapokee ndani yao wenyewe adhabu kamili, kwa sababu ya kosa lao.’—Ro 1:24-27.

FEBRUARI 8-14

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | HESABU 1-2

“Yehova Anawapanga Watu Wake”

it-1 397 ¶4

Kambi

Kambi ya Waisraeli ilikuwa kubwa sana. Kulikuwa na wanaume 603,550 wapiganaji walioandikishwa, pia kulikuwa na wanawake na watoto, wazee na walemavu, Walawi 22,000 na “kundi kubwa lenye mchanganyiko wa watu” ambao hawakuwa Waisraeli—huenda kwa pamoja idadi ya watu ilikuwa 3,000,000 au zaidi. (Kut 12:38, 44; Hes 3:21-34, 39) Haijulikani ni kiasi gani cha eneo ambalo kambi hiyo ilitumia; makadirio yanatofautiana sana. Walipopiga kambi Yeriko katika Jangwa Tambarare la Moabu, kambi yao inafafanuliwa kuwa ‘ilianzia Beth-yeshimothi mpaka Abel-shitimu.’—Hes 33:49.

Hazina za Kiroho

it-2 764

Uandikishaji

Uandikishaji mara nyingi wa jina na ukoo kulingana na kabila na familia. Unahusisha mengi zaidi ya kuhesabu watu. Biblia inataja kuhusu uandikishaji wa kitaifa uliofanywa kwa makusudi mbalimbali, kama vile kukusanya kodi, migawo ya utumishi wa jeshi, au (ambayo ilihusisha Walawi) kuwekwa rasmi kutumikia katika patakatifu.

FEBRUARI 15-21

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | HESABU 3-4

“Utumishi wa Walawi”

it-2 683 ¶3

Kuhani

Chini ya Agano la Sheria. Waisraeli walipokuwa utumwani Misri, Yehova alijitakasia kila mzaliwa wa kwanza katika Israeli, alipomuua kila mzaliwa wa kwanza nchini Misri kupitia pigo la kumi. (Kut 12:29; Hes 3:13) Wazaliwa wa kwanza walikuwa mali ya Yehova, yaani, waliwekwa kwa kusudi la kumtolea utumishi wa pekee. Mungu angeweza kutumia wazaliwa hao wa kwanza wa Israeli kama makuhani na watunzaji wa mahali patakatifu. Badala yake, ilipatana na kusudi lake kutumia wazaliwa wa kiume wa kabila la Walawi kufanya utumishi huo. Kwa sababu hiyo, aliruhusu taifa hilo liwakilishwe na Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa makabila 12 (wana wa Yosefu; Efraimu na Manase, walihesabiwa kuwa makabila mawili). Wazaliwa wa kwanza walipohesabiwa, iligundulika kwamba kulikuwa na wazaliwa wa kwanza 273 zaidi ambao hawakuwa Walawi wenye umri wa mwezi mmoja na kuendelea kuliko idadi ya Walawi, basi Mungu akaamuru kwamba bei ya fidia ya shekeli tano (dola 11 za Marekani) ilipwe na kila mmoja wa hao 273, na pesa hizo apewe Haruni na wanawe. (Hes 3:11-16, 40-51) Kabla ya fidia hiyo kulipwa, Yehova alikuwa tayari amewaweka rasmi wanaume wa familia ya Haruni ya kabila la Walawi kuwa makuhani wa Israeli.—Hes 1:1; 3:6-10.

it-2 241

Walawi

Migawo. Walawi walitoka katika familia tatu za wana wa Lawi, yaani, Gershoni (Gershomu), Kohathi, na Merari. (Mwa 46:11; 1Nya 6:1, 16) Kila familia ilipewa eneo karibu na hema la ibada nyikani. Familia ya Wakohathi ya akina Haruni, ilipiga kambi mbele ya hema la ibada upande wa mashariki. Wakohathi wengine walipiga kambi upande wa kusini, Wagershoni upande wa magharibi, na Wamerari upande wa kaskazini. (Hes 3:23, 29, 35, 38) Kazi ya Walawi ilitia ndani kusimamisha, kufungua, na kubeba hema la ibada. Wakati wa kuhama ulipofika, Haruni na wanawe walifungua pazia iliyotenganisha Patakatifu na Patakatifu Zaidi na kulifunika sanduku la Ushahidi, madhabahu, na vyombo vingine vitakatifu. Kisha, Wakohathi walibeba vitu hivyo. Wagershoni walibeba vitambaa vya hema la ibada, vifuniko, mapazia, mapazia ya ua yanayoning’inia, kamba za hema (huenda kamba za hema la ibada), na Wamerari walikuwa na jukumu la kutunza viunzi vya hema la ibada, nguzo, vikalio vyake, vigingi na kamba za hema (kamba za ua linalozunguka hema la ibada).—Hes 1:50, 51; 3:25, 26, 30, 31, 36, 37; 4:4-33; 7:5-9.

it-2 241

Walawi

Katika siku za Musa, Mlawi alipaswa kuwa na umri wa miaka 30 ili aruhusiwe kutimiza majukumu kikamili yaliyotia ndani kubeba hema la ibada lilipokuwa likihamishwa pamoja na vyombo vyake. (Hes 4:46-49) Baadhi ya migawo ilifanywa na wale waliokuwa na umri kuanzia miaka 25, hata hivyo inaonekana kazi hizo hazikuwa kazi ngumu kama ile ya kuhamisha hema la ibada. (Hes 8:24) Katika siku za Mfalme Daudi, umri huo ulipunguzwa kufikia miaka 20. Daudi alisema kwamba alifanya hivyo kwa sababu hema la ibada (ambalo nafasi yake ilichukuliwa na hekalu) halingehitaji kubebwa tena. Mtu aliacha utumishi wa lazima alipofikisha umri wa miaka 50. (Hes 8:25, 26; 1Nya 23:24-26; ona UMRI.) Walawi walipaswa kuijua vizuri sana Sheria, na mara nyingi walipewa mgawo wa kuisoma na kufundisha watu.—1Nya 15:27; 2Nya 5:12; 17:7-9; Ne 8:7-9.

FEBRUARI 22-28

HAZINA ZA NENO LA MUNGU | HESABU 5-6

“Unaweza Kuwaigaje Wanadhiri?”

it-2 477

Mnadhiri

Wanadhiri waliapa kuepuka mambo matatu: (1) Hawakupaswa kunywa divai na vinywaji vingine vyenye kileo; hawakupaswa kula chochote kinachotokana na mzabibu, iwe zabibu ambazo hazijaiva, zilizotoka kuchumwa, au zilizokaushwa, wala hawakupaswa kunywa maji ya zabibu hizo, iwe hayajachachishwa, au yamechachishwa, wala kunywa siki ya divai. (2) Hawakupaswa kukata nywele za vichwa vyao. (3) Hawakupaswa kugusa mwili wa mtu aliyekufa, hata ikiwa ni baba, mama, kaka, au dada.—Hes 6:1-7.

Nadhiri za Pekee. Mtu aliyeweka nadhiri hii ya pekee alipaswa “kuishi akiwa Mnadhiri [yaani, aliyewekwa wakfu, aliyewekwa kando] kwa Yehova” na si kuonyesha kwamba ana msimamo mkali wa imani ili tu kujipatia sifa machoni pa watu. Badala yake, “atakuwa mtakatifu kwa Yehova siku zote atakazokuwa Mnadhiri.”—Hes 6:2, 8; linganisha Mwa 49:26.

Hivyo, sifa za kustahili kuwa Mnadhiri zilikuwa na maana ya pekee katika ibada ya Yehova. Kama tu kuhani mkuu, ambaye kwa sababu ya mgawo wake mtakatifu hakupaswa kugusa mwili wa mtu aliyekufa, hata ikiwa alikuwa mtu wa ukoo wa karibu, Wanadhiri pia hawakupaswa kufanya hivyo. Kwa sababu kuhani mkuu na makuhani wengine walikuwa na migawo mizito, walikatazwa kunywa divai au kileo walipokuwa wakitimiza migawo yao mitakatifu mbele za Yehova.—Law 10:8-11; 21:10, 11.

Kwa kuongezea, Mnadhiri (Kiebrania, na·zirʹ) aliendelea “kuwa mtakatifu kwa kuacha nywele za kichwa chake ziwe ndefu.” Nywele hizo zingewasaidia wengine kutambua mara moja kwamba ameweka kiapo kitakatifu cha Unadhiri. (Hes 6:5) Neno hilo la Kiebrania, na·zirʹ lilitumika pia kurejelea mizabibu ambayo haikupaswa ‘kupunguzwa matawi’ katika mwaka wa Sabato takatifu na Mwadhimisho wa Miaka 50. (Law 25:5, 11) Inapendeza kwamba bamba la dhahabu lililowekwa juu ya kilemba cha kuhani mkuu, lililokuwa na maneno yaliyochongwa yanayosema “Utakatifu ni wa Yehova,” liliitwa pia “ishara takatifu ya wakfu [Kiebrania, neʹzer, kutokana na mzizi wa neno na·zirʹ].” (Kut 39:30, 31) Pia, taji lililovaliwa na wafalme wa Israeli waliotiwa mafuta, liliitwa pia neʹzer. (2Sa 1:10; 2Fa 11:12; ona TAJI; WAKFU.) Katika kutaniko la Kikristo, mtume Paulo anasema kwamba mwanamke amepewa nywele ndefu badala ya kitu cha kujifunika kichwani. Hilo linamkumbusha kiasili kwamba yeye ana majukumu tofauti na mwanamume; anapaswa kutambua sehemu yake na kujitiisha chini ya mpango wa Mungu. Hivyo, matakwa kama vile kutonyoa nywele (jambo ambalo kiasili mwanamume hufanya), kuepuka kunywa divai, na kuwa safi bila unajisi wowote—yalimkumbusha Mnadhiri aliyejiweka wakfu umuhimu wa kujinyima na kujitiisha kabisa ili kutimiza kusudi la Yehova.—1Ko 11:2-16; ona NYWELE; KUFUNIKA KICHWA; ASILI.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki