Marejeo ya Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha
JANUARI 10-16
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | WAAMUZI 17-19
“Kukosa Kutii Sheria ya Mungu Huleta Matatizo”
it-2 390-391
Mika
1. Mwanamume Mwefraimu. Mika alivunja amri ya nane kati ya zile Amri Kumi (Kut 20:15), alipochukua vipande 1,100 vya fedha kutoka kwa mama yake. Alipoungama na kumrudishia, mama yake alimwambia hivi: “Nitazitakasa fedha hizi kwa ajili ya Yehova zitoke mikononi mwangu ili mwanangu azitumie kutengeneza sanamu ya kuchongwa na sanamu ya chuma. Sasa nakurudishia fedha hizi.” Kisha mama yake akachukua vipande 200 vya fedha na kumpa mfua fedha, ambaye ‘alitengeneza sanamu ya kuchongwa na sanamu ya chuma’ na kuiweka katika nyumba ya Mika. Mika, ambaye alikuwa na “nyumba ya miungu,” alitengeneza efodi na sanamu za terafimu kisha akamweka mmoja wa wanawe awe kuhani wake. Ingawa lengo la mpango huo lilikuwa kumtukuza Yehova, halikufaa hata kidogo, kwa kuwa lilivunja amri iliyokataza ibada ya sanamu (Kut 20:4-6) na kukosa kuheshimu mpango wa Yehova wa hema la ibada na ukuhani wake. (Amu 17:1-6; Kum 12:1-14) Baadaye, Mika alimchukua Yonathani, mzao wa Gershomu, mwana wa Musa, akamleta nyumbani kwake, na kumwajiri Mlawi huyo kuwa kuhani. (Amu 18:4, 30) Kwa kujidanganya Mika aliridhika na mpango huo na kusema: “Sasa najua kwamba Yehova atanitendea mema.” (Amu 17:7-13) Lakini Yonathani hakuwa mzao wa Haruni na hivyo hakustahili kutumikia akiwa kuhani, na hilo liliongezea kwenye kosa la Mika.—Hes 3:10.
it-2 391 ¶2
Mika
Muda mfupi baadaye, Mika na kikundi cha wanaume wakawafuatilia watu wa kabila la Dani. Walipowafikia na kuulizwa kuna shida gani, Mika alisema: “Mmechukua miungu niliyojitengenezea na kuondoka na kuhani wangu pia. Mkaniacha bila chochote.” Aliposema hivyo wanaume wa kabila la Dani wakamwonya kwamba watamshambulia ikiwa ataendelea kuwafuata akilalamika. Mika alipoona kwamba watu wa kabila la Dani walikuwa wamemzidi yeye na kikundi chake nguvu, akageuka na kurudi nyumbani kwake. (Amu 18:22-26) Baada ya hapo watu wa kabila la Dani wakashambulia jiji la Laishi na kuliteketeza, nao wakajenga jiji la Dani mahali hapo. Yonathani na wanawe wakawa makuhani wa kabila la Dani, nao “wakaisimamisha ile sanamu ya kuchongwa iliyotengenezwa na Mika, na sanamu hiyo ikaendelea kuwa huko sikuzote ambazo nyumba ya Mungu wa kweli [hema la ibada] ilikuwa Shilo.”—Amu 18:27-31.
FEBRUARI 21-27
HAZINA ZA NENO LA MUNGU | 1 SAMWELI 6-8
“Mfalme Wako Ni Nani?”
it-2 163 ¶1
Ufalme wa Mungu
Kuomba Mfalme wa Kibinadamu. Karibu miaka 400 baada ya Kutoka Misri na zaidi ya miaka 800 baada ya Mungu kufanya agano na Abrahamu, Waisraeli waliomba mfalme wa kibinadamu awaongoze, kama mataifa mengine yalivyokuwa na watawala wa kibinadamu. Ombi lao lilikuwa sawa na kumkataa Yehova asiwatawale. (1Sa 8:4-8) Ni kweli, watu walitarajia ufalme usimamishwe na Mungu kupatana na ahadi yake kwa Abrahamu na Yakobo, iliyotajwa tayari. Walikuwa na msingi wa ziada wa kutarajia hilo kutokana na unabii ambao Yakobo alitoa kabla ya kufa kumhusu Yuda (Mwa 49:8-10), pia kutokana na maneno ya Yehova kwa taifa la Israeli baada ya Kutoka Misri (Kut 19:3-6), pia kutokana na maneno ya agano la Sheria (Kum 17:14, 15), na pia kutokana na ujumbe ambao Mungu alimfanya nabii Balaamu atoe (Hes 24:2-7, 17). Hana aliyekuwa mwaminifu, mama ya Samweli, alitaja jambo hilo katika sala. (1Sa 2:7-10) Hata hivyo, Yehova hakuwa amefichua ‘siri yake takatifu’ kuhusu Ufalme, wala hakuwa ameonyesha wakati wake wa kusimamisha ufalme huo ungefika lini, na pia hakuwa amefunua serikali hiyo ingekuwa na muundo gani au ingefanyizwa na nani—iwe ingekuwa ya kidunia au ya kimbingu. Kwa hiyo, ulikuwa kimbelembele kwa watu kudai wapewe mfalme wa kibinadamu wakati huo.