-
Atumia Mtini Kufundisha Kuhusu ImaniYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 105
Atumia Mtini Kufundisha Kuhusu Imani
MATHAYO 21:19-27 MARKO 11:19-33 LUKA 20:1-8
MTINI ULIONYAUKA—SOMO KUHUSU IMANI
WAULIZA KUHUSU MAMLAKA YA YESU
Yesu anaondoka Yerusalemu Jumatatu alasiri na kurudi Bethania, upande wa mashariki wa mteremko wa Mlima wa Mizeituni. Inawezekana kwamba usiku huo anakaa nyumbani kwa rafiki zake, yaani, Lazaro, Maria, na Martha.
Sasa ni asubuhi ya Nisani 11. Yesu na wanafunzi wake wako njiani tena, wakirudi Yerusalemu ambako atakuwa hekaluni kwa mara ya mwisho. Na ni siku yake ya mwisho ya huduma ya hadharani kabla ya kusherehekea Pasaka, kuanzisha Ukumbusho wa kifo chake, kisha akabili kesi na kuuawa.
Wakiwa njiani kutoka Bethania kwenye Mlima wa Mizeituni kuelekea Yerusalemu, Petro anauona mtini ambao Yesu aliulaani asubuhi ya siku iliyotangulia. Anasema hivi akiwa amesisimka: “Rabi, ona! ule mtini ulioulaani umenyauka.”—Marko 11:21.
Lakini kwa nini Yesu aliufanya mtini huo unyauke? Anaonyesha sababu anapojibu hivi: “Kwa kweli ninawaambia, mkiwa na imani nanyi msiwe na shaka, hamtafanya tu nilichoufanyia mtini huo, bali hata mkiuambia mlima huu, ‘Ng’oka, ukatupwe baharini,’ jambo hilo litatendeka. Na mambo yote mnayoomba katika sala, mkiwa na imani, mtapokea.” (Mathayo 21:21, 22) Basi anarudia jambo alilosema hapo awali kwamba imani inaweza kuhamisha mlima.—Mathayo 17:20.
Kwa hiyo, kwa kuufanya mti huo unyauke, Yesu anafundisha somo muhimu kuhusu uhitaji wa kuwa na imani katika Mungu. Anasema: “Mambo yote mnayosali na kuomba, iweni na imani kwamba mmeyapokea, nanyi mtayapata.” (Marko 11:24) Hilo ni somo muhimu sana kwa wafuasi wote wa Yesu! Somo hilo hasa linawafaa mitume kwa sababu ya majaribu makali ambayo watakabili hivi karibuni. Pia kuna uhusiano mwingine kati ya ule mtini ulionyauka na ubora wa imani.
Kama mtini huo, taifa la Israeli liko kinyume na jinsi linavyoonekana. Watu wa taifa hilo wako katika agano pamoja na Mungu, na kwa nje huenda wanaonekana kwamba wanafuata Sheria. Hata hivyo, kwa ujumla taifa zima limethibitisha kwamba halina imani na halizai matunda mazuri. Hata wanamkataa Mwana wa Mungu! Hivyo, kwa kuufanya mtini usiozaa unyauke, Yesu anaonyesha matokeo yatakayolipata taifa hilo lisilozaa matunda, na lisilo na imani.
Muda mfupi baadaye, Yesu na wanafunzi wake wanaingia Yerusalemu. Kama ilivyo desturi yake, Yesu anaingia hekaluni na kuanza kufundisha. Wakuu wa makuhani na wazee wa watu, labda wakikumbuka jambo ambalo Yesu aliwafanyia watu waliokuwa wakibadili pesa siku iliyotangulia, wanamuuliza: “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Au ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?”—Marko 11:28.
Yesu anawajibu: “Nitawauliza swali moja. Mkinijibu, nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani. Je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? Nijibuni.” Sasa wapinzani wake ndio wanaopaswa kujibu. Makuhani na wazee wanashauriana jinsi watakavyojibu: “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Basi, kwa nini hamkumwamini?’ Lakini je, tutathubutu kusema, ‘Ulitoka kwa wanadamu’?” Wanafikiria kwa njia hiyo kwa sababu wanauogopa umati, “kwa maana umati wote uliamini kwa kweli Yohana alikuwa nabii.”—Marko 11:29-32.
Wale wanaompinga Yesu wanashindwa kutoa jibu linalofaa. Basi wanasema: “Hatujui.” Naye Yesu anawaambia: “Nami siwaambii ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.”—Marko 11:33.
-
-
Mifano Miwili Kuhusu Mashamba ya MizabibuYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 106
Mifano Miwili Kuhusu Mashamba ya Mizabibu
MATHAYO 21:28-46 MARKO 12:1-12 LUKA 20:9-19
MFANO KUHUSU WANA WAWILI
MFANO WA WAKULIMA WA SHAMBA LA MIZABIBU
Akiwa hekaluni, Yesu ametoka kuwashangaza wakuu wa makuhani na wazee wa watu, ambao walikuwa wamemuuliza kuhusu mamlaka anayotumia kufanya mambo. Jibu la Yesu linawanyamazisha. Kisha anatoa mfano unaofunua jinsi walivyo kihalisi.
Yesu anasimulia hivi: “Mtu fulani alikuwa na watoto wawili. Akamwendea wa kwanza, akamwambia, ‘Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.’ Akamjibu, ‘Sitaenda,’ lakini baadaye akajuta na akaenda. Akamwendea wa pili na kumwambia jambo hilohilo. Naye akamjibu, ‘Nitaenda Baba,’ lakini hakwenda. Kati ya hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya baba yake?” (Mathayo 21:28-31) Jibu ni wazi—yule wa kwanza ndiye ambaye mwishowe alifanya mapenzi ya baba yake.
Basi, Yesu anawaambia hivi wapinzani wake: “Kwa kweli ninawaambia wakusanya kodi na makahaba wanawatangulia ninyi kuingia katika Ufalme wa Mungu.” Mwanzoni, wakusanya kodi na makahaba hawakutaka kumtumikia Mungu. Hata hivyo, kama yule mwana wa kwanza, baadaye walitubu na sasa wanamtumikia Mungu. Kinyume chake, viongozi wa kidini ni kama yule mwana wa pili, wanadai kwamba wanamtumikia Mungu lakini kwa kweli hawamtumikii. Yesu anasema hivi: “Yohana [Mbatizaji] alikuja kwenu katika njia ya uadilifu, lakini hamkumwamini. Hata hivyo, wakusanya kodi na makahaba walimwamini, nanyi, ijapokuwa mliona hilo, hamkujuta na kumwamini.”—Mathayo 21:31, 32.
Baada ya kutoa mfano huo, Yesu anasimulia mfano mwingine. Pindi hii Yesu anaonyesha kwamba kosa la viongozi wa kidini sio tu kukataa kumtumikia Mungu. Kwa kweli wao ni waovu. Yesu anasimulia hivi: “Mtu fulani alipanda shamba la mizabibu akalizungushia ua, akachimba shinikizo la divai, akajenga mnara, kisha akalikodisha kwa wakulima, naye akasafiri kwenda ng’ambo. Majira yalipofika akatuma mtumwa kwa wakulima ili achukue kutoka kwao baadhi ya matunda ya shamba la mizabibu. Lakini wakamkamata, wakampiga na kumfukuza mikono mitupu. Akamtuma tena mtumwa mwingine kwao, na huyo wakampiga kichwani na kumwaibisha. Akamtuma mwingine, na huyo wakamuua, akawatuma wengine wengi, wakawapiga baadhi yao na kuwaua wengine.”—Marko 12:1-5.
Je, wale wanaomsikiliza Yesu wataelewa mfano huo? Huenda wakakumbuka maneno haya ya shutuma yaliyosemwa na Isaya: “Shamba la mizabibu la Yehova wa majeshi ni nyumba ya Israeli; watu wa Yuda ndilo shamba alilolipenda sana. Aliendelea kutumaini haki itendwe, lakini tazama! kulikuwa na ukosefu wa haki.” (Isaya 5:7) Mfano wa Yesu unafanana na maneno hayo. Yehova ndiye anayemiliki shamba, nalo shamba la mizabibu ni taifa la Israeli, ambalo limezunguzishiwa ua na kulindwa na Sheria ya Mungu. Yehova aliwatuma manabii wawafundishe watu wake na kuwasaidia wazae matunda mazuri.
Hata hivyo, “wakulima” waliwatendea vibaya na kuwaua “watumwa” waliotumwa kwao. Yesu anaeleza hivi: “[Mwenye shamba la mizabibu] alikuwa na mmoja zaidi, mwana wake mpendwa. Mwishowe akamtuma kwao akisema: ‘Watamheshimu mwanangu.’ Lakini wakulima wakaambiana, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, na urithi utakuwa wetu.’ Kwa hiyo wakamkamata, wakamuua.”—Marko 12:6-8.
Sasa Yesu anauliza: “Mwenye shamba la mizabibu atafanya nini?” (Marko 12:9) Viongozi wa kidini wanajibu: “Kwa sababu ni waovu, atawaangamiza kabisa na kulikodisha shamba la mizabibu kwa wakulima wengine, ambao watampa matunda yatakapoiva.”—Mathayo 21:41.
Hivyo, bila kujua wanajihukumu wao wenyewe, kwa maana wao ni kati ya “wakulima” wa “shamba la mizabibu” la Yehova, taifa la Israeli. Matunda ambayo Yehova anatazamia kutoka kwa wakulima hao yanatia ndani kumwamini Mwana wake, yaani, Masihi. Yesu anawatazama moja kwa moja viongozi hao wa kidini na kusema: “Je, hamkusoma kamwe andiko hili: ‘Jiwe ambalo wajenzi walilikataa, limekuwa jiwe kuu la pembeni. Hili limetoka kwa Yehova, na ni lenye kustaajabisha machoni petu’?” (Marko 12:10, 11) Kisha Yesu anakazia jambo kuu: “Ndiyo sababu ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa taifa linalozaa matunda yake.”—Mathayo 21:43.
Waandishi na wakuu wa makuhani wanatambua kwamba “mfano aliosema uliwahusu.” (Luka 20:19) Kuliko wakati mwingine wowote, wanataka kumuua yule aliye na haki ya kuwa “mrithi.” Lakini wanauogopa umati, ambao unamwona Yesu kuwa nabii, basi hawajaribu kumuua wakati huo.
-
-
Mfalme Awaita Wale Walioalikwa Kwenye Karamu ya NdoaYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 107
Mfalme Awaita Wale Walioalikwa Kwenye Karamu ya Ndoa
MFANO WA KARAMU YA NDOA
Huduma ya Yesu inapokaribia kwisha, anaendelea kutumia mifano ili kufunua uovu wa waandishi na wakuu wa makuhani. Basi, wanataka kumuua. (Luka 20:19) Lakini bado Yesu hajamaliza kufunua uovu wao. Anasimulia mfano mwingine.
“Ufalme wa mbinguni ni kama mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya ndoa. Akawatuma watumwa wake wawaite wale walioalikwa kwenye karamu ya ndoa, lakini hawakutaka kuja.” (Mathayo 22:2, 3) Yesu anaanza mfano huo kwa kutaja “Ufalme wa mbinguni.” Basi, kwa hakika “mfalme” ni Yehova Mungu. Namna gani mwana wa mfalme na wale walioalikwa kwenye karamu ya ndoa? Pia, si vigumu kutambua kwamba mwana wa mfalme ni Mwana wa Yehova ambaye yuko hapo akisimulia mfano huo, na pia kuelewa kwamba wale walioalikwa ndio watakaokuwa pamoja na Mwana katika Ufalme wa mbinguni.
Ni nani wanaoalikwa kwanza? Yesu na mitume wamekuwa wakiwahubiria nani kuhusu Ufalme? Wamewahubiria Wayahudi. (Mathayo 10:6, 7; 15:24) Taifa hilo lilikubali agano la Sheria mwaka wa 1513 K.W.K., na hivyo kupata nafasi ya kwanza ya kutokeza “ufalme wa makuhani.” (Kutoka 19:5-8) Lakini ni wakati gani hasa ambapo wangealikwa kwenye “karamu ya ndoa”? Inapatana na akili kwamba mwaliko huo ulitolewa mwaka wa 29 W.K., Yesu alipoanza kuhubiri kuhusu Ufalme wa mbinguni.
Waisraeli wengi waliitikiaje mwaliko huo? Kama Yesu alivyosema, “hawakutaka kuja.” Idadi kubwa ya viongozi wa kidini na watu hawakukubali kwamba Yesu ndiye Masihi na Mfalme aliyechaguliwa na Mungu.
Hata hivyo, Yesu anaonyesha kwamba Wayahudi wangepewa nafasi nyingine: “Tena [mfalme] akawatuma watumwa wengine, akasema, ‘Waambieni wale walioalikwa: “Tazameni! Nimetayarisha chakula changu cha mchana, ng’ombe dume wangu na wanyama waliononeshwa wamechinjwa, na vitu vyote viko tayari. Njooni kwenye karamu ya ndoa.”’ Lakini wakapuuza na kwenda zao, wengine kwenye mashamba yao, na wengine kwenye biashara zao; lakini wengine wakawakamata wale watumwa wakawatendea kwa dharau na kuwaua.” (Mathayo 22:4-6) Hilo linapatana na jambo ambalo lingetokea baada ya kutaniko la Kikristo kuanzishwa. Wakati huo bado Wayahudi walikuwa na nafasi ya kuwa katika Ufalme. Hata hivyo, wengi walikataa mwaliko huo hata wakawatendea vibaya ‘watumwa wa mfalme.’—Matendo 4:13-18; 7:54, 58.
Taifa hilo litapatwa na matokeo gani? Yesu anasimulia hivi: “Mfalme akakasirika sana, akatuma majeshi yake yakawaue wauaji hao na kulichoma jiji lao.” (Mathayo 22: 7) Wayahudi walipatwa na jambo hilo mwaka wa 70 W.K. Waroma walipoharibu “jiji lao,” Yerusalemu.
Wanapokataa mwaliko wa mfalme, je, inamaanisha kwamba hakuna watu wengine watakaoalikwa? Mfano wa Yesu hauonyeshi hivyo. Anaendelea kusema hivi: “Kisha [mfalme] akawaambia watumwa wake, ‘Karamu ya ndoa iko tayari, lakini walioalikwa hawakustahili. Kwa hiyo, nendeni kwenye barabara zinazotoka jijini, na kumwalika kwenye karamu ya ndoa mtu yeyote mtakayemwona.’ Basi watumwa wakaenda barabarani na kuwaalika wote waliowaona, waovu na wema; na chumba cha sherehe za harusi kikajaa wageni.”—Mathayo 22:8-10.
Kwa kupatana na jambo hilo, baadaye mtume Petro angeanza kuwasaidia Watu wa Mataifa—watu ambao hawakuwa Wayahudi kwa kuzaliwa au kwa kugeuzwa imani—wawe Wakristo. Katika mwaka wa 36 W.K., ofisa wa jeshi Mroma, Kornelio na familia yake walipokea roho ya Mungu, na hivyo wakawa na tumaini la kuwa katika Ufalme wa Mbinguni ambao Yesu alitaja.—Matendo 10:1, 34-48.
Yesu anaonyesha kwamba si wote wanaokuja kwenye karamu ambao mwishowe watakubalika mbele za “mfalme.” Anasema: “Mfalme alipoingia kuwakagua wageni, akamwona mtu ambaye hakuwa amevaa vazi la ndoa. Basi akamuuliza, ‘Mwenzangu, umeingiaje humu bila vazi la ndoa?’ Akakosa la kusema. Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu, kisha mmtupe nje gizani. Huko ndiko atalia na kusaga meno yake.’ Kwa maana kuna wengi walioalikwa, lakini waliochaguliwa ni wachache.”—Mathayo 22:11-14.
Huenda viongozi wa kidini wanaomsikiliza Yesu wasielewe maana au matokeo ya mambo anayosema. Hata hivyo, wanakasirika na kuazimia hata zaidi kumuua mtu anayewaaibisha hivyo.
-
-
Yesu Apangua Njama za KumtegaYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 108
Yesu Apangua Njama za Kumtega
MATHAYO 22:15-40 MARKO 12:13-34 LUKA 20:20-40
VITU VYA KAISARI KWA KAISARI
JE, KUTAKUWA NA NDOA KATIKA UFUFUO?
AMRI KUU ZAIDI
Viongozi wa kidini ambao ni maadui za Yesu wamekasirika. Ametoka tu kusimulia mifano inayofunua uovu wao. Sasa Mafarisayo wanapanga njama ili kumnasa. Wanajaribu kumfanya aseme jambo litakalofanya wamkabidhi kwa gavana Mroma, basi wanawalipa baadhi ya wanafunzi wao ili wamtege.—Luka 6:7.
Wanasema: “Mwalimu, tunajua wewe husema na kufundisha kwa usahihi na huna ubaguzi, bali unafundisha njia ya Mungu kupatana na kweli: Je, ni halali au si halali kwetu kumlipa Kaisari kodi?” (Luka 20:21, 22) Yesu hapumbazwi wanapomsifu-sifu, kwa maana wamejaa unafiki na hila moyoni. Akisema, ‘Hapana, si halali kulipa kodi,’ anaweza kushtakiwa kwa uchochezi dhidi ya Roma. Lakini akisema, ‘Ndiyo, lipeni kodi hiyo,’ watu waliochoshwa kuwa chini ya utawala wa Roma, wanaweza kumwelewa vibaya na kuanza kumshambulia. Basi anajibuje?
Yesu anajibu hivi: “Kwa nini mnanijaribu, ninyi wanafiki? Nionyesheni sarafu ya kodi.” Wanaleta dinari, kisha anawauliza: “Sura hii na maandishi haya ni ya nani?” Wanajibu: “Ni ya Kaisari.” Kisha Yesu anatoa mwongozo huu thabiti: “Basi, mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari, na Mungu vitu vya Mungu.”—Mathayo 22:18-21.
Watu hao wanashangazwa na maneno ya Yesu. Wakiwa wamenyamazishwa baada ya Yesu kuwajibu kwa ustadi, wanaondoka. Lakini bado siku haijaisha, wala jitihada za kumnasa hazijakwisha. Mafarisayo wanapokosa kufanikiwa, viongozi wa kikundi kingine cha kidini wanamkaribia Yesu.
Masadukayo, ambao husema hakuna ufufuo, wanauliza swali linalohusu ufufuo na desturi ya mtu kuoa mke wa ndugu yake aliyekufa. Wanauliza hivi: “Mwalimu, Musa alisema: ‘Mtu yeyote akifa bila kupata watoto, ndugu yake anapaswa kumwoa mke wake ili kumwinulia ndugu yake uzao.’ Basi kulikuwa na ndugu saba kati yetu. Wa kwanza akaoa kisha akafa, na kwa sababu hakuwa na watoto, akamwachia ndugu yake mke wake. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa pili na wa tatu, na kwa wote saba. Mwishowe, yule mwanamke akafa. Basi, katika ufufuo, atakuwa mke wa nani kati ya wale saba? Kwa maana aliolewa na wote.”—Mathayo 22:24-28.
Akirejelea maandishi ya Musa, ambayo Masadukayo wanayakubali, Yesu anajibu hivi: “Ninyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko wala nguvu za Mungu. Kwa maana wanapofufuliwa kutoka kwa wafu, wanaume hawaoi wala wanawake hawaolewi, bali wao ni kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuliwa kwa wafu, je, hamkusoma katika kitabu cha Musa, simulizi kuhusu kile kichaka cha miiba kwamba Mungu alimwambia: ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Mmekosea sana.” (Marko 12:24-27; Kutoka 3:1-6) Umati unashangazwa na jibu lake.
Yesu amewanyamazisha Mafarisayo na Masadukayo, basi wapinzani hao wa kidini wanaungana kisha wanakuja kumjaribu tena. Mwandishi mmoja anauliza: “Mwalimu, ni amri gani iliyo kuu zaidi katika Sheria?”—Mathayo 22:36.
Yesu anajibu: “Ya kwanza ni hii, ‘Sikilizeni, enyi Waisraeli, Yehova Mungu wetu ni Yehova mmoja, nawe lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote.’ Ya pili ni hii, ‘Lazima umpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ Hakuna amri nyingine iliyo kubwa kuliko amri hizi.”—Marko 12:29-31.
Yule mwandishi anaposikia jibu hilo anasema: “Mwalimu, umesema vema kupatana na kweli, ‘Yeye ni Mmoja, na hakuna mwingine isipokuwa yeye’; na kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa uelewaji wote na kwa nguvu zote na pia mtu kumpenda jirani yake kama anavyojipenda mwenyewe ni bora kuliko matoleo yote mazima ya kuteketezwa na dhabihu.” Yesu anapoona kwamba mwandishi huyo amejibu kwa kutumia akili, anamwambia hivi: “Wewe huko mbali na Ufalme wa Mungu.”—Marko 12:32-34.
Kwa siku tatu (Nisani 9, 10, na 11) Yesu amekuwa akifundisha hekaluni. Baadhi ya watu, kama vile mwandishi huyo, wamefurahia kumsikiliza. Lakini sivyo kwa viongozi wa kidini ambao sasa ‘hawathubutu tena kumuuliza swali.’
-
-
Awashutumu Wapinzani wa KidiniYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 109
Awashutumu Wapinzani wa Kidini
MATHAYO 22:41–23:24 MARKO 12:35-40 LUKA 20:41-47
KRISTO NI MWANA WA NANI?
YESU AWAFUNUA WAPINZANI WANAFIKI
Wapinzani wa kidini wanashindwa kumharibia sifa Yesu au kumnasa na kumkabidhi kwa Waroma. (Luka 20:20) Sasa wakiwa bado hekaluni Nisani 11, Yesu anawageukia na kuwaonyesha utambulisho wake halisi. Kwanza anawauliza: “Mna maoni gani kuhusu Kristo? Ni mwana wa nani?” (Mathayo 22:42) Ni wazi kwamba Kristo au Masihi, atatoka katika ukoo wa Daudi. Hivyo ndivyo wanavyojibu.—Mathayo 9:27; 12:23; Yohana 7:42.
Yesu anauliza: “Basi, kwa nini Daudi akiongozwa na roho anamwita Bwana, akisema, ‘Yehova alimwambia Bwana wangu: “Keti kwenye mkono wangu wa kuume mpaka niwaweke maadui wako chini ya miguu yako”’? Basi ikiwa Daudi anamwita Bwana, anawezaje kuwa mwanawe?”—Mathayo 22:43-45.
Mafarisayo wananyamaza, kwa kuwa wanatumaini kwamba mtu kutoka ukoo wa Daudi atawakomboa kutoka kwa utawala wa Roma. Lakini Yesu anatumia maneno ya Daudi katika Zaburi 110:1, 2, kuonyesha kwamba Masihi atakuwa zaidi ya mtawala wa kibinadamu. Yeye ndiye Bwana wa Daudi, na baada ya kukaa katika mkono wa kuume wa Mungu, atakuwa mtawala. Maneno ya Yesu yanawanyamazisha wapinzani wake.
Wanafunzi na wengine wengi wamekuwa wakisikiliza. Sasa Yesu anazungumza nao, akiwaonya kuhusu waandishi na Mafarisayo. Watu hao “wamejiketisha kwenye kiti cha Musa” ili kufundisha Sheria ya Mungu. Yesu anawaambia hivi wasikilizaji wake: “Fanyeni mambo yote wanayowaambia, lakini msitende kama wao, kwa maana wao husema lakini hawatendi mambo wanayosema.”—Mathayo 23:2, 3.
Kisha Yesu anatoa mifano kuhusu unafiki wao, akisema: “Wanapanua visanduku vyenye maandiko wanavyovaa kama ulinzi.” Baadhi ya Wayahudi walivaa kwenye paji la uso au mkononi visanduku hivyo vidogo vilivyokuwa na mafungu mafupi ya Sheria. Mafarisayo huongezea ukubwa wa visanduku vyao ili kujionyesha kwamba wana bidii ya kufuata Sheria. Pia, ‘wanarefusha pindo zenye nyuzi za mavazi yao.’ Waisraeli walipaswa kutengeneza pindo kwenye mavazi yao, lakini Mafarisayo wanahakikisha kwamba pindo zao ni ndefu sana. (Hesabu 15:38-40) Wanafanya mambo yote hayo “ili waonwe na watu.”—Mathayo 23:5.
Hata wanafunzi wa Yesu wanaweza kuathiriwa na tamaa ya umashuhuri, hivyo anawashauri hivi: “Msiitwe Rabi, kwa maana Mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Zaidi ya hayo, msimwite mtu yeyote baba yenu duniani, kwa maana Baba yenu ni mmoja, Yule aliye mbinguni. Wala msiitwe viongozi, kwa maana Kiongozi wenu ni mmoja, Kristo.” Hivyo basi, wanafunzi wanapaswa kujionaje na kutendaje? Yesu anawaambia: “Aliye mkuu zaidi kati yenu lazima awe mhudumu wenu. Yeyote anayejiinua atanyenyekezwa, na yeyote anayejinyenyekeza atainuliwa.”—Mathayo 23:8-12.
Kisha Yesu anawatangazia ole waandishi na Mafarisayo wanafiki: “Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa sababu mnawafungia watu Ufalme wa mbinguni; kwa maana ninyi wenyewe hamwingii, na mnawazuia wale wanaotaka kuingia.”—Mathayo 23:13.
Yesu anawashutumu Mafarisayo kwa sababu hawathamini mambo ya kiroho, kama inavyoonyeshwa na maamuzi yao yasiyo na msingi. Kwa mfano, wanasema: “Yeyote akiapa kwa hekalu, si kitu; lakini yeyote akiapa kwa dhahabu ya hekalu, yuko chini ya wajibu.” Hivyo wanaonyesha jinsi walivyo vipofu kimaadili, kwa maana wanakazia zaidi dhahabu ya hekalu kuliko thamani ya kiroho ya mahali pa kumwabudu Yehova. Nao ‘wamepuuza mambo mazito zaidi ya Sheria, yaani, haki, rehema, na uaminifu.’—Mathayo 23:16, 23; Luka 11:42.
Yesu anawaita Mafarisayo hao “viongozi vipofu, ambao huchuja mbu lakini hummeza ngamia!” (Mathayo 23:24) Wanachuja mbu kutoka kwenye divai yao kwa sababu mdudu huyo si safi kisherehe. Lakini wanapopuuza mambo mazito ya Sheria ni kama wanammeza ngamia, ambaye pia ni mnyama asiye safi kisherehe, lakini mkubwa zaidi.—Mambo ya Walawi 11:4, 21-24.
-
-
Siku ya Mwisho ya Yesu HekaluniYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 110
Siku ya Mwisho ya Yesu Hekaluni
MATHAYO 23:25–24:2 MARKO 12:41–13:2 LUKA 21:1-6
YESU AZIDI KUWASHUTUMU VIONGOZI WA KIDINI
HEKALU LITAHARIBIWA
MJANE MASKINI ACHANGIA SARAFU MBILI NDOGO
Katika siku ya mwisho ya Yesu hekaluni, anaendelea kufunua hadharani unafiki wa waandishi na Mafarisayo akiwaita wanafiki. Anatumia lugha ya mfano, akisema: “Mnasafisha upande wa nje wa kikombe na wa sahani, lakini ndani vimejaa pupa na kutojizuia. Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe na sahani ili upande wa nje uwe safi pia.” (Mathayo 23:25, 26) Ingawa Mafarisayo wako makini kuhusu usafi wa kisherehe na jinsi wanavyoonekana kwa nje, wanapuuza utu wa ndani nao wanakosa kusafisha mioyo yao ya mfano.
Pia, wanaonyesha unafiki wao kupitia jinsi walivyo tayari kujenga na kupamba makaburi ya manabii. Lakini kama Yesu anavyosema, wao “ni wana wa wale waliowaua manabii.” (Mathayo 23:31) Wamethibitisha hivyo kupitia jitihada zao za kumuua Yesu.—Yohana 5:18; 7:1, 25.
Kisha Yesu anataja kitakachowapata viongozi hao wa kidini ikiwa hawatatubu: “Ninyi nyoka, wana wa nyoka, mtaikimbiaje hukumu ya Gehena?” (Mathayo 23:33) Bonde la Hinomu lililo hapo karibu hutumiwa kuteketeza takataka, mfano huo unaonyesha uharibifu wa milele unaowasubiri waandishi na Mafarisayo waovu.
Wanafunzi wa Yesu watamwakilisha wakiwa “manabii na watu wenye hekima na walimu wa watu wote.” Watatendewaje? Akizungumza na viongozi wa kidini, Yesu anasema: “Baadhi [ya wanafunzi wangu] mtawaua na kuwatundika kwenye miti, na baadhi yao mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwatesa katika jiji baada ya jiji, ili damu yote ya waadilifu iliyomwagwa duniani ije juu yenu, kuanzia damu ya Abeli mwadilifu mpaka damu ya Zekaria . . . ambaye mlimuua.” Anaonya hivi: “Kwa kweli ninawaambia, mambo yote haya yatakipata kizazi hiki.” (Mathayo 23:34-36) Hivyo ndivyo inavyokuwa mwaka wa 70 W.K. jeshi la Roma linapoharibu Yerusalemu na kuangamiza maelfu ya Wayahudi.
Anapofikiria hali hiyo yenye kuogopesha Yesu anahuzunika sana. Anasema hivi kwa huzuni: “Yerusalemu, Yerusalemu, muuaji wa manabii na aliyewapiga mawe wale waliotumwa kwake—nilijaribu mara ngapi kuwakusanya watoto wako, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga wake chini ya mabawa yake! Lakini hamkutaka. Tazama! Mmeachiwa nyumba yenu.” (Mathayo 23:37, 38) Wale wanaosikia maneno hayo wanajiuliza anamaanisha “nyumba” gani. Je, huenda anamaanisha hekalu lenye utukufu lililo Yerusalemu, ambalo inaonekana kwamba linalindwa na Mungu?
Kisha Yesu anaongezea hivi: “Ninawaambia, tangu sasa hamtaniona tena mpaka mtakaposema, ‘Amebarikiwa yule anayekuja katika jina la Yehova!’” (Mathayo 23:39) Ananukuu maneno ya unabii kwenye Zaburi 118:26: “Amebarikiwa yule anayekuja katika jina la Yehova; tunakubariki kutoka katika nyumba ya Yehova.” Ni wazi kwamba hekalu hilo litakapoharibiwa, hakuna mtu atakayeingia humo katika jina la Mungu.
Sasa Yesu anaenda kwenye sehemu ya hekalu iliyo na masanduku ya hazina yenye umbo la tarumbeta. Watu wanaweza kutumbukiza michango yao humo kupitia matundu madogo yaliyo juu. Yesu anawaona Wayahudi wengi wakifanya hivyo, matajiri “wakitumbukiza sarafu nyingi” kama zawadi. Kisha Yesu anamwona mjane maskini akitumbukiza “sarafu mbili ndogo zenye thamani ndogo sana.” (Marko 12:41, 42) Bila shaka, Yesu anajua jinsi Mungu anavyopendezwa na zawadi ya mjane huyo.
Yesu anawaita wanafunzi wake, na kuwaambia hivi: “Kwa kweli ninawaambia mjane huyu maskini ametumbukiza zaidi ya wote waliotumbukiza pesa ndani ya masanduku ya hazina.” Inawezekanaje? Anafafanua hivi: “Wote walitumbukiza kutokana na ziada yao, lakini yeye, ingawa ni maskini, alitumbukiza kila kitu alichokuwa nacho, riziki yake yote.” (Marko 12:43, 44) Mwanamke huyo anatofautiana sana na viongozi hao wa kidini kwa mawazo na matendo!
Siku ya Nisani 11 inapoendelea, Yesu anaondoka hekaluni kwa mara ya mwisho. Mmoja kati ya wanafunzi wake anasema hivi kwa mshangao: “Mwalimu, ona! jinsi mawe na majengo haya yalivyo maridadi!” (Marko 13:1) Kwa kweli, baadhi ya mawe katika ukuta wa hekalu ni makubwa sana, nayo yanafanya lionekane imara na lenye kudumu. Ni wazi kwamba inashangaza Yesu anaposema: “Unayaona majengo haya makubwa? Hakuna jiwe litakaloachwa hapa juu ya jiwe lingine bila kuangushwa chini.”—Marko 13:2.
Baada ya kusema mambo hayo, Yesu na mitume wake wanavuka Bonde la Kidroni kisha wanapanda na kwenda mahali fulani kwenye Mlima wa Mizeituni. Pindi fulani, Yesu yuko pamoja na mitume wake wanne—Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana. Wanapotazama chini wakiwa hapo, wanaweza kuona hekalu lenye utukufu.
-
-
Mitume Waomba IsharaYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 111
Mitume Waomba Ishara
MATHAYO 24:3-51 MARKO 13:3-37 LUKA 21:7-38
WANAFUNZI WANNE WAOMBA ISHARA
UTIMIZO KATIKA KARNE YA KWANZA NA BAADAYE
TUNAPASWA KUENDELEA KUWA MACHO
Ni siku ya Jumanne mchana, na Nisani 11 inakaribia kwisha. Pia, ni mwisho wa siku zenye shughuli nyingi kwa Yesu hapa duniani. Mchana amekuwa akifundisha hekaluni, na usiku amekuwa akilala nje ya jiji. Watu wanapendezwa sana naye, hivi kwamba wamekuwa “wakija hekaluni asubuhi na mapema ili wamsikilize.” (Luka 21:37, 38) Sasa hayo yamepita, naye Yesu amekaa kwenye Mlima wa Mizeituni na wanafunzi wake wanne—Petro, Andrea, Yakobo na Yohana.
Wanafunzi hao wanne wamekuja kuongea naye faraghani. Wanahangaikia hekalu kwa kuwa Yesu ametoka kutabiri kwamba hakuna jiwe la hekalu litakaloachwa juu ya jiwe lingine. Hata hivyo, pia wanafikiria mambo mengine. Hapo awali, Yesu aliwahimiza hivi: “Endeleeni kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa binadamu atakuja saa msiyotazamia.” (Luka 12:40) Pia, alikuwa amezungumzia “siku ambayo Mwana wa binadamu atafunuliwa.” (Luka 17:30) Je, maelezo hayo yanahusiana kwa vyovyote na mambo ambayo ametoka tu kusema kuhusu hekalu? Mitume wanataka kujua mengi zaidi. Wanamuuliza: “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, na ni nini itakayokuwa ishara ya kuwapo kwako na ya umalizio wa mfumo wa mambo?”—Mathayo 24:3.
Huenda wanafikiria kuhusu kuharibiwa kwa hekalu wanaloliona. Pia, wanauliza kuhusu kuwapo kwa Mwana wa binadamu. Labda wanakumbuka kwamba Yesu alitoa mfano kuhusu “mtu fulani wa familia mashuhuri” ambaye ‘alisafiri ili akapokee mamlaka ya kifalme kisha arudi.’ (Luka 19:11, 12) Na mwishowe wanajiuliza “umalizio wa mfumo wa mambo” utahusisha nini.
Katika majibu yake, Yesu anatoa ishara inayoonyesha wakati ambao mfumo wa Kiyahudi uliopo, kutia ndani hekalu lake utakoma. Hata hivyo, anazungumzia mengi zaidi. Ishara hiyo itawasaidia Wakristo wakati ujao kujua ikiwa wanaishi wakati wa “kuwapo” kwake na karibu na mwisho wa mfumo mzima wa mambo duniani.
Kadiri miaka inavyopita, mitume wanaona unabii wa Yesu ukitimizwa. Naam, mambo mengi aliyotabiri yanaanza kutukia wakiwa hai. Hivyo, Wakristo walio macho wanaoishi miaka 37 baadaye, mwaka wa 70 W.K., wamejiandaa na wako tayari kwa ajili ya uharibifu unaokaribia wa mfumo wa Kiyahudi na hekalu lake. Hata hivyo, si mambo yote ambayo Yesu anatabiri yanatukia kabla na baada ya mwaka wa 70 W.K. Hivyo basi, ni nini kitakachoonyesha kuwapo kwake katika utawala wa Kifalme? Yesu anawafunulia mitume wake jibu.
Yesu anatabiri kwamba kutakuwa na “vita na habari za vita” na kwamba “taifa litapigana na taifa na ufalme kupigana na ufalme.” (Mathayo 24:6, 7) Pia, anasema kwamba “kutakuwa na matetemeko makubwa ya ardhi, na magonjwa na upungufu wa chakula katika sehemu mbalimbali.” (Luka 21:11) Yesu anawaonya hivi wanafunzi wake: “Watu watawakamata ninyi na kuwatesa.” (Luka 21:12) Manabii wa uwongo watatokea na kuwapotosha wengi. Uasi sheria utaongezeka na upendo wa wengi utapoa. Pia, anasema kwamba “habari njema ya Ufalme itahubiriwa katika dunia yote inayokaliwa ili kuwa ushahidi kwa mataifa yote, na ndipo ule mwisho utakapokuja.”—Mathayo 24:14.
Ingawa unabii wa Yesu ulitimizwa kwa kadiri fulani kabla na wakati Yerusalemu lilipoharibiwa na Waroma, je, huenda Yesu alikuwa akizungumzia utimizo mkubwa zaidi baadaye? Je, unaona uthibitisho kwamba unabii muhimu wa Yesu umekuwa ukitimizwa kwa kiwango kikubwa katika nyakati zetu?
Jambo moja ambalo Yesu anataja katika ishara ya kuwapo kwake ni kuonekana kwa “kitu chenye kuchukiza sana kinachosababisha ukiwa.” (Mathayo 24:15) Mwaka wa 66 W.K., kitu hicho chenye kuchukiza kilikuwa “majeshi yaliyopiga kambi” ya Roma, yakiwa na sanamu zao. Waroma walizunguka Yerusalemu na kuvunja baadhi ya kuta zake. (Luka 21:20) Hivyo, “kitu chenye kuchukiza” kilisimama mahali ambapo hakikupaswa kusimama, mahali ambapo Wayahudi walipaona kuwa “patakatifu.”
Pia, Yesu anatabiri hivi: “Kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijawahi kutokea tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka sasa, hapana, wala haitatokea tena.” Katika mwaka wa 70 W.K., Waroma wanaliharibu Yerusalemu. Kuharibiwa kwa ‘jiji takatifu’ la Wayahudi, kutia ndani hekalu lake kunathibitika kuwa dhiki kuu, na watu wengi sana wanauawa. (Mathayo 4:5; 24:21) Ni uharibifu mkubwa zaidi kuliko uharibifu wowote ambao jiji hilo na Wayahudi wote wamewahi kushuhudia, nao unakomesha mfumo wote wa ibada ambao umefuatwa na Wayahudi kwa miaka mingi. Kwa hiyo, baadaye, utimizo wowote mkubwa wa unabii wa Yesu utakuwa wenye kuogopesha kwelikweli.
UHAKIKA KATIKA SIKU ZILIZOTABIRIWA
Mazungumzo ya Yesu na mitume wake kuhusu ishara ya kuwapo kwake katika utawala wa Ufalme na mwisho wa mfumo wa mambo hayajamalizika. Sasa anawaonya kuhusu kuwafuata “Kristo wengi wa uwongo na manabii wa uwongo.” Anasema watajaribu, “kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale waliochaguliwa.” (Mathayo 24:24) Lakini wachaguliwa hao hawatapotoshwa. Kristo wa uwongo wanaweza kuonekana kwa macho. Tofauti na hilo, kuwapo kwa Yesu hakutaonekana kwa macho.
Akizungumza kuhusu dhiki kubwa zaidi ambayo itatokea mwishoni mwa mfumo huu wa mambo, Yesu anasema: “Jua litatiwa giza, mwezi hautatoa nuru yake, nyota zitaanguka kutoka mbinguni, na nguvu za mbingu zitatikiswa.” (Mathayo 24:29) Mitume wanaosikiliza maneno hayo yanayoogopesha hawajui kikamili mambo yatakayotokea, lakini ni wazi kwamba yatakuwa yenye kushtua.
Matukio hayo yenye kushtua yatawaathirije wanadamu? Yesu anasema: “Watu watazimia kwa woga wakitarajia mambo yatakayotokea juu ya dunia inayokaliwa, kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa.” (Luka 21:26) Bila shaka, Yesu anafafanua kuhusu kipindi kigumu zaidi katika historia ya wanadamu.
Yesu anawatia moyo mitume wake anapowafunulia kwamba si watu wote watakaokuwa wakiomboleza ‘Mwana wa binadamu atakapokuja akiwa na nguvu na utukufu mwingi.’ (Mathayo 24:30) Tayari ametaja kwamba Mungu ataingilia kati “kwa sababu ya wale waliochaguliwa.” (Mathayo 24:22) Wanafunzi hao waaminifu wanapaswa kutendaje watakapoona mambo hayo yenye kushtua ambayo Yesu anazungumzia? Yesu anawatia moyo wafuasi wake hivi: “Mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni wima na kuinua vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu unakaribia.”—Luka 21:28.
Hata hivyo, wanafunzi wa Yesu wanaoishi katika kipindi hicho kilichotabiriwa watatambuaje kwamba mwisho umekaribia? Yesu anawapa mfano wa mtini: “Mara tu matawi yake machanga yanapokuwa laini na kuchipua majani, mnajua kwamba kiangazi kinakaribia. Vivyo hivyo, ninyi pia mtakapoona mambo yote hayo, jueni kwamba yuko karibu milangoni. Kwa kweli ninawaambia kizazi hiki hakitapitilia mbali kamwe mpaka mambo haya yote yatukie.”—Mathayo 24:32-34.
Kwa hiyo, wanafunzi wake wanapoona mambo mbalimbali ya ile ishara yakitimizwa, wanapaswa kutambua kwamba mwisho umekaribia. Akiwashauri wanafunzi ambao watakuwa hai wakati huo muhimu, Yesu anasema hivi:
“Kuhusu siku hiyo na saa hiyo, hakuna mtu anayejua, hata malaika wa mbinguni wala Mwana, ila Baba tu. Kwa maana kama siku za Noa zilivyokuwa, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa. Kwa maana kama walivyokuwa katika siku hizo kabla ya Gharika, wakila na kunywa, wanaume wakioa na wanawake wakiolewa, mpaka siku ambayo Noa aliingia ndani ya safina, nao hawakujali mpaka Gharika ikaja na kuwafagilia mbali wote, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa.” (Mathayo 24:36-39) Tukio ambalo Yesu anatumia kama mfano—Gharika ya kihistoria ya siku za Noa—liliathiri dunia nzima.
Bila shaka, mitume wanaomsikiliza Yesu kwenye Mlima wa Mizeituni wanatambua umuhimu wa kuendelea kuwa macho. Yesu anasema: “Jiangalieni wenyewe ili mioyo yenu isilemewe kamwe na kula na kunywa kupita kiasi na mahangaiko ya maisha, na siku ile iwakute ghafla kama mtego. Kwa maana itakuja juu ya wale wote wanaoishi juu ya uso wa dunia. Basi, endeleeni kukesha sikuzote mkiomba dua ili mfanikiwe kuponyoka mambo yote hayo ambayo lazima yatukie, na kusimama mbele ya Mwana wa binadamu.”—Luka 21:34-36.
Kwa mara nyingine tena, Yesu anawaonyesha kwamba mambo anayotabiri hayatatokea kwa kiwango kidogo. Hatabiri kuhusu matukio ambayo yatatokea miaka michache ijayo na yatakayoathiri jiji la Yerusalemu au taifa la Wayahudi peke yake. Hapana, anazungumzia mambo ambayo yatakuja “juu ya wale wote wanaoishi juu ya uso wa dunia.”
Anasema kwamba wanafunzi wake watahitaji kuendelea kuwa macho, kuendelea kukesha, na kuwa tayari. Yesu anakazia onyo hilo kwa mfano mwingine: “Jueni jambo hili: Ikiwa mwenye nyumba angejua mwizi atakuja katika kesha gani, angekaa macho na hangeruhusu nyumba yake ivunjwe. Kwa hiyo ninyi pia iweni tayari, kwa sababu Mwana wa binadamu atakuja saa msiyotazamia.”—Mathayo 24:43, 44.
Yesu anaendelea kuwapa wanafunzi wake sababu ya kuwa na tumaini. Anawahakikishia kwamba unabii wake utakapokuwa ukitimizwa, kutakuwa na “mtumwa” atakayekuwa macho na mwenye bidii. Yesu anazungumzia hali ambayo mitume wanaweza kuilewa kwa urahisi: “Kwa kweli ni nani mtumwa mwaminifu na mwenye busara ambaye bwana wake alimweka rasmi asimamie watumishi wake wa nyumbani na kuwapa chakula chao kwa wakati unaofaa? Mwenye furaha ni mtumwa huyo ikiwa bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo! Kwa kweli ninawaambia, atamweka rasmi asimamie mali zake zote.” Hata hivyo, “mtumwa” huyo akikuza mtazamo mwovu na kuanza kuwatesa wengine, bwana wake “atamwadhibu kwa ukali sana.”—Mathayo 24:45-51; linganisha na Luka 12:45, 46.
Hata hivyo, Yesu hasemi kwamba kikundi cha wafuasi wake kitakuwa na mtazamo mwovu. Hivyo basi, Yesu anataka kuwafundisha wanafunzi wake somo gani? Anataka wawe macho na wenye bidii, kama anavyoonyesha tena katika mfano mwingine.
-
-
Somo Kuhusu Kuwa Macho—MabikiraYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 112
Somo Kuhusu Kuwa Macho—Mabikira
YESU ATOA MFANO WA MABIKIRA KUMI
Yesu amekuwa akijibu maswali ya mitume wake kuhusu ishara ya kuwapo kwake na ya umalizio wa mfumo wa mambo. Akiwa na jambo hilo akilini, sasa anawapa himizo lenye hekima kwa kutumia mfano mwingine. Wale wanaoishi wakati wa kuwapo kwake wangeona utimizo wa mfano huo.
Anaanza kusimulia mfano huo hivi: “Ufalme wa mbinguni ni kama mabikira kumi waliochukua taa zao na kwenda kumpokea bwana harusi. Watano kati yao walikuwa wapumbavu, na watano walikuwa wenye busara.”—Mathayo 25:1, 2.
Yesu hamaanishi kwamba nusu ya wanafunzi wake wanaorithi Ufalme ni wapumbavu na nusu nyingine ni wenye busara. Badala yake, anamaanisha kwamba kuhusiana na Ufalme, kila mwanafunzi wake ana uwezo wa kuchagua kuwa macho au kukengeushwa. Hata hivyo, Yesu hana shaka kwamba kila mtumishi wake anaweza kuendelea kuwa mwaminifu na kupokea baraka kutoka kwa Baba yake.
Katika mfano huo, mabikira wote kumi wanaenda kumpokea bwana harusi na kujiunga na msafara wa harusi. Atakapowasili, mabikira watamwangazia njia kwa taa zao, wakimsifu anapomleta bibi harusi katika nyumba aliyotayarishiwa. Hata hivyo, hali inakuwaje?
Yesu anaeleza hivi: “Wale wapumbavu walibeba taa zao lakini hawakubeba mafuta, lakini wale wenye busara walibeba mafuta kwenye chupa zao pamoja na taa zao. Bwana harusi alipokawia kuja, wote walisinzia na kulala.” (Mathayo 25:3-5) Bwana harusi hafiki mapema kama ilivyotarajiwa. Inaonekana anachelewa sana, nao mabikira wanalala usingizi. Mitume wanaweza kukumbuka kwamba Yesu aliwasimulia kuhusu mwanamume fulani kutoka familia mashuhuri aliyesafiri na ‘mwishowe akarudi baada ya kupokea mamlaka ya kifalme.’—Luka 19:11-15.
Katika mfano wa mabikira kumi, Yesu anafafanua kile kinachotokea mwishowe bwana harusi anapowasili: “Katikati ya usiku kukatokea mwito, ‘Huyu hapa Bwana harusi! Nendeni mkamlaki.’” (Mathayo 25:6) Hali ya mabikira ikoje kuhusu kuwa tayari na kuwa macho?
Yesu anaendelea kusema: “Ndipo mabikira wote wakasimama na kuzitayarisha taa zao. Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, ‘Tugawieni mafuta yenu, kwa sababu taa zetu zinakaribia kuzimika.’ Wale wenye busara wakawajibu: ‘Labda hayatatutosha sisi sote. Nendeni kwa wauzaji mkajinunulie.’”—Mathayo 25:7-9.
Basi wale mabikira watano hawako macho na hawako tayari kwa ajili ya kuwasili kwa bwana harusi. Hawana mafuta ya kutosha kwa ajili taa zao nao wanahitaji kuyatafuta. Yesu anasimulia hivi: “Walipokuwa wakienda kununua mafuta, bwana harusi akaja. Mabikira waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye kwenye karamu ya ndoa, na mlango ukafungwa. Baadaye wale mabikira wengine pia wakaja, wakisema, ‘Bwana, Bwana, tufungulie!’ Akawajibu, ‘Kwa kweli ninawaambia, siwajui ninyi.’” (Mathayo 25:10-12) Hayo ni matokeo mabaya sana ya kutoendelea kuwa macho na kutokuwa tayari!
Mitume wanaweza kutambua kwamba bwana harusi ambaye Yesu anamtaja, ni Yesu mwenyewe. Hapo awali hata alijilinganisha na bwana harusi. (Luka 5:34, 35) Namna gani wale mabikira wenye busara? Alipokuwa akizungumza kuhusu “kundi dogo” ambao watapewa Ufalme, Yesu alitumia maneno haya: “Vaeni mavazi, muwe tayari na mwashe taa zenu.” (Luka 12:32, 35) Basi, katika mfano huu unaohusu mabikira, mitume wanaweza kuelewa kwamba Yesu anamaanisha wao wenyewe. Sasa Yesu anawasilisha ujumbe gani katika mfano huo?
Yesu hawaachi na shaka hata kidogo kuhusu jambo hilo. Anamalizia mfano wake kwa kusema: “Kwa hiyo, endeleeni kukesha kwa sababu hamjui ile siku wala saa.”—Mathayo 25:13.
Ni wazi kuwa Yesu anawahimiza wafuasi wake waaminifu kwamba kuhusu kuwapo kwake, watahitaji, ‘kuendelea kukesha.’ Yeye atakuja, nao wanapaswa kuwa tayari na kuwa macho—kama wale mabikira watano—ili wasije wakasahau tumaini lao lenye thamani na kukosa thawabu wanayoweza kupata.
-
-
Somo Kuhusu Bidii—TalantaYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 113
Somo Kuhusu Bidii—Talanta
YESU ATOA MFANO WA TALANTA
Yesu akiwa bado na mitume wake wanne kwenye Mlima wa Mizeituni, anawasimulia mfano mwingine. Siku chache zilizopita, alipokuwa Yeriko, alitoa mfano kuhusu mina ili kuonyesha kwamba Ufalme utakuja baadaye, wakati ujao. Mfano anaosimulia sasa una mambo kadhaa yanayofanana na mfano huo. Ni sehemu ya jibu lake kwa swali kuhusu kuwapo kwake na umalizio wa mfumo wa mambo. Unakazia kwamba lazima wanafunzi wake wafanye kwa bidii kazi anayowakabidhi.
Yesu anaanza hivi: “Ni kama mtu aliye karibu kusafiri ng’ambo, aliyewaita watumwa wake na kuwakabidhi mali zake.” (Mathayo 25:14) Kwa kuwa tayari Yesu alikuwa amejilinganisha na mtu fulani aliyesafiri kwenda ng’ambo ‘kupokea mamlaka ya kifalme,’ mitume wanaweza kuelewa kwamba Yesu ndiye “mtu fulani” anayezungumziwa sasa.—Luka 19:12.
Kabla mtu anayezungumziwa kwenye mfano huo hajasafiri kwenda ng’ambo, anawakabidhi watumwa wake vitu vyake vyenye thamani. Katika kipindi cha miaka mitatu na nusu cha huduma yake, Yesu alikazia fikira kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu, na kuwazoeza wanafunzi wake kufanya kazi hiyo. Sasa anaondoka akiwa na uhakika kwamba wataendelea kufanya kazi aliyowazoeza kufanya.—Mathayo 10:7; Luka 10:1, 8, 9; linganisha na Yohana 4:38; 14:12.
Katika mfano huo, mtu huyo anagawa mali zake jinsi gani? Yesu anasema hivi: “Akampa mmoja talanta tano, mwingine mbili, na mwingine moja, kila mtumwa kulingana na uwezo wake, kisha akaenda ng’ambo.” (Mathayo 25:15) Watumwa hao watafanya nini na mali waliyokabidhiwa? Je, watafanya kazi kwa bidii na kumletea bwana wao faida? Yesu anawaambia hivi mitume wake:
“Mara moja yule aliyepokea talanta tano akaenda kufanya biashara nazo, akapata talanta tano zaidi. Vivyo hivyo, yule aliyepokea mbili akapata talanta mbili zaidi. Lakini mtumwa aliyepokea moja tu akaenda akachimba shimo ardhini na kuficha zile pesa za bwana wake.” (Mathayo 25:16-18) Ni nini kitakachotokea bwana wao atakaporudi?
Yesu anaendelea kusema hivi: “Baada ya muda mrefu, bwana wa watumwa hao akarudi na kufanya hesabu nao.” (Mathayo 25:19) Wale wawili wa kwanza walifanya yote waliyoweza, “kila [mmoja] kulingana na uwezo wake.” Kila mtumwa alifanya kazi kwa bidii sana na kupata faida kutokana na kile alichokabidhiwa. Yule aliyepokea talanta tano alizalisha talanta tano nyingine, na aliyepokea talanta mbili alifanya vivyo hivyo. (Nyakati hizo, mfanyakazi angefanya kazi kwa miaka 19 ili apate kiasi kinacholingana na talanta moja.) Bwana wao anawapongeza hivi wote wawili: “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu katika mambo machache. Nitakuweka juu ya mambo mengi. Ingia katika shangwe ya bwana wako.”—Mathayo 25:21.
Hata hivyo, mambo ni tofauti kwa mtumwa aliyepokea talanta moja. Anasema hivi: “Bwana nilijua wewe ni mtu mgumu, ambaye huvuna mahali ambapo hukupanda na kukusanya mahali ambapo hukupepeta. Kwa hiyo, niliogopa nikaenda na kuficha talanta yako ardhini. Chukua mali yako.” (Mathayo 25:24, 25) Hata hakuweka pesa hizo benki ili kupata angalau faida kidogo kwa ajili ya bwana wake. Badala yake amemletea bwana wake hasara.
Kwa kufaa, bwana wake anamwita “mtumwa mwovu na mvivu.” Kile alicho nacho kinachukuliwa na kupewa mtumwa aliye tayari kufanya kazi kwa bidii. Bwana anaweka kanuni hii: “Kila mtu aliye na kitu ataongezewa, naye atakuwa na vitu vingi. Lakini mtu asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.”—Mathayo 25:26, 29.
Wanafunzi wa Yesu wana mambo mengi ya kufikiria, hata kuhusu mfano huu. Wanaweza kutambua kwamba kazi ambayo Yesu anawakabidhi ni yenye thamani sana, yaani, pendeleo kubwa la kufanya wanafunzi. Naye anatarajia wafanye kazi hiyo kwa bidii. Yesu hafikirii kwamba lazima wote watimize kiwango kilekile wanapofanya kazi ya kuhubiri ambayo amewaagiza wafanye. Kama alivyofafanua, kila mmoja anapaswa kufanya yote anayoweza “kulingana na uwezo wake.” Bila shaka, hilo halimaanishi kwamba Yesu atafurahi ikiwa mtu atakuwa “mvivu” na kukosa kujitahidi kabisa kuendeleza mali za Bwana.
Hata hivyo, lazima mitume wanafurahi sana wanapohakikishiwa hivi: “Kila mtu aliye na kitu ataongezewa”!
-
-
Kristo Akiwa na Mamlaka Awahukumu Kondoo na MbuziYesu—Njia, Kweli, na Uzima
-
-
SURA YA 114
Kristo Akiwa na Mamlaka ya Kifalme Awahukumu Kondoo na Mbuzi
YESU ATOA MFANO WA KONDOO NA MBUZI
Akiwa kwenye Mlima wa Mizeituni, Yesu ametoka tu kusimulia mfano wa mabikira kumi na mfano wa talanta. Anamaliziaje jibu lake kwa swali la mitume kuhusu ishara ya kuwapo kwake na ya umalizio wa mfumo wa mambo? Anamalizia kwa kutoa mfano wa mwisho, unaohusu kondoo na mbuzi.
Yesu anaanza kwa kueleza jinsi hali itakavyokuwa, anaposema: “Mwana wa binadamu atakapokuja katika utukufu wake, pamoja na malaika wote, ataketi kwenye kiti chake cha ufalme chenye utukufu.” (Mathayo 25:31) Hakuna shaka yoyote kwamba yeye, yaani, Yesu ndiye mhusika mkuu katika mfano huo. Mara nyingi amejiita “Mwana wa binadamu.”—Mathayo 8:20; 9:6; 20:18, 28.
Mfano huo utatimizwa wakati gani? Utatimizwa Yesu “atakapokuja katika utukufu wake” pamoja na malaika na kuketi kwenye “kiti chake cha ufalme chenye utukufu.” Tayari alikuwa amezungumza kuhusu “Mwana wa binadamu [kuja] juu ya mawingu ya mbinguni akiwa na nguvu na utukufu mwingi” pamoja na malaika zake. Jambo hilo lingetokea wakati gani? “Mara tu baada ya dhiki.” (Mathayo 24:29-31; Marko 13:26, 27; Luka 21:27) Basi, mfano huo utatimizwa wakati ujao Yesu atakapokuja akiwa na utukufu. Kisha atafanya nini?
Yesu anaeleza hivi: “Mwana wa binadamu atakapokuja . . . , mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu mmoja kutoka kwa mwenzake, kama vile mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi. Naye atawaweka kondoo kwenye mkono wake wa kuume, lakini mbuzi kwenye mkono wake wa kushoto.”—Mathayo 25:31-33.
Kuhusu kondoo ambao wanawekwa upande wenye kibali, Yesu anasema: “Ndipo Mfalme atawaambia wale walio kwenye mkono wake wa kuume: ‘Njooni, ninyi ambao mmebarikiwa na Baba yangu, urithini Ufalme uliotayarishwa kwa ajili yenu tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu.’” (Mathayo 25:34) Kwa nini kondoo wanapata kibali cha Mfalme?
Mfalme anaeleza hivi: “Nilikuwa na njaa mkanipa chakula; nilikuwa na kiu mkanipa kinywaji. Nilikuwa mgeni mkanikaribisha vizuri; nilikuwa uchi, mkanivika nguo. Nilikuwa mgonjwa mkanitunza. Nilikuwa gerezani mkanitembelea.” Kondoo hao, “waadilifu,” wanapomuuliza mfalme jinsi walivyofanya mambo hayo mazuri anawajibu hivi: “Kwa kadiri ambavyo mlimtendea aliye mdogo zaidi kati ya hawa ndugu zangu, mlinitendea mimi.” (Mathayo 25: 35, 36, 40, 46) Hawafanyi matendo hayo mazuri wakiwa mbinguni kwa maana huko hakuna wagonjwa au watu wenye njaa. Bila shaka, matendo hayo yanafanywa kwa ajili ya ndugu za Kristo hapa duniani.
Namna gani mbuzi ambao wanawekwa upande wa kushoto? Yesu anasema hivi: “Kisha [Mfalme] atawaambia wale walio kwenye mkono wake wa kushoto: ‘Ondokeni kwangu ninyi mliolaaniwa, nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika zake. Kwa maana nilikuwa na njaa, lakini hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu, lakini hamkunipa kinywaji. Nilikuwa mgeni, lakini hamkunikaribisha; nilikuwa uchi, lakini hamkunivika nguo; nilikuwa mgonjwa na nilikuwa gerezani lakini hamkunitunza.’” (Mathayo 25:41-43) Mbuzi wanastahili hukumu hiyo kwa sababu hawakuwatendea kwa fadhili ndugu za Kristo hapa duniani, kama walivyopaswa kufanya.
Mitume wanajifunza kwamba wakati huo ujao wa hukumu utakuwa na matokeo ya kudumu, yaani, ya milele. Yesu anawaambia: “Ndipo [Mfalme atawaambia]: ‘Kwa kweli ninawaambia, kwa kadiri ambavyo hamkumtendea mmoja wa hawa wadogo zaidi, hamkunitendea mimi.’ Hao watakatiliwa mbali milele, lakini waadilifu watapata uzima wa milele.”—Mathayo 25:45, 46.
Jibu la Yesu kwa swali la mitume linawapa wafuasi wake mambo mengi ya kufikiria, likiwasaidia kuchunguza mitazamo na matendo yao.
-