Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Kesi Mbele ya Sanhedrini, Kisha Apelekwa kwa Pilato
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Yesu asimama mbele ya Pilato

      SURA YA 127

      Kesi Mbele ya Sanhedrini, Kisha Apelekwa kwa Pilato

      MATHAYO 27:1-11 MARKO 15:1 LUKA 22:66–23:3 YOHANA 18:28-35

      • KESI ASUBUHI MBELE YA SANHEDRINI

      • YUDA ISKARIOTE ANAJARIBU KUJINYONGA

      • YESU APELEKWA KWA PILATO AKAHUKUMIWE

      Usiku unakaribia kwisha Petro anapomkana Yesu kwa mara ya tatu. Washiriki wa Sanhedrini wamemaliza kesi yao isiyo halali nao wametawanyika. Ijumaa asubuhi, wanakusanyika tena labda ili kufanya kesi waliyofanya usiku ionekane kuwa halali. Yesu analetwa mbele yao.

      Mahakama inauliza tena: “Ikiwa wewe ndiye Kristo, tuambie.” Yesu anajibu: “Hata nikiwaambia, hamtaamini hata kidogo. Isitoshe, ikiwa ningewauliza, hamngenijibu.” Hata hivyo, kwa ujasiri Yesu anawaonyesha utambulisho wake kama ilivyotabiriwa katika Danieli 7:13. Anasema: “Tangu sasa Mwana wa binadamu ataketi kwenye mkono wa kuume wenye nguvu wa Mungu.”—Luka 22:67-69; Mathayo 26:63.

      Wanasisitiza hivi: “Kwa hiyo, je, wewe ndiye Mwana wa Mungu?” Yesu anajibu: “Ninyi wenyewe mnasema kwamba mimi ndiye.” Inaonekana hilo linafanya iwe halali kumuua Yesu kwa kosa la kukufuru. “Kwa nini tutafute ushahidi zaidi?” wanauliza. (Luka 22:70, 71; Marko 14:64) Basi wanamfunga Yesu na kumpeleka kwa Gavana Mroma Pontio Pilato.

      Huenda Yuda Iskariote anamwona Yesu akipelekwa kwa Pilato. Yuda anapotambua kwamba Yesu amehukumiwa, anajuta na kukata tamaa. Hata hivyo, badala ya kumrudia Mungu na kutubu kikweli, anaenda kurudisha vile vipande 30 vya fedha. Yuda anawaambia hivi wakuu wa makuhani: “Nilitenda dhambi niliposaliti damu isiyo na hatia.” Lakini anajibiwa kwa ukali: “Hilo linatuhusuje? Shauri yako!”—Mathayo 27:4.

      Yuda anatupa vile vipande 30 vya fedha hekaluni na kisha anaongezea kosa lingine kwa kujaribu kujiua. Yuda anapojaribu kujinyonga, tawi la mti analofunga kamba linavunjika. Mwili wake unaanguka kwenye miamba iliyo chini na kupasuka.—Matendo 1:17, 18.

      Bado ni asubuhi na mapema Yesu anapopelekwa kwenye jumba la Pontio Pilato. Lakini Wayahudi wanaompeleka huko wanakataa kuingia ndani. Wanafikiri kwamba watakuwa najisi wakishirikiana na watu wa mataifa. Jambo hilo litafanya wasistahili kula mlo siku ya Nisani 15, siku ya kwanza ya Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu, ambayo huonwa kuwa sehemu ya kipindi cha Pasaka.

      Pilato anatoka na kuwauliza: “Mna mashtaka gani kumhusu mtu huyu?” Wanajibu hivi: “Kama mtu huyu hangekuwa mkosaji, hatungemkabidhi kwako.” Huenda Pilato anahisi kwamba wanajaribu kumlazimisha, basi anasema hivi: “Mchukueni mkamhukumu kulingana na sheria yenu.” Wayahudi wanafunua lengo lao la kutaka kumuua, wanasema: “Si halali kwetu kumuua mtu yeyote.”—Yohana 18:29-31.

      Kwa kweli, wakimuua Yesu wakati wa sherehe ya Pasaka, jambo hilo litasababisha vurugu kati ya watu. Lakini wakifanya Waroma wamuue Yesu kwa mashtaka ya kisiasa, kwa kuwa Waroma wana mamlaka ya kufanya hivyo, hilo litasaidia kuzuia Wayahudi hao wasilaumiwe na watu.

      Viongozi hao wa kidini hawamwambii Pilato kwamba wamemhukumu Yesu kwa kukufuru. Sasa wanamshtaki kwa makosa mengine: “Tulimkuta mtu huyu [1] akipindua taifa letu na [2] kuwakataza watu wasimlipe Kaisari kodi, [3] akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo mfalme.”—Luka 23:2.

      Akiwa mwakilishi wa Roma, Pilato ana sababu ya kuhangaikia shtaka kwamba Yesu anadai kuwa mfalme. Basi anaingia tena kwenye jumba la mfalme, anamwita Yesu na kumuuliza: “Je, wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?” Kwa maneno mengine, ‘Je, umevunja sheria ya milki kwa kujitangaza kuwa mfalme ili kumpinga Kaisari?’ Labda ili ajue mambo ambayo tayari Pilato amesikia kumhusu, Yesu anauliza: “Je, unauliza hivyo kwa kujitungia, au uliambiwa na watu wengine kunihusu?”—Yohana 18:33, 34.

      Akionyesha kwamba hajui mengi kumhusu Yesu, lakini anataka kujua, Pilato anajibu: “Mimi si Myahudi, sivyo?” Anaongezea hivi: “Taifa lako na wakuu wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Ulifanya nini?”—Yohana 18:35.

      Yesu hajaribu kuepuka suala muhimu—ufalme. Anajibu kwa njia ambayo bila shaka inamshangaza Gavana Pilato.

      SHAMBA LA DAMU

      Yuda anatupa vipande 30 vya fedha hekaluni

      Makuhani wakuu hawajui watafanya nini na vile vipande vya fedha ambavyo Yuda alivitupa hekaluni. Wanasema hivi: “Si halali [kuviweka] katika hazina takatifu, kwa sababu ni bei ya damu.” Basi wanatumia pesa hizo kununua shamba la mfinyanzi kwa ajili ya kuzika wageni. Baadaye likajulikana kama “Shamba la Damu.”—Mathayo 27:6-8.

      • Kwa nini washiriki wa Sanhedrini wanakutana tena asubuhi?

      • Yuda anakufa jinsi gani, na vile vipande 30 vya fedha vinatumiwa kufanya nini?

      • Wayahudi wanataka Pilato aagize Yesu auawe kwa mashtaka gani?

  • Pilato na Herode Wakosa Kumpata na Hatia
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Herode na wanajeshi wake wakimdhihaki Yesu

      SURA YA 128

      Pilato na Herode Wakosa Kumpata na Hatia

      MATHAYO 27:12-14, 18, 19 MARKO 15:2-5 LUKA 23:4-16 YOHANA 18:36-38

      • YESU AHOJIWA NA PILATO NA HERODE

      Yesu hajaribu kumficha Pilato kwamba kwa kweli yeye ni mfalme. Hata hivyo, Ufalme wake si tishio kwa Roma. “Ufalme wangu si sehemu ya ulimwengu huu,” Yesu anasema. “Kama Ufalme wangu ungekuwa sehemu ya ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini, kama ilivyo, Ufalme wangu hautoki katika chanzo hiki.” (Yohana 18:36) Naam, Yesu ana Ufalme, lakini si sehemu ya ulimwengu huu.

      Pilato hapuuzi jambo hilo. Anauliza hivi: “Kwa hiyo, wewe ni mfalme?” Yesu anataka Pilato ajue kwamba jibu lake ni sahihi, anaposema: “Wewe mwenyewe unasema kwamba mimi ni mfalme. Nimezaliwa kwa ajili ya hili, na kwa ajili ya hili nimekuja ulimwenguni, ili nitoe ushahidi kuhusu kweli. Kila mtu aliye upande wa kweli huisikiliza sauti yangu.”—Yohana 18:37.

      Hapo awali Yesu alikuwa amemwambia hivi Tomasi: “Mimi ndiye njia na kweli na uzima.” Sasa hata Pilato anasikia kwamba kusudi la Yesu kutumwa duniani ni ili kutoa ushahidi kuhusu “kweli,” hasa kweli kuhusu Ufalme wake. Yesu ameazimia kushikamana na kweli hiyo hata kama itamgharimu uhai wake. Pilato anauliza: “Kweli ni nini?” lakini hasubiri ufafanuzi zaidi. Anafikiri kwamba mambo aliyosikia yanatosha kumhukumu mtu huyu.—Yohana 14:6; 18:38.

      Pilato anarudi kuongea na umati unaosubiri nje ya jumba la mfalme. Inaonekana Yesu yuko kando yake anapowaambia hivi wakuu wa makuhani na wale wote walio pamoja nao: “Sioni mtu huyu akiwa na kosa lolote.” Umati ukiwa umekasirishwa na uamuzi huo, unasisitiza hivi: “Anawachochea watu kwa kufundisha katika Yudea yote, kuanzia Galilaya mpaka hapa.”—Luka 23:4, 5.

      Lazima Pilato anashangazwa na ushupavu wa Wayahudi usio na msingi. Wakuu wa makuhani na wanaume wazee wanapoendelea kupaza sauti, Pilato anamuuliza Yesu: “Je, husikii ni mambo mangapi wanayoshuhudia dhidi yako?” (Mathayo 27:13) Yesu hatoi jibu lolote. Utulivu wake anapokabili mashtaka ya uwongo unamshangaza Pilato.

      Wayahudi walisema kwamba Yesu ‘alianzia Galilaya.’ Pilato anapofuatilia jambo hilo, anagundua kwamba kwa kweli Yesu ni Mgalilaya. Hilo linampa Pilato wazo la jinsi anavyoweza kuepuka jukumu la kumhukumu Yesu. Herode Antipa (Mwana wa Herode Mkuu) ndiye mtawala wa Galilaya, naye yuko Yerusalemu majira hayo ya Pasaka. Basi Pilato anaagiza Yesu apelekwe kwa Herode. Herode Antipa ndiye aliyeamuru Yohana Mbatizaji akatwe kichwa. Baadaye aliposikia kwamba Yesu alikuwa anafanya miujiza, Herode alikuwa na wasiwasi kwamba huenda Yesu ni Yohana ambaye amefufuka kutoka kwa wafu.—Luka 9:7-9.

      Sasa Herode anafurahi anapotazamia kumwona Yesu. Si kwamba anataka kumsaidia Yesu au anataka kujua kama kweli kuna mashtaka halali dhidi yake. Kwa ufupi, Herode ni mdadisi, naye ‘anatamani kumwona akifanya miujiza.’ (Luka 23:8) Hata hivyo, Yesu hatoshelezi udadisi wa Herode. Kwa kweli, Herode anapomuuliza maswali, Yesu hajibu. Herode na wanajeshi wake wakiwa wamekasirika, wanamtendea Yesu “kwa dharau.” (Luka 23:11) Wanamvika vazi la kifahari na kumdhihaki. Kisha Herode anaagiza Yesu arudishwe kwa Pilato. Herode na Pilato walikuwa maadui, lakini sasa wanakuwa marafiki.

      Yesu anaporudi, Pilato anawaita pamoja wakuu wa makuhani, viongozi wa Wayahudi, na watu wote na kusema: “Nilimhoji mbele yenu lakini sikupata msingi wa mashtaka yenu dhidi yake. Kwa kweli, hata Herode hakupata, ndiyo maana alimrudisha kwetu, tazama! ni wazi hajafanya jambo lolote linalostahili kifo. Kwa hiyo nitamwadhibu na kumfungua.”—Luka 23:14-16.

      Pilato anataka kumweka Yesu huru, kwa kuwa anagundua kwamba makuhani wamemleta kwake kwa sababu ya wivu. Pilato anapojaribu kumweka Yesu huru, anapata sababu nyingine inayomchochea kufanya hivyo. Akiwa kwenye kiti chake cha hukumu, mke wake anamtumia ujumbe huu: “Mwache mtu huyo mwadilifu, kwa maana niliteseka sana leo katika ndoto [inaonekana ilitoka kwa Mungu] kwa sababu yake.”—Mathayo 27:19.

      Pilato anawezaje kumweka huru mtu huyu asiye na hatia, kama anavyopaswa kufanya?

      • Yesu anasema “kweli” jinsi gani kuhusu yeye kuwa mfalme?

      • Pilato anafanya uamuzi gani kumhusu Yesu, watu wanaitikiaje, naye Pilato anafanya nini?

      • Kwa nini Herode Antipa anafurahi kumwona Yesu, naye anamtendeaje?

      • Kwa nini Pilato anataka kumweka Yesu huru?

  • Pilato Asema: “Tazama! Mwanamume!
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Yesu, akiwa amevaa taji la miiba na joho la zambarau anatolewa nje na Pilato

      SURA YA 129

      Pilato Asema: “Tazama! Mwanamume!”

      MATHAYO 27:15-17, 20-30 MARKO 15:6-19 LUKA 23:18-25 YOHANA 18:39–19:5

      • PILATO AJARIBU KUMWEKA YESU HURU

      • WAYAHUDI WAOMBA BARABA AACHILIWE

      • YESU ADHIHAKIWA NA KUTESWA

      Pilato aliuambia hivi umati unaotaka Yesu auawe: “Sikupata msingi wa mashtaka yenu dhidi yake. Kwa kweli, hata Herode hakupata.” (Luka 23:14, 15) Sasa ili kujaribu kumlinda Yesu, Pilato anatumia njia nyingine, anawaambia hivi watu: “Mna desturi kwamba niwafungulie mtu siku ya Pasaka. Basi, mnataka niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?”—Yohana 18:39.

      Pilato ana habari kuhusu mfungwa anayeitwa Baraba, anayejulikana kuwa mwizi, mchochezi, na muuaji. Basi Pilato anauliza: “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu anayeitwa Kristo?” Wakichochewa na wakuu wa makuhani, watu wanaomba Baraba afunguliwe bali si Yesu. Pilato anauliza tena: “Mnataka niwafungulie nani kati ya hawa wawili?” Umati unapaza sauti: “Baraba”!—Mathayo 27:17, 21.

      Akiwa amefadhaika, Pilato anauliza: “Basi, nifanye nini na Yesu anayeitwa Kristo?” Watu wanasema kwa sauti kubwa: “Atundikwe mtini!” (Mathayo 27:22) Bila aibu, wanataka mtu asiye na hatia auawe. Pilato anawauliza: “Kwa nini? Amefanya kosa gani? Mimi sikuona jambo lolote linalofanya astahili kifo; kwa hiyo nitamwadhibu kisha nimfungue.”—Luka 23:22.

      Licha ya jitihada nyingi za Pilato, umati wenye hasira unapaza sauti hivi kwa pamoja: “Atundikwe mtini!” (Mathayo 27:23) Viongozi wa kidini wameuchochea sana umati huo hivi kwamba wanataka kumwaga damu! Na si damu ya mhalifu fulani, wala muuaji fulani. Ni damu ya mtu asiye na hatia ambaye siku tano zilizopita alikaribishwa Yerusalemu kama Mfalme. Ikiwa wanafunzi wa Yesu wako hapo, wanakaa kimya na kuwa waangalifu.

      Pilato anaona kwamba maombi yake yanakataliwa. Vurugu zinaanza kutokea, basi anachukua maji na kunawa mikono yake mbele ya umati. Anawaambia: “Mimi sina hatia ya damu ya mtu huyu. Shauri yenu.” Ingawa hivyo, watu hawabadili mtazamo wao. Badala yake wanasema: “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu.”—Mathayo 27:24, 25.

      Gavana huyo anataka kuwafurahisha watu hao badala ya kufanya kile anachojua kwamba ni haki. Basi kulingana na ombi la umati, Pilato anamweka huru Baraba. Anaagiza Yesu avuliwe nguo na kisha apigwe mijeledi.

      Baada ya kupigwa na kuteswa sana, wanajeshi wanampeleka Yesu kwenye jumba la gavana. Kikosi cha wanajeshi kinakusanyika na kumtendea vibaya hata zaidi. Wanasokota taji la miiba na kulikandamiza juu ya kichwa chake. Pia, wanajeshi wanaweka utete kwenye mkono wa kuume wa Yesu na kumvika vazi la zambarau, kama lile linalovaliwa na wafalme. Wanasema hivi kwa dharau: “Salamu, ewe Mfalme wa Wayahudi!” (Mathayo 27:28, 29) Zaidi ya hayo, wanamtemea mate na kumpiga makofi usoni. Wanauchukua utete alioshika mkononi, wanampiga nao kichwani, na hivyo kufanya adungwe zaidi na miiba mikali iliyo kwenye “taji” walilomvisha kichwani ili kumshushia heshima.

      Yesu anajiendesha kwa heshima na uthabiti licha ya hayo yote hivi kwamba Pilato anafanya jaribio lingine la kujiondolea lawama, akisema: “Ona! Namtoa nje kwenu ili mjue kwamba sijampata na kosa lolote.” Je, Pilato anafikiri kwamba sasa akimtoa Yesu nje akiwa amechubuka na akivuja damu, umati utamhurumia? Yesu anaposimama mbele ya umati wenye hasira, Pilato anasema: “Tazama! Mwanamume!”—Yohana 19:4, 5.

      Ingawa amepigwa na kuumizwa, Yesu anatenda kwa heshima na utulivu hivi kwamba hata Pilato anatambua jambo hilo, kwa kuwa maneno yake yanaonyesha heshima na huruma.

      KUPIGWA MIJELEDI

      Kiboko kilichotumiwa kupiga mijeledi

      Dakt. William D. Edwards katika kitabu The Journal of the American Medical Association anafafanua desturi ya Waroma ya kupiga mijeledi:

      “Kwa kawaida kifaa kilichotumiwa ni kiboko kifupi (flagramu au flagelamu) chenye kamba kadhaa za ngozi zenye urefu mbalimbali, kamba mojamoja au zilizosokotwa, ambazo zilifungwa vipande vidogo vya chuma au vipande vya mifupa ya kondoo vilivyoachana na vilivyokuwa na ncha kali. . . . Wanajeshi Waroma walipompiga kwa nguvu zote mfungwa mgongoni kwa kurudia rudia, vile vipande vya chuma vingesababisha michubuko yenye kina kirefu, na zile kamba za ngozi na mifupa ya kondoo ingekata ngozi na sehemu zilizo chini ya ngozi. Kisha, walipoendelea kumpiga mijeledi, majeraha yalipasuka kufikia kwenye misuli na kutokeza nyuzinyuzi zinazoning’inia za minofu inayotoka damu.”

      • Pilato anajaribuje kumweka Yesu huru na hivyo kujiondolea lawama?

      • Kupigwa mijeledi kulihusisha nini?

      • Baada ya Yesu kupigwa mijeledi, anatendewaje vibaya hata zaidi?

  • Yesu Akabidhiwa na Kupelekwa Akauawe
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Yesu akijaribu kubeba mti mzito wa mateso, na wanajeshi wanamwamuru Simoni wa Kirene aubebe kwa ajili yake

      SURA YA 130

      Yesu Akabidhiwa na Kupelekwa Akauawe

      MATHAYO 27:31, 32 MARKO 15:20, 21 LUKA 23:24-31 YOHANA 19:6-17

      • PILATO AJARIBU KUMWEKA YESU HURU

      • YESU AHUKUMIWA NA KUPELEKWA KUUAWA

      Licha ya kwamba Yesu amenyanyaswa kikatili na kudhihakiwa, jitihada za Pilato za kumweka huru haziwafanyi wakuu wa makuhani na wenzao wabadili mawazo. Hawataki jambo lolote lizuie Yesu asiuawe. Wanaendelea kupaza sauti: “Atundikwe mtini! Atundikwe mtini!” Pilato anajibu: “Mchukueni mkamuue ninyi wenyewe, kwa maana mimi sijampata na kosa lolote.”—Yohana 19:6.

      Wayahudi wanashindwa kumsadikisha Pilato kwamba Yesu anapaswa kuuawa kwa mashtaka ya kisiasa, lakini namna gani mashtaka ya kidini? Wanarudia mashtaka yaliyohusu kukufuru ambayo yalizushwa katika kesi ya Yesu mbele ya Sanhedrini. Wanasema hivi: “Sisi tuna sheria, na kulingana na sheria anapaswa kufa, kwa sababu alijifanya kuwa mwana wa Mungu.” (Yohana 19:7) Pilato anasikia kuhusu mashtaka hayo kwa mara ya kwanza.

      Anarudi kwenye jumba lake la kifalme na kujaribu kutafuta njia ya kumwachilia mtu huyu ambaye amevumilia mateso makali na ambaye mke wa Pilato aliota ndoto kumhusu. (Mathayo 27:19) Namna gani kuhusu mashtaka hayo mapya ya Wayahudi—kwamba mfungwa huyo ni “mwana wa Mungu”? Pilato anajua kwamba Yesu anatoka Galilaya. (Luka 23:5-7) Lakini anamuuliza Yesu: “Umetoka wapi?” (Yohana 19:9) Je, inawezekana kwamba Pilato anajiuliza ikiwa Yesu amewahi kuishi zamani, na kwa njia fulani anatokana na Mungu?

      Pilato alisikia moja kwa moja kutoka kwa Yesu kwamba yeye ni mfalme lakini Ufalme wake si sehemu ya ulimwengu huu. Yesu haoni haja ya kufafanua jambo alilosema hapo awali, basi anakaa kimya. Yesu anapokosa kujibu, Pilato anaona kwamba anadharuliwa, na kwa hasira anamwambia hivi Yesu: “Unakataa kuzungumza nami? Je, hujui kwamba nina mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukuua?”—Yohana 19:10.

      Kwa ufupi Yesu anasema: “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Ndiyo maana mtu aliyenitia mikononi mwako ana dhambi kubwa zaidi.” (Yohana 19:11) Inawezekana kwamba Yesu hazungumzii mtu mmoja tu. Badala yake anamaanisha kwamba Kayafa, wenzake, na Yuda Iskariote wana lawama kuliko Pilato.

      Akiwa amevutiwa na utulivu na maneno ya Yesu, na hofu kwamba huenda Yesu ametoka kwa Mungu, Pilato anajiribu tena kumweka huru. Hata hivyo, Wayahudi wanatokeza jambo lingine ambalo lazima linamtia Pilato hofu. Wanamtisha hivi: “Ukimfungua mtu huyu, wewe si rafiki ya Kaisari. Kila mtu anayejifanya mfalme anasema vibaya kumhusu Kaisari.”—Yohana 19:12.

      Gavana huyo anamtoa Yesu nje tena, na akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, anawaambia hivi watu: “Oneni! Mfalme wenu!” Hata hivyo, Wayahudi hawabadili mawazo yao. Wanapaza sauti hivi: “Mwondoe! Mwondoe! Atundikwe mtini!” Pilato anawauliza: “Je, mnataka nimuue mfalme wenu?” Kwa muda mrefu Wayahudi wamekandamizwa na utawala wa Waroma, lakini wakuu wa makuhani wanajibu: “Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.”—Yohana 19:14, 15.

      Kwa woga, Pilato anakubali maombi ya Wayahudi wanaosisitiza, naye anamkabidhi Yesu akauawe. Wanajeshi wanamvua Yesu lile vazi la zambarau na kumvika mavazi yake ya nje. Yesu anapoondoka, analazimika kuubeba mti wake wa mateso.

      Sasa ni Ijumaa asubuhi, Nisani 14. Yesu amekuwa macho tangu Alhamisi asubuhi na mapema na amepatwa na mateso mengi yenye kuumiza. Yesu anapojaribu kuubeba ule mti, anaishiwa na nguvu. Basi, wanajeshi wanamlazimisha mpita njia anayeitwa Simoni kutoka Kirene huko Afrika, aubebe mti mpaka kwenye eneo la kuuawa. Watu wengi wanafuata, baadhi yao wakijipigapiga kwa huzuni na kuomboleza jambo linalotendeka.

      Yesu anawaambia hivi wanawake wanaoomboleza: “Binti za Yerusalemu, acheni kunililia. Bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu; kwa maana tazama! siku zinakuja ambapo watu watasema, ‘Wenye furaha ni wanawake walio tasa, na matiti ambayo hayakunyonyesha!’ Ndipo wataanza kuiambia milima, ‘Tuangukieni!’ na vilima, ‘Tufunikeni!’ Ikiwa wanafanya mambo haya wakati mti ni mbichi, itakuwaje utakapokauka?”—Luka 23:28-31.

      Yesu anazungumza kuhusu taifa la Wayahudi. Ni kama mti unaokufa ambao bado una umajimaji, kwa kuwa bado Yesu yuko na pia baadhi ya Wayahudi wanaomwamini. Watu hao watakapoondolewa kutoka katika taifa hilo, taifa la kiroho lililokauka ndilo litakalobaki, kama mti uliokufa. Kutakuwa na kilio kikubwa majeshi ya Waroma yatakapotumiwa na Mungu kuliangamiza taifa hilo!

      • Viongozi wa kidini wanatoa mashtaka gani dhidi ya Yesu?

      • Kwa nini Pilato anaanza kuogopa?

      • Wakuu wa makuhani wanafauluje kumfanya Pilato aagize Yesu auawe?

      • Yesu anamaanisha nini anapotaja mti ‘mbichi’ kisha mti ‘uliokauka’?

  • Mfalme Asiye na Hatia Ateseka Kwenye Mti
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Yesu anamwahidi mhalifu aliyetundikwa pamoja naye, “Utakuwa pamoja nami katika Paradiso”

      SURA YA 131

      Mfalme Asiye na Hatia Ateseka Kwenye Mti

      MATHAYO 27:33-44 MARKO 15:22-32 LUKA 23:32-43 YOHANA 19:17-24

      • YESU ATUNDIKWA KWENYE MTI

      • ISHARA ILIYOBANDIKWA JUU YA KICHWA CHA YESU YALETA DHIHAKA

      • YESU AMPA MHALIFU TUMAINI LA KUISHI KATIKA PARADISO DUNIANI

      Yesu anapelekwa katika eneo lisilo mbali sana na jiji, mahali ambapo yeye na wahalifu wawili watauawa. Mahali hapo panaitwa Golgotha, au Mahali pa Fuvu la Kichwa, na panaonekana “kwa mbali.”—Marko 15:40.

      Wanaume hao watatu waliohukumiwa wanavuliwa nguo. Kisha wanapewa divai iliyotiwa manemane na nyongo chungu. Inaonekana wanawake kutoka Yerusalemu wameandaa mchanganyiko huo, na Waroma hawawakatazi kuwapa wale wanaouawa kinywaji hicho cha kutuliza maumivu. Hata hivyo, Yesu anapoonja, anakataa kukinywa. Kwa nini? Anataka awe na uwezo kamili wa kufikiri wakati wa jaribu hili kubwa; hataki kupoteza fahamu na anataka kuwa mwaminifu mpaka kifo.

      Yesu ananyooshwa kwenye mti. (Marko 15:25) Wanajeshi wanagonga misumari kwenye mikono na miguu yake, wakichoma minofu na misuli, na kumsababishia maumivu makali. Mti unaposimamishwa wima, maumivu yanakuwa makali hata zaidi uzito wa mwili wa Yesu unapopasua majeraha. Lakini Yesu hawashutumu wanajeshi. Anasali hivi: “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui wanachofanya.”—Luka 23:34.

      Waroma wana desturi ya kubandika ishara inayoonyesha kosa la mhalifu aliyehukumiwa. Wakati huu, Pilato amebandika ishara iliyoandikwa: “Yesu Mnazareti Mfalme wa Wayahudi.” Imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki, basi kila mtu anaweza kusoma. Kwa kufanya hivyo, Pilato anaonyesha kwamba anawadharau Wayahudi waliosisitiza Yesu auawe. Wakuu wa makuhani wakiwa wamekasirika wanapinga: “Usiandike, ‘Mfalme wa Wayahudi,’ andika kwamba alisema, ‘Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’” Hata hivyo, ili wasimsumbue tena, Pilato anajibu: “Yale ambayo nimeandika, nimeandika.”—Yohana 19:19-22.

      Wakiwa wamekasirika, makuhani wanarudia ushahidi wa uwongo uliotolewa hapo awali wakati wa kesi mbele ya Sanhedrini. Haishangazi kwamba wapita njia wanatikisa vichwa vyao wakimdhihaki na kumtukana: “Aha! Wewe uliyetaka kuliangusha chini hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe kwa kushuka kutoka kwenye mti wa mateso.” Pia, wakuu wa makuhani na waandishi wanaambiana hivi: “Acheni Kristo, Mfalme wa Israeli, ashuke sasa kutoka kwenye mti wa mateso, ili tuone na kuamini.” (Marko 15:29-32) Hata wahalifu waliohukumiwa walio upande wa Yesu wa kushoto na kulia wanamshutumu, ingawa kwa kweli yeye peke yake ndiye asiye na hatia.

      Pia, wanajeshi wanne Waroma wanamdhihaki Yesu. Huenda walikuwa wakinywa divai kali, sasa wanamdhihaki kwa kuiweka mbele ya Yesu, ambaye kwa kweli hawezi kuifikia na kunywa. Kwa dhihaka Waroma wanazungumzia ishara iliyo juu ya kichwa cha Yesu na kusema: “Ikiwa wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi, jiokoe.” (Luka 23:36, 37) Hebu fikiria! Mtu ambaye amethibitika kuwa njia, kweli, na uzima, sasa anatukanwa na kudhihakiwa isivyostahili. Hata hivyo, anakabili mateso hayo yote bila kuwashutumu Wayahudi wanaomtazama, wanajeshi Waroma wanaomdhihaki, au wale wahalifu wawili waliohukumiwa ambao wametundikwa kando yake.

      Wanajeshi wanapigia kura vazi la ndani la Yesu

      Wale wanajeshi wanne wamechukua mavazi ya nje ya Yesu na kuyagawa vipande vinne. Wanapiga kura ili kugawana vipande hivyo. Hata hivyo, vazi la ndani la Yesu lina ubora sana, “halikuwa na mshono, lilikuwa limefumwa kutoka juu mpaka chini.” Wanajeshi wanaambiana: “Tusilirarue, badala yake tupige kura ili tuamue litakuwa la nani.” Basi wanatimiza andiko linalosema: “Waligawana mavazi yangu, na wakalipigia kura vazi langu.”—Yohana 19:23, 24; Zaburi 22:18.

      Baada ya muda, mmoja kati ya wale wahalifu anatambua kwamba kwa kweli Yesu ni mfalme. Anamkemea mwenzake kwa kumwambia: “Je, wewe humwogopi Mungu hata kidogo, kwa kuwa umepata hukumu ileile? Sisi tunastahili kuteseka kwa sababu ya makosa tuliyofanya; lakini mtu huyu hakufanya kosa lolote.” Kisha anamsihi Yesu hivi: “Unikumbuke utakapoingia katika Ufalme wako.”—Luka 23:40-42.

      Yesu anamjibu hivi: “Kwa kweli ninakuambia leo, utakuwa pamoja nami,” si katika Ufalme, bali “katika Paradiso.” (Luka 23:43) Ahadi hiyo inatofautiana na ahadi aliyowapa mitume wake, kwamba wataketi pamoja naye kwenye viti vya ufalme katika Ufalme. (Mathayo 19:28; Luka 22:29, 30) Hata hivyo, huenda mhalifu huyo Myahudi amesikia kuhusu Paradiso ya duniani ambayo hapo mwanzoni Yehova aliwapa Adamu, Hawa, na wazao wao iwe makao yao. Sasa mhalifu huyo atakufa akiwa na tumaini hilo.

      • Kwa nini Yesu anakataa kunywa divai anayopewa?

      • Ni ishara gani inayobandikwa juu ya kichwa cha Yesu, na Wayahudi wanatendaje kuihusu?

      • Unabii unatimizwaje kuhusiana na jinsi wanajeshi wanavyogawana mavazi ya Yesu?

      • Yesu anampa tumaini gani mmoja wa wale wahalifu?

  • “Hakika Mtu Huyu Alikuwa Mwana wa Mungu”
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Baada ya Yesu kufa pamoja na wale wahalifu wawili, ofisa wa jeshi anasema: “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu”

      SURA YA 132

      “Hakika Mtu Huyu Alikuwa Mwana wa Mungu”

      MATHAYO 27:45-56 MARKO 15:33-41 LUKA 23:44-49 YOHANA 19:25-30

      • YESU AFA KWENYE MTI

      • MATUKIO YASIYO YA KAWAIDA WAKATI WA KIFO CHA YESU

      Sasa ni “saa sita” mchana. Kunakuwa na giza lisilo la kawaida “katika nchi yote mpaka saa tisa” alasiri. (Marko 15:33) Giza hilo linalotisha halijasababishwa na kupatwa kwa jua ambako hutokea wakati wa mwezi mpya. Haya ni majira ya Pasaka, mwezi unapokuwa mpevu. Na giza hilo linakaa muda mrefu kuliko dakika chache za kupatwa kwa jua. Basi Mungu ndiye amesababisha giza hilo!

      Wazia jinsi wale waliokuwa wakimdhihaki Yesu wanavyohisi. Wakati wa giza hilo wanawake wanne wanaenda kwenye mti wa mateso. Nao ni mama ya Yesu, Salome, Maria Magdalene, na Maria mama ya mtume Yakobo Mdogo.

      Mtume Yohana yuko na mama ya Yesu anayeomboleza “kando ya mti wa mateso.” Maria anamtazama mwana aliyemzaa na kumlea akining’inia akiwa na maumivu makali. Ni kama Maria anachomwa kwa “upanga mrefu.” (Yohana 19:25; Luka 2:35) Hata hivyo, licha ya maumivu makali, Yesu anafikiria hali njema ya mama yake. Anajitahidi kutikisa kichwa kumwelekea Yohana na kumwambia mama yake: “Mwanamke, ona! Mwanao!” Kisha anatikisa kichwa kumwelekea Maria na kumwambia Yohana: “Ona! Mama yako!”—Yohana 19:26, 27.

      Yesu anamkabidhi mtume anayempenda sana kazi ya kumtunza mama yake ambaye sasa inaelekea ni mjane. Yesu anajua kwamba ndugu zake wa kambo, wana wengine wa Maria, bado hawajamwamini Yesu. Basi anafanya maandalizi kwa ajili ya mahitaji ya kimwili na pia ya kiroho ya mama yake. Huo ni mfano mzuri sana!

      Giza linapokaribia kwisha, Yesu anasema: “Nina kiu.” Kwa kusema hivyo, anatimiza maandiko. (Yohana 19:28; Zaburi 22:15) Yesu anahisi kwamba Baba yake amemwondolea ulinzi ili utimilifu wa Mwana wake ujaribiwe kikamili. Kristo anapaza kilio kwa maneno haya ambayo huenda ni ya Kiaramu cha Galilaya: “Eli, Eli, lama sabakthani?” maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?” Baadhi ya watu waliosimama hapo karibu hawamwelewi, basi wanasema kwa sauti kubwa: “Sikia! Anamwita Eliya.” Mmoja wao anakimbia na kuweka sifongo katika divai kali kwenye utete, anampa Yesu anywe. Lakini wengine wanasema: “Mwacheni! Acheni tuone kama Eliya atakuja kumshusha.”—Marko 15:34-36.

      Kisha Yesu anapaza sauti hivi: “Imetimizwa!” (Yohana 19:30) Naam, ametimiza mambo yote ambayo Baba yake alimtuma kufanya duniani. Mwishowe Yesu anasema: “Baba, naiweka roho yangu mikononi mwako.” (Luka 23:46) Hivyo, Yesu anamkabidhi Yehova nguvu za uhai wake, akiwa na uhakika kwamba Mungu atamrudishia. Akimtegemea kabisa Mungu, Kristo anainamisha kichwa chake na kufa.

      Wakati huo, tetemeko kali la ardhi linatokea na kuvunja miamba. Lina nguvu sana hivi kwamba makaburi yaliyo nje ya Yerusalemu yanafunguka na maiti zinatupwa nje. Wapita njia wanapoona maiti zilizofukuliwa wanaingia “katika jiji takatifu” nao wanatoa taarifa kuhusu kilichotokea.—Mathayo 12:11; 27:51-53.

      Yesu anapokufa, pazia refu na zito linalotenganisha Patakatifu na Patakatifu Zaidi katika hekalu la Mungu linapasuka mara mbili, kuanzia juu mpaka chini. Tukio hilo la kushangaza linaonyesha hasira ya Mungu dhidi ya wale waliomuua Mwana wake na linamaanisha kwamba njia ya kwenda Patakatifu Zaidi, yaani mbinguni kwenyewe, sasa imefunguliwa.—Waebrania 9:2, 3; 10:19, 20.

      Kwa kweli watu wanaogopa sana. Ofisa wa jeshi aliyekuwa akisimamia mauaji anasema hivi: “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” (Marko 15:39) Huenda alikuwapo wakati wa kesi ya Yesu mbele ya Pilato alipoulizwa kama yeye ni Mwana wa Mungu au la. Sasa amesadiki kwamba Yesu ni mwadilifu, na kwa kweli, yeye ni Mwana wa Mungu.

      Wengine walioshangazwa na matukio hayo yasiyo ya kawaida, wanarudi nyumbani kwao, “wakijipigapiga vifua,” kama ishara ya huzuni kubwa na aibu. (Luka 23:48) Miongoni mwa watu wanaotazama kwa mbali ni wanafunzi wengi wanawake ambao nyakati fulani walisafiri pamoja na Yesu. Wao pia wanahuzunishwa sana na matukio hayo ya kushangaza.

      “ATUNDIKWE MTINI”

      Maadui wa Yesu walipaza sauti: “Atundikwe mtini!” (Yohana 19:15) Neno la msingi la Kigiriki “mti” ambalo limetumiwa katika masimulizi ya Injili ni stau·rosʹ. Kitabu History of the Cross kinasema: “Stauros humaanisha ‘nguzo iliyo wima,’ mti imara, kama ule unaotumiwa na wakulima kujengea ua, wigo, au mihimili—na si vinginevyo.”

      • Kwa nini giza lililotokea kwa saa tatu halikusababishwa na kupatwa kwa jua?

      • Yesu anatuwekea mfano gani mzuri kuhusu kuwatunza wazazi waliozeeka?

      • Tetemeko la ardhi linasababisha nini, na kupasuka kwa pazia la hekaluni vipande viwili kunamaanisha nini?

      • Kifo cha Yesu na mambo yanayotokea yanawaathirije watu walio hapo?

  • Mwili wa Yesu Watayarishwa na Kuzikwa
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
    • Mwili wa Yesu ukitayarishwa kwa ajili ya mazishi

      SURA YA 133

      Mwili wa Yesu Watayarishwa na Kuzikwa

      MATHAYO 27:57–28:2 MARKO 15:42–16:4 LUKA 23:50–24:3 YOHANA 19:31–20:1

      • MWILI WA YESU WASHUSHWA KUTOKA KWENYE MTI

      • MWILI WATAYARISHWA KWA AJILI YA KUZIKWA

      • WANAWAKE WAPATA KABURI LIKIWA TUPU

      Siku inakaribia kwisha Ijumaa alasiri, Nisani 14. Siku ya Sabato, Nisani 15 itaanza jua litakapotua. Tayari Yesu amekufa lakini wezi wawili walio kando yake bado wako hai. Kulingana na Sheria, maiti hazipaswi kubaki “mtini usiku kucha,” badala yake, zinapaswa kuzikwa “siku hiyohiyo.”—Kumbukumbu la Torati 21:22, 23.

      Isitoshe, kipindi cha Ijumaa mchana kinaitwa Matayarisho kwa sababu watu huandaa vyakula na kumalizia kazi ambazo zinapaswa kufanywa kabla ya Sabato. Jua litakapotua, Sabato “kuu” itaanza. (Yohana 19:31) Hii ni kwa sababu Nisani 15 itakuwa siku ya kwanza ya siku saba za Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu, na kwa kawaida siku hiyo huwa ni Sabato. (Mambo ya Walawi 23:5, 6) Pindi hii, siku hiyo ya kwanza itakuwa siku moja na siku ya Sabato, siku ya saba ya juma.

      Basi Wayahudi wanamwomba Pilato aharakishe kifo cha Yesu na wezi wawili walio kando yake. Jinsi gani? Kwa kuagiza miguu yao ivunjwe. Hilo litawazuia wasitumie miguu yao kuinua miili yao ili kupumua. Wanajeshi wanakuja na kuvunja miguu ya wale wezi wawili. Lakini wanaona kwamba Yesu amekufa, basi hawaivunji miguu yake. Hilo linatimiza andiko la Zaburi 34:20: “Anailinda mifupa yake yote; haujavunjwa hata mmoja.”

      Ili kuhakikisha kabisa kwamba Yesu amekufa, mwanajeshi mmoja anamchoma Yesu ubavuni kwa mkuki, na kutoboa sehemu iliyo karibu na moyo wake. ‘Mara moja damu na maji vinatoka.’ (Yohana 19:34) Hilo linatimiza andiko lingine: “Watamtazama yule waliyemchoma.”—Zekaria 12:10.

      Pia, Yosefu kutoka jiji la Arimathea, ambaye ni “tajiri” na mshiriki anayeheshimiwa wa Sanhedrini, yuko hapo Yesu anapouawa. (Mathayo 27:57) Anafafanuliwa kuwa “mtu mwema na mwadilifu,” ambaye “alikuwa akiungojea Ufalme wa Mungu.” Kwa kweli, akiwa “mwanafunzi wa Yesu lakini kwa siri kwa sababu aliwaogopa Wayahudi,” hakuunga mkono uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo katika kesi ya Yesu. (Luka 23:50; Marko 15:43; Yohana 19:38) Kwa ujasiri, Yosefu anamwomba Pilato amruhusu auchukue mwili wa Yesu. Pilato anamwita mwanajeshi anayesimamia, ili ahakikishe kwamba Yesu amekufa. Kisha Pilato anampa Yosefu ruhusa.

      Yosefu ananunua kitani bora na safi, kisha anaushusha mwili wa Yesu kutoka kwenye mti. Anaufunga mwili huo kwa kitani ili kuutayarisha kwa ajili ya mazishi. Nikodemo “aliyemjia [Yesu] usiku mara ya kwanza,” anasaidia kufanya matayarisho hayo. (Yohana 19:39) Analeta karibu pauni 100 za Kiroma (kilogramu 33) za mchanganyiko wa bei ghali wa manemane na udi. Mwili wa Yesu unafungwa kwa vitambaa vilivyo na manukato hayo, kulingana na desturi za mazishi ya Wayahudi.

      Yosefu anamiliki kaburi lililo tupu ambalo limechimbwa katika mwamba ulio hapo karibu, nao wanaulaza mwili wa Yesu humo. Kisha jiwe kubwa linaviringishwa mbele ya kaburi hilo. Wanafanya hivyo haraka haraka, kabla Sabato haijaanza. Huenda Maria Magdalene na Maria mama ya Yakobo Mdogo wamekuwa wakisaidia kuutayarisha mwili wa Yesu. Sasa wanaharakisha kurudi nyumbani ili “kutayarisha manukato na mafuta yenye marashi” ambayo wataupaka mwili wa Yesu baada ya Sabato.—Luka 23:56.

      Siku inayofuata, ambayo ni siku ya Sabato, wakuu wa makuhani na Mafarisayo wanaenda kwa Pilato na kusema: “Tumekumbuka mjanja huyo alipokuwa hai alisema, ‘Nitafufuliwa baada ya siku tatu.’ Kwa hiyo, amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu, ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu, ‘Alifufuliwa kutoka kwa wafu!’ Kisha udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya zaidi kuliko ule wa kwanza.” Pilato anawaambia: “Mnaweza kuweka walinzi. Nendeni mkalilinde jinsi mnavyotaka.”—Mathayo 27:63-65.

      Asubuhi na mapema siku ya Jumapili, Maria Magdalene, Maria mama ya Yakobo, na wanawake wengine wanaleta manukato kwenye kaburi ili waupake mwili wa Yesu. Wanaulizana: “Ni nani atakayetuviringishia lile jiwe kutoka kwenye mwingilio wa kaburi?” (Marko 16:3) Lakini tetemeko la ardhi limetokea. Isitoshe malaika wa Mungu ameliviringisha lile jiwe na kuliondoa, walinzi hawapo, na kaburi liko tupu!

      • Kwa nini siku ya Ijumaa inaitwa Matayarisho, na kwa nini hii ni Sabato “kuu”?

      • Yosefu na Nikodemu wanahusikaje katika mazishi ya Yesu, nao wana uhusiano gani na Yesu?

      • Makuhani wanaomba jambo gani lifanywe, lakini ni nini kinachotokea asubuhi na mapema siku ya Jumapili?

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki