HIFADHI YETU YA VITU VYA KALE
Walitoa Kilicho Bora
Vita vya Pili vya Ulimwengu vilipokwisha katika mwaka wa 1945, sehemu kubwa ya Ujerumani ilikuwa magofu. Majiji yalikuwa yameharibiwa, shule zilikuwa tupu, hospitali hazingeweza kutumiwa, na makombora ambayo bado hayajalipuka yalikuwa kila mahali. Mbali na hilo, hakukuwa na chakula cha kutosha, kwa sababu hiyo kilikuwa na bei ghali sana. Kwa mfano, katika soko la magendo gramu 500 za siagi zilikuwa sawa na mshahara wa majuma sita!
Mashahidi wa Yehova walikuwa miongoni mwa wale walioathiriwa, kwa kuwa walikuwa wamefungwa miaka mingi gerezani na katika kambi za mateso kwa sababu ya imani yao. Mnamo 1945, waliachiliwa wakiwa tu na mavazi waliyovaa. Mashahidi wengine walikuwa wamepoteza nyumba na mali zao. Wengine walikuwa na njaa kali sana hivi kwamba walizimia wakati wa mikutano ya Kikristo.
Mashahidi Katika Nchi Nyingine Watenda Upesi
Mashahidi wa Yehova katika maeneo mengine ulimwenguni walitenda upesi ili kushughulikia uhitaji huo mkubwa wa chakula na mavazi. Ndugu katika makao makuu ya ulimwenguni pote nchini Marekani waliiomba ofisi ya tawi iliyokuwa Bern, Uswisi, iwasaidie akina ndugu nchini Ujerumani. Nathan H. Knorr, mwakilishi kutoka kwenye makao makuu, alitembelea bara la Ulaya ili kuratibu na kuharakisha kazi ya kutoa msaada.
Nathan H. Knorr akitoa hotuba mbele ya akina ndugu huko Wiesbaden, Ujerumani, mnamo 1947. Juu yake andiko la mwaka katika Kijerumani linasema: “Msifuni Yehova, Enyi Mataifa Yote”
Mashahidi nchini Uswisi walitoa chakula, mavazi, na pesa kwa ukarimu. Michango hiyo ilipelekwa kwanza Bern, ambapo ilichanganuliwa na kupakiwa kabla ya kusafirishwa hadi Ujerumani. Mashahidi katika nchi nyingine kutia ndani, Sweden, Kanada, na Marekani walisaidia pia katika kazi ya kutoa msaada, na hilo halikuwanufaisha tu watu wa Yehova waliokuwa Ujerumani bali pia katika nchi nyingine nyingi barani Ulaya na Asia zilizokuwa zimeathiriwa vibaya na vita hivyo.
Matokeo Yenye Kustaajabisha
Ndani ya miezi michache, ofisi ya tawi ya Uswisi ilisafirisha kahawa, maziwa, sukari, nafaka, matunda yaliyokaushwa, mboga, na pia nyama na samaki katika makopo. Michango ya pesa pia ilitolewa.
Isitoshe, Mashahidi nchini Uswisi walituma tani tano za mavazi, kutia ndani makoti, nguo za akina mama, na suti za wanaume. Toleo la Mnara wa Mlinzi la Januari 15, 1946 lilisema hivi: “Akina ndugu hawakutoa vitu vyao vibovu, bali katika kila jambo walitoa kilicho bora. Walijidhabihu kikweli kuwasaidia ndugu zao nchini Ujerumani.”
Pia, Mashahidi nchini Uswisi walitoa angalau pea 1,000 za viatu, ambavyo vilikaguliwa ikiwa vilikuwa katika hali nzuri kabla ya kutumwa. Ndugu na dada katika eneo la Wiesbaden, Ujerumani, waliopakua bidhaa hizo walishangazwa na ubora na unamnanamna wake. Shahidi mmoja aliandika hivi, “Nina hakika hakuna duka lolote nchini Ujerumani lililo na unamnanamna wa mavazi na viatu vya hali ya juu kama huu.”
Misaada iliendelea kutumwa hadi Agosti 1948. Kwa ujumla, Mashahidi nchini Uswisi walituma jumla ya kreti 444 za misaada, zilizo na uzito wa tani 25 kwa ajili ya ndugu zao nchini Ujerumani. Kama ilivyotajwa, si Mashahidi nchini Uswisi peke yao waliohusika katika kazi hiyo ya kutoa msaada. Lakini walikuwa kati ya vikundi vidogo zaidi vilivyojitolea. Wakati huo Uswisi ilikuwa na Mashahidi 1,600 tu!
‘Muwe na Upendo Miongoni Mwenu’
Yesu Kristo alisema hivi: “Kwa jambo hili wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu—mkiwa na upendo miongoni mwenu.” (Yohana 13:34, 35) Upendo uliwachochea watu wa Yehova kutoa si vitu ambavyo hawakuhitaji bali kutoa kilicho bora. (2 Wakorintho 8:1-4) Barua kutoka jiji la Zurich ilitaja kwamba “ndugu wengi ambao hawakuwa na chochote, lakini ambao walitaka kusaidia, walitoa kadi zao za posho na pesa.”
Hali ya watu wa Yehova nchini Ujerumani ilikuwa nzuri upesi baada ya mateso na madhara ya vita. Sababu moja ya hilo ni kwamba waabudu wenzao waliwaonyesha upendo wa kujidhabihu na hivyo kutoa msaada kwa utaratibu mzuri na kwa ukarimu.