Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb92 kur. 66-115
  • Hawaii

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Hawaii
  • 1992 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • Sherehe za Kidini Zenye Kutia Woga za Wakati Uliopita
  • Wenye Maendelea Katika Ushirikiano wa Kikabila
  • Ziara ya Msimamizi wa Sosaiti
  • Kupanda Mbegu za Kwanza
  • Kufanya Kazi Pamoja na Kikundi cha Kwanza
  • Kutoa Ushuhuda Akiwa Dereva wa Teksi
  • Wanafunzi wa Kwanza Wabatizwa
  • Kuacha Kuwa Mfuasi wa Freemason na Kuwa Shahidi
  • Kubadilishana Mahali Katika Shule ya Jumapili
  • Kutoka Italia kwenda Hawaii
  • Alikuwa Mbuddha
  • Wavulana “Watukutu”
  • “Moto Uwakao, Uliofungwa Ndani ya Mifupa Yangu”
  • Uamuzi Mzito Wafanywa
  • Ofisi ya Tawi na “Jumba la Ufalme” la Kwanza Ulimwenguni
  • “Afya Yangu Ilifanya Maendeleo”
  • Gari Lenye Vipaaza Sauti Laeneza Ujumbe
  • Painia Ahamia Hawaii
  • Kundi la Pili Lazaliwa
  • Shambulio la Pearl Harbor
  • Molokai na Mzigo wa Kilo 20
  • Katika Kile Kisiwa Kikubwa cha Hawaii
  • “Kaisari Asema Hatuwezi Kujenga”
  • Wamisionari wa Kwanza Wawasili
  • Roho ya Kweli ya Painia
  • Wakaribisha Mamia ya Wajumbe
  • Mwangalizi Mpya wa Tawi
  • Kuna Kasoro Fulani
  • Hali ya Kiroho ya Kila Siku Yakaziwa
  • Kupanua Kazi Katika Micronesia
  • Kwenda Kwenye Mashamba Yasiyoguswa
  • Vijana Waweka Rekodi Nzuri
  • Kimbunga Pamela—Mema Kutoka Mabaya
  • Ujenzi wa Tawi la Guamu—Chini ya Joto Kali na Jasho
  • Wimbi la Pili la Wahamiaji
  • Ofisi ya Tawi Iliyosongamana
  • “Kama Tu Kujenga Hekalu la Sulemani!”
  • Mvua Yenye Kuanguka—Roho Yenye Kupanda
  • Mfano Mwema kwa Wote
  • Hali ya Kazi Leo
1992 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb92 kur. 66-115

Hawaii

Ripoti ya Kitabu-mwaka 1992

KATIKA Julai 12, 1776, meli iitwayo Resolution ilianza safari ya baharini kutoka Plymouth, Uingereza, kutafuta Mlango Bahari wa Kaskazini-magharibi wa kihadithi—njia ya mkato kati ya Ulaya na Asia. Mwenye kushika usukani alikuwa Kapteni James Cook—mwanamume mwenye maungo na sura nzuri akiwa na macho yenye nuru ya kutaka kugundua nchi ambaye alikuwa mwana wa Mskochi aliyekuwa mfanyakazi wa shamba.

Ijapokuwa hakujua hivyo, hii, iliyokuwa safari yake ya tatu ya baharini ya kuzunguka dunia, ingekuwa ndiyo yake ya mwisho. Baada ya kutembelea tena New Zealand, alisafiri kuelekea kaskazini-mashariki akafika Tonga, kisha Tahiti. Akiondoka Tahiti, Cook alisafiri kwenda mahali ambapo si wavumbuzi wengi wa nchi walikuwa wamejasiria kwenda, kuingia katika maji ya Pasifiki ya Kaskazini. Huko alifanya ugunduzi mkubwa—kikundi cha visiwa ambavyo aliviita Visiwa vya Sandwich, kwa heshima ya rafiki yake kabaila (mheshimiwa) katika jamii ya wakuu wa manoari.

Wakati Cook na wafanyakazi wake walipotua visiwani katika 1778, wakawa ndio Wazungu wa kwanza kukanyaga mchanga wa visiwa hivyo nao walishangaa kusalimiwa kwa heshima kubwa na wenyeji wa kutoka utawala wa makabaila wenye maendeleo ya hali ya juu sana wa Wapolinesia. Walakini, mwaka mmoja baadaye, Cook aliuawa wakati wa kugombana na wenyeji. Leo, vikundi hivyo vya visiwa vya volkano vimekuwa njia panda ya Pasifiki. Ndivyo Visiwa vya Hawaii.

Vikiwa vinakaa kwenye ukingo wa kaskazini wa Tropiki, kikundi hiki chenye kupendeza cha visiwa 132, miamba, na maji yasiyo na vilindi, hutapakaa katika Pasifiki ya Kati kuanzia kusini-mashariki mpaka kaskazini-mashariki kwa mwendo wa kilometa 2,451. Visiwa vyake vikubwa vyenye wakaaji ni Niihau, Kauai, Oahu, Molokai, Lanai, Maui, na Hawaii (kinachoitwa kile Kisiwa Kikubwa).

Kutoka maporomoko ya maji hadi vilele vya volkano vyenye kufunikwa na theluji, uzuri wenye kupendeza wa visiwa hivi umesimuliwa na kusimuliwa tena na tena kwa muziki, mashairi, michoro, na sinema. Kweli kweli, kwa mamilioni ya watu jina Hawaii huchochea akilini picha za minazi ikiyumbayumba katika upepo mwanana wa kitropiki na mawimbi matulivu ya bahari yakipita-pita kwa upole juu ya fuo (kingo za bahari) zenye rangi kama ya pembe za ndovu. Lo! ni kikumbusho chenye kupendeza kama nini cha tamaa ya mwanadamu ya ulimwengu wote mzima ya uzuri wa Paradiso! Hata hivyo, uzuri wa kweli wa Hawaii umo katika ‘vitu vingine vyenye kutamanika,’ yaani katika watu wa Yehova wapole, wenye mfano wa kondoo wanaokaa katika paradiso ya kiroho. (Hag. 2:7) Hii ndiyo hadithi yao.

Sherehe za Kidini Zenye Kutia Woga za Wakati Uliopita

Dini bandia yenye ukuhani wenye kutia woga na wafalme waliofanywa kuwa miungu vilitawala sana miongoni mwa wakaaji wa kwanza Wapolinesia. Ikiwa mtu alivunja jambo lililokatazwa kidini, mara nyingi adhabu ilikuwa kifo. Lakini, jambo lenye kupendeza ni kwamba, miji ya makimbilio iliandaa kimbilio takatifu. Kwa karne nyingi kuabudu miungu mingi, pamoja na mazoea ya kutoa dhabihu za wanadamu, yaliweka dini mbele daima katika maisha ya Hawaii ya kale.

Wamisionari Waprotestanti waliwasili kutoka pwani ya mashariki ya Amerika wakati wa miaka ya 1820 wakaingia ndani ya mazingira hayo. Kwa kushtushwa na maisha ya kijamii na sherehe za kidini za wenyeji, wamisionari hao walileta mabadiliko makubwa kwenye visiwa hivi. Mojayapo mabadiliko hayo lilikuwa kuweka lugha nzuri ya Kihawaii katika namna ya maandishi. Upesi, Biblia na vitabu vingine vya mafundisho vilichapwa. Pia, jitihada zilianzishwa za kuelimisha wenyeji katika njia za Magharibi. Kwa muda mfupi, Uprotestanti ukawa kwa kweli ndiyo dini yenye kuzoewa, ikichukua mahali pa ule ukuhani wa kipagani wa wakati uliopita. Katika 1827 wamisionari wa kwanza Wakatoliki waliwasili Hawaii. Kisha, wahamiaji wafanyakazi Wachina na Wajapani wakaja pamoja na imani zao za wenyeji wa Asia. Hivyo, kufikia mwishoni mwa karne ya 19, maisha ya kidini ya Wahawaii ilitia ndani Uprotestanti, Ukatoliki, Ubuddha, Utao, na Ushinto.

Wenye Maendelea Katika Ushirikiano wa Kikabila

Katika pindi hii ya wakati watu wa kutoka mataifa mengi walichangamana na muundo wa Wahawaii na kubadili utamaduni wake. Wahawaii wa kale walikuwa wa vizazi vya Wapolinesia ambao walikuwa watu wenye maungo, warefu, wenye mifupa imara, wenye rangi ya ngozi ambayo ni mchanganyiko wa manjano-kahawia, macho makubwa ya rangi kahawia, na nywele nyingi za rangi ya kahawia-nyeusi au nyeusi kabisa. Baada ya Kapteni James Cook kutua nchini katika miaka ya mwisho-mwisho ya karne ya 18, mfululizo wenye kufuatana wa wahamiaji kutoka China, Japani, Okinawa, Korea, Ufilipino, Visiwa Madeira na Azores vya Ureno, Puerto Riko, Hispania, Skandinavia, na Ujerumani waliokuwa wakitafuta maisha bora zaidi walikuja wakiwa wafanyakazi kwa mkataba kwenye mashamba makubwa ya miwa. Mchanganyiko huo wa kimataifa uliongezeka wakati wa karne ya 20 kwa mmiminiko wenye kuongezeka wa watu kutoka Samoa na visiwa vingine vya Pasifiki, lakini baada ya 1930, walio wengi walikuja kutoka bara la United States (Amerika).

Kisehemu hiki cha binadamu chenye kupendeza cha Hawaii kimechangamana kwa mafanikio kwa muda wa miaka iliyopita. Karibu asilimia 40 ya ndoa zote mpya ni za mchanganyiko wa jamii mbalimbali, hiyo ikitokeza mchanganyiko wa watu wa kimataifa ambao huvutia na kustaajabisha wageni wengi. Na bado, yajapokuwa malezi yao yenye kutofautiana, watu wa Hawaii kwa ujumla ni wachangamfu na wenye urafiki. Hiyo, pamoja na mazingira yao ya kitropiki na hali ya hewa ambayo kwa ujumla ni yenye jua lenye kuangaza imefanya Hawaii kuwa mahali penye kupendeza pa kwenda likizo (mapumziko). Ilikuwa miongoni mwa watu hao wenye kupatana na kupendeza kwamba Mashahidi wa Yehova wangevuna vuno zuri katika huu wakati wa mwisho.

Ziara ya Msimamizi wa Sosaiti

Katika 1912, maji yakiwa yanasukwa-sukwa, ile meli iitwayo Shinyo Maru iliingia katika bandari ya Honolulu na kutia gudini. Melini alikuwamo Charles T. Russell, msimamizi wa kwanza wa Watch Tower Society, ambaye alikuwa ameanza ziara ya kuzunguka ulimwengu.

Baada ya kutembelea shule za Kamehameha na Taasisi ya Pasifiki-Kati, aliandika maoneleo yake katika toleo la Mnara wa Mlinzi (Kiingereza), la Aprili 15, 1912: “Sisi tuliuliza kuhusu mafundisho ya Kikristo nasi tukaarifiwa kwamba kujaribu kuyatoa kungetenganisha wanafunzi na hivyo kutokeza mafarakano ya shule. . . . Ni maoni yetu kwamba kazi katika Hawaii ni nzuri, ikionwa kwa maoni ya kuwafadhili binadamu, lakini imeshindwa kabisa ikionwa kwa maoni ya kuwafanya watu Wakristo. Kwa kadiri tulivyoweza kufahamu, imani katika damu ya Yesu yenye kufidia (kukomboa), katika ufufuo wake na katika ufalme wake unaokuja haijapata kufundishwa kamwe.”

Kupanda Mbegu za Kwanza

Katika 1915 Walter Bundy, pilgrimu (kama alivyoitwa huko nyuma mhudumu mwenye kusafiri) mmoja, alimwomba Ellis Wilburn Fox aandamane naye na mke wake wafunge safari ya kwenda Honolulu, Hawaii, akijitolea kulipa nauli yake. Ndugu Fox akakubali mwaliko huo, akiacha kazi yake akiwa mwendeshaji mkuu wa jumba la sinema katika Vancouver, B.C. Ndugu Bundy na mke wake, pamoja na Ndugu Fox, wakisafiri kwa meli kutoka Vancouver kwenda Honolulu, walijaribu kupanda mbegu za kwanza za kweli miongoni mwa Wahawaii wenye urafiki na ujirani mwema. Miongoni mwa mizigo yao mlikuwamo mashine ndogo ya kupigia chapa iliyoendeshwa kwa mikono ambayo ingetumiwa kuchapia vikaratasi vya mwaliko za kutangaza hotuba za watu wote ambazo hao ndugu wawili walipanga kutoa. Ndugu Fox alitarajia kukaa Honolulu kwa majuma machache tu na kisha arudie kazi yake yenye mshahara mnono huko Vancouver. Yeye hakujua hata kidogo kwamba, hayo majuma machache yangegeuka kuwa miaka saba.

Jumapili ya kwanza katika Februari 1915, mkutano wa kwanza wa Wanafunzi wa Biblia (kama walivyoitwa Mashahidi wa Yehova wakati ule) ulifanywa katika chumba cha hoteli moja iliyokuwa kwenye pembe ya Fort Street na Beretania Street katika Honolulu, nao ulihudhuriwa na watu watano: Akina Bundy, Ellis Fox, na mwanamume mwenye kupendezwa pamoja na mke wake.

Wakiwa melini siku moja au mbili hivi kabla ya kufika Honolulu, wote watatu walikuwa wamekubaliana kwamba yule atakayepata kazi kwanza angewapa wale wengine wawili riziki, Ndugu Bundy, mpigaji piano, alipata kazi mara moja katika duka la muziki.

Kuhusu siku hizo za mapema, Ellis akumbuka hivi: “Tulitayarisha hotuba ya watu wote kila Jumapili. Walter alikuwa akiandika matangazo kwa ajili ya hotuba ya Jumapili, huku kazi yangu ikiwa kupanga herufi, kuchapa vikaratasi vya mwaliko, na kujaribu kuvieneza sehemu kubwa ya Honolulu kwa kadiri nilivyoweza kila juma. Ndugu huyo hakuonekana akielekea kamwe kuishiwa na hotuba za watu wote.”

Kwa kuhisi hofu ya Ellis juu ya kusema mbele ya watu wengi, Walter alikuwa akienda pamoja naye kwenye bustani, ambapo walikuwa wakifanyia maendeleo sarufi na usemi wake. Kama alivyosema Ellis baadaye, “Kwa subira nyingi yeye alijaribu kunigawia baadhi ya sifa zake.”

Kufanya Kazi Pamoja na Kikundi cha Kwanza

Mazoezi hayo yalihitajiwa kabisa na yalikuwa yenye thamani isiokadirika, kwa kuwa kufikia mwishoni mwa 1915, Ndugu Russell alimwomba Ndugu Walter Bundy arudi akachukue mgawo mwingine katika bara la United States. Ellis Fox alibaki Honolulu akiwa mzee pekee wa kikundi kidogo cha wapya waliopendezwa karibuni. Ndipo akapata kujua kwamba hangekuwa akirudi kwenye kazi yake yenye mshahara mnono huko Kanada katika wakati ujao ulio karibu. Lakini alikuwa mwenye idili juu ya kweli na alikuwa na mwelekeo unaofaa kuhusu kubaki Honolulu na kuweka faida za Ufalme mbele ya zile za namna ya vitu vya kimwili.

Ellis alithibitika pia kuwa mwenye kiasi na mnyenyekevu katika kutunza madaraka yake wakati wa siku hizo za mapema. Funzo la Tabernacle Shadows lilikuwa gumu. Akitambua ujuzi wake wa kiasi, alikuwa akiweka chini karatasi na penseli (kalamu) na kutangaza mbele ya wote kwamba swali lolote ambalo kikundi hicho hakingeweza kujibu, swali hilo lingeandikwa kwenye karatasi hiyo, na wakati wa juma lifuatalo, kila mmoja angelifanyia utafiti. Lakini kama vile ungetazamia, utafiti ulio mwingi aliachiwa Ndugu Fox aufanye, naye alilazimika kufanya kazi ngumu ili apate majibu sahihi.

Kutoa Ushuhuda Akiwa Dereva wa Teksi

Kipande cha chaki na teksi, muunganisho wa kiajabu wa kutangazia ujumbe wa Ufalme—lakini si kwa Ellis Fox. Alipokuwa akifanya kazi akiwa dereva wa teksi, Ndugu Fox alikuwa akitoa ushuhuda kwa wale madereva wengine. Kwa kutumia chaki kuandika sakafuni, alitoa vielezi vya ahadi za Yehova na kueleza orodha ya tarehe ya Biblia, kama vile urefu wa Nyakati za Mataifa, hivyo akichochea maswali mengi yaliyotokeza mazungumzo machangamfu.

Dereva mwingine, James Harrub, akiwa na idili juu ya kweli hizo za Biblia, aliomba habari zaidi azisome. Baada ya kukisoma mbio-mbio kitabu “Kiumbe Kipya,” (Kiingereza) na vitabu vingine katika ile seti ya Studies in the Scriptures, alisadikishwa kwamba pasipo shaka ujumbe vilivyokuwa nao ulikuwa ni kweli ya Neno la Mungu lenye kupuliziwa pumzi yake.

Kufikia 1918 Ellis alikuwa akiongoza funzo la Biblia kwa ukawaida pamoja na James na mke wake, Dora. Kupendezwa kwa Dora, Mwepiskopali, kulichochewa na kipande cha karatasi kutoka kwa gazeti alichopewa mume wake na Ellis. Kilikuwa na masimulizi ya mjadala kati ya “Reverendi” Troy na msimamizi wa pili wa Watch Tower Society, Joseph F. Rutherford, wakati ambao Ndugu Rutherford alifichua kwa mafanikio mafundisho ya Utatu, moto wa mateso, na kutokufa kwa nafsi kuwa si ya kimaandiko. Akichochewa na kichembe hicho cha habari, alianza funzo la Maandiko na matumizi yayo ya miaka zaidi ya 50.

Wanafunzi wa Kwanza Wabatizwa

James Harrub alipoonyesha tamaa yake ya kubatizwa, Ndugu Fox alipata ruhusa ya kutumia kanisa ambalo lilikuwa limechakaa na sasa lilikuwa tupu na lilikuwa na kidimbwi chake cha ubatizo chini ya mlango wa kuinuliwa juu. Hata hivyo, lile tanki la bati lilivuja kama kichungi. Baada ya kufanya wawezayo kuziba mashimo kwa chuma cha kuchomelea risasi, walipata kwamba tanki hilo lingeweza kuweka kiasi cha maji walichohitaji ikiwa tu maji yangefunguliwa kabisa na kuachwa yakitiririka. Ndugu Fox asimulia hivi: “Nilikuwa nimemaliza hotuba ya ubatizo nami nilikuwa nikisimama ndani ya maji nikingojea James atoke kwenye chumba cha kubadilishia mavazi wakati jambo fulani lilipotukia ghafula na kunishangaza kabisa. Huyo Dora Harrub mwenye sura ya kuvutia na mwenye macho makali aliteremka ili aweze kuninong’onezea sikioni bila wengine kusikia naye akauliza, ‘Ellis, mimi naweza kubatizwa pia?’ ‘Bila shaka, waweza! Ingia humo ubadilishe mavazi yako.’ Lo, jambo hilo lilikuwa lenye kusisimua kama nini kwa wote wawili mimi na mume wake!” Hivyo, Wanafunzi Wakristo wawili wa kwanza katika Hawaii wakabatizwa katika Novemba 19, 1919.

Kikundi hicho cha Wanafunzi wa Biblia kilihamisha mahali pao pa mikutano kutoka Hoteli Leonard, alipokuwa akiishi Ellis, kwenda kwenye makao ya akina Harrub kwenye Spreckles Street katika Honolulu. Watu tisa walihudhuria kwa ukawaida mazungumzo ya Jumatano ya “sala, sifa na ushuhuda” na Jumapili Funzo la Mnara wa Mlinzi.

Kuacha Kuwa Mfuasi wa Freemason na Kuwa Shahidi

Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya 1, Ndugu Fox alifanya kazi akiwa meneja wa biashara fulani ya mjini humo. Asubuhi ya Jumapili moja, akiwa nyumbani kwake Honolulu, alitembelewa na David Solomon. Bw. Solomon, ambaye akiwa anaendesha gereji katika kituo kimoja cha kijeshi cha humo mjini, alitaka bidhaa naye akamuuliza Ellis kama angefungua duka amuuzie bidhaa alizotaka, naye Ellis akakubali kufanya hivyo.

Ndugu Fox hukumbuka hivi: “Tulipokuwa tukienda dukani kwa gari, yeye alitaja kwamba lazima mimi niwe mfuasi wa chama cha Mesoni kwa kuwa nilikuwa mwenye kusaidia sana jinsi hiyo. Alipoambiwa kwamba mimi ni mhudumu anayetumikia pamoja na Wanafunzi wa Biblia wenyeji, akauliza, ‘Je! nyinyi hutoa hotuba nje ya kanisa lenu wakati wowote?’ Nikajibu ‘Ndiyo, nikialikwa.’ Ndipo akaniambia kwamba yeye ndiye mkubwa wa nyumba ya chama cha Mesoni kwenye Fort Schofield naye akanialika nikatoe hotuba huko. Bila shaka, mimi sikumwambia kwamba sijapata kamwe kutoa hotuba ya watu wote. Nilitayarisha na kutumia chati kama ile inayopatikana kwenye ukurusa wa mbele wa Buku la 1 la Studies in the Scriptures. Kutayarisha na kutoa hotuba hiyo ya watu wote ya kwanza kulinipa nafasi ya kutumia baadhi ya mambo niliyokuwa nimejifunza kutoka kwa Walter Bundy.”

Baada ya hapo David Solomon alikutana kwa ukawaida pamoja na kile kikundi kidogo cha Wanafunzi wa Biblia. Ujapokuwa upinzani mkali, baadaye yeye alijiuzulu kutoka chama cha Mesoni naye akabatizwa na Ndugu Fox.

Kubadilishana Mahali Katika Shule ya Jumapili

Akiwa mjuzi wa kubuni mambo sikuzote na mwenye uwezo mwingi wa kuchukua hatua ya kwanza, Ndugu Fox alikuwa chonjo kuona fursa (nafasi) za kueneza kweli. Kwa kielelezo, alikuwa akiingia kwa ujasiri makanisani na shule za Jumapili. Wakati wa ibada alikuwa akizusha maswali ya kimafundisho, na hivyo kutokeza fursa humo humo kanisani ya kuwatolea ushuhuda washiriki wenye kuhudhuria.

Jumapili moja aliingia kanisa moja ambamo, yule mhudumu wa kawaida akiwa hayupo, mtu fulani aitwaye Bw. Elder alikuwa akiongoza somo juu ya Mathayo sura ya 24. Ndipo Ndugu Fox alipoanza kuuliza maswali na kutoa maelezo ya Kimaandiko kuhusu habari iliyokuwa ikizungumzwa. Bw. Elder alivutiwa sana hivi kwamba alimwuliza Ndugu Fox mbele ya wote kama angependa kubadilishana mahali naye. Mazungumzo mazuri yalifuata katika somo hilo la shule ya Jumapili mpaka yule mhudumu wa kawaida aliporudi, naye, kama vile ingetazamiwa, alikomesha kwa haraka mpango huo. Naye Bw. Elder, aliacha kanisa na kufungua duka lake lililokuwa mjini jioni moja kila juma ili Wanafunzi wa Biblia walitumie kwa funzo la Biblia.

Katika 1922 hali zilizuka ambazo zilimtaka Ndugu Fox aondoke Visiwa vya Hawaii na kwenda Kalifornia. Akikabidhi James Harrub kazi pamoja na wale waliobaki, aliondoka akiamini kwamba kazi ya kuhubiri ilikuwa imeanzishwa juu ya msingi mdogo lakini ulio imara.

Kutoka Italia kwenda Hawaii

Ilikuwa katika 1923 kwamba Sosaiti ilimtuma O. E. Rosselli wa Italia kwenye safari ya kuzunguka dunia ili atie moyo kitabu The Harp of God (Kinubi cha Mungu) kitumiwe, ambacho kilikusudiwa kuwasaidia wanafunzi wapya katika funzo la Biblia. Mojawapo vituo vyake kilikuwa Hawaii. Ndugu Rosselli alikuwa akiwaka moto, mwenye bidii kwa ajili ya kweli, naye alitembelea kila kisiwa kikubwa akiwa na Harp, kutia na kile kisiwa Niihau kilichokuwa mali ya mtu binafsi na ambacho kwa kawaida vizuizi vya kuingia humo viliwekwa.

Pia Ndugu Rosselli alitia nguvu kile kikundi kidogo cha ndugu Wahawaii kwa kusimulia mambo yaliyoonwa yenye kuchangamsha aliyokuwa amefurahia wakati wa safari zake. Miongoni mwa wale aliotolea ushuhuda alikuwa Amy Ing, alipokuwa akifanya kazi katika duka la babaye huko Honolulu. Alimwangushia seti (fungu) ya Studies in the Scriptures, ambayo angeiona kuwa hazina kwa miaka mingi ijayo. Aliolewa na Harry Lu, na wote wawili wakawa wategemezaji thabiti wa kweli ya Ufalme.

Alikuwa Mbuddha

Kameichi Hanaoka na Albert Kinoshita walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakihudhuria mikutano ya kujifunza Biblia iliyofanyiwa nyumbani mwa akina Harrub. Ile mbegu ndogo ya kweli iliyopandwa ndani ya mioyo yao iliwafanya wakomae na kuwa miti mikubwa ya imani. Ndugu hao wawili wenye kusema Kijapani walishiriki katika kufanyiza funzo la kwanza la lugha ya Kijapani, lililopangwa kitengenezo katika 1924. Wote wawili walivumilia katika utumishi wa Ufalme kwa muda uliobaki wa maisha yao. Ndugu Hanaoka alisaidia kufungua kazi katika Japani baada ya Vita ya Ulimwengu ya 2, akimaliza miaka 20 ya utumishi wake wa wakati wote huko kufikia wakati wa kifo chake katika 1971.

James Nako, wa ukoo wa Okinawa, alikuwa mfuasi thabiti wa Buddha, na ndivyo walivyokuwa wengine wote wa familia yake. Alipokuwa akipitia-pitia vitabu katika duka moja la vitabu, Biblia moja ilinasa macho yake, naye akaanza kuisoma lakini bila kuelewa mengi. Hata hivyo, hiyo ilitosha, ikamsukuma kuacha imani ya Buddha na kujiunga na Kanisa Kongregeshonali la Makiki.

James alisema: “Nilisoma kwamba hotuba ingetolewa kwa Kijapani kwenye Nuuanu YMCA katika Honolulu juu ya kichwa cha habari ‘Mamilioni Wanaoishi Sasa Hawatakufa Kamwe.’ Hilo lilikuwa jambo tofauti sana na yale niliyokuwa nimesikia hapo mbele, kwa hiyo nikaamua kuhudhuria. Kwa kuwa tangazo lilikuwa limetualika tuje na Biblia zetu, nilifanya hivyo. Nilivutiwa sana sana na msemaji, aliyejibu kwa Biblia maswali yote yaliyoulizwa. Nilijaza kikaratasi nikisema kwamba nilitaka kujifunza Biblia.” Jambo hilo lilimwongoza kwenye kile kikundi cha funzo cha watu 12 ambao ndio waliokuwa washiriki wote wa Wanafunzi wa Biblia walioshirikiana pamoja katika 1926. James Nako alifanya maendeleo haraka naye akabatizwa katika Julai 1927.

Akieleza vile ilivyokuwa kutoa ushuhuda huko Honolulu katika 1927, Ndugu Nako alisimulia hivi: “Nilikuwa na Ford kuukuu ya Muundo wa T, ambayo ilikuwa lazima iwashwe kwa mpini wa kuzungushwa kwa mkono. Nilikuwa nikiijaza sehemu ya kuweka mizigo na The Golden Age na Mnara wa Mlinzi katika Kijapani. Magazeti hayo yalikuwa yametafsiriwa kutoka Kiingereza katika Kijapani huko Japani na kutumwa kwetu kwa gharama ya kulipia tu usafirishaji shehena (mzigo). Tuliyagawanya bure, tukiwauliza watu kama wangependa kujifunza Biblia. Mimi nakumbuka kwamba Ndugu Hanaoka nami tulipokea magazeti yapatao elfu moja kila mwezi ili tuyagawanye.”

Wavulana “Watukutu”

Kufanya kazi akiwa mpishi siku za Jumapili kulimzuia James kushiriki utumishi wa shambani, kwa hiyo akaamua aanzishe biashara yake mwenyewe. Hata hivyo, hilo, lilithibitika kuwa jambo lenye kula wakati sana matokeo yakawa kwamba alipata kuwa asiyetenda kiroho.

Ingawa hivyo, yeye alihangaikia sana hali njema ya kiroho ya familia yake. Kwa sababu hiyo alimwuliza mmoja wa akina ndugu, James Watson, ajifunze Biblia pamoja na familia yake, jambo ambalo Ndugu Watson alifanya kwa uaminifu na kwa subira.

“Ulipofika wakati wa funzo,” akakumbuka Ndugu Nako, “wavulana wangu wawili watukutu, Richard na Tommy, walikuwa wakipanda na kutokea katika dirisha la chumba cha kulala na kujificha huko nje. Binti yangu mkubwa zaidi, Adeline, nami tulikuwa tukitafuta-tafuta eneo hilo na kwa kawaida tuliwapata barabara chini bustanini.” Kufikia leo hii, Adeline anatumikia katika shamba la kimisionari katika Japani na ndivyo wale wavulana wawili “watukutu” pamoja na wake zao.

Je! baba yao alipata kuwa mtendaji tena wakati wowote katika kutoa ushuhuda wa Ufalme? Ndiyo, na mara nyingi alifanya utumishi wa painia msaidizi mpaka kifo chake katika 1972. Mjane wake, Alice, hushiriki mara nyingi utumishi wa painia msaidizi katika Honolulu.

Lakini, acheni turudi nyuma kwenye wakati upinzani wa familia ulipotokea kutoka kwa watu wa ukoo Wabudda kwa sababu maisha ya Kikristo ya Nako iliondoka kwa njia yenye kupindukia kutoka mazoea yaliyokubaliwa miongoni mwa Waokinawa wenye kuabudu mababu waliokufa. Watu wa ukoo hakuweza kuelewa kwa nini akina Nako hawangeshiriki katika jambo lililoonekana kuwa dogo la kufukiza uvumba kwenye maziko na pindi nyinginezo kwa kuwaheshimu wafu. Watu wa ukoo walikuwa wakiuliza, “Kwa nini mnaamini hivyo?” na kabla ya Jumba la Ufalme kujengwa huko Honolulu katika 1935, walikuwa wakiwadhihaki akina Nako, wakiuliza, “Liko wapi kanisa lenu?” Hata hivyo, James Nako na mke wake walitumiwa katika kusaidia hesabu fulani ya watu wa ukoo wao wa vizazi vitatu waje katika kweli.

“Moto Uwakao, Uliofungwa Ndani ya Mifupa Yangu”

Joseph Dos Santos, mzaliwa wa Kireno, alilelewa Hawaii katika nyumba ya Wakatoliki wa Roma. Kufikia umri mchanga wa miaka 12, tayari alikuwa amepoteza imani katika kanisa hilo. Baada ya Kuhudhuria Chuo cha Kikairoprakta cha Berkeley katika Kalifornia, katika 1927 alihamia Inglewood, Kalifornia. Akitafuta kweli ya Biblia kwa moyo mweupe, alitumia wakati wake wa ziada akisikiliza programu za kidini kwenye redio na kutembelea makanisa mbalimbali lakini akapata kwamba hayo yalimwacha akijihisi kuwa tupu, bila kutosheka kokote.

Hisia hiyo ilitoweka wakati, katika 1929, bibi mwenye kumkodisha nyumba alipomwazima nakala moja ya The Golden Age iliyozungumza juu ya Baraza la Kuhukumia Wazushi la Kikatoliki. Alisema: “Niliyosoma katika gazeti hilo yalianza kubadili maoni yangu yote juu ya maisha. Yalianza kujaza ule utupu. Mwanafunzi wa Biblia mwenyeji alisikia juu ya kupendezwa kwangu naye akanipatia vitabu zaidi. Upesi sikuwa na shaka kwamba nilikuwa nimepata kweli.”

Wakati wa mwaka huo, alirudi Hawaii akatumie utabibu wa kairoprakta, naye aliendelea kusoma kwa bidii kweli za Kimaandiko kama zilivyofafanuliwa katika vitabu vya Sosaiti. “Kama ilivyokuwa kwa habari ya Yeremia, kweli ya Biblia ilikuwa kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu,” akakumbuka. “Nami sikuweza kukaa kimya.” (Yer. 20:9) Ijapokuwa alikuwa peke yake na hakuwa na uwasiliano na wale Wanafunzi wa Biblia wengine wenyeji, alianza kwa kuchukua hatua yeye mwenyewe kutembelea majirani wake nyumbani kwao katika wilaya ya Aiea ya Oahu. Kwa moyo wa bidii, alipanga kitengenezo kikundi cha funzo pamoja na wafanyakazi wahamiaji wachache wa kutoka Ufilipino, na kufikia 1931 hudhurio kwenye funzo hilo lilikuwa limepanda kufikia 22. Kwa kuwa hakukuwa na vitabu katika lahaja yao, Ndugu Dos Santos alisoma maandiko kutoka Biblia yake ya Kiingereza na kisha kuwaomba wanafunzi wasome katika Biblia zao wenyewe za Kifilipino.

Kazi hii ya kutoa ushuhuda kwa juhudi haikukosa kuonwa na jamii ya makasisi. Haikumchukua muda mrefu padri Mkatoliki kuanzisha uvumi kwamba Ndugu Dos Santos alikuwa pupule (linalotamkwa poo pooʹ lay, kumaanisha “-enye kichaa” katika Kihawaii). Hilo likafanya ajulikane katika eneo hilo kuwa Pupule Joe.

Siku moja, alipokuwa akitembelea rafiki yake, alishtuka kuona kitabu Prophecy. Kufikia wakati huo alikuwa amehisi kwa moyo mnyofu kwamba ni yeye peke yake katika Hawaii aliyekuwa na vitabu vya Wanafunzi wa Biblia. Kwa hamu nyingi alimwuliza rafiki yake jinsi alivyokuwa amepata kitabu hicho. Ulikuwa mshangao na furaha kama nini kwake kujua juu ya James Watson na wale Wanafunzi wa Biblia wengine watano wenye kutenda katika kisiwa hicho!

Uamuzi Mzito Wafanywa

“Wakati wa uamuzi maishani mwangu ukafika,” akasimulia Ndugu Dos Santos. “Nilijua moyoni ilikuwa lazima nifanye uamuzi dhahiri, ama nifuatie kazi yangu ya maisha ya kairoprakta, ambayo ingeweza kuwapunguzia maumivu kwa muda watu wenye kuugua kimwili, au nijitoe mwenyewe kabisa kwa kazi ya kufanya wanafunzi, ambayo itatokezea wanadamu faida za milele.” Akisadiki maneno ya Yesu juu ya nira yenye fadhili ya uanafunzi, alimpelekea Yehova jambo hilo kwa sala. (Mt. 11:29, 30) Ilikuwa vigumu kungoja mpaka amwambie David Solomon (mwangalizi wa bohari [mahali pa kuweka vichapo] la Sosaiti katika Honolulu) kwamba alikuwa ameamua kujitoa kabisa kwa ajili ya kazi ya kuhubiri na kwamba alitaka kuhubiri katika vile visiwa vilivyo nje ya Hawaii, na hivyo aachie wale Wanafunzi wa Biblia wengine sita waeneze Honolulu. Hata ingawa hakuna mtu aliyekuwa amepeleka habari njema nje ya kisiwa cha Oahu, Ndugu Solomon alisadikishwa na azimio la mwanamume huyo kijana na kwa hiyo akamjengea lori ambalo lingetumika kama nyumba alitumie katika kazi ya kolpota. Ndivyo ikawa katika 1929 kwamba kazi ya maisha ya kuhubiri wakati wote ya Joseph Dos Santos ikaanza. Baadaye alieleza hivi: “Nilienda kotekote katika kikundi cha visiwa vya Hawaii nikiwa katika gari langu la aina ya Doji la 1927 kwa miaka mitatu na nusu, nikipanda mbegu za kweli bila hata panchari moja!”

Kwa kuwa eneo lilikuwa kubwa mno na alikuwa ndiye mfanyakazi pekee, yeye alikaza fikira katika kueneza ujumbe sana sana kwa kuangusha vitabu. Akieleza namna ilivyokuwa, aliandika hivi: “Kwa sababu ya mwendo wa kasi wa kazi ya Ufalme katika wakati huo, Wanafunzi wa Biblia walitumia mikoba au mifuko mikubwa ya vitabu kubebea vifaa vya vita ya kiroho. Watu walikuwa wenye fadhili, na hakukuwa na matusi au kufunga milango kwa kishindo. Ilikuwa kama kula tamutamu! Watu walifurahia sana kukuona na kwa haraka walichanga dola moja kwa vitabu vinne, ambavyo vilikuwa ndivyo toleo la kawaida. Wakati huo nilikuwa kijana na mwenye nguvu nami ningeweza kutembea kilometa nyingi katika vijia vya milimani na kupanda milima nikiwa na mifuko miwili iliyojaa vitabu, nami niliona mambo mengi mazuri ajabu yenye kufurahisha. Mahali pengine barabara zilikuwa mbaya na zenye mawe-mawe sana hivi kwamba sikuweza kuendesha gari wala kutembea, hasa katika wilaya ya Kohala katika kile Kisiwa Kikubwa. Nyakati fulani nilitambaa kihalisi ili nifikie nyumba. Hata niliachia wakoma vifaa vya kuwasaidia kuona kiroho katika makao ya wakoma katika Molokai.”

Alidumisha ratiba ngumu, akihubiri siku sita kwa juma na kufanya wastani wa saa 230 za utumishi kila mwezi. Katika ile miaka mitatu na nusu aliyotumia akifanya kazi peke yake kotekote katika kile kikundi cha Visiwa vya Hawaii, aliangusha vipande vya vitabu 46,000.

Aliporudi Honolulu katika 1933, Ndugu Dos Santos alimwambia Ndugu Solomon kwamba hatua yake ambayo ingefuata ingekuwa kuzunguka ulimwengu kupeleka habari njema. Hata hivyo, kama vile ilivyotukia, yeye alisafiri kufika Ufilipino tu, ambako alitumia karibu miaka 17. Wakati wa pindi hiyo, alistahimili upinzani mkali, kutia miaka mitatu ya kifungo cha kutendewa ukatili na majeshi ya Japani yaliyokalia nchi hiyo wakati wa vita ya pili ya ulimwengu.

Katika 1949 Ndugu Dos Santos alirudi Hawaii pamoja na familia yake, ambako yeye na mke wake waliendelea katika utumishi wa painia mpaka alipomaliza mwendo wake wa kidunia katika 1983 akiwa na umri wa miaka 88. Azimio lake na bidii motomoto ya kimisionari vilikuwa na matokeo makubwa katika kazi ya Ufalme katika Hawaii na katika Ufilipino pia.

Ofisi ya Tawi na “Jumba la Ufalme” la Kwanza Ulimwenguni

Baada ya kutumikia zaidi ya miaka minane katika Betheli ya Brooklyn, Don na Mabel Haslett walipewa mgawo kwenda Honolulu katika masika ya 1934 wakasaidie wale ndugu wachache wenye kutenda watimize mgawo wao wa kuhubiri. Bila kupoteza wakati, ofisi ya tawi mpya ya Watch Tower Society ilianzishwa. Ndugu Haslett aliwekwa rasmi kuwa mwangalizi wayo. Katika mwaka uliofuata, J. F. Rutherford, msimamizi wa Watch Tower Society, alitembelea visiwa hivyo naye akakubali uwanja ununuliwe kwenye pembe ya Pensacola Street na Kinau Street katika Honolulu uwe mahali pa kujengwa vifaa vya ofisi ya tawi mpya. Pia aliongoza Ukumbusho, uliofanyiwa katika nyumba iliyokodiwa iliyokuwa ikitumiwa kwa mikutano katika Young Street. Jumla ya watu 25 walihudhuria.

Kwa kuona uwezekano wa ongezeko visiwani, Ndugu Rutherford alipanga pia ndugu wenyeji wajenge jumba la mikutano wakati wa kujenga jengo la tawi jipya. James Harrub alimwendea na kuuliza, “Utapaitaje mahali hapa pamalizikapo?” jibu la Ndugu Rutherford likakuwa, “Hudhani twapaswa kupaita ‘Jumba la Ufalme,’ kwa kuwa ndivyo tunavyofanya, kuhubiri habari njema za Ufalme?” Hivyo, katika 1935, likabuniwa jina ambalo lingeitwa makumi ya maelfu ya mahali pa mikutano ya Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote. Nyumba hiyo ndogo ya ibada kwenye 1228 Pensacola Street, ambayo tangu hapo imepanuliwa na kujengwa upya mara tatu, nayo inashikilia utofautisho unaostahili kuangaliwa wa kuwa ya kwanza kuitwa Jumba la Ufalme.

“Afya Yangu Ilifanya Maendeleo”

Ilikuwa katika Januari 1933 kwamba hatimaye James na Dora Harrub waliona utimizo wa ndoto yao waliyoingojea kwa muda mrefu ya kuingia katika utumishi wa painia. Wakati wa mwaka wao wa kwanza, walikaa Honolulu, wakingojea nyumba yao ya kukokotwa na gari iundwe ambayo ingekuwa makao yao ya painia ikiwa juu ya magurudumu. Baada ya kumalizika, walihamia Maui, wakaeneza kisiwa hicho kwa miezi sita, wakiangusha vitabu na kutumia kinanda kupigia watu hotuba za Biblia. Kile Kisiwa Kikubwa cha Hawaii ndicho kilichofuata kuenezwa, ambako walitumia mwaka mzima wakieneza eneo hilo lakini itikio lilikuwa dogo sana.

Wakihamia kisiwa cha Kauai katika 1936, walifanya makao yao katika upande wa mashariki wa kisiwa hicho karibu na Kapaa. James alipenda watu wa huko sana-sana hivi kwamba aliandikia Sosaiti na kuomba ruhusa afanye Kauai kuwa mgawo wake wa kudumu. Ruhusa ikatolewa.

Wakati James na Dora walipoanza kupainia, wote wawili walikuwa na afya isiyo nzuri. Dora alikumbuka hivi: “Afya yangu ilifanya maendeleo kwa kupainia, nami sikuwa na wasiwasi juu yake.” Kwa msaada wa Yehova waliendelea wakamaliza muda wa maisha wenye baraka tele, wakionea shangwe utumishi wa wakati wote. Ile roho ya kujidhabihu na ya imani kamili ya mume na mke hao iliwafanya wapendwe na kustahiwa huko Kauai, ambako watu wengi wangali wanawakumbuka kwa upendo wenye shauku. Baada ya kifo cha James katika 1954, Dora aliuza makao yao na, kwa kupatana kabisa na tabia yao, akatumia pesa hizo kugharimia ujenzi wa Jumba la Ufalme katika Kapaa huko Kauai. Yeye alimaliza utumishi wake wa kidunia akiwa painia wa kawaida, katika Agosti 1984 akiwa na umri wa miaka 94. Yeye na mume wake walikuwa na lile tumaini tukufu la kupokea thawabu katika mbingu.

Gari Lenye Vipaaza Sauti Laeneza Ujumbe

Wakati uo huo, huko nyuma katika 1935, baadhi ya akina ndugu wa Australia walisaidia akina Haslett wanunue gari, aina ya Plymouth, ambalo lingetumiwa likiwa na vifaa kamili vya kutolea sauti. Kipaaza sauti kikiwa kimekazwa juu ya gari kingetangaza hotuba kwa watu wote kwa lugha ya Kiingereza, Kijapani, Iloko, au Tagalog huku gari hilo likienda kwa mwendo wa polepole katika barabara za mji. Wakati wa mwaka huo, watu zaidi ya 17,000 walisikia jina Yehova kupitia vifaa hivyo. Baada ya kila hotuba, ziara za nyumba kwa nyumba zilifanywa katika ujirani, na ujumbe huo ukagawanywa kwa maandishi.

Njia hiyo ya kuhubiri ilikuja katika wakati wenye kufaa kabisa kwa kuwa wapinzani, wakiwa wamechochewa na ziara ya Ndugu Rutherford huko Honolulu katika 1935, walishurutisha kituo cha redio cha humo nchini kiache kutangaza hotuba za Ndugu Rutherford. Hata hivyo, inaonekana kwamba hesabu kubwa zaidi ya watu walifikiwa kwa njia ya gari lenye vipaaza sauti kuliko ilivyokuwa wakati uliotangulia kwa njia ya redio.

Painia Ahamia Hawaii

Eddie Medalio aliwasili Honolulu katika 1936 ili kutia nguvu kile kikundi kidogo cha wahubiri. Baada ya ubatizo wake katika 1932 huko Los Angeles, Kalifornia, yeye aliandikia makao makuu ya Sosaiti katika Brooklyn juu ya tamaa yake ya kwenda Ufilipino kwa gharama yake mwenyewe akahubiri kwa wakati wote miongoni mwa wananchi wenzake katika Manila. Hata hivyo, Sosaiti ilidokeza kwamba badala ya hivyo aende Hawaii akapainie huko pamoja na akina Haslett ili kufikia Wafilipino wengi huko.

Eddie alikuwa askari aliyestaafu wa Vita ya Ulimwengu ya 1 alitumia zawadi yake ya malipo baada ya kustaafu kulipia nauli yake ya meli kwenda Honolulu. Don na Mabel walisisimuka sana kupata msaada! Walimkaribisha Eddie kwa moyo na kumwalika akae katika ofisi ya tawi. Baadaye, alimwoa Eulalie, nayo familia hiyo ikaondoka kwenda kwa mgawo wao katika Hilo, ambako Eddie aliwekwa rasmi kuwa mwangalizi wa kundi hilo dogo. Walipokuwa wakipainia, akina Medalio walikuwa wakieneza ile miji ya viungani na katika mitaa ya jamii za makabila ya wafanyakazi katika mashamba ya miwa, iliyoitwa kambi.

Kanuni ya Eddie ya upainia ilikuwa: ‘Mtumaini Yehova kwa moyo wako wote.’ (Mit. 3:5) Aliendelea kuyarudia maneno hayo kwake mwenyewe na kwa wengine mchana kutwa kila siku, na sikuzote alikuwa akiyatia ndani ya shauri lake la upole kwa vijana waliotafuta shauri kwake. Kwa mwendo wake wa maisha, ingeweza kuonwa kwamba yeye aliishi kikweli kupatana na maneno hayo yenye pumzi ya Mungu. Yeye hakuchoka katika bidii yake, akijaa juhudi katika kuishi na kwa ajili ya ibada ya Yehova. Eddie alipendwa pia kwa sababu ya ucheshi wake na roho chanya (ifaayo) bila kujali matatizo aliyokabili yeye binafsi. Kicheko chake kilichosikiwa mara nyingi chenye sauti nyembamba na chenye kuambukiza kilikuwa ndiyo chapa yake ya kumtambulisha. Wachanga wengi walithamini kupendezwa kwake nao kwenye kina na kwa moyo mweupe, nao kwa upendo wenye shauku walimwita Babu.

Ndugu Medalio alitumika akiwa painia wa kawaida mpaka kifo chake katika Januari 3, 1990, kilichosababishwa na ugonjwa wa kichomi cha mapafu. Alikuwa na umri wa miaka 93 na alikuwa amemaliza miaka 58 ya utumishi wa nafsi yote kwa Yehova. Mpaka mwisho yeye alidumisha akili nyepesi na alikuwa mwenye nia moja katika kujitoa kwa Yehova. Katika ripoti yake ya utumishi ya mwisho aliyoitoa siku mbili tu kabla ya kifo chake, yeye aliandika hivi: “Roho yangu inataka, lakini mwili wangu unazidi kuwa dhaifu. Nazidi kusali Yehova anipe msaada.”

Akina ndugu katika Hawaii wamebarikiwa kikweli kwa kushirikiana na ndugu za Kristo wapakwa-mafuta kama huyo, wengi wao walitumia nishati zao za maisha katika kutumiwa na Yehova kupainia kazi ya Ufalme. Baada ya utumishi kama huo wa maisha, ingeweza kusemwa kikweli kwa habari yao: “Wenye furaha ni wale wafu ambao hufa katika muungano pamoja na Bwana kutoka wakati huu na kuendelea. Ndiyo, yasema roho, acheni wao wapumzike kutoka kazi zao ngumu, kwa maana mambo waliyotenda yafuatana moja kwa moja pamoja nao.”—Ufu. 14:13, NW.

Kundi la Pili Lazaliwa

Kwa kutokeza, katika 1939, hesabu ya wahubiri iliongezeka kufikia 30, ikilinganishwa na mwaka uliyotangulia uliokuwa na wahubiri 18. Kundi la pili liliundwa, katika Hilo.

Kazi ya kutoa ushuhuda ilizidisha mwendo, kwa misafara ya wahubiri wenye kupiga miguu wakivalia nyuma na mbele kadibodi (karatasi ngumu) zikitangaza hotuba zilizorekodiwa ambazo zingetolewa katika Hilo na Honolulu. Programu ya kulisha iliyofurahiwa na watu wa Yehova ilitia ndani pia kutangazwa kwa hotuba za Ndugu Rutherford kwa redio kwa shortwave (wimbi la umbali mfupi) ambazo zilipokewa kwenye Jumba la Ufalme katika Honolulu na katika visiwa vya nje. Kwa kuwa ni watu wachache sana visiwani waliokuwa wamechukua msisimamo upande wa Yehova, ilitia moyo sana kusikia ujumbe wa kweli ukienezwa kwa kadiri kubwa hivyo.

Shambulio la Pearl Harbor

“Tulikuwa tumejaa gari la aina ya stesheni-wagoni tukielekea Jiji la Pearl kwa siku nzima ya kutoa ushuhuda, kupita mbele tu ya Pearl Harbor,” akasema Mabel Haslett kuhusu Desemba 7, 1941. “Tulirudishwa na Polisi pamoja na wingu la moshi uliokuwa kama wimbi tulipokuwa kwenye Barabara ya Pearl Harbor. Vita!” Majeshi yenye silaha ya Wajapani yalikuwa yameanzisha shambulio lao la hewani lenye kukumba juu ya Pearl Harbor ambalo liliteketeza kundi la manowari za Waamerika zilizokuwa zimetia gudini hapo. Mabel akaendelea kusema: “Siku chache baada ya Desemba 7, mlango ulibishwa. Wanaume wanne wakiwa na bastola walimchukua Don kumpeleka kwenye makao makuu ya kijeshi akahojiwe. Sheria ya kijeshi ilikuwa inatumika. Huku maofisa wakiwa wanamtupia maswali mmoja baada ya mwingine, Don alikuwa akijibu kwa Maandiko. Mmoja akasema kwa hasira, ‘Acha kutumia Biblia hapa!’ Lakini Don akajibu, ‘Siwezi—ndiyo kinga yangu.’ hatimaye (mwishowe), yule aliyekuwa msimamizi akasimama, kwa wazi akiwa ameridhika, na muda mrefu baada ya wakati wa ‘taa zote kuzimwa’ walimleta Don nyumbani. . . . Ijapokuwa tulisumbuliwa pindi kwa pindi, kazi iliendelea.”

Vita ya Ulimwengu ya 2 ilileta hali ya mafuta kuuzwa kwa vipimo, kuzimwa kwa taa zote jioni, kafyu (hali ya hatari) na magumu ya usafirishaji wa bidhaa. Yajapokuwa magumu hayo, kile kikundi kidogo cha wahubiri na mapainia waliotawanyika kotekote visiwani waliendelea na kazi ya kuhubiri. Kwa kweli, mapainia mume na mke James na Dora Harrub waliandikia ofisi ya tawi katika 1942 wakasema hivi: “Kabla ya [shambulio la] Pearl Harbor, wengi walichukua vitabu, lakini walio wengi walikataa kuamini kwamba shida yoyote kubwa ingefika Hawaii. Hayo yote yamebadilika sasa, na mara nyingi maswali yanaulizwa juu ya wakati ujao ulio karibu, n.k. Wanapoambiwa kwamba fasihi (vichapo) ya WATCH TOWER itajibu maswali yao yote, wanafurahia sana kuichukua.”

Molokai na Mzigo wa Kilo 20

Ilikuwa ni baada ya kujifunza kweli katika Honolulu na baada ya makombora kuangushwa juu ya Pearl Harbor kwamba Harold Gale alipokea mgawo wake wa kwanza wa painia. Yeye aripoti hivi: “Mgawo wangu ulikuwa kisiwa cha Molokai, ambako nilikuwa sijapata kufika. Nikiwa peke yangu na sanduku langu la nguo likiwa mikononi, sikujua hata ningekaa wapi ule usiku wa kwanza. Lakini kwa msaada wa Yehova, niliweza kukaa katika kao la mmojawapo Wahawaii mashuhuri zaidi kisiwani. Baadaye alinifanyia mpango nikodi nyumba kubwa kwa dola 7 tu kwa mwezi, ambayo ilikuwa katika shamba la nusu hekta, ambalo lilikuwa na minazi 16. Lilikuwa ng’ambo tu ya ufuo wa bahari, karibu kilometa 8 kusini mwa mji bandari wa Kaunakakai.”

Kwa kuwa hakuwa na njia yoyote ya usafiri, Gale alikuwa akitembea kwa miguu umbali wapata kilometa 30 kwa siku huku akiburuta mzigo wa kilo 20 uliotia ndani kibweta cha vitabu, vijitabu, na magazeti katika lugha sita na kinanda pamoja na rekodi 11 katika lugha nyingi kadiri iyo hiyo. Nyakati nyingi Wafilipino walimwomba wanunue rekodi hizo na hata walikuwa wakitaka kununua kinanda kile. Baadaye, Gale alitumiwa baiskeli na ndugu mmoja kutoka Oahu, naye akaweza kueneza kilometa zapata 60 kwa siku. Norman Chock, ndugu Mchina, alikuja kupainia pamoja naye, akaja na gari lake la aina ya Willys sedan. Ingawa waliruhusiwa galoni kumi tu za mafuta kwa mwezi yakiuzwa kwa vipimo kwa sababu ya hali za wakati wa vita, walieneza kotekote katika kisiwa hicho kama kwamba walikuwa kikundi cha wacheza-muziki chenye kusafiri. Katika muda wa miezi mitatu, walikuwa wakiongoza mafunzo ya Biblia 18.

Upande wa kaskazini wa kisiwa lilikuwako kao Kalaupapa la wakoma lililotengwa peke yalo, ambalo lingeweza kufikiwa tu kwa mashua au ndege au kwa kushuka pali, au mteremko wa ghafula wa meta 600. Ndugu Gale akumbuka hivi: “Huku nikiwa ninabeba vibweta viwili vya vitabu, nilishika kijia hicho cha mteremko wa ghafula na kumwachia Bw. Anderson nakala 65 za kitabu Children, aliyekuwa msimamizi na ambaye aliahidi kuvipitisha kwa wakoma hao ambao mimi sikuweza kuwafikia kibinafsi.”

Katika Kile Kisiwa Kikubwa cha Hawaii

Shinichi na Masako Tohara walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakija katika kweli wakati wa miaka hiyo ya vita yenye msukosuko. Ndugu Tohara alipata vitabu mara ya kwanza katika 1935 na akawatazama Mashahidi katika 1938 wakipiga miguu katika barabara za Hilo wakiwa wanaangika mabegani kadibodi zenye maandishi mbele na nyuma. Baadaye Ralph Garoutte akaanza kujifunza naye, na baada ya mwezi mmoja tu wa funzo, Shinichi alianza kutolea rafiki zake ushuhuda katika mahali pake pa kazi wakati wa chakula cha mchana, kile kiwanda cha kutengeneza sake (pombe ya mchele na divai) katika Hilo.

Akikumbuka mwonjo wake wa kwanza wa kutoa ushuhuda nyumba kwa nyumba, yeye asema hivi: “Asubuhi moja katika Machi 1942, nilitayarisha mkoba wa vitabu, nikaujaza vitabu mpaka pomoni. Nilikuwa nimeazimia kutoka nje niende kutoa ushuhuda nikiwa pamoja na mwanangu Loy. Nilienda kwenye nyumba ya kwanza na kugonga mlango, lakini moyo wangu ulikuwa ukigonga hata zaidi. Sikumbuki niliwezaje kumaliza ziara hii ya kwanza. Lakini sikuwa na ujasiri wa kuendelea na nyumba iliyofuata, kwa hiyo nikaenda nyumbani.” Baada ya kusaidiwa na Mashahidi wenye ujuzi zaidi, hofu zake zikatoweka upesi. Wakati wa mwezi uliofuata, alichukua likizo ya juma moja kutoka kwa kazi yake ajiunge na mapainia waliokuwa wakifanya kazi katika visiwa Waimea na Kohala vilivyo mbali. Aliufurahia wakati huo kweli kweli! Katika Aprili 19, 1942, yeye na mke wake walibatizwa katika maji yenye utulivu ya Pasifiki ya Ghuba ya Hilo.

Wakikumbushwa mfano wa Yesu wa mfanya biashara mwenye kusafiri aliyeuza mara moja vitu alivyokuwa navyo ili apate lulu ya thamani kubwa, mwezi mmoja tu baada ya ubatizo wao akina Tohara waliuza vitu vya nyumba yao wakaanza kujenga nyumba ya kukokotwa. Kufikia Juni walipokea mgawo wao wa kwanza wa painia, katika Pahala, wilaya ya mashambani katika eneo lenye volkano la kile Kisiwa Kikubwa cha Hawaii. Baada ya kufanyia kazi eneo hilo la mbali, walihamishwa kupelekwa wilaya ya Kona, ambako walitembea vijia vingi vya milimani ili kuwatolea ushuhuda wakulima wa kahawa wanyenyekevu.

“Kaisari Asema Hatuwezi Kujenga”

Lile Jumba la Ufalme la Honolulu lilikuwa likijaa sana kwa sababu ya hudhurio lenye kuongezeka. Kwa kuwa ilikuwa wazi kwamba mahali pa mikutano pakubwa palihitajiwa, ilionekana kuwa ni jambo lenye kupatana na akili kupanua jengo hilo, ambalo lilikuwa la kwanza katika ulimwengu kuitwa “Jumba la Ufalme.” Lakini katika 1943 vifaa vya ujenzi vilikuwa vichache na Hawaii ilikuwa chini ya sheria ya kijeshi. Ni kwa sababu hiyo ile serikali ya kijeshi ikasema hapana kwa upanuzi.

Mabel Haslett alikumbuka, “Nilipokuja nyumbani siku moja, Don alikuwa ameketi, akiwa na mawazo mazito, barua ikiwa mkononi mwake. Ilikuwa ruhusa kutoka kwa Ndugu Knorr, msimamizi mpya wa Sosaiti, ya kujenga Jumba la Ufalme jipya uwanjani nyuma ya tawi. Don akasema: ‘Kaisari asema hatuwezi kujenga. Tengenezo la Yehova lasema, “Jenga.” Bila shaka, tutajenga.’”

Wakitiwa nguvu na roho ya Yehova, akina ndugu walishinda vizuizi, wakifanya kazi mchana na usiku, kuleta mchanga kutoka ufuoni mwa bahari na miamba kutoka milimani. Vyuma vya reli vilivyotupwa vilinunuliwa kwa bei ya chini kutoka Kampuni ya Reli ya Oahu, na mbao zilizotupwa kwenye jaa zilitumiwa kufanyiza namna za sementi.

Hata akina dada walifanya kazi ngumu bila kuchoka, wakiondoa kutu kutoka kwa vile vyuma vya reli, na kisha kuvipaka rangi. Rafiki mmoja wa Harry Lu alituazima mashine ya kuchomelea vyuma yenye kuendeshwa kwa mafuta, na ijapokuwa kupimiwa mafuta, sikuzote kulikuwa na mafuta ya kutosha kuchomelea vile vyuma vya reli viwe mikingiko.

Harold Gale, mmoja wa wenye kujitolea, alikumbuka hivi: “Tulimwuliza kondrakta mmoja jengo hilo lingaligharimu kiasi gani kama lingalijengwa kwa kondrakti na lingalichukua muda gani kulijenga. Akataarifu kwamba lilikuwa la thamani yapata dola 17,000 na lingechukua mwaka mmoja na nusu kulijenga. Baada ya jengo hilo kumalizika, tulihesabu gharama halisi kuwa dola zapata 700, kutia na milo kwa ajili ya ndugu 65; na iliwachukua akina ndugu miezi mitatu kulimaliza!”

Wamisionari wa Kwanza Wawasili

Udugu ulitoka katika vita ya ulimwengu ya pili ukiwa na hali yenye ufanisi kiroho. Katika 1946 kulikuwa na kilele cha wahubiri 129, zaidi ya mara mbili ya hesabu iliyokuwako wakati wa shambulio la Pearl Harbor miaka mitano mapema kidogo. Wakati wa mwaka huo, wapya 38 walizamishwa.

Jambo la maana sana katika kipindi hicho cha baada ya vita lilikuwa ziara ya Nathan H. Knorr na Milton G. Henschel kutoka makao makuu ya Sosaiti katika New York. Wakati wa ziara hiyo, ilidokezwa kwamba wamisionari waliozoezwa katika Shule ya Gileadi ya Sosaiti ya Watchtower watumwe Hawaii waongezee kazi mwendo.

Walipowasili katika Septemba 27, 1947, Martha Hess na Ruth Ulrich, wahitimu wa darasa la saba la Gileadi, walipokea ukaribishaji ulio desturi ya Wahawaii kwenye gati, kwa muziki wa Kihawaii kama unavyopigwa na Bendi ya Kihawaii ya Kifalme huku wasichana wa hula wakicheza. Akina ndugu na dada walifurahishwa sana na kuja kwa wamisionari hao hivi kwamba waliwatwika shingoni mashada mengi ya maua.

Kazi ya kudhamiria na ya moyo mweupe ya wamisionari hao wawili ingekaribishwa kama harufu nzuri kwa Wahawaii ikilinganishwa na ya wamisionari wa Jumuiya ya Wakristo, waliokuwa wameacha sifa mbaya. Martha hukumbuka akimsikia mcheza michezo ya kutumbuiza watu mwenyeji akisema kwa uchungu, “Wale wamisionari wa kwanza walikuja visiwani, wakakupa Biblia na kukuambia utazame juu kwa yule Mungu mkuu aliye katika mbingu, na ulipokuwa unatazama, walikupokonya ardhi yako yote.”

Wakati wa kuwasili kwa wale wahitimu wawili wa Gileadi, wale wahubiri 129 katika Hawaii walikuwa wakitumika wakishirikiana na makundi matatu katika Oahu (Honolulu, Maili, na Waimea) na mawili katika kile Kisiwa Kikubwa (Hilo na Kona), pamoja na vikundi vidogo katika Kauai, Maui, na Molokai.

Kwa miaka kumi na nusu, hao dada wawili wamisionari walifanya kazi kwa bidii yenye kuendelea katika Hawaii, wakisaidia wengi waingie katika njia iongozayo kwenye uzima. Kielelezo chao chema na juhudi kwa ajili ya huduma ndivyo vilivyoamsha roho ya painia miongoni mwa vijana wengi. Katika 1957 Martha na Ruth walipewa mgawo kwenda Japani, ambako waendelea wakiwa wamisionari wenzi hadi leo hii.

Wakati uhitaji mkubwa ulipotokea katika Japani, Ndugu Knorr aliuliza hivi kwa barua katika 1947: “Ni nani miongoni mwa ndugu Wahawaii wangependa kwenda Japani?” Wahawaii-Wajapani Jerry na Yoshi Toma, Shinichi na Masako Tohara, na Elsie Tanigawa wakajitolea. Akiandikia Ndugu Knorr, Don aliuza, “Lakini namna gani akina Haslett?” Hivyo wao nao wakatiwa ndani. Baadaye hao saba wakawa tisa, kwa kuwa binti wawili wachanga wa akina Tohara, ambao waliandamana nao kwenda katika Shule ya Gileadi na baadaye wakaenda Japani, walipata kuwa wamisionari pia walipofikia utu mzima. Wote hao wangali wako katika migawo yao ya kimisionari katika Japani, isipokuwa akina Haslett, ambao wakiwa Wakristo wapakwa-mafuta walimaliza mwendo wao wa kidunia.

Roho ya Kweli ya Painia

Kazi ikiwa imepangwa vizuri kitengenezo katika Oahu, sasa fikira zingeweza kuelekezwa katika kueneza maeneo yasiyofanyiwa kazi katika visiwa jirani. Wakati ulikuwa umefika kwa wale wenye nia na wenye bidii wapainie katika maeneo hayo yaliyo peke yake wakiwa na habari njema. Hata hivyo, kupainia katika miaka ya 1950 mara nyingi ilimaanisha kuwezana na hali zenye kujaribu sana.

John Ikehara alihamia Kona katika kile Kisiwa Kikubwa cha Hawaii katika Aprili 1, 1955, ili kusaidia kikundi kidogo huko. Kwa kutoweza kupata kazi ya kuajiriwa ya nusu wakati, alijiruzuku sana-sana kwa mboga na matunda yaliyokuzwa katika bustani iliyokuwa kwenye Jumba la Ufalme. Akieleza juu ya funzo lake aliloongoza pamoja na mwanamume mmoja Mfilipino aliyeishi katika mojayapo mashamba ya kahawa, akumbuka, “Macho yangu yalikuwa yakiwasha kwa sababu ya moshi kutoka kwa taa ya mafuta ya taa. Alikuwa akitoa majibu yake kwa Kiingereza na kusoma mafungu kwa lugha ya Iloko.” John alikuwa akilitazamia hilo funzo la Biblia kwa hamu, kwa sababu zaidi ya moja. Alieleza, “Kabla ya kujifunza kila juma, mwanafunzi wangu alisisitiza kwamba tule kwanza.” Hilo lilithaminiwa sana, kwa kuwa mlo huo ulimwandalia John protini kuongezea chakula chake cha mboga.

Mambo yaliyoonwa kama hilo katika Kona yalimwandalia mazoezi bora sana kwa ajili ya mgawo wake wa misionari katika Japani, ambako alitumikia mpaka kifo chake. Badala ya kulalamika, John aliandika hivi wakati mmoja: “Mimi namshukuru Yehova kwa baraka zake nyingi ambazo amemimina juu yangu mimi na juu ya maelfu wengine pia. Mimi naishukuru sana Sosaiti kwa kuwa wenye kunisaidia sana na wenye subira kwangu.”

Katika vuli ya 1954, Keith Stebbins, wakati huo akiwa mwangalizi wa tawi, alimwendea Nathaniel Miller, misionari kutoka Japani ambaye alikuwa Hawaii kwa sababu ya afya ya mke wake, akamwuliza kama angekubali mgawo wa painia wa pekee katika Kekaha, Kauai.

Ingawa hakuwa na gari linalohitajiwa sana kwa mgawo huo wa mashambani, Nat Miller na mke wake, Allene, walikubali kuondoka mara hiyo. Kwa kuwa afya ya Allene ilimzuia kutimiza takwa la saa kwa mapainia wa pekee, wote wawili walilazimika kujiruzuku kwa alawansi ya Nat ya painia wa pekee ya dola 30.00 kwa mwezi.

Tatizo la usafiri lilitatuliwa wakati Harry Lu alipowapa akina Miller gari la aina ya Doji la 1933. Beringi zilikuwa zikigongana-gongana, na jambo hilo lilizuia mwendo usipite kilometa 40 kwa saa, lakini halikukwama wakati wowote wasiweze kurudi nyumbani. Hata hivyo, nyakati fulani, ilichukua dakika 30 hivi kuliwasha ili lianze mwendo.

Wakiwa na pesa kidogo tu za kununua mafuta, walifanya mwingi wa utendaji wao katika eneo lililokuwa karibu zaidi na Jumba la Ufalme katika miji ya Kekaha na Waimea. Wapata mwaka mmoja baadaye, baada ya Allene kuanza kufanya painia wa pekee, wakaanza kuhubiri katika Hanapepe, Port Allen, na Koloa. Walikuwa wakichukua vifurushi vya chakula cha mchana na cha jioni, na kisha kutoa ushuhuda siku nzima na kuongoza mafunzo katika Koloa mpaka saa 4:00 za usiku. Upesi, kundi katika Kekaha likawa kubwa mara mbili, na kundi jingine likaundwa katika mji wa karibu wa Koloa.

Wakaribisha Mamia ya Wajumbe

Ilisisimua akina ndugu sana katika Hawaii kuarifiwa kwamba wangekuwa wakaribishaji kwa mamia ya wajumbe waliokuwa wakisafiri katika safari ya kuzunguka ulimwengu iliyopangwa na Sosaiti kwa ajili ya “Habari Njema za Milele” Makusanyiko katika 1963. Programu iliratibiwa ifanyiwe kwenye Waikiki Shell, uwanja wa maonyesho unaopakana na Waikiki Beach inayojulikana sana.

Ushirika mchangamfu pamoja na ndugu wengi sana hivyo wenye kututembelea lilikuwa jambo lenye kufurahisha sana. Watu zaidi ya 6,000 walihudhuria kusikiliza hotuba kuu ya Ndugu Knorr, ambayo iliwasilishwa kwa televisheni moja kwa moja kotekote katika kikundi cha visiwa vile alipokuwa akiitoa. Jumuiya ingeweza kuona wazi kwamba Mashahidi wa Yehova ni watu wa kimataifa kikweli. Wajumbe walifurahiwa pia kuwa na kusanyiko kwenye Shell yenyewe yenye kupendeza, ikikaa vizuri chini ya Diamond Head yenye sifa kubwa, ambapo upepo mwanana wa daima wa msimu wa kaskazini-mashariki ulikuwa ukiwapepea wasikilizaji.

Mwangalizi Mpya wa Tawi

Baada ya kumaliza programu ya mazoezi kwenye Shule ya Gileadi yaliyotayarishwa hasa kwa ajili ya waangalizi wa tawi, Keith Stebbins alipewa mgawo mpya pamoja na mke wake kwenda Jamhuri ya Dominika katika 1964. Wakati wa miaka 11 ya utumishi wao katika Hawaii, alikuwa ameona jinsi Yehova alivyokuwa amebariki kazi kwa ukuzi wenye kutokeza. Hesabu ya wahubiri ilikuwa imekuwa zaidi ya mara mbili, kutoka 770 kufika 2,064. Makundi yalikuwa yameongezeka mara tatu kutoka 12 kufika 37. Uwezo wa Ndugu Stebbins wa kupanga mambo kitengenezo uliimarisha tengenezo la humo Visiwani na kuweka msingi kwa ajili ya ongezeko zaidi katika wakati ujao.

Kwenye “Tunda la Roho” kusanyiko la wilaya katika Hilo katika 1964, Ndugu Knorr alitangaza kuwekwa rasmi kwa Robert K. Kawasaki, Sr., awe mwangalizi wa tawi. Ndugu Kawasaki, aliyezaliwa na kulelewa Hawaii, alikuwa wakati huo akitumika akiwa mwangalizi wa wilaya kufuatia kuhitimu kwake katika Shule ya Gileadi katika 1961.

Kuna Kasoro Fulani

Wakati wa 1965, akina ndugu kwenye ofisi ya tawi walitatizika na kuhangaika wakati ripoti za utumishi wa shambani kwa miezi mitatu ya kwanza ya mwaka wa utumishi zilipofunua upungufu wenye kufuatana katika hesabu za wahubiri wenye kuripoti. Hilo lilikuwa jambo lisilo la kawaida kabisa, kwa kuwa Hawaii sikuzote ilifurahia ongezeko lenye kuendelea.

Kwa mwelekezo wa Ndugu Knorr, mkutano wa pekee uliongozwa pamoja na waangalizi wa mzunguko na wa wilaya walioteuliwa. Baada ya saa tisa za mazungumzo mazito na ya sala, sababu mbili za upungufu zilitambuliwa—kupenda vitu vya kimwili na hali ya kiroho iliyodhoofika.

Wakati ule, uchumi wa Hawaii ulikuwa ukisitawishwa sana na utalii. Kazi ya ujenzi ilifurahia ufanisi usiopata kuonwa kamwe. Kama tokeo, gharama ya maisha ilipanda sana. Baadhi ya akina ndugu walishawishwa kuchukua kazi mbili za kuajiriwa. Baadhi ya wake walienda kufanya kazi ya kimwili ya wakati wote, na vijana wengi walichagua kazi ya kimwili kuliko upainia. Hata baadhi ya akina ndugu wenye madaraka katika makundi wakawa wanashughulishwa sana na pato la vitu vya kimwili.

Hata hivyo, jambo zito hata zaidi na lenye kuimarika sana lilikuwa ukosefu wa hali ya kiroho miongoni mwa akina ndugu na dada. Wengi walikuwa hawasomi Biblia kila siku hata kidogo, wala hawakuwa wakizungumza Andiko la kila siku. Wazazi hawakuwa wakijifunza pamoja na watoto wao.

Shauri la Ndugu Knorr kutoka makao makuu lilikuwa lenye kufaa kama nini: “Sisi tunahitaji kuwapa shauri lote la upole la kiroho tuwezalo ili kujenga HALI YA KIROHO ya makundi. Watu wanapokuwa wenye nguvu kiroho wanakuwa wa kawaida katika utendaji wa shambani. Kazi ya shambani huitia nguvu hali ya kiroho ya mtu pia. Hata hivyo, mtu hawezi kuwa na nguvu katika shamba, ikiwa yeye hajilishi mambo ya kiroho.”

Hali ya Kiroho ya Kila Siku Yakaziwa

Kwa msaada wa mwelekezo huo wa wakati ufaao, shauri lilikatwa kwamba kupitia waangalizi wasafirio, kichwa cha hali ya kiroho ya kila siku kingepokea mkazo wenye nguvu. Kusoma Biblia kila siku, funzo la jamaa la ukawaida, na mazungumzo ya Andiko la kila siku yangekaziwa katika makundi. Kampeni ya kugawanya Kitabu cha Mwaka (ambacho wakati huo kilikuwa na maandiko ya kila siku) ilianzishwa kwa mafanikio ili kila mhubiri na mwanafunzi wa Biblia awe na nakala yake binafsi.

Mipango ilifanywa pia ya kuwa na mkusanyiko wa wilaya wa kila mwaka katika kila kisiwa kikubwa cha kikundi cha visiwa vya Hawaii. Kwa njia hiyo akina ndugu kotekote nchini humo wangeweza kwa urahisi kuhudhuria mkusanyiko, wakiondolewa zile gharama kubwa za kusafiri kwa ndege kwenda Honolulu.

Kutumia njia hizi za kukazia hali ya kiroho katika maisha za kibinafsi za akina ndugu kulianza kuvuna matokeo bora sana. Katika 1966 kulikuwako ongezeko la asilimia 4 katika wahubiri, na kuanzia 1967 kufika 1969, kulikuwako mfululizo wa maongezeko ya asilimia 10. Jinsi ilivyo kweli kwamba kutumia mara moja maagizo kutoka kwa tengenezo la Yehova hakika huleta baraka zake!

Hali ya kiroho iliyoongezeka huchochea bidii ya Kikristo. Jambo hilo lilipata kuwa wazi zaidi na zaidi miongoni mwa vijana. Wengi walianza kujitahidi kufikia mapendeleo ya utumishi yaliyopanuliwa. Mwaka wa utumishi wa 1968 uliona mapainia kumi wenye kufanya kazi kwa bidii wakipokea mialiko waende kwenye Shule ya Gileadi, katika Betheli ya Brooklyn, na migawo ya misionari katika Micronesia.

Kupanua Kazi Katika Micronesia

Kabla tu ya ziara ya Ndugu Knorr ya eneo la dunia katika Aprili 1968, Kampuni kubwa ya usafiri wa ndege ilitangaza katika gazeti Honolulu Star Bulletin kuwa inaanzisha utumishi wa safari za ndege kati ya Hawaii, Micronesia, na Guamu. Kwa kuwa wilaya ya Visiwa vya Marshall (katika sehemu za mbali za mashariki ya Micronesia) vilikuwa vimegawiwa tawi la Hawaii hivi karibuni, akina ndugu kwenye ofisi ya tawi walimwonyesha Ndugu Knorr kwa hamu makala katika gazeti hilo. Ndugu Kawasaki asimulia hivi: “Niliweza kuona macho yake yakiangaza alipoanza kuona akilini mwake uwezekano ambao njia hii mpya ya ndege ingeandaa ili kupanua kazi katika zile wilaya saba za Micronesia na Guamu.” Baada ya nukta chache za kimya na kutafakari, alimrudia Ndugu Kawasaki na kusema: “Ndugu [Nathaniel] Miller aweza kutumikia visiwa hivi akiwa mwangalizi wa mzunguko, nawe unaweza kwenda pia, mkipokezana zamu.”

Micronesia hutia ndani visiwa 2,000, ambavyo 97 kati yavyo vina wakaaji, vikitawanyika juu ya eneo la kilometa za mraba 7,800,000 za bahari, magharibi mwa Hawaii. Kila wilaya ya kisiwa ina lugha yake yenyewe, ingawa lazima ikumbukwe kwamba Japani ilisimamia sehemu iliyo kubwa zaidi ya eneo hili baada ya kupewa mamlaka juu yalo na Ushirika wa Mataifa kufuata vita ya ulimwengu ya kwanza. Kwa hiyo, kwa miaka yapata 25, Kijapani kilifundishwa katika shule, na wengi katika eneo wakapata kuwa wenye ufasaha katika lugha hiyo. Kwa kuwa Ndugu Miller alijifunza Kijapani alipokuwa misionari katika Japani, alikuwa anafaa zaidi kufanya ziara kotekote katika visiwa hivyo.

Kwa kweli matukio hayo yalikuwa ya kulitayarisha tawi la Hawaii kwa mgawo ambao ungefuata Januari 1, 1969, wa kuwa na uangalizi juu ya Guamu na maeneo mengine yaliyobaki ya Micronesia. Kwa sababu ya ukaribiano walo na visiwa hivi, ilionekana kwamba tawi la Hawaii lingekuwa katika hali nzuri ya kutoa utumishi bora zaidi na kuwasiliana kwa ukaribu zaidi na wahubiri hao wachache katika mpaka huo wa kiroho. Huku Ndugu Miller akitumikia eneo hilo akiwa mwangalizi wa mzunguko, Ndugu Kawasaki, Sr., alifanya ziara kwenye makao tisa ya kimisionari mara moja kwa mwaka. Hata baada ya baadhi ya wamisionari hao kuwekwa rasmi watumikie wakiwa waangalizi wa mzunguko, hao ndugu wawili walifanya ziara za kila mwaka kwenye makao ya kimisionari na kutumikia wakiwa waangalizi wa wilaya kotekote katika Guamu na Micronesia. Hivyo ikaanza sura yenye shughuli na yenye kuthawabisha mno kiroho katika historia ya tawi la Hawaii.

Kwenda Kwenye Mashamba Yasiyoguswa

Shauri lilikatwa pia kuweka wafanyakazi mapainia kutoka Hawaii kwenye makao yaliyokuwapo ya kimisionari katika Micronesia. Ndugu Knorr alikuwa amekata shauri kwamba walio wengi wao wangejipatanisha kwa urahisi na njia ya maisha ya visiwa hivyo na kufaana vizuri na watu wenyeji. Huo ulikuwa uamuzi wa maana, kwa kuwa ungewawezesha vijana wengi wenye bidii kutoka Hawaii kupata ile fursa ya mara moja maishani ya kupainia kikweli kazi ya Ufalme wakiwa kama wamisionari katika mashamba ambayo yalikuwa karibu hayajaguswa.

Ingawa taraja la kutumikia kama misionari katika Micronesia lilikuwa lenye kusisimua, hakika halingekuwa bila jitihada. Sehemu iliyo kubwa ya vita ya ulimwengu ya pili ilipiganwa katika visiwa hivi hivi kati ya Japani na mataifa yenye muungano Mahali kama vile Kwajalein, Visiwa Truki, Saipani, Guamu, na Peleliu palikuwa mahali penye sifa mbaya ya mapigano yenye kuogopesha sana. Uharibifu kotekote katika wilaya hiyo ulikuwa wenye kuenea sana, na kurudia hali ya kawaida kukawa kwenye mwendo wa polepole. Kulikuwako barabara chache tu zilizotengenezwa kwa mawe, na zile zilizokuwa zimebaki zilikuwa mara njia zenye mavumbi-mavumbi au matope-matope, ikitegemea hali ya hewa. Utumishi wa umeme ulikuwa ama wa mara kwa mara usiotegemeka au haukuwako kabisa. Ukosefu wa mifumo ya kuondolea kinyesi na maji yenye kubebeka mara nyingi ulitokeza matatizo ya kiafya kutokana na vijidudu vya matumboni. Tena lilikuwako lile joto na jasho la kitropiki lisilokwisha, kali zaidi na la kupita kiasi kuliko katika Hawaii.

Ilikuwa katikati ya hali hizo kwamba wamisionari, walio wengi wao wakiwa mapainia kutoka Hawaii, walianzisha kazi. Walikuwa wakitembea katika maji kuvuka vijito, wakisafiri kwa mashua ndogo, na kutembea kwa miguu kupitia misitu mizito ili kufikia makao ya watu. Hali ya hewa yenye mvua nyingi na matope-matope ilifanya isifae kuvaa viatu. Kwa hiyo wamisionari walio wengi wakaanza kuvaa malapa (viatu vya mpira) walipokuwa katika kazi ya kuhubiri.

Wakaaji wa visiwa vya Micronesia walithibitika kuwa watu wenye asili ya kirafiki na ya upole. Heshima yao kubwa kwa Biblia ilifanya kuhubiri miongoni mwao kuwe jambo lenye kufurahisha sana.

Wasiwasi wowote uliokuwapo mwanzoni juu ya kama Yehova angebariki mpango huu wa kuipa ofisi ya tawi ya Hawaii mgawo wa uangalizi wa kazi katika Micronesia uliondolewa na ripoti ya utumishi wa shambani ya Agosti 1970: Guamu iliripoti ongezeko la asilimia 88.6 katika wahubiri, Visiwa Marshall ongezeko la asilimia 25, Ponape ongezeko la asilimia 82.4, na Saipani ongezeko la asilimia 114.3. Wamisionari walikuwa pia wakifanikiwa kufungua kazi katika Belau (Palau), Yapu, na Visiwa Truki.

Vijana Waweka Rekodi Nzuri

Wakati wa miaka ya 1960 na ya 1970, roho yenye afya ya painia ilienea miongoni mwa vijana katika Hawaii. Ilikadiriwa katika 1971 kwamba wakiisha kuhitimu katika kidato cha sita katika shule za upili, asilimia 95 ya vijana waliingia katika utumishi wa wakati wote. Baadaye wengi wa hao walijasiria kwenda Micronesia wakiwa wamisionari na walitumika katika kuzidisha kutangaza ujumbe wa Ufalme katika visiwa hivyo vilivyo mbali sana. Vijana wengi, ndugu wenye afya walipendelewa kutumika Betheli katika Brooklyn na Mashamba ya Watchtower.

Kikundi imara cha waangalizi wasafirio, ambao bidii yao motomoto ilikuwa yenye kuambukiza walichochea bidii hiyo ya utumishi wa wakati wote. Wazee wengi wa makundi walikuwa wakitenda kwa bidii na hivyo kuweka kielelezo chema katika huduma, nao sikuzote walikuwa na mwelekeo chanya katika kuweka mbele ya vijana utumishi wa wakati wote kuwa kazi ya maisha yenye mafanikio. Wazazi na makundi kwa ujumla walikuwa wenye kuunga mkono sana mapainia. Si ajabu kwamba vijana wengi walisitawi kiroho.

Kimbunga Pamela—Mema Kutoka Mabaya

Katika Mei 13, 1976, kimbunga Pamela chenye kukumba sana kilikumba Guamu. Pepo zake zenye kuendelea za mwendo wa kilometa 230 kwa saa zilikifanya kuwa mojawapo vimbunga vibaya sana vilivyopata kukumba kisiwa hicho. Asilimia 80 ya nyumba kisiwani ziliharibiwa, angalau nusu ya hizo kufikia kiasi cha kutotengenezeka. Jumba la Ufalme na kao la misionari lililokuwa karibu vilibomolewa kabisa. Kwa shukrani, hakuna wamisionari au wahubiri wowote waliopoteza maisha zao.

Uhitaji wa kujenga upya kufuata msiba huo ulisukuma ndugu kwenye ofisi ya tawi katika Hawaii wafikirie tena kwa uangalifu jinsi kazi katika Guamu na Micronesia ilivyokuwa ikisimamiwa. Baada ya kufikiriwa kwa sala, ilitambulikana kwamba ofisi ya tawi katika Guamu pengine ingesimamia kwa uangalifu zaidi kazi katika Micronesia. Kwa hiyo, mapendekezo na ramani kwa ajili ya ofisi ya tawi vilipeleka kwa Baraza Linaloongoza, na hivyo vilikubaliwa. Tawi hilo jipya lingesimamia kazi ya kuhubiri Ufalme katika Guamu na katika visiwa vingine vyote katika wilaya za Micronesia. Jengo la kisasa lenye vyumba vya kulala sita, ofisi, na vifaa fulani vya uchapaji pamoja na Jumba la Ufalme kubwa lenye nafasi ya kutosha kukaa watu 400. Mradi huo ulithibitika kuwa kazi kubwa nao haukukamilishwa kwa urahisi kama ilivyotazamiwa hapo mwanzoni.

Ujenzi wa Tawi la Guamu—Chini ya Joto Kali na Jasho

Kisehemu kizuri cha ardhi, kilichokuwa mahali panapofaa na pa kati, kilinunuliwa. Ujenzi ulianza Januari 1978. Miongoni mwa Mashahidi katika Hawaii na bara la United States walitoka maseremala, mafundi wa mabomba, wapaka rangi, wachoraji ramani, mafundi wa umeme, na mhandisi (injinia) mmoja wa mambo ya ujenzi. Wengi waliokuwa wakifanya kazi hiyo ya kujitolea walikuwa na stadi bora sana za ujenzi. Kazi ikawa na mwanzo mzuri sana.

Hata hivyo, ule mkazo wa kufanya kazi ngumu ya ujenzi chini ya joto na jasho lenye kuchosha la kitropiki la Guamu katikati ya makao yenye kusongamana watu ulianza kutokeza madhara. Mara nyingi mahitaji ya kazi yalitokeza kupuuzwa kwa mikutano na utumishi wa shambani kwa vipindi virefu vya wakati.

Akina ndugu katika tawi la Hawaii walipendekeza kwamba ili kupunguza mkazo, mkazo na uangalifu zaidi wapasa uelekezwe kwenye hali ya kiroho ya wale wanaofanya kazi katika mradi ule. Hilo lilisaidia kuleta maendeleo kwa roho yote kwa ujumla. Kwa sifa yao, wale wafanyakazi wa kujitolea walidhabihu mengi ili washikamane na kazi. Ndugu na dada hao waliofanya kazi ngumu pamoja, mara nyingi chini ya jua kali, walionyesha nia halisi ya kujitahidi bila choyo. Yehova Mungu alibariki uaminifu na uvumilivu wao kwa kukamilishwa kwa mafanikio kifaa hicho cha tawi chenye kuvutia, kilichopambwa kwa uzuri na kikiwa kwenye mazingira ya mashambani ya kitropiki. Katika Aprili 20, 1980, Ndugu Milton Henschel wa Baraza Linaloongoza, wakati wa ziara yake ya eneo la dunia katika Guamu, aliweka wakfu jengo hilo kwa ibada safi ya Yehova.

Katika Mei 1, 1980, tawi la Guamu likaanza kutenda, likitoa uangalizi wenye kufaa kwa visiwa vya Micronesia na Guamu. Nathaniel Miller wa Halmashauri ya Tawi la Hawaii, ambaye alikuwa amesafiri sana kotekote katika wilaya za visiwa hivi vilipokuwa vikiangaliwa na Hawaii, aliwekwa rasmi awe mratibu wa Halmashauri ya Tawi, kwa tawi hilo la Guamu lililopangwa kitengenezo karibuni. Hideo Sumida na Arthur White, pia wakiwa hapo kwanza washiriki wa Halmashauri ya Tawi la Hawaii, walihamishwa kutoka Hawaii ili kukamilisha Halmashauri ya Tawi la Guamu.

Kwa miaka 11 tawi la Hawaii lilitumikia visiwa vya Micronesia na Guamu. Lilikuwa pendeleo kama nini kufanya kazi pamoja na wamisionari na wahubiri wenyeji wenye kufanya kazi kwa bidii, ambao walipainia kihalisi kazi ya Ufalme katika visiwa hivi vilivyotawanyika, na vilivyo peke yavyo, wakipanda na kumwagilia maji mbegu za kweli katika mioyo ya wakaaji wenyeji wenyenyekevu wa visiwani!

Wimbi la Pili la Wahamiaji

Wakati wa miaka ya 1980, Yehova alibariki Hawaii kwa ukuzi mfululizo wenye kuendelea. Katika Oktoba 1983, kilele cha wahubiri kilipita hesabu ya 5,000 kwa mara ya kwanza katika historia ya Hawaii, wakiwako 5,019 wenye kuripoti utumishi wa shambani wakishirikiana na makundi 60.

Katika miaka ya karibuni wimbi la pili la wahamiaji kutoka mataifa ya vile visiwa vingine vya Pasifiki walimiminika Hawaii, wakivutiwa na ufanisi wa vitu vya kimwili humo ukilinganishwa na wa kwao. Bila shaka, walikuja na utamaduni na lugha zao. Ili kuwapa nafasi wale wa mfano wa kondoo waliokuwa miongoni mwao, ilikuwa lazima makundi zaidi ya lugha za kigeni yapangwe kitengenezo. Kwa mfululizo wenye kwenda kasi, makundi ya Kijapani, Kikorea, Kisamoa, Kihispania, na Iloko yakaundwa. Akina ndugu katika makundi hayo wana utaratibu mzuri na wana bidii sana katika kuangalia madaraka yao ya Kikristo.

Ofisi ya Tawi Iliyosongamana

Ukuzi katika hesabu ya wahubiri ulimaanisha uhitaji mkubwa zaidi wa vitabu na hesabu iliyoongezeka ya makundi ya kutumikiwa na ofisi ya tawi. Ile gereji ndogo iliyokuwa bohari ambayo ilikuwa imeunganishwa na ofisi ilikuwa inazidiwa na kazi. Ofisi pia ilikuwa inakuwa na watu wengi mno kadiri wafanyakazi walivyokuwa wakihitajiwa ili kushughulikia kazi iliyokuwa ikiongezeka ya mawasiliano kwa barua.

Ofisi iliyokuwa kwenye Pensacola Street, ambayo ilikuwa imetumikia masilahi ya watu wa Yehova katika Hawaii kwa karibu miaka 50, sasa ilikuwa ndogo mno. Ikiwa katika eneo la kati la Honolulu lenye idadi kubwa mno ya watu, upanuzi katika uwanja ule ule lilikuwa jambo lisilowezekana. Kwa sababu hiyo, ukaanzishwa utafutaji wa mahali penye kufaa kwa ajili ya tawi jipya lililopanuliwa.

Katika 1985 mwakilishi mwenyeji wa kampuni yenye kushughulika na uuzaji wa rasilimali alituma ujumbe wa haraka kwenye ofisi ya tawi wenye kutangaza uuzaji wa uwanja wa hekta 0.45 ukiwa na jengo la meta za mraba 2,300, ambalo hapo kwanza lilikuwa duka kubwa la bidhaa. Palikuwa mahali penye kufaa sana, karibu sana na uwanja wa ndege katika sehemu ya chini ya mji. Ijapokuwa mtu mwingine alikuwa amekubali kwa kanuni kununua mali hiyo, kwa kukubaliwa na Baraza Linaloongoza, ndugu katika Halmashauri ya Tawi waliwasiliana na yule mwakilishi wampe toleo lao. Kwa kushangaza, yule mtu wa kwanza alijiondoa katika majadiliano ya bei. Kuonyesha ushuhuda zaidi ulio wazi wa mkono wa Yehova katika shughuli hiyo, mwenye mali hiyo alikuwa na mwelekeo wenye kufaa sana kwa Mashahidi wa Yehova. Kwa miezi michache mifupi shughuli hiyo ilikamilishwa, na katika Novemba 1985, Sosaiti ikapewa hati ya umilikaji mali.

Kugeuza jengo ambalo hapo kwanza lilikuwa duka kubwa liwe ofisi ya tawi, bohari, Kao la Betheli, na Majumba ya Ufalme mawili kulitokeza tatizo lenye kupendeza. Akina ndugu katika Hawaii hawakuwa wamepata kamwe kufanya mradi wa ujenzi mkubwa kadiri hiyo. Halmashauri ya ujenzi iliwekwa rasmi, ramani za ujenzi zikachorwa, na idara mbalimbali za ujenzi zikapangwa. Kulikuwako uhakika kamili wa utayari wa udugu wa nchini kuandaa stadi zilizohitajiwa na wafanyakazi ili kukamilisha kazi hiyo ngumu. Lakini, bila shaka, ilitambuliwa kwamba msingi wa kufanikiwa kwa mradi huo ulionyeshwa wazi na mtunga zaburi kwenye Zaburi 127:1: ‘Yehova asipojenga nyumba, ni kazi bure kwamba wajenzi wameifanyia kazi kwa bidii.’

“Kama Tu Kujenga Hekalu la Sulemani!”

Ili kumwarifu kila mtu juu ya mipango ya kujenga jengo la ofisi ya tawi, mikutano ya pekee ilifanywa kuanzia Februari 1987 kwenye mahali saba mbalimbali katika taifa zima. zaidi ya 5,000 walikusanyika katika Waikiki Shell. Akina ndugu katika halmashauri ya ujenzi walieleza yale yaliyokuwa yamekwisha timizwa, na kutoa maelezo juu ya ratiba ya ujenzi, ambayo lengo lilikuwa kuanza Machi 1, 1987.

Kazi ilianza kwa moyo wa bidii. Kihalisi maelfu ya ndugu na dada katika Oahu na katika visiwa vingine walipanga mambo yao ili washiriki. Baadhi yao walisafiri kuja mahali pa ujenzi wakati wa miisho ya juma, wengine kwa vipindi virefu zaidi. Mashahidi wengi katika Oahu walifungua makao yao kwa moyo wa fadhili kwa ajili ya wafanyakazi wenye kusafiri kutoka vile visiwa jirani. Wakati wa pindi za upeo wa ujenzi, wenye kujitolea wapatao 150 walikuja wakati wa siku za katikati ya juma na 250 hadi 300 wakati wa miisho juma.

Ingawa kazi ilihitaji jitihada na saa zilikuwa ndefu, roho yenye nia na ya furaha ilikuwa yenye kuendelea. Mkazo ulitiwa juu ya hali ya kiroho. Andiko lilizungumzwa kila siku, na funzo la Mnara wa Mlinzi liliongozwa kila juma. Hotuba za Biblia zilitolewa kwa ukawaida, jeshi lote la kazi likihudhuria.

Ushirikiano wa mafundi mbalimbali na kikundi kikubwa cha wafanyakazi wenye bidii ulitokeza kazi yenye mwendo wa utaratibu mpaka ikakamilishwa. Mfanyakazi mmoja wa kujitolea alitoa elezo hili: “Hii ni kama tu kujenga hekalu la Sulemani!” Basi, ulikuwapo utofautiano wa kadiri fulani katika hekalu la Sulemani na lile jengo jipya la tawi. Kwa sehemu hekalu lilikuwa limepambwa kwa dhahabu katika muundo ambao ulikuwa “umetangulia kufanyizwa,” hivi kwamba kulikuwako kelele kidogo sana wakati wa kulijenga. Jengo la tawi lilijengwa kwa sementi, mbao, chuma, na kelele nyingi sana. Hata hivyo, jambo moja lilikuwa linafanana—roho ile ile iliyoendesha wafanyakazi wa hekalu katika siku za Sulemani ilikuwa ikiwachochea akina ndugu na dada katika Hawaii. Jengo la tawi lenye kuvutia likajengwa kutokana na duka kubwa lililokuwa tupu na lenye kuharibika-haribika. Ilikuwa karibu ni muujiza!

Ujapokuwa utendaji wenye kumaliza wakati uliohusiana na ujenzi wa tawi, vilele vipya vitano vya wahubiri vilifikiwa katika 1986. Mwishoni mwa mwaka wa utumishi, makundi mapya mawili yaliundwa. Vilikuwapo vilele vipya vitatu vya wahubiri katika 1987, na makundi matatu zaidi yalianzishwa. Kufikia Julai 1987 jengo lile lilikamilishwa. Mwezi uliofuata utendaji wa ofisi ya tawi ulihamishiwa mahali pale papya.

Mvua Yenye Kuanguka—Roho Yenye Kupanda

Mvua ilikuwa ikianguka mapema katika Aprili 3, 1988, katika Honolulu, lakini hiyo haikupozesha roho ya wale 5,870 waliokusanyika katika Neal Blaisdell Center kwa ajili ya programu ya kuwekwa wakfu kwa tawi. Ndugu wengine 2,838, wakiwa wamekusanyika Maui, Kauai, na kile Kisiwa Kikubwa cha Hawaii, walifunganishwa kwa nyuzi za simu kwa ajili ya programu ya siku nzima iliyokuwa ikitoka Honolulu. Mratibu wa Halmashauri ya Tawi alipitia historia na maendeleo ya kazi ya Ufalme katika Hawaii. Wale wahubiri waliokuwa wamehubiri visiwani mle kwa miaka zaidi ya 38 walikuwa wameketi katika mistari ya mbele ya uwanja ule, nao walikubaliana kwa moyo na maneno ya msemaji kwamba Yehova alikuwa amebariki kwa wingi sana watu wake katika Hawaii.

Slaidi zilionyeshwa kwa dakika 30, zikionyeshwa wakati ule ule mmoja katika kila mahali pa kusanyiko, zikitoa habari ya kugeuzwa umbo kwa lile jengo lililokuwa hapo mwanzo duka kubwa liwe ofisi mpya ya tawi. Kila mmoja wa washiriki wanne wenye kutembelea wa Baraza Linaloongoza walipokezana zamu katika kusema na ile idadi kubwa ya wasikilizaji. Katika utoaji wenye kuchochea, Daniel Sydlik alieleza uadilifu wa Yehova kuwa usioweza kubadilika wenye kudumu kama milima. (Zab. 36:6) Lyman Swingle aliwatia moyo wasikilizaji ‘Wahesabu Baraka Zao’ kupatana na Zaburi 144:15b. Lloyd Barry alionyesha ulingano katika roho ya kushangilia ambayo iliandamana na mwadhimisho wa Sikukuu ya Vibanda na nyakati za ki-siku-hizi wakati ambapo hali kadhalika waabudu wa kweli wanaadhimisha mkusanyo mkubwa unaotimizwa na Yehova. (Law. 23:40) Katika hotuba yake ya wakfu, Milton Henschel alitaarifu hivi: “Mungu wetu ni Mungu wa kusudi, na katika shughuli zake yeye hudhihirisha mamlaka yake kuu. Wakfu huu wa kifaa kipya cha tawi ni sehemu ya Kusudi la Yehova. Tunataka kutambua jinsi jengo hili jipya litakavyotumiwa kuhusiana na mapenzi ya Yehova.”

Siku hii ya pekee ya ibada ilipokuwa inakaribia mwisho nao umati ulikuwa unaungana katika wimbo na sala ya kumalizia, hisia zao za moyoni zilikuwa kama za wale Waisraeli baada ya kuwekwa wakfu kwa hekalu la Sulemani. Walienda kwenye makao yao ‘wakifurahi na kuchangamka moyoni kwa wema wote ambao Yehova alikuwa amewafanyia.’ (1 Fal. 8:66) Lilikuwa tukio tukufu la kiroho, hatua kuu kihalisi katika historia ya miaka 70 ya watu wa Yehova katika Hawaii.

Kama ilivyotarajiwa, ujenzi wa kifaa hicho kipya cha tawi uliwasukuma ndugu wengi wafikirie kwa uzito kuyatengeneza upya majumba ya Ufalme yao yaliyokuwa yakichakaa au kufikiria uwezekano wa kujenga mapya kwa makundi yaliyokuwa yakisitawi. Katika Mei 1986 Jumba la Ufalme la kwanza lililojengwa kwa haraka katika Hawaii lilijengwa katika Kekaha, Kauai. Tangu hapo, majumba ya Ufalme mapya sita kotekote nchini yamejengwa na mawili yakafanywa upya kabisa. Pia, ile iliyokuwa hapo kwanza ofisi ya tawi na Jumba la Ufalme katika Pensacola Street imefanywa upya, na miradi ya ujenzi ya Majumba ya Ufalme mengine sita imepangwa.

Mfano Mwema kwa Wote

Jambo lililofanya “Haki ya Kimungu” Mikusanyiko ya Wilaya ya 1988 iwe yenye kusisimua kwa njia isiyo na kifani ni wale wamisionari 63 ambao walirudi ili kutembelea nyumbani Hawaii. Kwa wote waliohudhuria, pigo la moyo liliongeza mwendo na macho yakajawa na machozi ya shangwe wakati wamisionari hao wote walipokusanyika pamoja jukwani kwenye mkusanyiko katika Honolulu wakati wa hotuba ya Jumamosi “Kinachotakwa ili Utendaji wa Kimisionari Uwe Wenye Mafanikio.” Akina ndugu na dada waliohudhuria hawakuweza kujizuia na, kwa kuthamini, walifuata programu hiyo kwa kupiga makofi kwa nguvu na kwa mfululizo wenye kuendelea kwa muda mrefu sana.

Lilikuwa kumbukumbu kama nini kwamba wengi sana hivyo kutoka Hawaii wamejitahidi kufikilia mapendeleo makubwa zaidi ya utumishi! Tangu mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya 2, wamisionari 164 wametumwa kutoka Hawaii kwenda Japani, Taiwani, Okinawa, Korea, Samoa, na nchi katika Amerika ya Kusini na Afrika. Walio wengi wao wakiwa wametumwa kwenye visiwa vya Micronesia. Kwa sasa, 77 wangali wanatumikia katika migawo yao wakiwa wamisionari, waangalizi wasafirio, na mapainia wa pekee na wa kawaida.

Kwa wengine, utumishi wa Betheli umekuwa ndio mradi, hasa ndugu vijana wenye nguvu. Wa kwanza alialikwa akatumikie Betheli ya Brooklyn katika miaka ya mapema ya 1960. Tangu wakati huo 127 wameshiriki katika pendeleo hili la utumishi wa wakati wote. Kwa wakati wa sasa, 25 wanatumika katika Betheli ya Brooklyn na Mashamba ya Watchtower Society, na 13 wanatumika wakiwa washiriki wa jamaa ya Betheli ya Hawaii.

Sababu ya kupendezwa isivyo kawaida na utumishi wa wakati wote, hasa miongoni mwa vijana, yaweza kuonwa kuwa kile kielelezo kilichowekwa na wamisionari wa mapema wenye bidii, na baadaye, na wazee na waangalizi wasafirio wenye bidii ya kazi. Pia, wazazi wenye kuunga mkono huko nyumbani Hawaii wamekuwa kitia-moyo kikuu kwa watoto wao wanaotumika katika nchi za ng’ambo wakiwa wamisionari au wakiwa Wanabetheli. Hiyo imewezesha wengi wao washikamane na migawo yao, badala ya kushindwa na ile hisia isiyozuilika ya tamaa kubwa ya kutaka kurudi nyumbani pamoja na ile ya kuvunjika moyo. Hivyo, wanavuna zile faida za muda mrefu zinazowajia wale wanaoshikamana na mapendeleo yao ya utumishi.

Hali ya Kazi Leo

Katika Agosti 1990 kilele kisichopata kufikiwa cha wahubiri 6,194 kilifikiwa. Kama tokeo, sasa Hawaii huonea shangwe uwiano mzuri wa mhubiri mmoja wa Ufalme kwa kila watu 180 katika idadi ya watu (ikitegemea tarakimu za idadi ya watu ya 1989). Maeneo ya yale makundi 72 yanafanyiwa kazi mara nyingi, kwa wastani wa mara moja kila majuma manne kufika sita nchini kote. Pia, katika Agosti, kilele kisichopata kufikiwa cha wahubiri 608 waliripoti wakiwa mapainia wa kawaida. Kwa furaha twaona kwamba wengi wa hao wamo katika miaka yao ya utineja na ya 20 na kitu.

Jumuiya ya watu yenye kuvutia pamoja na malezi yao yenye kutofautiana ya kitaifa na kitamaduni yaweza kufanya utumishi wa shambani kuwa jambo lenye kusisimua. Kwa kielelezo, si jambo lisilo la kawaida kuwakuta wenye nyumba Wakaukasia, Wajapani, Wachina, Wafilipino, na Wahawaii wadaio kuwa na imani ya Kikatoliki, Kiprotestanti, Kibuddha, na Kimormoni. Na wote wakiishi kwenye barabara ile ile moja! Ijapokuwa yaonekana kuwa ubaridi kuelekea ujumbe wa Ufalme unaongezeka, watu wenye mfano wa kondoo wanaendelea kumiminika kuja kwenye mlima wa Yehova, kama vile inavyoweza kuonwa kutokana na hudhurio la Ukumbusho la 15,245 katika Aprili 1990.

Kama vile ilivyo katika maeneo mengine ya ulimwengu watu wa Yehova katika Hawaii hawakingwi na matatizo na mashambulio ya Adui yetu mkuu, Ibilisi. Hata ingawa kazi za kuajiriwa ni nyingi kwa sababu ya utalii na rasilimali zilizowekwa na watu wa nchi za kigeni, wakaaji wa Hawaii wangali wanalazimika kuwezana na gharama za juu isivyo kawaida za maisha. Kushindana na mikazo hiyo ya kiuchumi ambayo mara nyingi inawalazimisha wote wawili mume na mke kufanya kazi ya kimwili ili waiweze hali, watu wa Mungu wanajitahidi kudumisha mwelekeo wa kiroho wenye afya. Matumizi haramu ya madawa ya kulevya yanaenea sana katika baadhi ya mitaa nayo inavuna zao lake lenye kuhuzunisha sana, kwa sababu hiyo vijana wanahitaji kukataa ushawishi wake wenye kudhuru kisiri-siri. Pia, kwa sababu ya hali nzuri ya hewa ya Hawaii na yenye jua wakati wote wa mwaka, Hawaii ni mahali ambapo inakuwa rahisi kufanya michezo na kuona raha, hivyo kufanya tafrija na kutafuta raha liwe jambo kubwa la kugeuzia mbali fikira. Kwa wazi, inataka kujiangalia daima ili kuepuka kushindwa na vishawishi hivyo vyenye hila vya Shetani.

Hata hivyo, watu wa Hawaii, kama ilivyo kwa jamii nyingi za visiwani, wajulikana kwa mwenendo mpole, urafiki, na ukaribishaji wageni wao. Pengine sababu ni kule kuchangamana kwa mafanikio kwa watu na tamaduni mbalimbali au ile hali yenye jua daima na hali ya hewa yenye kupendeza. Na hasa miongoni mwa watu wa Yehova, sifa hizo zenye kuvutia zimeongezwa zaidi kwa kusitawishwa kwa tunda la roho.

Mashahidi wa Yehova katika Hawaii wanaendelea kuwa watendaji na wenye bidii, maisha zao zikiwa zategemea utendaji wao wa kiroho. Na muda wote wa historia ya ki-siku-hizi ya Hawaii, wamejithibitisha wenyewe kuwa washikamanifu na wenye kuunga mkono kwa moyo wote tengenezo la Yehova.

Pasipo shaka uzuri mwingi wa paradiso ya kitropiki wapatikana katika Visiwa vya Hawaii. Lakini uzuri wa kweli wenye kupendeza wa Hawaii unaenea katika paradiso ya kiroho iliyomo miongoni mwa watumwa washikamanifu wa Yehova 6,000, ambao huthamini kwa moyo na kufurahia sana kumtolea utumishi. Jinsi wanavyoshukuru kwamba amehakikisha kwamba ‘mlima wa nyumba ya Yehova umesimamishwa imara’ hata katika hivi Visiwa vya Hawaii vilivyo mbali sana vyenye uzuri wenye kuvutia.—Isa. 2:2.

[Chati katika ukurasa wa 115]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Hawaii 8,000

1950 320

1960 1,589

1970 3,340

1980 4,494

1990 6,194

Kilele cha Wahubiri

1,000

1950 30

1960 80

1970 447

1980 591

1990 938

Wast. Mapainia

[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 66]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

VISIWA VYA HAWAII

HAWAII

Hilo

Kailua-Kona

Pahala

LANAI

MAUI

MOLOKAI

Kalaupapa

Kaunakakai

OAHU

Aiea

Pearl Harbor

Honolulu

KAUAI

Kekaha

Kapaa

Hanapepe

Koloa

NIIHAU

Bahari ya Pasifiki

[Sanduku]

VISIWA VYA HAWAII

Mji Mkuu: Honolulu

Lugha Rasmi: Kiingereza

Dini Kubwa: Imani tofauti-tofauti

Idadi ya Watu: 1,112,100

Ofisi ya Tawi: Honolulu

[Picha katika ukurasa wa 71]

Fuo za rangi ya pembe za ndovu na ghuba ndogo-ndogo tulivu hupamba kwa uzuri Visiwa vya Hawaii

[Picha katika ukurasa wa 72]

Ellis Fox, pamoja na akina Bundy, walianza kazi ya kuhubiri, katika 1915

[Picha katika ukurasa wa 73]

Dora Harrub na mume wake, James, walikuwa wa kwanza kubatizwa, katika 1919

[Picha katika ukurasa wa 79]

Joseph Dos Santos alianza kupainia katika 1929. Kwa nini akabandikwa jina “Pupule Joe”?

[Picha katika ukurasa wa 83]

Don na Mabel Haslett. Akawa mwangalizi wa kwanza wa tawi la Hawaii, katika 1934

[Picha katika ukurasa wa 84]

Mahali pa kwanza pa mikutano kuitwa Jumba la Ufalme palijengwa katika Honolulu, katika Pensacola Street, katika 1935

[Picha katika ukurasa wa 85]

Magari yenye vipaaza sauti yatangaza ujumbe wa Biblia. Hili moja lilisafirishwa kutoka Honolulu likatumiwe katika visiwa vya nje katika 1937

[Picha katika ukurasa wa 88]

Magari yenye vipaaza sauti yakiendeshwa kwa mwendo wa polepole katika barabara za mji, yakitangaza hotuba za Biblia na kupiga sahani za santuri zenye hotuba zilizorekodiwa

[Picha katika ukurasa wa 94]

Don Haslett, Nathan Knorr, Mabel Haslett, na Milton Henschel. Ziara ya Knorr katika Honolulu mwaka 1947 ilianzisha kutumwa kwa wamisionari katika Hawaii

[Picha katika ukurasa wa 95]

Wamisionari wawili wa kwanza waliwasili Honolulu katika Septemba 27, 1947. Martha Hess, mstari wa mbele, wa nne kutoka kushoto, na Ruth Ulrich, mstari wa nyuma, wa pili kutoka kushoto. Hess na Ulrich sasa wanatumikia Japani

[Picha katika ukurasa wa 96]

Waikiki Shell, mahali palipofanyiwa “Habari Njema za Milele” Kusanyiko katika 1963. Wengi walibatizwa kwenye Waikiki Beach

[Picha katika ukurasa wa 101]

Nathaniel na Allene Miller waliwasili katika Hawaii mwaka wa 1954 na wakatumikia huko mpaka walipopewa mgawo kwenda Guamu katika 1980a

[Maelezo ya Chini]

a Allene Miller alikufa akiwa mwaminifu katika Novemba 1989.

[Picha katika ukurasa wa 105]

Ofisi ya tawi ya Guamu na Jumba la Ufalme viliwekwa wakfu Aprili 20, 1980. Guamu huangalia kazi ya kuhubiri katika vile visiwa 2,000 vya Micronesia

[Picha katika ukurasa wa 107]

Ofisi ya tawi na Jumba la Ufalme, lililoko kwenye Pensacola Street, vilitumikia faida za Ufalme kwa miaka karibu 50, mpaka Agosti 1987

[Picha katika ukurasa wa 108]

Lililokuwa hapo kwanza duka kubwa la bidhaa ambalo liligeuzwa umbo likawa ofisi ya tawi, bohari, Kao la Betheli, na Majumba ya Ufalme mawili liliwekwa wakfu Aprili 3, 1988

[Picha katika ukurasa wa 109]

Washiriki wa Halmashauri ya Tawi na wake zao. Kushoto kwenda kulia, Robert na Hatsuko Kawasaki, Frans na Endeline van Vliet, na Gary na Carol Wong

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki