Mahali pa Kubatizia Ushuhuda wa Desturi Iliyosahaulika
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA
“ABATIZWA kwa Kuzamishwa Kwenye Kanisa Kuu,” ndivyo kilivyosema kichwa cha gazeti moja la Ufaransa mnamo 2001. Hata hivyo, picha katika makala hiyo ilionyesha muumini mpya Mkatoliki akisimama ndani ya kidimbwi kikubwa cha ubatizo, maji yakiwa yamemfikia magotini na askofu Mkatoliki akimmwagilia maji kichwani. Tukio hilo ambalo hurudiwa sehemu nyingi ulimwenguni linaonyesha utamaduni wa Kanisa Katoliki tangu Baraza la Pili la Vatican lianze kubatiza waumini wapya kwa kutozamisha mwili wote. Maswali yanazuka: Kwa kuwa Wakatoliki wengi walibatizwa wakiwa watoto kwa kunyunyiziwa maji machache, ni ubatizo wa aina gani unaopatana na kielelezo kilichowekwa na Yohana Mbatizaji na mitume wa Yesu? Wakristo wanapaswa kubatizwaje leo? Historia ya mahali pa kubatizia itasaidia kujibu maswali hayo.
Chanzo na Maana ya Ubatizo
Mwanzoni, ubatizo wa Kikristo ulifanywa kwa kuzamishwa kabisa katika maji. Simulizi la Biblia kuhusu ofisa Mwethiopia aliyebatizwa na Filipo linatusaidia kuelewa jambo hilo. Baada ya kumtambua Kristo, ofisa huyo alisema hivi alipoona maji mengi: “Ni nini kinachozuia nisizamishwe?” (Matendo 8:26-39, The Emphatic Diaglott) Mzizi wa Kigiriki wa neno hili “zamishwa” ni ba·ptiʹzo, linalomaanisha “kutumbukiza,” au “kuzamisha,” ambapo neno la Kiswahili “batiza” linatolewa. Hilo hurejezea kuzamisha kabisa. Jambo hilo linakaziwa na wazo la kwamba ubatizo unalinganishwa na kuzika. (Waroma 6:4; Wakolosai 2:12) Jambo la kupendeza ni kwamba, watafsiri kadhaa wa Kifaransa wa Biblia (kama vile Chouraqui na Pernot) humwita Yohana Mbatizaji, Yohana Mzamishaji.
Katika karne za kwanza-kwanza za Ukristo, watu walibatizwa kwa kuzamishwa kabisa mahali popote palipokuwa na maji ya kutosha, ndani ya mito, baharini, au ndani ya beseni za bafu za watu binafsi. Hata hivyo, idadi ya wageuzwa-imani ilipozidi kuongezeka, mahali pa kubatizia palijengwa katika maeneo mengi ya milki ya Roma, kuanzia Dalmatia hadi Palestina na kuanzia Ugiriki hadi Misri. Kati ya majengo ya kubatizia ya zamani sana kuchimbuliwa ni lile linalopatikana kwenye fuo za Mto Efrati huko Syria, na inakadiriwa kwamba lilijengwa mnamo 230 W.K.
“Ukristo” ulipofanywa kuwa dini rasmi katika Milki ya Roma, katika karne ya nne W.K., mamilioni ya watu wakawa “Wakristo” na walipaswa kubatizwa. Hivyo majengo ya kubatizia yalijengwa kila mahali kwa kusudi hilo. Kufikia karne ya sita, kulikuwa na majengo 25 huko Roma pekee, kutia ndani moja katika basilika ya Mt. John Lateran. Huko Gaul huenda kila dayosisi ilikuwa na mahali pake pa kubatizia. Kulingana na kitabu kimoja, kulikuwa na mahali 150 pa kubatizia. Inawezekana kwamba kulikuwa na mamia ya majengo hayo vijijini, karibu na makanisa madogo, makaburi, au makao ya watawa.
Jinsi Yalivyojengwa na Kujazwa Maji
Mara nyingi majengo ya kubatizia yalikuwa ya duara au yenye pembe nyingi yakiwa yamejengwa kando ya kanisa au yakiwa yameunganishwa na kanisa. Uchimbuzi unaonyesha kwamba majengo hayo yalikuwa madogo (kwa kawaida mita 200 za mraba) lakini yalikuwa yamepambwa kwa nguzo, marumaru, na michoro ambayo nyakati nyingine ilielezea matukio ya Biblia. Vidimbwi vingine kama kile kilichoko Mariana, Corsica vilikuwa vimefunikwa kwa paa maridadi. Vidimbwi vyenyewe vilikuwa na umbo la mraba, duara, pembe sita, yai, msalaba, au pembe nane. Upana na kina cha vidimbwi vya ubatizo vya zamani kinaonyesha kuwa vilikusudiwa kwa ajili ya kuwabatiza watu wazima. Vilikuwa vikubwa na vingeweza kutoshea angalau watu wawili. Kwa mfano, huko Lyon, jiji lililo mashariki ya kati ya Ufaransa, kuna kidimbwi chenye upana wa mita 3.25. Vidimbwi vingi vilikuwa na ngazi zilizoshuka majini. Mara nyingi ngazi hizo zilikuwa saba.
Wajenzi walihangaika kuhusu mahali ambapo maji yangepatikana. Majengo mengi ya kubatizia yalijengwa karibu na chemchemi za kiasili au kwenye magofu ya bafu za maji moto, kama ile ya Nice, kusini mwa Ufaransa. Mara nyingi maji yaliingizwa na kutolewa kwenye vidimbwi kupitia mabomba. Katika visa vingine maji ya mvua yalichotwa kwenye kisima kilichokuwa karibu.
Mahali pa Kubatizia pa Mt. Yohana huko Poitiers, magharibi mwa Ufaransa, palipojengwa mnamo 350 W.K. hivi, ni mfano mzuri wa mahali pa kubatizia pa “Wakristo” katika karne ya nne. Ndani ya chumba chenye umbo la mstatili, kilichozungukwa na vyumba vingine, kulikuwa na kidimbwi kikubwa cha pembe nane chenye ngazi tatu. Kina cha kidimbwi hicho ni mita 1.41 na upana wa mita 2.15. Kilikuwa kimeunganishwa na mfereji ulioingiza maji jijini kutoka kwenye chemchemi iliyokuwa karibu.
Kuzamisha Kabisa au Nusu?
Je, watu walizamishwa kabisa katika majengo hayo ya zamani ya kubatizia? Wanahistoria fulani Wakatoliki wanakataa jambo hilo, wakidai kwamba kubatiza kwa kunyunyiza (kummwagilia mtu maji kichwani) kulifanywa mapema katika historia ya Kanisa Katoliki. Pia wanasema kwamba vidimbwi vingi havikuzidi kina cha mita 1 na hivyo havikuwa na kina cha kutosha kumzamisha kabisa mtu mzima. Ensaiklopedia ya Kikatoliki inasema kwamba huko Poitiers “anayebatiza [kasisi] angesimama kwenye ngazi ya tatu bila kugusa maji.”
Hata hivyo, michoro ya ubatizo huo huonyesha kwamba ilikuwa kawaida kuzamishwa kikamili. Michoro hiyo ilionyesha maji yakiwa yamemfikia mtu anayebatizwa kifuani au shingoni kabla ya ubatizo. (Ona picha juu.) Je, ingewezekana kumzamisha mtu kikamili ikiwa kina cha maji kilimfikia kiunoni mtu mwenye kimo cha kawaida? Kitabu kimoja kinadokeza kwamba kidimbwi kingezibwa hadi mtu anayebatizwa aliyepiga magoti au kuchuchumaa azamishwe.a Pierre Jounel profesa wa desturi na sherehe za Kikatoliki huko Paris, anasema: Mtu anayebatizwa “alisimama maji yakiwa yamemfikia kiunoni. Akiweka mkono juu ya kichwa chake, kasisi au shemasi alimwinamisha majini ili mwili wote uzamishwe.”
Vidimbwi vya Ubatizo Vyapunguzwa Ukubwa
Hatimaye ubatizo wa kawaida uliokuwa umefanywa katika nyakati za mitume ulibadilika na kuanza kuhusisha desturi yenye kutatanisha, nguo na ishara za pekee, sala za kufukuza pepo, kubariki maji, kukariri kanuni ya imani, na kutiwa mafuta. Desturi ya watu kuzamishwa nusu ikaendelea kuenea. Vidimbwi vya ubatizo vilipunguzwa vikawa nusu ya ukubwa wa awali. Kwa mfano, huko Cazères, kusini mwa Ufaransa, kidimbwi cha awali kilichokuwa na kina cha mita 1.13 kilipunguzwa hadi kikawa na kina cha nusu mita hivi kufikia karne ya sita. Baadaye, karibu karne ya 12, Wakatoliki waliacha kuwazamisha watu nusu na wakaanza kuwanyunyizia maji. Kulingana na msomi Mfaransa Pierre Chaunu, hilo lilitokea kwa sababu “kuwabatiza watoto kulikuwa kumeanza kuenea katika nchi zenye hali mbaya ya hewa, kwa kuwa haingewezekana kumtumbukiza mtoto mchanga ndani ya maji baridi.”
Mambo hayo yalisababisha vidimbwi kuwa vidogo hata zaidi. Katika uchunguzi wake kuhusu historia ya ubatizo, mwanahistoria Frédéric Buhler anasema: “Uchimbuzi wa vitu vya kale, hati, na sanaa, kwa ujumla zinaonyesha kwamba njia za kuwabatiza watu zilibadilika hatua kwa hatua kutoka kuwazamisha kabisa watu wazima katika karne za kwanza za Ukristo, kuwazamisha nusu, kuwazamisha watoto kabisa, na hatimaye kuwanyunyizia watoto wachanga maji.”
Leo, zoea la kuwazamisha nusu watu wazima linazidi kuwa maarufu, kwa kuwa vidimbwi vikubwa zaidi vya kubatizia vinajengwa. Na kupatana na kile ambacho Buhler anasema kuwa ni msisimko wa kurudia uzamishaji wa zamani, sasa kuliko wakati mwingine wowote, Kanisa Katoliki linapendekeza watu wabatizwe kwa kuzamishwa kabisa. Kwa kupendeza, tangu zamani Biblia imeonyesha kwamba ubatizo wa Kikristo unaofaa ni kuzamishwa kabisa.
[Maelezo ya Chini]
a Mashahidi wengi wa Yehova wamebatizwa kwa kuzamishwa kabisa katika vidimbwi vidogo vya kuogelea au hata beseni kubwa za bafuni.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Mahali pa kubatizia pa Mt. Yohana huko Poitiers, Ufaransa
[Picha katika ukurasa wa 13]
Mahali pa kubatizia pa karne ya tano palipojengwa upya huko Mariana, kwenye Kisiwa cha Corsica
[Hisani]
© J.-B. Héron pour “Le Monde de la Bible”/Restitution: J. Guyon and J.-F. Reynaud, after G. Moracchini-Mazel
[Picha katika ukurasa wa 14]
MICHORO YA UBATIZO WA YESU
Maji ya Yordani yanamfikia Yesu kwenye kiuno huku malaika wakimletea mataulo ya kujipangusia, karne ya tisa
[Hisani]
Cristal de roche carolingien - Le baptême du Christ © Musée des Antiquités, Rouen, France/Yohann Deslandes
Yesu akiwa Mto Yordani maji yakiwa yamemfikia shingoni. Upande wa kushoto, malaika wawili wameshikilia kitambaa tayari kumpangusa, karne ya 12
[Hisani]
© Musée d’Unterlinden - F 68000 COLMAR/Photo O. Zimmermann