-
Kwa Nini Sisi Hununua Vitu?Amkeni!—2013 | Juni
-
-
HABARI KUU: JE, TUNANUNUA VITU KUPITA KIASI?
Kwa Nini Sisi Hununua Vitu?
Matokeo ya uchunguzi uliofanywa ulimwenguni pote ambayo yalitolewa mwaka wa 2012 yalionyesha kwamba nusu ya waliohojiwa walikiri walinunua vitu ambavyo hawakuvihitaji. Asilimia 66 wana wasiwasi kwamba watu wananunua vitu kupita kiasi. Huenda wana sababu nzuri ya kuwa na wasiwasi. Wanunuzi wengi wameshindwa kulipa madeni yao yanayozidi kuongezeka. Watafiti wanasema kwamba badala ya kutuletea uradhi, kununua vitu kupita kiasi kunaweza kusababisha mikazo mingi na kukosa furaha! Basi, kwa nini tunanunua vitu kupita kiasi?
WANUNUZI hufurikwa na mbinu nyingi za wauzaji bidhaa. Lengo la wauzaji ni nini? Ni kufanya uamini unahitaji vitu ambavyo si vya lazima. Wauzaji wanajua kwamba wanunuzi huchochewa sana na hisia. Kwa hiyo matangazo ya kibiashara na ununuzi wenyewe umekusudiwa uwasisimue wanunue.
Kitabu Why People Buy Things They Don’t Need (Kwa Nini Watu Hununua Vitu Ambavyo Hawahitaji) kinasema hivi: “Wanapopanga kununua bidhaa mpya, mara nyingi wanunuzi huanza kujiwazia wakitafuta bidhaa hiyo, wakiipata, na mwishowe kuinunua.” Wataalamu fulani husema kwamba wanunuzi wanaweza kusisimuka sana wanaponunua vitu, hivi kwamba homoni ya adrenalini inaongezeka mwilini. Jim Pooler, ambaye ni mtaalamu wa uuzaji anaeleza hivi: “Muuzaji anapotambua hisia hizo za mnunuzi, anaweza kutumia msisimuko huo kwa faida yake na hivyo kumfanya mteja ashindwe kujizuia kununua bidhaa fulani.”
Unawezaje kujilinda dhidi ya mbinu za werevu za wauzaji bidhaa? Usiathiriwe na hisia zako, linganisha mambo ambayo wauzaji wanakuahidi na mambo halisi.
AHADI: “Boresha Maisha Yako”
Ni jambo la kawaida kutaka kuwa na maisha bora. Makampuni ya matangazo ya kibiashara hutoa ujumbe wa kwamba tamaa zetu zote, iwe ni kuwa na afya nzuri, usalama, kutuliza mkazo, na kuboresha mahusiano, zinaweza kutoshelezwa kwa kununua vitu vinavyofaa.
UKWELI WA MAMBO:
Kadiri tunavyozidi kuwa na vitu vingi, ndivyo hali yetu ya maisha inavyozorota. Mtu anahitaji wakati na pesa za ziada ili kutunza vitu vya ziada anavyonunua. Mkazo huongezeka kwa sababu ya madeni, na mtu anakosa wakati wa kuwa pamoja na familia na marafiki.
Kanuni: “Uhai wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.”—Luka 12:15, Biblia Habari Njema.
AHADI: “Jipatie Umashuhuri na Heshima”
Si watu wengi watakubali kwamba wao hununua vitu ili wawapendeze wengine. Hata hivyo, Jim Pooler anasema hivi: “Watu wanaponunua vitu, jambo muhimu linalowachochea ni kutaka kushindana na marafiki, majirani, wafanyakazi, na watu wa ukoo.” Kwa sababu hiyo, makampuni yanapotangaza bidhaa fulani mara nyingi yanaonyesha watu waliofanikiwa maishani na matajiri wakitumia bidhaa hizo. Ujumbe ambao matangazo hayo unapitisha kwa wanunuzi ni: “Hata wewe unaweza kufanikiwa na kuwa tajiri.”
UKWELI WA MAMBO:
Kupima thamani yetu kwa kujilinganisha na wengine hutufanya tusiridhike. Mtu akipata kitu alichokuwa akitamani, mara moja anaanza kutamani kitu kingine.
Kanuni: “Anayependa fedha hatatosheka na fedha.”—Mhubiri 5:10.
AHADI: “Jionyeshe Wewe Ni Nani”
Kitabu Shiny Objects (Vitu Vinavyong’aa) kinaeleza hivi: “Njia moja ambayo tunawaonyesha wengine sisi ni watu aina gani (au tungependa kuonwa kuwa watu wa aina gani) ni jinsi tunavyotumia au kuonyesha mali zetu.” Wauzaji bidhaa wanatambua jambo hilo na wao huhusianisha bidhaa zenye majina maarufu—hasa bidhaa za bei ghali—na mtindo fulani wa maisha au kiwango cha maisha.
Una maoni gani kujihusu, na ungependa watu wawe na maoni gani kukuhusu? Je, ungependa kuonekana kuwa mtu anayependa mitindo ya kisasa ya kifahari au mwenye umbo lenye kuvutia? Chochote unachotamani, wauzaji bidhaa wanakuahidi kwamba ukinunua bidhaa za kampuni fulani, unaweza kuwa mtu yeyote yule unayetaka.
UKWELI WA MAMBO:
Hakuna bidhaa yoyote unayonunua inayoweza kukubadili au kukupa sifa zenye kupendeza kama vile unyoofu na kushikilia kanuni za maadili.
Kanuni: “Kujipamba kwenu kusiwe . . . kule kujivika mapambo ya dhahabu au kuvaa mavazi ya nje, bali kuwe yule mtu wa siri wa moyoni.”—1 Petro 3:3, 4.
-
-
Jinsi ya Kuepuka Kununua Vitu Kupita KiasiAmkeni!—2013 | Juni
-
-
Jinsi ya Kuepuka Kununua Vitu Kupita Kiasi
Mbali na kushinikizwa na wauzaji bidhaa, hisia zetu pamoja na mazoea yetu yanaweza kutuchochea kununua vitu kupita kiasi. Yafuatayo ni madokezo sita yatakayokusaidia kudhibiti ununuzi wako.
Epuka kununua vitu ambavyo hukupangia. Je, wewe hufurahia msisimuko unaotokana na kununua vitu, hasa vile vilivyopunguzwa bei? Ikiwa ndivyo, huenda ukawa na mwelekeo wa kununua vitu ambavyo hukupangia. Ili kuepuka tabia hiyo, tua na ufikirie matokeo ya kununua, kumiliki, na kudumisha kitu unachotaka kununua. Fikiria kuhusu vitu ulivyonunua bila kupangia na baadaye ukajuta kwamba ulivinunua. Chukua muda kufikiria kwa uzito kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Epuka kununua vitu ili tu ujihisi vizuri. Kununua vitu kunaweza kukutuliza kwa muda unapohisi kuwa umeshuka moyo. Lakini hisia zisizofaa zinaporudi, huenda ukahisi kwamba unahitaji kununua vitu vingine ili upate kitulizo. Badala ya kununua vitu ili ujihisi vizuri, zungumza na marafiki wanaoweza kukusaidia au jihusishe katika utendaji fulani kama vile kwenda matembezi.
Usifanye ununuzi wa vitu kuwa tafrija. Maduka makubwa ya kifahari yamefanya ununuzi wa vitu kuwa burudani. Ingawa huenda lengo lako la kwenda madukani au kutazama bidhaa kwenye Intaneti likawa ni kufurahisha macho tu, vitu unavyoona vimekusudiwa kuchochea tamaa yako ya kununua. Nenda madukani wakati tu unahitaji kununua kitu fulani hususa, na ununue kitu hicho tu.
Uwe mwangalifu unapochagua marafiki. Mtindo wa maisha na mazungumzo ya marafiki wako yanaweza kuchochea tamaa yako. Ikiwa unanunua vitu vingi kupita kiasi ili tu ufanane na marafiki wako, basi chagua marafiki ambao hawakazii sana pesa au mali.
Chukua mikopo kwa hekima. Ni rahisi kuchukua mikopo bila kufikiria matokeo. Iwe unatumia njia gani kuchukua mkopo, jaribu kulipa kiasi fulani cha mkopo huo kila mwezi. Jua ni kiasi gani cha riba utakachotozwa kwa mkopo unaochukua. Jihadhari na mashirika ya kifedha yanayotoa mkopo wa kiasi kikubwa cha pesa bila masharti mengi. Badala ya kuchukua mkopo au kununua vitu kwa mkopo, weka pesa akiba hadi utakapoweza kununua kitu unachohitaji kwa pesa taslimu.
Fahamu hali yako ya kifedha. Ni rahisi kutumia pesa kupita kiasi kwa sababu hujui hali yako ya kifedha. Weka rekodi ya matumizi yako na ujue hali yako ya kifedha kwa ujumla. Panga bajeti ya matumizi ya kila mwezi ikitegemea mapato yako na matumizi ya wakati uliopita. Linganisha matumizi yako na bajeti uliyopanga. Mwombe rafiki unayemwamini akusaidie kuelewa mambo ya kifedha ambayo hujui.
-