Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Je, Maandamano Yatatatua Matatizo?
    Amkeni!—2013 | Julai
    • [Picha katika ukurasa wa 6]

      HABARI KUU

      Je, Maandamano Yatatatua Matatizo?

      Mashahidi wa Yehova ambao ndio wachapishaji wa gazeti hili, hawajihusishi katika siasa. (Yohana 17:16; 18:36) Kwa hiyo, ingawa makala hii inaripoti mifano hususa ya maasi ya kijamii, haipendelei taifa moja au kuunga mkono upande wowote wa masuala ya kisiasa.

      SUBIRA ya Mohamed Bouazizi ilifikia kikomo mnamo Desemba 17, 2010. Alikuwa mchuuzi wa barabarani nchini Tunisia, mwenye umri wa miaka 26, na alikuwa amekata tamaa kwa sababu ya kukosa kazi nzuri. Pia alijua kwamba maofisa wafisadi walikuwa na zoea la kudai hongo. Asubuhi ya tarehe hiyo, maofisa walichukua mapeasi, ndizi, na matofaa ambayo Mohamed alikuwa akiuza. Walipochukua mizani yake, alikataa, na watu fulani walioshuhudia jambo hilo walisema kwamba alipigwa kofi na mwanamke ambaye ni ofisa wa polisi.

      Akiwa amefedheheshwa na kukasirika, Mohamed alienda kwenye ofisi ya serikali iliyokuwa karibu ili kutoa malalamiko yake lakini hakuna aliyemsikiliza. Akiwa mbele ya jengo hilo, inasemekana kwamba alisema hivi kwa sauti kubwa, “Mnataka niiruzuku familia yangu kwa njia gani?” Baada ya kujimwagia petroli, alijiwasha moto. Alikufa kutokana na majeraha ya moto majuma matatu hivi baadaye.

      Tendo hilo la Mohamed Bouazizi lilikuwa na athari kubwa kwa watu wa Tunisia na nchi nyingine. Watu wengi wanasema kwamba tendo lake ndilo lililochochea maasi yaliyoipindua serikali ya nchi hiyo, na punde si punde maandamano yakaenea katika nchi nyingine za Kiarabu. Bunge la Uingereza lilimtunukia Bouazizi na watu wengine wanne Tuzo la Sakharov la Uhuru wa Kutoa Maoni, na gazeti The Times la London lilimweka katika orodha yao ya mtu aliyekuwa na uvutano mkubwa zaidi katika mwaka wa 2011.

      Kama kisa hicho kinavyoonyesha, maandamano yanaweza kuwa na uvutano mkubwa sana. Lakini ni nini chanzo cha maandamano ambayo yametukia kwa wingi hivi karibuni? Je, kuna suluhisho lingine?

      Kwa Nini Maandamano Yameongezeka?

      Maandamano mengi yanachochewa na mambo yafuatayo:

      • Kutoridhishwa na mifumo ya kijamii. Kwa kawaida watu hawana tamaa ya kuandamana wanapoona kwamba serikali na hali ya uchumi inatimiza mahitaji yao. Wao hupeleka matatizo yao kwa wenye mamlaka. Kwa upande mwingine, watu wanapoona wenye mamlaka ni wafisadi, hawafuati haki, na wanawapendelea tu watu wachache, basi wao huasi.

      • Kichocheo. Mara nyingi, tukio fulani huwasukuma watu watende, waache kufikiri kwamba hawawezi kufanya lolote na kuanza kuamini kwamba lazima wachukue hatua fulani. Kwa mfano, kisa cha Mohamed Bouazizi kilianzisha maandamano makubwa nchini Tunisia. Nchini India, mgomo wa kususia chakula ulioanzishwa na mwanaharakati Anna Hazare ili kupinga ufisadi ulitokeza maandamano yaliyofanywa na wafuasi wake katika majiji na miji 450.

      • Kama vile Biblia ilivyosema hapo zamani, tunaishi katika “ulimwengu ambapo watu fulani wana mamlaka na wengine lazima wateseke chini yao.” (Mhubiri 8:9, Good News Translation) Ufisadi na ukosefu wa haki umeenea sana leo kuliko wakati huo. Sasa kuliko wakati mwingine wowote, watu wanaona jinsi ambavyo mifumo ya kiuchumi na kisiasa imewakatisha tamaa. Simu za hali ya juu, Intaneti, na taarifa za habari ambazo hutolewa saa 24 zinafanya matukio yaliyotokea hata katika sehemu za mbali sana yawachochee watu katika maeneo mengine mengi.

      Maandamano yametimiza nini?

      Watu wanaounga mkono maasi ya kijamii wanadai kwamba maandamano yametimiza mambo yafuatayo:

      • Yameleta kitulizo kwa maskini. Kufuatia ghasia zilizotokea huko Chicago, Illinois, Marekani kwa sababu ya kuongezeka kwa kodi ya nyumba wakati wa ule Mshuko Mkubwa wa Kiuchumi wa miaka ya 1930, wasimamizi wa jiji waliacha kuwafukuza wapangaji na wakafanya mipango ili baadhi ya wafanya ghasia wapate kazi. Maandamano kama hayo katika jiji la New York City yalifanya wapangaji 77,000 waliokuwa wamefukuzwa kutoka nyumba zao warudishwe.

      • Yametatua ukosefu wa haki. Hatimaye, ule mgomo wa mwaka wa 1955/1956 wa kukataa kupanda mabasi ya jiji huko Montgomery, Alabama, Marekani ulifanya sheria kuhusu ubaguzi wa rangi kwenye mabasi ziondolewe.

      • Yamesimamisha miradi ya ujenzi. Mnamo Desemba 2011, kwa sababu ya wasiwasi kuhusu uchafuzi wa mazingira, makumi ya maelfu ya watu waliandamana kupinga kujengwa kwa mtambo wa kutokeza umeme unaotumia makaa ya mawe karibu na Hong Kong, kwa hiyo ujenzi huo ulifutiliwa mbali.

      [Picha katika ukurasa wa 7]

      Ingawa huenda waandamanaji fulani wakatimiza malengo yao, Ufalme wa Mungu unatoa suluhisho bora zaidi

      Bila shaka si kila mara waandamanaji hupata wanachotaka. Kwa mfano, huenda viongozi wakawaadhibu badala ya kuwatimizia matakwa yao. Hivi karibuni rais wa nchi moja huko Mashariki ya Kati alisema hivi kuhusu harakati za maandamano huko: “Ni lazima tuwachukulie hatua kali,” na maelfu wamekufa katika maasi hayo.

      Hata waandamanaji wakitimiza malengo yao, matokeo ya maandamano huleta matatizo mapya. Mtu mmoja aliyesaidia kumtoa mamlakani kiongozi wa nchi moja Afrika aliliambia hivi gazeti Time kuhusu utawala mpya: “Ulikuwa ushindi ambao mara moja uligeuka kuwa machafuko.”

      Je, kuna suluhisho bora kuliko maandamano?

      Watu wengi maarufu wamesema kwamba kuandamana ili kupinga mifumo yenye kukandamiza ni wajibu wa mwanadamu. Kwa mfano, Václav Havel, aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Cheki, ambaye alifungwa gerezani kwa miaka mingi kwa sababu ya harakati zake za kutetea haki za kibinadamu, aliandika hivi katika mwaka wa 1985: “Hakuna jambo lolote ambalo [mpinzani] anaweza kutoa isipokuwa uhai wake—na anautoa kwa sababu hakuna njia nyingine yoyote ya kuonyesha msimamo wake kuhusu mambo anayoamini kuwa kweli.”

      Maneno hayo ya Havel yalithibitishwa wazi na mambo ambayo Mohamed Bouazizi na wengine walifanya kwa kutamauka. Katika nchi moja barani Asia, kumekuwa na visa vingi vya watu kujiteketeza ili kupinga ukandamizaji wa kisiasa na kidini. Akieleza ni kwa nini wanachukua hatua hiyo kali, mtu mmoja aliwaambia hivi waandishi wa gazeti Newsweek: “Hatuna bunduki. Hatutaki kuwaumiza wanadamu wengine. Watu wanaweza kufanya jambo gani lingine zaidi ya hilo?”

      Biblia inatoa suluhisho la ukosefu wa haki, ufisadi, na ukandamizaji. Inaeleza kuhusu serikali ambayo Mungu ameisimamisha mbinguni itakayochukua mahali pa mifumo ya kisiasa na kiuchumi ambayo imeshindwa kutimiza mahitaji ya watu na hivyo kusababisha maandamano. Unabii kumhusu Mtawala wa serikali hiyo unasema hivi: “Atamkomboa maskini anayelilia msaada, pia mwenye kuteseka na yeyote ambaye hana msaidizi. Ataikomboa nafsi yao kutoka katika ukandamizaji na katika jeuri.”—Zaburi 72:12, 14.

      Mashahidi wa Yehova wanaamini kwamba Ufalme wa Mungu ndio tumaini pekee la kweli litakalowaletea wanadamu ulimwengu wenye amani. (Mathayo 6:9, 10) Kwa sababu hiyo, Mashahidi wa Yehova hawajihusishi katika maandamano. Lakini je, kweli inapatana na akili kuamini kwamba serikali ya Mungu itaondoa mambo yanayofanya watu waandamane? Huenda isionekane hivyo. Hata hivyo, watu wengi wamejifunza kuutumaini utawala wa Mungu. Mbona usijichunguzie mwenyewe?

  • Niliona Ukosefu wa Haki Kila Mahali
    Amkeni!—2013 | Julai
    • Niliona Ukosefu wa Haki Kila Mahali

      Limesimuliwa na Patrick O’Kane

      [Picha katika ukurasa wa 8]

      NILIZALIWA mwaka wa 1965 katika familia maskini huko Ireland Kaskazini. Nililelewa Mkoa wa Derry wakati wa ile “Mizozo,” yaani, vita vyenye jeuri kati ya Wakatoliki na Waprotestanti ambavyo viliendelea kwa zaidi ya miaka 30. Wakatoliki waliokuwa wachache walihisi kwamba wamebaguliwa na serikali iliyokuwa na Waprotestanti wengi, na walilalamika kwamba kulikuwa na matendo ya ukosefu wa haki kama vile kukandamizwa na polisi, hila katika uchaguzi, kunyimwa ajira, na upendeleo katika kutoa makao.

      Niliona ukosefu wa haki na ukosefu wa usawa kila mahali. Hata siwezi kukumbuka ni mara ngapi nilipigwa, niliburutwa kutoka kwenye gari na kuelekezewa bunduki, au kuhojiwa na kupekuliwa na polisi au askari-jeshi. Nilihisi kwamba ninaonewa, na nikajiambia, ‘Mambo ni mawili, ama nikubali kutendewa hivi, ama nilipize kisasi!’

      Nilishiriki katika maandamano ya mwaka wa 1972 yaliyoitwa Jumapili Yenye Umwagaji wa Damu, ili kuwakumbuka watu 14 waliopigwa risasi na kuuawa na wanajeshi wa Uingereza, na pia nilishiriki katika maandamano ya kuwakumbuka wafungwa waliopinga utawala wa Uingereza huko Ireland Kaskazini ambao walisusia chakula na kufa katika mwaka wa 1981. Nilisimamisha bendera za Ireland Kaskazini zilizokuwa zimepigwa marufuku na nikaandika mahali popote ukutani maneno yenye kupinga utawala wa Uingereza. Ni kana kwamba kila mara kulikuwa na ukatili au mauaji ya Mkatoliki yaliyofanya watu waandamane. Mara nyingi maandamano hayo yaligeuka kuwa ghasia.

      Nilipokuwa katika chuo kikuu, nilijiunga na kikundi cha wanafunzi walioandamana ili kutetea mazingira. Baadaye nilihamia London, na nikiwa huko nilijiunga na vikundi vya waandamanaji wa kijamii waliokuwa wakipinga sera za serikali ambazo ziliwanufaisha tu matajiri na kuwaumiza maskini. Nilishiriki katika migomo ya vyama vya wafanyakazi ili kupinga kupunguzwa kwa mishahara, na pia nilishiriki katika maandamano ya kupinga kodi ya kichwa ya mwaka wa 1990. Maandamano hayo yalisababisha uharibifu mkubwa katika uwanja wa Trafalgar Square.

      Hata hivyo, mwishowe nilikatishwa tamaa. Badala ya kutimiza malengo yake, mara nyingi maandamano yalichochea chuki tu.

      Licha ya kuwa na nia nzuri, wanadamu hawawezi kuleta haki na usawa

      Katika kipindi hicho, rafiki yangu alinijulisha kwa Mashahidi wa Yehova. Walinionyesha katika Biblia kwamba Mungu anajali tunapoteseka na kwamba ataondoa madhara yote ambayo yamesababishwa na wanadamu. (Isaya 65:17; Ufunuo 21:3, 4) Licha ya kuwa na nia nzuri, wanadamu hawawezi kuleta haki na usawa. Tunahitaji mwongozo wa Mungu na pia uwezo wake wa kushinda roho wasioonekana ambao ndio wanaosababisha matatizo ulimwenguni.—Yeremia 10:23; Waefeso 6:12.

      Sasa naona kwamba maandamano niliyoshiriki ya kupinga ukosefu wa haki yalikuwa bure tu kama vile kupanga vyombo katika nyumba inayoteketea. Nimefarijika sana kujua kwamba kuna siku hakutakuwa na ukosefu wa haki katika dunia hii, kutakuwa na usawa kila mahali.

      Biblia inafundisha kwamba Yehova Mungu ni “mpenda-haki.” (Zaburi 37:28) Hiyo ni sababu moja inayotuhakikishia kwamba ataleta haki kwa njia ambayo serikali za kibinadamu zimeshindwa kufanya. (Danieli 2:44) Ikiwa ungependa kujifunza mengi, wasiliana na Mashahidi wa Yehova katika eneo lenu au tembelea Tovuti yetu kwenye www.jw.org/sw.

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki