Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 9/13 kur. 14-15
  • Zheng He

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Zheng He
  • Amkeni!—2013
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MAMLAKA, BIASHARA, NA HESHIMA
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2013
  • Vijana Wanatumia Intaneti!
    Amkeni!—2007
  • Jinsi Hali ya Hewa Inavyoweza Kubadili Historia
    Amkeni!—2011
  • “Meli za Kitimu” Zatawala Baharini
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2013
g 9/13 kur. 14-15
[Picha katika ukurasa wa 14]

TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA

Zheng He

“Tumesafiri zaidi ya lia elfu mia moja kupitia bahari kubwa sana na tumeona mawimbi makubwa ya bahari yakiinuka juu sana kama milima, na tumejionea maeneo ya mbali ya watu wasio na ustaarabu . . . huku matanga yetu yaliyo kama mawingu yakitusukuma usiku na mchana kama nyota inayofuata mkondo wake, tukipita juu ya mawimbi hayo makubwa kana kwamba tunakanyaga barabara kuu.”​—Maandishi ya karne ya kumi na tano yanayosemekana yaliandikwa na Zheng He katika jiji la Changle, mkoa wa Fujian, nchini China.

CHINA ni nchi ya mambo makubwa. Ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi na ni moja kati ya nchi zenye ardhi kubwa zaidi duniani. Wachina ndio waliojenga ule Ukuta Mkubwa, ambao ni mojawapo ya miradi mikubwa zaidi ya ujenzi katika historia. Meli zilizojengwa na Maliki Yongle na Xuande wa China wa milki ya Ming, zilikuwa nyingi kuliko zile ambazo nchi yoyote ingeweza kuunda kwa karne tano zilizofuata. Ofisa mkuu wa meli hizo alikuwa Mwislamu kutoka kusini-magharibi mwa China anayeitwa Zheng He.

MAMLAKA, BIASHARA, NA HESHIMA

Kulingana na maandishi yaliyoonyeshwa kwa sehemu mwanzoni mwa makala hii, utume wa Zheng He ulikuwa “kuonyesha mamlaka ya (maliki) ya kubadili mambo na kuwatendea watu wa maeneo ya mbali kwa fadhili.” Kutokana na safari hizo, maandishi hayo yanasema, “nchi zilizo mbali na watu kutoka miisho ya dunia wamekuwa wote raia [wa China] . . . watu wasio na ustaarabu upande ule mwingine wa bahari . . . wamekuja kwenye [ua wa maliki] wakiwa na vitu na zawadi zenye thamani.”

[Ramani katika ukurasa wa 15]

Baadhi ya bandari ambazo meli za Zheng He zilipitia

Kusudi la maliki wa milki ya Ming la kufunga safari hizo limejadiliwa kwa muda mrefu. Wengine humwona Zheng He kuwa balozi wa utamaduni na amani kwa ajili ya taifa lenye nguvu na lenye amani. Wengine huona safari zake kuwa za kueneza ukoloni dhidi ya mataifa mengine. Kwa kweli, Zheng He aliwapa watawala waliomkaribisha zawadi nzuri na utegemezo wa kisiasa, lakini wale waliokataa kujitiisha kwa maliki wa China, aliwatiisha na kuwafanya kuwa wafungwa. Kwa sababu ya safari za Zheng He, watawala wengi sana katika maeneo ya Bahari ya Hindi walituma mabalozi nchini China ili kumpa maliki heshima ya pekee.

Vyovyote vile, meli za Zheng He zilibeba pia vyombo vya mbao vyenye mapambo na vilivyopakwa vanishi, vyombo vya kauri, na hariri. Vitu hivyo vilitengenezwa na mafundi Wachina ili vikauzwe katika bandari za mbali. Meli hizo zilirudi zikiwa na vito, pembe za tembo, vikolezo, mbao za maeneo yenye joto, na vitu vingine vyenye thamani vilivyopendwa na Wachina. Pia, zilibeba twiga, ambaye alitokeza msisimuko mkubwa sana nchini China. Kupitia kubadilishana huko kwa bidhaa na mawazo, ulimwengu ulipata kuona sehemu ndogo ya ustaarabu wa China wa karne ya 15.

Safari hizo kubwa hazikuendelea. Miaka kadhaa tu baada ya safari za Zheng He, China iliacha kabisa kujihusisha katika biashara na uhusiano wowote na nchi nyingine. Akihisi kwamba hakuna uhitaji wa kuwa na uhusiano wowote na nchi nyingine, maliki mpya pamoja na washauri wake Wakonfyushasi walijaribu kuzuia China isiathiriwe na uvutano kutoka nje. Waliamua meli hizo zilizobeba hazina zifutwe katika historia, na wakaharibu rekodi zozote kuhusiana na safari zake kubwa pamoja na meli zenyewe. Ni katika miaka ya karibuni tu ndipo watu, nchini China na pia nje, wamegundua kuhusu kipindi hicho muhimu ambapo meli nyingi sana za Zheng He zilifunga safari zake.

a Neno li ni kipimo cha Kichina ambacho kwa karne mbalimbali kimerejelea urefu tofauti-tofauti. Inaaminiwa kwamba wakati wa Zheng He, li moja ilirejelea umbali wa nusu kilomita hivi.

TAARIFA FUPI

  • Meli za milki ya Ming zikiwa chini ya uongozi wa Zheng He zilisafiri mara saba kati ya mwaka wa 1405 na 1433.

  • Huenda kulikuwa na meli 200 au zaidi—meli za vita, meli za mizigo, meli zilizobeba maji, meli za kusafirisha farasi, na kadhalika. Zilibeba zaidi ya mabaharia 27,000, maofisa wa serikali, wanajeshi, wafanyabiashara, watu wa kufanya ukarabati, na wengine.

  • Hakuna taifa lingine ambalo liliwahi tena kukusanya meli nyingi kama zile za Zheng He hadi wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Meli zake zilisafiri hadi bandari za Mashariki ya Mbali na Bahari ya Hindi, kufika hata Afrika Mashariki.

  • Mabaharia watatu wa Zheng He waliandika kuhusu mambo waliyojionea yanayotusaidia kujua mengi kuhusu safari zake.

Meli za Hazina za Zheng He Zilikuwa na Ukubwa Gani na Zilikuwa Ngapi?

[Picha]

Rekodi za kihistoria za milki ya Ming zinaonyesha kwamba meli za hazina za Zheng He zilikuwa na ukubwa wa ajabu—urefu wa mita 136 na upana wa mita 56. Ni vigumu kwa wasomi kukubali na kuthibitisha vipimo hivyo, kwa sababu meli zilizotengenezwa kwa mbao zenye urefu unaozidi mita 90 zinaweza kuvunjika kwa urahisi.

“Mambo yote yanaonyesha kwamba masimulizi kuhusu ukubwa wa meli hizo yametiliwa chumvi,” inasema makala moja kuhusu habari hiyo. “Huenda ikapatana na akili kusema kuwa meli hizo zilikuwa na urefu wa mita 60 hadi 75 hivi badala ya mita 135.” Vyovyote vile, katika karne ya 15, lilikuwa jambo la ajabu kuona meli yenye urefu wa zaidi ya mita 60, na Zheng He alikuwa na meli 62 zenye urefu huo!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki