Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 10/13 kur. 6-7
  • Mtaalamu wa Biokemia Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mtaalamu wa Biokemia Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu
  • Amkeni!—2013
  • Habari Zinazolingana
  • Mwanabiologia Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu
    Amkeni!—2014
  • Imarisha Imani Yako Katika Muumba
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2021
  • Mwanabiolojia Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu
    Amkeni!—2014
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2013
g 10/13 kur. 6-7
[Picha katika ukurasa wa 6]

MAHOJIANO | DAVEY LOOS

Mtaalamu wa Biokemia Anaeleza Kwa Nini Anamwamini Mungu

Dakt. Davey Loos ni mtaalamu wa biokemia nchini Ubelgiji. Wakati fulani, alitilia shaka kuwepo kwa Muumba na badala yake akaamini nadharia ya mageuzi. Baadaye, alibadili maoni yake. Ni nini kilichomfanya mtafiti huyo abadili maoni yake kuhusu chanzo cha uhai? Mwandishi wa Amkeni! alimhoji Dakt. Loos kuhusu taaluma yake na imani yake.

Ulianzaje kupendezwa na mambo ya kisayansi?

[Picha katika ukurasa wa 6]

Nilipoenda kwenye chuo kikuu, niliamua kusomea kemia. Nilipendezwa hasa na protini na kemikali zilizo ndani ya kiini cha chembe, ambazo ndizo molekuli tata zaidi duniani. Baada ya muda, nilivutiwa sana na jinsi molekuli fulani zinavyotenda zinapopigwa na mwangaza wa jua.

Je, uliwahi kuamini kwamba kuna Mungu?

Nilimwamini nilipokuwa mvulana. Lakini baadaye, nilipokuwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Leuven, nilifundishwa kwamba viumbe hai vilitokea kupitia mageuzi. Maprofesa walifanya mageuzi hayo yaonekane kuwa mambo yenye kustaajabisha sana. Walikuwa wanasayansi wenye uzoefu, kwa hiyo niliamini walichosema. Mwishowe, ilikuwa vigumu sana kwangu kuamini kwamba kuna Mungu.

Ni nini kilichokufanya ubadili maoni yako kuhusu chanzo cha uhai?

Katika mwaka wa 1999, nilikutana na rafiki tuliyekuwa tumesoma pamoja ambaye sasa ni Shahidi wa Yehova na nikahudhuria mkutano wao. Pia katika kipindi hichohicho, Shahidi mwingine wa Yehova alinitembelea nyumbani na kuniachia kitabu Je, Kuna Muumba Anayekujali?a

Ulikionaje kitabu hicho?

Nilivutiwa sana na utafiti uliokuwa umefanywa. Nilianza kujiuliza ikiwa vitu vya asili vilijitokeza vyenyewe.

Ni nini kilichokuvutia ulipochunguza vitu vya asili?

Kazi yangu nikiwa mtaalamu wa biokemia ilihusisha kuchunguza jinsi ambavyo molekuli za bakteria fulani hufanya kazi. Bakteria hizo zinaishi baharini na hazitegemei viumbe wengine ili kupata chakula. Watafiti fulani wanafikiri kwamba bakteria hizo ndizo zilizotokea kwanza kabla ya vitu vingine vyote duniani. Kwa kutumia nishati ya jua, bakteria hizo hutumia utaratibu tata sana wa kikemikali kubadili maji na kaboni dioksidi kuwa chakula, ingawa utaratibu huo bado haujaeleweka vizuri kabisa. Pia nilishangazwa na jinsi ambavyo bakteria hizo zinaweza kunasa nuru kwa njia yenye kustaajabisha.

Kwa kuwa majani pia hutumia nuru ya jua kutengeneza chakula, ni nini kilichokushangaza kuhusu bakteria hizo?

Kadiri unavyoingia ndani zaidi ya bahari, ndivyo unavyopata nuru kidogo zaidi. Kwa hiyo, lazima bakteria hizo zinase nuru yoyote ile inayozifikia, nazo hufanya hivyo kwa kutumia vipapasio vya pekee sana. Nishati inayokusanywa inaelekezwa kwenye vituo vya kutokeza chakula kwa ustadi wa hali ya juu sana. Ubuni huo wa kunasa nuru umewavutia sana watu wanaotengeneza vifaa ya kutokeza umeme kwa kutumia nishati ya jua. Bila shaka, vifaa hivyo vilivyotengenezwa na wanadamu haviwezi kufanya kazi vizuri sana kama mifumo inayopatikana katika bakteria.

Hilo lilikufanya ufikie mkataa gani?

Nilifikiria kuhusu mainjinia wanaojaribu kuiga mifumo yenye kustaajabisha inayopatikana katika viumbe hai, na nikafikia mkataa kwamba lazima uhai uwe ulibuniwa na Mungu

Nilifikiria kuhusu mainjinia wanaojaribu kuiga mifumo yenye kustaajabisha inayopatikana katika viumbe hai, na nikafikia mkataa kwamba lazima uhai uwe ulibuniwa na Mungu. Lakini sikufikia mkataa huo kwa sababu tu ya mambo niliyojifunza kutokana na sayansi. Ulitegemea pia mambo niliyojifunza kwa makini katika Biblia.

Ni nini kilichokusadikisha kwamba Biblia imetoka kwa Mungu?

Jambo moja lililonisadikisha ni utimizo wa unabii wa Biblia hata katika mambo madogo-madogo. Kwa mfano, Isaya alitabiri mambo mengi hususa kuhusu kifo na maziko ya Yesu karne kadhaa kabla ya mambo hayo kutukia. Tunajua kwamba unabii huo uliandikwa kabla ya Yesu kufa kwa sababu Kitabu cha Kukunjwa cha Isaya, kilichopatikana kule Qumran, kilinakiliwa karibu miaka 100 kabla ya Yesu kuzaliwa.

Unabii huo unasema hivi: “Atafanya kaburi lake liwe pamoja na waovu, na pamoja na jamii ya matajiri katika kifo chake.” (Isaya 53:9, 12) Na hivyo ndivyo ilivyotokea. Yesu aliuawa kando ya wahalifu lakini akazikwa katika kaburi la familia tajiri. Huo ni mfano mmoja tu wa unabii mwingi uliotimizwa ulionisadikisha kwamba Biblia imeongozwa na roho ya Mungu. (2 Timotheo 3:16) Baada ya muda, nikawa Shahidi wa Yehova.

Kwa nini unafurahia kuwa Shahidi wa Yehova?

Imani yetu haipingani na mambo hakika ya kisayansi

Imani yetu haipingani na mambo hakika ya kisayansi. Pia, kanuni zinazotuongoza zinatoka katika Biblia. Nikiwa Shahidi wa Yehova, ninafurahia kuwaeleza wengine ujumbe wenye kufariji wa Biblia na kuwasaidia kupata majibu ya maswali yao.

a Kimechapishwa na Mashahidi wa Yehova.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki