Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w18 Agosti kur. 31-32
  • Jinsi Mbegu za Kwanza za Ufalme Zilivyopandwa Nchini Ureno

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jinsi Mbegu za Kwanza za Ufalme Zilivyopandwa Nchini Ureno
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2018
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2018
w18 Agosti kur. 31-32

HIFADHI YETU YA VITU VYA KALE

Jinsi Mbegu za Kwanza za Ufalme Zilivyopandwa Nchini Ureno

MAWIMBI ya bahari ya Atlantiki yalipokuwa yakipiga meli iliyokuwa njiani kwenda Ulaya, abiria George Young, alikuwa akitafakari kwa furaha matokeo mazuri ya mambo aliyokuwa ametimiza kwa ajili ya Ufalme nchini Brazili.a Hata hivyo, safari ilipokuwa ikiendelea, Ndugu Young alikazia fikiria mgawo wake mpya—mgawo katika maeneo mengi ambayo hayakuwa yamehubiriwa nchini Hispania na Ureno. Alitumaini kwamba baada ya kuwasili huko, angefanya mipango ili Ndugu J. F. Rutherford aje kutoa hotuba za Biblia na kisha kusambaza trakti 300,000!

George Young akisafiri kwa meli

George Young alisafiri mara nyingi baharini katika safari zake za kuhubiri

Alipowasili jijini Lisbon katika majira ya kuchipua ya mwaka wa 1925, Ndugu Young alikuta hali ikiwa imevurugika. Mabadiliko yaliyotokea katika nchi ya Ureno mwaka wa 1910 yalikuwa yamekomesha utawala uliokuwepo na kufanya Kanisa Katoliki lipoteze cheo chake. Watu walipata uhuru mwingi zaidi, lakini kuliendelea kuwa na vurugu nchini.

Mara tu baada ya Ndugu Young kumaliza kufanya mipango ili Ndugu Rutherford atoe hotuba yake, serikali iliweka sheria ya kijeshi kwa sababu ya jaribio lililokuwa limefanywa la kuipindua serikali. Mwandishi wa shirika la British and Foreign Bible Society alimwonya Ndugu Young kwamba hapana shaka atakabili upinzani mwingi. Hata hivyo, Ndugu Young aliomba apewe kibali cha kutumia ukumbi wa michezo wa Shule ya Sekondari ya Camões, na akaruhusiwa kuutumia!

Kisha Mei 13 ikafika—siku iliyokuwa imepangwa ili Ndugu Rutherford atoe hotuba. Watu walikuwa wakiisubiri kwa hamu! Kulikuwa na mabango kwenye kuta za majengo na matangazo kwenye magazeti yakitangaza hotuba ya watu wote yenye kichwa “Jinsi ya Kuishi Duniani Milele.” Wapinzani wa kidini walichapisha haraka-haraka makala kwenye gazeti lao wakiwaonya wasomaji kuhusu “manabii wa uwongo” waliokuwa wamekuja karibuni. Pia, kwenye mwingilio wa ukumbi wa michezo wapinzani waligawa broshua nyingi zenye habari zilizopinga mafundisho ambayo Ndugu Rutherford alifundisha.

Hata hivyo, watu 2,000 hivi walikusanyika kwenye ukumbi huo, na idadi sawa na hiyo haikuruhusiwa kuingia kwa sababu hakukuwa na nafasi. Baadhi ya watu walisikiliza kwa makini wakiwa wamejishikilia kwenye ngazi zilizotengenezwa kwa kamba zilizoning’inia kwenye kingo za ukumbi; na wengine wakiwa wameketi juu ya vifaa vya kufanyia mazoezi.

Hata hivyo, hakukukosa vurugu. Wapinzani walipiga kelele kwa sauti kubwa na kuvunja viti. Lakini Ndugu Rutherford hakuwa na wasiwasi na kwa utulivu alipanda juu ya meza ili aweze kusikika. Alipomaliza hotuba yake saa sita hivi usiku, zaidi ya watu 1,200 walitoa majina na anwani zao ili watumiwe machapisho ya Biblia. Siku iliyofuata, gazeti la O Século lilichapisha makala kuhusu hotuba ya Ndugu Rutherford.

Kufikia Septemba 1925, toleo la gazeti la Mnara wa Mlinzi katika Kireno lilianza kuchapishwa nchini Ureno. (Tayari toleo la gazeti hilo katika Kireno lilikuwa limechapishwa nchini Brazili.) Karibu na kipindi hicho, Virgílio Ferguson, Mwanafunzi wa Biblia nchini Brazili, alianza kufanya mipango ya kuhamia nchini Ureno ili asaidie katika kazi ya Ufalme. Awali, alifanya kazi na Ndugu Young kwenye ofisi ndogo ya tawi ya Wanafunzi wa Biblia nchini Brazili. Baada ya muda mfupi, Virgílio alifunga safari pamoja na mke wake, Lizzie, kwenda kuungana na Ndugu Young kwa mara nyingine tena. Ndugu Ferguson alifunga safari hiyo kwa wakati mwafaka kwa sababu baada ya muda mfupi Ndugu Young angeenda kwenye migawo mingine ya kuhubiri, iliyotia ndani kuhubiri maeneo ya Muungano wa Sovieti.

Kibali cha makazi cha Lizzie na Virgílio Ferguson, mwaka wa 1928

Kibali cha makazi cha Lizzie na Virgílio Ferguson, mwaka wa 1928

Mapinduzi ya kijeshi nchini Ureno yalipoanzisha utawala wa kidikteta, upinzani uliongezeka. Ndugu Ferguson hakuogopa, badala yake alichukua hatua ambazo ziliwalinda Wanafunzi wa Biblia na kuwasaidia kuongeza utendaji wao. Aliomba ruhusa ili nyumba yake itumiwe kwa ukawaida kufanyia mikutano. Katika mwezi wa Oktoba 1927, akapata ruhusa hiyo.

Katika mwaka wa kwanza wa utawala huo wa Kidikteta, watu 450 hivi nchini Ureno walijiandikisha kupokea gazeti la Mnara wa Mlinzi. Zaidi ya hilo, kupitia trakti na vijitabu, neno la ile kweli lilienea katika maeneo yote yaliyokuwa chini ya Milki ya Ureno, yaani, Angola, Msumbiji, Timor Mashariki, Visiwa vya Azores, Cape Verde, Goa, na Madeira.

Mwishoni mwa miaka ya 1920, mtunza bustani wa hali ya chini mwenye asili ya Ureno aliyeitwa Manuel da Silva Jordão, alihamia jijini Lisbon. Alipokuwa akiishi Brazili, alisikia hotuba ya watu wote iliyotolewa na Ndugu Young. Mara moja alitambua kwamba hiyo ilikuwa kweli na alitamani sana kumsaidia Ndugu Ferguson kupanua kazi ya kuhubiri. Ili kufanya hivyo, Manuel alianza kutumikia akiwa kolpota, kama mapainia walivyojulikana wakati huo. Sasa kwa kuwa kulikuwa na mipango mizuri ya kuchapisha na kusambaza machapisho ya Biblia, kutaniko hilo jipya jijini Lisbon lilisitawi!

Mwaka wa 1934, Ndugu na Dada Ferguson walilazimika kurudi Brazili. Hata hivyo, mbegu za kweli zilikuwa tayari zimepandwa. Vurugu zilipokuwa zikiendelea barani Ulaya wakati wa Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe nchini Hispania na Vita vya Pili vya Ulimwengu, kikundi hicho cha ndugu waaminifu kilifanikiwa kubaki imara kiroho. Kwa muda fulani walikuwa kama makaa ya moto ulio hafifu, lakini katika mwaka wa 1947 moto huo ulichochewa kwa njia ya mfano wakati mmishonari wa kwanza kutoka Gileadi, John Cooke alipowasili. Baada ya hapo, idadi ya wahubiri wa Ufalme ilizidi kuongezeka. Hata serikali ilipopiga marufuku utendaji wa Mashahidi wa Yehova katika mwaka wa 1962, idadi ya wahubiri ilizidi kuongezeka. Mashahidi wa Yehova walipotambuliwa kisheria katika mwezi wa Desemba 1974, kulikuwa na zaidi ya wahubiri 13,000 nchini humo.

Leo, wahubiri wa Ufalme zaidi ya 50,000 wanahubiri habari njema ya Ufalme wa Mungu nchini Ureno na katika visiwa kadhaa ambako Kireno kinazungumzwa, kutia ndani visiwa vya Azores na Madeira. Miongoni mwao ni wahubiri wa kizazi cha tatu cha baadhi ya wale waliohudhuria hotuba ya kihistoria ya Ndugu Rutherford ya mwaka wa 1925.

Tunamshukuru Yehova na ndugu na dada hao waaminifu wa zamani ambao walikuwa mstari wa mbele na waliongoza kwa ujasiri kazi ya kuhubiri wakiwa ‘watumishi wa watu wote wa Kristo Yesu kwa mataifa.’—Rom. 15:15, 16.—Hifadhi yetu ya vitu vya kale nchini Ureno.

a Tazama makala yenye kichwa, “Kuna Kazi Zaidi ya Mavuno Inayopaswa Kufanywa” katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Mei 15, 2014, uku. 31-32.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki