Sierra Leone na Guinea
KARIBU miaka 500 hivi iliyopita, mti wa msufi uliota karibu na eneo ambalo Mto Sierra Leone unaingiza maji yake baharini. Kwa miaka 300 mti huo uliendelea kukua na wakati uleule misafara ya watumwa ikipita kando ya mti huo. Wafanyabiashara ya utumwa wakatili waliwasafirisha wanaume, wanawake, na watoto karibu 150,000 hadi nchi za ng’ambo kwenye masoko ya utumwa.
Mti wa Msufi wa kihistoria ulio jijini Freetown
Mnamo Machi 11, 1792, mamia ya watumwa waliowekwa huru kutoka Marekani, walikusanyika chini ya mti huo ili kusherehekea kuwekwa kwao huru na kurudishwa Afrika. Siku hiyo wakaanzisha makazi ambayo yalikuwa alama ya matumaini yao—Freetown, yaani, mji huru. Watumwa waliowekwa huru waliendelea kuwasili Freetown, mwishowe jiji likawa na zaidi ya makabila 100 ya watu wenye asili ya Afrika. Raia hao wapya waliamua kuufanya ule Mti wa Msufi kuwa alama ya uhuru na matumaini.
Karibu miaka 100 hivi, Mashahidi wa Yehova nchini Sierra Leone wamekuwa wakiwafariji jirani zao kwa kuwajulisha tumaini la kupata uhuru mkubwa zaidi, yaani, “uhuru wenye utukufu wa watoto wa Mungu.” (Rom. 8:21) Uhuru huo utamaanisha kuwekwa huru kwa wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na kifo, wakati Ufalme wa Mungu wa Kimasihi utakapoleta amani na Paradiso duniani.—Isa. 9:6, 7; 11:6-9.
Katika miaka 50 iliyopita, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Sierra Leone imekuwa ikisimamia pia kazi ya kuhubiri nchini Guinea. Nchi ya Guinea imekabiliana na misukosuko ya kisiasa, kijamii, na kiuchumi, jambo ambalo limewafanya raia wengi wa nchi hiyo wakubali ujumbe wa Biblia unaogusa moyo.
Mashahidi wa Yehova nchini Sierra Leone na Guinea wametangaza habari njema chini ya vizuizi vingi. Vizuizi hivyo vinatia ndani hali ngumu ya maisha, umaskini uliokithiri, kutojua kusoma na kuandika, tamaduni zilizokita mizizi, migawanyiko ya kikabila, na jeuri mbaya sana. Habari ifuatayo inaonyesha wazi imani yao imara na ibada ya moyo wote ya watumishi hao washikamanifu wa Yehova. Tunatumaini kwamba maelezo yao yatachochea moyo wako na kuimarisha imani yako katika “Mungu anayetoa tumaini.”—Rom. 15:13.