Luka
24 Hata hivyo, siku ya kwanza ya juma walienda mapema sana kwenye kaburi, wakichukua yale manukato waliyokuwa wametayarisha. 2 Lakini wakapata jiwe limebingirishwa kutoka kwenye kaburi la ukumbusho, 3 nao walipoingia hawakuupata mwili wa Bwana Yesu. 4 Walipokuwa wakifadhaika juu ya hilo, tazama! wanaume wawili waliovaa mavazi yenye kumweka walisimama kando yao. 5 Kwa kuwa hao wanawake waliogopa sana na kuweka nyuso zao zikiwa zimegeuzwa kuelekea ardhi, wale wanaume wakawaambia: “Kwa nini mnatafuta yule Aliye hai miongoni mwa wafu? 6 [[Yeye hayupo hapa, bali amefufuliwa.]] Kumbukeni jinsi yeye alivyowaambia alipokuwa angali katika Galilaya, 7 akisema kwamba Mwana wa binadamu lazima akabidhiwe ndani ya mikono ya watu wenye dhambi na kutundikwa mtini na bado siku ya tatu afufuliwe.” 8 Kwa hiyo wakakumbuka semi zake, 9 nao wakarudi kutoka kwenye kaburi la ukumbusho wakaripoti mambo yote haya kwa wale kumi na mmoja na kwa wengine wote. 10 Walikuwa Magdalene Maria, na Yoana, na Maria mama ya Yakobo. Pia, wengineo kati ya wanawake waliokuwa pamoja nao walikuwa wakiwaambia mitume mambo haya. 11 Hata hivyo, semi hizi zilionekana kama upuuzi kwao nao wakawa hawaamini hao wanawake.
12 [[Lakini Petro akainuka akakimbia kwenda kwenye kaburi la ukumbusho, na, akiinama mbele, akaona yale mabendeji pekee. Kwa hiyo akaenda zake, akistaajabu ndani yake mwenyewe juu ya lililokuwa limetukia.]]
13 Lakini, tazama! siku ileile wawili kati yao walikuwa safarini kwenda kijiji kilicho karibu kilometa kumi na moja umbali wa kutoka Yerusalemu na kiitwacho jina Emausi, 14 nao walikuwa wakiongea pamoja juu ya mambo yote haya yaliyokuwa yametukia.
15 Sasa walipokuwa wakiongea na kuzungumza, Yesu mwenyewe alikaribia akaanza kutembea pamoja nao; 16 lakini macho yao yalizuiwa wasimtambue. 17 Akawaambia: “Ni mambo gani haya ambayo nyinyi mnajadiliana kati yenu wenyewe mtembeapo?” Nao wakasimama tuli wakiwa na nyuso zenye huzuni. 18 Kwa kujibu yule aliyeitwa jina Kleopasi akamwambia: “Je, wewe unakaa peke yako kama mgeni wa nchi nyingine katika Yerusalemu na kwa hiyo huyajui mambo ambayo yametukia ndani yalo siku hizi?” 19 Naye akawaambia: “Mambo gani?” Wakamwambia: “Yale mambo kuhusu Yesu Mnazareti, aliyekuwa nabii mwenye nguvu katika kazi na neno mbele ya Mungu na watu wote; 20 na jinsi makuhani wakuu wetu na watawala walivyomkabidhi kwenye hukumu ya kifo na kumtundika mtini. 21 Lakini sisi tulikuwa tukitumaini kwamba mtu huyu alikuwa ndiye aliyekusudiwa kukomboa Israeli; ndiyo, na mbali na mambo yote haya, hii ndiyo siku ya tatu tangu mambo haya yalipotukia. 22 Zaidi ya hayo, wanawake fulani kutoka miongoni mwetu walitushangaza pia, kwa sababu walikuwa wamefika mapema kwenye kaburi la ukumbusho 23 lakini hawakupata mwili wake nao wakaja wakisema walikuwa pia wameona ono la malaika lizidilo nguvu za asili, waliosema yeye yuko hai. 24 Na zaidi, baadhi ya hao walio pamoja nasi walienda zao kwenye kaburi la ukumbusho; nao wakalikuta hivyo, sawa na vile wale wanawake walivyokuwa wamesema, lakini hawakumwona.”
25 Kwa hiyo yeye akawaambia: “Enyi wasio na akili na wazito katika moyo kuamini juu ya mambo yote waliyosema manabii! 26 Je, haikuwa lazima Kristo kupatwa na mambo haya na kuingia ndani ya utukufu wake?” 27 Na akianza kutoka Musa na Manabii wote akawafasiria mambo yanayohusiana na yeye mwenyewe katika Maandiko yote.
28 Mwishowe wakaja karibu na kijiji walikokuwa wakienda, naye akafanya ni kama kwamba alikuwa akifunga safari kwenda mbele mbali zaidi. 29 Lakini wakamkaza, wakisema: “Kaa pamoja nasi, kwa sababu ni kuelekea jioni na mchana tayari umekwisha.” Ndipo akaingia akae pamoja nao. 30 Naye alipokuwa akiegama pamoja nao kwenye mlo aliuchukua mkate, akaubariki, akaumega na kuanza kuwapa huo. 31 Ndipo macho yao yakafunguliwa kikamili nao wakamtambua; naye akatoweka kutoka kwao. 32 Nao wakaambiana: “Je, mioyo yetu haikuwa ikiwaka alipokuwa akisema nasi barabarani, alipokuwa akitufungulia kabisa yale Maandiko?” 33 Na saa hiyohiyo wakainuka wakarudi Yerusalemu, nao wakawakuta wale kumi na mmoja na wale walio pamoja nao wamekusanyika pamoja, 34 wakisema: “Kwa kweli Bwana alifufuliwa naye alimtokea Simoni!” 35 Sasa wao wenyewe wakasimulia yale matukio barabarani na jinsi yeye alivyopata kujulikana kwao kwa kule kuumega mkate.
36 Walipokuwa wakisema juu ya mambo hayo yeye mwenyewe akasimama katikati yao [[na kuwaambia: “Na mwe na amani.”]] 37 Lakini kwa sababu wao walikuwa wameogofishwa, na walikuwa wameogopa sana, walikuwa wakiwazia waliona roho. 38 Kwa hiyo yeye akawaambia: “Kwa nini mwafadhaika, na kwa nini shaka zatokea mioyoni mwenu? 39 Oneni mikono na miguu yangu, kwamba ni mimi mwenyewe; niguseguseni mwone, kwa sababu roho haina nyama na mifupa sawa na vile mwonavyo kwamba mimi ninavyo.” 40 [[Naye alipokuwa akisema hilo akawaonyesha mikono yake na miguu yake.]] 41 Lakini walipokuwa bado hawaamini kwa ajili ya shangwe tupu na wakistaajabu, yeye akawaambia: “Je, mna kitu fulani hapo cha kula?” 42 Nao wakampa kipande cha samaki wa kuchomwa; 43 naye akakichukua akakila mbele ya macho yao.
44 Yeye sasa akawaambia: “Haya ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa ningali pamoja nanyi, kwamba mambo yote yaliyoandikwa katika sheria ya Musa na katika Manabii na Zaburi juu yangu lazima yatimizwe.” 45 Ndipo akafungua kabisa akili zao ili kuifahamu maana ya Maandiko, 46 naye akawaambia: “Katika njia hii imeandikwa kwamba Kristo angeteseka na kufufuliwa kutoka miongoni mwa wafu siku ya tatu, 47 na juu ya msingi wa jina lake toba kwa msamaha wa dhambi ingehubiriwa katika mataifa yote—kuanzia Yerusalemu, 48 nyinyi mwapaswa kuwa mashahidi wa mambo haya. 49 Na, tazameni! ninatuma juu yenu kile ambacho kimeahidiwa na Baba yangu. Ingawa hivyo, nyinyi kaeni katika jiji mpaka mpate kuwa mmevishwa nguvu kutoka juu.”
50 Lakini yeye akawaongoza waende hadi Bethania, naye akainua mikono yake na kuwabariki. 51 Alipokuwa akiwabariki aliachanishwa nao akaanza kuchukuliwa juu mbinguni. 52 Nao wakamsujudia na kurudi Yerusalemu kwa shangwe kubwa. 53 Nao kwa kuendelea walikuwa katika hekalu wakimbariki Mungu.