Luka
23 Kwa hiyo umati wa hao ukainuka, wote, na kumwongoza kwa Pilato. 2 Ndipo wakaanza kumshtaki, wakisema: “Mtu huyu tulimkuta akipindua taifa letu na kukataza ulipaji wa kodi kwa Kaisari na kusema yeye mwenyewe ni Kristo mfalme.” 3 Sasa Pilato akamuuliza hili swali: “Je, wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Katika kumjibu akasema: “Wewe mwenyewe unasema hilo.” 4 Ndipo Pilato akawaambia makuhani wakuu na ule umati: “Mimi sipati uhalifu katika mtu huyu.” 5 Lakini wao wakaanza kuwa wasisitivu, wakisema: “Yeye huwachochea watu kwa kufundisha katika Yudea yote, hata kuanzia Galilaya hadi hapa.” 6 Aliposikia hilo, Pilato akauliza kama huyo mtu alikuwa Mgalilaya, 7 na, baada ya kuhakikisha kwamba alikuwa wa kutoka eneo la mamlaka ya Herode, akamtuma kwa Herode, ambaye yeye mwenyewe pia alikuwa katika Yerusalemu siku hizi.
8 Herode alipomwona Yesu alishangilia sana, kwa maana kwa muda mrefu alikuwa akitaka kumwona kwa sababu alikuwa amesikia juu yake, na alikuwa akitumaini kuona ishara fulani yenye kufanywa naye. 9 Sasa akaanza kumuuliza maswali kwa maneno mengi sana; lakini yeye hakumtolea jibu. 10 Hata hivyo, makuhani wakuu na waandishi wakafuliza kusimama na kumshtaki kwa ukali. 11 Ndipo Herode pamoja na askari-jeshi wake walinzi wakamfedhehesha, naye akamfanyia ucheshi kwa kumvisha vazi jangavu na kumrudisha kwa Pilato. 12 Wote wawili Herode na Pilato sasa wakawa marafiki siku hiyohiyo; kwa maana kabla ya hapo walikuwa wameendelea kuwa wenye uadui kati yao wenyewe.
13 Ndipo Pilato akawaita pamoja makuhani wakuu na watawala na watu 14 na kuwaambia: “Mliniletea mtu huyu kama mwenye kuwachochea watu waasi, na, tazameni! mimi nilimchunguza mbele yenu lakini sikupata katika mtu huyu msingi wa mashtaka mnayoleta dhidi yake. 15 Kwa kweli, wala Herode hakupata, kwa maana alimrudisha kwetu; na, tazama! hakuna kitu chochote kinachostahili kifo kimefanywa naye. 16 Kwa hiyo hakika nitamwadhibu na kumfungua.” 17 —— 18 Lakini wakiwa pamoja na umati, wao wote wakapaaza kilio, wakisema: “Mwondolee mbali huyu, lakini tufungulie Baraba!” 19 (Huyo ni mtu aliyekuwa ametupwa ndani ya gereza kwa sababu ya uchochezi wa uasi fulani wenye kutukia katika jiji na kwa kuua kimakusudi.) 20 Tena Pilato akawapaazia sauti, kwa sababu alitaka kumfungua Yesu. 21 Ndipo wakaanza kupiga kelele, wakisema: “Tundika mtini! Mtundike mtini!” 22 Mara ya tatu akawaambia: “Kwa nini, ni jambo gani baya alilofanya mtu huyu? Mimi sikupata jambo lolote linalostahili kifo katika yeye; kwa hiyo hakika mimi nitamwadhibu na kumfungua.” 23 Ndipo wakaanza kufanya hima-hima, kwa sauti zilizo kubwa, wakidai kwamba atundikwe mtini; na sauti zao zikaanza kushinda. 24 Kwa hiyo Pilato akatoa hukumu ili dai lao litimizwe: 25 akamfungua huyo mtu aliyekuwa ametupwa ndani ya gereza kwa uchochezi wa uasi na kuua kimakusudi na ambaye wao walikuwa wakidai, lakini akamsalimisha Yesu wamfanye kama wapendavyo.
26 Sasa walipokuwa wakimwongoza kumpeleka, walimshika Simoni, mzaliwa fulani wa Kirene, akija kutoka mashambani, nao wakamwekea mti wa mateso auchukue nyuma ya Yesu. 27 Lakini kulikuwa na umati mkubwa wa watu na wa wanawake ambao walimfuata waliofuliza kujipiga wenyewe kwa kihoro na kutoa sauti za kumwombolezea. 28 Yesu akageukia hao wanawake na kusema: “Binti za Yerusalemu, komeni kutoa machozi kwa ajili yangu. Kwa kinyume, toeni machozi kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu; 29 kwa sababu, tazameni! siku zinakuja ambazo katika hizo watu watasema, ‘Wenye furaha ni wanawake walio tasa, na matumbo ya uzazi ambayo hayakuzaa na matiti ambayo hayakunyonyesha!’ 30 Ndipo watakapoanza kuiambia milima, ‘Tuangukieni!’ na vilima, ‘Tufunikeni kabisa!’ 31 Kwa sababu ikiwa wao wafanya mambo haya wakati mti ni wenye unyevunyevu, kutatukia nini uwapo umenyauka?”
32 Lakini watu wengine wawili, watenda-maovu, walikuwa pia wakiongozwa wakafishwe pamoja naye. 33 Nao walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, huko wakatundika mtini yeye na wale watenda-maovu, mmoja upande wake wa kuume na mmoja upande wake wa kushoto. 34 [[Lakini Yesu alikuwa akisema: “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui wanalofanya.”]] Zaidi ya hilo, ili kugawa mavazi yake, wakapiga kura. 35 Na wale watu wakasimama wakitazama. Lakini wale watawala walikuwa wakicheka kwa dharau, wakisema: “Wengine aliokoa; mwacheni ajiokoe yeye mwenyewe, ikiwa huyu ndiye Kristo wa Mungu, Yule Mchaguliwa.” 36 Hata wale askari wakamfanyia ucheshi, wakija karibu na kumtolea divai iliyochacha 37 na kusema: “Ikiwa wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, jiokoe wewe mwenyewe.” 38 Kulikuwa pia na mwandiko juu yake: “Huyu ndiye mfalme wa Wayahudi.”
39 Lakini mmoja wa wale watenda-maovu walioangikwa akaanza kumwambia kwa maneno yenye kuudhi: “Wewe ndiwe Kristo, sivyo? Jiokoe mwenyewe na sisi.” 40 Kwa kujibu yule mwingine akamkemea na kusema: “Je, wewe humhofu Mungu hata kidogo, kwamba sasa wewe umo katika hukumu ileile? 41 Nasi, kwa kweli, tuko hivyo kwa haki, kwa maana sisi tunapokea kwa ukamili kile tustahilicho kwa mambo tuliyofanya; lakini mtu huyu hakufanya jambo lolote lisilopaswa.” 42 Naye akaendelea kusema: “Yesu, nikumbuke mimi uingiapo katika ufalme wako.” 43 Naye akamwambia: “Kwa kweli mimi nakuambia wewe leo, Utakuwa pamoja na mimi katika Paradiso.”
44 Basi, kufikia sasa ilikuwa karibu saa ya sita, na hata hivyo giza liliangukia dunia yote hadi saa ya tisa, 45 kwa sababu nuru ya jua ilikosekana; ndipo pazia la patakatifu likapasuliwa katikati. 46 Na Yesu akaita kwa sauti kubwa na kusema: “Baba, ndani ya mikono yako naikabidhi roho yangu.” Alipokuwa amesema hilo, akaisha. 47 Kwa sababu ya kuona lililotukia yule ofisa-jeshi akaanza kumtukuza Mungu, akisema: “Kwa kweli mtu huyu alikuwa mwadilifu.” 48 Na umati wote uliokuwa umekusanyika pamoja hapo kwa ajili ya kituko hiki, ulipoyaona mambo yaliyotukia, ukaanza kurudi, ukipiga vifua vyao. 49 Zaidi ya hayo, wote wale waliojuana naye walikuwa wamesimama umbali fulani. Pia, wanawake, waliokuwa wamemfuata pamoja kutoka Galilaya, walikuwa wamesimama wakiona mambo haya.
50 Na, tazama! mwanamume aliyeitwa jina Yosefu, aliyekuwa mshiriki wa Baraza, mtu mwema na mwadilifu— 51 mtu huyu hakuwa amepiga kura katika kuunga mkono mbinu yao na tendo—alikuwa wa kutoka Arimathea, jiji moja la Wayudea, naye alikuwa akingoja ufalme wa Mungu; 52 mtu huyu alimwendea Pilato akaomba mwili wa Yesu. 53 Naye akaushusha chini na kuufunga katika kitani bora, naye akamlaza katika kaburi lililochongwa katika mwamba, ambalo katika hilo hakuna mtu aliyepata kulala. 54 Sasa ilikuwa ni siku ya Matayarisho, na nuru ya jioni ya siku ya sabato ilikuwa ikikaribia. 55 Lakini wale wanawake, waliokuwa wamekuja pamoja naye kutoka Galilaya, wakafuata nyuma wakalitazama kaburi la ukumbusho na jinsi mwili wake ulivyolazwa; 56 nao wakarudi kutayarisha manukato na mafuta yaliyotiwa marashi. Lakini, bila shaka, walipumzika siku ya sabato kulingana na amri.