Luka
22 Sasa msherehekeo wa keki zisizotiwa chachu, ule uitwao kwa kawaida sikukuu ya Kupitwa, ulikuwa ukikaribia. 2 Pia, makuhani wakuu na waandishi walikuwa wakitafuta sana njia yenye matokeo ya wao kumwondoa, kwa maana walikuwa wakihofu watu. 3 Lakini Shetani akaingia katika Yudasi, aitwaye Iskariote, aliyehesabiwa miongoni mwa wale kumi na wawili; 4 naye akaenda zake akaongea pamoja na makuhani wakuu na makapteni wa hekalu juu ya njia yenye matokeo ya kumsaliti kwao. 5 Basi, wao wakashangilia na kupatana kumpa sarafu za fedha. 6 Kwa hiyo akakubali, naye akaanza kutafuta sana fursa nzuri ya kumsaliti kwao bila umati kuwa karibu.
7 Siku ya keki zisizotiwa chachu sasa ikawasili, ambayo katika hiyo kafara ya sikukuu ya kupitwa lazima adhabihiwe; 8 naye akatuma Petro na Yohana, akisema: “Nendeni mkatutayarishie sikukuu ya kupitwa ili tule.” 9 Wakamwambia: “Ni wapi utakapo tuitayarishe?” 10 Akawaambia: “Tazameni! Mwingiapo katika jiji mwanamume mwenye kuchukua chombo cha udongo cha maji atakutana nanyi. Mfuateni mwingie katika nyumba ambayo katika hiyo yeye aingia. 11 Nanyi lazima mmwambie bwana-kabaila wa hiyo nyumba, ‘Mwalimu akuambia wewe: “Kiko wapi chumba cha wageni ambacho katika hicho mimi naweza kula sikukuu ya kupitwa pamoja na wanafunzi wangu?”’ 12 Na mtu huyo atawaonyesha nyinyi chumba kikubwa cha juu chenye vifaa. Kitayarisheni huko.” 13 Kwa hiyo wakaondoka na kukipata kikiwa sawa na vile alivyokuwa amewaambia, nao wakatayarisha sikukuu ya kupitwa.
14 Hatimaye saa ilipofika, aliegama mezani, na wale mitume pamoja naye. 15 Naye akawaambia: “Nimetamani sana kula hii sikukuu ya kupitwa pamoja nanyi kabla sijateseka; 16 kwa maana nawaambia nyinyi, Hakika mimi sitaila tena mpaka iwapo imetimizwa katika ufalme wa Mungu.” 17 Na, akipokea kikombe, akashukuru na kusema: “Chukueni hiki mkipitishe kwa mmoja hadi kwa mwingine miongoni mwenu wenyewe; 18 kwa maana nawaambia nyinyi, Kutoka sasa na kuendelea hakika mimi sitakunywa tena kutokana na zao la mzabibu mpaka ufalme wa Mungu uwasilipo.”
19 Pia, akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema: “Huu wamaanisha mwili wangu ambao wapasa kutolewa kwa ajili yenu. Fulizeni kufanya hili katika ukumbuko wangu.” 20 Pia, kikombe kwa njia ileile baada ya wao kula mlo wa jioni, yeye akisema: “Kikombe hiki chamaanisha agano jipya kwa msingi wa damu yangu, ambayo yapasa kumwagwa kwa ajili yenu.
21 “Lakini, tazameni! mkono wa msaliti wangu upo pamoja nami kwenye meza. 22 Kwa sababu Mwana wa binadamu anashika njia yake kwenda kulingana na lililotiwa alama; hata hivyo, ole wa mtu ambaye kupitia huyo yeye asalitiwa!” 23 Kwa hiyo wakaanza kuzungumza miongoni mwao wenyewe swali la ni yupi kati yao angekuwa kwa kweli ndiye ambaye alikuwa karibu kufanya hilo.
24 Hata hivyo, kukatokea pia bishano kali miongoni mwao juu ya ni yupi kati yao aliyeonekana kuwa mkubwa zaidi ya wote. 25 Lakini yeye akawaambia: “Wafalme wa mataifa hupiga ubwana juu yao, na wale walio na mamlaka juu yao huitwa Wafadhili. 26 Ingawa hivyo, nyinyi hampaswi kuwa hivyo. Lakini acheni yeye aliye mkubwa zaidi ya wote miongoni mwenu awe kama aliye mchanga zaidi ya wote, na yule anayetenda kama mkuu kama yule anayehudumu. 27 Kwa maana ni yupi aliye mkubwa zaidi, yule anayeegama kwenye meza au yule anayehudumu? Je, si yule anayeegama kwenye meza? Lakini mimi nimo katikati yenu kama yule anayehudumu.
28 “Hata hivyo, nyinyi ndio mmeshikamana nami katika majaribu yangu; 29 nami nafanya agano pamoja nanyi, sawa na vile Baba yangu amefanya agano pamoja nami, kwa ajili ya ufalme, 30 ili mpate kula na kunywa kwenye meza yangu katika ufalme wangu, na kuketi juu ya viti vya ufalme kuyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
31 “Simoni, Simoni, tazama! Shetani amedai kuwapata nyinyi watu ili awapepete kama ngano. 32 Lakini mimi nimeomba dua kwa ajili yako ili imani yako isipate kufifia; na wewe, mara uwapo umerudi, watie nguvu ndugu zako.” 33 Ndipo akamwambia: “Bwana, mimi niko tayari kwenda pamoja nawe kuingia gerezani na pia kuingia katika kifo.” 34 Lakini yeye akasema: “Nakuambia wewe, Petro, Jogoo hatawika leo mpaka uwe umekana mara tatu kuwa hunijui mimi.”
35 Akawaambia wao pia: “Wakati nilipowatuma nyinyi bila kibeti na mfuko wa chakula na makubazi, hamkukosa kitu chochote, ndivyo?” Wakasema: “La!” 36 Ndipo yeye akawaambia: “Lakini sasa acheni yule ambaye ana kibeti akichukue, vivyo hivyo pia mfuko wa chakula; na acheni yule asiye na upanga auze vazi lake la nje na kununua mmoja. 37 Kwa maana nawaambia nyinyi kwamba lazima hili ambalo limeandikwa litimizwe katika mimi, yaani, ‘Naye alihesabiwa pamoja na waasi-sheria.’ Kwa maana kile kinihusucho mimi kinakuwa na utimizo.” 38 Ndipo wakasema: “Bwana, tazama! hapa pana panga mbili.” Yeye akawaambia: “Yatosha.”
39 Alipotoka nje kama ilivyo desturi alienda kwenye Mlima wa Mizeituni; na wanafunzi pia wakamfuata. 40 Wakiisha fika hapo mahali aliwaambia: “Endelezeni sala, ili msiingie katika kishawishi.” 41 Naye mwenyewe akajiondoa kutoka kwao karibu umbali wa mtupo wa jiwe, na kukunja magoti yake akaanza kusali, 42 akisema: “Baba, ikiwa wataka, ondoa kikombe hiki kutoka kwangu. Hata hivyo, acha, si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.” 43 Ndipo malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. 44 Lakini akiingia katika maumivu makali akaendelea kusali kwa bidii zaidi; na jasho lake likawa kama matone ya damu yakianguka kwenye ardhi. 45 Naye akainuka kutoka kwenye sala, akawaendea wanafunzi akawakuta wakisinzia kutokana na kihoro; 46 naye akawaambia: “Kwa nini mnalala usingizi? Inukeni mwendeleze sala, ili msiingie katika kishawishi.”
47 Alipokuwa bado akisema, tazama! umati, na yule mtu aitwaye Yudasi, mmoja wa wale kumi na wawili, alikuwa akienda mbele yao; naye akamkaribia Yesu ambusu. 48 Lakini Yesu akamwambia: “Yudasi, je, wewe wamsaliti Mwana wa binadamu kwa busu?” 49 Wale waliokuwa kandokando yake walipoona lililokuwa linaelekea kutukia, wakasema: “Bwana, je, tupige kwa upanga?” 50 Mtu fulani kati yao hata alimpiga mtumwa wa kuhani wa cheo cha juu akakata sikio lake la kuume. 51 Lakini kwa kujibu Yesu akasema: “Achieni hapa.” Naye akagusa sikio na kumponya. 52 Ndipo Yesu akawaambia makuhani wakuu na makapteni wa hekalu na wanaume wazee waliokuwa wamekuja hapo kumchukua: “Je, mlitoka mkiwa na panga na marungu kama kwamba dhidi ya mpokonyaji? 53 Nilipokuwa pamoja nanyi katika hekalu siku baada ya siku hamkunyoosha mikono yenu dhidi yangu kunishika. Lakini hii ndiyo saa yenu na ndiyo mamlaka ya giza.”
54 Ndipo wakamkamata wakamwongoza kwenda zao na kumwingiza katika nyumba ya kuhani wa cheo cha juu; lakini Petro alikuwa akifuata kwa umbali fulani. 55 Walipowasha moto katikati ya ua na kuketi chini pamoja, Petro alikuwa ameketi miongoni mwao. 56 Lakini msichana-mtumishi fulani akamwona ameketi kando ya ule moto mwangavu akamtazama kwa kumchunguza na kusema: “Mtu huyu pia alikuwa pamoja naye.” 57 Lakini yeye akakana hilo, akisema: “Mimi simjui, wee, mwanamke.” 58 Na baada ya muda mfupi mtu mwingine akimwona akasema: “Wewe pia ni mmoja wao.” Lakini Petro akasema: “Wee, mtu, mimi siye.” 59 Na baada ya karibu muda wa saa moja kupita mtu fulani mwingine akaanza kusisitiza kwa nguvu: “Kwa hakika mtu huyu pia alikuwa pamoja naye; kwa maana, kwa kweli, yeye ni Mgalilaya!” 60 Lakini Petro akasema: “Wee, mtu, mimi sijui unalosema.” Na mara hiyo, alipokuwa bado akisema, jogoo akawika. 61 Na Bwana akageuka akamtazama Petro, na Petro akakumbuka tamko la Bwana alipomwambia: “Kabla jogoo hajawika leo utanikana mara tatu.” 62 Naye akaenda nje akatoa machozi kwa uchungu.
63 Sasa wale wanaume waliokuwa wakimlinda kifungoni wakaanza kumfanyia ucheshi, wakimpiga; 64 na baada ya kumfunika kabisa wakawa wakiuliza na kusema: “Toa unabii. Ni nani huyo aliyekupiga?” 65 Nao wakaendelea kusema mambo mengine mengi katika kukufuru dhidi yake.
66 Hatimaye wakati ulipopata kuwa mchana, kusanyiko la wanaume wazee wa watu, makuhani wakuu na waandishi pia, wakakusanyika pamoja, nao wakamburuta ndani ya jumba lao la Sanhedrini, wakisema: 67 “Ikiwa wewe ndiwe Kristo, tuambie.” Lakini yeye akawaambia: “Hata kama ningewaambia, nyinyi hamngeamini hilo hata kidogo. 68 Zaidi ya hilo, kama ningewauliza nyinyi, hamngejibu hata kidogo. 69 Hata hivyo, kutoka sasa na kuendelea Mwana wa binadamu atakuwa akiketi kwenye mkono wa kuume wenye nguvu wa Mungu.” 70 Ndipo wote wakasema: “Kwa hiyo, je, wewe ndiwe Mwana wa Mungu?” Akawaambia: “Nyinyi wenyewe mnasema kwamba mimi ndiye.” 71 Wakasema: “Kwa nini twahitaji ushahidi zaidi? Kwa maana sisi wenyewe tumelisikia kutoka katika kinywa chake mwenyewe.”