Luka
21 Sasa alipotazama juu aliwaona matajiri wakitumbukiza zawadi zao ndani ya masanduku ya hazina. 2 Ndipo akaona mjane fulani mwenye uhitaji akitumbukiza sarafu ndogo mbili za thamani ndogo sana humo, 3 naye akasema: “Nawaambia nyinyi kwa kweli, Mjane huyu, ijapokuwa ni maskini, alitumbukiza nyingi kuliko wao wote. 4 Kwa maana wote hawa walizitumbukiza ndani zawadi kutokana na ziada yao, lakini mwanamke huyu kutokana na uhitaji wake alitumbukiza ndani njia yote ya kujipatia riziki aliyokuwa nayo.”
5 Baadaye, watu fulani walipokuwa wakisema kuhusu hekalu, jinsi lilivyorembwa kwa mawe bora na vitu vilivyowekwa wakfu, 6 alisema: “Kwa habari ya vitu hivi ambavyo nyinyi mnaviona, siku zitakuja ambazo katika hizo hakuna jiwe juu ya jiwe ambalo litaachwa hapa lisiangushwe.” 7 Ndipo wakamuuliza swali, wakisema: “Mwalimu, ni wakati gani mambo haya yatakapokuwa kwa kweli, na itakuwa nini ishara wakati mambo hayo yakusudiwapo kutukia?” 8 Akasema: “Jihadharini msiongozwe vibaya; kwa maana wengi watakuja juu ya msingi wa jina langu, wakisema, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati upasao umekaribia.’ Msiwafuate. 9 Zaidi ya hilo, wakati msikiapo juu ya vita na mivurugo, msiogofishwe. Kwa maana mambo hayo ni lazima yatukie kwanza, lakini mwisho hautokei mara hiyo.”
10 Ndipo akaendelea kuwaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme; 11 na kutakuwa na matetemeko makubwa ya dunia, na katika mahali pamoja baada ya pengine magonjwa ya kuambukiza na upungufu wa chakula; na kutakuwa na mambo ya kuonwa yenye kutia hofu na kutoka mbinguni ishara zilizo kubwa.
12 “Lakini kabla ya mambo yote hayo watu watawawekea mikono ili wawashike na kuwanyanyasa nyinyi, wakiwakabidhi nyinyi kwenye masinagogi na magereza, nyinyi mkiwa mnaburutwa mbele ya wafalme na magavana kwa ajili ya jina langu. 13 Itageuka kwenu kuwa ushahidi. 14 Kwa hiyo azimieni mioyoni mwenu kutokariri kimbele jinsi ya kufanya ujiteteaji wenu, 15 kwa maana hakika mimi nitawapa nyinyi kinywa na hekima, ambacho wapingaji wenu wote wakiwa pamoja hawataweza kukinza au kubisha. 16 Zaidi ya hayo, mtatolewa hata na wazazi na akina ndugu na jamaa zenu na marafiki, nao watafanya baadhi yenu wauawe; 17 nanyi mtakuwa vitu vya kuchukiwa na watu wote kwa sababu ya jina langu. 18 Na bado hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautaangamia kwa vyovyote. 19 Kwa uvumilivu kwa upande wenu mtajipatia nafsi zenu.
20 “Zaidi ya hilo, wakati mwonapo Yerusalemu limezingirwa na majeshi yaliyopiga kambi, ndipo jueni kwamba kufanywa ukiwa kwalo kumekaribia. 21 Ndipo waacheni wale walio katika Yudea waanze kukimbia hadi kwenye milima, na waacheni wale walio katikati yalo waondoke, na waacheni wale walio katika sehemu za mashambani wasiingie ndani yalo; 22 kwa sababu hizi ni siku za kupatiliza haki, ili mambo yote yaliyoandikwa yapate kutimizwa. 23 Ole wa wanawake wenye mimba na wale wanaonyonyesha mtoto mchanga siku hizo! Kwa maana kutakuwa na uhitaji mkubwa juu ya nchi na hasira ya kisasi juu ya watu hawa; 24 nao wataanguka kwa makali ya upanga na kuchukuliwa mateka ndani ya mataifa yote; na Yerusalemu litakanyagwa-kanyagwa na mataifa, hadi nyakati zilizowekwa rasmi za mataifa ziwe zimetimizwa.
25 “Pia, kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota, na juu ya dunia maumivu makali ya mataifa, bila kujua njia ya kutokea kwa sababu ya kunguruma kwa bahari na msukosuko wayo, 26 huku watu wakizimia moyo kutokana na hofu na tarajio la mambo yanayokuja juu ya dunia inayokaliwa; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa. 27 Na ndipo watakapomwona Mwana wa binadamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mkubwa. 28 Lakini mambo haya yaanzapo kutukia, jisimamisheni wenyewe wima na kuinua vichwa vyenu juu, kwa sababu ukombozi wenu unakaribia.”
29 Ndipo akawaambia kielezi: “Angalieni mtini na miti mingine yote: 30 Wakati iwapo tayari imechipuka, kwa kuangalia hilo mwajua wenyewe kwamba sasa kiangazi kiko karibu. 31 Katika njia hii nyinyi pia, wakati mwonapo mambo hayo yakitukia, jueni kwamba ufalme wa Mungu uko karibu. 32 Kwa kweli nawaambia nyinyi, Kizazi hiki hakitapitilia mbali kwa vyovyote mpaka mambo yote yatukie. 33 Mbingu na dunia zitapitilia mbali, lakini maneno yangu hayatapitilia mbali kwa vyovyote.
34 “Lakini kazieni uangalifu kwa nyinyi wenyewe kwamba mioyo yenu isiwe kamwe yenye kulemewa na kula kupita kiasi na kunywa sana na mahangaiko ya maisha, na kwa ghafula siku hiyo iwe juu yenu mara hiyo 35 kama mtego. Kwa maana itakuja juu ya wote wale wanaokaa juu ya uso wa dunia yote. 36 Basi, fulizeni kuwa macho wakati wote mkiomba dua ili mpate kufanikiwa kuponyoka mambo yote hayo yaliyokusudiwa kutukia, na kusimama mbele ya Mwana wa binadamu.”
37 Kwa hiyo wakati wa mchana akawa akifundisha katika hekalu, lakini wakati wa usiku akawa akitoka kwenda na kukaa juu ya mlima uitwao Mlima wa Mizeituni. 38 Na watu wote wakawa wakimjia mapema katika siku katika hekalu ili wamsikie.