Luka
20 Mojawapo zile siku alipokuwa akifundisha watu katika hekalu na kutangaza habari njema, makuhani wakuu na waandishi pamoja na wanaume wazee walikuja karibu, 2 nao wakasema, wakimwambia: “Tuambie ni kwa mamlaka gani wewe wafanya mambo haya, au ni nani aliyekupa mamlaka hii.” 3 Kwa kujibu akawaambia: “Hakika mimi pia nitawauliza nyinyi swali, nanyi mniambie: 4 Je, ubatizo wa Yohana ulikuwa wa kutoka mbinguni au wa kutoka kwa wanadamu?” 5 Ndipo miongoni mwao wenyewe wakafikia kauli, wakisema: “Tukisema, ‘Kutoka mbinguni,’ atasema, ‘Kwa nini hamkumwamini?’ 6 Lakini tukisema, ‘Kutoka kwa wanadamu,’ watu wote watatupiga kwa mawe, kwa maana wao wameshawishwa kwamba Yohana alikuwa nabii.” 7 Kwa hiyo wakajibu kwamba hawakujua chanzo cha huo. 8 Naye Yesu akawaambia: “Wala mimi siwaambii nyinyi ni kwa mamlaka gani nafanya mambo haya.”
9 Ndipo akaanza kuwaambia watu kielezi hiki: “Mtu alipanda shamba la mizabibu akalikodisha kwa walimaji, naye akasafiri nchi ya nje muda mrefu. 10 Lakini katika majira yapasayo akatuma mtumwa kwa walimaji, ili wapate kumpa baadhi ya matunda ya shamba la mizabibu. Hata hivyo, hao walimaji wakamwacha aende bila kitu, baada ya kumpiga sana. 11 Lakini akarudia na kutuma kwao mtumwa tofauti. Huyo pia walimpiga sana na kumvunjia heshima na kumwacha aende bila kitu. 12 Na bado tena akatuma wa tatu; huyo pia walimjeruhi na kumtupa nje. 13 Ndipo mwenye kumiliki shamba la mizabibu akasema, ‘Nitafanya nini? Nitatuma mwana wangu mpendwa. Yaelekea watamstahi huyu.’ 14 Walimaji walipomwona mara hiyo walianza kujadiliana kwa kutoa sababu, wakisema, ‘Huyu ndiye mrithi; acheni tumuue, ili urithi upate kuwa wetu.’ 15 Ndipo wakamtupa nje ya shamba la mizabibu na kumuua. Kwa hiyo, mwenye kumiliki shamba la mizabibu atawafanya nini? 16 Atakuja awaangamize walimaji hawa na atawapa wengine shamba la mizabibu.”
Waliposikia hilo wakasema: “Hilo lisitukie kamwe!” 17 Lakini yeye akawatazama na kusema: “Basi, hili ambalo limeandikwa humaanisha nini, ‘Jiwe walilolikataa wajenzi, limekuwa ndilo jiwe la pembeni lililo kuu’? 18 Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjwavunjwa. Kwa habari ya yeyote ambaye laangukia, litamponda tikitiki.”
19 Waandishi na makuhani wakuu sasa wakatafuta sana kunyoosha mkono ili wamshike saa hiyohiyo, lakini waliwahofu watu; kwa maana walifahamu kwamba yeye alisema kielezi hicho akiwafikiria wao. 20 Na, baada ya kumtazama sana, wakatuma watu walioajiriwa kwa siri wasingizie kwamba walikuwa waadilifu, ili wapate kumnasa katika usemi, ili wamkabidhi kwa serikali na kwa mamlaka ya gavana. 21 Nao wakamuuliza swali, wakisema: “Mwalimu, sisi twajua wewe husema na kufundisha kwa usahihi na huonyeshi ubaguzi wowote, bali wewe hufundisha njia ya Mungu kwa kupatana na kweli: 22 Je, yaruhusika kisheria sisi kumlipa Kaisari kodi au la?” 23 Lakini yeye akagundua ujanja wao na kuwaambia: 24 “Nionyesheni dinari. Ina sanamu na mwandiko wa nani?” Wakasema: “Wa Kaisari.” 25 Akawaambia: “Kwa vyovyote, basi, mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari, lakini mlipeni Mungu vitu vya Mungu.” 26 Basi, hawakuweza kumnasa katika usemi huu mbele ya watu, bali, wakiwa na mshangao kwa jibu lake, hawakusema kitu.
27 Hata hivyo, baadhi ya Masadukayo, wale wasemao hakuna ufufuo, wakaja na kumuuliza swali, 28 wakisema: “Mwalimu, Musa alituandikia, ‘Ikiwa ndugu ya mtu afa akiwa na mke, lakini huyu alikaa bila mtoto, ndugu yake apaswa kumchukua huyo mke na kuinua uzao kutokana naye kwa ajili ya ndugu yake.’ 29 Basi kulikuwa na ndugu saba; na wa kwanza akachukua mke na kufa bila mtoto. 30 Kwa hiyo wa pili, 31 na wa tatu wakamchukua mwanamke huyo. Hivyohivyo hata wa saba: hawakuacha watoto nyuma, bali walikufa mmoja baada ya mwingine. 32 Mwishowe, yule mwanamke akafa pia. 33 Kwa sababu hiyo, katika ufufuo, ni kwa yupi kati yao yeye awa mke? Kwa maana wale saba walimpata kama mke.”
34 Yesu akawaambia: “Watoto wa mfumo huu wa mambo huoa na huozwa, 35 lakini wale ambao wamehesabiwa kustahili kupata mfumo huo wa mambo na ufufuo kutoka kwa wafu hawaoi wala hawaozwi. 36 Kwa kweli, wala hawawezi kufa tena kamwe, kwa maana wao ni kama malaika, nao ni watoto wa Mungu kwa kuwa watoto wa ufufuo. 37 Lakini kwamba wafu wafufuliwa hata Musa alifunua, katika usimulizi juu ya kijiti cha miiba, amwitapo Yehova ‘Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo.’ 38 Yeye ni Mungu, si wa wafu, bali wa walio hai, kwa maana kwake, wao wote wako hai.” 39 Kwa kujibu baadhi ya waandishi wakasema: “Mwalimu, ulisema vema.” 40 Kwa maana hawakuwa tena na moyo wa kumuuliza hata swali moja.
41 Naye akawaambia: “Ni jinsi gani wao husema kwamba Kristo ni mwana wa Daudi? 42 Kwa maana Daudi mwenyewe asema katika kitabu cha Zaburi, ‘Yehova alimwambia Bwana wangu, Keti kwenye mkono wangu wa kuume 43 mpaka niweke maadui wako kuwa kibago kwa ajili ya miguu yako.’ 44 Basi, Daudi amwita ‘Bwana’; kwa hiyo yeye ni mwana wake jinsi gani?”
45 Ndipo, watu wote walipokuwa wakisikiliza akawaambia wanafunzi: 46 “Jihadharini na waandishi ambao hutamani kutembea wakizunguka wamevaa kanzu nao hupendezwa na salamu katika mahali pa masoko na viti vya mbele katika masinagogi na mahali pa kutokeza zaidi sana kwenye milo ya jioni, 47 na ambao humeza nyumba za wajane na kwa kisingizio hufanya sala zilizo ndefu. Hawa watapokea hukumu nzito zaidi.”