2 Wathesalonike
Ya Pili kwa Wathesalonike
1 Paulo na Silvano na Timotheo kwa kutaniko la Wathesalonike katika muungano na Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo:
2 Na mwe na fadhili isiyostahiliwa na amani kutoka kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo.
3 Tunawajibika kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, akina ndugu, kama inavyofaa, kwa sababu imani yenu inakua mno na upendo wa kila mmoja na wa nyinyi nyote unaongezeka mmoja kuelekea mwingine. 4 Tokeo ni kwamba sisi wenyewe twawaonea nyinyi fahari miongoni mwa makutaniko ya Mungu kwa sababu ya uvumilivu wenu na imani katika minyanyaso yenu yote na dhiki mnazohimili. 5 Hii ni ithibati ya hukumu ya uadilifu ya Mungu, inayoongoza kwenye kuhesabiwa kwenu kustahili ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili ya huo kwa kweli mnateseka.
6 Hili ni kwa kuzingatia kwamba ni jambo la uadilifu kwa upande wa Mungu kulipa dhiki kwa wale wawafanyiao nyinyi dhiki, 7 lakini, kwenu nyinyi mpatwao na dhiki, kitulizo pamoja nasi kwenye ufunuo wa Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika zake wenye nguvu 8 katika moto wenye kuwaka mwali, aletapo kisasi juu ya wale wasiomjua Mungu na wale wasiotii habari njema juu ya Bwana wetu Yesu. 9 Hawahawa watapatwa na adhabu ya kihukumu ya uharibifu udumuo milele kutoka mbele ya Bwana na kutoka katika utukufu wa nguvu yake, 10 wakati ajapo kutukuzwa kuhusiana na watakatifu wake na kuonwa kwa kustaajabiwa katika siku hiyo kuhusiana na wote wale waliodhihirisha imani, kwa sababu ushahidi tuliotoa ulikubaliwa kwa imani miongoni mwenu.
11 Kwa madhumuni yaleyale kwa kweli sisi twasali sikuzote kwa ajili yenu, kwamba Mungu wetu apate kuwahesabia nyinyi kuwa wenye kustahili wito wake na kufanya kabisa yote apendayo ya wema na kazi ya imani kwa nguvu; 12 ili jina la Bwana wetu Yesu lipate kutukuzwa katika nyinyi, nanyi katika muungano na yeye, kwa kupatana na fadhili isiyostahiliwa ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.