2 Yohana
Ya Pili ya Yohana
1 Mwanamume mzee kwa bibi-mchaguliwa na kwa watoto wake, ambao mimi nawapenda kweli, na si mimi peke yangu, bali pia wote wale ambao wamekuja kuijua kweli, 2 kwa sababu ya kweli ambayo hukaa katika sisi, nayo itakuwa pamoja na sisi milele. 3 Pamoja na sisi kutakuwa fadhili isiyostahiliwa, rehema na amani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Yesu Kristo Mwana wa Baba, pamoja na kweli na upendo.
4 Mimi nashangilia sana kwa sababu nimekuta baadhi ya watoto wako wanatembea katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kutoka kwa Baba. 5 Kwa hiyo sasa nakuomba wewe, bibi, nikiwa mtu anayekuandikia, si amri mpya, bali ambayo tulikuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane. 6 Na hili ndilo upendo humaanisha, kwamba tuendelee kutembea kulingana na amri zake. Hii ndiyo amri, kama vile nyinyi watu mmesikia tangu mwanzo, kwamba mwapaswa kuendelea kutembea katika hiyo. 7 Kwa maana wadanganyi wengi wameenda kuingia katika ulimwengu, watu ambao hawaungami Yesu Kristo kuwa alikuja katika mwili. Huyu ndiye mdanganyi na mpinga-Kristo.
8 Jiangalieni nyinyi wenyewe, kwamba msipoteze mambo ambayo sisi tumefanya kazi kutokeza, bali kwamba mpate kuwa na thawabu yenye kujaa. 9 Kila mtu ambaye hujisukuma mbele na hakai katika fundisho la Kristo hana Mungu. Yeye ambaye akaa katika ufundishaji huu ndiye ambaye ana Baba na Mwana pia. 10 Ikiwa yeyote aja kwenu na haleti ufundishaji huu, msimpokee kamwe nyumbani mwenu wala kusema salamu kwake. 11 Kwa maana yeye asemaye salamu kwake ni mshiriki katika kazi zake mbovu.
12 Ijapokuwa nina mambo mengi ya kuwaandikia nyinyi, sitaki kufanya hivyo kwa karatasi na wino, lakini ninatumaini kuja kwenu na kusema pamoja nanyi uso kwa uso, ili shangwe yenu ipate kuwa katika kipimo kilichojaa.
13 Watoto wa dada yako, yule mchaguliwa, wakupelekea wewe salamu zao.