18 Bildadi+ Mshua akajibu:
2 “Utaendelea kusema maneno haya mpaka lini?
Onyesha uelewaji kidogo ili nasi tuseme.
3 Kwa nini tuonwe kama wanyama+
Na kuonekana wapumbavu machoni pako?
4 Hata ukijirarua vipandevipande kwa hasira,
Je, dunia itaachwa kwa ajili yako,
Au mwamba kuhama mahali pake?
5 Naam, nuru ya mwovu itazimwa,
Na mwali wa moto wake hautang’aa.+
6 Hakika nuru iliyo ndani ya hema lake itakuwa giza,
Na taa iliyo juu yake itazimwa.
7 Hatua zenye nguvu zimefupishwa,
Na shauri lake mwenyewe litamwangusha.+
8 Kwa maana miguu yake itamwongoza kwenye wavu,
Naye atatangatanga kwenye kamba za wavu.
9 Mtego utamnasa kisigino;
Na kitanzi kitamkamata.+
10 Kamba imefichwa ardhini kwa ajili yake,
Na mtego uko kwenye kijia chake.
11 Vitisho vinamwogopesha pande zote+
Na kumfuatia miguuni pake.
12 Nguvu zake zimepungua,
Na msiba+ utamfanya ayumbeyumbe.
13 Ngozi yake imeliwa;
Ugonjwa hatari sana unakula viungo vyake.
14 Ameng’olewa kutoka katika hema lake lililo salama+
Na kupelekwa kwa mfalme wa vitisho.
15 Wageni watakaa katika hema lake;
Kiberiti kitatawanywa juu ya makao yake.+
16 Chini yake, mizizi yake itakauka,
Na juu yake, matawi yake yatanyauka.
17 Hakuna atakayemkumbuka duniani,
Na jina lake halitajulikana mtaani.
18 Ataondolewa kwenye nuru na kupelekwa gizani
Na kufukuzwa kutoka duniani.
19 Hatakuwa na mtoto wala mzao miongoni mwa watu wake,
Wala hakuna atakayebaki katika makao yake.
20 Siku yake itakapofika, watu wa Magharibi watashtuka sana
Na watu wa Mashariki watashikwa na hofu.
21 Hivyo ndivyo inavyokuwa kwa mahema ya mkosaji
Na kwa makao ya mtu ambaye hajamjua Mungu.”