Kukabiliana na Kazi ya Zamu ya Usiku
WAFANYA kazi wa zamu ya usiku wamepatikana kuwa na matatizo ya nyonga, vidonda vya tezi, uzoefu wa kileo, na talaka kuliko wenzao wanaofanya kazi mchana. Lakini utafiti uliofanywa na Fred Jung, mwuguzi aliyesajiliwa na naibu wa mfunzi kwenye Chuo Kikuu cha Texas kule Austin School of Nursing, unadokeza kwamba badiliko la vigezo vya kulala huenda vikaondoa baadhi ya matatizo hayo.
Bw. Jung alifanya uchunguzi juu ya usingizi kwa kikundi cha waajiriwa kazi ya zamu ya usiku kwenye kiwanda cha uundaji. Katika kikundi alichochunguza, kilichotia ndani wanaume na wanawake wenye mchanganyiko wa stadi za kuunda, yeye alikata maneno kwamba kazi ya zamu yenyewe inasababisha namna fulani ya mkazo.
Watu katika uchunguzi huo walipatwa na dalili zinazofanana na zile za uchovu wa kuruka na eropleni ambazo zilionekana zinazidi wakati mazoea ya usingizi yalipobadilishwa kuwa usingizi wa usiku wakati wa siku za kutokuwa kazini. Kwa hiyo, Jung alikata maneno kwamba, vigezo vya usingizi vilivyofuatwa wakati wa juma la kazi yafaa viendelezwe juma lote, kwa kuwa inachukua siku kadhaa kwa taratibu za mwili za kibayolijia kujirekebisha kulingana na kigezo kipya cha usingizi.
Utafiti wa Bw. Jung unadokeza kwamba kulala angalau kipindi cha saa nne wakati ambao kwa desturi unatumiwa kwa ajili ya usingizi katika juma la kazi yaelekea kunasaidia kudumisha taratibu za kibayolojia. Anauita huo kuwa usingizi-nanga. Ulaji, vigezo vya kijamii, na kujiweka wazi kwenye nuru pia vilionekana vina matokeo juu ya rekebisho la wafanya kazi wa zamu.
Akitumia habari hiyo ya utafiti wake, Bw. Jung amebuni miongozo kadhaa kwa ajili ya wafanya kazi wa zamu ya usiku:
◻ Jaribu kulala wakati ule ule wa siku, hasa iwe baadaye asubuhi na mapema alasiri.
◻ Panga utendaji wako nje ya kipindi chako cha kulala.
◻ Usitie wasiwasi kama huwezi kulala sikuzote wakati ule unaopendelea; hata usingizi kidogo wa kawaida mchana utakuwa ni afadhali kuliko kukosa kabisa.
◻ Ondoa kelele zenye kusumbua (tumia viziba-masikio au ujipatie kidude cha kujibu simu) na ulale katika chumba chenye giza.
◻ Kula chakula kingi, chenye protini nyingi mwanzoni mwa siku yako. Protini huandaa mmiminiko wenye kudumishwa wa glukozi yenye kutoa nishati nayo itasisimua tezi-adrenali zikuweke katika hali ya kuwa chonjo. Halafu ule chakula cha kadiri chenye protini katikati ya siku na uepuke vitafuno vyenye karbohaidreti. Huenda vikakuchangamsha kwa muda lakini vitakufanya uchoke saa moja au mbili baadaye. Acha karbohaidreti uzitumie kwenye chakula chako cha mwisho kwa siku hiyo. Vitu hivyo vinakutayarisha kwa ajili ya usingizi wenye kupumzisha. Hata hivyo, usile mara tu kabla ya kwenda kulala; unahitaji saa kadhaa kusaga mwilini chakula chako.
◻ Usinywe kileo kuwa njia ya kupatia usingizi. Kileo kinakunyang’anya aina ya usingizi unaohitaji kwa ajili ya afya ya kisaikolojia na hali njema.
◻ Uamkapo, washa taa; au ikiwa kuna nuru nje, nenda nje kwenye nuru ya mchana, fanya mazoezi, tembea-tembea, na ongea na watu. Utendaji huo na nuru vitasisimua ubongo wako na kukusaidia upatanishe mwili wako tena na ratiba yako ya kazi ya usiku.
◻ Jiangalie vizuri. Usizidishe mkazo huo kwa kuishi kwa njia yenye kuharibu afya. Kuingiza mazoezi ya kawaida, chakula kinachofaa, na usingizi wa kutosha wenye kupumzisha katika kawaida yako ya kila siku kutakusaidia utende, uhisi vizuri zaidi na hata kuwa na sura bora zaidi.
Hayo ni maoni ya mtafiti mmoja. Huenda wengine wakatokeza matatuzi tofauti kwa tatizo hilo.