“Naitaka Sasa!” Muhula wa Utoshelezo wa Papo Hapo
Mkao wa Johnny mchanga unapasa uonyeshe mteseko mkubwa, lakini ukimtazama unajikaza usicheke. Mabega yake yamelegea, magoti yake ni hafifu, hatua zake zikiwa legevu na nzito. Uso wake unaigiza huzuni—kipaji cha uso kilichokunjamana, macho yenye kusihi, na mdomo uliokunjwa kwa uguo. Yeye ana kitu kimoja akilini: matunda ya kuliwa baada ya chakula.
“Lakini Mama,” yeye anung’unika. Nung’uniko lake linafikia hapo tu. Mama yake amgeukia akiwa na bakuli na kijiko mkononi. “Kwa mara ya mwisho, Johnny, LA!” mama yake asema kwa uthabiti. “Ukila matunda sasa, utaharibu hamu yako ya kula chakula cha jioni. Isitoshe, zimebaki dakika 15 tu kisha tule!”
“Lakini nataka kidogo SASA!” yeye alia. Mama yake aacha kukoroga na kukaza macho kwa mtoto wake. Yeye ajua macho hayo; kwa akili aondoka, aende akaugue kwenye chumba kingine. Upesi kwa kukengeushwa akili, amekwishasahau habari ya kula wakati mlo mkuu unapokuwa tayari.
Nyakati nyingine watoto huonekana ni kama wamekuwa watumwa wa kutaka kitu papo hapo. Wanapotaka kitu, hukitaka sasa. Wazo la kungojea zawadi nzuri zaidi, au la kukataa raha fulani kwa sababu inaweza kuwadhuru baadaye, linakuwa gumu sana kwao kuelewa. Na bado, ndilo wazo ambalo wao—kutia na sisi—twahitaji kujifunza.
Uchunguzi mmoja wa hivi majuzi uliofanywa na wanasayansi kwenye Chuo Kikuu cha Columbia katika United States uliangalia juu ya uwezo wa watoto wachanga wa kuahirisha utoshelezo wa papo hapo kwa ajili ya zawadi wanayotamani. Watoto hao waliambiwa wachague kati ya mapendezi mawili, moja likiwa lenye kutamanika zaidi kushinda lingine—tuseme, biskuti moja kwa kulinganisha na mbili. Wangeweza kupata lile pendezi bora zaidi la biskuti mbili ikiwa tu wangengoja mpaka mwalimu arudi. Kwa upande mwingine, wangeacha kungojea wakati wowote kwa kubonyeza kengele, ambapo ingemaanisha kupata pendezi lisilo bora la biskuti moja na kupoteza lile bora zaidi la biskuti mbili. Wanasayansi waliandika chini tabia zao na baada ya miaka kumi wakaangalia maendeleo ya watoto wale wale.
Gazeti Science laripoti kwamba watoto ambao walikuwa na utayari zaidi wa kuahirisha utoshelezo wa papo hapo walikuwa vijana bora baadaye. Walikuwa wanafaa kijamii na kielimu na pia walikuwa na uwezo wa kudhibiti mkazo wa akili na mvunjiko wa moyo. Kwa wazi, uwezo wa kuahirisha utoshelezo—kuahirisha kile tunachotaka—ni ustadi wa maana sana kwa maisha zetu. Na hunufaisha watu wazima pia.
Siku zote sisi huwa na msongo wa kuchagua kati ya utoshelezo wa papo hapo na utoshelezo ulioahirishwa. Mambo mengine ya kuchagua huonekana madogo: ‘Je, nile keki hiyo au nichunguze uzito wangu?’ ‘Je, niitazame TV, au kuna kitu cha maana zaidi ambacho ninaweza kufanya sasa?’ ‘Je, nijibu neno hilo au ninyamaze tu?’ Katika kila hali, lazima tupime mvuto wa utoshelezo wa papo hapo dhidi ya madhara yatokeayo baadaye. Ni kweli, hayo si mambo mazito sana.
Mambo mazito zaidi ambayo watu hukabili ni maamuzi ya maadili: ‘Je, nidanganye ili nitoke katika hali hii au nitafute njia ya unyofu na yenye busara?’ ‘Je, niitikie ubembe wake na kuona kitakachotokea, au nihifadhi ndoa yangu?’ ‘Je, nijiunge na umati nivute bangi, au niheshimu sheria na kulinda mwili wangu?’ Bila shaka, kama vile umekwisha ona, mwendo wa utoshelezo wa papo hapo waweza kugeuza maisha ya mtu yaharibike mara moja.
Kama vile gazeti Science linavyoliweka jambo hilo: “Ili kutenda kwa kufaa, kila mtu mmoja mmoja ni lazima aahirishe kwa hiari kupata utoshelezo wa papo hapo na kudumu katika kutafuta tabia zenye lengo fulani kwa ajili ya matokeo ya baadaye.” Kwa hiyo labda hatutaishi maisha mazuri ikiwa tunatosheleza tamaa zetu zote papo hapo.
Hata hivyo, twaishi katika ulimwengu wenye kushikilia sana matoshelezo ya papo hapo, ulimwengu uonekanao kama umejawa na watu wazima wenye tabia ya Johnny mchanga, wenye mbetuko wa kupata wanachotaka sasa, wakiwa vipofu kwa madhara ya baadaye. Mwelekeo wao ndio umefanyiza ulimwengu wetu wa kisasa, na si kwa ubora wa ulimwengu.