Mbona Gogota Hawavunjiki Shingo?
JE! UMEPATA kusikia ndege gogota akitoboa mti? Kwa kuwa kuna jamii ya gogota karibu 200 ulimwenguni pote, huenda umeona kudonoa kwake kwenye kufuliza kunakosikika kama bunduki-mimina-risasi. Nilipomwona mmoja, huku mdomo wake ukidonoa kisiki cha mti, ilinifanya nijiulize, ‘Mbona havunjiki shingo au kuharibu ubongo wake?’ Kama sisi tukiwa binadamu tungefanya kitendo chenye jeuri kama hicho, tungehitaji kuchunguzwa na daktari wa mifupa au mpasuaji wa ubongo! Kwa hiyo, siri ni nini?
Kama kielelezo, fikiria gogota tumbo-jekundu apatikanaye katika upande wa mashariki wa United States. Kitabu Book of North American Birds chasema: “Kwa mdomo wake mzito, wenye muundo kama wa patasi, yeye hudonoa wadudu kutoka chini ya gome la mti, hutoboa mashimo ili kufikia mendemilia mwenye kutoboa miti, hukatakata vipande vya mti huku akichimba shimo la kiota.” Yeye hujilindaje dhidi ya mavumbi ya mti? “Mianzi yake ya pua imefunikwa kwa kufaa na kifuniko kidogo cha manyoya mororo yaliyosimama wima.”
Vipi juu ya kichwa kupigwa-pigwa? “Ili kuzuia ubongo usiharibiwe . . . , shingo yenye nguvu, fuvu nene, na nafasi yenye kupunguza mpigo kati ya ngozi nzito ya nje na ubongo wenyewe huwa ulinzi wa kipekee.”
Gogota mwingine, tumbo-manjano afyonzaye utomvu, hutoboa safu ya mashimo laini katika gome, ambayo yeye hufyonza utomvu. Tofauti na gogota tumbo-jekundu, mwenye ulimi mrefu ajabu wenye kujipinda-pinda na wenye ncha kali ya kufumia (kuchomea) wadudu, yule mfyonza utomvu ana ulimi mfupi zaidi wenye nywele-nywele laini za kusaidia kunywa utomvu.
Kwa kweli unamna-namna huo wa ubuni wenye uzuri waonyesha kuna Mbuni, Yehova Mungu. Twapaswa kuyakariri maneno ya Ayubu kwa unyenyekevu: “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.” Na Daudi aliandika: “Matendo yako ni ya ajabu, na nafsi yangu yajua sana.”—Ayubu 42:2; Zaburi 139:14.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Leonard Lee Rue, 111/ H. Armstrong Roberts
Kushoto: H. Armstrong Roberts