Amkeni!—Msingi wa Mtihani
WANAFUNZI katika nchi ya Amerika Kusini ya Suriname walipofunua kijitabu chao cha mtihani wa mwingilio wa shule ya upili katika Julai 1993, waligundua kwamba wasomaji wa kawaida wa gazeti la Amkeni! walikuwa na manufaa ya ziada. Hii ilikuwa kwa sababu karibu nusu ya maswali katika kijitabu hicho chenye kurasa 36, kilichokuwa kimetayarishwa na Idara ya Mtihani ya Wizara ya Elimu, yalitegemea makala mbili kutoka kwa Amkeni!
Kurasa za 1 hadi 9 zilikazia makala “Mitaa ya Hali ya Chini—Nyakati Ngumu Katika Matatizo ya Maisha ya Mjini,” iliyotokea katika Amkeni! la Oktoba 8, 1992. Kulikuwa na maswali 21 ambayo yalitahini ufahamu juu ya habari hiyo. Kurasa 10 hadi 16 za kijitabu hicho cha mtihani zilikuwa na maswali 14 juu ya makala “Capybara—Kasoro au Ajabu ya Uumbaji?,” iliyotokea katika Amkeni! la Septemba 22, 1992 (Kiingereza).
“Kwa kutumia makala hizi ili kuchunguza ufahamu wa maneno wa wanafunzi kotekote nchini,” alieleza mwalimu mkuu mmoja katika sehemu ya magharibi ya Suriname, “mamlaka za shule zaonyesha kwamba zinaona Amkeni! kuwa kigezo kwa sarufi sahihi na uandikaji wa ufupisho.”
Ikiwa ungependa nakala ya Amkeni! au ungependa mtu akutembelee nyumbani kwako ili kuzungumzia jambo hili, tafadhali andikia I.B.S.A., Box 47788, Nairobi, Kenya, au anwani yoyote ifaayo iliyoorodheshwa kwenye ukurasa 5.