Je, Kutakuwako na Maji ya Kutosha?
“Ni asilimia 2 ya jumla ya maji yote ya Dunia ambayo ni safi, na thuluthi 2 ya huo ugavi uwezao kutumiwa umeganda nchani na katika kanda za barafuto, yakiacha [chini ya] asilimia 1 yakiwa maji safi.” —Research and Exploration, kichapo cha National Geographic.
JE, MNA maji ya mfereji yanayofaa kunywewa nyumbani mwenu? Basi nyinyi ni miongoni mwa wale waliobarikiwa. Mamilioni ya watu hulazimika kujichotea maji, mara nyingi kilometa nyingi kutoka nyumbani—na kisha mara nyingi hayafai kamwe kwa kunywewa. Wengine hulazimika kukusanyika kwenye mifereji ya umma ama kwenye malori ili kupata ugavi wa hayo maji yenye thamani. Research and Exploration lilitaarifu hivi: “Kadiri binadamu wanavyozidi kurudufika, ndivyo tatizo la utumizi na usimamizi wa maji linavyozidi kukua. Matatizo haya ni mabaya zaidi katika ulimwengu unaositawi, ambapo watu wapatao bilioni 1 tayari huona vigumu ama hawawezi kupata maji ya kunywa yafaayo.” Hilo lamaanisha kwamba karibu 1 katika 5 ya idadi ya watu ulimwenguni ina tatizo kubwa la kupata maji ya kutumia.
Mbegu za migongano ya wakati ujao tayari zimepandwa katika upungufu huu wa maji. Mtaalamu mmoja alisema hivi: “Idadi yenye kuongezeka ya watu watashindwa kuboresha maisha zao, kuishi katika mitaa ya vibanda ambapo majaribio ya kushinda umaskini, ulemavu wa kimila, na magomvi ya kikabila yatakomeshwa na ukosefu wa maji ya kunywa, ardhi ya kulima, nafasi ya kujiruzukia.”
Sisi mmoja-mmoja tunaweza kufanya nini ili kutumia rasilimali hii yenye thamani kwa hekima? Itumie kwa kufaa na kwa umakini—hayo ni yenye thamani na yawezayo kumalizika.
1) Usitumie maji vibaya. Usiache maji yamwagike ivi hivi tu mferejini—kama wakati unapopiga mswaki ama kunyoa ndevu. Usitumie muda mrefu bafuni—ikiwa umebarikiwa kuwa na moja!
2) Usiharibu maji ama kuyachafua. Ikiwa mto au kijito kilichochafuliwa kinapita karibu na mahali unapoishi, mtu fulani huko juu anaharibu mfereji wa uhai ulio muhimu kwa jumuiya yako. Mara nyingi wenye kutokeza uchafuzi huu ni mamlaka za mji, wanaviwanda, wakulima, na wengine ambao huenda wakaruhusu uchafu usiochujwa na bidhaa za kikemikali kutiririka ama kuvuja kwenye vijito na mito.
Mungu, akiwa Mfanyi na Mpangishaji wa dunia, ana mamlaka ya kututoza kuhusu jinsi tunavyotumia sayari yetu. Biblia ilitabiri kwamba kwa hakika Yehova ‘atawaharibu hao waiharibuo nchi.’—Ufunuo 11:18.