Familia za Mzazi Mmoja—Mwelekeo wenye Kuongezeka
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
“KUNA familia nyingi zaidi za mzazi mmoja katika Uingereza kuliko nchi nyingineyo yoyote katika Ulaya,” laripoti The Times la London. “Wazazi walio peke yao . . . sasa watunza karibu familia moja kati ya kila tano katika Uingereza wakiwa na watoto walio chini ya miaka 18, ikilinganishwa na familia moja kati ya kila saba katika Denmark na moja kati ya nane katika Ujerumani na Ufaransa.”
Kwa kila wazazi kumi walio peke yao katika Uingereza, tisa ni wanawake. Zile familia za kitamaduni, ama zilizofanyizwa na baba na mama pamoja na watoto wao sasa zaonekana kuwa “dhana [moja tu] ya familia” miongoni mwa dhana nyinginezo. Lakini kwa nini aina ya familia ya mzazi mmoja imeenea sana kuliko awali?
Talaka na mtengano ni visababishi vikuu. Kuhusu hilo, Uingereza yafuata ule mwelekeo katika Marekani, ambako karibu nusu ya ndoa zote huishia katika talaka. Pia, lile ambalo watu hutazamia kuhusu ndoa limebadilika. Kulingana na Zelda West-Meads, wa shirika la kutoa mwongozo wa ndoa la Relate, miaka 20 ama 30 iliyopita, “mafungu ya watu wa jinsia tofauti yalibainishwa waziwazi zaidi. Mwanamume alikuwa mtoa-riziki; mwanamke alikuwa mtunza-nyumba.” Lakini vipi kuhusu wakati wa sasa? “Ndoa za sasa huenda zikawa zenye kusisimua na kufurahisha zaidi, lakini pia zaweza kuwa ngumu zaidi. Wanawake wanataka mengi zaidi kutoka kwa ndoa kuliko yale ambayo mama na nyanya zao walitarajia. Wanataka usawa, mpenzi mzuri, rafiki mzuri, kazi-maisha kwa ajili yao wenyewe—na watoto pia.”
Kufanya ngono na yeyote umtakaye kunakoonyeshwa kotekote katika vitumbuizo vya ulimwengu huchochea dharau kwa familia ya kitamaduni. Vijana wanaofanya ngono katika umri wao wa mapema sana mara nyingi huwa hawajui yale yawezayo kuwa matokeo. Kwao ndoa ni tatizo, upungufu wa uhuru wao wa kibinafsi, jambo fulani lisilo la lazima maishani.
Wengine ni wazazi walio peke yao kwa kupenda; wengine huwa hivyo kwa sababu ya hali. Wanapolazimika kuwa mzazi mmoja, watu wengi waliooa au kuolewa hawafurahi kuwa peke yao. Miongoni mwa hawa ni wenzi waliokuwa katika ndoa yenye furaha lakini wamepoteza mwenzi wao katika kifo.
Kwa upande ule mwingine, kuna wale ambao ndoa zao zimekuwa na uhasama mkali. Wao hupata kitulizo kulea watoto wao wakiwa peke yao. Wengi wa hawa hueleza kuhusu uhusiano wa karibu ambao wamesitawisha na watoto wao.
Ingawa kuna visababishi vingi vya mwelekeo wenye kuongezeka wa kuwa na familia za mzazi mmoja, inapokuja kwa madaraka mbalimbali na magumu ya maisha ya kila siku, wazazi walio peke yao wanakuwa na mahangaiko hususa. Hayo ni yapi? Na ni vipi wazazi walio peke yao wanaweza kuchukua madaraka yao kwa kufanikiwa?