Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 10/8 kur. 4-7
  • Kuwa Mzazi Aliye Peke Yake Mwenye Kufanikiwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuwa Mzazi Aliye Peke Yake Mwenye Kufanikiwa
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Komboa Wakati
  • Ridhika na Mahitaji ya Lazima
  • Ili Kupata Marafiki, Uwe Mwenye Urafiki
  • Kutenda Kama Baba na Mama
  • Familia za Mzazi Mmoja Zaweza Kufanikiwa!
    Siri ya Furaha ya Familia
  • Je, Unawajali Wazazi Wasio na Wenzi wa Ndoa?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
  • Mzazi Mmoja, Matatizo Mengi
    Amkeni!—2002
  • Wazazi Wasio na Wenzi Wanashinda na Matatizo ya Ulimwengu wa Leo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1981
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 10/8 kur. 4-7

Kuwa Mzazi Aliye Peke Yake Mwenye Kufanikiwa

“Kitu kimoja ambacho wazazi wote walio peke yao hawana kamwe kwa kutosha ni wakati.” —The Single Parent’s Survival Guide.

“Ukosefu wa fedha ndilo tatizo kubwa zaidi.” —Times la London.

‘Upweke ni chanzo kikuu cha mkazo kwa mzazi aliye peke yake.’—Give Us a Break, uchunguzi fulani kuhusu fursa za kupumzika za wazazi walio peke yao.

WAZAZI wote hukabili magumu, shangwe, na matatizo. Lakini wazazi walio peke yao hufanya hivyo bila mwenzi. Kama tokeo, wakati, fedha, na upweke mara nyingi huwa mambo yenye kutokeza zaidi katika maisha zao.

Ingawa maisha yao huenda yakawa magumu kihalisi, wazazi walio peke yao wanaweza kufaulu katika maisha ya familia zao, na wengi hufaulu. Mengi hutegemea viwango wanavyokubali na kadiri wanavyoshikamana navyo.

Kwa kupendeza, Biblia ilitabiri kale ule mvurugo wa sasa wa kimaadili na kijamii. Ona jinsi Paulo mtume Mkristo alivyomtahadharisha Timotheo mwanafunzi kijana kuhusu hili. “Lakini fahamu neno hili,” akaonya, “ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, . . . wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu.”—2 Timotheo 3:1-3.

Biblia si kitabu ambacho kilitabiri mitazamo ya leo kwa usahihi tu. Ni yenye kanuni ambazo, zikifuatwa, huhakikisha mafanikio katika maisha ya familia. (2 Timotheo 3:16, 17) Ebu fikiria jinsi baadhi ya hizi zinaweza kusaidia wazazi walio peke yao kukabiliana na matatizo ya wakati, fedha, na upweke.

Komboa Wakati

Hata uwe mwenye utaratibu wa jinsi gani, wakati ni kitu adimu. Ili kutumia wakati wako vyema, kwanza wahitaji kutambulisha kwa kweli vile unavyoutumia. Kisha utaweza kuamua ni utendaji gani ulio wa muhimu sana kwako. “Weka ‘maandishi ya utumizi wa wakati,’” lapendekeza shirika moja la wazazi walio peke yao. “Katika hayo weka rekodi ya kila kitu ukifanyacho siku ama juma zima, na uone ni kiasi gani cha wakati unachotumia. Baada ya hilo, chunguza uone ni wapi wakati waweza kukombolewa, ama kutumiwa vizuri zaidi, kwa kubadilisha vipaumbele ama kwa kutofanya mambo mengine.”

Ushauri timamu kama huo huonyesha ile hekima ya Kimaandiko iliyoko katika maagizo ya mtume: ‘Angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima, bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.’—Waefeso 5:15, 16.

Kwa kielelezo, je, kutazama televisheni hutokeza sana katika kawaida yako ya kila siku? Kupunguza hilo kutakupa wakati wa ziada wa kuzungumza na watoto wako na kufanya mambo pamoja. Hilo laweza kusaidia kujenga uhusiano mzuri pamoja nao.

‘Jitihada zangu za kukaa kitako na kuzungumza na watoto wangu huishia kwa kimya chenye vishindo vikuu,’ huenda ukasema. Huenda ikawa hivyo, lakini usiache hilo likushinde. Washauri wa wazazi walio peke yao hupendekeza kwamba utambue hisia katika mazungumzo ya kila siku ya watoto wako, kama vile yale wanayosema kuhusu marafiki wa shuleni ama kile wanachopanga kufanya. Lakini huwezi kamwe kufanya hivyo televisheni inasapo uangalifu wako, je, unaweza? Hata ukiifungua kwa sauti ndogo, ukengeushi utakunyima habari muhimu kuhusu mawazio na hisia za ndani za watoto wako. Hivyo tafuta wakati kwa ajili ya watoto wako. Fanyeni kazi ndogo-ndogo za nyumbani pamoja, na mnapoendelea kuzifanya, zungumza nao—nawe usikilize wanaposema!

Soma nao pia. Utafiti waonyesha uhusiano wenye nguvu kati ya mtoto kujua kusoma na kuandika akiwa na umri wa miaka mitano na mafanikio yake ya baadaye. Hii ni sababu muhimu hata zaidi ya kukomboa wakati ili kusoma pamoja nao. Dakika chache kabla ya kwenda kulala, ama mapema jioni kabla ya kuhisi kuchoka mno, utakuwa wakati uliotumiwa kwa hekima.

Ridhika na Mahitaji ya Lazima

Wazazi wengi walio peke yao hujipata wamenaswa katika hali mbaya ya kifedha. Viwavyo vyote ni lazima wapate fedha za kutosha kulipia nyumba, chakula, na mavazi. Lakini kwenda kazini hutokeza lile suala la jinsi ya kuandaa utunzi unaofaa kwa watoto.

Makao ya kutunza watoto sikuzote si rahisi kupatikana, wala si rahisi kugharamia. Wazazi wengine walio peke yao hufaulu kwa kupata msaada wa watu wa ukoo—wazazi-wakuu, shangazi, na wajomba. Wengine hutegemea shule za watoto, maeneo ya kuchezea, na makao ya kutunza watoto yanayoandaliwa na waajiri wao. Upaji wa serikali, ikiwa wapatikana, sikuzote haulipi kabisa karo ambayo huenda ikahitajika kwa ajili ya utunzi wa watoto kama huo. Katika mabara mengine, wazazi walio peke yao wenye vitoto vichanga huenda waamue kutotafuta kuajiriwa lakini wakae nyumbani na kujiruzuku kwa fedha ziandaliwazo na serikali.

Kukiwa na idadi yenye kuongezeka ya wazazi walio peke yao wanaohitaji kutunzwa, serikali mbalimbali nazo hugeukia wale wenye daraka la kutoa utunzi huo. Katika Uingereza jambo hili tayari limefanya baba watoro ambao hawatoi fedha kwa ajili ya watoto wao wawekewe masharti makali. Mashirika ya kutegemeza watoto hufuatilia baba wasiolipa ili kupata tena malipo waliyokosa kulipa. Mama walio peke yao wanapokataa kusaidia hayo mashirika kumtafuta baba, yaelekea watapoteza mapato fulani ya kifedha. “Katika Sweden yakadiriwa kwamba asilimia 40 ya wanaokosa kulipa wanashikwa kupitia mashirika ya bima ya jamii ya huko, na katika Ufaransa mahakama hufikiliza sheria za utunzaji na ufuatiliaji wa wale wanaokosa kulipa,” laripoti The Times la London.

Iwe kuna mahakama ama hakuna mahakama, iwe kuna misaada ya serikali ama hakuna misaada ya serikali, wazazi wengi walio peke yao hupata njia za kujisaidia ili kujiendeleza kwa fedha chache kuliko zile walizozoea awali. Jinsi gani? Kwa kupanga matumizi kwa njia tofauti.

Kujifunza kupanga matumizi kwa njia tofauti ni ustadi. Hilo kwa kawaida humaanisha kubadilisha vipaumbele katika matumizi—kwa kielelezo, kuweka fedha kando kwa ajili ya bili ya nyumba na umeme kwanza, kisha za kununua chakula, na halafu za kulipa mikopo. “Tukiwa na chakula na nguo,” akaeleza mtume Paulo, “tutaridhika na vitu hivyo.”—1 Timotheo 6:8.

Je, umepata kufikiria kushiriki gharama na wengine? Kununua vyakula na vifaa vya nyumbani kwa wingi pamoja na wazazi wengine kwaweza kuokoa fedha zako. Hata iwe wapanga matumizi kwa njia gani, kumbuka wahitaji kukaa kitako na kupiga hesabu matumizi yako. (Linganisha Luka 14:28.) Kwa nini usishirikishe watoto wako katika kupanga matumizi? Kisha wataliona kuwa ni pendeleo kukusaidia kuyafuata. Hata huenda ukapata kwamba unaweza kuweka fedha akiba.

Ili Kupata Marafiki, Uwe Mwenye Urafiki

“Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa,” akashauri Yesu. “Kwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.” (Luka 6:38) Hilo ni kweli pia katika mahusiano ya kibinafsi. Kupendezwa na wengine kwaweza kutokeza maitikio ya kirafiki. Njia iliyo bora zaidi ya kushinda upweke ni kuwa wa kwanza kufanya marafiki. Labda utaweza kupata marafiki wenye kutegemeka ambao watatunza watoto wako ili uweze kutembea mahali fulani. Lililo bora hata zaidi, kwa nini usiwaombe marafiki wakutembelee?

Lakini tahadhari yahitajiwa. Kumbuka, ‘mashirika mabaya huharibu tabia njema.’ (1 Wakorintho 15:33) Upweke waweza kushindwa tu kwa kufanikiwa wakati marafiki unaofanya wanapokuwa wenye kujenga kikweli na kuleta uradhi.

Kutenda Kama Baba na Mama

Wazazi walio peke yao lazima wawe mama na baba kwa watoto wao—hilo si jukumu rahisi kwa yeyote. Na usisahau, watoto huzaliwa wakiwa waigaji. Wao hujifunza kuwa watu wazima wenye kuchukua daraka kwa kutazama yale watu wazima hufanya. Hivyo basi, mengi hutegemea aina ya kiolezo cha kuigwa unachoandaa kwa watoto wako. Likieleza kuhusu kutokuwako kwa akina baba idadi kubwa ya wavulana waliokulia kwenye vitovu vya majiji ya Amerika, The Sunday Times la London lataarifu: “Ile jeuri na vurugu ya kijamii . . . hutueleza jinsi kizazi cha wanaume hutenda wakati nusu yacho hufikia ubalehe bila ya kufunzwa kinachomaanishwa kuwa mwanamume mtu-mzima.”

Watoto wanapolelewa na wazazi walio peke yao, afya yao na kazi ya shuleni na hata matazamio yao ya kiuchumi yaweza kuathiriwa vibaya sana, akasema Duncan Dormor katika The Relationship Revolution. Watafiti wengine hubisha ugunduzi huo. Umaskini na unyimivu wa kijamii ndizo wao hulaumu. Hata hivyo, wengi hukubaliana na uchanganuzi wa mwanasayansi wa kijamii Charles Murray: “Mtoto mwenye mama na hana baba, akiishi katika ujirani wa akina mama bila ya akina baba, yeye huamua mambo kulingana na anayoona. Mnaweza kupeleka wafanyakazi wa kijamii na walimu wa shule na makasisi ili kumweleza kijana mwanamume kwamba atakapokuwa mkubwa anapaswa kuwa baba mzuri kwa watoto wake. Lakini hajui kinachomaanishwa na hilo mpaka aone.” Naam, wavulana wahitaji baba na mama, nao wasichana wahitaji pia.

Kwenye Zaburi 68:5, (New World Translation) inamfafanua Yehova Mungu kuwa “baba wa vijana mayatima.” Mama wanaomtegemea Mungu kwa uongozi hupata katika yeye kielelezo kilicho bora zaidi kwa watoto wao. Akina baba ambao hulea watoto wao peke yao huthamini msaada kutoka kwa wanawake wenye kuchukua daraka, waliokomaa. Naam, wanachohitaji wazazi wote walio peke yao ni utegemezo wenye upendo. Labda kwa upande huu unaweza kusaidia!

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Baba Ambao Pia Ni “Akina Mama”

Wanaume wanaotunza familia za mzazi mmoja ni wachache. Lakini kadiri ndoa zaidi zinavyovunjika, wanaume wengi zaidi wanaamua kutunza watoto wao peke yao. “Moja ya matatizo makubwa kupita yote ambayo wanaume huelekea kuyakabili ni yale ya binti mbalehe,” laeleza The Single Parent’s Survival Guide. Fedheha husababisha akina baba wengine kuepuka kuzungumza mambo ya kingono. Wengine hupanga mwanamke wa ukoo mwenye kuaminika kuzungumza na binti zao. Wazazi wote walio peke yao, waume kwa wake, watanufaika sana kwa kusoma pamoja na watoto wao kile kitabu Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi.a Kitabu hiki kina sehemu zenye vichwa “Ngono na Maadili” na “Urafiki na Mtu wa Jinsia Tofauti, Upendo, na Jinsia Tofauti.” Kila sura humalizia kwa sehemu yenye Maswali Kwa Ajili Ya Mazungumzo, iliyobuniwa ili kuhakikisha pitio lifaalo la hata mambo ya ndani sana.

[Maelezo ya Chini]

a Kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kutumia wakati wenye kujaa maana pamoja na watoto wako hujenga mahusiano mazuri

[Picha katika ukurasa wa 7]

Hata iwe wapanga matumizi kwa njia gani, kaa kitako na upige hesabu matumizi yako

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki