Kuutazama Ulimwengu
“Kujipinga” kwa Vatikani
“Mtakatifu, kwa nini Vatikani bado huuza sigareti?” padri fulani akauliza John Paul 2 wakati wa mkutano wake wa mwaka pamoja na makasisi wa Roma. Yeye aliendelea: “Licha ya kudhuru kiafya, biashara hii yapinga himizo lako kuhusu kulinda afya na kazi yetu ya uchungaji.” Kwa Ugo Mesini, padri mwenye umri wa miaka 76, uhakika wa kwamba Vatikani huuza tumbaku na sigareti zenye taarifa “kuvuta sigareti hudhuru afya yako” ni “ushuhuda ulio kinyume” na “kujipinga” kwa ujumbe wa papa. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la habari la Roma Il Messaggero, papa alijibu kuhusu habari ya tumbaku kwamba, ‘dhamiri yake ni safi.’ Ingawa hivyo, aliahidi kuzungumza na kadinali msimamizi wa Vatikani kuhusu uuzaji wa sigareti.
“Karne ya Shetani”
“Kwa kuifikiria mabaya yote, hii imekuwa karne ya Shetani,” wasema uhariri wa New York Times. “Katika historia ya binadamu watu hawajapata kamwe kudhihirisha ustadi mkubwa hivyo, na tamaa kubwa hivyo ya kuua mamilioni ya watu wengine kwa sababu za kijamii, kidini ama tabaka.” Ukiwa uthibitisho, wataja kambi ya kufishia ya Auschwitz iliyovumbuliwa miaka 50 iliyopita. Wale walioiweka huru kambi hii ya mateso ya Ujerumani walipata “watumwa wakiwa wembamba kama vijiti, watoto waliokatwa viungo katika majaribio ya maabara yenye kichaa, na yale masalio ya vyumba vinne vya kufishia kwa gesi na mahali pa kuchomea ambavyo wakati mmoja vilitwaa majeruhi wapatao 20,000 kwa siku,” uhariri huo ukasema, na yaliyokazika kikiki akilini mwao ni “ile miili iliyowekwa marundo kama kuni, zile jozi 43,000 za viatu, yale marundo ya nywele za binadamu.” Huo waongezea: “Hadi sasa, yale yaliyotukia katika Auschwitz yashinda utimamu na ufahamu.”
Upungufu wa Chakula Watazamiwa
“Ikiwa hakutakuwa na kuchangia kwingi ili kubadili tekinolojia, twaelekea kuona cha mtema-kuni,” akasema Ismail Serageldin, mtaalamu wa usitawishaji kutoka Misri na makamu wa rais wa Benki ya Ulimwengu. Yeye azungumzia kuhusu uhitaji wenye kuongezeka wa chakula cha msingi—uhitaji ambao tayari unapita utokezaji wa mazao katika maeneo fulani ya Asia na Afrika, ambako ukuzi wa watu ni wa kasi mno. “Tutapata bilioni mbili zaidi [za watu] katika miaka 20 ijayo hata iweje, na asilimia 95 yao watakuwa katika nchi zilizo maskini kupita zote,” yeye akasema. Ingawa maongezeko makubwa katika mazao ya mimea ya msingi yamefikiwa katika miaka 25 iliyopita, mazao ya ziada yamekuwa vigumu sana kuyafikia kwa sababu ya vizuizi vya kimazingira na kibiolojia. Mazao pia yatishwa na wadudu wasumbufu zaidi na maradhi ya mimea na kutokana na kudhoofika kwa ardhi. Worldwatch Institute yakubali hivi: “Uthibitisho kwamba ulimwengu uko katika njia ya kiuchumi ambayo haifai kimazingira waweza kuonekana katika uvuvi wa samaki wenye kudidimia, viwango vya maji vyenye kupungua, idadi ya ndege yenye kuyoyomea, joto jingi na maghala ya nafaka yenye kupungua, kutaja tu mambo machache,” inasema katika ripoti yayo ya State of the World 1995.
Umri na Mlo
Watafiti fulani sasa wasema kwamba watu wenye umri zaidi ya miaka 50 hawahitaji kuhangaika kuhusu ongezeko la uzani katika umri wa makamu, laripoti The Times la London. Mathalani, David Dickinson, mhariri wa gazeti la Consumers’ Association, asema hivi: “Ushauri kwamba kila mtu mwenye uwiano wa kimo kwa uzani wa juu zaidi kwamba ni mnene mno na anapaswa kuwa mwembamba ni kosa. Kuwa mwembamba kwaweza kudhuru afya yako kando na matokeo yao ya uwiano wa kimo kwa uzani. Watu wengi walio na umri wa zaidi ya miaka 50 hawahitaji kuwa wembamba.” Profesa wa Lishe na Mlo Tom Sanders aeleza hivi: “Zile hatari za kunenepa mno mara nyingi hutiwa chumvi. Unene huongeza hatari ya ugonjwa wa kisukari na yabisi baridi, lakini hatari za afya za unene ni chache sana. Hata huenda ukawa wenye manufaa kwa wanawake.” Na Dakt. Martin Wiseman wa Idara ya Afya ashauri hivi: “Katika umri wowote ule ni muhimu kutokuwa mnene mno ama mwembamba mno. Kula kwa kiasi na kuwa mtendaji ndio njia bora zaidi ya kufikia hilo lakini kadiri tunavyozeeka ni afadhali kuwa wanene kuliko kuwa wembamba.”
Je, Ni Aksidenti Yenye Manufaa?
Behewa lililojazwa vichezeo vya plastiki 29,000—mabata, makasa, panya wa majini, na vyura—lilifagiliwa baharini kutoka melini na dhoruba ya Pasifiki Kaskazini katika Januari 1992. Aksidenti hii imekuwa yenye manufaa kwa wanasayansi. Kinyume na viatu vya riadha 61,000 vya Nike vilivyomwagwa baharini miaka miwili mapema, hivyo vichezeo vyepesi vilielea juu ya maji na vilipelekwa na upepo na pia mikondo ya bahari-kuu. Jambo hilo limewezesha wasomi wa bahari-kuu wanaochunguza kupwa kwa Pasifiki Kaskazini kutia ndani athari ya upepo katika uchunguzi wao. Vichezeo vya kwanza vilianza kutokea katika fuo kusini-mashariki mwa Alaska miezi mitano baada ya huo mmwagiko, na 400 zaidi viliwasili kwenye ufuo utandao kilometa 850 katika Ghuba ya Alaska mnamo miezi kumi iliyofuata. Hivyo vichezeo vidogo, vyenye urefu upatao sentimeta 13, vilikuwa vikisafirishwa kutoka Hong Kong hadi Tacoma, Washington, Marekani. Inatazamiwa kwamba hatimaye vingine vitapitia Mpito wa Bering, visafiri kwenye barafu kuvuka Bahari-Kuu ya Aktiki, na kuwasili Atlantiki Kaskazini.
Ushindi-Nusu wa Polio
Ugonjwa wa Paralytic poliomyelitis, kwa kawaida uitwao polio, yasemekana kuwa umeua ama kulemaza zaidi ya watu milioni 10 katika historia. Ulionyeshwa kwenye michongo huko nyuma katika Misri, Ugiriki, na Roma za kale. Mara nyingi ukiwapata vijana, unaweza kusababisha ulemavu ama kifo kwa kusongwa pumzi. Sasa, kulingana na Pan American Health Organization, tanzu la Shirika la Afya Ulimwenguni, ugonjwa wa polio umekomeshwa katika Kizio cha Magharibi. Kisa cha mwisho kilichoripotiwa kilikuwa cha mtoto wa Peru katika 1991, aliyepona akiwa na mguu uliodhuriwa. Hata hivyo, kinyume na ndui, uliokomeshwa ulimwenguni pote katika 1977, virusi ya polio bado yapatikana katika maeneo mengine na kuna uwezekano wa kuuanzisha upya katika Amerika kupitia wahamiaji ama wasafiri. Ripoti ya mwisho iliyo kamili ilionyesha visa vipunguavyo 10,000 mwaka huo. Mpaka ukomeshwe kabisa, uchanjaji dhidi ya huo ugonjwa lazima uendelee, wasema wataalamu wa afya.
Tashwishi ya Taiwan ya Orangutan
Mamlaka mbalimbali katika Taiwan zakabili tatizo lisilo la kawaida: Jinsi ya kushughulikia orangutan ambao walikuja kuwa wanyama wa kufugwa maarufu katika 1986 baada ya mmoja kuonyeshwa kwenye televisheni akiwa “mwandamani afaaye.” Kama ilivyoripotiwa katika New Scientist, orangutan wadogo wapatao elfu moja waliletwa katika hiyo nchi na kuuzwa wakiwa wanyama wa kufugwa. Sasa, hao wanyama kadiri wafikiapo ukomavu wa kijinsia na kuwa wakali na bila kubashirika, kwa mamia wanaachwa na wenyewe. Kwa sababu ni wanyama wapweke na hawaingiliani na vikundi vya kijamii kama ilivyo na sokwe-mtu na nyani-mtu, orangutan waliofugwa wanaweza kurudishwa porini. Hata hivyo, hao wanyama wa kufugwa wamechukua maradhi mbalimbali ya kibinadamu, kama vile mchochota wa ini B na kifua kikuu, na wangeweza kuhatarisha idadi iliyohatarishwa tayari ya orangutan wa mwituni. Huenda wengi waangamizwe, jambo ambalo wengi waonelea kuwa ni afadhali kuliko wao kuishi maisha yabakio kizimbani.
Watoto wa Mitaani wa Toronto
Maofisa wasema kwamba watoto wa mitaani wapatao 10,000 humanga-manga katika jiji la Toronto kwa ukawaida. “Hiyo idadi imepanda kwa haraka sana katika mwongo uliopita,” laripoti The Toronto Star. “Watoto walio wengi wa mitaani husimulia kuhusu matatizo nyumbani, yakienea kutoka kutendwa vibaya hadi sheria za mzazi waziasizo. Wao husimulia ulimwengu wa dawa za kulevya, jeuri na umalaya, na vipindi virefu vya uchoshi usioisha.” Yakadiriwa kwamba asilimia 54 ya watoto wa mitaani wa Toronto hufanya umalaya. Mmoja kati ya wasichana watano atapata mimba, asilimia 80 hutumia dawa za kulevya ama alkoholi, asilimia 67 wametendwa vibaya, na asilimia 43 wamejaribu kujiua. “Yeyote akikuambia maisha ya mitaani ni murua na yenye kusisimua, usiamini. Ni kama kifo, huko si kuishi kamwe,” adai kijana mmoja. “Wengine hawawezi kuacha dawa za kulevya, umalaya na uhalifu wenye kuongezeka; wengine, walio wakubwa kwa umri na werevu zaidi, watumaini kupata elimu na kazi fulani,” laongezea Star.
Okoa Jino Hilo!
Jino ling’olewapo kwa aksidenti fulani, usilitupe, yashauri UC Berkeley Wellness Letter. “Utafiti waonyesha kwamba una uwezo wa asilimia 50 wa kulirudisha kwa mafanikio ukimfikia daktari wa meno mnamo dakika 30.” Unapaswa kufanyaje? Jaribu kuwa mtulivu iwezekanavyo. Shika sehemu ya juu ya jino hilo na ulitie kwa uanana ndani ya maji yaliyo vuguvugu—usilisugue. Mpigie simu daktari wako wa meno kumweleza kuzuru kwako na, asipokuambia vingine, liweke hilo jino mahali palo kwa uanana. Uma kwa uthabiti ukitumia nguo ama kitambaa cha mkono kilicho safi kwa dakika tano ili kulihimilisha hilo jino, na endelea kuuma kwa nguvu ya kadiri mpaka umwone daktari wa meno. Ikiwa huwezi kuliingiza tena hilo jino, liweke katika mate kinywani mwako. Kwa watoto walio wachanga mno hivi kwamba huenda wameze hilo jino, litie ndani ya mfuko wa plastiki ama kikombe na ulichovye ndani ya maziwa ama maji yenye chumvi kidogo. Hata ikiwa wakati mrefu umepita, ni bora zaidi kumwona daktari wa meno na kumwacha aamue la kufanya. “Kuokoa jino kwa hakika kwastahiki hiyo jitihada,” yasema hiyo ripoti.