Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 2/8 kur. 11-14
  • Wakastrati—Ulemazo Katika Jina la Dini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wakastrati—Ulemazo Katika Jina la Dini
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matowashi Katika Historia ya Kale
  • Matowashi Katika Jumuiya ya Wakristo
  • Kwaya za Kanisa
  • Ulemazo kwa Ajili ya Muziki
  • Kupendwa, Wazazi, na Maoni ya Wengi
  • Uhasishaji—Katika Miaka ya 1990?
  • Mwisho wa Uhasishaji!
  • Kujifunza Kuimba Opera
    Amkeni!—2008
  • Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Je, Wajua?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
  • Uasi-Imani—Njia ya Kwenda Kwa Mungu Yazibwa
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 2/8 kur. 11-14

Wakastrati—Ulemazo Katika Jina la Dini

Wakastrati—walikuwa waimbaji wa kiume waliokuwa na nguvu za mwanamume lakini wenye sauti ya mvulana. Enzi ya wakastrati kwa kweli ilikuwa kipindi chenye kuhuzunisha. Wao walikuwa nani? Jibu linahusiana na zoea lenye kushtua—ulemazo katika jina la dini.

MATOWASHI wanaweza kuzaliwa wakiwa hivyo, lakini wengi wanafanywa kuwa hivyo na wanadamu. Katika umbo la mwili na kimo, wao ni wanaume, lakini hawawezi kuzaa. Kufikia hatua fulani katika ukuzi wao wa kimwili au hata baadaye maishani, wao wamehasiwa, ama kwa kutaka ama kwa kulazimishwa.

Kwa nini wanaume wachague kujilemaza au kulemaza wanaume wengine kwa namna hii? Mara nyingi, wamefanya hivyo katika jina la dini.

Matowashi Katika Historia ya Kale

Maelfu ya miaka iliyopita, uhasishaji ulitumiwa na Waashuru ukiwa namna ya adhabu. Katika Misri ulikuwa adhabu ya uzinzi. Mnyang’anyi aliyepatwa akiiba hekaluni katika Friesland ya kale, iliyo sehemu ya Uholanzi sasa, alihasiwa kabla ya kuuawa.

Katika Roma uhasishaji ulikatazwa wakati wa tawala za Maliki Domitian na Nerva katika karne ya kwanza W.K. lakini ukarudishwa katika miaka ya kumalizika kwa hiyo milki. Sheria zilizowekwa katika karne ya tisa na mfalme wa Uingereza Alfred Mkubwa zilitaka mtumishi aadhibiwe kwa uhasishaji ikiwa alimlala kinguvu mtumishi wa kike.

Matowashi pia walikuwa na sehemu kubwa katika kawaida za kidini. Matowashi na vilevile mabikira walitumikia kijimungu kike Artemi katika jiji la Efeso. Wanaume walijihasi katika sherehe zenye kichaa ili kumwabudu Astarte Mwashuri wa Hierapolis, ambapo baada ya hilo walivaa mavazi ya wanawake kwa muda wote wa maisha yao.

“Yeye ambaye hujihasi au kuhasi mtu mwingine si mmoja wa wafuasi wangu,” akatangaza Muhammad. Hata hivyo, licha ya katazo hilo, matowashi walikuwa na bei kubwa wakiwa watumwa katika nchi za Kiislamu, wakiwa walinzi wa nyumba za masuria na wake na sehemu zilizo takatifu. Likiwa tokeo, biashara hii ya utumwa iliendelea kwa muda mrefu. Wanaume vijana waliotolewa Sudan na nchi jirani za Afrika Kaskazini waliandaa faida kubwa mno kwa wafanyabiashara ya utumwa.

Mapema katika karne ya 19, Johann L. Burckhardt alizuru Misri Kusini, ambapo aliona wavulana waliohasiwa wakitayarishwa kuuzwa wakiwa watumwa. Upasuaji huo ulifanyiwa wavulana wenye umri wa kati ya miaka 8 na 12. Wapasuaji walikuwa watawa wawili wa Kanisa Koptiki. “Kazi yao,” akasema Burckhardt, “ilidharauliwa.”

Hili latokeza swali, Ni kwa kadiri gani Jumuiya ya Wakristo imejihusisha katika zoea hili, na kwa sababu zipi?

Matowashi Katika Jumuiya ya Wakristo

Origen—ajulikanaye sana kwa tafsiri zake za Hexapla, za Maandiko ya Kiebrania yaliyopangwa kwa safu sita—alizaliwa karibu 185 W.K. Kufikia alipokuwa na umri wa miaka 18, tayari alikuwa amejulikana sana kwa mihadhara yake juu ya Ukristo. Hata hivyo, alikuwa na wasiwasi kwamba umashuhuri wake miongoni mwa wanawake usieleweke vibaya. Kwa hiyo, akichukua kihalisi maneno ya Yesu, “wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni,” yeye alijihasi. (Mathayo 19:12)a Hilo lilikuwa tendo la kutokomaa, la msukumo—ambalo alikuja kulisikitikia sana katika miaka ya baadaye.

Kwa kupendeza, maandiko yaliyokubalika ya kwanza kabisa ya Baraza la Nicaea katika mwaka 325 W.K. yaliondoa kutoka ukuhani wanaume ambao walikuwa wamejihasi. Dakt. J. W. C. Wand asema hivi kuhusu mkataa huo: “Inawezekana kwamba watu fulani walikuwa wameonyesha tamaa ya kufuata kielelezo cha Origen kwa habari hii na kujifanya kuwa matowashi . . . , na ilikuwa muhimu kwamba Wakristo wasitiwe moyo kufuata desturi ambayo ilifanana sana na ile ya wajitoaji wa dini fulani za kipagani.”

Kwa kufanya uamuzi huo wa maana, viongozi wa kidini wa Jumuiya ya Wakristo walitafuta kupiga marufuku kabisa swala lenye kukirihisha la uhasishaji. Kama tutakavyoona, mambo hayakuwa hivyo. Fikiria simulizi lifuatalo linalojulikana sana.

Katika mwaka 1118, Peter Abelard, mwanafalsafa na mwanafunzi wa theolojia, alikuja kumpenda sana Héloïse, msichana mchanga aliyekuwa akimfunza kibinafsi. Abelard hakuwa ametawazwa bado na kwa hivyo hakuwa chini ya kiapo cha useja, kwa hiyo wakafunga ndoa kisiri na kupata mwana. Lakini kwa sababu mjomba wa Héloïse, Fulbert, kasisi katika kanisa kuu la Katoliki ya Kiroma la Paris, alihisi kwamba Héloïse alikuwa ameshawishiwa, aliamuru Abelard ahasiwe kinguvu. Tendo hilo la kinyama, lililotokana na ofisa wa kanisa wa cheo cha juu hivyo, liliongoza kwenye adhabu ya kuhasiwa kwa wawili wa wenye kufanya kitendo hicho.

Kwa hiyo uhasishaji bado ulikubalika kuwa adhabu katika hali fulani. Hata hivyo, zoea hilo lisilo la kimungu lilikuwa upesi liendelezwe katika Kanisa Katoliki ya Kiroma kwa sababu ya uimbaji wa kanisa.

Kwaya za Kanisa

Uimbaji umekuwa na fungu la maana sana katika Othodoksi ya Mashariki na desturi za Katoliki ya Kiroma, tegemezo kuu la kwaya ya kanisa likiwa soprano (sauti ya wavulana). Ingawa hivyo, sauti ya mvulana huwa nzito mapema katika utineja. Kanisa lingeweza kushindaje badiliko hilo la daima katika waimbaji na mazoezi yaliyohusika? Ni kweli, sauti ya juu zaidi isiyopendeza iitwayo Falseto mara nyingi ilitumiwa, lakini hii haikuwa kibadala kilichokubalika cha soprano ya wavulana.b

Sauti za kike zilikuwa kibadala dhahiri, lakini tangu nyakati za mapema papa alikuwa amekataza wanawake kuimba kanisani. Tatizo zaidi lilikuwa kwamba waimbaji wa kanisani wangeweza kuitwa kusaidia kasisi, kazi ambayo ilikuwa ya wanaume pekee. Kwa hiyo wanawake hawangeweza kutumiwa kukuza kwaya za kanisa.

Katika 1588, Papa Sixtus 5 alipiga marufuku wanawake kuimba jukwaani katika jumba lolote la maonyesho la umma au nyumba ya opera. Marufuku hiyo ilirudiwa na Papa Innocent 11 miaka 100 hivi baadaye. “Kukatazwa kwa wachezaji wa maonyesho wa kike na kuhusianisha jina lao na ukahaba na uasherati kulikuwa pokeo la kale, likirudi nyuma hadi siku za [Mtakatifu] Augustine na hata mapema zaidi,” aonelea mtafiti Angus Heriot. Hata hivyo, kwa kuchukua msimamo huu usionyumbuka, kanisa lilifungua njia kwa tatizo jingine zito zaidi—wakastrati!

Wakastrati walikuwa nani, na Jumuiya ya Wakristo ilijihusishaje nao?

Ulemazo kwa Ajili ya Muziki

Opera na majumba ya maonyesho ya umma yalihitaji soprano, na ndivyo ilivyokuwa na kwaya ya kipapa. Ni nini kingeweza kufanywa? Ilikuwa imejulikana kwa muda mrefu kwamba ikiwa mvulana angehasiwa, sauti yake haingekuwa nzito. Vinyuzi vya sauti hukua kidogo tu, ilhali kifua na kiwambotao hukua kikawaida. Likiwa tokeo, mkastrato ana nguvu za mwili wa mwanamume lakini ana sauti ya mvulana—“aina ya sauti ambayo malaika walifikiriwa kuwa nayo,” aeleza Maria Luisa Ambrosini katika The Secret Archives of the Vatican. Inawezekana pia kupima sauti kwa kadiri fulani kwa kutofautisha umri ambao mtoto anahasiwa.

Kanisa la Kigiriki lilikuwa limeajiri wakastrati kuwa waimbaji katika kwaya kuanzia karne ya 12 kuendelea, lakini Kanisa Katoliki ya Kiroma lingefanya nini? Je, sasa hilo pia lingeidhinisha na kuajiri wakastrati?

Padre Soto, mwimbaji katika kwaya ya kipapa mwaka 1562, anaorodheshwa katika rekodi Vatikani kuwa na sauti ya falseto. Lakini Soto alikuwa mkastrati. Hivyo angalau miaka 27 kabla ya 1589, wakati ambapo agizo la Papa Sixtus 5 lilipopanga tena waimbaji wa Basilika ya St. Peter ili kuongeza wakastrati wanne, Vatikani ilikuwa imeweka kando kimya-kimya ile mamlaka ya Baraza la Nicaea.

Tangu 1599 kuwapo kwa wakastrati katika Vatikani kulikubaliwa. Mara tu mamlaka ya juu zaidi katika kanisa ilipoidhinisha zoea hilo waziwazi, wakastrati wakakubaliwa. Gluck, Handel, Meyerbeer, na Rossini wamo miongoni mwa wale waliotunga miziki mitakatifu na ya kilimwengu kihususa kwa ajili ya wakastrati.

Kupendwa, Wazazi, na Maoni ya Wengi

Wakastrati walikuja kupendwa na wengi kwa haraka. Kwa kielelezo Papa Clement 8 (1592-1605), alivutiwa sana na unyumbufu na utamu wa sauti zao. Hata ingawa yeyote aliyejulikana kuwa na uhusiano wowote na tendo la uhasishaji alipaswa kuondoshwa kanisani, kulikuwa na mmiminiko wenye kuendelea wa wavulana wachanga kadiri mahitaji ya kimuziki ya kanisa yalivyoendelea.

Maduka yalisemekana kutangaza, “Qui si castrono ragazzi (Wavulana wanahasiwa hapa).” Duka moja la kinyozi katika Roma lilitangaza hivi kwa majivuno: “Waimbaji huhasiwa hapa kwa ajili ya kwaya za mahali pa ibada pa kipapa.” Inadaiwa kwamba katika karne ya 18, wavulana Waitalia wapatao 4,000 huenda walihasiwa kwa kusudi hilo. Haijulikani ni wangapi waliokufa wakihasiwa.

Kwa nini wazazi waliruhusu wana wao walemazwe namna hiyo? Kwa ujumla, wakastrati walizaliwa na wazazi maskini. Ikiwa mwana alionyesha kipawa chochote cha muziki, basi angeweza kuuzwa, nyakati fulani moja kwa moja kwa chuo cha kimuziki. Wengine walitolewa katika kwaya za Basilika ya St. Peter katika Roma na vitovu vingine kama hivyo vya kanisa. Kwa kawaida wazazi walitumaini kwamba mkastrati wao angekuwa mashuhuri na kuwatunza vizuri katika umri wao wa uzee.

Hata hivyo, mara nyingi sana, msiba ulifuatia wakati ilikuwa wazi kwamba huyo mvulana hakuwa na sauti ya kuweza kuzoezwa. Johann Wilhelm von Archenholz, akiandika A Picture of Italy mwishoni mwa karne ya 18, alieleza kwamba wakataliwa hao, pamoja na wakastrati wowote wa ziada, “waliruhusiwa kuwa makasisi” na kuruhusiwa kuongoza Misa. Hili lilifuata kiolezo kisicho cha kawaida kilichowekwa katika St. Peter yenyewe wakati ambapo, kwa kuvunja kanuni ya kanisa, wakastrati wawili waliruhusiwa kuwa makasisi wa Katoliki ya Kiroma katika 1599 na wengine wakafuata.

Papa Benedict 14 mwenyewe alirejezea nyuma kwa uamuzi wa Baraza la Nicaea na kukubali kwamba uhasishaji ulikuwa kinyume cha sheria. Lakini katika 1748 alipinga kwa dhati dokezo kutoka kwa maaskofu wake mwenyewe kwamba wakastrati wapigwe marufuku, kwa kuwa alihofia kwamba makanisa yangekuwa matupu ikiwa angefanya hivyo. Huo ulikuwa uvutio na umaana wa muziki wa kanisa. Kwa hiyo waimbaji wakastrati waliendelea kuimba katika kwaya za kanisa za Kiitalia, katika St. Peter, na katika Kanisa la Sistine ya papa mwenyewe.

Katika 1898 kukiwa kumejaa maoni ya wengi dhidi ya uhasishaji, Papa Leo 13 kwa utambuzi aliwastaafisha wakastrati wa Vatikani, na aliyemfuata, Papa Pius 10, alipiga marufuku wakastrati kirasmi kutoka kanisa la kipapa katika 1903. Lakini agizo la Papa Sixtus 5 ambalo liliwaingiza halijaondoshwa kirasmi.

Mkastrati wa kulipwa wa mwisho, Alessandro Moreschi, alikufa katika 1922. Mirekodio ya uimbaji wake ilifanywa katika 1902 na 1903 na yaweza bado kusikiwa. Kwenye vibandiko vya maelezo ya mirekodio hii, anafafanuliwa kuwa “Soprano della Cappella Sistina (Soprano ya Kanisa la Sistine).” “Hiyo sauti,” aandika mchambuzi wa muziki Desmond Shawe-Taylor, “ambayo ni soprano bila shaka, hufanana na sauti isiyo ya mvulana wala ya mwanamke.”

Hivyo ukaisha ulemazo wa kiholela wa wavulana kwa sababu ya sanaa. “Zoea lenye kukirihisha,” yasema The Encyclopædia Britannica, walakini lililovumiliwa na Kanisa Katoliki ya Kiroma kwa karne nyingi.

Uhasishaji—Katika Miaka ya 1990?

Kwa hiyo wakastrati hawako tena. Lakini je, hilo lamaanisha kwamba uhasishaji katika jina la dini umekwisha? Kwa kuhuzunisha, la! The Independent Magazine laripoti kwamba India ina matowashi wengi kufikia milioni moja, wanaoishi katika jumuiya za kidini. Ni akina nani hao? Wahijra.

Wahijra wengi ni Waislamu kwa kuzaliwa—ingawa kuna Wahindu wengi miongoni mwao—nao wote huabudu Bharuchra Mata, kijimungu kike cha Kihindu kutoka Gujarat. Hata ingawa wengi huchagua kuhasiwa, inadaiwa na watu fulani kwamba kila mwaka wanaume wengi mno Wahindu kufikia elfu moja wanahasiwa kinguvu ili kuwalazimisha kujiunga na wahijra, ambapo baada ya hilo wanapigwa mnada kwa mwalimu wa Kihindu mwenye kutoa pesa nyingi zaidi.

Wahijra wanaongozwa na walimu wa Kihindu wenye vyeo vya juu, mbari tofauti za wahijra zinazogawanya majiji kuwa maeneo. Wahijra huishi kwa kuomba-omba na kupiga ukahaba hekaluni. Kwa ujumla wao hudharauliwa, lakini wanahofiwa pia kwa sababu huonwa kuwa wana mizungu mibaya. Kwa sababu hii watu watawalipa ili wabariki watoto na maarusi wapya.

Inasemekana kwamba wahijra fulani hutoroka. Lakini “maharamia wahijra ambao inaripotiwa hudhibiti uhasishaji,” laripoti India Today, “hutenda kazi chini ya ufuniko wa usiri na ogofyo.”

Mwisho wa Uhasishaji!

Je, ulimwengu utapata kuwa huru kutokana na maovu kama hayo? Ndiyo, kwa sababu dhambi za milki ya ulimwengu ya dini bandia—inayotambulishwa katika Biblia kuwa kahaba, ‘Babiloni Mkubwa’—“zimefika hata mbinguni.” Jinsi inavyoimarisha imani kujua kwamba mazoea yote hayo yenye kumvunjia Mungu heshima karibuni yatafikia mwisho wenye kutazamisha! Kwa nini usisome mwenyewe jambo hili katika kitabu cha kumalizia cha Biblia, Ufunuo, sura ya 18? Tazama hasa mstari wa 2 na wa 5.

[Maelezo ya Chini]

a Kuhusu maneno ya Yesu, kielezi-chini cha Westminster Version of the Sacred Scriptures: The New Testament ya Katoliki ya Kiroma hutaarifu hivi: “Si kimwili kwa ulemazo wa viungo, bali kiroho kwa kusudi au nadhiri.” Vivyohivyo, A Commentary on the New Testament, kilichoandikwa na John Trapp, chaeleza hivi: “Haimaanishi kujihasi, kama Origen na wengine katika nyakati za kale, kwa kuelewa kimakosa maandishi haya . . . bali humaanisha kuishi wakiwa waseja, ili waweze kumtumikia Mungu wakiwa na uhuru zaidi.”

b Falseto huanzia mahali ambapo hali ya kiasili ya sauti humalizikia na yasemekana kuwa hutokezwa na kingo za vinyuzi-sauti.

[Sanduku katika ukurasa wa13]

Kiwango cha Juu Zaidi ya Vyote

Hakuna towashi aliyekubaliwa kuwa sehemu ya kutaniko la Israeli, kama Sheria ya Yehova ilivyotaarifu waziwazi. (Kumbukumbu la Torati 23:1) Chini ya Sheria hii uhasishaji haukuruhusiwa. “Sheria ya Kiyahudi,” yaonelea Encyclopaedia Judaica, “ilikirihi pasuaji hizi.” Likiwa tokeo, hakuna Waisraeli wala wakazi wageni waliofanywa kuwa matowashi kwa ajili ya utumishi katika majumba ya wafalme Waisraeli, kama wale matowashi waliotumika katika nyua nyinginezo za kifalme, kama ule wa mfalme Ahasuero wa Uajemi.—Esta 2:14, 15; 4:4, 5.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Uamuzi uliofanywa na Papa Sixtus 5 ulifungulia wakastrati njia

[Credit Line

The Bettmann Archive

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki