Ni Nani Aliye Mzazi? Ni Nani Aliye Mtoto?
MWANASAIKOLOJIA mmoja katika California, Marekani, aomboleza kuhusu kiwango ambacho mamlaka ya wazazi imemomonyoka katika miaka ya juzijuzi. “Katika ofisi yangu,” yeye aandika, “nimeshuhudia mazungumzo mengi kati ya wazazi na watoto ambayo yaliongozwa kana kwamba ni kati ya watu wazima wawili, si kati ya mtoto na mzazi. Majadiliano yanayostahili kufanywa kati ya mashirika yetu makubwa zaidi yamefanywa kuhusu kila jambo kuanzia wakati mtoto apaswa kwenda kulala hadi posho hadi madaraka ya nyumbani. Nyakati nyingine imekuwa vigumu kujua ni nani aliye mzazi na ni nani aliye mtoto.”
Biblia huandaa shauri lenye usawaziko kwa wazazi. Huwaonya kuhusu hatari ya wao kuweka masharti sana hivi kwamba wamwudhi mtoto wao, labda hata kumfanya mtoto ashuke moyo na kukata tamaa. (Wakolosai 3:21) Lakini pia yawaonya wazazi dhidi ya kupita kiasi kwa upande ule mwingine—kuwa wenye uendekevu kupita kiasi, kuachilia madaraka yao. Mithali 29:15 hutaarifu: “Mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.” Mithali nyingine ya Biblia husema: “Amwendekezaye mtumishi wake tangu ujana na kuendelea, katika maisha yake ya baadaye hata atakuwa asiye na shukrani.” (Mithali 29:21, NW) Ingawa andiko hili larejezea mtumishi, kanuni hiyo yafaa pia kwa watoto.
Wazazi wanaowanyima watoto wao uongozi na nidhamu inayohitajika hatimaye hulipa bei kubwa sana yaani, nyumba isiyoweza kuongozwa. Ni bora zaidi jinsi gani kutumia shauri la Biblia! Kweli, kufanya hivyo kwahitaji jitihada, lakini kwaweza kuleta manufaa yenye kudumu muda wote wa maisha. Biblia husema: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”—Mithali 22:6.