Sababu kwa Nini Nyota Haziwezi Kuonekana
NI NANI ambaye hajakodoa macho kwenye anga ya usiku na kustaajabia uzuri wenye kumetameta wa nyota zisizohesabika zinazoenea mbali zaidi kwenye anga? Hata hivyo, mwono huu wenye kutia kicho unatoweka polepole kutoka machoni petu. Kwa nini? Uchafuzi wa nuru.
Uchafuzi wa nuru ni mwako wenye nguvu nyingi, wenye kupofusha unaotokezwa na nuru bandia za barabarani, nyumbani, majengo ya biashara, majengo ya umma na nyanja za michezo. Nusu ya nuru hii huenea juu kwenye anga, ikibiza mwono wetu wa nyota zilizo nyingi. Tatizo hili ni zito kadiri gani? Kwa kielelezo, katika usiku ulio mwangavu, katika kaskazini mwa Ulaya, bila msaada wa kifaa chochote jicho laweza kuona karibu nyota 2,000. Lakini idadi hii hupungua kufikia 200 kwa wale wanaoishi kwenye vitongoji vya mji, na katikati ya jiji lililo na nuru yenye kung’aa sana, mtu aweza kuona nyota 20 tu. Waastronomia fulani wanahofu kwamba isipokuwa kuwe na tahadhari, hakuna nyota zitakazoonekana kaskazini mwa Ulaya katika miaka 25 ijayo.
Bila shaka, nuru fulani ni muhimu. Inazuia uhalifu na kuwafanya wenye nyumba wanaoweza kushambuliwa kwa urahisi wajihisi wakiwa salama zaidi. Hata hivyo, nuru nyingi mno yenye kupenya, huchangia mkazo na kuvuruga taratibu za usingizi. Si wanadamu tu wanaoathiriwa na nuru hii. Ndege-wahamaji na wadudu wanaweza kukanganywa na nuru, na taratibu za kiasili za mimea zaweza kuvurugwa.
Lakini ni jambo gani linaloweza kufanywa ili kupunguza tatizo hilo? Hatua moja ya maana ni kuhakikisha kwamba nuru ya nje imetiwa kivuli cha kufaa na kupindwa kuelekea upande wa chini. Taa za usalama zaweza kutengenezwa zikiwa na kifaa kinachotambua mabadiliko fulani, badala ya kuwaka daima. Kiunga kimoja cha Ufaransa kilishinda tatizo hili kwa kuanzisha taa za nje zenye mvuke wa sodiamu, ambazo hutokeza mmuliko ulioelekezwa sawasawa, na kwa kuweka vifuniko kwenye taa za barabarani zisizo na nuru nyingi, zikielekeza nuru upande wa chini. Barabara zilisakifiwa tena kwa lami nyeusi yenye kufyonza nuru, na taa zilizimwa katika majengo ya umma baada ya saa 5:00 usiku. Jambo hili halikuondoa kabisa tu uchafuzi wa nuru iliyo wima na kupunguza nuru iliyoakisiwa kwa thuluthi mbili bali ufanisi wa nishati uliongezwa kwa kiwango cha asilimia 30.
Bila shaka, utatuzi kama huo huhitaji pesa na wakati—vitu vyenye thamani visivyopatikana kwa urahisi siku hizi. Jinsi ilivyo vizuri kujua kwamba karibuni serikali ya Ufalme wa Mungu kupitia kwa Mwana wake, Kristo Yesu, itaondoa aina zote za uchafuzi! Kisha raia wake kwa mara nyingine tena wataweza kuona waziwazi kazi ya mikono ya Muumba wetu, mbingu maridadi zenye nyota nyingi.—Zaburi 19:1, 2; Ufunuo 11:18.