Mbayuwayu Mwenye Kuruka kwa Kasi
NA MLETA-HABARI WA “AMKENI!” KATIKA KENYA
MOJAWAPO WA VIUMBE HAI wenye kwenda kwa kasi sana duniani huruka hewani kwa mabawa yenye umbo la mundu. Ni ndege mdogo mwenye uzito wa gramu chache tu, ila anaweza kuruka angani kwa mwendo wa kasi sana. “Mbayuwayu huruka angani kwa mwendo wa zaidi ya kilometa 160 kwa saa,” chataarifu The Encyclopedia Americana.
Mbayuwayu huonekana wakipuruka angani kwa wepesi mno wanapopaa juu ya nchi, wakipiga kona na kujipinda kwa mwendo wa kufa na kupona wanapowinda wadudu. Mbayuwayu hupuruka hewani kwa muda mrefu zaidi kuliko ndege wengine, huku wakitafuta chakula, kula, kunywa, kukusanya vifaa vya ujenzi wa viota, na hata kujamiiana hewani. Wao huruka angani kwa muda mrefu sana hivi kwamba watazamaji fulani katika nyakati za kale waliamini kwamba mbayuwayu huishi mbinguni, mahali fulani pasipoonekana mawinguni. Mbayuwayu fulani huweza kuruka hewani kwa muda wa karibu miezi tisa kwa mwaka. Yaonekana ndege hao wadogo wenye kushangaza hata hulala wanaponyiririka hewani!
Wamebuniwa kwa Kusudi la Kuruka
Mbayuwayu ni maajabu ya ubuni wa elimu ya mwendo hewani. Wao huwa na mabawa mepesi yenye umbo la hilali yenye kujipinda nyuma ili kuondoa mbururo unaopunguza mwendo wa ndege wengi. Wawapo hewani, wao huchapuka kwa kupigapiga mabawa yao haraka-haraka japo kwa wepesi huku wakinyiririka mara kwa mara.
Uwezo wao usio wa kawaida wa kubadili mwendo angani unasababishwa kwa sehemu na uwezo wao wa kupigapiga bawa moja kwa kasi zaidi ya bawa jingine. Mpigo unaotofautiana wa mabawa humwezesha mbayuwayu apige kona kali pasipo kupunguza mwendo. Hili huwawezesha waruke kwa kasi sana wanapojipinda na kuwapita wadudu wanaoruka kisha huwabamba kwa vinywa vyao vilivyo wazi. Mbayuwayu hulazimika kula wadudu wengi sana ili waweze kupata nishati nyingi inayohitajiwa kwa ajili ya mwendo wao wa kasi. Wapurukaji hawa hodari huweza kusafiri mamia ya kilometa kila siku wanapowinda wadudu.
Umbo duni la mbayuwayu huficha umahiri wao wa kuruka angani. Mbayuwayu wa kiume na wa kike hawavutii, wengi huwa wa rangi ya kijivu au ya kikahawia isiyomeremeta. Mbayuwayu wa jamii mbalimbali hupatikana kotekote ulimwenguni hasa katika maeneo ya kitropiki na yaliyo karibu na tropiki. Wakati wa majira ya baridi kali wale wanaoishi katika Kizio cha Kaskazini huhama kwa maelfu ya kilometa hadi kwenye maeneo yenye joto.
Viota vya Gundi
Mbayuwayu hujenga viota vyao kwa kutumia kifaa cha ujenzi kisicho cha kawaida—mate yao! Wakiwa na tezi mate za pekee, wanaweza kutokeza kiasi kikubwa sana cha mate ambayo hushikanisha vifaa vya viota.
Ni nadra sana kwa mbayuwayu kutua kwenye nchi tambarare, na hawawezi kutua juu kama ndege wengineo. Miguu yao ina nyayo ndogo zenye umbo la kulabu na ni fupi sana hivi kwamba haziwezi kuwainua juu vya kutosha kuweza kupuruka mara moja. Lakini, nyayo zao zinafaa katika kujishikilia kwenye sehemu zilizo wima, kama vile magenge, mapango, na kuta za majengo. Wakati wa kujenga kiota unapowadia, mbayuwayu hushindwa kukusanya matawi, vijiti, au matope, kama ndege wengine. Yeye hutumia njia tofauti.
Mbayuwayu aina ya chimney hukusanya vitawi vidogo kwa kuruka mbio kati ya matawi ya miti, hunyakua kitawi, na kukikata kwa nguvu anapopita kwa kasi. Kisha hushikanisha vitawi hivyo pamoja, na kuviunganisha kwa mate yake yenye kunata kwenye sehemu iliyo wima. Mbayuwayu-kijivu wa Marekani huruka hewani kwa uhodari akichopoa nywele, manyoya, vipande vya pamba na vitu vingine vyepesi vinavyoelea, ambavyo huvitumia pamoja na mate yake kujenga kiota.
Aina nyingine ya mbayuwayu huitwa kwa kufaa mbayuwayu mdogo mwenye kiota kinacholiwa. Kiota chake karibu chote hujengwa kwa mate yake tu yenye kunata kwa nguvu. Kwa karne nyingi mate ya kujenga viota hivyo yamekuwa kiungo muhimu cha mchuzi mtamu wa kiota cha ndege unaopendwa huko Mashariki. Imeripotiwa kwamba kila mwaka mamilioni ya viota hutumiwa kutayarisha mchuzi huo bora.
Mojawapo ya viota vyenye kuvutia zaidi hufanyizwa kwa mate yanatayo kama gundi ya mbayuwayu-kijivu wa Afrika. Ndege huyo mdogo mno hugandisha manyoya membamba chini ya kuti la mnazi. Kwa kawaida kiota hicho kinachoning’inia hupeperushwa huku na huku na upepo. Yai lake dogo hubakije ndani ya kiota? David Attenborough, katika kitabu chake Trials of Life, aeleza: “Huenda likaonekana kuwa jambo lisilowezekana kwa yai moja kubaki ndani ya kiota hicho kidogo. Kwa kweli, lingeanguka hakika kama huyo ndege hangenatisha kiota kwenye kuti na yai kwenye kiota.” Ndege wazazi hushikilia kwa nguvu ubavu wa kiota kwa kucha zao na huatamiza yai hilo kwa zamu kwani kiota na yai vimegandishwa imara kwenye kuti la mnazi. Baada ya kinda kuanguliwa, hujishikilia kwenye kiota chake kinachopeperushwa na upepo hadi linapomea manyoya ya kuruka na kisha hupuruka mbali.
Ni tamasha ya kupendeza kuona maelfu ya mbayuwayu wakiruka angani na kuzunguka-zunguka kwa kasi sana, wakilia kwa sauti nyororo kana kwamba kwa msisimuko. Anapowatazama akiwa chini, mtu hupatwa na hisia ya kicho kwa ajili ya uhuru wao wa kuruka na pia uthamini kwa sababu ya uzuri wa ubuni wao wa kiakili. Kwa kweli, ni rahisi kuelewa kwa nini wanasarakasi hawa wa angani, wakiwa wepesi na wenye mwendo wa kasi, wanastahili kwa kweli kuitwa swift (wenye mbio) katika Kiingereza!
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mbayuwayu wa Alpine
Mbayuwayu aitwaye “Common European”
[Hisani]
Animals/Jim Harter/Dover Publications, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mbayuwayu aina ya chimney
[Hisani]
© Robert C. Simpson/ Visuals Unlimited
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
© D. & M. Zimmerman/VIREO