Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 2/11 kur. 3-4
  • Ni Nini Huwafanya Watu Wavutiwe na Uchawi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ni Nini Huwafanya Watu Wavutiwe na Uchawi?
  • Amkeni!—2011
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Nini Niepuke Mafumbo ya Kiuchawi?
    Amkeni!—1991
  • Ni Nani Chanzo Halisi cha Uchawi?
    Amkeni!—2011
  • Kuna Hatari Gani Kujihusisha Kidogo Tu na Mambo ya Mizungu?
    Amkeni!—2002
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2011
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2011
g 2/11 kur. 3-4

Ni Nini Huwafanya Watu Wavutiwe na Uchawi?

HUENDA jibu la swali hilo likategemea kwa kiasi kikubwa mahali mtu anapoishi, na pia imani yake ya kidini pamoja na malezi. Ni nini huwafanya watu katika eneo lenu wavutiwe na uchawi? Huenda wakavutiwa na moja ya sababu zifuatazo.

● Udadisi Wanadamu wamezaliwa wakiwa wadadisi, na uchawi ni moja kati ya mambo yanayochochea udadisi wao. Kwa hiyo, watu fulani wangependa kujua ikiwa kuna nguvu iliyofichika inayoongoza uchawi. Wengine huwaendea wachawi ili wajue ni nani wanaowaloga na wengine husimama barabarani kuwatazama watu wanaofanya miujiza. Huenda hata wengine wakahudhuria mkutano wa kuwasiliana na pepo.

● Burudani Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la ghafula katika burudani—vitabu, sinema, na michezo ya kompyuta—kuhusu uchawi na ushirikina wa dini za kipagani za kale. Pia, baadhi ya burudani hizo huonyesha jeuri na ngono waziwazi.

● Mahangaiko kuhusu wakati ujao Biblia ilitabiri hivi: “Katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” (2 Timotheo 3:1) Kwa kweli tunaishi katika siku za mwisho, na watu wengi wanawatembelea watu wanaofanya mambo ya uchawi—kama vile, viongozi wa kidini wanaodai kuzungumza na Mungu na wachawi wanaodai kuwa wanaweza kufanya uaguzi—ili kupata mwongozo. Mtu fulani ambaye husoma akili za watu alisema: “Hii ni moja kati ya biashara chache ambazo haziathiriwi na kuporomoka kwa uchumi. Kwa kawaida watu hawaji kukuona wanapokuwa na furaha.” Mbashiri mmoja huko Kanada alisema: “Siku hizi mimi hupigiwa simu na wafanyabiashara mashuhuri ambao hupendelea kuzungumza kupitia simu zao za kibinafsi kazini au kupitia simu zao za mkononi nao hunong’oneza wanapozungumza wakiwa nje ya ofisi zao.” Pia aliongeza hivi: “Hawa ni watu ambao, awali walikuwa na shaka kuhusu kumwendea mtu anayesoma akili za watu.”

● Magonjwa Mara nyingi katika nchi fulani wagonjwa wengi wanaougua sana huacha matibabu ya hospitali na kutafuta msaada kutoka kwa waganga wa kienyeji wanaotumia uchawi. Huenda wakaambiwa kuwa wao ni wagonjwa kwa sababu wamelogwa. Ili kumsaidia mtu aliyelogwa, huenda marafiki au watu wa familia wakatafuta msaada kutoka kwa mchawi ambaye huenda akawaambia walipe kiasi kikubwa cha pesa.

● Kutafuta ulinzi na bahati njema Katika maeneo fulani ya Afrika, wanakijiji hutafuta “nabii” wa kanisa lenye uvutano mkubwa au mchawi ili afukuze roho waovu kutoka katika jamii. Desturi hizo hutia ndani kunywa michanganyiko fulani na “maji matakatifu.” Kwingineko pia watu hutumia wachawi ili kuleta bahati katika nyumba mpya au kaburi kwa kuwa inaaminiwa kwamba roho za wafu zinaweza kuwaletea bahati.

● Kuwalinda watoto Huko Papua New Guinea, huenda mama akakataa kutoka nje usiku akiwa na mtoto wake mchanga. Kwa nini? Anahofu kwamba huenda roho waovu wakamdhuru mtoto wake. Huko Uganda, ni kawaida kwa akina mama kuwafunga watoto wao hirizi mikononi na miguuni, ambazo wakati mwingine huwa zimetengenezwa kwa makoa na shanga, ili kuwalinda kutokana na madhara.

● Kifo cha mpendwa Mwandikaji Mwingereza Sir Arthur Conan Doyle aliwapoteza mwana, kaka, ndugu-mkwe, na mpwa wake wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Akiwa amehuzunika sana, Doyle pamoja na mke wake walienda kwenye mikutano ya kuwasiliana na pepo wakiwa na matumaini ya kuzungumza na mwana wao aliyekufa. Leo pia, watu wengi huwaendea watu wanaowasiliana na pepo wakiwa na matumaini ya kuzungumza na wapendwa wao waliokufa. Katika nchi fulani, dini za kienyeji pamoja na zile zinazodai kuwa za Kikristo hufundisha kwamba kifo husababishwa na roho waovu waliokasirika. Makanisa hayo hudai kwamba lazima watu wafanye matambiko fulani ambayo hugharimu pesa nyingi sana ili watu zaidi katika jamii wasife.

● Kuwahofu wafu Imani kuhusu kifo na wafu imewaathiri sana wanadamu. Kwa hiyo, katika nchi nyingi watu hufanya matambiko ya kila aina yanayotia ndani kuwa na karamu mwaka mmoja baada ya mtu kufa, kufagia boma lote la aliyekufa, kunyoa nywele zote, na pia kujiumiza, ili wawafurahishe wafu au “kuthibitisha” kwamba wanawapenda. Jamii fulani katika visiwa vya Pasifiki huwalazimisha wajane kuvaa mavazi meusi na kuomboleza kwa miezi mingi, wakiwa wamejifungia ndani ya nyumba na bila kula vyakula ambavyo mpendwa wao aliyekufa alipenda sana. Watu wanaojihusisha na desturi hiyo wanaweza kushuka moyo au kupata magonjwa yanayoletwa na njaa au hata kufa.

Ni wazi kwamba kuna mambo mengi yanayowavutia watu kufanya uchawi. Hivyo, ni jambo la maana tuelewe chanzo halisi cha mafundisho kuhusu uchawi! Acheni sasa tuchunguze Biblia, kwa sababu ndicho kitabu pekee kinachoeleza wazi kuhusu uchawi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki