Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • gt sura 100
  • Kielezi cha Zile Mina

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kielezi cha Zile Mina
  • Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Habari Zinazolingana
  • Kielezi cha Zile Mina
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Mfano wa Mina Kumi
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Waokolewa Wasichinjwe Pamoja na Adui za Mfalme
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Kupata Utajiri kwa Ajili ya Mfalme Mpya wa Dunia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
Pata Habari Zaidi
Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
gt sura 100

Sura 100

Kielezi cha Zile Mina

LABDA Yesu angali nyumbani mwa Zakayo, ambako amesimama akiwa njiani kwenda Yerusalemu. Wanafunzi wake waamini kwamba wafikapo Yerusalemu, yeye atajulisha wazi ndiye Mesiya na kuanzisha Ufalme wake. Ili asahihishe wazo hili na kuonyesha kwamba Ufalme ungali mbali, Yesu atoa kielezi.

“Mtu mmoja, kabaila,” yeye asimulia, “alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.” Yesu ndiye huyo “kabaila,” na mbinguni ndiko “nchi ya mbali.” Yesu awasilipo huko, Baba yake atampa mamlaka ya kifalme.

Hata hivyo, kabla ya kuondoka, kabaila huyo aita watumwa kumi na kumpa kila mmoja wao fungu la fedha [mina ya fedha, NW], akisema: “Fanyeni biashara hata nitakapokuja.” Watumwa kumi hao katika utimizo wa kwanza wawakilisha wanafunzi wa mapema wa Yesu. Katika utumizi uliopanuliwa, wao wafananisha wote wenye kutazamiwa wawe pamoja naye katika Ufalme wa kimbingu.

Zile mina za fedha ni vipande vya pesa vilivyo na thamani kubwa, kila kimoja kikiwa ni mshahara wa miezi mitatu hivi kwa mkulima. Lakini mina hizo zawakilisha nini? Na watumwa hao wapaswa kufanya nazo biashara ya aina gani?

Mina hizo zawakilisha mali zenye thamani ambazo wanafunzi wapakwa-mafuta kwa roho wangeweza kutumia ili watokeze warithi zaidi wa Ufalme wa kimbingu mpaka wakati wa kuja kwa Yesu akiwa Mfalme katika Ufalme ulioahidiwa. Baada ya yeye kufufuliwa na kuwatokea wanafunzi wake, aliwapa zile mina za ufananisho ili zitumiwe kufanya wanafunzi zaidi na kuongezea hivyo ile jamii ya Ufalme wa mbinguni.

“Lakini,” Yesu aendelea, “watu [raia, NW] wa mji wake walimchukia [kabaila huyo], wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatutaki huyu atutawale.” Raia hao ni Waisraeli, au Wayahudi, bila kuwahusisha ndani wanafunzi wake. Baada ya Yesu kuondoka kwenda mbinguni, Wayahudi hawa kwa kuwanyanyasa wanafunzi wake walijulisha kwamba hawakumtaka yeye awe mfalme wao. Kwa njia hii walikuwa wanatenda kama raia waliotuma wale wajumbe.

Wale watumwa kumi watumiaje mina zao? Yesu aeleza hivi: “Ikawa aliporudi ameupata ufalme wake, aliamuru waletwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. Akaja wa kwanza, akasema Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lili dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limepata mafungu matano ya faida. Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.”

Mtumwa yule mwenye mina kumi hufananisha jamii, au kikundi kimoja, cha wanafunzi kuanzia Pentekoste 33 W.K. mpaka sasa ambacho chatia ndani mitume. Yule mtumwa aliyepata mina tano pia awakilisha kikundi kimoja katika kipindi kile kile, kikundi ambacho kinaongezea mali za mfalme wao duniani kulingana na fursa zao na uwezo mbalimbali. Vikundi vyote viwili vinahubiri habari njema kwa bidii, na tokeo ni kwamba watu wengi wenye mioyo ifaayo wapata kuwa Wakristo. Tisa kati ya watumwa hao walifanya biashara yenye mafanikio wakaongezea mali walizomiliki.

Lakini, Yesu aendelea kusema, “akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso. Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi [mina kumi, NW].”

Kwa mtumwa huyo mwovu, kupoteza mina ya ufananisho kwamaanisha kupoteza fursa ya kuwa katika Ufalme wa kimbingu. Ndiyo, yeye apoteza pendeleo la kutawala, kana kwamba, ni juu ya majiji kumi au matano. Angalia, pia, kwamba mtumwa huyo hatangazwi kuwa mwovu kwa ubaya wowote afanyao, bali ni kwa kutofanya kazi aongezee utajiri wa ufalme wa bwana wake.

Wakati mina ya mtumwa mwovu ipewapo kwa mtumwa wa kwanza, upinzani huu wafanywa: “Bwana, anayo mafungu kumi.” Hata hivyo, Yesu ajibu: “Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho. Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.” Luka 19:11-27; Mathayo 28:19, 20.

▪ Ni nini chafanya Yesu atoe kielezi chake juu ya zile mina?

▪ Yule kabaila ni nani, na ni nchi gani aendako?

▪ Wale watumwa ni akina nani, na ni nini kinachowakiliswa na zile mina?

▪ Wale raia ni akina nani, nao waonyeshaje chuki yao?

▪ Kwa nini mtumwa mmoja aitwa mwovu, na kupoteza mina yake kwamaanisha nini?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki