Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w74 6/1 kur. 247-253
  • Kupata Utajiri kwa Ajili ya Mfalme Mpya wa Dunia

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kupata Utajiri kwa Ajili ya Mfalme Mpya wa Dunia
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MFANO
  • “FANYENI BIASHARA MPAKA NITAKAPORUDI”
  • Waokolewa Wasichinjwe Pamoja na Adui za Mfalme
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Mfano wa Mina Kumi
    Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Kielezi cha Zile Mina
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Kielezi cha Zile Mina
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
w74 6/1 kur. 247-253

Kupata Utajiri kwa Ajili ya Mfalme Mpya wa Dunia

“Upendeleo wa mfalme humwelekea mtumwa atendaye kwa busara; bali ghadhabu yake itakuwa juu yake aletaye aibu.”​—Mit. 14:35.

1. Ni mwanamume wa namna gani aliyesema maneno yaliyoamuru adui wachinjwe na mfalme katika mfano wa unabii?

“TENA, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.” Maneno hayo ya mfalme yapaswa kutia hofu mioyoni mwa wale ambao kwao yalielekezwa! Lakini n’nani aliyeyasema maneno hayo? Alikuwa ni mwanamume ambaye huenda watu walio wengi wakafikiri asingeweza hata kidogo kutoa agizo hilo kali sana. Yeye alionyesha maneno hayo yalisemwa na mfalme ambaye alikuwa akizungumza juu yake katika mfano wa unabii wake. Lakini kwa kweli alikuwa akijisemea mwenyewe, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye aliyefananishwa na mfalme huyo katika mfano huo.​—Luka 19:27.

2. (a) Wakati huo, Yesu alikuwa akielekea wapi, akafanye nini? (b) Alipokuwa akishuka katika Mlima wa Mizeituni, ni unabii gani juu ya Yerusalemu alioutaja Yesu?

2 Wakati huo, Yesu Kristo alikuwa katika mji wa Yeriko, karibu maili kumi na nne mashariki ya kaskazini ya Yerusalemu, nao mwezi wa masika wa Nisani ya mwaka wa 33 C.E. ulikuwa ukianza. Yesu alikuwa ameuvuka Mto Yordani naye akaingia Yeriko, ambapo alikaa usiku huo. Alikuwa akielekea Yerusalemu, akapande kwa ushindi kuingia katika mji mtakatifu Jumapili, Nisani 9, siku tano mbele ya sikukuu ya kupitwa ya Kiyahudi. Ulikuwa ni wakati wa kupanda huku kwa ushindi kwamba akayasimamisha maandamano ya wanafunzi wake walipokuwa wakishuka chini ya Mlima wa Mizeituni naye akatiririsha machozi kwa ajili ya mji wa Yerusalemu, akisema: “Laiti ungalijua, hata wewe, katika siku hii, yapasayo amani! lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.”​—Luka 19:41-44.

3. Ni wakati gani machinjo yaliyotabiriwa hivyo na Yesu yalipotokea, na kwa kadiri gani?

3 Hivyo je! Yesu alikuwa akisimulia namna ambavyo mfalme wa mfano wa unabii angewafanya adui zake wachinjwe kwa sababu ya kutomtaka yeye kama mfalme wao? Kama mambo yalivyotukia, mji wa Yerusalemu haukumkaribisha Yesu Kristo kama Mfalme alipokuwa akipanda kwa ushindi kuingia katika huo. Zilipopita siku tano, au katika Siku ya Kupitwa, adui katika Yerusalemu walimfanya Yesu auawe kama mhalifu aliyelaaniwa juu ya mti nje ya kuta za mji. Adui walipinga kwa nguvu kwa maana Gavana wa Kirumi Pontio Pilato aliandika mwandiko juu ya mti, ukitangaza katika Kiebrania, Kirumi na Kigiriki: “YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI.” (Yohana 19:17-22) Wao hawakumtaka mwanamume ambaye walimshtaki juu ya kuwa mkufuru Mungu wao na mfitini juu ya Rumi wa kifalme aitwe Mfalme wao. Miaka 33 ilipopita wakati wao wenyewe walipouasi Rumi, haikuwa ni kwa kumkubali Yesu kama Masihi wao na Mfalme, bali kwa kuzikubali nia zao za Kimasihi za kujitakia makuu. Katika mwaka wa tano wa uasi wao juu ya Rumi, yalifika machinjo yenye kuogofya yaliyotabiriwa na Yesu. Mnamo mazingiwa ya Kirumi na uharibifu wa Yerusalemu, Wayahudi milioni moja na mia moja elfu wenye kuasi walipoteza maisha zao, wakiokoka 97,000 peke yao na kuelekezwa utumwani.

4. (a) Machinjo hayo katika Yerusalemu yalifananisha nini? (b) Ni kwa kufanya nini sasa tunavyoweza kuokoka machinjo hayo?

4 Lakini, kufuata uharibifu huo wa Yerusalemu na hekalu lake ulioletwa na Warumi katika mwaka wa 70 C.E., Yesu Kristo hakuuamuru ufalme wake kwa nguvu juu ya Wayahudi wenye kuokoka ama katika nchi ya Palestina ama katika sehemu nyingine yote ya dunia inayokaliwa na watu. Milki ya Kirumi iliendelea kulishika eneo la Palestina kwa karne nyingi nyumaye. Kwa wazi, basi, machinjo ya Wayahudi wenye kumpinga Kristo katika Yerusalemu yaliyoletwa na Warumi katika mwaka wa 70 C.E. yalikuwa mfano tu wa machinjo kwa kadiri kubwa zaidi, kwa kadiri ya ulimwenguni pote, ya wale wote walioko duniani wasiomtaka Yesu Kristo kama mfalme mpya wa dunia wakati wa kuja kwake kwa mara ya pili. Kwa hiyo wakati ungali utakuja​—lakini unakaribia sana​—ambapo, katika utimizo wa mfano wake, Yesu Kristo aliyefufuliwa na kutukuzwa atawaamuru malaika wake wa kimbinguni wakawalete adui zake walioko duniani mbele yake na kuwachinja kama adui wasiopatanishwa wa ufalme wake. Hii yamaanisha kwamba sisi leo twaishi katika wakati wenye hatari nasi twahitaji kujua kama tu adui za ufalme wake au sivyo. Kwa kuchukua msimamo ufaao sasa twaweza kuokolewa kutoka machinjo yajayo.

MFANO

5, 6. Wanafunzi wa Yesu walikuwa wakimtazamia akafanye nini Yerusalemu, na kwa hiyo kwa nini yeye akawapa mfano?

5 Kama msaada wa kutuelekeza katika kuuchukua msimamo ufaao sasa, yatupasa tuchunguze na kuipata maana ya mfano wote uliotolewa na Yesu Kristo huko Yeriko katika masika ya mapema ya mwaka wa 33 C.E. Kama matokeo ya ziara ya Yesu katika nyumba ya mkuu wa watoza kodi katika Yeriko, mwanamume huyu Zakayo aliyedharauliwa alikuwa amekwisha mwamini Yesu kama Masihi wa Kiyahudi au Kristo. (Luka 19:1-10) Kwa kuwa Yesu aliazimia kupanda Yerusalemu, wanafunzi wake walifikiri kwamba alikuwa akienda akajitangaze mwenyewe kama Masihi Yerusalemu na kuurudisha ufalme kwa taifa la Israeli, akiwanyang’anya Warumi wa kifalme utawala. Ili kuyaondoa maoni haya yenye makosa katika akili za wanafunzi wake, Yesu Kristo aliutoa mfano kuonyesha kwamba ufalme wake ulikuwa mbali.

6 Juu ya hili twasoma: “Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila (mwanamume wa uzaliwa ulio bora, NW), alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.”​—Luka 19:11, 12.

7. (a) Katika mfano huo, Yesu alionyeshaje kwamba kujipatia na kuutumia uwezo wa kifalme vingechukua wakati mrefu tangu wakati huo? (b) Yesu alikuwa “kabaila” wa kweli namna gani?

7 Kwa njia hii Yesu alidokeza kwamba yeye hakuwa na uwezo wa kifalme bado, lakini kwamba ilimpasa kusafiri mbali akajipatie huo. Kwa sababu ya utaratibu unaopaswa wa kusafiri miaka 1,900 iliyopita, safari ya mahali pa mbali kisha safari ya kurudi ingeonyesha kupita kwa kipindi kirefu cha wakati. Yesu hakuwa akisafiri kwenda mahali pa karibu kama Yerusalemu, maili kumi na nne kutoka Yeriko, akajipatie uwezo wa kifalme aliokuwa amehesabiwa kuupata kwa sababu ya ukabaila wake. (Luka 19:12, Jerusalem Bible; New American Bible; New English Bible; New World Translation) Ajapokuwa Yesu alikuwa amekuwa seremala wa vivi hivi katika mji wa Nazareti, hata hivyo alikuwa mtu mwenye cheo kweli kweli au “kabaila.” Alikuwa mzao wa asili wa Mfalme Daudi, ambaye mji wake mkuu ulikuwa umekuwa Yerusalemu. Akiwa mtu kama huyo, alihesabiwa kuurithi ufalme wa Daudi juu ya Israeli yote, Yerusalemu ukiwa mji wake mkuu. Yesu alikuwa amefanya miujiza mingi kwa uwezo wa Mungu, na sasa wanafunzi wake walifikiri kwamba “ufalme wa Mungu” wa Kimasihi ungejitokeza kwa njia ya mwujiza kwa kumfanya Yesu Mfalme mwenye kushikilia cheo juu ya Israeli kujapokuwa kukaliwa kwa nchi na Warumi. Hivyo ufalme wa Mungu wa Kimasihi ungeweza kusimamishwa mara hiyo. Lakini Yesu alijua kwamba Ufalme haukuwa karibu sawa na wakati ambao ingemchukua kufika Yerusalemu.​—Luka 3:23-31; Mt. 1:1-17.

8, 9. (a) Je! wakati uliopaswa ndio kadiri ya wakati uliotumiwa kusafiri kwenda Rumi na kurudi, na kwa sababu gani sivyo? (b) Katika maneno yake kwa Mfalme Sedekia wa Yerusalemu, Yehova alionyeshaje kwamba ndiye Yeye aliyepaswa kutoa uwezo wa kifalme?

8 Wala wakati uliopaswa haukuwa wakati uliotumika kusafiri kutoka Palestina kufika Rumi wa kifalme katika Italia kisha kurudia Yerusalemu. Rumi hapakuwa mahali alipopaswa Yesu Kristo kuupata uwezo wake wa kifalme. Chanzo cha uwezo wake wa kifalme hakikuwa Kaisari wala Taifa la Kirumi. Uhakika wenyewe ulionyeshwa wazi wakati ambapo askari za Kirumi walimtundika mtini Siku ya Kupitwa kama mdai mwenye fitina wa ufalme. Mahali pa mbali alipopaswa Yesu kusafiri akaupate uwezo wa kifalme palikuwa ndipo mahali pa Yeye ambaye alikuwa ameusimamisha ufalme wa Kimasihi wa babu yake Yesu Daudi. Huyo alikuwa Yehova Mungu, napo mahali pake palikuwa mbinguni. Yehova alionyesha kwamba Yeye Ndiye aliyepaswa kuuweka uwezo wa kifalme juu ya mzao aliyestahili wa Mfalme Daudi, alipomwambia Mfalme Sedekia wa Yerusalemu hivi, muda mfupi mbele ya kuvuliwa taji kwake katika mwaka wa 607 B.C.E.:

9 “Kiondoe kilemba [cha kifalme], ivue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka. Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa.”​—Eze. 21:26, 27.

10. Kwa nini Yesu hakuwa akijiona ama kujitanguliza kwa kumwiga kabaila na kufunga safari ndefu akajipatie uwezo wa kifalme?

10 Yesu Kristo hakuwa akijiona ama kujitanguliza alipoazimia kumwiga kabaila wa mfano na kwenda safari ambayo ingeelekea kumaliza wakati mwingi sana akajipatie ufalme. Mbele tu ya kuchukuliwa katika tumbo la uzazi la mama yake wa kidunia Mariamu wa nyumba ya kifalme ya Daudi, malaika Gabrieli alisema hivi juu ya mwana wake ambaye angemwita Yesu: “Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na [Yehova] Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” (Luka 1:31-33) Sasa ilihitaji mwujiza wa kimungu ili uhai wa Mwana huyu wa Aliye Juu Zaidi Sana uhamishwe mbinguni kuletwa duniani. Kwa hiyo, sasa, ilimpasa Yesu Kristo kurudia mbinguni akajipatie ufalme wa mfano wa ule wa Daudi kwa Baba yake wa kimbinguni kwa njia gani?

11, 12. (a) Ni kwa mwujiza gani alivyowezeshwa Yesu kuifunga safari ndefu ya mahali pa kupatia uwezo wa kifalme? (b) Kwa sababu gani ufufuo huo wa Yesu si makisio yetu juu ya shauri hili?

11 Kanuni ya kimungu imeandikwa kwa njia isiyogeuka: “Nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu.” (1 Kor. 15:50) Kwa wazi, basi, ilipaswa kuwa kwa njia ya mwujiza mwingine kwamba Yesu Kristo angesafiri kurudia mbinguni kwenye Mwenye Mamlaka Kuu Zaidi Sana ambaye angeweza kumpa Ufalme. Kwa wazi ingemlazimu Yesu kuweka “nyama na damu” yake kando. Hii ingemhitaji kuutoa uhai wake mkamilifu wa kibinadamu bila ya hatia kama dhabihu ya kibinadamu. Lakini kifo hiki cha dhabihu kisingemweka yeye mbinguni. Ingemlazimu Mungu kumrudisha Mwana wake aliyetolewa dhabihu kwenye uzima tena, lakini siyo kama Mwana wa “nyama na damu” tena. Ilipaswa kuwa kama Mwana mwenye mwili wa kiroho, asiyeonekana kwa macho ya kibinadamu lakini anayeonekana kwa macho ya kimbinguni. Kwa hiyo hii ingemhitaji Mungu Mwenye Nguvu Zote Yehova si afanye mwujiza wa kumfufua tu Mwana wake aliyetolewa dhabihu bali vile vile amfufue kama mtu wa kiroho, akiwa na thawabu iliyoahidiwa ya kutokufa na kutokuharibika. Lili hili ndilo Yehova alilolifanya. Haya siyo makisio yetu, bali mtume Petro anaandika:

12 “Kristo pia alifia dhambi mara moja kwa ajili ya wote, wenye haki kwa wasio haki, kwamba aweze kutuleta sisi kwa Mungu, akiuawa katika mwili lakini akiuhishwa katika roho; kisha akaenda na kuzihubiria roho zilizomo kifungoni.”​—1 Pet. 3:18, 19, Revised Standard Version ya mwaka wa 1952.

13, 14. (a) Yesu alipokufa kama mtu mwenye “nyama na damu,” yeye alikwenda wapi? (b) Twajuaje kama Yesu alipokwisha kufufuliwa alianza mara hiyo safari yake ya “nchi ya mbali” ya mfano au sivyo?

13 Bila shaka, wakati wa kufa kwa Yesu kama mtu mwenye “nyama na damu,” hakwenda “nchi ya mbali” ya mfano, yaani, mbele za Baba yake mbinguni. Alikuwa amekufa kweli, nao mwili wake uliwekwa kaburini, hivi kwamba, kwa vipindi vya siku tatu, Yesu alikuwamo katika ile waliyoiita Wayahudi Sheol na waliyoiita Wagiriki Haʹdes. Wakati wa ufufuo wake kama mtu wa kiroho siku ya tatu, Yesu alikuwa nao ubora au ustahili wa uhai wake wa kibinadamu uliotolewa dhabihu, lakini hakuanza kusafiri mara hiyo kwenye “nchi ya mbali.” Siku iyo hiyo alimtokea Mariamu Magdalene katika bustani ya kaburi naye akamwambia:

14 “Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.” (Yohana 20:17) Kwa siku 40 aliendelea kuwako katika ujirani wa dunia kwa kutokuonekana, nyakati nyingine akijivika mwili wa kibinadamu na kuwatokea wanafunzi wake kuwahakikishia kwamba alikuwa hai tena, akiwa amefufuliwa kutoka kwa wafu.​—Matendo 1:1-5.

15, 16. (a) Ni wakati gani Yesu aliyefufuliwa alipoianza safari ya hiyo “nchi ya mbali,” na mbele ya mashahidi gani? (b) Bila shaka alikuwa amekwisha ifikia hiyo “nchi ya mbali” wakati gani, naye Petro anahakikishaje hili?

15 Wakati Yesu Kristo aliyefufuliwa alipopaa kwenye Baba yake wa kimbinguni huo ndio uliokuwa wakati ambapo alianza kusafiri kwenye “nchi ya mbali.” Hii ilikuwa katika siku ya 40 tangu kufufuliwa kwake kutoka kwa wafu. Wakati hesabu fulani ya wanafunzi juu ya Mlima wa Mizeituni walipokuwa wakiuona mwili wa kujivika ambao Yesu alikuwa ametokea nao ukipaa angani na kutoweka, malaika wawili walisimama karibu na kusema: “Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.” (Matendo 1:11) Hatujui ilichukua muda mrefu namna gani kwa Yesu Kristo aliyekuwamo katika makao ya kiroho kuifikia “nchi ya mbali” ya mfano, lakini ilikuwa katikati ya siku kumi, au mbele ya sikukuu ya Pentekoste ya mwaka huo wa 33 C.E. Siku hiyo roho takatifu ilimiminwa juu ya wanafunzi wa Kristo Yerusalemu, naye mtume Petro alihutubu akiongozwa na roho ya Mungu na kuwaambia hivi maelfu ya Wayahudi wenye kusikiliza:

16 “Maana Daudi hakupanda mbinguni; bali yeye mwenyewe anasema, [Yehova] alimwambia Bwana wangu, Keti upande wa mkono wangu wa kuume. Hata nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako. Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.”​—Matendo 2:34-36.

“FANYENI BIASHARA MPAKA NITAKAPORUDI”

17. Mfano wa Yesu waonyeshaje mambo waliyopaswa kufanya wanafunzi wake duniani wakati wa kutokuwapo kwake kwa muda mrefu?

17 Kwa hiyo Yesu Kristo angekuja tena​—lakini wakati huu akiwa na “uwezo wa kifalme” (NW). Mfano ambao Yesu alitoa kwa sababu wanafunzi wake “walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara,” ulionyesha kwamba Yesu Kristo, kama “kabaila,” angekuwa hayuko kwa muda mrefu. (Luka 19:11, 12) Basi, je! wanafunzi wake walipaswa kufanya nini wakati huo, wakikungoja kurudi kwake akiwa na “uwezo wa kifalme”? Yesu hakuwaacha bila maagizo ya waziwazi juu ya walivyopaswa kufanya. Mfano wa Yesu ulionyesha kwamba angefanya hivi. Juu ya kabaila anayeondoka twasoma: “Akiwaita watumwa wake kumi akawapa mina kumi na kuwaambia, ‘Fanyeni biashara mpaka nitakaporudi.’”​—Luka 19:13, NW.

18. (a) Ni thamani gani zinazopewa mina kumi za fedha na tafsiri mbalimbali za Biblia na Aid to Bible Understanding? (b) Iliwapasa watumwa kufanya nini na mina za fedha?

18 An American Translation inaipa mina ya kale thamani nayo yautafsiri mstari huu hivi: “Naye akawaita kumi wa watumwa wake na kuwapa kila mmoja shilingi mia moja na arobaini na kuwaambia wazifanyie biashara atakapokuwa hayupo.” Tafsiri ya Biblia ya Moffatt inaipa mina thamani ya Kiingereza nayo yasema: “Kwanza akawaita watumishi wake kumi, akiwapa kila mmoja noti ya shilingi mia moja, na kuwaambia, ‘Ifanyieni biashara mpaka nitakaporudi.’” The New English Bible ya mwaka wa 1970 inaipa mina thamani ya “shilingi ishirini” tu. The New American Bible haionyeshi wazi nayo yasema kwamba kabaila aliwapa watumishi wake “hesabu za makumi.” Kitabu cha mwaka wa 1971 kinachoitwa “Aid to Bible Understanding” kinaihesabu mina ya fedha ya karne ya kwanza C.E. kuwa karibu shilingi 104.00. Hii ilikuwa fedha nyingi sana siku za Yesu, ikilingana na drakma 100, ijapokuwa ilikuwa na thamani ya sehemu moja tu kwa 60 ya talenta ya fedha yenye shilingi 5,920.00. Bila ya kujali n’nini ingekuwa thamani ya mina ya fedha leo, walipaswa watumwa wa kabaila kufanya biashara na mina za fedha na kwa njia hiyo kumpatia utajiri aliyetazamiwa kuwa mfalme.

19. “Watumwa kumi” walifananisha nani, nazo “mina kumi” zilifananisha nini?

19 Watumwa kumi wa mfano wa Yesu waliwafananisha wanafunzi wa Bwana Yesu. Alipokwisha kufufuliwa kwa wafu, je! aliwakabidhi nini wanafunzi wake mbele ya kupaa mbinguni siku kumi mbele ya sikukuu ya Pentekoste ya mwaka wa 33 C.E.? Penye kifo chake juu ya mti katika Kalvari, Yesu alikuwa amenyang’anywa kabisa kila kitu cha kimwili chenye thamani yo yote duniani. Wakati wa ufufuo wake kutoka kwa wafu siku ya tatu, hata vitambaa vya mazishi vilivyomfunga na kitambaa cha kichwani viliachwa nyuma kaburini. (Yohana 20:6, 7) Basi, je! Yesu alikuwa na nini cha kuwakabidhi wanafunzi wake mbele ya kupaa kwenye “nchi ya mbali” ya kimbinguni? Lilikuwa jambo fulani ambalo, kama mina kumi za fedha, lilikuwa na thamani ambayo ingeweza kuwa kama msingi au mali ya kufanyia ongezeko lenye thamani kwa ajili ya aliyetazamiwa kuwa Mfalme, Masihi. Kwa kuwa hakikuwa kitu kiwezacho kugusika, kilikuwa kisichoonekana na hali kilikuwapo. Nini hicho? Shamba la faida ambalo Yesu alikuwa amelisitawisha juu ya ufalme wa Mungu wa Kimasihi kwa njia ya huduma yake ya waziwazi ya karibu miaka mitatu u nusu katika Israeli.

20. (a) Ni sifa gani bora iliyokuwa imeshirikishwa na shamba la utendaji ambayo wanafunzi wa Yesu wangeweza kuletea faida kana kwamba walikuwa wakifanya biashara na mina kumi? (b) Mtumwa mmoja na Yesu mwenyewe walionyeshaje ubora huo wenye faida ulioshirikishwa na shamba la utendaji?

20 Ndiyo, “mina” hizo kumi za mfano za fedha ziliyafananisha matokeo ambayo kufundisha kwingi na kuhubiri kwa Yesu kulikuwa kumetokeza katika ulimwengu wa Kiyahudi au wa Kiisraeli hivyo kwamba watu wateule wa Yehova wakaelekea kumkubali Yesu kama Masihi aliyeahidiwa. Hivyo lilikuwako shamba lililotayarishwa kwa ajili ya wanafunzi wake Yesu ambapo wangeweza kufanyia kazi, kujenga na kutia Wayahudi moyo wawe na nia ya kuamini hata kukomaa au wapate kusadikishwa kwamba Yesu alikuwa ndiye Mtiwa Mafuta wa Yehova kwa sababu ya aliyoyafundisha Yesu na kufanya katika utimizo wa unabii wa Biblia. Lilikuwa shamba ambalo wanafunzi wake Yesu wangeweza kulifanya liwe na mazao sana kwa kujishughulisha na mambo ambayo Yesu aliwaambia wafanye. Katika mfano mmojawapo wa wale watumwa kumi aliyafananisha na shamba wakati mtumwa huyu alipomwambia mfalme aliyerudi: “Wavuna usichopanda.” (Luka 19:21) Vile vile Yesu alifananisha hili mapema alipowaambia wanafunzi wake wakiwa Samaria: “Neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.”​—Yohana 4:37, 38.

21. (a) Yesu alitaka nini zaidi? (b) Iliwapasa wanafunzi kufanya nini, shamba la Kiyahudi lisipokuwa na matokeo ya kutosha?

21 Hivyo wanafunzi wake Yesu walikuwa na jambo lenye faida, jambo lenye thamani, jambo liwezalo kutumiwa kwa kufaa, lenye matokeo, la kuanza ‘kufanyia biashara’ na kupata ongezeko. Si fedha zaidi wala dhahabu ambayo Yesu alitamani kupata kupitia kwa watumwa-wanafunzi wake. Alichotaka zaidi ni wanafunzi waliofuata nyayo zake na waliomkubali yeye kama Mfalme wa Kimasihi. Na iwapo shamba la Kiyahudi lililokwisha kusitawishwa tayari lisingewatokeza wote, zaidi wale warithi wa Ufalme pamoja na Yesu 144,000, basi wanafunzi wangeweza kulipanua shamba la utendaji wao kwenye makao ya Mataifa au watu wasio Wayahudi. Kwa njia hii wangeliongezea shamba lililositawishwa ambalo lingetokeza eneo zaidi mara tano au kumi la lile linalositawishwa kusudi litokeze wafuasi wa ufalme wake Kristo.

22. Kwa kuwa “watumwa” walikuwa kumi katika hesabu wanafananisha nani, katika utimizo kamili wa mfano?

22 “Watumwa wake kumi” katika mfano wa Yesu hawakutimizwa wote na mitume na wanafunzi wa karne ya kwanza ya Wakati wetu wa Kawaida. Kwa kufaa, hesabu ya “watumwa” iliwekwa kuwa “kumi,” kwa maana kumi katika mifano ya Biblia inatumiwa kusimamia uzima au ukamilifu, zaidi kwa habari ya mambo ya kidunia. Hivyo ‘watumwa kumi’ wa mfano wangefananisha vizuri watumwa wote wa Yesu Kristo waliotiwa mafuta na kuzaliwa kwa roho ambao ni wanaotazamiwa kuwa warithi pamoja naye katika ufalme wa kimbinguni na waliotokezwa mnamo hizi karne zote kumi na tisa zilizopita mpaka kuja kwake Kristo katika uwezo wa kifalme mwishoni mwa Majira ya Mataifa katika mwaka wa 1914 C.E. na hata sasa. Lazima iwe hivyo, kwa maana mitume na wanafunzi wengine wa karne ya kwanza C.E. hawakuendelea kuishi wakiwa na mwili mpaka kurudi kwake Kristo kusikoonekana akiwa na uwezo wa Ufalme katika hii karne ya 20.

23. (a) Sehemu zenye kufikia upeo za mfano zinalingana na wanafunzi wa Kristo wa kipindi gani? (b) Kwa sababu ya machinjo yanayokaribia, ni kwa faida yetu kufanya nini juu ya mfano?

23 Kwa hiyo, sehemu za mwisho zenye kufikia upeo za mfano wa Yesu wa ‘watumwa kumi’ wenye mina kumi lazima ziwafananishe wanafunzi wa Yesu Kristo waliotiwa mafuta, wakabatizwa na kuzaliwa kwa roho walio hai duniani mnamo hii karne ya 20. Uchunguzi wafunua kwamba kuna mabaki karibu 10,000 ambao wangali duniani, ‘wanaofanya biashara’ na mina kumi za mfano kwa ajili ya kuuongezea utajiri wa Mfalme mpya wa dunia. Hawa 10,000 ni hesabu iliyobaki iliyo ndogo kweli kweli tunapowalinganisha wao na hesabu ya wanafunzi 144,000 watakaoungana na Yesu Kristo watawale pamoja naye kwa miaka 1,000 kwa utukufu wa Mungu na baraka ya milele ya wanadamu wote. Namna ambavyo watumwa kumi hawa wa mfano walivyofanya biashara na “mina kumi” za anayetazamiwa kuwa Mfalme ni hadithi ya kupendeza. Kwa sababu ya machinjo yanayokaribia ya adui za Mfalme wa Kimasihi na dunia anayestahili, itakuwa kwa faida yetu kuifuata hadithi hii hata mwisho na kuona ni sehemu gani ifaayo tunayoweza kuishiriki katika utimizo wa kisasa wa mfano wa Yesu.

[Picha katika ukurasa wa 251]

Katika mfano wa Yesu kabaila mwenye kuondoka alimpa kila mmoja wa watumwa kumi mina moja, akiwaambia: “Fanyeni biashara mpaka nitakaporudi.” Wale watumwa kumi waliwafananisha wanafunzi wa Yesu

[Picha katika ukurasa wa 252]

Yesu alipokwisha kufufuliwa alizitoa mina za mfano, kama inavyoonyeshwa katika Mathayo 28:18-20

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki