Ulimwengu Huu Unaelekea Wapi?
Matatizo makubwa na matukio yenye kushtua hutukia kila siku ulimwenguni pote! Yana maana gani?
USALAMA: Mabomu yalipuliwa sokoni. Walimu na wanafunzi wapigwa risasi shuleni. Watoto wachanga watekwa nyara wazazi wakiwa wameangalia kwingineko. Wanawake na wanaume wazee wavamiwa na kuibiwa vitu wakati wa mchana.
HALI YA DINI: Makanisa yaunga mkono majeshi yanayopigana. Viongozi wa kidini washtakiwa kwa kushiriki mauaji ya umati. Makasisi wafanya ngono na watoto; makanisa yaficha. Watu wanaoenda kanisani wapungua; makanisa yauzwa.
MAZINGIRA: Misitu yakatwa kwa ajili ya miradi ya kibiashara. Maskini waharibu misitu wakitafuta kuni. Visima vyachafuliwa, maji yaharibiwa. Takataka za viwandani na baadhi ya njia za kisasa za uvuvi zawaangamiza samaki. Uchafuzi mbaya sana wa hewa.
MAPATO: Inasemekana kwamba katika nchi zilizo kusini ya jangwa la Sahara, mshahara wa wastani wa mtu mmoja ni dola 480 hivi za Marekani kwa mwaka. Makampuni yafilisika na maelfu wapoteza kazi kwa sababu ya wakurugenzi wenye pupa. Wanabiashara wadanganywa na kupoteza pesa zao zote.
UPUNGUFU WA CHAKULA: Watu wapatao 800,000,000 ulimwenguni pote hulala njaa kwa ukawaida.
VITA: Katika karne ya 20, vita vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 100,000,000. Silaha za nyuklia zilizopo zinatosha kuwaangamiza kabisa wanadamu wote. Vita vya wenyewe kwa wenyewe. Ugaidi waenea ulimwenguni pote.
TAUNI NA MAGONJWA MENGINE: Kuanzia mwaka wa 1918, homa ya Kihispania iliwaua watu 21,000,000. Sasa UKIMWI ndio “ugonjwa hatari zaidi wa kuambukiza kuwahi kutokea.” Kansa na ugonjwa wa moyo unawaua watu ulimwenguni pote.
Angalia matukio hayo yote kwa ujumla. Je, ni matukio yasiyohusiana? Au ni matukio yenye maana sana yanayotukia wakati uleule ulimwenguni pote?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]
Je, Kweli Mungu Anajali?
Wanapofadhaishwa na matukio yenye kushtua au msiba, watu wengi hushangaa ni kwa nini Mungu hakomeshi mambo hayo.
Mungu anajali. Anatoa mwongozo unaotegemeka na kitulizo cha kweli sasa. (Mathayo 11:28-30; 2 Timotheo 3:16, 17) Ameweka msingi wa kuja kukomesha kabisa jeuri, magonjwa, na kifo. Maandalizi yake yanaonyesha kwamba anawajali watu wa mataifa, makabila, na lugha zote wala si watu wa taifa moja tu.—Matendo 10:34, 35.
Sisi tunajali kadiri gani? Je, unamjua Muumba wa mbingu na dunia? Jina lake ni nani? Kusudi lake ni nini? Anajibu maswali hayo katika Biblia. Humo anatuambia hatua ambazo anachukua kukomesha jeuri, magonjwa, na kifo. Tunapaswa kufanya nini ili tufaidike? Tunapaswa kujifunza kumhusu yeye na kusudi lake. Tutafaidikaje na maandalizi hayo ikiwa hatumwamini? (Yohana 3:16; Waebrania 11:6) Ni lazima pia tutii matakwa yake. (1 Yohana 5:3) Je, unajali sana hivi kwamba uko tayari kutii matakwa ya Mungu?
Ili kufahamu kwa nini Mungu ameruhusu hali zilizopo leo, ni lazima tuelewe suala fulani muhimu. Biblia hueleza suala hilo. Suala hilo linafafanuliwa kwenye ukurasa wa 15 wa broshua hii.