Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa
—Ujeremani (Inaendelea)
KUGAWA tangazo lililokubaliwa katika Berlin katika Ujeremani yote siku moja tu baada ya kazi kupigwa marufuku katika Prussia kulikuwa ishara kwa polisi wa Hitler wachukue hatua. Juni 27 maafisa wote wa polisi waliagizwa ‘wafanye upekuzi mara moja wa vikundi vyote vya eneo hilo na sehemu za biashara na kuchukua vifaa vyo vyote vyenye uadui kwa serikali.’ Siku moja baadaye, Juni 28, jengo lililokuwa Magdeburg lilikaliwa na watu 30 wa SA, waliokifunga kiwanda na kupandisha juu ya jengo hilo swastika (namna fulani ya msalaba, wenye mfano wa jua, bahati nzuri, au Unazi). Kulingana na amri rasmi ya maafisa wa polisi, ilikatazwa hata kujifunza Biblia na kusali katika uwanja wa Sosaiti. Juni 29 hatua hii iliripotiwa kwa taifa lote la Ujeremani na radio.
Vitabu, Biblia na picha zenye uzito wa jumla ya kilogramu 65,189 vilichukuliwa kutoka kiwanda cha Sosaiti Agosti 21, 23 na 24, vikapakiwa katika malori 25 kisha vikachomwa hadharani katika mpaka wa Magdeburg ijapokuwa Ndugu Harbeck, mwangalizi wa tawi Switzerland, alifanya majaribio ya kujitahidi sana jambo hili lisitokee. Gharama za kuchapa vifaa hivyo zilijumlika kuwa karibu mark 92,719.50. Tena, vitabu vingi vilichukuliwa kisha vikachomwa au vikaharibiwa katika makundi mbalimbali, kwa mfano katika Cologne, ambako vitabu vyenye thamani ya walau mark 30,000 viliharibiwa. The Golden Age liliripoti katika toleo lake la Juni 1, 1934 kwamba yawezekana jumla ya thamani ya mali (viti, meza, vitanda, n.k.) vilivyoharibiwa ilikuwa kati ya mark milioni mbili na milioni tatu.
Hasara hiyo ingalikuwa kubwa hata zaidi kama hatua za kuhamisha vitabu kutoka Magdeburg zisingalichukuliwa, vingine kwa meli, na kuviweka katika sehemu nyingine zenye kufaa. Kwa njia hii iliwezekana kuficha vitabu vingi sana visionekane wala kuchukuliwa na wapelelezi kwa miaka mingi. Vingi kati yavyo vilitumiwa katika utendaji wa kuhubiri kwa siri miaka iliyofuata. Kwa sababu serikali ya Amerika iliingilia jambo hili, jengo la Sosaiti katika Magdeburg lilirudishwa kwa Sosaiti katika Oktoba. Hati ya kuliachilia, ya Oktoba 7, 1933, ilisema kwamba ‘mali ya Sosaiti iliachiliwa yote kabisa itumiwe kwa uhuru, ingawa utendaji wo wote ulikuwa bado umekatazwa usiendeshewe humo, kuchapa vitabu au kuwa na mikutano.’
MWANZO WA UTENDAJI WA SIRI
Ingawa katika mwaka wa kwanza wa kupata kwa Nazi mamlaka utendaji wa kutoa ushuhuda wa siri ulielekea kutokuwa na usimamizi wo wote na mikutano ya vikundi vikundi haikufanywa kila mahali, Gestapo (mapolisi) walipata sababu mpya za kukamata akina ndugu.
Mara baada ya ndugu wa kwanza kukamatwa na nyumba zao kupekuliwa, wenye mashaka walianza kuwaza kwamba hatua hizi zilikuwa mwanzo tu wa shughuli kali zaidi ya mateso. Walijua kwamba ilikuwa kazi bure kabisa kujaribu kuamua maulizo haya penye meza ya mkutano. Njia ya pekee iliyofaa ilikuwa kupigania kweli.
Lakini idadi kubwa ilisita-sita, wakiona ni bora kungoja, kwa maana bila shaka Yehova angefanya jambo fulani kuzuia watu wake wasiteswe. Ijapokuwa kikundi hiki kilikuwa kikipoteza wakati kwa kusita-sita, kikijaribu sana kisiharibu mambo zaidi kwa kuchukua hatua fulani, wahubiri wengine walikuwa wameamua kuendeleza kazi. Ndugu hodari walianza kufanya mikutano karibuni vikundi vikundi katika nyumba zao, ingawa walijua kwamba jambo hili lingeweza kufanya wakamatwe na kuteswa vikali.
Mahali pengine akina ndugu walianza kutumia chombo cha kunakilia nakala za Watchtower, ambazo chache kati yazo zilipitishwa kwa siri sikuzote kutoka nchi jirani. Karl Kreis wa Chemnitz alikuwa kati ya ndugu wa kwanza kufanya mipango hiyo. Baada ya kuandika stencil alikuwa akizipeleka kwa Ndugu Boschana katika Schwarzenberg, ambako walikuwa wakitoa nakala nyingi. Kati ya waliokuwa wenye bidii sana wakati huo alikuwa Hildegard Hiegel na Ilse Unterdorfer. Mara marufuku ilipowekwa waliamua kutoacha lo lote liwazuie wasitimize agizo lao walilopewa na Mungu. Dada Unterdorfer alinunua pikipiki na kusafiri-safiri kati ya Chemnitz na Olbernahau akiletea akina ndugu nakala za The Watchtower. Aliwatembelea waliokuwa wakiishi karibu kwa baiskeli yake asifanye watu waanze kufikiria lililokuwa likiendelea.
Ndugu Johann Kölbl alipanga nakala 500 za The Watchtower zitengenezewe Munich kisha wa huko wakagawiwa na pia katika maeneo ya mbali ya Mwitu wa Bavaria.
Katika Hamburg Ndugu Niedersberg ndiye aliyechukua hatua ya kwanza bila kukawia. Alikuwa amekuwa ndugu mhaji kwa miaka kadha kabla ya kuacha kwa sababu ya ugonjwa uitwao multiple sclerosis (ugonjwa ufanyao kingo za mishipa ya damu kuwa ngumu). Kijapokuwa kizuizi hiki yeye alikuwa amefanya yote aliyoweza. Basi wakati huu wa kujaribiwa akina ndugu walifurahia kumtembelea, kwa maana jambo hili lilitia imani yao nguvu sikuzote. Upesi upendo wake kwa akina ndugu ulimvuta achukue hatua za kuhakikisha wanapata chakula cha kiroho kawaida kwa mara nyingine. Alianza kunakili The Watchtower nyumbani mwake. Alifundisha Helmut Brembach kuandika stencil na kumwonyesha namna ya kutumia mashine ya kunakilia. Halafu, alipoona kazi ingeweza kuendeshwa bila yeye, alieleza wengine kwamba alikuwa na mpango wa kufunga safari ya kuzuru makundi katika pwani ya magharibi ya Schleswig-Holstein kuwatia moyo na kupanga mipango ya kuwapelekea The Watchtower. Kwa mara nyingine alizungumza na akina ndugu kwa uangalifu namna magazeti yangeweza kutumwa na kuandikiana mambo fulani ya siri ambayo kwayo wangejua kutokana na aliyoandika watatuma nakala ngapi kwa kila kundi.
Mbali na nakala za The Watchtower zilizochapiwa Ujeremani, nyingine zilitumwa Ujeremani kutoka Switzerland, Ufaransa, Czechoslovakia, ndiyo, hata kutoka Poland, na zilitokea kwa namna mbalimbali, mara nyingi zikiwa na ukubwa mbalimbali. Kwanza makala nyingi za Watchtower zilitumwa kutoka Zurich, Switzerland, zikiwa na kichwa “Yonadabu.” Baada ya Gestapo (mapolisi) kugundua njia hii, maafisi yote ya posta katika Ujeremani yaliagizwa yachukue bahasha zote zenye kichwa hiki na kuchukua hatua ifaayo juu ya wale ambao magazeti hayo yalikuwa yakitumwa. Mara nyingi hii ilifanya wakamatwe.
Baadaye kichwa na njia pia ya kufunga The Watchtower ilibadilishwa karibu kila toleo. Mara nyingi kichwa cha makala ya Watchtower kilitumiwa, kwa kawaida kikitokea mara moja tu, kwa mfano “Karamu Tatu,” “Obadia,” “Mpiganaji,” “Wakati,” “Waimbaji wa Hekaluni,” na kadhalika. Lakini hata nyingine za nakala hizi zilianguka mikononi mwa Gestapo, hivyo barua ikawa inazungushwa kwenye kila kituo cha polisi katika Ujeremani kuwapasha habari kwamba gazeti hili lilipigwa marufuku. Lakini mara nyingi habari hizi zilifika zimechelewa mno, kwa maana makala nyingine ya Watchtower yenye mfano tofauti kabisa na kichwa tofauti kabisa wakati huo ilikuwa imekwisha tokea. Karibuni Gestapo wakapaswa wakubali kwa uchungu mwingi kwamba mashahidi wa Yehova walikuwa wamewashinda kwa akili.
Ndivyo ilivyokuwa kwa The Golden Age. Kwa muda fulani halikuwa limepangwa kati ya magazeti yaliyopigwa marufuku. Baadaye, lilipokwisha pigwa marufuku rasmi, lilitumwa kwa ndugu Wajeremani kwa faragha, kwa kawaida kutoka kwa ndugu wa nchi za kigeni, hasa kutoka Switzerland. Sikuzote waliotuma magazeti walihakikisha anwani iliandikwa kwa mkono na mtu tofauti kila mara.
Kadiri Gestapo (mapolisi) walivyoshindwa kufanikiwa katika majaribio yao kukatiza vyanzo hivi vya ugawaji, ndivyo walivyozidi kuwa wakatili waliposhughulika na akina ndugu. Kwa kawaida waliwakamata baada ya kupekua nyumba zao, ingawa mara nyingi walifanya hivyo bila sababu. Katika makao makuu ya polisi akina ndugu kwa ujumla walitendwa kikatili katika jaribio la kuwalazimisha wakubali kuwa wenye hatia.
UCHAGUZI ‘WA HIARI’
Silaha nyingine iliyotumiwa kuogofya watu, na hasa iliyoelekezwa kwa mashahidi wa Yehova kuwalazimisha waridhiane, ulikuwa uitwao uchaguzi ‘wa hiari.’ Waliokataa kujiacha walazimishwe kupiga kura walitangazwa kuwa “Wayahudi,” “wasaliti wa Nchi yao” na “walaghai.”
Max Schubert wa Oschatz (Saxony) aliitwa mara tano na wafanya kazi wa uchaguzi waliomtaka aende kwenye kura siku ya uchaguzi. Mke wake alitembelewa na wanawake wenye kusudi lilo hilo. Walakini, ndugu Schubert aliwaambia wageni wake wakati wote kwamba alikuwa mmoja wa mashahidi wa Yehova na alikuwa amepigia Yehova kura, iliyokuwa imetosha na haikuwa lazima kupigia mtu mwingine kura.
Alipatwa na magumu kesho yake. Yeye alikuwa karani wa kutoa tikiti wa gari-moshi naye alionana na watu kila mara. Siku hiyo walipanga hasa kumsalimu kwa kusema “Mtukuze Hitler.” Alirudisha salamu hizo kwa kusema “Nimeshinda vema” au jambo kama hilo. Walakini, aliona kwamba jambo fulani lilikuwa linakaribia na kuzungumza hili na mkewe wakati wa chakula cha mchana, akamwambia awe tayari kwa tukio lo lote. Baada ya kumaliza utumishi wake alasiri hiyo alichukuliwa karibu saa kumi na moja jioni na polisi na kupelekwa kwenye nyumba ya msimamizi wa mahali hapo wa chama cha National Socialist Party. Kigari kidogo chenye kuvutwa na farasi wawili kikasimama mlangoni. Ndugu Schubert alilazimishwa kusimama katikati akiwa amezungukwa na watu kadha wa SA walioketi kando yake, kila mmoja akiwa na mwenge mkononi. Mbele mwingine alikuwa amesimama akiwa na mbiu na nyuma mwingine akiwa na ngoma, nao walipokezana zamu kupiga kamsa ili kila mtu atazame na kuyaona maandamano. Watu wawili wa SA walikuwa wameshika ishara kubwa katika kigari iliyosema hivi: “Mimi ni mlaghai na msaliti wa Nchi yangu, kwa maana sikupiga kura.” Upesi mtu fulani nyuma ya maandamano alikuwa ameunda kikundi kilichoendelea kupayuka-payuka maneno yaliyokuwa katika ishara hiyo. Mwishoni mwa sentensi walikuwa wakiuliza: “Apelekwe wapi?” halafu watoto katika kundi la watu wakawa wakipaza sauti pamoja: “Katika kambi ya mateso!” Ndugu Schubert alipelekwa kupitia barabara za mji zenye watu karibu 15,000 kwa saa mbili na nusu. Kituo cha radio cha Luxembourg kilitoa habari za kisa hiki kesho yake.
Mradi wao ulikuwa kunyang’anya mashahidi wa Yehova njia yao ya kujiruzuku—kuwafuta kazini, kuwafukuza watoke kazini pao, kufunga biashara zao na kuwakataza wasiendeshe shughuli zao.
VIJANA WAKABILI MAJARIBU
Mara nyingi watoto wa mashahidi wa Yehova walinyimwa nafasi ya kupata elimu. Mwache Helmut Knoller asimulie yaliyompata kwa maneno yake mwenyewe:
“Wakati ule ule utendaji wa mashahidi wa Yehova ulipopigwa marufuku katika Ujeremani, wazazi wangu walibatizwa kuonyesha wakf wao kwa Yehova! Wakati wangu wa kuamua ulifika nilipokuwa mwenye umri wa miaka kumi na mitatu marufuku ilipotangazwa. Mara nyingi yalikuwako maamuzi mengi ya kufanya shuleni kuhusiana na kusalimu bendera, niliyoyaamua kwa kupendelea uaminifu na wakf kwa Yehova. Chini ya hali hizi, kuendelea kupata elimu ya juu kulikuwa hakuwaziki na kwa hiyo nikaanza kujifunza biashara kama mwanafunzi katika Stuttgart; hii ilitia na kuhudhuria shule ya biashara mara mbili kwa juma ambako sherehe za kupandisha bendera zilifanywa kila siku. Kwa kuwa mimi nilikuwa mrefu zaidi kuliko wanadarasa wenzangu wote, bila shaka mimi nilionekana vyepesi isivyofaa nilipokataa kusalimu bendera.
“Mwalimu alipoingia darasani, wanafunzi walitakiwa wasimame, waamkie kwa maneno ‘Mtukuze Hitler’ na kuinua mkono wa kuume. Mimi sikufanya hivi. Kwa kawaida mwalimu alikaza fikira kwangu peke yangu na mara nyingi kulikuwa na matukio kama haya: ‘Knoller, njoo hapa! Sababu gani huamkii kwa kusema “Mtukuze Hitler?” ‘ ‘Hiyo haipatani na dhamiri yangu, mwalimu.’ ‘Wasemaje? Ewe nguruwe! Toka hapa—unanuka—nenda mbali. Aibu! Msaliti!’ n.k. Ndipo nikahamishwa kwenda darasa jingine. Baba alizungumza na makuu wa shule akapewa maelezo haya: ‘Mungu wenu, mnayetumaini, aweza kuwapa hata kipande cha mkate? Adolf Hitler aweza, naye amehakikisha hilo.’ Hii ilimaanisha watu walipaswa wamheshimu na kumsalimu kwa maneno ‘Mtukuze Hitler.’”
Alipomaliza uanafunzi wake, Vita ya Ulimwengu ya Pili ilitokea na Ndugu Knoller akaitwa aingie utumishi wa jeshi. Yeye atoa habari hizi:
“Niliandikwa jina langu niingie utumishi wa jeshi Machi 17, 1940. Kwa muda mrefu nilikuwa nimefikiria litakalotukia. Niliwaza kwamba nikienda kwenye kituo kikuu cha kupitisha nguvu za umeme halafu nikatae kuapa ningeletwa mbele ya mahakma ya vita na kupigwa risasi. Kwa kweli, mimi nilipendelea kufanyiwa hivyo kuliko kutiwa katika kambi ya mateso! Lakini mambo hayakuwa hivyo. Sikujaribiwa mbele ya mahakma ya jeshi, bali nilitiwa gerezani nikipimiwa chakula na maji. Siku tano baadaye Gestapo (mapolisi) walikuja na kunichukua wakanipeleka kwenye kesi iliyochukua saa nyingi ambako tisho la kila namna lilifanywa. Usiku huo nilirudishwa gerezani. Nilifurahi sana; hakukuwa na dalili ya hofu tena, bali ya furaha tu na ya kutazamia yaliyokuwa katika wakati ujao na namna Yehova angenisaidia tena. Juma tatu baadaye wakuu wa Gestapo walinisomea amri ikisema kwamba lazima nikae rumande nikilindwa kwa sababu ya uadui wangu kwa serikali na hatari ambayo naweza kuleta kwa kufanya bidii nikifanyia kazi International Bible Students waliopigwa marufuku. Hiyo ilikuwa na maana ya kupelekwa katika ‘kambi ya mateso.’ Kwa hiyo mambo yalitukia tofauti hasa na nilivyotumaini. Nikiwa na wafungwa wengine, nilitupwa katika kambi ya mateso Juni 1.”
Ndugu Knoller alizoelea maisha si katika Dachau tu bali pia katika Sachsenhausen. Baadaye alihamishwa, pamoja na wafungwa wengine, akapelekwa kwenye kisiwa cha English Channel cha Alderney. Safari ya kutazamisha ilimfikisha Steyr, Austria, ambako yeye na waliokuwa naye walifunguliwa mwishowe Mei 5, 1945. Msukosuko wa miaka hiyo waweza kuonekana katika uhakika wa kwamba Ndugu Knoller, aliyekuwa ameteswa sana, hakuwa amepata nafasi ya kuonyesha wakf wake kwa Yehova kwa kubatizwa katika maji, ingawa miaka yake ya uaminifu akiwa katika hali zenye magumu makubwa ilikuwa uhakikisho wa kwamba alikuwa amefanya wakf huo. Katika kikundi kidogo cha waokokaji waliorudi nyumbani naye walikuwako ndugu wengine tisa, wote wakiwa walistahimili kati ya miaka minne na mitano katika kambi za mateso na ambao sasa walichukua nafasi ya kubatizwa katika Passau kwa shukrani.
Inaendelea.—Kutoka 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses.