Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa
—Ujeremani (Inaendelea)
“MACHI 27 nilipashwa habari kwamba mke wangu alikuwa amekufa na kwamba ningefunguliwa kwa siku tatu nimalize shughuli ya lazima. Mara hiyo nikaenda hospitalini ambako mke wangu alikuwa ameletwa baada ya kumzaa mtoto, ingawa alikuwa amekufa kabla ya kufika huko. Daktari na mmoja wa wauguzi, ambao walikuwa wangali wanajua mimi ni mmoja wa mashahidi wa Yehova, waliniomba kwa nguvu ‘kumshitaki daktari na mkunga, kwa maana mke wako alikuwa mwenye afya na hakukuwa na kosa lo lote kwake,’ lakini mimi nikajibu kwa uchovu tu: ‘Hapo itanilazimu nifanye mengi.’ Nyumbani niliwakuta watoto wengine wawili wale, wenye umri wa miaka tisa na kumi, wakiwa na huzuni ya ajabu, na mtoto aliyekufa akiwa amelala chumbani. Sasa niwaache peke yao bila ya mtu wa kuwaangalia, pengine nisiwaone tena?”
Wakwe za Ndugu Ruef wakaomba kwamba mwili wa mke wake upelekwe Pocking, ambako hakuna mtu wa nje ya jamaa hiyo aliruhusiwa aseme kando ya kaburi. Hivyo Ndugu Ruef mwenyewe ndiye aliyetoa hotuba ya mazishi ya mkewe, Yehova akimpa nguvu za kufanya hivyo.
Ndugu Ruef hakuweza kulivumilia wazo la kulazimika sasa kuwaacha watoto wawili wake nyuma bila ya mtu wa kuwaangalia. Zikiwa zimebaki saa chache tu za kuachiliwa kwake kwa muda kutoka kifungoni, akapeleka mmoja wa watoto wawili wake kwa wakwe zake, ingawa hawakuwa mashahidi wa Yehova, na mwingine yule akampeleka kwa ndugu waliokuwa wanaishi karibu na mpaka wa Switzerland. Mwishowe, akatoroka kwa ghafula akapita mpaka na kuingia Switzerland, ambako alipata kimbilio pamoja na mtoto wake.
KWANZA ADHABU, KISHA “URAFIKI,” KUVUNJA UKAMILIFU
Zilikuwako nyakati watoto waliotenganishwa na wazazi wao walipolegea katika imani kwa muda na kwa kweli wakawa katika hatari ya kuingizwa katika kambi ya Nazi, kama vile viongozi wa mipango hiyo walivyowaza ingekuwa. Kwa mfano, mchukue Horst Henschel wa Meissen, ambaye, mwaka wa 1943, alibatizwa akiwa mwenye umri wa miaka kumi na miwili pamoja na baba yake. Anaandika hivi:
“Utoto wangu ulijawa na mema na mabaya. Nilijitenga na chama cha Vijana wa Hitler—kwa kadiri hii ilivyowezekana—nami nilikuwa mwenye furaha na nguvu. Nilipokataa kutoa salamu ya Hitler, iliyotakiwa kila siku shuleni, nilikuwa nikipigwa, lakini nilifurahi kujua kwamba nilikuwa nimebaki mwaminifu, kwa kuimarishwa na wazazi wangu. Lakini zilikuwako nyakati ambapo nilikuwa nikisema ‘Mtukuze Hitler’ ama kwa sababu ya adhabu ya kimwili au kwa kuogopa hali. Nakumbuka namna nilivyokuwa nikienda nyumbani, macho yangu yamejawa na machozi na namna tulivyokuwa tukisali pamoja kwa Yehova na namna nilivyokuwa napata uhodari tena kupinga mashambulio ya adui wakati uliofuata. Kisha lile lile lilikuwa likitukia tena.
“Siku moja Gestapo (polisi) walikuja wakapekua nyumba yetu. ‘Wewe ni mmoja wa mashahidi wa Yehova?’ mmoja wa watu wa SS mwenye mabega mapana akamwuliza mama yangu. Kana kwamba ni leo, naweza kumwona mama akiegemea kizingiti cha mlango na kusema kwa imara ‘Ndiyo,’ ingawa alijua hii ilimaanisha atakamatwa baadaye. Alikamatwa, juma mbili baadaye.
“Alikuwa akifanya kazi ya kumwangalia dada mdogo wangu, ambaye kesho yake angekuwa mwenye umri wa mwaka mmoja, polisi walipokuja wakiwa na cheti cha kuwaruhusu wamkamate. . . . Kwa kuwa wakati huo baba alikuwa nyumbani tulibaki tukiangaliwa naye. . . . Juma mbili baadaye baba alikamatwa pia. Ningali naweza kumwona ameinama mbele ya stovu ya jikoni akikazia moto macho. Kabla sijakwenda shuleni nilikuwa nimemkumbatia sana kama nilivyoweza, lakini yeye hakugeuka anitazame. Mara nyingi nimefikiria ugumu aliokuwa nao nami namshukuru Yehova mpaka leo hii kwamba Mungu alimpa nguvu zilizokuwa za lazima kunipa mfano mwema huo. Nilikuja nyumbani nikajikuta peke yangu. Baba alikuwa amekwisha amriwa afanye utumishi wa jeshi akawa amekwenda kwenye mahali pa kujiandikisha mjini akaeleze kukataa kwake. Alikamatwa papo hapo. Babu na nyanya na jamaa wengine wetu—ambao wote walipinga mashahidi wa Yehova na ambao kati yao wengine walikuwa wanachama wa Nazi—walikuwa wamechukua hatua nilindwe pamoja na dada mdogo wangu mwenye umri wa mwaka mmoja tusitiwe katika makao ya watoto au pengine hata katika shule ya kufunzia adabu. Dada mwingine wangu wa pili, aliyekuwa amekwisha kuwa na umri wa miaka 21, alikamatwa juma mbili baada ya baba, yangu, akafa juma tatu baadaye katika kifungo kwa sababu ya ugonjwa wa ndani ya koo na homa nyekundu.
“Sasa dada mdogo wangu na mimi tulikuwa pamoja na babu na nyanya. Nakumbuka nikipiga magoti mbele ya kitanda cha dada mdogo wangu nisali. Sikuruhusiwa kusoma Biblia, lakini baada ya kupata moja kwa mwanamke jirani kwa siri, niliisoma.
“Babu yangu, ambaye hakuwa katika kweli, wakati mmoja alimtembelea baba kifungoni. Akarudi nyumbani amekasirika sana sana. ‘Mvunja sheria huyu, goigoi huyu! Awezaje kuwaacha watoto wake mwenyewe” Akiwa amefungwa minyororo mikono na miguu, baba aliletwa mbele ya babu, ambaye, akiwa pamoja na wengine, alijaribu kubishana naye aingie utumishi wa jeshi kwa ajili ya watoto. Lakini yeye aliendelea kuwa mwaminifu akalikataa shauri hilo kwa imara, ndipo afisa mmoja akamweleza babu hivi: ‘Hata kama mtu huyu angekuwa na watoto kumi, asingetenda kwa njia tofauti.’ Ingawa jambo hilo lilimkasirisha babu sana alipolisikia, kwangu mimi ulikuwa uhakikisho kwamba baba alikuwa anaendelea kuwa mwaminifu na kwamba Yehova alikuwa anamsaidia.
Wakati fulani baadaye nikapokea barua kutoka kwake. Ilikuwa ndiyo barua yake ya mwisho. Kwa kuwa hakujua mama alikuwa amefungwa wapi, aliiandika kwangu. Nikapanda chumbani mwangu gorofani nikasoma maneno ya kwanza: ‘Ufurahi upokeapo barua hii, kwa sababu mimi nimevumilia. Baada ya saa mbili hukumu yangu itakatwa. . . . ’ Nilihuzunika nikalia, ingawa sikuifahamu maana kuu ya shauri hilo wakati huo kama ninavyoifahamu leo.
“Yajapokuwa matukio yote haya ya kukata maneno niliendelea kuwa mwenye nguvu za kadiri. Bila shaka Yehova alinipa nguvu zilizokuwa za lazima kutatua magumu yangu. Lakini Shetani ana njia nyingi za kushawishi mtu aingie mtegoni nami karibuni ningepatwa na jambo hili. Mmoja wa jamaa zangu alifikia waalimu wangu akawaomba wanivumilie. Kwa ghafula wote wakawa wenye urafiki sana sana kwangu. Waalimu hawakuniadhibu, hata nilipokataa kusalimu kwa kusema ‘Mtukuze Hitler,’ nao jamaa zangu wakawa wenye urafiki na wema zaidi kwangu. Ndipo mambo yalipotokea.
“Kwa kupenda kwangu mwenyewe nilijiunga na chama cha Vijana wa Hitler, ingawa hakuna aliyenilazimisha kufanya hivyo, na ingawa ilikuwa miezi michache tu kabla ya mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Jambo ambalo Shetani alikuwa ameshindwa kutimiza kwa ukali, aliweza kulitimiza kwa ubembelezi na ujanja. Leo mimi naweza kusema kwamba mateso makali yanayotoka nje yanaweza kujaribu uaminifu wetu, lakini mashambulio ya hila ya Shetani yanayotoka pande nyingine ni hatari sawasawa na mashambulio ya ukatili. Leo nafahamu ilimlazimu mama apatwe na majaribu magumu namna gani alipokuwa kifungoni. Nilikuwa nimepokea barua ya mwisho ya baba akihakikisha uaminifu wake na wakf mpaka kufa nayo ilinitia nguvu sana. Mama, kwa upande mwingine, alipelekewa mavazi na suti za baba, zilizokuwa zingali na madoa ya damu, huo ukiwa ni ushuhuda wa taabu za kifo chake. Baadaye mama aliniambia kwamba mambo yote haya yalikuwa magumu kwake kuvumilia, lakini kwamba jaribu lake gumu zaidi wakati huo zilikuwa barua zangu zilizokuwa zikionyesha nilikuwa nimeacha kumtumikia Yehova.
(Inaendelea)
—Kutoka 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses