Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa
—Ujeremani (Inaendelea)
KWANZA wengi walifanya kazi na Biblia peke yake, ijapokuwa vijitabu na vitabu vya zamani zaidi vilivyokuwa vimeokolewa visishikwe na Gestapo (polisi) viliangushwa wakati wa kufanya ziara za kurudia. Wengine walitengeneza kadi za kutoa ushuhuda. Wengine nao waliandika barua kwa watu waliowajua, wakitumia kwa faida wakati fulani wa pekee. Utendaji wa nyumba kwa nyumba uliendelea, ingawa hatari kubwa zilikuwako. Kila mara mtu alipofungua mlango angeweza kuwa mtu wa SA au SS. Walipomaliza mlango mmoja, kwa kawaida wahubiri waliruka kwenda nyumba nyingine yenye vyumba vingi au hata kwenye barabara nyingine nyakati ilipokuwa hatari sana.
Kwa karibu miaka miwili iliwezekana katika karibu kila mahali Ujeremani—mahali pengine muda mrefu hata zaidi—kuhubiri nyumba kwa nyumba. Bila shaka hii iliwezekana kwa sababu ya ulinzi wa pekee wa Yehova tu.
Hesabu ndogo za vitabu vilivyopatikana kwa utendaji wa kuhubiri karibuni zilimalizika. Kwa hiyo tukaangalia kama kuna uwezekano wa kupata vitabu kutoka nchi za ugenini. Ernst Wiesner wa Breslau anatufahamisha mambo fulani ya kupendeza juu ya namna hii ilivyofanywa:
“Tulipelekewa vitabu kutoka Switzerland kupitia Czechoslovakia. Viliwekwa mpakani vikiwa na watu wa nje kisha vikatolewa huko kupitia Riesen Mountains kuingia Ujeremani. Kazi, ambayo ilifanywa na kikundi cha ndugu waliokomaa wenye nia ya kufanya hivyo ilikuwa yenye hatari sana na yenye kuchosha sana sana. Tukawa tunavuka mpaka usiku wa manane. Akina ndugu walikuwa na mpango mzuri nao walikuwa na mifuko mikubwa ya kubebea vitu mgongoni. Wakawa wakifunga safari hiyo mara mbili kwa juma, ingawa zaidi ya hilo walipaswa wawe kazini pao kila siku. Wakati wa masika walitumia magari yasiyo na miguu ya kutelemkia milima yenye theluji. Walijua kila kijia, walikuwa na mienge mizuri, darubini za macho mawili na viatu vya kutembelea. Kuwa wenye busara ndiyo iliyokuwa sheria kuu zaidi. Kufika katika mpaka wa Ujeremani karibu na usiku wa manane na hata baada ya kuuvuka hakuna aliyethubutu kusema neno kwa muda mrefu. Ndugu wawili walitangulia na walipokutana na mtu ye yote wakawa wanaonyesha ishara kwa mienge (tochi) yao. Hii ilikuwa ishara ndugu wenye mifuko ya kubebea vitu mgongoni waliokuwa wanafuata karibu mita 100 nyuma wajifiche vichakani kando ya njia mpaka ndugu wale wawili waliokuwa mbele yao warudi na kusema neno fulani la siri walilolijua wenyewe kwa wenyewe (password) ambalo lilisaidia kujulisha wale wengine kwamba wenzao ndio wamekuja, nalo lilibadilishwa kila juma.
“Hili likawa linatukia mara kadha kila usiku. Mara njia ilipokuwa haina watu tena, ndugu walikuwa wakielekea kwenye nyumba fulani katika kijiji kilichokuwa upande wa Ujeremani ambako vitabu viliwekwa katika visanduku vidogo vidogo usiku uo huo au mapema asubuhi iliyofuata vikiwa na anwani, kisha vikapelekwa kwenye afisi ya posta katika Hirschberg au miji mingine ya karibu kwa baiskeli. Ndugu katika Ujeremani yote walipokea vitabu vyao kwa njia hii. . . . Kikundi hiki cha akina ndugu ambacho kilikuwa chenye bidii na chenye ufundi mwingi isivyo kawaida, kiliweza kuingiza vitabu vingi katika Ujeremani kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili bila ya kushikwa, kwa njia hiyo wakatia wengi nguvu katika nchi yote.” Mipango kama hiyo ilitumiwa pia katika mipaka ya Ufaransa, Saar, Switzerland na [Holland].
Tulikuwa na wakati wa kutosha kuficha vitabu mahali mbalimbali kabla marufuku haijatangazwa. Walakini, ili kuelewa yaliyotukia, ni jambo la maana kukumbuka kwamba akina ndugu hawakuwa wamekuwa na ujuzi wo wote wakati wo wote wa kuweka vitabu wakiwa chini ya marufuku. Kwa hiyo badala ya kuvigawa kati ya ndugu wengi, mwanzoni maelekeo yalikuwa kuviweka katika mabohari makubwa, hii ikidhaniwa ni salama zaidi, hasa kwa sababu wale waliosimamia walidhani marufuku ingekuwa ya muda tu. Mabohari mengine yalikuwa na nafasi ya kuwekea tani 30 mpaka 50 za vitabu. Walakini, wakati ulipozidi kupita, ndugu wengine walianza kuwa na wasiwasi, wakishangaa kungetukia nini adui wakiona na kuchukua vilivyokuwa katika mabohari haya makubwa. Kwa sababu hiyo ndugu waliokuwa wanasimamia mabohari wakaanza kutoa vitabu vitumiwe katika huduma bila kujali kama vingeweza kuangushwa kwa mchango au sivyo.
UKUMBUSHO
Kwa kuwa tulikuwa tumekata shauri tusiache kukutana pamoja, kupatana na amri ya Yehova, ni wazi kwamba tulikuwa tukikumbuka sana kuadhimisha Ukumbusho. Siku kama hizo Gestapo (polisi) walikuwa wakifanya kazi zaidi, mara nyingi wakiwa wamejua tarehe ya Ukumbusho ama kutokana na vitabu vilivyochapwa nje ya Ujeremani au kutokana na Watchtower lililonakiliwa na mashine ya mimiografu. Barua ya siri yenye kuzungushwa pote ya Aprili 3, 1935, ilisema hivi:
“Shambulio la ghafula likifanywa wakati huu juu ya viongozi wanaojulikana wa Wanafunzi wa Biblia litafanikiwa sana. Tafadhalini toeni habari zo zote juu ya kufanikiwa kufikia Aprili 22, 1935.”
Lakini hakukuweza kuwa na mazungumzo mengi juu ya ‘habari juu ya kufanikiwa,’ kwa maana wingi wa maafisa, kama vile mmoja katika Dortmund. Waliweza kutoa habari za kwamba nyumba tu za walioaminiwa kuwa viongozi wa Bible Students Association zilikuwa zimewekwa chini ya ulinzi lakini mikutano yo yote haikufanywa. Ili watulize mambo wakaongezea kwamba “washiriki wenye kuongoza na wenye bidii wa Wanafunzi wa Biblia katika wilaya hii tayari wako katika ulinzi kifungoni kwa hiyo hakuna mtu aliyebaki kupanga mikutano hiyo.”
Walakini, makachero walikuwa wanakosea, kwa maana muda mfupi ya barua hii ya siri kuzungushwa pote, sisi tulipokea nakala yake kutoka kwa rafiki aliyependa kweli aliyefanikiwa kupata habari hizo za siri. Wasimamizi wa utumishi wa majimbo walionya watumishi wote kwa muda mrefu wakawapa mashauri ya pekee juu ya namna ya kuepuka kugunduliwa na bado watii maagizo ya Bwana wetu.
Kwa hiyo wengi wakakutana pamoja mara baada ya saa kumi na mbili jioni, ijapokuwa wengine walingoja mpaka Gestapo (polisi) walipokuwa wamekwisha kuja na kwenda kabla hawajaondoka wakakutane pamoja na ndugu zao vikundi vikundi, wengine wakiadhimisha Ukumbusho usiku wa manane. Hata hivyo, idara nyingi za Gestapo zilituma ripoti zilizokuwa kama ile iliyotumwa kutoka Dortmund. Walakini, sikuzote akina ndugu walikuwa tayari kama wakitokewa kwa ghafula, na hili lilikuwa jambo jema. Walijaribu kuunganisha kuhudhuria kwao Ukumbusho na utendaji fulani wa kila siku usiodhuru wala si kuhudhuria mikutano ya kila juma peke yake, na mara nyingi hii iliwaepusha na kukamatwa. Franz Kohlhofer wa karibu na Bamberg anatoa habari hizi:
“Siku hiyo wapelelezi walifanya kazi nyingi zaidi wakichungulia nyumba za mashahidi wa Yehova wakitumaini kushika wengine wao wakiendesha utendaji haramu kisha wawakamate. . . . Tulikuwa tumeamua siku kadha kabla ya hapo tukutane pamoja kwa ajili ya mwadhimisho huo nyumbani kwa ndugu mmoja aliyefuga nguruwe Kila mtu alipaswa alete kikapu kilichojaa maganda ya viazi na takataka nyingine. Haya yote yalipaswa yafanwe haraka, kwa kuwa Gestapo (polisi) wangeweza kutokea wakati wo wote Basi, tukaleta karata zetu za kuchezea pia tuweze kuhadaa (kudanganya) polisi wakitutokea kwa ghafula. Na lo! ebu wazia lililotukia! Mara ile ile ndugu alipokuwa amemaliza sala yake ya mwisho mlango ukabishwa. Lakini wakati huo sisi wanne tukawa tumeketi kuzunguka meza kwa upole tukicheza karata. Walishangaa sana tulipokuwa tukiwakodolea macho kwa unyamavu na unyofu. Kwa kuwa walishindwa kutupata wakati unaofaa, ikawalazimu kuondoka bila ya kutimiza walilokuwa wameondoka wakafanye.”
—Kutoka 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses.