Historia ya Mashahidi wa Yehova katika Nyakati za Kisasa
—Ujeremani (Inaendelea)
“MWAKA wa 1941 watu kadha wenye kupendezwa walisema wanataka kubatizwa. Tulipoona kwamba kulikuwa na watu kadha wenye tamaa iyo hiyo katika ujirani tukaanza kutafuta mahali panapofaa tukapapata katika Dehme karibu na Mto Weser. Baada ya kila jambo kufikiriwa na kupangwa kwa uangalifu, ubatizo ukapangwa uwe wa Mei 8, 1941. Akina ndugu na wataka kubatizwa tayari walikuwa huko mapema asubuhi. Watu wengine walidhani tulikuwa kikundi cha watu wanaofurahia kuogelea. Halafu wengine wakatumwa wakalinde ili mtu ye yote asitutokee kwa ghafula nasi baada ya kuzungumza juu ya ubora wa ubatizo tukasali kwa Yehova. Kisha watu 60 wakabatizwa mtoni. Wengine, waliokuwa wazee mno au wagonjwa-wagonjwa hata wasiweze kuingia katika maji ya baridi, walibatizwa faraghani katika birika la kuogea, jumla ya waliobatizwa siku hiyo wakawa watu 87.
KAANZA KUWINDWA
Albert Wandres alikuwa amekuwa mmoja wa wasimamizi wa utumishi wa jimbo hata kabla ya Oktoba 7, 1934, jina lake likajulikana sana na Gestapo (polisi). Yeye hakukamatwa na watesi wake mpaka baada ya kuwindwa kwa miaka mitatu na nusu. Na tusikilize Ndugu Wandres anapotuambia baadhi ya mambo aliyoona katika utendaji wake wa siri.
“Nilipofika Kassel, mtumishi wa kundi, Ndugu Hochgrafe, akaniambia: ‘Huwezi kukaa hapa. Ondoka mara moja. Gestapo (polisi) wamekuwa wakija nyumbani hapa kila asubuhi kwa juma nzima.’ Tukakubaliana atangulie mbele yangu kwa karibu mita 50 anionyeshe njia ya mahali ninapoweza kuviacha vitabu. Kabla hatujaweza kwenda zaidi ya mita 200 kando kando ya Kastanienallee penye kupendeza mawakili wa Gestapo (polisi) wanaomfahamu sana mtumishi wa kundi wakatukaribia. Kwa kuwa mimi nilikuwa nikifuata nyuma karibu mita 50, niliweza kuona kicheko chao cha dharau lakini hawakumsimamisha. Baada ya dakika chache vitabu ambavyo kwavyo akina ndugu wangeweza kutiwa nguvu imani yao vikawa vimeletwa mahali salama kwa mara nyingine.
“Wakati mwingine nilikuwa nimebeba vikasha vya kuchukulia nguo vilivyokuwa na vitabu katika Burgaolma karibu na Wetzlar. Ilikuwa saa tano usiku giza likiwa tititi. Ilikuwa vigumu kwa ye yote kuniona lakini bado nilikuwa nikijisikia ninatazamwa. Nilipofika nilikokuwa naenda, nikashauri ndugu wafiche vikasha hivyo mahali salama. Karibu na saa 11:30 asubuhi yake sajini wa polisi wa mjini akaja. Nilikuwa nimesimama katikati chumbani nikiwa ndio sasa najitayarisha kuogo alipomgeukia dada akasema: ‘Jana jioni mtu fulani mwenye vikasha viwili vizito alikuja hapa. Bila shaka mmepata vitabu tena. Mmeviweka wapi?” Dada akajibu: ‘Mume wangu amekwisha kwenda kazini. Nami sijui lililotukia jana jioni maana sikuwa nyumbani!’ Sajini akajibu: ‘Usipovitoa vikasha hivyo kwa moyo wa kupenda, itatulazimu tupekue nyumba. Naenda kumleta jumbe (mayor), maana bila yeye siwezi kupekua. Lakini wewe huruhusiwi kutoka nyumbani mpaka nitakaporudi.’ Wakati wa mazungumzo haya yote mimi nilikuwa nimesimama chumbani kati-kati nikishangaa sababu gani wakili huyo alikuwa mkavu wa macho namna hiyo na sababu gani hakusema nami hata kidogo. Nikaweza kukisia alikuwa kana kwamba amepofushwa. Alipoondoka akamlete jumbe, nikajitayarisha kuondoka mara moja. Nikatoka nje nikangoja nyuma ya nyumba mpaka jumbe na sajini wa polisi wakaingia nyumbani upande wa mbele. Jirani walioniona bila shaka walifurahi kwamba nilitoroka. Nikamaliza kuvalia vichakani nikakimbia upesi kama nilivyoweza kuelekea kituo cha magari-moshi kilichofuata nikazidi kukimbia.”
Wasimamizi wengine wa utumishi wa jimbo waliona mambo yale yaliyolingana na hayo.
Wakati wa miaka ya 1934 mpaka 1936 wachungaji waaminifu walikuwa wakisaidia ndugu zao katika Ujeremani yote, wakiwatia moyo washiriki kuhudhuria mikutano na, ikiwezekana, katika pande zote za utumishi, yajapokuwa mateso. Wakati huo kesi ilifanywa katika Halle Desemba 17, 1935, juu ya Balzereit, Dollinger na wengine saba walioonwa kuwa ndugu “wakuu.” Huo ndio uliokuwa mwisho wa mbio ya Kikristo kwa karibu nusu yao.
Ndugu wengi walikubali waziwazi mambo waliyokuwa wamefanya kuendeleza faida za Ufalme wakiwa katika hali zenye kujaribu walipokuwa katika kesi kadha zilizofanyiwa Ujeremani wakati huo. Lakini, watu hawa waliokuwa wakifanyiwa kesi katika Halle walikataa kwamba hawakufanya lo lote lililokatazwa na serikali. Balzereit, alipoulizwa na mwenyekiti yeye angesema nini, akasema kwamba mara marafuku ilipotangaza katika Bavaria yeye alitoa maagizo kazi isifanywe huko, na kwamba ndivyo ilivyokuwa katika maeneo mengine. Akasema kwamba yeye hakutoa maagizo wakati wo wote akitia mtu ye yote moyo aidharau marufuku.
Muda mfupi baadaye Rutherford akaandika barua ifuatayo kwa ndugu Wajeremani:
“Kwa watu wa Yehova waaminifu katika Ujeremani:
“Yajapokuwa mateso mabaya yanayowapata, na upinzani mkuu unaoletwa na mawakili wa Shetani katika nchi hiyo, inafurahisha kujua Bwana angali ana maelfu wachache katika nchi hiyo wanaomwamini Yeye na wanaoendelea kuutangaza ujumbe wa ufalme Wake. Uaminifu wenu kwa kukaa imara kuwapinga watesi na kuendelea kuwa waaminifu kwa Bwana unatofautiana kabisa na hatua iliyochukuliwa na yeye ambaye hapo kwanza alikuwa msimamizi kwa ajili ya Sosaiti katika Ujeremani, na wengine walioshirikiana naye. Majuzi nilipewa nakala ya ushuhuda uliochukuliwa katika kesi ya wale watu katika Halle nami nastaajabu kuona humo kwamba hata mmoja kati ya waliokuwa kesini wakati huo hakutoa ushuhuda wa uaminifu na wa kweli kwa jina la Yehova. Hasa ulikuwa wajibu wa aliyekuwa msimamizi Balzereit kutoa ushuhuda juu ya Bwana na kujitangaza kuwa upande wa Mungu na ufalme wake katikati ya upinzani wote, lakini hata neno moja hakulisema akionyesha anamtegemea Yehova kabisa. Mara nyingi mimi nimekaza fikira zake kwenye mambo ambayo yangeweza kufanywa katika Ujeremani akanihakikishia kwamba alikuwa anajitahidi sana kutia akina ndugu moyo waendelee kutoa ushuhuda. Lakini kwenye kesi alisema kwa mkazo kwamba hakuna lililofanywa. Ni kazi bure kwangu kuendelea kuzungumza jambo hilo. Nitamalizia kwa kusema kwamba Sosaiti haitakuwa na uhusiano wo wote naye tena, wala na ye yote kati ya wale waliokuwa na nafasi ya kutolea jina la Yehova na ufalme Wake ushuhuda wakati huo lakini wakakosa kufanya hivyo. Sosaiti haitajaribu hata kidogo kuwafungua kifungoni, hata ikiwa na uwezo wa kufanya lo lote.
“Acheni sasa wote wale wanaopenda Bwana wamwelekee Yeye, Yehova na Mfalme Wake, na waendelee kuwa waaminifu na imara upande wa ufalme, hata kama mtapatwa na upinzani wa namna gani. . . . ”
Jambo hili lilizungumzwa katika toleo la Kijeremani la Watchtower la Julai 15, 1936 kuonya wale wanaotaka kwa unyofu wa moyo kuwa mashahidi waaminifu kwa ajili ya Yehova chini ya hali zote.
Ijapokuwa ndugu wengi waaminifu katika Ujeremani walihukumiwa vifungo vya kufikia miaka mitano, Balzereit alihukumiwa kifungo cha miaka miwili na nusu na Dollinger miaka miwili. Alipoisha kutumikia kifungoni Balzereit akatiwa katika kambi ya mateso ya Sachsenhausen, ambako aliaibishwa sana. Alikuwa ametia sahihi juu ya tangazo lililomwambia aseme hatashirikiana na akina ndugu naye akaacha kushirikiana nao kabisa. Kwa sababu ya mwenendo wake akafunguliwa karibu mwaka mmoja baadaye, lakini wakati huo aliaibishwa sana, kwa maana askari wa SS pia walichukia wasaliti. Askari wa SS wenyewe ndio waliompa jina “Beelzebuli,” na wakati mmoja askari wa SS alimwagiza asimame mbele ya ndugu zake wote, waliokuwa karibu ndugu 300 kambini wakati huo, kisha arudie kusema ametia sahihi juu ya tangazo lenye kusema asishirikiane na mashahidi wa Yehova, akafanya hivyo!
Mwaka wa 1946, ambao kufikia wakati huo Balzereit alikuwa amekuwa mpinzani mbaya sana wa kweli, aliandika barua kwa wakuu wa malipo akifunua nia ya ukatili aliokuwa nao kabla kesi haijafanywa. Hivyo ukafika mwisho wa kipindi chenye giza katika historia ya watu wa Mungu katika Ujeremani, ambacho kilikuwa kimekwisha anza miaka ya 1920.
GESTAPO WASHAMBULIA
Miezi sita ya kwanza ya mwaka wa 1936 makachero wa Serikali walitunga faili kubwa yenye anwani za watu waliotiliwa mashaka kuwa mashahidi wa Yehova au angaa kuwa rafiki zao. Faili hii kwa kadiri kubwa ilikuwa yenye anwani zilizopatikana katika kitabu Daily Heavenly Manna, kilichochukuliwa wakati nyumba zilipokuwa zikipekuliwa. Hata masomo ya pekee yalifanywa kwa ajili ya mawakili wa Gestapo (mapolisi). Walifundishwa namna ya kuongoza funzo la Mnara wa Mlinzi; walipaswa wajifunze kwa uangalifu makala za karibuni zaidi za Mnara wa Mlinzi waweze kujibu maulizo kana kwamba walikuwa ndugu. Mwishowe, hata walipaswa kusali. Haya yote yalikuwa na kusudi la kuingia ndani ndani ya tengenezo ikiwezekana na kuliharibu tokea ndani.
Anton Kotgen wa Munster anaeleza kwamba, baada ya kumtolea bibi ‘mwenye urafiki’ vitabu, alikamatwa mara hiyo akatiwa gerezani. Wakati uo huo, Ndugu Kotgen anaendelea kusema, “Mawakili wa Gestapo (au mapolisi) walimjia mke wangu aliyekuwa nje katika bustani. Wakasema wao ni ndugu, lakini kwa kusudi la kupata majina ya ndugu wengine. Walakini, mke wangu akagundua hila yao akawaeleza waziwazi kwamba wao ni mawakili wa Gestapo.” Lakini Gestapo (mapolisi) hawakutambuliwa kila mara katika wakati unaofaa.
“Kwa sasa Gestapo walikuwa wamepata habari kwamba tulikuwa tukikutana bustani zilimowekwa jamii za wanyama mbalimbali wakiwa wamefungwa vitunduni nao wakawa wamekwisha pata habari nyingine nyingi juu ya tengenezo letu. Habari hizi zilipatikana kwa njia nyingi, kutia ndani na njia ya kutisha kwamba wasipoambiwa ilivyokuwa mambo yangekuwa mabaya. Ndugu Klohe anatuambia hivi:
“Siku chache baadaye maafisa watano wenye bastola wakatokea kwa ghafula, wakaniambia nivae nguo zangu za kiraia, wakanipeleka mahali palipo karibu na kidimbwi cha samaki wadogo wenye rangi ya dhahabu ambapo Ndugu Carduhn alikodisha viti vyake vya bustani. Wao hawakumdhania kuwa mmoja wa mashahidi wa Yehova, hata hivyo. Sasa ikawa mimi ndimi nitakayekuwa ‘chambo’ cha kunasia ndugu zangu ambao mwishowe wangetokea wakija kwenye mkutano uliopangwa uwepo na ambao sasa Gestapo walikuwa wamepata habari zake.
“Nilipokuwa tu namaliza kuketi chini mahali nilipoagizwa niketi nikamwona Dada yetu Hildegard Mesch akinikaribia. Alikuwa ameshangaa sababu gani sikwenda walikokuwa, kwa maana nilikuwa nimetazamiwa nifanye hivyo, naye sasa alitaka kuona sababu gani sikwenda. Kwa kuwa mifupa yangu ya miguu ilikuwa sana kwa sababu ya mapigo niliyopata, maafisa hawakutia shaka lo lote wakati kwa ghafula nilipoinama nikikunja uso kwa maumivu wakati ule ule alipokuwa anapita upande mwingine wa kijia huku mimi nikijaribu kumwonyesha ishara kwa macho yangu kwamba Gestapo walikuwa katika bustani za wanyama. Akafahamu, akasita kwa nukta moja tu kisha akamrudia Ndugu Varduhn, akamweleza hali ilivyokuwa. Ikawa hatari kubwa zaidi kwa Ndugu Winkler, aliyekuja muda mfupi baada ya hapo akakaa kitako juu ya kiti kitupu bila ya kuwaza lo lote linaweza kutokea. Muda mfupi sana baada ya hapo Ndugu Varduhn akamkaribia, akaomba malipo ya kiti alichokalia na wakati ule ule akampasha habari kwamba mawakili wa Gestapo wamo katika bustani za wanyama. Ndugu Winkler upesi akasimama, akaacha mfuko wake nyuma akakimbia mawakili wa Gestapo wakiwa kila mahali, kama ilivyoelekea kuwa. Nikapata habari kwamba baadaye usiku huo aliingia nyumba mwa Ndugu Kassing ambako kikundi cha mawakili wa Gestapo kilikuwa kikimngojea kikampeleka ulinzini.”
Baada ya siku chache karibu nusu ya wasimamizi wa utumishi wa majimbo katika Ujeremani, pamoja na maelfu ya ndugu na rafiki wengine, walikuwa wamekamatwa Hii ilitia ndani na Ndugu Georg Bar, anayetoa habari hizi:
“Kila jioni karibu na saa nne nikawa nasikia wafungwa wakitolewa katika vijumba vyao mbalimbali vya kifungo. Muda si muda nikawa nawasikia wakipigwa katika orofa ya chini; nilisikia vilio vyao na kuwasikia wakilia kwikwi. Kila jioni niliposikia milango ya vijumba vya kifungo ikifunguliwa nilikuwa nikiwaza, Sasa ni zamu yangu. Lakini sikusumbuliwa mpaka mwishowe siku ya nne au ya tano hivi karibu na saa 12:00 nilipoitwa nihojiwe. Wakati huu askari wa SS ndiye aliyeniongoza chumbani mwake akaniambia niketi. Kisha akasema: ‘Twajua waweza kutupasha habari zaidi.’ Akasimama, akachukua kalamu ya mate akaichonga katika ukingo cha takataka, akaendelea na habari yake ndogo: ‘Mimi sitakufanyia magumu; njoo.’ Akaniomba nikaribie kimeza chake, akanionyesha kurasa kadha zilizoandikwa kwa taipureta akaniruhusu nizisome. Ilikuwa orodha ya watumishi wote wenye kusafiri katika Ujeremani, jina langu likiwa mwisho. Nikayasoma majina ya makundi tuliyokuwa tumezuru, na pia majina ya ndugu wa huko. Nikasoma imeandikwa ni vitabu vingapi, gramofoni na sahani za santuri tulizokuwa tumeagiza. Michango na pesa nyingine pia tulizokuwa tumetoa zilikuwa zimepangwa orodhani. Nilishangaa sana. Mpango wetu wa siri ndio huu sasa uliokuwa mikononi mwa Gestapo (mapolisi). Kwa kweli niliduwaa kwa muda. Gestapo waliweza kupata maandishi haya wapi? nikajiuliza. Sikuweza kutilia mashaka ukweli wa ripoti hiyo maana utendaji wangu mwenyewe ulikuwa umeandikwa orodhani kwa usahihi. Askari huyu wa SS wa Dresden, Bauch, aliyekuwa akiongoza kesi, akanipa wakati wa kuwaza. Uso wangu ukaonyesha hali ya kupumbaa niliporudi kuketi. Halafu akasema, ‘Kwa kweli, sasa hakuna sababu ya kuendelea kunyamaa.’
“Nikawa nateseka kwa miezi mingi nilipowaza juu ya mahali ambapo Gestapo walipata maandishi yetu. Baadaye nikapata habari kwamba maagizo yetu yote, ripoti na pesa tulizokuwa tumetoa zilikuwa zimewekwa kwa uangalifu katika faili katika Berlin. Baadaye zikapatikana zikachukuliwa na Gestapo.”
Bila shaka “barua ya wazi” ilipoenezwa Gestapo walishangaa kwa kuwa hawakuwa wakiitazamia, kwa maana walikuwa wamejivuna miezi mingi kwamba walikuwa wameangamiza tengenezo kabisa. Hii ikawaongezea wasiwasi. Ilikuwa kana kwamba mtu fulani alikuwa amevuruga kichuguu cha mchwa. Wakakimbia-kimbia hapa na pale wakiwa wamevurugika kama wenye wazimu wasio na mradi wa wazi, hasa watu kama Theiss katika Dortmund.
Lakini wakati wa Theiss pia wa kufanikiwa ulikuwa umefikia kikomo. Kwa maana Theiss alidhani hapaswi kuwa na rehema kwa alivyokuwa akitenda mashahidi wa Yehova, akaagiza nyumba moja ya mtu aliyekuwa ndugu hapo kwanza aitwaye Wunsch ipekuliwe siku moja, lakini kwa sasa huyu alikuwa ameiacha kweli akawa anatumikia kama sajini meja (askari mkuu) katika jeshi la hewani la Hitler. Wunsch aliporudi nyumbani, mkewe akamwambia kwamba nyumba imepekuliwa. Moja kwa moja akamwendea Theiss katika Dortmund akamwuliza sababu gani amefanya hivyo. Kwa kushtuka kuona sajini meja wa jeshi la hewani amesimama mbele yake, Theiss akasema kwa kukokoteza maneno: “Wewe u pamoja na Wanafunzi wa Biblia?” Wunsch akajibu: “Nilisikia baadhi ya hotuba zao, lakini nilikwenda kila mahali nilipoweza kusikia jambo fulani.” Sasa Bi. Theiss akakatiza. Akiwa na wasiwasi, Theiss halafu akakatiza akasema: “Laiti ningalijua, nisingalianza kamwe kujaribu kuwaangamiza Wanafunzi wa Biblia. Hii inaweza kumtia mtu wazimu. Mtu anadhani amefunga mmoja wa hayawani hao halafu kwa ghafula wengine kumi wanatokea wakija mbio. Nasikitika kwa kulianza jambo hili.”
Isidhaniwe kwamba dhamiri ya wakili huyu wa Ibilisi ilitulia. Bali, kitabu Kreuzzug gegen das Chsistentum (Pigano la Kuuondoa Ukristo) kilimalizia kwa kusema hivi chini ya kichwa kidogo “Umeshinda wewe, Mgalilaya!”:
“Tunapata habari kwamba Theiss wa Dortmund, ambaye ametajwatajwa mara nyingi, amekuwa akipatwa na maumivu ya kuogofya ya dhamiri kwa sababu ya matendo yake maovu na kwamba mashetani wanazidi kumtia wazimu pole kwa pole. Miezi kadha iliyopita alijivunia ‘kuvunja-vunja’ mashahidi wa Yehova 150. Yeye ndiye kasema hivi kwa dharau: ‘Yehova, mimi nakutangazia wewe dhihaka ya milele; na aishi milele mfalme wa Babeli.’
“Walakini, sasa yeye amewaheshimu watu hawa, ameahidi hatawatesa tena naye anawaomba sana wamwambie inampasa afanye nini aiepuke adhabu inayoonekana ataipata na kujiondolea mateso mabaya sana ya akilini. Yeye asema kwamba alipokea ‘amri ya kuwatenda vibaya kutoka juu’ na sasa ataka kuacha, kwa maana mashahidi wa Yehova wapya wanazidi kutokea wakati wote. Kama vile Yuda alipoisha kusaliti Bwana kwa adui, Theiss anajaribu kutubu asiweze. Viko visa, ingawa vichache, ambapo mawakili wa Gestapo na wanachama wengine wamefadhaishwa sana na uthabiti wa mashahidi wa Yehova hata wakaona kosa la njia zao wakaacha kazi zao.”
YALIYOTOKEA BAADA YA KUSANYIKO LA PARIS LA 1937
Kama vile kusanyiko la mwaka uliotangulia lililofanyiwa Lucerne, kusanyiko la mwaka wa 1937 lililofanyiwa Paris lingehudhuriwa na Ndugu Rutherford. Wakati huu ni ndugu wachache tu walioweza kwenda Ujeremani. Adui walikuwa wametia mapengo makubwa kati ya akina ndugu. Ndugu Riffel, mmoja wa wachache walioweza kuhudhuria, baadaye alieleza kwamba katika Loorrach na ujirani wake peke yake ndugu na dada 40 walikuwa wamekwisha tiwa gerezani, kumi kati yao wakanyongwa, wakauawa kwa gas au kwa kupigwa risasi, au wakanyimwa chakula hata wakafa au wakafa kwa sababu ya kupasuliwa miili yao kwa sababu madaktari walitaka kujifunza mambo ya matibabu kwa kuchunguza miili yao iliyopasuliwa.
Azimio jingine likakubaliwa Paris, kwa mara nyingine likaonyesha hali yetu safi na isiyovunjika kuhusu Yehova na ufalme wake ukiwa chini ya utawala wa Yesu Kristo nalo likakaza fikira waziwazi kwenye mateso ya ukatili katika Ujeremani, likiwaonya wenye kuwatesa juu ya hukumu ya Mungu yenye haki.
Ndugu Dietschi alikuwa ametumikia katika utendaji wa siri kwa miaka mingi bila kukata tamaa wala hakurudi nyuma ijapokuwa kulikuwa na hatari. Alihukumiwa kifungo cha miaka minne, lakini yeye hakuwekwa katika kambi ya mateso baada ya kutumika katika kifungo chake kama ndugu zake wengi walivyokuwa wamefanyiwa.
Mwaka wa 1945, wakati kazi ilipoanza kutengenezwa upya, yeye alikuwa kati ya ndugu wa kwanza kutumikia makundi kama “mtumishi kwa akina ndugu.” Lakini, jambo la kusikitisha ni kwamba, miaka kadha baadaye alianza kukuza mashauri yake mwenyewe akaliacha tengenezo la Yehova.
Lakini na turudie mwaka wa 1937. Mapengo yenye hatari yalipotokezwa tena kati ya akina ndugu, Ndugu Wandres alijaribu kuyaziba, angaa kwa muda, ili kuhakikisha akina ndugu wanapata chakula chao cha kiroho. Yeye alikwenda kwa eneo la Ndugu Franke alipokamatwa, lakini sasa akajiona ni mwenye madaraka ya kuangalia pia maeneo yasiyo na watu wa kuyaangalia, kwa hiyo akamwomba Dada Auguste Schneider wa Bad Kreuznach awape chakula cha kiroho ndugu katika Bad Kreuznach, Mannheim, Kaiserslautern, Ludwigshafen, Baden-Baden na eneo lote la Saar. Dada huyu akapewa jina jingine kama ndugu wote waliopaswa kusafiri katika wakati huu wenye magumu mengi sana; kuanzia wakati huo akawa “Paula.”
Akitambua kwamba adui walikuwa wamekasirika zaidi katika Saxony, Ndugu Wandres akamwomba Hermann Emter wa Freiburg aangalie eneo hili. Septemba 3, wote wawili wakasafiri pamoja kwenda Dresden. Ingawa Ndugu Wandres hakuwa amekwisha kwenda huko wakati mwingine wo wote, Gestapo walikuwa wakiwangojea. Ndipo kuwindwa kwake kulikokuwa kumechukua miaka mitatu kulipomalizika!
Kuelekea katikati ya Septemba na kupatana na mipango aliyofanya na Ndugu Wandres, “Paula” alikuwa akingoja katika kituo cha magari-moshi katika Bingen akiwa na mifuko miwili mikubwa ya nguo iliyojawa na vitabu naye hakutazamia lo lote linaloweza kutokea. Kwa ghafula bwana mmoja akamkaribia akasema: “Salamu, Paula! Albert hatakuja nawe lazima uende pamoja nami!” Ilikuwa kazi bure kujaribu kupinga, kwa maana mgeni huyo alikuwa wakili wa Gestapo (mapolisi). Akaendelea kusema: “Hakuna haja ya kumngoja Albert; tumekwisha mkamata tukachukua pesa zake zote. . . . Bw. Wandres alisema ungekuwa hapa ukiwa na mifuko miwili mikubwa ya nguo na kwamba wewe naitwa Paula!” Mpaka leo hii haijulikani Gestapo walipata habari hizi wapi. Lakini hii ilikuwa njia ya kawaida sana waliyotumia Gestapo, yaani, kudai kwamba ndugu fulani walikuwa wamesema mambo fulani ili wafanye ndugu waache kuaminiana, kuwafanya wajitenge na “wasaliti” hao.
Heinrich Kaufmann wa Essen alipokwisha kutumika katika kifungo chake akavaa mavazi yake ya kiraia aliambiwa wazi na wakili mwenye kushughulika na wavunja sheria kwamba atapelekwa katika kifungo cha ulinzi. Walakini, kwanza wakampeleka nyumbani kwake ambako hakuwa amekwenda kwa mwaka mmoja na nusu, wakamwuliza: “Ungependa kuacha imani yako umfuate Hitler?” Wakati uo huo wakamwonyesha funguo za nyumba yake na kisanduku cha ratili 20 za vyakula, wakimwahidi kwamba mke wake pia angerudishwa kutoka kambi ya mateso ya Ravensbruck. Ndugu Kaufmann akakataa toleo hilo.
Nyakati nyingine kulikuwa na majaribio ya kupumbaza akina ndugu kwa hila, kama anavyoeleza Ernst Wiesner. Muda mfupi kabla hajafunguliwa karatasi iliwekwa mbele yake. Maneno yaliyoandikwa humo yalikuwa ya kawaida tu hata alipoisha kuisoma kwa uangalifu akaamua angeweza kuitia sahihi. Lakini sasa ndipo hila ikaingia. Ndugu Wiesner alipaswa atie sahihi mwishoni mwa ukurasa huo, lakini sehemu ya mwisho ya ukurasa ilikuwa haina maandishi yo yote. Hakukuwa na shaka kwamba Gestapo (polisi) baadaye wangeongeza mambo mengine ambayo Ndugu Wiesner asingaliweza kutilia sahihi akiwa na dhamiri njema. Lakini yeye akagundua mara moja walilokuwa wakitaka naye akatia sahihi yake pale chini ya maandishi yaliyochapwa kwa taipureta, kabla hawajaweza kumzuia. Kwa sababu hiyo hakufunguliwa ingawa alitia sahihi, bali alipashwa habari na makachero juma tatu kabla ya kumalizika kwa kifungo chake kwamba kwa mara nyingine angehamishwa apelekwe kwenye kambi ya mateso.
KAMBI ZA MATESO—SHIMO KUBWA LILILO WAZI KABISA
Katika vierteljahresheft fur Zeitgeachichte (Gazeti la Kihistoria la kila miezi mitatu) Hans Rothfels anaandika hivi katika kikaratasi cha pili cha 1962: “Kutiwa katika kambi za mateso ndiko kulikokuwa sehemu ya mwisho na iliyo ngumu zaidi kwa Wanafunzi wa Biblia wenye Bidii wakati wa kipindi chao cha kutaabishwa na Wasoshialisti wa Kitaifa. . . . ”
Wenye kufariji wengi ulikuwa uhakika wa kwamba tayari walikuwako ndugu waaminifu waliofungwa walio fanywa imara na mateso. Kuwa pamoja nao na kuangaliwa nao kwa njia yenye upendo kulifariji na kutia nguvu mioyo ya wale waliofungwa karibuni.
Serikali ilifikiria kuongoza mateso ya ndugu zetu wakati wo wote imara yao ilipoonekana serikali ikapashwa habari. Ikawa kwamba kwa muda fulani mashahidi wa Yehova walikuwa wakipigwa viboko 24 kwa kawaida kwa kiboko cha chuma, zaidi ya kuteswa kwa njia nyingine za ukatili sana walipofika kambini. Kazi yao ya utumwa ilianza 10:30 asubuhi, wakati kengele ya kambi ilipolia kuamsha kila mtu. Muda mfupi baada ya hapo machafuko yakatokea: kutandika vitanda, kuoga, kunywa kahawa, kuitwa majina ya waliopo—haya yote yakifanywa haraka haraka. Hakuna aliyeruhusiwa kufanya jambo lo lote kwa mwendo wa kawaida. Walipiga miguu kiaskari wakaitwe majina ya kuonyesha kama wote wapo, kisha wakatoka nje kujiunga na wengine wenye kazi mbalimbali. Lililofuata sasa lilikuwa jambo la kutazamisha kweli kweli: kuchukua changarawe, mchanga, mawe, miti, sehemu nzima za nyumba za askari, nayo haya yalifanywa mchana kutwa—tena haraka haraka. Wanyapara, ambao walikuwa wakipaza sauti kupigia wafungwa kelele saa zote na kuwataabisha hata kufikia upeo wa uvumilivu wao, walikuwa ndio watu wabaya kabisa ambao Hitler angeweza kutumia.
Kukumbuka kwamba Yesu alipatwa na mambo kama hayo kuliwafariji kukawatia moyo na kuwapa nguvu za kustahimili wakitendwa kikatili.
Ili mambo yawe yakibadilika-badilika, “mazoezi ya adhabu” yalifanywa nyakati nyingine bila sababu ya pekee. Mara nyingi akina ndugu walilazimishwa kukaa bila chakula. Lilikuwa jaribu kweli kweli wakati ndugu mchovu alipolazimishwa asimame wima miguu yote miwili ikiwa pamoja (atensheni) kwa saa nyingine nne au tano katika ua badala ya kuketi ale chakula, kwa sababu tu mmojawapo wa akina ndugu alikuwa hana kifungo kimoja katika koti lake au kwa sababu ya kukosea sheria kidogo tu.
Mwishowe walikuwa wakiruhusiwa kwenda kulala, na waliweza kufanya hivyo ikiwa tu njaa haikuwa kali sana. Lakini siku hazikuwa za kulala tu. Mara nyingi mmoja au wengi wa “viongozi wa safu za nyumba” waliokuwa waovu walikuwa wakitokea usiku wa manane kutisha wafungwa. Mambo haya yakawa yakianza nyakati nyingine risasi zikipigwa juu hewani au katika mbao za paa za majengo ya askari. Halafu wafungwa wakawa walilazimishwa kukimbia-kimbia hapa na pale katika majengo ya askari, au, nyakati nyingine, kuyapanda majengo haya, wakiwa na shati zao za usiku, nalo jambo hili likawa linafanyika kwa muda ambao “viongozi wa safu za nyumba” walitaka. Inafahamika kwamba ndugu waliokuwa wazee zaidi ndio waliotaabika zaidi kwa kutendwa hivyo, wengi wakapoteza maisha zao.—Kutoka 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses.