Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w75 11/15 kur. 523-528
  • Historia ya Mashahidi wa Yehova katika Nyakati za Kisasa —Ujeremani (Inaendelea)

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Historia ya Mashahidi wa Yehova katika Nyakati za Kisasa —Ujeremani (Inaendelea)
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Vichwa vidogo
  • JARIBU LA UAMINIFU KWA WENZI WA NDOA
  • KUFANYA WANAFUNZI HATA KATIKA KIJUMBA CHA KIFO GEREZANI
  • CHAKULA CHA KIROHO KATIKA KAMBI ZA MATESO
  • UMATI WA WAFUNGWA WAONDOKA KAMBINI HARAKA HARAKA
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
w75 11/15 kur. 523-528

Historia ya Mashahidi wa Yehova katika Nyakati za Kisasa

​—Ujeremani (Inaendelea)

WENYE kuhukumiwa kufa sio tu waliotiwa moyo na ndugu waliokuwa nje; wale waliokuwa nje wakiwa huru walitiwa moyo mara nyingi hata zaidi na ndugu zao waliokuwa gerezani. Dada Auschner wa Kempten anahakikisha hili. Alipokea barua kutoka kwa mwana wake mwenye umri wa miaka 21 Februari 28, 1941, iliyokuwa na mistari mifupi inayofuata iliyoandikwa kwa ndugu yake mwenye umri wa miaka kumi na minane na nusu: “Ndugu yangu mpendwa. Katika barua yangu ya mwisho nilikuelekeza kwenye kitabu fulani nami natumaini umethamini niliyokuambia, kwa maana yanaweza kukusaidia wewe tu.” Miaka miwili na nusu baadaye Dada Auschner akapokea barua ya kumwaga kutoka kwa mwana wake huyo mdogo. Mwana huyo alithamini yaliyoandika na kaka yake akamfuata kwa uaminifu mpaka kufa.

Ndugu wawili Ernst na Hans Rehwald wa Stuhm, Prussia ya Mashariki, walisaidiana kwa njia iyo hiyo. Baada ya Ernst kufikishwa katika mahakma ya kijeshi na kuhukumiwa kufa, alimwandikia ndugu yake Hans akiwa katika kijumba alimokuwa akingojea kufa naye ndugu yake akiwa katika gereza Stuhm: “Mpendwa Hans, Ikiwa jambo lili hili litakupata wewe, kumbuka uwezo wa sala. Mimi siogopi hata kidogo, maana amani ya Mungu imo moyoni mwangu.” Muda mfupi baadaye ndugu yake akawa katika hali ile ile na, ingawa alikuwa mwenye umri wa miaka kumi na tisa tu wakati huo, akauawa.

JARIBU LA UAMINIFU KWA WENZI WA NDOA

Lilikuwa jambo la kuvutia kuona namna watu wa ukoo wa karibu walivyotia wapendwa wao moyo wasiyumbe-yumbe katika ukamilifu wao. Dada Hohne wa Frankfurt/Oder alifuatana na mumewe kwenda kwenye kituo cha magari-moshi alipopokea agizo la kuingia jeshi, asimwone tena. Maneno yake ya mwisho kumwambia mumewe yalikuwa haya: “Uwe mwaminifu”​—naye Ndugu Hohne aliyakumbuka mpaka kufa kwake.

Katika visa vingi akina ndugu walikuwa wameoa karibuni na kama upendo wao kwa Yehova na kwa Kristo Yesu usingalikuwa wenye nguvu, bila shaka wasingaliweza kuvumilia kuwa mbali bila kusemezana na wapendwa wao. Dada wawili ambao wamekuwa wajane kwa zaidi ya miaka 32 sasa wanakumbuka nyakati hizo zenye msukosuko na kushukuru kwa msaada aliowapa Yehova. Dada Buhler na Dada Ballreich wa Neulosheim karibu na Speyer waliolewa karibu na mwanzo wa marufuku wakajifunza kweli karibu wakati uo huo. Mwaka wa 1940 waume wao wote wawili waliitwa jeshini na walipokataa kuingia utumishi wa jeshi wakakamatwa.

Dada Ballreich akawafikia wakuu wa jimbo wa uandikishaji wa jeshi katika Mannheim, akapata habari kwamba ndugu hao wawili walikuwa wamepelekwa Wiesbaden waonekane mbele ya mahakma ya kijeshi. Dada Ballreich akapata ruhusa kumtembelea mumewe kwa sharti la kwamba atajaribu kumsihi abadili nia yake. Dada Biihler alipewa ruhusa kumtembelea mumewe kwa sharti lile lile. Mara moja dada hawa wawili wakaenda Wiesbaden. Dada Biihler asema hivi:

“Ni vigumu kwangu kueleza namna kuungana kwetu tena kulivyokuwa kwenye masikitiko. Akaniuliza (yaani mumewe): ‘Mbona umekuja?’ Nikajibu nimeambiwa nijaribu kumshawishi. Lakini yeye akanifariji, akanipa mashauri ya Biblia akaniambia nisiwe mwenye huzuni kama wengine wasio na tumaini bali nimtumaini Mungu wetu mkuu kabisa, Yehova. . . . Karani kijana wa mahakma aliyekuwa amefuatana nasi gerezani akatushauri tukae Wiesbaden mpaka Jumanne, nayo hiyo ndiyo iliyokuwa siku ya kusikiwa kwa kesi. Tukiwa huko bila shaka tungeruhusiwa kuhudhuria. Basi tukakaa hata Jumanne. Tukangojea barabarani mpaka waume zetu walipoelekezwa barabarani kama wahalifu stadi, wakifuatwa na askari wawili wenye bunduki zilizojazwa risasi. Hiyo kweli ilikuwa tamasha kwa wanadamu na malaika. Dada Ballreich na mimi tukasonga mbele. Tukaweza kuhudhuria kesi. Ilichukua punde kuliko saa moja, ikafikia mwisho wanaume hao wawili mashujaa wasio na lawama wakiwa wamehukumiwa kufa. Baada ya hapo tukaruhusiwa kuwa nao kwa karibu saa mbili katika chumba kilichokuwa katika orofa ya chini. Lakini tulipokwisha kutoka katika nyumba ya mahakma tukatembea katika barabara za Wiesbaden kama kondoo wawili waliopotea.”

Muda mfupi baadaye dada hao wawili vijana walipokea habari za kwamba waume wao wamepigwa risasi wakafa Juni 25, 1940 baada ya kutamka: “Sisi tu wa Yehova hata milele!”

KUFANYA WANAFUNZI HATA KATIKA KIJUMBA CHA KIFO GEREZANI

Inasikika vigumu kuamini inawezekana kufanya wanafunzi hata katika kijumba cha kifo gerezani, lakini Ndugu Massors asema ndivyo iliyotokea katika barua aliyomwandikia mkewe ya tarehe ya Septemba 3, 1943:

“Miaka ya 1928/30/32 nilifanya upainia katika Prague. Hotuba zilitolewa nao mji ukajazwa vitabu. Wakati huo nilikutana na msemaji wa kisiasa wa serikali jina lake Anton Rinker. Nikasema naye kwa muda mrefu. Akachukua Biblia na vitabu kadha lakini akaniambia hana wakati wa kujifunza vitu hivyo, maana lazima aangalie jamaa yake na kutafuta riziki. Walakini, akasema watu wote wa ukoo wake wanapenda dini sana, ingawa hawakuwa wakienda kanisani.

“Katikati ya mwaka wa 1940 na 1941 mwenzi mpya aliletwa katika kijumba changu gerezani kama kawaida. Alikuwa mwenye huzuni sana, lakini kila mtu anakuwa hivyo mara ya kwanza. Baada tu ya mlango wa kijumba kufungwa ndipo mtu anazinduka na kutambua yuko wapi. ‘Mimi naitwa Anton Rinker na natoka Prague,’ kaniambia mwenzi wangu mpya. Nikamtambua mara moja nikamwambia: ‘Anton, naam, Anton hunijui?’ ‘Naam, inaonekana nilikuona mahali fulani . . . ’ Baada ya muda mfupi akakumbuka kwamba nilifika kwake katikati ya miaka ya 1930 na 1932 akachukua Biblia na vitabu kadha wakati huo. ‘Ala!’ kasema Anton, ‘kumbe upo hapa kwa sababu ya imani yako? Mimi sielewi; hakuna kiongozi wa dini anayefanya hivyo. Wewe unaamini nini hasa?’ Alitaka kujua na angejua.

“‘Lakini mbona viongozi wa dini hawatuambii mambo haya?’ akauliza. ‘Hii ndiyo kweli. Sasa najua sababu ya kuja kwangu katika gereza hii. Franz mpendwa, kabla sijaingia katika kijumba hiki nilimwomba Mungu anipeleke kwa mtu mwenye kuamini, ama sivyo ningefikiria kujiua. . . .

“Juma na miezi ikapita. Kisha Anton kaniambia: ‘Kabla sijaondoka katika ulimwengu huu, Mungu na amsaidie mke wangu na watoto wangu wapate kweli, ili niweze kuwaacha kwa amani.’ . . . Siku moja akapokea barua ya mke wake yenye kusema hivi:

“‘. . . Sisi tungekuwa wenye furaha namna gani kama tu ungeweza kusoma Biblia na vitabu ulivyonunua kwa yule Mjeremani miaka kadha iliyopita. Mambo yote yamekuwa sawasawa na vile vitabu vilivyosema. Hii ndiyo kweli ambayo hatukuwa na wakati wa kuiangalia.’”

CHAKULA CHA KIROHO KATIKA KAMBI ZA MATESO

Miaka hiyo ndugu walipokuwa “peke yao,” hasa waliokuwa katika kambi za mateso, walikuwa na nafasi ndogo sana ya kupata Biblia au vitabu vingine. Walitumia jitihada zaidi kujikumbusha yaliyokuwa katika makala za maana za Mnara wa Mlinzi wakati walipopaswa kusimama saa nyingi uani, au nyakati za jioni kulipokuwa kimya kidogo katika majumba ya majeshi. Walifurahi sana sana walipoweza kupata Biblia.

Wakati ulipopita ikawezekana kupitisha kwa siri makala mpya za Mnara wa Mlinzi katika kambi za mateso. Hivi ndivyo ilivyofanywa katika kambi ya mateso ya Birkenfeld: Alikuwako ndugu mmoja kati ya wafungwa ambaye kwa sababu ya maarifa yake ya ujenzi, alifanya kazi na raia aliyekuwa rafiki ya mashahidi wa Yehova. Kupitia kwa rafiki huyu ndugu huyo alipashana habari na ndugu waliokuwa nje ya kambi nao wakampa magazeti ya karibuni zaidi ya Mnara wa Mlinzi.

Kila mtu akapanga njia tofauti, na baada ya muda fulani kukawa na Biblia kadha kambini. Ndugu mmoja alimwandikia mkewe katika Danzig kwamba angefurahia kula “mkate wa tangawizi wa Elberfelder,” halafu furushi lile jingine la chakula (ambacho akina ndugu wangeweza kupokea katika kambi hii wakati huo) lilipotumwa akapokea Biblia ya lugha ya Elberfelder ikiwa imeokwa kwa uangalifu ndani ya mkate wa tangawizi. Wengine walionana na wafungwa waliofanya kazi mahali pa kuchomea maiti. Hawa wakaeleza kwamba vitabu na magazeti mengi yalichomewa hapo, kwa hiyo akina ndugu wakafanya mipango ya siri wazipokee Biblia na magazeti hayo, kwa kubadilishana na watu hao vyakula vyao.

Wakati wa masika yenye baridi kali sana katikati ya miaka ya 1939/1940 Mashahidi walimwomba Yehova kwa sala wapate vitabu, na lo! wazia mwujiza uliotokea! Yehova alimlinda ndugu mmoja aliyeweza kupitisha kwa siri Minara mitatu ikiwa ndani ya mguu wake wa mbao, ingawa alichunguzwa kwa uangalifu. Ijapokuwa iliwalazimu akina ndugu kutambaa uvunguni mwa vitanda vyao na kusoma kwa msaada wa mwenge (tochi) huku wengine wakiwa wamesimama wakilinda kwa kutazama kuliani na kushotoni, huo ulikuwa uhakikisho wa uongozi wa ajabu wa Yehova. Yeye akiwa Mchungaji mwema haachi watu wake.

Iliendelea kuwa vyepesi pia kugawia akina ndugu katika kambi za mateso chakula cha kiroho. Daktari Kersten alisaidia sana kufanya hivyo, kwa maana alisafiri mara nyingi kutoka nyumbani kwake Sweden kwenda kwenye shamba lake katika Harzwalde na kurudi. Sikuzote akawa anaruhusu dada ambao Himmler alimpa wamfanyie kazi shambani mwake na nyumbani kwake Sweden watayarishe mifuko yake ya kuchukulia nguo. Mapatano ya siri yakawa yamefanywa kati yao kwamba dada aliyeko Sweden atakuwa akitia Minara kadha katika mifuko ya nguo ya Kersten wakati anapoitayarisha. Akiisha kufika Harzwalde alikuwa akimwambia dada mwenye kumfanyia kazi huko afungue mfuko wake atoe vilivyomo akiwa peke yake. Dada hao walipokwisha kuisoma Minara hiyo kwa uangalifu, walikuwa wakiipeleka kwenye kambi ya mateso iliyo karibu.

Shamba la Bw. Kersten katika Harzwalde lilikuwa katikati, karibu kilomita 35 kusini ya kambi ya wanawake katika Ravensbrück na karibu kilomita 30 kaskazini ya kambi ya wanaume katika Sachsenhausen. Vitu vikawa vinasafirishwa sikuzote kutoka Harzwalde na kupelekwa kwenye kambi zote mbili, kwa hiyo haikuwa vigumu kupitisha kwa siri chakula cha kiroho na kukiingiza katika kambi za akina ndugu na dada.

Kwa njia hiyo kukawa na kupashana habari sana kati ya kambi mbalimbali na nyumba za watu wenyewe ambako dada zetu walipelekwa kufanyia kazi jamaa za askari wa SS.

Ndugu Engelhardt alikuwa angali huru wakati huo naye alikuwa amewapa ndugu waliokuwa wanaishi karibu maagizo ya kujaribu kutafuta njia ya kuingiza Minara kambini. Baada ya kutatua magumu fulani, Sandor Beier wa Herford na Martha Tiinker wa Lemgo walichunguza hali ilivyokuwa kwa kutembelea tu sehemu hiyo kama vile vijana waliooana wanavyoweza kutembea. Karibuni wakaonana na akina ndugu kisha wakawa wakiwapa Minara kwa kawaida baada ya hapo. Mara ya kwanza walikutana na akina ndugu katika kaburi fulani; wakati ule mwingine, walificha magazeti katika fungu la majani makavu, au wakayapeleka kwa akina ndugu wenyewe usiku wa manane katika mahali palipochaguliwa mapema. Mahali papya pa kukutania pakapangwa pa kuleta magazeti mapya kila mara. Baada ya Ndugu Engelhardt na dada waliokuwa wakichapa na kugawa magazeti kukamatwa, ulizo lilitokea juu ya namna wale walio huru bado watakavyogawiwa chakula cha kiroho.

Wakati huu akina ndugu katika Wewelsburg walijaribu kujitafutia suluhisho wenyewe. Wakaweza kupata taipuraita, halafu mmojawapo wa akina ndugu akaitumia kuandika stencils. Ndugu mwingine alitengeneza mashine ya kunakilia ya kienyeji (mimeograph) kwa kutumia mbao. Dada waliokuwa nje wakipashana habari na ndugu hawa waliwaletea vifaa vizuri vya kunakilia. Mwishowe nakala nyingi sana za Mnara wa Mlinzi zikawa zinachapwa huko hata sehemu kubwa ya Ujeremani ya kaskazini ikaweza kugawiwa. Elisabeth Ernsting anakumbuka kwamba sikuzote yeye alikuwa akipokea nakala 50 za kugawa katika eneo lake. Hivyo kwa karibu miaka miwili, mpaka kuanguka kwa serikali ya Hitler mwaka wa 1945, iliwezekana kuwapa ndugu waliokuwa wanaishi Westfalen na wilaya nyingine Mnara wa Mlinzi.

Asubuhi moja baadhi ya wakuu wa Makachero walikuja Sachsenhausen. Shambulio lao la ghafula juu ya akina ndugu lilikuwa limepangwa vizuri. Wenye kufanya kazi ndani ya kambi waliitwa wakaagizwa wasimame uani, na huko wakahojiwa juu ya maandiko ya kila siku kisha wakapekuliwa-pekuliwa. Vitabu kadha vikapatikana. Halafu wakapigwa kama kawaida. Lakini Gestapo wakashindwa kufanya akina ndugu warudi nyuma, kwa maana Yehova alikuwa amewalisha sana wakiwa katikati ya adui zao. Waliliona waziwazi agizo lao nao hawakuogopa kutetea kwa umoja utawala wa kitheokrasi.

Ernst Seliger alijulikana kuwa ndiye mwenye kupashana habari na Ndugu Fritsche, kwa hiyo akachunguzwa kwa njia ya pekee. Yeye alijaribu kufunga, si vidonda halisi tu, bali pia vidonda vya kiroho, nayo hali yake ya unyenyekevu ya kutenda kama baba ilikuwa imesaidia sana kuleta umoja uliokuwa katika kambi hii. Lakini aliudhiwa sana na matokeo ya kuhojiwa alikofanyiwa mara ya kwanza na kwa hiyo akamwomba Yehova ampe ushindi, kwa maana yeye mwenyewe alijiona kuwa ‘ameshindwa.’ Lakini hili halikupaswa liwe jaribu la mtu mmoja tu. Wilhelm Roger wa Hilden anaieleza hali yenyewe ifuatavyo: “Sasa ikawa lazima wote wamsaidie yeye kwa maana yeye pia alikuwa amewasaidia wote.” Ndugu wote wakahakikisha maneno ya Ndugu Seliger kwamba alikuwa amegawa maandiko ya kila siku ili kuwatia moyo. Wakahakikisha kwamba walisoma vitabu ambavyo Ndugu Seliger alileta kambini na kwamba wangeendelea kutiana moyo na kuzungumza juu ya tumaini lao la wakati ujao.

Siku nne zikapita. Jumapili asubuhi Ndugu Seliger akawafikia wasimamizi wa kambi waandikiane mkataba. Anaeleza yaliyotokea: “Kwanza, nilitoa ushuhuda katika vyumba vitatu vya hospitali [alikofanya kazi kama msaidizi] . . . Kisha nikiwa na furaha nyingi nikaingia katika pango la simba. Daktari na mwuza dawa walikuwa wakichunguza barua tulizokuwa tumetuma nje ya kambi kwa njia haramu. Kukawa na majadiliano makali ya saa mbili. Mkataba ulipokuwa karibu kumalizwa mkuu mwenye kuhoji akasema hivi: ‘Seliger, sasa wewe utafanya nini? Unakusudia kuendelea kuandika maandiko ya kila siku na kutia ndugu zako moyo? Na je! unakusudia kuendelea kuuhubiri ujumbe humu kambini kati ya wafungwa wengine?’ ‘Ndiyo, ndivyo nitakavyofanya hasa, wala si mimi tu, bali pia ndugu zangu wote!’ . . . Saa 8:00 nikaacha kuhojiwa nao akina ndugu wakapewa tangazo lililofanywa kwa jina lao wote, kisha wote kwa shangwe wakaingia katika kazi ya kuhubiri”​—katika majumba ya majeshi yaliyokuwa kambini.

“Aprili 26, 1944, Gestapo walishambulia kwa njia nyingine. Saa 4:00 asubuhi hiyo wakuu wawili wa Gestapo walikuja Lichterfelde kunichunguza sana sana kwa kuwa nilikuwa nikipashana habari na waliokuwa Sachsenhausen na Lichterfelde. Wakanionyesha barua mbili za haramu nilizokuwa nimeandikia ndugu wa Berlin. Barua hizo zilionyesha wazi njia zetu za utendaji. [Tunaweza kuona namna ulivyo upumbavu wa kuandika barua zenye habari kama hizo, kwa maana karibuni wakuu watazipata wanapotukamata au kufanya upekuzi.] Hivyo wakuu walipata habari zote zilizohusu tengenezo na halafu tena walijua kwamba tulikuwa tumepokea chakula cha kiroho kwa kawaida kutoka kwa ‘mama’ yetu.

“Ijapokuwa walichunguza kila kitu, walipata Mnara wa Mlinzi mmoja tu. Nikalazimishwa kusimama langoni huku ndugu wengine wakiletwa kutoka kazini. Wao pia wakapekuliwa wakalazimishwa wasimame langoni. Huu ulikuwa mshindo mkuu, kwa maana mapolisi wengi hawakuwa wametuingilia hivyo kwa muda mrefu. Tulipigwa sana na kutukanwa tulipokuwa tukiulizwa maulizo, na Minara kadha na maandiko yalipatikana. Ripoti ndefu juu ya mambo yaliyoonwa katika Sachsenhausen, Biblia moja na karatasi nyingine zilifichwa wasizipate. Akina ndugu hawakuficha uhakika wa kwamba walikuwa wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii kwa ajili ya faida za Theokrasi na kusoma Minara. Tukalazimishwa kusimama langoni mpaka saa 5:00 usiku huo. Kwa sasa lori la polisi lilikuwa limekwisha fika kuhamisha viongozi kumi na wawili kuwapeleka Sachsenhausen. Hii ilimaanisha kwamba wangenyongwa. Wakaagizwa warudishe vijiko na bakuli zao, na kadhalika. Lakini hawakuhamishwa. Wala siku iliyofuata hawakuhamishwa, ingawa matangazo ya kuuawa kwao yalikuwa yameandikwa kwa watu wa ukoo. Siku ya tatu kukawa na mshangao. Ndugu wale kumi na wawili hawakuuawa, bali walirudishwa kazini.”

Ndugu wa Lichterfelde wakaagizwa baada ya hapo watie sahihi katika tangazo lenye kusema hivi: “Mimi, . . . . . . . . . . . . . . . . . . . mmoja wa mashahidi wa Yehova, ambaye amekuwa kambini tangu . . . . . . . . . . . . . . . . . . .. najidai kuwa ni wa ‘kikundi cha kitheokrasi’ kilichomo katika kambi ya mateso Sachsenhausen. Nimepokea maandiko ya kila siku na vitabu ambavyo nimesoma na kupelekea wengine.” Kila mtu akafurahi sana kutia sahihi.

Mapolisi waliingia vivyo hivyo katika kambi nyingine wakapata matokeo yale yale, nayo kambi mojawapo iliyoingiliwa Mei 4, 1944 ilikuwa Ravensbrück, kwa sababu ilionekana wazi kutokana na barua zile kwamba ndugu wa Sachsenhausen na wa Ravensbrück walikuwa wakipashana habari. Hatua kali zilichukuliwa juu ya “viongozi” wa kambi hiyo. Lakini haukupita muda mwingi na akina dada wakarudishwa kwenye kazi zao za zamani huko pia, baada ya wakuu waliosimamia idara zao kuomba warudishwe. Huu ulikuwa uhakikisho zaidi kwamba uwezo wa waonezi kufikia hapo ulikuwa umevunjwa kweli kweli.

Jeshi la Ujeremani liliposhindwa katika mpaka wa Mashariki mwaka wa 1944 watu wengi sana walikufa hata wazee na vijana wa Hitler wakaingizwa vitani, lakini hata wafungwa walipewa nafasi ya kuonyesha ushujaa wao katika mpaka wa Mashariki. Kwa sababu hiyo halmashauri zikaja kambini kuwapa wafungwa waliotiwa ndani kwa sababu za kisiasa nafasi ya kujiunga na kikosi kilichoshindwa cha Jemadari Dirlewanger. Kama wangejionyesha mashujaa huko vitani, basi wangechukuliwa kama Wajeremani huru. Walakini, inafaa kuangalia kwamba wafungwa wote wenye alama ya mchoro wa pembe tatu (triangle) wa rangi ya zambarau sikuzote waliagizwa kwenda kwenye majumba yao kabla toleo hili halijafanywa kwa wengine. Walijua wangejibiwaje na mashahidi wa Yehova na kwa hiyo wakaacha kuwauliza.

UMATI WA WAFUNGWA WAONDOKA KAMBINI HARAKA HARAKA

Mwaka wa 1945, kumiminika kwa makombora ya majeshi ya hewani ya Waamerika na Waingereza mchana na usiku na kutoroka kwa jeshi la Wajeremani kabisa kulionyesha kila mtu kwamba mwisho wa vita ya ulimwengu ya pili ulikuwa karibu. Askari wa SS walikuwa wameacha kupiga ubwana. Inaonekana hawakuwa katika vyeo vya kuheshimiwa unapokumbuka kwamba mamia ya maelfu katika kambi za mateso walikuwa wakingojea kukombolewa kwa wasiwasi. Walikuwa umati mkubwa sana sana hata askari wa SS wakawaogopa wafungwa. Lakini Himmler aliendelea kufuata amri za Fuhrer (Hitler) wake akatuma simu hii ya chini kwa maamiri wa Dachau na Flossenbürg: “Hatuwezi kamwe kukubali tumeshindwa. Wafungwa wote na watoke kambini mara moja. Hakuna mfungwa atakayeingia mikononi mwa adui akiwa hai. (Ikatiwa sahihi Heinrich Himmler)” Maagizo kama hayo yakatumwa kwenye kambi nyingine.

Huu ndio uliokuwa mpango wa mwisho wa kiibilisi wenye kuhatirisha maisha za watumishi waaminifu wa Mungu waliofungwa kambini. Lakini wao hawakuwa na wasiwasi kupita kiasi. Walimtumaini Yehova, hata wapatwe na nini wakati huo.

Wakuu wa SS waliokuwa na kazi ya kuchovya wafungwa majini walikuwa na kazi isiyo na suluhisho. Ndugu Walter Hamann aliyekuwa amepewa mgawo wa kufanya kazi katika mkahawa mdogo wa SS alisikia mazungumzo ya kupendeza ya wakuu wa SS. Asimulia hivi: “Wakuu hao walizungumza juu ya kuua wafungwa kwa kuwatia katika vyumba vyenye kujaa gas, lakini vyumba vyenyewe vilikuwa vidogo sana nao hawakuwa na gas ya kutosha. Kisha nikasikia mazungumzo katika simu juu ya kuletwa kwa mafuta ya kuwashia tanuru; lakini haikuwezekana yaletwe. Halafu ikatajwa kwamba kambi zingelipuliwa pamoja na waliomo. Tayari masanduku ya baruti zenye nguvu yalikwa yamewekwa katika majumba mbalimbali, hasa katika sehemu ya kulala ya hospitali. Lakini mpango huu pia ukaachwa. Mwishowe, ikaamuliwa wafungwa hao 30,000 waondolewe kambini; waliambiwa watapelekwa kwenye kambi kubwa zaidi na kumbe ilikuwa kambi ya uongo​—kwa hakika walikuwa wakitaka kutuzamisha sote katika Ghuba la Lübecker. Wasingehatiji gas yo yote, mafuta wala baruti kuweza kufanya hivyo.”

Kwa sasa majeshi ya Mwungano yalikuwa yakija kasi kasi. Sasa askari wa SS wakaanza kuona wasiwasi juu ya maisha zao wenyewe na kuvurugika zaidi na zaidi, hasa baada ya uamuzi wa serikali kugharikisha kambi kujulikana. Walipopatwa na magumu mengi sana, wakaelekeza wafungwa barabarani na kuwalazimisha watembee wakiwa na chakula haba. Ye yote aliyeendea njia waliyopitia wafungwa hawa walioitwa “watembezi waelekeao kifoni,” angeweza kuona kwamba wote walikuwa wanaelekezwa mahali pamoja. Lengo lao lilikuwa kuwapeleka kwenye Ghuba la Lübecker, au kwenye bahari iliyo pana upande wa kaskazini, ambako ndipo wangepakiwa melini na kuzamishwa kabla majeshi ya adui hayajafika.

Karibuni chakula kikaisha na, nyakati nyingine, hata tone moja la maji halikupatikana. Hata hivyo, wafungwa wenye kufa njaa wakalazimishwa kutembea mchana kutwa kwa siku nyingi na isitoshe, walitembea mvua ikiwa inakunya na kunya kweli kweli. Usiku walilazimishwa kulala misituni katika ardhi iliyonyweshwa maji na mvua. Wasioweza kutembea kwa mwendo uliotakiwa walipigwa risasi ya shingo na mlinzi wa SS aliyekuwa nyuma. Hesabu ya waliokufa wakati wa kuondoka kambini inaweza kuonekana kutokana na mfano wa Sachsenhausen. Kati ya wafungwa 26,000 waliokuwa bado hai wakati wa kuondoka, 10,700 waliachwa wamelazwa katika barabara ya kutoka Sachsenhausen kwenda Schwerin, wakiwa wamepigwa risasi hata kufa.

Ndugu wachache waliokuwa Mauthausen walikuwa hatarini pia. Mahandaki makubwa yalikuwa yamechimbwa kuingia katika mlima ambamo roketi za “V-2” zilizoogopwa zilitengenezewa. Siku moja mojawapo la mahandaki lilifunguliwa baruti zikatiwa ndani. Mpango ulikuwa kusingizia kwamba ndege zinashambulia kutoka hewani, kwa njia hiyo wafungwa 18,000 waingizwe katika handaki hilo kisha lilipuliwe. Lakini wasimamizi wa kambi walizukiwa kwa ghafula na vifaru vya Warusi, kwa hiyo askari wa SS wakaona afadhali kuacha wafungwa peke yao wajaribu kuokoa maisha zao wenyewe, ikiwezekana. Lakini hawakufaulu. Siku chache tu baadaye amiri wa kambi aliyesema hivi: ‘Mimi nataka kuona hati tu za kuonyesha waliouawa,’ aligunduliwa na wafungwa akakanyagwa-kanyagwa mpaka kufa. Wafungwa waliotiwa ndani kwa sababu za kisiasa ndipo wakatafuta kulipiza kisasi juu ya wafungwa wenzao ambao, walipokuwa wazee wa kambi, wazee wa majumba na wanyapara, walikuwa na hatia nyingi ya kumwaga damu.

Wafungwa walitembea kutoka Dachau kupitia katika misitu wakielekea kifoni, na wale wasioweza kutembea kwa mwendo uliotakiwa wakapigwa risasi na askari wa SS. Walikuwa wakitaka kuelekeza wafungwa kwenye Milima ya Ötztaler, ambako wenye kufika huko wangepigwa risasi. Ndugu waliendelea kuwa wenye umoja na kusaidiana, kwa njia hiyo wakazuia wengine wasiuawe mpaka walipofika Bad Tolz, ambako waliachwa huru. Ndugu Ropelius anakumbuka kwamba usiku wa mwisho walilala wamefunikwa na theluji katika msitu wa Waalkirchen. Kulipokuwa kunapambauka Polisi wa Bavaria wakaja wakawaambia wako huru na kwamba askari wa SS wamekwisha toroka. Walipokuwa wakiendelea na safari yao wakaona silaha zinaegemea miti bila askari wa SS.

Askari wa SS walithamini maagizo ya serikali kugharikisha wafungwa wote kwa maji. Siku chache tu kabla Wajeremani hawajakubali kushindwa, vikundi vikundi vya wafungwa viliunganishwa katika Neuengamme vikapakiwa katika meli ya mizigo kupelekwa iliko ‘Cap Arcona,’ meli ya starehe, iliyokuwa imetia nanga katika Ghuba la Neustadter. Karibu wafungwa 7,000 walikuwa wamekwisha ingia katika meli hiyo ya urefu wa mita 200. Askari wa SS walipanga kusafirisha meli hiyo ‘Cap Arcona’ katika bahari pana ambako wangeizamisha ikiwa na wafungwa. Lakini meli hiyo ilikuwa ingali ikipeperusha bendera yake na kwa hiyo ikazamishwa Mei 3, 1945 na ndege za vita za Waingereza. Meli iitwayo ‘Thielbeck,’ yenye karibu wafungwa 2,000 au 3,000 hivi ilizamishwa pia. Karibu wafungwa 9,000 walididimia wakafa maji katika Ghuba la Neustadter. Kwa hiyo ni wazi kuona kwa nini waokokaji wanatetema wanapokumbuka tukio hilo. Mpaka leo hii karibu magofu kumi na mawili au kumi na saba hivi ya wafungwa hawa waliozamishwa yanapatikana kila mwaka katika pwani ya Neustadter na waogeleaji na wakati sehemu hizo zinapochimbuliwa.

Tukio lile lile lilikuwa limepangwa kuletwa juu ya wafungwa waliokuwa katika Sachsenhausen, kutia na ndugu 220. Walitembea kilomita karibu 200 kwa juma mbili walipokuwa wakielekezwa kifoni.

Mashahidi walikuwa wamejua mapema hatari iliyokuwa inakaribia, kwa hiyo wakatengeneza viatu vyao na kukusanya pamoja vigari vya mkokoteni kusafirisha mali chache za walio dhaifu, halafu wakawaweka hao ndani. Kama sivyo ndugu hawa wangalikuwa kati ya watu zaidi ya 10,000 waliofia njiani. Lakini kwa njia hiyo ndugu waliokuwa na nguvu kidogo za kimwili waliweza kuwakokota. Huko njiani wengine waliingizwa katika mikokoteni walipoishiwa nguvu. Wakiisha kupata nguvu tena baada ya kupumzika siku kadha nao pia walianza kukokota vigari hivyo. Kwa njia hiyo waliendelea kuwa jamaa kubwa yenye kufurahia ulinzi wa Yehova mpaka mwisho, walipokuwa wakielekea kifoni.

Halafu alasiri moja wakati kikundi hiki cha wafungwa wenye kukimbia kilipokuwa mwendo wa siku tatu tu kutoka Lubeck, askari wa SS wakaagiza kila mtu apige kambi katika msitu uliokuwa karibu na Schwerin. Wakati wa safari hiyo akina ndugu walikuwa wamejikusanya vikundi vikundi na kutengeneza hema za safari kwa kutumia blanketi zao. Wakafunika sakafu na matawi madogo kumaliza baridi ya usiku. Usiku huo risasi za Warusi zilipokuwa zikipita juu yao nao Waamerika wakazidi kuja, sehemu hii ya Ujeremani ilianguka. Waliokuwako walishangilia kweli kweli kwa vifijo na vigelegele usiku wa manane sauti zilipokuwa zikipazwa kwa kurudiwa-rudiwa mara elfu-elfu: “TUKO HURU!” Askari karibu 2,000 wa SS waliokuwa wamekuwa wakisimamia wafungwa mpaka wakati huo wakawa wamevua mavazi yao kwa siri ili waonekane kuwa raia, hata wengine wakavaa mavazi ya wafungwa wasijulikane. Walakini, saa chache baadaye wengine wao walitambuliwa wakachinjwa bila huruma.

Lakini hata baada ya hapo ndugu wakakaa saa chache zaidi, kwa maana mkulima mmoja aliyekuwa kati ya watoro aliwapa akina ndugu ratili 200 za mbaazi. Chakula kizuri sana kikapikwa na kuliwa. Lo! ndugu walifurahije!

Walishukuruje walipogundua hakuna hata mmoja wao asiyekuwako!

Sasa hawakuwa na haraka kubwa ya kusonga mbele. Mle mle katika msitu huo uliokuwa karibu na Schwerin wakaanza kuandika ripoti ya mambo yaliyowapata kwa kutumia taipuraita ambayo askari walitupa kutoka afisi ya kibanda fulani. Ripoti hii ilikuwa na azimio lililoandikwa kwa msisimko wa ajabu. Azimio lenyewe ndilo hili: (Inaendelea)

​—Kutoka 1974 Yearbook of Jehovah’s Witnesses.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki