Historia ya Mashahidi wa Yehova Katika Nyakati za Kisasa
—United States of Amerika
MAPATANO ya kuacha vita yalitiwa sahihi Novemba 11, 1918, nayo Vita ya Ulimwengu ya Kwanza ikafikia kikomo. Lakini Wanafunzi wa Biblia wanane wale walikuwa bado gerezani. Walibaki humo huku waamini wenzao wakiwa na kusanyiko katika Pittsburgh, Pennsylvania, Januari 2-5, 1919. Kusanyiko hilo liliunganishwa na mkutano ule wa maana sana wa kila mwaka wa Watch Tower Bible and Tract Society Jumamosi, Januari 4, 1919.
Majina yaliitwa, uchaguzi ukafanywa na J. F. Rutherford akachaguliwa kuwa msimamizi, C. A. Wise kuwa msimamizi mdogo, na W. E. Van Amburgh akawa katibu mweka-hazina. Anapotazama nyuma, Anna K, Gardner aeleza hivi: “Kulikuwa na furaha nyingi sana baada ya mkutano huo kuona tena Yehova akiongoza watu wake.”
Sasa twende gerezani Atlanta. Ni Jumapili, Januari 5, 1919. J. F. Rutherford agonga-gonga ukuta wa kijumba cha jela cha Ndugu Macmillan na kusema: “Chomoa mkono wako nje.” Kisha ampa Macmillan barua ya simu. Ujumbe wake wasemaje? Rutherford amechaguliwa tena kuwa msimamizi. Baadaye siku hiyo Ndugu Rutherford alimwambia A. H. Macmillan hivi: “Nataka kukuambia jambo fulani. Jana ulisema jambo ninalofikiria juu ya kuwekwa kwetu katika cheo cha Ndugu Russell nasi tungaliongoza uchaguzi kama tungalikuwa Pittsburgh na Bwana asingalipata nafasi ya kuonyesha aliyemtaka. Nakuambia ndugu, nikitoka hapa, kwa neema ya Mungu nitaharibia mbali jambo hili la kuabudu viumbe. Isitoshe, nitachukua upanga wa kweli, nami nitayapasua matumbo ya Babeli wa kale. Wao ndio waliotuingiza humu, lakini tutatoka.” Rutherford hakuwa akicheza. Tangu wakati wa kufunguliwa kwake mpaka kufa kwake mapema mwaka wa 1942, alitimiza ahadi hiyo kwa kufunua wazi uovu wa dini ya uongo.
Machi 21, 1919, Hakimu Louis D. Brandeis wa United States Supreme Court aliagiza dhamana iwekwe kwa ndugu wanane wenye kufungwa na kuamuru kwamba wapewe haki ya kuomba rufani Aprili 14 ya mwaka huo. Walifunguliwa upesi na Jumanne, Machi 25, wakaondoka katika gereza la Atlanta kwa gari-moshi. Walipokuwa wamerudi Brooklyn Machi 26, 1919, wakuu wa serikali walifungua ndugu hao kila mmoja wao akiwekewa dhamana ya $10,000 na kungojea kesi zaidi.
Kesi ya Wanafunzi wa Biblia wanane hao ingesikilizwa kwa sababu ya kuomba rufani Aprili 14, 1019 Kesi wakati huo ilifanywa mbele ya Federal Second Circuit Court of Appeals katika mji wa New York. Mei 14, 1919, mashtaka yao yasiyo ya kweli yalibadilishwa. Wenye kusimamia wakati huo walikuwa Mahakimu Ward, Rogers na Manton. Hakimu Ward alisema hivi akiahirisha kesi: “Washtakiwa katika kesi hii hawakujaribiwa bila upendeleo kama walivyostahili, na kwa sababu hiyo hukumu imebadilishwa.”
MAONI MAPYA
Baada ya kipindi chao chenye majaribu cha 1917-1919, watu wa Yehova walijichunguza sana. Wakitambua kwamba walikuwa wametenda kwa njia zisizompendeza Mungu, waliomba msamaha katika sala, wakatubu juu ya mwendo wao wa zamani. Yehova aliwasamehe na kuwabariki.— Mit. 28:13.
Mojawapo la mambo ya kukubaliana na wapinzani wao lilikuwa kukata kurasa za kitabu The Finished Mystery, wakiwa na kusudi la kuwapendeza wale waliojitwalia cheo cha kukataa sehemu za vitabu walizoona kuwa hazifai. Jambo jingine lilikuwa wakati The Watch Tower la Juni 1, 1918, liliposema: “Kulingana na azimio la Baraza Kuu la Aprili 2, na kulingana na tangazo la Rais wa United States la Mei 11, inapendekezwa kwamba watu wa Bwana kila mahali wafanye Mei 30 iwe siku ya sala na maombi.” Baadaye maelezo yalitolewa ya kuitukuza United States nayo hayakupatana na hali ya kutokuwamo ya Kikristo.—Yohana 15:19; Yak. 4:4.
“MAKAO YA BETHELI YATARUDISHWA?”
Hilo lilikuwa ulizo jingine kubwa. Brooklyn Tabernacle ilikuwa imekwisha uzwa. Ingawa Betheli ilikuwa ya Sosaiti bado, ilikuwa haina vifaa nao utendaji wa makao makuu ulikuwa umehamishwa ukapelekwa Pittsburgh. Huko akina ndugu walikuwa na pesa chache na makao yao yaliyokuwa katika Federal Street hayakuwa na nafasi ya kutosha kuweza kupanuliwa. Vifaa vya kuchapia havikuwako, na hata mengi ya mabamba ambayo kwayo vitabu vya Sosaiti vilichapwa yalikuwa yamekwisha haribiwa. Hakukuwa na matumaini maangavu.
Walakini, wakati J. F. Rutherford alipokuwa California, jambo la kupendeza lilitukia katika makao makuu ya Sosaiti Pittsburgh. Asubuhi moja Mkristo mmoja, George Butterfield, mtu tajiri, aliingia afisini. A. H. Macmillan ndiye aliyesema naye sebuleni, akamwambia kwamba Ndugu Rutherford alikuwa California, kisha yakatokea yafuatayo, kulingana na ripoti ya Macmillan mwenyewe:
“Akasema, ‘Mna chumba cha faragha hapa?’
“‘Tutafunga mlango huu, hapa ni faraghani. Wataka kufanyaje, George?’
“Akaanza kuvua shati lake nilipokuwa nikisema naye. Nilidhani ana kichaa. Alionekana mchafu kidogo na mwenye kuchoka kwa kusafiri, ijapokuwa kwa kawaida alikuwa mtu malidadi na nadhifu. Akatoa kisu chini ya fulana yake. Kisha akakata kiraka kidogo kilichokuwa hapo akatoa furushi la pesa. Zilikuwa noti za $10,000 (shilingi 80,000 au 5.000Z).
“Akaziweka chini akasema, ‘Hizi zitawasaidieni kuanzisha kazi hii. Sikutaka cheki maana sikujua ni nani aliye hapa. Sikulala kitandani katika gari-moshi maana sikutaka ye yote azichukue akijua ninazo, kwa hiyo nikaketi usiku kucha. Sikujua mwenye kusimamia kazi, lakini kwa kuwa sasa nawaona nyie ndugu mlio hapa ninaowajua na kutumaini, nafurahi kwamba nimekuja!’ . . . Lilikuwa jambo la kushangaza na kupendeza na kutia moyo.”
Ndugu Rutherford aliporudi kwenye afisi za Sosaiti Pittsburgh, alimwagiza msimamizi mdogo wa Sosaiti, C. A. Wise, aende Brooklyn akaone kama Betheli inaweza kufunguliwa tena na kukodi sehemu ambako Sosaiti ingeweza kuanza uchapaji. Mazungumzo yalikuwa hivi:
“Nenda ukaone kama ni mapenzi ya Bwana kwetu turudi Brooklyn.”
“Nitajuaje kama ni mapenzi ya Bwana kwetu turudi au siyo?”
“Tulirudi Pittsburgh kutoka Brooklyn kwa sababu ya kukosa makaa ya mawe. Tuamue kwa makaa ya mawe. Nenda kaagize makaa ya mawe.” [Katika New York makaa ya mawe yalikuwa yangali yakiuzwa kwa kiasi kidogo mwishoni mwa vita.]
“Wadhani imenipasa niagize tani ngapi?”
“Agiza nyingi; agiza tani mia tano.”
Ndivyo Ndugu Wise alifanya. Alipofanya ombi kwa wakuu, akapewa hati ya kupata tani mia tano za makaa ya mawe. Mara moja akampigia simu J. F. Rutherford. Makaa ya mawe ya kiasi hicho yalitosha kutumiwa miaka mingi. Lakini wangeyaweka wapi yote? Sehemu kubwa za chini za makao ya Betheli zikawa za kuwekea akiba ya makaa ya mawe. Jaribio hilo lenye kufanikiwa lilichukuliwa kuwa wonyesho thabiti kwamba yalikuwa mapenzi ya Mungu wahamie Brooklyn. Ndivyo walivyofanya, Oktoba 1, 1919.—Kutoka 1975 Yearbook of Jehovah’s Witnesses.